Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rashid Abdalla Rashid (6 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia Wizara yetu hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Napenda sana kumpongeza Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wao kwa ujumla kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutengeneza bajeti hii na hadi kuikamilisha kuileta ndani ya Bunge letu hili Tukufu kwa ajili ya kujadiliwa. Lazima tuthamini nguvu zao, jitihada zao kwa sababu sote tunajua kwamba utayarishaji wa bajeti ya Wizara kama hii unahitaji umakini wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika michango yangu katika Jeshi la Polisi na muda ukiruhusu nitaingia katika idara yetu ya Uhamiaji. Naomba Mheshimiwa Waziri akubali kwamba, Wizara hii kwa maana ya Jeshi la Polisi kwenye Wilaya ya Mkoani ilichukua zaidi ya miaka 20; lilikosa utetezi. Nasema kwamba jeshi hili lilikosa utetezi kwa sababu, majengo yote ya vituo vya Polisi pamoja na Makao Makuu ya Wilaya, basi kimsingi majengo haya hayakubaliki kufanya kazi yakitumika kama ni majengo ya ofisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukianza na Kituo cha Polisi Kengeja hiki kimeoza kabisa na hakifai. Hata Kituo cha Polisi Mtambile nacho kadhalika, hakifai. Tukija kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Polisi Mkoani, hii ndiyo kabisa hayafai kabisa. Kwa sababu, majengo haya yalijengwa kabla ya uhuru. Ni majengo yaliyokuwa yakitumika na Masultani kwa kule Zanzibar. Sasa nilisema yamekosa utetezi kwa sababu majengo haya yalikosa watu wa kuwatetea kwa sababu majimbo hayakuwepo kwenye watu ambao ni makini kwa ajili ya kutetea Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi lilikuwa linaonekana kama ni maadui, kwa hiyo, hata makazi yao yalikuwa yanaonekana vile vile ni ya kiadui adui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mvua sasa zinaendelea kunyesha katika Wilaya ya Mkoani, tena ni mvua kubwa, ofisi hazikaliki, zinavuja. Hapa niliposema kwamba walikuwa na kazi kubwa ya kufanya bajeti ya Wizara, ni kwa sababu walikosa hadidurejea ya kuangalia kwamba bajeti iliyopita kulikuwa na makosa gani? Kulikuwa na mahitaji gani katika Wilaya ya Mkoani? Ndiyo maana hapa Mheshimiwa Waziri katuambia kwamba atajenga nyumba 14 katika Mkoa wa Kusini Pemba, lakini kama angekuwa na hadidurejea za bajeti iliyopita, nadhani angelielekeza kwenye ujenzi wa angalau ile ofisi ya Wilaya ya Mkoani badala ya nyumba 14 kwenye Mkoa wa Kusini Pemba.

Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Waziri ni mtu mmoja mkakamavu, makini sana, kwa sababu katika Wizara ambayo alikuwepo aliwahi kufanya ziara ya kuja kukagua mambo mbalimbali ambapo naamini alipotoshwa, lakini alipokuja na akaupata ukweli, mambo yakaenda vizuri. Sasa hapa nayeeleza haya siyo kwa upotoshaji. Nayaeleza ili aandae ziara na nitaomba tuambatane pamoja twende katika Kituo cha Polisi Kengeja, Kituo cha Polisi Mtambile na Makao Makuu ya Wilaya ya Polisi Mkoani, tuone hali zao zilivyo, wanatia Imani. Hili wakati mwingine linasababisha hata ufanyaji kazi unakuwa ni wa kudorora dorora.

Mheshimiwa Spika, mwezi mmoja uliopita, Makamu wa Pili wa Rais alifanya ziara kwenye Wilaya ya Mkoani, akataka kujua kuna kesi ngapi ziko Mahakamani, ngapi ziko Polisi na ngapi ziko DPP, lakini jibu lililotoka pale ni kwamba kuna kesi 21 bado ziko Polisi zikiwa na miezi tisa zinasubiri ushahidi. Kuna ushahidi mwingine hauhitaji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Abdalla Rashid Abdalla. (Kicheko)

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Haya. (Kicheko)

SPIKA: Ndiyo ubaya wa dakika tano. (Kicheko)

MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, nitamwasilishia kwa maandishi na ninaunga mkono hoja...
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na pumzi ya kuweza kunifanya leo kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi nzuri anayowafanyia wananchi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza naomba nijielekeze kwenye fedha hizi za UVICO-19 ambako Zanzibar nayo ilipata mgao wake na kwa Jimbo langu nami nimnufaika mkubwa katika fedha hizi ambapo zaidi ya madarasa 40 nimepata yenye thamani Shilingi Bilioni Tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zimefanya kazi vizuri kwa sababu katika Ward yangu ya Muhambe kuna shule ambayo kwa Zanzibar ni ya kipekee ambayo ilikuwa inaenda mikondo mitatu, sasa fedha hizi zimesaidia kuondoa mikondo ile mitatu kwa kupata madarasa 29 ya ghorofa ambapo itasaidia sana wananchi wa Jimbo langu watoto wetu kusoma vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni mwendelezo wa majengo ambayo tulishayaanzisha wenyewe kwa nguvu zetu wenyewe, fedha hizi zimeingia na majengo sasa hivi Wakandarasi wako kazini kazi inaendelea vizuri, kwa hili lazima tuipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupeleka mgao kule Zanzibar na Zanzibar nao ikafanya mgao ule na wengine tukanufaika katika fedha zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili uende kwenye TASAF. TASAF vilevile kwenye jimbo langu ni mnufaika mkubwa, nimepata kituo cha afya chenye thamani ya Shilingi ya Milioni 400 kazi inaendelea, kituo hiki kitanufaisha Majimbo mengine mawili ya Chambani na Mtambile kwani ni kituo kikubwa ambacho kitaweza kusaidia kupunguza gharama za wananchi kutoka katika vituo vyetu vidogo kutumia masafa na gharama kwenda katika hospitali kubwa ya Mkoa ya Abdallah Mzee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki ninachoomba ni Serikali iongeze tena fedha kwa ajili ya kupata x-ray pamoja na theater ambapo nimshukuru Waziri Mkuu mwenyewe mbali na kuahidi katika hotuba yake lakini kituo hiki yeye ndie ambaye aliweka jiwe la msingi na akaona kazi inavyoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanakamati wa kituo hiki kama tunavyojua kwamba fedha hizi kuna asilimia 20 ni nguvu za wananchi, wananchi kupitia kamati ambayo wameiteua wanafanya kazi kubwa, waliacha kuvuna karafuu, waliacha kulima msimu wa kilimo wakasimamia kituo hichi na kituo sasa kiko katika hatua ya rangi. Kwa hiyo, lazima tuipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu bado naendelea kuomba Serikali kutuingizia tena fedha ili tukamilishe X-Ray, theater pamoja na uzio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala zima la vijana katika uhifadhi wa mazingira. Katika Jimbo langu kuna vikundi zaidi ya 35 ambavyo vimeshajisajili na vinafanya kazi kubwa ya kutunza mazingira katika maeneo yao. Ninaomba kwamba vijana hawa au vikundi hivi viwezeshwe kwanza kwa kupatiwa mafunzo lakini na fedha kwa ajili ya kufanya kazi zao za upandaji wa mikoko na utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno yangu hayo na maombi yangu hayo na kwa ajili ya kutunza muda, naunga mkono hoja hii ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Pia naomba Hansard itambue kwamba jina langu kamili ni Rashid Abdalla Rashid, na sio Rashid A. Rashid. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme, naisifu na naipongeza hotuba hii ya Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini nataka nijielekeze kwenye Wilaya yangu ya Mkoani kuhusiana na suala zima la Jeshi la Polisi na hasa kwenye miundombinu ya majengo.

Mheshimiwa Spika, Wilaya yetu ya Mkoani ina Vituo vinne ambavyo ni Kengeja, Mtambile, Mkoani na Shidi. Nataka nikwambie kwamba vituo hivi vilianza kujengwa toka mwaka 1926. Vituo hivi vimechoka na kwa kweli havifai kabisa kufanya kazi kwenye Jeshi la Polisi, yaani wafanyakazi wa Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Mkoani wana mazingira magumu sana. Naamini Mheshimiwa Waziri anatambua ubovu na uchakavu mkubwa wa vituo hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye Kituo kikuu ambacho ni Ofisi ya Polisi Wilaya ya Mkoani, kwa kweli hali ni mbaya mno; hii imegeuka kama gofu. Yaani ina mipasuko ambapo miti ile ambayo inaota kwenye viambaza imeota. Mvua hizi zinazoendelea kunyesha kule Zanzibar sasa hivi ukweli ni kwamba askari hawana mahali pa kufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu ni kwamba bajeti ni nyingi kuna bajeti zaidi ya miaka 70 iliyopita haijawahi kugusa Wilaya ya Mkoani kwenye ukarabati wa majengo. Namwomba Mheshimiwa Waziri afanye anavyofanya, lakini katika vituo vinne hivi, kwenye Wilaya ya Mkoani tupate kituo kimoja, kijengwe angalau kiwe na hadhi ya Jeshi la Polisi kama lilivyo Jeshi lenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti ya mwaka 2021 uliopita, niliomba hapa na nikaahidiwa kwamba linachukuliwa na litafanyiwa kazi, lakini cha kushangaza ni kwamba kwenye bajeti hii Wilaya ya Mkoani haikuguswa. Vile vile niseme kwenye jambo hili kuna Kituo cha Polisi Kengeja, hiki ndio ambacho kimeoza kabisa, hakifai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miezi kama nane iliyopita, mahabusu wa pale walivunja na wakakimbia, na walikuwa na kesi mbaya kabisa. Cha kushangaza, matokeo ya kukimbia mahabusu wale, ni kuwahamisha Polisi wote walioko kwenye Kituo kile na kuleta wengine, lakini hakuna hatua madhubuti zilizofanywa za ujenzi au ukarabati wa kituo kile. Naomba Mheshimiwa Waziri alione hili na ajue kwamba hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kuna watumishi wa Polisi kutoka Tanzania Bara na wengine kutoka Tanzania Zanzibar. Watumishi hawa wamehamishwa tangu mwaka 2020. Watumishi hawa bado hawajapatiwa stahiki zao. Kwa kweli haipendezi. Ni watumishi wanaolitumikia Jeshi kwa uzalendo kabisa, lakini tunashindwa kuwapatia hata zile stahiki zao za uhamisho. Wako waliotoka Pemba kuja huku na waliotoka huku kwenda kule, lakini hakuna suala la uhamisho ambalo limefanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna watumishi wa Jeshi la Polisi ambao kipindi kifupi tu kilichopita nadhani sote tuliona, walifanya kitendo kimoja cha kiungwana sana cha kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 2.2 lakini hata barua ya pongezi hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunakumbuka hapa Mwalimu baada ya vita vile vya Uganda wanajeshi walipokuja hapa aliwapa ahsante. Wanajeshi hawa tuliona fedha nyingi walikusanya lakini hata barua ya pongezi hakuna, hili jambo halipendezi. (MakofI)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RASHID A. RASHID: Mheshimia Spika, naona kengele imelia, lakini pia niseme kwamba juzi nilimwona IGP Sirro Arumeru akihimiza ulinzi shirikishi na watu wakachangamka sana… (Makofi)

SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. RASHID A. RASHID: Mheshimiwa Spika, haya naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii na mimi leo niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Kwanza na mimi niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumikia wananchi; lakini hii ni moja kati ya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kadhalika nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi naye kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kuhusiana na hotuba hii ya Waziri Mkuu kwa kuanza na TASAF. Kwanza nishukuru Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya katika jimbo langu la kuniletea shilingi milioni 475 kwa ujenzi wa kituo kikubwa cha daraja la pili, kitu ambacho kitawasaidia wananchi wa Jimbo la Kiwani pamoja na jimbo jirani. Kituo hiki kilipata baraka kubwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kuweka jiwe la msingi lakini na Mheshimiwa Makamo wa Rais Dkt. Mpango kwenda kukifungua. Hata hivyo, changamoto kubwa ya kituo hiki kwa sasa ambayo wananchi tunakabiliana nacho ni vifaa tiba, wakati Makamo wa Rais anafungua kituo kile aliagiza kwamba vifaa tiba kwenye kituo kile vipatikane ili lile lengo la Serikali la kujenga kituo kile na wananchi kupata huduma liweze kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Waziri ambaye anahusika, kwamba sasa hivi vitu ambavyo tunahitaji pale kituoni ni ultra sound X-ray pamoja na kile kiti cha meno, tukianza hivyo vitu kile kituo kitafanya kazi na wananchi wataweza kunufaika na kile kituo na zile ahadi ambazo tuliziweka za kuimarisha huduma za afya tutakuwa tumeweza kuzitekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande huo huo wa TASAF nishukuru huu mpango wa ajira za muda ambao ni programu maalum iliyotekelezwa na TASAF ya kuwapatia wananchi wetu ajira za muda lakini sambamba na kutengeneza miundo mbinu ya barabara kwa kiwango cha udongo. Hata hivyo hapa napo kuna changamoto ndogo ambayo napenda TASAF kwa mara nyingine waweze kuongeza bajeti ili zile kazi ziweze kufanikiwa na kuleta ufanisi wa hali ya juu na zile fedha ambazo zimetumika kwa kuwalipa wananchi ziweze kufanya kazi inavyopaswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwa upande wa mazingira pia nishukuru Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia mradi mmoja mkubwa sana wa shilingi zaidi ya bilioni moja na nusu za ujenzi wa tuta la kuzuia maji ya chumvi katika jimbo langu na jimbo jirani la Mtambile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kazi ni kubwa na kazi hii kwa kweli lazima tushukuru kwamba imewasaidia sana wananchi na wanafunzi ambao walikuwa wanatumia kivuko cha maji, lakini sasa tunapata daraja hili la kuzuia maji lakini kadhalika tunapata njia za kutumia. Nishukuru kwa kuleta fedha hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wizara wa Mambo ya Ndani, nishukuru kwamba tumepiga kelele hapa na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara kwenye Kituo cha Polisi Kengeja na juzi katika kujibu swali hapa alituahidi kwamba tayari wameshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo kile. Haya yatakuwa ni mapinduzi makubwa kwenye kituo kile ambacho kilijengwa tangu enzi za wakoloni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije katika suala la zima hili la habari ushoga. Suala hili ilikuwa niseme kwamba, mpango ule wa akinamama wajawazito kuwa ni lazima kupimwa ni mpango mzuri na umeleta matokeo mazuri sana na mafanikio makubwa yamepatikana. Ninachoomba sasa, sisi tunapiga kelele sana juu ya jambo hili, lakini ninachosema kama kuna taratibu za sheria, kanuni kwamba Bunge liamue sasa kwanza Wabunge wote wapimwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakipimwa hawa Wabunge tutaweza kujua kwamba Wabunge sasa tunatoka tunakwenda kufanya kazi hii ya kuhakikisha tunawalinda wananchi wetu baada ya sisi kuwa tumeshatangulia kupimwa. Sasa kama humu wamo, tunajua kwamba wale watu wa unga kulikuwa kuna Sober house wanaweka na kama humu ndani watakuwa wamo Wasenge na Wasagaji, nao sasa iwepo namna ya kuhakikisha kwamba tunawaweka kwenye Sober house. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia Wizara yetu hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwanza, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri fupi ambayo imejaa mambo yote ambayo yanahusu masuala ya kijeshi. Kipekee nawapongeza watendaji wake ambao wameandaa hotuba hii kwa kweli wamefanya kazi nzuri na wameisoma na tumeifahamu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa upande wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kwa kuwashukuru sana kwa kuwapatia eneo wananchi wa Kimbini Kengeja, eneo ambalo linamilikiwa na Jeshi lakini kuwaruhusu wananchi kufanya shughuli zao pale kwa masharti ambayo wananchi wanayatimiza ya kutojenga, kutouza ili wafanye shughuli za kilimo na za kijamii tu, na wananchi kweli hakuna mgogoro na jeshi wanafanya shughuli zao kama kawaida, na yale masharti na matakwa ambayo wamepewa na jeshi wanayafuata.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikwambie kwamba wananchi wa Kengeja Mwambe wanashukuru sana jeshi la wananchi kwa kuwapatia eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar tuna school mbili ambazo zinamilikiwa na jeshi. Kuna School ya Nyuki iliyopo kisiwa cha Unguja na na School ya Ally Khamis Camp iliyopo Vitongoji Chakechake Pemba. School hii ya Ally Khamis Camp ni miongoni mwa school zinazofanya vizuri sana kwa upande wa Pemba na hata kwa Zanzibar. Inafanya vizuri kwa upande wa msingi, na pia inafanya vizuri kwa upande wa sekondari. Nilikuwa naomba tu hata Mheshimiwa Waziri, najua hana muda mrefu katika Wizara hii, lakini afanye jitihada za makusudi za kufika Kisiwani Pemba na kwenda kuikagua school hii aone jinsi watoto wanavyofanya vizuri katika masomo yao na ukakamavu ambao wanao, na matokeo bora ambayo wanayapata katika kila mwaka kwenye mitihani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri atambue kwamba, skuli hii ina changamoto ya mabweni ya wanafunzi wa kike na wa kiume, ili wanafunzi wafanye vizuri lazima wapate mahali pazuri pa kusomea. Ningeomba Mheshimiwa Waziri atenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika skuli ile ili watoto waendelee kufanya vizuri na kulijengea heshima Jeshi la Wananchi, lakini pia na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, katika Kambi ya Jeshi la Wananchi katika eneo la Uwanja wa Ndege, makazi yao kwa kweli siyo mazuri. Wanajeshi wale wanafanya kazi kwa uzalendo mkubwa sana kama lilivyo Jeshi lenyewe, na yale maadili yao ambayo wanayo, lakini kwa kweli yale majengo yaliyoko katika eneo lile la uwanja wa ndege hayaridhishi kabisa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe kwamba, katika bajeti yako siyo kambi kubwa sana lakini ni ulinzi mkuba kwa uwanja wetu wa ndege hasa kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sasa hivi miongoni mwa miradi yake mikubwa ni kuutanua uwanja wetu wa ndege wa Pemba ili ndege kubwa ziweze kutua. Sasa kwa style ile ya nyumba zile au ofisi zile au kambi ile ya jeshi kwa kweli, haileti picha nzuri.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri utakapofanya safari yako upite huko uone. Najua kwamba, Jeshi lina maadili, hawawezi kila taarifa wakazitoa, lakini hili kwa sababu wanatulinda nasi tulioko humu tunawatetea, ni vema ile kambi nayo ikafanyiwa ukarabati mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo alilieleza katika ukurasa wa 14 la kuendelea kutoa huduma za afya kwa Maafisa, wapiganaji na wananchi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Ninakiri kwamba, katika kisiwa chetu cha Pemba kuna hospitali kubwa ya Jeshi ambayo inatuhudumia wananchi wengi, lakini hospitali hii ina upungufu wa vifaatiba. Ameeleza hapa kwamba, wanao mpango wa kununua vifaatiba, kaviorodhesha, ukiangalia katika ukurasa wa 14 utavikuta. Nimuombe Mheshimiwa Waziri na ile Hospitali ya Jeshi ya Vitongoji tunaomba na wao wapelekewe vifaa hivi ili huduma zile za tiba tuweze kuzipata vizuri pale Jeshini na kwa nidhamu nzuri ambayo tunaipata kutoka Jeshini.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo jingine ambalo Jeshi la Wananchi Tanzania kwa upande wa Zanzibar limefanya ni jambo kubwa sana na ni jambo la kushukuru sana. Jeshi hili wamefanya uwekezaji mkubwa katika eneo la Migombani, miongoni mwa uwekezaji ambao wameufanya ni ujenzi wa kituo cha mafuta pale maeneo ya Migombani, kituo ambacho kinatoa huduma masaa 24 pamoja na huduma za kifedha ambapo wananchi wa Zanzibar wanaamini kwamba, time yoyote ambayo unahitaji kupata huduma pale Jeshini unazipata. Kwa hiyo, tuwashukuru na tunawapongeza sana kwa kazi hii kubwa ambayo wameifanya, ni uwekezaji mkubwa na wanaendelea kujenga maduka mengi na makubwa ya kisasa kabisa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, kengele tayari ya kwanza imeniashiria huko na umeshanionesha, hata niombe dakika moja nizungumzie kidogo tu kwa upande wa JKT. Kwa upande wa JKT nao wanafanya vizuri na wanachukua vijana wetu hawa wa kujitolea, wanawajengea uzalendo na ujasiriamali. Ninaomba sana kwamba, katika kuwajengea ujasiriamali huu basi lazima kule JKT wajipange kwa vifaa ili watoto wetu wanapotoka kule, mbali ya kutegemea ajira hizi kupitia vyombo vya ulinzi na usalama na wao wakitoka waweze kujiajiri na wasikae tu mitaani na kusubiri kazi hizi za ulinzi. Vinginevyo hawa watu wamefundishwa uzalendo, wanaweza kutumia silaha vizuri, ndiyo sasa mara tunakuja kukuta hawa watu wanatumia silaha mitaani vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Niungane na wenzangu kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza mafungu ndani ya bajeti za Wizara zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri Engineer Masauni pamoja na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa anazozifanya na hasa Engineer Masauni, nimwambie kwamba ana Naibu Waziri wa kazi sana, ameshatembelea katika maeneo yetu na kuona matatizo mbalimbali ikiwemo Kituo cha Polisi Kengeja. Kaenda kukishuhudia mwenyewe na kuona kwamba kituo hiki kina hali ngumu sana. La kushukuru ni kutuambia kwamba ndani ya mwaka huu wa bajeti zimetengwa kiasi cha shilingi milioni 247 ili kwenda kuanza ujenzi wa kituo kile ambacho kimejengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nije katika upande wa Polisi Jamii, Polisi Jamii katika jimbo langu wamefanya jitihada kubwa na jitihada hizi zilifanyika kwa sababu ya kuahidiwa na RPC wa wakati huo ndani ya miaka 10 iliyopita na tukaweza kama wananchi kujenga zizi pale na sasa limefikia hatua ya kuezekwa na tayari hili nimeshaliombea sana tangu akiwa Mheshimiwa Simbachawene ambaye aliniahidi kwamba tutatumia Mfuko wa Tuzo na Tozo kwenda kukuezekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Masauni pia ameshaniahidi kwamba ujenzi huu wa Polisi Jamii tutakwenda kumaliza kuezekea, lakini mpaka sasa hivi ninapozungumza hakuna kinachoendelea. Nimwombe sana Mheshimiwa Masauni akanimalizie jengo langu hili la Polisi Jamii katika huu Mfuko wake wa Tuzo na Tozo ili wananchi waweze kuona umuhimu wa nguvu zao walizozitumia pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kingine ni Kituo cha Polisi Mkoani, ni kweli kituo hiki sasa hivi kinaendelea kujengwa, lakini nadhani changamoto zake Mheshimiwa Waziri anazijua kwamba amepata fedha tangu mwezi Desemba, 2022 na ujenzi wake umekwenda kuanza juzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni vizuri Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha akatuambia alikumbwa na tatizo gani hata kituo hiki kutoka Desemba hadi ujenzi umeanza Mei na ujenzi wenyewe nimwambie Mheshimiwa Waziri unahitaji usimamizi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamejengwa lakini ukuta umekaa upande, jana ukuta wameubomoa, nadhani Kamishna wa Zanzibar na yeye yupo hapa, afuatilie aone ni kwa nini huyo Engineer anaendeleza ujenzi huo pasi na umadhubuti, pesa milioni 700, ni pesa za kutosha kwa ajili ya huo ujenzi, lakini inaweza kutokea kwamba fedha zisitoshe kwa hali hiyo ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Ofisi ya NIDA, Wilaya ya Mkoani, Mheshimiwa Waziri anajua kwamba NIDA, Wilaya ya Mkoani hakuna Ofisi kuna kaofisi kadogo, kachumba, kastoo wameazimwa pale wilayani, shughuli zote zinafanyika humo humo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hili ni afadhali atoke mwenyewe aje akague ile ofisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, kuna suala zima la Ofisi ya Uhamiaji ambayo inaendelea kujengwa katika Wilaya ya Mkoani. Ofisi hii mkataba wake wa ujenzi kati ya Wizara na mkandarasi unamalizika Agosti, 2023. Ujenzi bado uko katika hatua nzuri, lakini niombe mkandarasi wampatie fedha ili aweze kumaliza ile ofisi kwa wakati ili wananchi wa Wilaya ya Mkoani tuweze kupata huduma kutoka katika Jeshi letu la Uhamiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna matatizo makubwa katika Jeshi letu la Polisi Mkoa wetu wa Kusini Pemba. Jeshi linafanya kazi vizuri, lakini pesa za Other Charge kwa maana ya OC hawapati fedha za kutosha. Tunajua kule tuna Viongozi Wakuu wa Serikali ambao wanaenda Pemba na huduma ambayo inatakiwa kutoka Jeshi la Polisi ni kuongoza misafara na mambo mengine, lakini inapotokea hizo shughuli kwa kweli ma-RPC wale tunawapa wakati mgumu sana wa kuona namna gani misafara ile wataiongoza kwa sababu fedha hawana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, hili suala la OC Mheshimiwa Waziri alifanyie jitihada za kutosha kwa hawa ma-RPC, wanapata shida kubwa kwelikweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ni kwamba, tunaomba tupate usafiri kwa patrol za hawa askari wetu. Askari wanafanya kazi za kutosha, lakini wakati mwingine wanaenda kwa miguu au watumie usafiri wa hizi bodaboda za kawaida, haipendezi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani sana kuona askari wetu wa kule Pemba au Zanzibar kwa ujumla wanafanya kazi za doria kama ambavyo wanazifanya askari wenzao wa huku bara. Inapendeza na inatia moyo, lakini unamkuta askari anatembea kwa miguu kufuata mhalifu ni shida. Hilo naomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi, bodaboda milioni tatu, milioni tatu na nusu, Waziri atupatie angalau bodaboda 12 kule Pemba, kila mkoa upate bodaboda sita ziweze kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)