Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rashid Abdalla Rashid (5 total)

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali na pia niishukuru Serikali kwa kupeleka fedha katika maeneo hayo ya ujenzi wat uta hilo. Na nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa, miradi hii inagharimu fedha nyingi katika utekelezaji wake, lakini katika utekelezaji huo Serikali haikutumia mafundi wazuri na hatukupata matokeo mazuri katika ujenzi wa tuta hilo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia mafundi bobezi ili wananchi waweze kunufaika na ujenzi huo wa tuta?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, Naibu Waziri atakuwa yuko tayari kufuatana nami ili kwa macho yake aende kushuhudia ujenzi wat uta uliofanyika katika phase II ya TASAF Awamu ya Pili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali haifanyi shughuli zake kwa kubahatisha upo utaratibu maalum ambao umeandaliwa wa kutumia wataalamu bobezi. Wataalam ambao wana uwezo mkubwa wa kujenga miradi hiyo, ili ufanisi uweze kupatikana.

Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili, niko tayari kwa sababu ya juhudi zake ambazo nimeziona katika jimbo lake kufuatananaye bega kwa bega, hatua kwa hatua mpaka katika jimbo hilo kuona sehemu husika.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza kwa kuwa eneo tayari lipo na kwa kuwa nafahamu kwamba kuna matofali ya kutosha katika Kambi ya Mfikiwa yaliyobaki kwa ajii ya ujenzi wa nyumba za Polisi Mfikiwa na mimi nikiwa mdau wa upatikanaji wa matofali hayo.

Je, ni lini Wizara itatupatia matofali hayo ili kwa kushirikiana na wananchi wangu wa Jimbo la Kiwani tuweze kuanza ujenzi wa kituo hicho?

Swali la pili, wananchi wa Shehia ya Kendwa kwa kushauriwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba walitakiwa waanzishe Jengo kwa ajili ya polisi jamii na wananchi hao kwa kutii walianzisha jengo hilo ambapo sasa lina miaka nane.

Je, ni lini Wizara italimaliza jengo hilo ili wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdalla, Mbunge wa Jimbo la Kiwani kutoka Kusini Pemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza linazungumzia kuhusu matofali; ni kweli katika eneo lile la Mfikiwa yapo matofali na matofali yale jumla yake ni 32,000 na matofali yale yaliletwa pale kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari makazi ya askari pale Mfikiwa na siyo matofali tu, lakini yapo na mabati ipo na rangi. Lakini kwa bahati nzuri au bahati mbaya ikafika wakati kidogo tukapungukiwa na fedha za kutosha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huu.

Kwa hiyo, matofali haya nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba hayapo tu kwamba maana yake kazi imekwisha, kazi ya ujenzi wa nyumba zile azma ya Serikali iko pale pale, kwa hiyo, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba aendelee kustahimili tupo mbioni tutahakikisha kwamba kwa kushirikiana yeye na wadau wengine werevu tupate matofali na vifaa vingine vya kutosha ili tukajenge Kituo cha Polisi hapo Kiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwambie tu kwamba azma ya Serikali ni kuendeleza kujenga nyumba hizi na nyumba hizi zipo katika hali ya kujengwa kwa sababu tayari ipo nyumba moja imeshaanza kujengwa na imeshafikia katika hatua ya lenta.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, ni lini sasa Serikali itamaliza boma lile la polisi jamii. Kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya katika Jimbo la Kiwani, kwa sababu amekuwa ni mdau mzuri ambaye anatusaidia Serikali hasa katika masuala ya ulinzi na usalama, hiki kituo ambacho kinazungumzwa cha polisi jamii amesaidia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba anasaidia wananchi kuweza kupata huduma hizi. Kwa hiyo kikubwa nimwambie tu kwamba tutajitahidi katika mwaka ujao wa fedha tuweke hilo fungu kwa ajili ya kumsaidia kumalizia hili boma ama hiki kituo ambacho kimeshaanza cha askari jamii katika Shehia hii ya Kendwa. Nakushukuru.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri nilikuwa naangalia kwenye jibu la msingi linaonesha kwamba huko Kiwani mpaka sasa hivi hakuna eneo lililotengwa; wakati huo huo kuna mahali kuna matofali yamewekwa na ujenzi umefika mahali. Sasa hebu fafanua kidogo, haya matofali yako wapi ili nijue swali la nyongeza la Mbunge linaendana na hili jibu la msingi au hapana?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali aliloliuliza kwamba kule Kusini Pemba kuna eneo la tuseme ni Kambi ya Askari Polisi panaitwa Mfikiwa, pale Mfikiwa Serikali kupitia Jeshi la Polisi iliamua ijenge nyumba za makazi ya askari polisi yaani Mfikiwa na huko Jimboni kwake ni mbali kidogo.

Kwa hiyo, kilichokuja kuamuliwa kwamba kuna matofali yale yeye ameona kwamba yako kwa muda mrefu yamekaa, kwa hiyo, anaona kwanini Serikali yale matofali yasichukuliwe yakapelekwa Kiwani ili wananchi wa Shehia za Jombwe, Kendwa, Muwambe, Mchake, Mtangani, Kiwani wajengewe kituo kile cha polisi sasa yale matofali azma ya Serikali ilikuwa ni kujenga nyumba za askari na kila kitu kipo tulipungukiwa kidogo na fedha ndicho ambacho anataka apelekewe yale matofali tukamwambia kwamba tutamfanyia maarifa tumpelekee matofali mengine.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina swali la nyongeza. Ni kweli vikundi vimepatiwa mafunzo haya na vinapatiwa tunzo, lakini ni lini vitapatiwa fedha ili ziweze kuwasaidia katika shughuli zao badala ya kukaa na mafunzo kwa takribani miaka miwili bila kupata fedha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Abdalla Rashid, Mbunge wa Kiwani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali tayari imeshafanya mafunzo kwa vikundi hivi vya uhifadhi wa mazingira na tayari tumeshafanya uwezeshaji wa wataalam, hivyo Serikali sasa kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakishirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar watafanya uwezeshaji wa vikundi hivi ili viweze kutekeleza miradi hii.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba uhakiki umefanyika na wananchi hao wamesharejeshwa, lakini ni lini sasa watapatiwa malimbikizo yao ya ruzuku kutoka pale ambapo walisimamishwa na ukizingatia kwamba hasa hawa ambao walisimamishwa ni wanawake?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rashid kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna makundi mawili; la kwanza ni wale ambao baada ya uhakiki walionekana wamekosa sifa na hawa ni 2,500 lakini wako ambao walipokosa sifa walikata rufaa wakarejeshwa, tutaangalia uwezekano wa kuanzia pale walipokuwa wamesimama au taratibu zinatakaje ili waweze kulipwa au wataendelea kuanzia hapa ambapo wamekuwa cleared.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili ni jambo la kulifanyia kazi, tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge muuliza swali Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi ili atuambie hasa ni wapi, lakini kimsingi Serikali ili wapembua kwa makundi hayo mawili na uamuzi huo ndio ulikuwa umefikiwa mpaka hatua za mwisho.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar imeshatoa eneo kwa ujenzi wa Chuo Kikuu Huria na Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere katika eneo la Mfikiwa. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Rashid Rashid kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyowaeleza kwenye majibu ya msingi, mradi wetu wa HEET unakwenda ku-cover karibu maeneo mengine sana. Amezungumza hapa suala la Chuo Kikuu Huria pamoja na Chuo chetu cha Mwalimu Nyerere ambayo tayari ina Kampasi kule Zanzibar, kwa hiyo, ni suala tu la upanuzi Kwa vile amezungumza hapa kwamba kuna eneo ambalo tayari limeshatolewa tunaomba tuchukue wazo hili tuweze kuangalia namna gani ile Kampasi iliyopo pale Zanzibar inaweza kupanuliwa kwa ajili ya kwenda eneo hilo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja. Nakushukuru sana.