Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Rashid Abdalla Rashid (5 total)

MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga tuta kuzuia maji ya Bahari ya Hindi yasiathiri mashamba na mazao ya Wakulima wa Vijiji vya Nanguji, Jundamiti, Mwambe na Kiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Abdalla Rashid, Mbunge wa Jimbo la Kiwani, kutoa maelezo mafupi yafuatayo kuhusu ongezeko la kina cha maji bahari (Sea Level Rise):-

Mheshimiwa Spika, mojawapo ya athari ya mabadiliko ya tabianchi katika dunia yetu ni kuongezeka kwa ujazo wa maji ya bahari (Sea Level Rise). Kwa mujibu wa takwimu za kisayansi zilizopo, kina cha maji ya bahari kimeongezeka kwa wastani wa sentimeta 21. Ili kutimiza lengo la kupambana na mabadiliko ya tabianchi, nchi wanachama wa mkataba zilianzisha mifuko ya fedha kama vile Least Developed Coutries Fund, Adaptation Fund, Green Climate Funds na Global Environment Facility. Nchi zilizoendelea ziliahidi kuchanga fedha na kuziweka kwenye mifuko hiyo. Hata hivyo, kuna changamoto ya urasimu ndani ya sekretarieti ya mifuko ambayo husababisha uidhinishaji wa miradi kuchukua muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdalla Rashid, Mbunge wa Jimbo la Kiwani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ujenzi wa kuta za bahari hugharimu fedha nyingi, ambazo ni vigumu kuzipata kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali itaendelea kuandaa miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kupata fedha kupitia mifuko hiyo na kuwezesha Serikali kujenga kuta hizo mara fedha zitakapopatikana. Aidha, wakazi wa maeneo ya Nanguji, Jundamiti, Mwambe na Kiwani kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge wanahimizwa kuibua miradi ya ujenzi wa matuta wakati wa TASAF ya III Awamu ya Pili ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwezi Septemba, 2021.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Jimbo la Kiwani ili kuepusha wananchi kufuata huduma za Polisi masafa marefu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdalla Rashid, Mbunge wa Kiwani kutoka Mkoa wa Kusini Pemba kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua hitajio la Kituo cha Polisi eneo la Kiwani na kwa sasa wananchi wa Kiwani wanapata huduma ya polisi kutoka katika Kituo cha Polisi Kengeja ambacho kipo umbali wa kilometa tano tokea Kiwani Central.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa sehemu ya Kiwani hakuna eneo lililotengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkoani kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi na nyumba za makazi ya askari.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya pamoja na wananchi ili kutoa eneo kwa Jeshi la Polisi litakalotosha kwa mahitaji ya ujenzi wa Kituo cha Polisi pamoja na makazi ya askari, ili Jeshi la Polisi liweze kutoa huduma karibu na wananchi katika eneo hilo la Kiwani, nashukuru.
MHE. MARIAM AZZAN MWINYI K.n.y. MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga tuta la kuzuia maji ya Bahari yanayoharibu mashamba ya Wananchi wa Vijiji vya Nanguli, Jundamiti, Mwambe na Kiwani katika Jimbo la Kiwani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdalla Rashid, Mbunge wa Kiwani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko ya tabianchi kote duniani kwa sasa yapo dhahiri na athari zake zinaendelea kuonekana hapa nchini. Mojawapo ya athari hizo ni kuongezeka kwa kina cha bahari katika maeneo mbalimbali ya fukwe likiwemo Jimbo la Kiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hiyo, Serikali imeanza kufanya upembuzi wa awali kwenye fukwe zilizoathiriwa nchini kutokana na kujaa maji ya bahari ili hatimaye kujenga kingo za kuzuia maji ya bahari kuingia kwenye makazi na mashamba ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza juhudi za wananchi na Mfuko wa TASAF katika Jimbo la Kiwani kwa kuanza kushughulikia changamoto hizi na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Jimbo la Kiwani ni miongoni mwa maeneo yatakayofanyiwa upembuzi yakinifu ili kubaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa baadaye. Ahsante.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaviwezesha vikundi vya uhifadhi mazingira Vijiji vya Chwaka, Kiwani, Jundamiti, Mwambe, Nanguji na Kendwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Kiwani. kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeshachukua hatua za kuvijengea uwezo vikundi vyote vilivyotajwa ili viweze kukua na kujiendesha vyenyewe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kuvipatia mafunzo ya awali yanayohusu taratibu za uendeshaji na uendelezaji wa vikundi vya ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali kupitia Idara ya Vyama vya Ushirika, Zanzibar imepanga kutoa mafunzo kwa Baraza la Wanaushirika la Wilaya ya Mkoani katika robo ya pili ya mwaka huu wa fedha (Oktoba – Disemba 2022).

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar imekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira kwa vikundi vya mazingira pamoja na kuwapatia tunzo ya mazingira na vifaa vya usafi kwa vikundi vinavyofanya vizuri katika uhifadhi wa mazingira, Unguja na Pemba.
MHE. RASHID ABDALLA RASHID aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Ofisi ya Polisi Jamii Shehia ya Kendwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshiniwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdalla Rashid, Mbunge wa Kiwani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Ofisi ya Polisi Jamii inayojengwa Jindamiti katika Shehia ya Kendwa, inajengwa kwa nguvu na michango ya wananchi na wadau na ujenzi wake umefikia hatua ya lenta. Lengo la kujenga ofisi hiyo ni kutumiwa na vikundi vya ulinzi shirikishi vya Shehia ya Kendwa. Wajibu wa Serikali ni kujenga Ofisi na Vituo vya Polisi ambavyo hutumiwa na Askari Polisi katika kudhibiti uhalifu.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kumshauri Mheshimiwa Mbunge aendelee na jitihada za kuwahamasisha wananchi na wadau kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo ili iweze kutumiwa na vikundi vya ulinzi shirikishi kama walivyofanya wananchi wa Chambani, ahsante.