Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ng'wasi Damas Kamani (10 total)

MHE. ASIA A. HALAMGA K.n.y. MHE. NG’WASI D. KAMANI Aliuliza:-

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka sasa wa kufanya masomo ya Ujasiriamalai na Usimamizi wa Fedha kuwa masomo ya lazima kwa kila mwanafunzi nchini kwa kuwa Elimu ya Ujasiriamali ni mbadala wa changamoto ya ajira kwa vijana?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufundisha masomo ya ujasiriamali na usimamizi wa fedha ili kuwajengea wanafunzi stadi na ujuzi utakaowasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali katika jamii ikiwemo suala la ajira.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa masomo hayo yanafundishwa kuanzia ngazi ya elimu msingi na sekondari kama ifuatavyo: Shule za Msingi, Ujasiriamali na Usimamizi wa Fedha hufundishwa katika masomo ya stadi za kazi, maarifa ya jamii na hisabati. Katika ngazi za Shule ya Sekondari, masomo haya hufundishwa katika masomo ya Civics na General Studies ambayo husomwa na wanafuzni wote. Aidha, masomo hayo hufundishwa katika masomo chaguzi kama vile Book Keeping, Commerce, Economics, Accountancy, Home Economics, Mathematics na Agriculture.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na zoezi la kuboresha mitaala na mihtasari ya masomo katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kwa lengo la kuandaa mitaala itakayokidhi mahitaji na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kijamii katika ulimwengu wa sasa.

Mheshimiwa Spika, katika hatua hii, Serikali itatilia mkazo mbinu tete na stadi za maisha hususan stadi za karne ya 21 ambazo ni fikra tunduizi, ubunifu, ushirikiano, uongozi na stadi za teknolojia habari na mawasiliano ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kukabiliana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika jamii yetu na dunia kwa ujumla likiwemo suala la ajira. Ahsante. (Makofi)
MHE. NG’WASI D. KAMANI Aliuliza: -

Je, Serikali imefikia hatua gani katika kuunganisha Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi hususan Vijana na kuwa na eneo moja la wazi la utoaji huduma?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa ridhaa yako kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu anayetujalia uhai tuendelee kutekeleza majukumu yetu ya kila siku. Lakini pili, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu mpenda wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuniamini na kuweza kuniendeleza kubaki katika nafasi ya Naibu Waziri katika Wizara hii ya Uwekezaji Viwanda na Biashara, ili niweze kuendelea kumsaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inasimamia Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 na Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004. Aidha, Serikali inaratibu utekelezaji wa mifuko na programu za uwezeshaji 62 ambapo mifuko na proramu 52 zinamilikiwa na Serikali na mifuko na programu 10 zinamilikiwa na taasisi za sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, kati ya mifuko hiyo na proramu 52 zinazomilikiwa na Serikali, mifuko 21 inatoa mikopo ya moja kwa moja kwa walengwa, mifuko tisa inatoa dhamana ya mikopo, mifuko 17 inatoa ruzuku na programu tano ni za uwezeshaji ambazo zinatoa huduma mbalimbali ikiwemo ujenzi, urasimishaji ardhi na uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha taarifa ya tathmini ya mifuko hiyo na taarifa hiyo itawasilishwa hapa Bungeni baada ya kukamilika. Nakushukuru sana.
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia Balozi zetu kuhakikisha Vijana wengi wa Kitanzania wanaajiriwa nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damasi Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mkakati maalum wa kuhakikisha kuwa vijana wa Kitanzania wenye sifa zilizowekwa wanapata fursa za ajira nje ya nchi kama ifuatavyo: -

i) Balozi zetu nje ya nchi zimeendelea kutafuta fursa za ajira mbalimbali kwenye maeneo yao ya uwakilishi kwa kuingia mikataba ya ajira nje ya nchi inayowawezesha vijana wetu kupata ajira na kuwahakikishia usalama na maslahi yao katika ajira hizo.

ii) Serikali kupitia Kanzi Data ya Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) inawawezesha vijana na wataalam mbalimbali kujiandikisha ili kuwasadia kuomba nafasi za ajira pindi zinapopatikana nje ya nchi.

iii) Wizara inafuatilia nafasi za ajira ambazo hutangazwa katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa na kuziwasilisha katika mamlaka mbalimbali ili kusaidia kuwatambua vijana ambao wanazo sifa kutoka Serikalini na Sekta Binafsi na kuwashawishi kuomba nafasi hizo. Ahsante sana.
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani kwa Makampuni Binafsi yanayouza Hisa na hayajatoa gawio miaka mingi pamoja na kujiendesha vizuri?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ulipaji wa gawio kwa wanahisa wa kampuni unafanyika kwa kuzingatia Kifungu cha 180 cha Sheria ya Kampuni, Sura 212.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria hii, Serikali haiwezi kuingilia maamuzi na taratibu za kampuni kulipa gawio. Aidha, napenda kutoa rai kwa wanahisa wa kampuni mbalimbali kushiriki vikao vya mwaka vya wanahisa katika kampuni zao ili kuwa sehemu ya maamuzi yanayotolewa kwenye Mikutano Mikuu wa Mwaka.
MHE. ASIA A. HALAMGA K.n.y. MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, lini Serikali itafupisha muda wa miaka saba kwa elimu ya msingi na sita ya sekondari ili kupunguza muda kwa wanafunzi wenye uwezo mkubwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la miaka inayotumika kumuandaa mhitimu wa elimu ya msingi na sekondari hutegemea kiasi cha maudhui yanayotakiwa kujengwa ili kumuwezesha mhitimu kupata stadi na ujuzi unaohitajika kulingana na mahitaji ya wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua uwepo wa wanafunzi wenye uwezo tofauti katika kujifunza mwaka 2019 ilitoa mwongozo kuhusu utaratibu wa kurusha darasa wanafunzi wa elimu ya msingi. Mwongozo huo unatoa utaratibu unaopaswa kufuatwa na uongozi wa shule kwa kushirikiana na mzazi wa mtoto husika katika kumrusha darasa mwanafunzi anayeonekana kuwa na uwezo mkubwa darasani. Aidha, baada ya kufanyika kwa tathmini ya utekelezaji wa mwongozo huo Serikali itaona namna ya kuendelea na utaratibu huo kwa ngazi nyingine za elimu. Nakushukuru sana.
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaona haja ya kuondoa malipo ya Kodi kwa Wajasiriamali kabla ya kuanza rasmi kufanya biashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng'wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019, kifungu cha 43 imetoa unafuu wa kutolipa kodi kwa kipindi cha miezi sita kwa biashara mpya tangu mhusika anapopewa namba ya Utambulisho wa Mlipakodi. Lengo la hatua ni kumpa mjasiriamali nafasi ya kustawi kibiashara.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana wanaojitolea kutumikia katika kada mbalimbali za utumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu Swali Na. 239, lililoulizwa na Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iliweka mazingira ya kuwawezesha vijana wanaohitimu katika vyuo mbalimbali kujitolea katika Taasisi za Umma kwa lengo la kuwawezesha kujipatia sifa za ziada zitakazowawezesha katika ushindani pindi nafasi mbalimbali za ajira zinapotangazwa. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kifungu Na. 2.1.2 cha Sera ya Menejimenti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Toleo la Pili la Mwaka 2008 na Kanuni D. 6 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 ikisomwa pamoja na Kanuni Namba 12(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022, ajira kwa nafasi zilizo wazi katika Utumishi wa Umma hujazwa kwa ushindani na uwazi kwa kufanya usaili na kupata washindi katika nafasi husika.

Mheshimiwa Spika, hivyo, nitumie nafasi hii kuwashauri na kuwahamasisha vijana wanaojitolea katika kada mbalimbali za utumishi wenye sifa stahiki, kuomba nafasi za kazi pindi zitakapotangazwa ili waweze kushindana na waombaji wengine wenye sifa stahiki.
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, kwa nini ukomo wa saa za kufundisha Wanafunzi haujawekwa kisheria kama ilivyowekwa kwa saa za kazi kwa Waajiriwa?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damasi Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Elimu haijaweka ukomo wa saa za kufundisha wanafunzi ili kutoa fursa ya mtaala kuwa nyumbufu kulingana na mahitaji maalumu ya ujifunzaji wa wanafunzi wote pamoja na mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mitaala ya Elimu ya Msingi na Sekondari imeweka bayana Muda (duration) unaopaswa wanafunzi kusoma. Mtaala wa Elimu ya Msingi unaeleza kuwa muda wa kusoma Elimu ya Awali na Darasa la I - II ni masaa matatu tu kwa siku na kipindi kimoja ni dakika 30. Aidha, Muda wa kusoma kwa darasa III - VII ni masaa sita kwa siku na kila kipindi ni dakika 40. Aidha, kwa upande wa Elimu ya Sekondari muda wa kusoma ni masaa matano na dakika 20 na kipindi kimoja ni dakika 40. Aidha, kwa mwaka wanafunzi hutakiwa kusoma kwa siku 194.
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza:-

Je, Serikali inatumia mfumo gani kuhakiki ubora na matokeo chanya ya programu mbalimbali zinazotolewa kwa vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Kamani, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu zote zinazotekelezwa ikiwemo programu za vijana. Katika kutekeleza hilo mwezi Januari, 2022 Serikali ilitoa Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miradi mbalimbali na Programu za Maendeleo. Kwa kuzingatia mwongozo huo, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu mbalimbali kila robo mwaka. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekuwa ikifanya tafiti ili kupima matokeo ya utekelezaji wa programu mbalimbali, ikiwemo utafiti wa nguvu kazi ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti wa nguvu kazi uliofanyika mwaka 2020/2021unaonesha kuwa kutokana na programu za vijana zinazotekelezwa ikiwemo Programu ya Kukuza Ujuzi, kiwango cha ujuzi cha juu kimeboreka. Kiwango cha ujuzi cha kati kimeongezeka kutoka asilimia 16.6 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 19.9 mwaka 2021, na kiwango cha ujuzi wa chini kimepungua kutoka asilimia 79.9 mwaka 2014 hadi asilimia 76.9 mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kusimamia utekelezaji wa programu hizo ili ziweze kuleta tija kwa Taifa. Sambamba na hatua hiyo, mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imepanga kufanya tathmini mahususi (tracer study) ya mafunzo yanayotolewa kupitia programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kubaini mafanikio yaliyopatikana kwa kuwezesha kujiajiri na kuajiriwa, ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa kuongeza nguvu kwenye uvuvi ili vijana wa Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa wanufaike na Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi boti za kisasa kwa mkopo usio na riba kupitia Benki ya Kilimo Tanzania (TADB). Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na TADB inakamilisha taratibu za kutoa maboti 158 kwa mkopo kwa Vyama vya Ushirika 45, Vikundi vya Wavuvi 71 na watu binafsi 43 ambao wengi wao ni vijana. Aidha, katika Ukanda wa Ziwa Victoria, jumla ya Vyama vya Ushirika 20 kwa maana ya Mkoa wa Mwanza 14, Vikundi 17 kwa maana ya Mkoa wa Mwanza 10, na watu binafsi 17 kwa Mwanza wanne, wanatarajiwa kunufaika na mkopo wa maboti hayo.

Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imetenga fedha kwa ajili ya miradi ya ufugaji samaki kwenye vizimba katika Ziwa Victoria kwa kuwawezesha vijana kupata pembejeo za ufugaji samaki kwa mikopo isiyo na riba. Aidha, jumla ya wanufaika 3,154 ambao wengi wao ni vijana wameainishwa kunufaika na mkopo huo ikijumuisha vikundi 67, kwa maana ya Mwanza 42, vyama vya ushirika 24, Mwanza 14; kampuni 10, kwa Mkoa wa Mwanza vitano; na watu binafsi 32, kwa Mkoa wa Mwanza 16 kutoka ukanda wa Ziwa Victoria.