Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Zahor Mohamed Haji (8 total)

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuza: -

Je, Serikali inaweza kutoa idadi na aina ya mikopo ya Zanzibar baada ya makubaliano na kuiwezesha Zanzibar kukopa yenyewe?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 15 cha Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepewa mamlaka ya kupokea misaada yenyewe kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Kwa mujibu wa kifungu cha 3 na 13, mamlaka ya kukopa na kutoa dhamana yamewekwa chini ya Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anaweza kuyakasimu kwa Waziri wa Fedha wa SMZ baada ya kushauriwa na Kamati ya Kitaifa ya Madeni yenye Wajumbe toka pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, yaani 2019/2020 - 2021/2022, thamani ya mikataba ya mikopo kutoka vyanzo vya nje iliyosainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya SMZ ikiwemo barabara, afya, elimu na mapambano dhidi ya janga la UVIKO-19 ni takribani shilingi trilioni 1.1. Ahsante.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, vikao vinavyopokea na kujadili changamoto za Muungano bado vipo na lini vilikaa mara ya mwisho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa kuwa vikao vya kupokea na kujadili changamoto za Muungano bado vipo na vitaendelea kuwepo kutokana na umuhimu wake kwa mustakabali wa Muungano wetu.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kulitaarifu Bunge kuwa, kwa mwaka 2021/2022 vikao hivyo vilifanyika kwa mujibu wa mwongozo huo ambapo kikao cha Kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya kushughulikia Masuala ya Muungano kilifanyika Tarehe 24 Agosti, 2021. Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuwasaidia Wananchi wa Mwera ambao hawakuingizwa TASAF na wanaishi chini ya viwango vya umaskini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unatekelezwa katika halmashauri 184 za Tanzania Bara na Unguja na Pemba katika vijiji, mitaa na shehia zote 410 (shehia 259 kwa Unguja na 151 kwa Pemba).

Kundi la kwanza la wanufaika wa TASAF waliingia kwenye Mpango mwaka 2014. Hata hivyo, si maeneo yote yalifanikiwa kuingia katika kipindi hicho. Kundi la pili liliandikishwa na kuanza kupata ruzuku mwaka 2021, ambapo Mwera waliandikishwa walengwa 924. Kundi hili ni la Walengwa ambao hawakuwa wamefikiwa katika kipindi cha kwanza na hivyo kukamilishwa kwa asilimia 100 ya idadi ya mitaa, vijiji na shehia zote nchini kuwa na wanufaika wa TASAF ikiwemo Jimbo la Mwera.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani kwa viongozi wanaowanyima wananchi kwa makusudi haki yao ya kuwa wanufaika wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali namba 18 lililoulizwa na Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji naomba kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini. Nataka nimwakikishie yeye na watanzania wote kwamba tutaendelea kufanya kazi na kazi itaendelea.

Mheshimiwa Spika, Sasa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji Mbunge wa Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, zoezi la utambuzi wa wanufaika wa TASAF ni zoezi shirikishi na hujumuisha Wataalam kutoka Halmashauri, Maafisa wa TASAF, Wananchi wa maeneo husika yanayosimamiwa na viongozi wa vijiji/mitaa/shehia.

Mheshimiwa Spika, inapotokea kiongozi au viongozi wamewanyima haki wananchi kwa makusudi bila sababu yoyote ile hatua zifuatazo huchukuliwa dhidi yao: -

(a) Endapo uongozi wa vijiji/mitaa/shehia utashinikiza kuondoa majina ya kaya kwenye orodha ya utambuzi bila kuafikiwa na jamii, zoezi la utambuzi husitishwa na taarifa hupelekwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri/Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar) na nakala hupelekwa kwa Mkurugenzi wa TASAF.

(b) Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri/Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Zanzibar) huchunguza tuhuma hizo na ikithibitisha tuhuma hizo mhusika husitishwa kujihusisha na shughuli zozote za Mpango wa TASAF. Aidha, baada ya kusimamishwa, mhusika huchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kupewa karipio au kuondolewa kwenye nafasi yake.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti mafuriko ambayo husababisha uchafuzi wa mazingira na kuongeza umaskini katika Jimbo la Mwera?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Jimbo la Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Magharibi A yakiwemo maeneo ya Jimbo la Mwera, hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni pamoja na hatua zifuatazo: -

(i) Kuunda Kamati ya Kukabiliana na Maafa ya Wilaya ya Magharibi A yenye jukumu kuu la kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Wilaya wa Kukabiliana na Maafa wa mwaka 2022; sambamba na kuwaelimisha wananchi.

(ii) Kuandaa mpango wa wilaya wa kukabiliana na maafa ambao umeainisha wadau, majukumu yao na mpango wa utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kufanya tathmini ya kina katika maeneo yote yanayokumbwa na mafuriko nchini ikiwemo maeneo ya Jimbo la Mwera.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, kwa nini Halmashauri ya Magharibi “A” imeweka Sheria ya Kodi na VAT kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge wa Mwera, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za Mfuko wa Jimbo hutolewa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Jimbo, Sura 96 ya mwaka 2009. Aidha, fedha hizi zinatumika kwa kuzingatia miongozo, kanuni na taratibu za usimamizi wa fedha za umma. Kila upande wa Serikali zetu mbili una utaratibu wa usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzizar kufuatilia utaratibu unaotumika na Halmashauri ya Magharibi “A” kwenye Mfuko wa Jimbo. Aidha, dhamira ya Serikali ni kuendelea kutoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa pande zote mbili kwa ajili ya kuboresha huduma za jamii na kuwaletea wananchi maendeleo.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kuleta marekebisho ya Sheria baada ya Serikali kukubaliana kuondoa baadhi ya changamoto za Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mbunge na mtumishi wa Wananchi wa Jimbo la Mwera kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Changamoto zote za Muungano zimekuwa zikitatuliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya Majadiliano na Maridhiano utaratibu ambao umekuwa na mafanikio makubwa. Aidha, katika utatuzi wa Changamoto hizo umeandaliwa utaratibu wa vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kushughulikia Masuala hayo ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu umetumika kwa mafanikio makubwa na kuhakikisha changamoto nyingi za Muungano zinatatuliwa. Hata hivyo, ushauri wa Mheshimiwa Mbunge ni mzuri na Serikali inaangalia uwezekano wa kufanya vikao vya pamoja baina ya SJMT na SMZ ili changamoto zilizotatuliwa kupewa na nguvu ya kisheria, nakushukuru.
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI aliuliza: -

Je, zipi athari za mvua zilizonyesha Novemba, 2023 na Serikali imejipangaje kuzuia athari hizo kujirudia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zahor Mohamed Haji, Mbunge wa Jimbo la Mwera, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha kuanzia Mwezi Oktoba, 2023 hadi sasa, tumeshuhudia mvua kubwa ambazo zimenyesha katika maeneo mbalimbali nchini. Mvua hizo, zimeleta athari mbalimbali ikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa ya milipuko kwa binadamu ikiwemo kipindupindu, matukio ya radi na matukio ya upepo mkali ambayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu, madhara ya kiafya, kiuchumi, kijamii na upotevu wa mali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na athari hizi, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na hali ikiwemo kuandaa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Nino kwa kipindi cha Septemba, 2023 mpaka Juni, 2024. Vilevile, kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa katika mikoa 18 nchini, kufuatilia mwenendo wa majanga, kutoa tahadhari kwa umma kupitia Kituo chetu cha Oparesheni na Mawasiliano ya Dharura na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupitia utekelezaji wa mikakati na mikataba ya Kikanda na Kimataifa, ikiwemo Mkakati wa Kimataifa wa Sendai wa Upunguzaji wa Athari za Maafa wa Mwaka 2015/2030; na Mkataba wa Makubaliano wa kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Oparesheni za Dharura cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, yapo madhara ambayo kwa msingi wake wa kuwa majanga ya asili pale yanapotekea hata athari zake hujirudia. Hivyo, Serikali imeendelea kujumuisha athari za majanga hayo katika mpango wa uzuiaji na urejeshaji wa hali pale inapobidi, ahsante.