Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zahor Mohamed Haji (6 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naomba kwanza kukishukuru Kiti chako. Vilevile naomba nishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuweza kuwasilisha kwetu hapa bajeti hii ambayo ndani yake mna changamoto nyingi, lakini naamini Bunge hili ndiyo sehemu sahihi kwa ajili ya kupatia ufumbuzi baadhi ya matatizo yao mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunaapishwa hapa ulitukabidhi Katiba na Katiba hii kabla ya kuikabidhiwa tulikula kiapo. Maana yake kama sikosei ni wajibu wa Bunge hili, kwa sababu Katiba hii inako ilikotoka mpaka ikaja hapa pamoja na changamoto zote, lakini kubwa ni kwamba tuliapa kuilinda Katiba hii, nadhani mwenyewe umesema hivyo.

Kwa hiyo, mimi naomba kwa wenzetu wa Wizara ya Katiba na Sheria, mimi si mwanasheria by profession lakini najaribu kuisoma hii kwa sababu ushauri wako umesema someni, someni, someni, nilikuwa najaribu kuangalia hasa vitu vinavyoitwa changamoto na hapa nataka nijielekeze kwenye changamoto za mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ikikupendeza ninukuu Katiba yako hii kwenye Sura ya Saba, Sehemu ya Kwanza na Sehemu ya Pili. Inasema: “Sehemu ya Kwanza, Mchango na Mgawanyo wa Mapato ya Jamhuri ya Muungano”.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zahor, tusomee Ibara.

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara inasema…

NAIBU SPIKA: Ibara namba ngapi?

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 133.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ninukuu, inasema hivi: “133. Serikali ya Jamhuri ya Muungano itatunza akaunti maalum itakayoitwa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja”…” Naomba kuishia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba twende kwenye Sehemu ya Pili, Ibara ya 135, inasema: “135.-(1)Fedha zote zitakazopatikana kwa njia mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, isipokuwa fedha za aina iliyotajwa katika ibara ndogo ya (2) ya ibara hii, zitawekwa katika mfuko mmoja maalum ambao utaitwa Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali.” Naomba niishie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yangu ni nini? Nimesema tulikubaliana kuilinda Katiba hii, ombi langu kwa wenzetu wa Wizara ya Katiba na Sheria; nimekuwa nikifuatilia na nikisikiliza maeneo mengi sana ibara hizi kila siku vinapigiwa kelele. Kwa hiyo, naomba Kiti chako na Bunge lako, endapo tutaona kwamba ibara hizi ni tatizo tokea Katiba hii imetengenezwa na ibara hizi kuwekwa kama sikosei ni mwaka 1984, maana yake tunalo tatizo sisi wenyewe kama Bunge kutokusimamia Katiba ambayo tumeapa kuilinda; ombi langu kwako, tulinde Katiba hii; hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, nimefuatilia mijadala mingi kuanzia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mpaka hotuba ya leo ya kaka yangu, Mheshimiwa Prof. Kabudi, lakini nimefuatilia michango ya Waheshimiwa Wabunge, wengi wakizungumzia juu ya ukosefu wa fedha za vitendea kazi na ukosefu wa fedha za maendeleo kwenye maeneo mbalimbali.

Sasa ambalo nimeliona kwa haraka haraka, inawezekana nitakosea mtanisahihisha, kubwa ni kwa sababu sisi kama Bunge la Jamhuri ya Muungano tumeacha kufanya kazi yetu ya kuilinda Katiba hii ya kwamba ni kusimamia na kuishauri Serikali. Ndiyo maana tumeiacha Wizara ya Fedha kuchukua nafasi kubwa ya Serikali Kuu yenyewe kuamua nini ifanye nini isifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ambalo nimeliona kwa haraka haraka, inawezekana nakosea, mtanisahihisha; kubwa ni kwa sababu sisi kama Bunge la Jamhuri ya Muungano tumeacha kufanya kazi yetu ya kuilinda Katiba hii ya kwamba ni kusimamia na kuishauri Serikali. Ndiyo maana tumeiacha Wizara ya Fedha kuchukua nafasi kubwa ya Serikali Kuu yenyewe ya kuamua nini ifanye nini isifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapitisha bajeti hapa kama Wabunge, lengo letu na imani yetu ni kwamba tunakwenda kutekeleza kitu ambacho tumekipanga. Sasa ushauri wangu ni mdogo tu, kwamba kwa sababu Katiba hii imetupa nafasi ya kuunda Joint Financial Account na Joint Financial Committee. Ombi langu ni kwamba turudi kwenye basics hizi za sheria, kwamba Katiba hii tukiisimamia Wizara ya Fedha ifanye kazi zake mbili tu; moja, kutengeneza policy ambayo itatuwezesha kutafuta fedha na pili, ifanye kazi ya kukusanya fedha, period. Ili tuwaondolee wenzetu wa fedha makelele kwamba hamtupi, hampendi, hamtaki. Siyo kama hawapendi, lakini fedha haitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Bunge hili lifanye kazi yake ya kusimamia na kushauri ili liwe na nafasi ya kuweza kusema; kwa sababu nadhani tunayo Appropriation Committee hapa, sasa hii ifanye kazi ya kusema tumekusanya mbili; hizi zitakuwa za kazi hii na hizi zitakuwa na kazi hii. Wizara ya Fedha ifanye kazi zake mbili tu ya kutengeneza policy na kukusanya fedha ili Bunge hili liamue kwamba fedha hizi zitumike kwa aina eneo gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kwa kuwapongeza wataalam wetu wa Wizara ya Mambo ya Nje wakiongozwa na mama yetu, hakika ndani ya nafsi yangu nafarijika kwamba Wizara imepata mtaalam ambaye kwa kweli amelelewa na kukulia ndani ya chombo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni muda mfupi nimewahi kufanya kazi naye lakini ndani ya nafsi yangu sina mashaka na uwezo wa Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake lakini Pamoja na hayo Wizara ikiongozwa na Waziri pamoja na wataalam wake ombi langu kwao warudishe heshima ya Taifa letu, warudishe umoja wa nchi yetu mbele ya jumuiya za kimataifa, tulitetereka kidogo hasa kwa sababu ya kutokuendana na wenzetu na mawazo ya wenzetu pamoja na kwamba sisi tunamini, lakini ni wajibu wetu kama walimwengu ambao tunaishi na wenzetu maana yake lazima tuishi na wenzetu ili tuweze kwenda nao pamoja na yale yote ambayo yanatupa changamoto kama walimwengu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mdogo ni suala la covid ambalo kwasasa nashukuru sana tumeanza kulivalia njuga na ninaamini sasa taaluma itatolewa na hatua za tahadhari zitaendelea ili tuendelee kuishi kama walimwengu, Tanzania siyo sehemu ya pekee Tanzania inaishi kama wanavyoishi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri Wizara ya Mambo ya Nje ni taaluma pekee, ni taaluma unique, siyo kila mmoja anaweza aka-practice mambo ya uhusiano wa kimataifa, ni taaluma iliyotukuka. Siyo kila mmoja anaweza kupangwa kwenda kufanyakazi Wizara ya Mambo ya Nje. Tumejifunza muda mfupi au miaka mchache iliyopita Pamoja na kwamba ni mamlaka ya Wizara yetu ya Utumishi kuweza kumtumia mfanyakazi yeyote kumpeleka popote ombi langu kwa Wizara yetu ya Utumishi lakini vilevile kwa wenzetu wa Wizara ya Foreign Affairs ikae ifanyekazi na wenzetu wakubaliane kwamba siyo kila mmoja anaweza akapangwa kwenda kufanyakazi hasa za kidiplomasia ndani ya Wizara hii. Tunaweza tukapeleka mwandishi wa habari, mhasibu, mpiga picha lakini kazi zinazohusu diplomasia tuwaache wanadiplomasia wafanyekazi za diplomasia ili nchi yetu iweze kufanyakazi zake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa maana hiyo hiyo ningeomba sana sasa tumezungumza wenzetu wengi hapa wamezungumza kuhusu economic diplomacy mana yake tunalazimika sasa kuondoka tulipokuwa tupo huko miaka ya nyuma, sasa hivi tunatakiwa kuangalia ni Nyanja gani na nani ambaye tunaweza kushirikiana naye hasa inapokuja maslahi ya Taifa letu. Marafiki wako wengi, lakini waswahili wanasema nionyeshe Rafiki yako nitakwambia wewe ni mtu wa aina gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa na mirengo ya siasa; kuna wenye siasa kali za kijamaa, kuna mabepari kuna na wasiofungamana, naamini kidogo tumeanza kutoka hapo sasa hivi tunaangalia economic diplomacy.

Ombi langu kwa Wizara tuchague marafiki zetu na tusione haya kuchagua ili mradi Taifa letu litafaidika pamoja na wananchi wake kuhakikisha kwamba tunatengeneza ajira, lakini na biashara zinafanyika ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imejaaliwa kuwa na bidhaa nyingi sana hasa zinazotokana na kilimo. Ombi langu sana kwa Wizara hii ifanye kazi ya makusudi wala isiogope kufungua balozi kwenye maeneo mengine eti kwa sababu tunaogopea gharama. Gharama ni pesa, lakini pesa zinatafutwa, lakini hakuna kazi kubwa duniani kama kutunza marafiki, ni kazi ya gharama, ni kazi ngumu, lakini lazima sisi kama Tanzania tuhakikishe kwamba tunaishi kama wanavyoishi wenzetu tuweze kuwatunza marafiki zetu. (Makofi)

Ombi langu sana tutafute mataifa ambayo balozi zetu zitafunguliwa, lakini kubwa liwe ni kuhakikisha kwamba Taifa letu linafaidika ili tuweze kufanyabiashara za ndani na nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo naomba nizungumzie hoja moja kuhusu wataalam wetu, ni kweli kwamba tunafundisha, ni kweli kwamba watoto wetu vijana wetu wanasoma kwenye maeneo mbalimbali, ombi langu kwa Serikali wenzetu hawa kama mtakumbuka hotuba aliyoisoma Mheshimiwa Waziri ukiipitia kwa ndani utagundua kwamba mambo mengi waliyoyapanga walishindwa kuyatekeleza kwa sababu tumeshindwa kuwapatia uwezo. Sasa tutaendelea kuwalaumu, tutawashambulia, lakini ukweli ni kwamba sisi kama Bunge tumepitisha bajeti, tumeidhinisha walichokitaka, bahati mbaya sana tulishindwa au Serikali haikuwapatia fedha kama ambazo walizoomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali ili wenzetu waweze kufanya kazi zao na ili kesho na kesho kutwa tuje tufanye tathmini walichokiomba na walichokifanya, naiomba sana Serikali tuwapatie uwezo wenzetu ili waende wakafanye majukumu waliyojipangia ili Taifa letu lifaidike. Kama unajipangia kazi za Serikali halafu Serikali yenyewe haikuwezeshi maana yake ni kama vile tunatwanga maji kwenye kitu. Ombi langu kwa Serikali tuhakikishe kwamba tunawapatia wenzetu hawa ili waweze kufanyakazi zao kama walivyojipangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo linaweza likaungana na hili niliwahi kusema kule nyumba kwamba tutawalaumu Wizara zote tutazilaumu tutalaumu Mambo ya Nje, Polisi, Jeshi tutawalaumu Wizara ya Maji, Miundombinu tatizo siyo Mawizara, tatizo ni sisi wenyewe kama Wabunge tumeshindwa kuchukua nafasi yetu ya kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wetu basi kuisimamia na kuishauri ili waweze kupatiwa fedha wenzetu hawa wahakikishe wanatekeleza majukumu yao, then ndiyo tuje tuwahukumu hapa kwamba kuna kitu hawakutekeleza tuanze kulalamika. Vinginevyo kila mwaka tutapitisha bajeti haiendi, kila mwaka tutapitisha bajeti kwa sababu tumeiachia Wizara ya Fedha kwa mujibu wa makubaliano yetu kwamba ndiyo iamue nani impe, nani isimpe, impe lini, impe kiasi gani, hili halijakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nawaomba sana naiomba sana Serikali naliomba sana Bunge hili tuone namna gani tunaweza kusimamia au kufanyakazi yetu kama Wabunge kusimamia Serikali lakini kuhakikisha yale tunayoamua humu ndani basi yanatekelezwa kwa mujibu ambavyo tumeamua, vinginevyo sisi hatufanyi wajibu wetu na Serikali hatuisaidii ili iweze kuwahudumia wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nishukuru kiti chako kwa ufupi. Pili, naomba niseme kwamba ninashikiri au niko kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama. Nimekuwa nikijaribu kuwasikiliza Waheshimiwa Wabunge hapa kwa muda mrefu toka tumeanza Bunge kuna jambo linaendelea kujitokeza sana. Sasa naomba hasa wenzetu wa Serikali hili walitafakari tena kwa kina na hatua za dharura zichukuliwe.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi tunapata mafunzo au tunachukua hatua tunapoona matokeo yanazidi kukithiri. Siku chache zilizopita tulisikia tatizo dogo kutoka kutoka TRA kwamba mifumo kila siku iko chini lakini baadaye tukasikia tatizo la TANESCO kwamba watu hawawezi kununua LUKU lakini hapa kiongozi amerudia tena kuongelea suala hili inaonekana limerudiarudia. Ombi langu kwa TANESCO, tuko kwenye cyber war, kuna kitu tunaita cyber war na kitu tunaita cyber-crime, umeme ndiyo unaotumika kupeleka athari zote kwenye mifumo yetu. Naomba sana na hili TANESCO mliangalie sana, vinavyotokea havitokei kwa bahati mbaya, ni mambo yanayopangwa na yanapangwa yatokee ili siku moja tu-collapse. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie wenzetu kwamba TANESCO tumewapa kuongoza Serikali kwa sababu leo maji tunalipia kwa internet, umeme tunalipia kwa internet maana yake ni kwamba hata benki zetu zinatumia internet kufanya mambo yake maana yake ndiko kelele ziliko. Hata hivyo, internet leo inawezeshwa kupitia kwenye umeme, ombi langu kwa TANESCO haya mambo hayaji kwa bahati mbaya iko siku sote tuta-faint kwa sababu tunaelekea kwenye cashless economy ni kwamba ni mitandao ndiyo inayotuwezesha kufanya mambo yote maana yake tumewapa kuendesha Serikali kwa kutumia umeme. Tunawaomba sana muwe makini na suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkiangalia attempt zinazofanywa BoT, iko siku tutawaomba hapa waje watuambie attempt za mara ngapi zinafanywa kwenye benki zetu kwa kutumia internet ambazo zinapitia kwenye umeme. Tunawaomba sana tumewapa shirika hili au taasisi hii muweze kutulindia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu alitukumbusha kwenye backup maana yake tuweze kujilinda lazima tuwe na plan B na plan C kwenye kujilinda ili tusifikie siku tukawa hatuwezi au kila kitu kime-paralyze kwa sababu ya internet kumbe siyo internet ni kwa sababu ya umeme. Kwa hiyo, nawaomba sana mlitilie maanani suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili naomba uendelee kutusaidia wataalam wetu walikumbuke kwamba umeme ndiyo unaotumika kupitisha kila kitu. Juzi Marekani nadhani mmeona wataalam, Serikali ya Marekani ililazimika kuwalipa wataalam wa IT ambao huku tunawaita hackers, si kwa sababu walipenda kwa sababu system zao za mafuta ziliingiliwa na hackers, waliwalipa! Pamoja na policy zao kwamba hatuzungumzi na watu ambao hawahusiki na system zetu lakini waliwalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba shirika letu au Wizara yetu ilisimamie suala hili ili kuhakikisha kwamba hatufiki mahali tukashindwa kufanya mambo yetu kwa sababu tumeshindwa huko. Lazima tuwe na wataalam wetu wa ndani ambao watalinda mifumo yetu ili tusishindwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru. Mimi napenda kuchangia kitu kimoja tu, lengo la Serikali yetu hii ni kuhakikisha kwamba tunaondoka tulipokuwepo tunapiga hatua za mwendokasi ili kuhakikisha wananchi wanayaona na wana-feel maendeleo ambayo Serikali yao imeamua kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewasikia Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wakizungumza juu ya maendeleo au mikwamo ya maendeleo inayotokana na jitihada za wananchi, hasa wakulima wetu. Mapendekezo yalitoka hapa na moja ya eneo ambalo bado hatukui, kila siku tunaendelea kupiga mark time, ni eneo hili tunaloliita la road and fuel toll, maana yake ni nini? Ukiangalia statistics za matumizi yetu ya mafuta kwa miaka yote hatukui, leo tuna miaka saba, lakini magari yanaendelea, kampuni zinakuja, mafuta yanatumika, lakini hesabu zinaonekana tuko palepale hatukui. Maana yangu ni nini, tunalo tatizo kwenye hesabu zetu au kwenye statistics zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Serikali imeleta maboresho, kwanza mnisamehe mimi si mwanasheria by profession, naomba nisome hiki ili nitafsiri kwa lugha isiyo sahihi au isiyo official. Kifungu 47 kinasema:

“The principal Act is amended in section 4A by deleting paragraph (a) and substituting for it the following:

“(a) Tanzania shillings 363 per litre imposed on petrol or diesel shall be deposited into the account of the Fund:

Provided that, Tanzania shillings 100 per litre imposed on petrol or diesel out of the Tanzania shillings 363 per litre shall be allocated to Tanzania Rural Roads Agency and the remaining Tanzania shillings 263 per litre shall be distributed amongst the Fund and the Tanzania Rural Roads Agency in the manner prescribed in the regulations made by the Minister in consultation with the Minister responsible for local government.”

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Tumekusudia kuondoka tulipokuwa kwenye shilingi 263. Waheshimiwa Wabunge wameomba tuongeze shilingi 100 iwe shilingi 363. Kwanza shilingi 100 hii imewekwa makusudi iende TARURA peke yake, lakini katika shilingi 263 tunayo shilingi 78.90 ambayo na yenyewe inarudishwa kwenye hii ili tuwe na shilingi 178.90 ili tuweze kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwenye hili ningeomba sana kusiwe na mchanganyiko hapa kwamba Waziri kwa kushauriana na nini, hapana. Tuiseme categorically kwamba shilingi 178.90 inakwenda kutumiwa na TARURA full stop. Tusiwape watu nafasi ili tuweze kuja kujitathmini kwamba tulipata hela hii tukaiweka hapa ili ifanyiwe kazi na TARURA. Tusimpe mtu mwingine nafasi ya kuweza kuamua kuwapa au kutokuwapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mchango wangu mimi kwenye hili ni kuipongeza Serikali kwa kusikiliza Wabunge, lakini kuliomba Bunge lako hili tuzungushe wigo hapa tusimpe mtu nafasi ya kuamua yeye. Sisi tumeamua utekelezaji ukafanywe moja kwa moja. Nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kidogo kwenye hoja hii, lakini naomba nianze kwenye kitabu chetu kitukufu, kinaitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba nianze kwenye Kifungu cha 62(1) Sura ya 3 ya Katiba hii. Kuna chombo kimoja kinaitwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba ninukuu: (Makofi)

Kifungu cha 62(1) kinasema: “Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambalo litakuwa na sehemu mbili; yaani Rais na Wabunge.” Naomba niendelee kwenye Kifungu 63 (1): “Rais kama sehemu moja ya Bunge atatekeleza madaraka yote aliyokabidhiwa na Katiba hii kwa ajili hiyo,” lakini 63 (2) inasema: “sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.” Hili ndiyo Bunge la Jamhuri ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee 63 (3) (d) kinasema hivi: “Kwa madhununi ya utekelezaji wa madaraka ya Bunge, laweza (b) kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa Bajeti.”

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie. Nimekuwa nikifuatilia bajeti zetu za miaka mingi, Bunge linakaa kama chombo chenye mamlaka iliyopewa na wananchi, lengo ni kuziandalia Wizara hizi na kuzipitishia bajeti zake kwa mujibu wa zilivyoomba. Marekebisho yanafanyika, lakini hatimaye Bunge linapeleka fedha kwenye Wizara husika. Matokeo yake ni nini? Matokeo yake ni kwamba mara nyingi tunarudi kwenye kuangalia Bunge au Serikali imetekelezaje bajeti kwa mwaka uliopita? Pia kuangalia kwa mwaka ujao.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi kwa masikitiko makubwa tunashindwa au Wabunge tunalalamika kwamba Serikali kupitia Wizara ya Fedha haipeleki fedha zinazotakiwa kama tulivyopitisha. Sasa maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Bunge kama Bunge linafanya kazi yake ya kupitisha lakini Bunge linashindwa kusimamia bajeti iliyoipitisha ili kuhakikisha kwamba kila Wizara inafanya kazi kwa mujibu wa maelekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ombi langu, ukiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Fedha ina majukumu 10 imejipangia pale. Moja katika hayo ni kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza bajeti kama ilivyoahidiwa au ilivyopitishwa na Bunge. Bahati mbaya sana kwamba kwa asilimia kubwa Wizara nyingi tunakuja kuzilaumu hapa kwamba hazikutekeleza; wenye maji wanalalamika, wenye barabara wanalalamika, wenye kilimo wanalalamika, uvuvi wanalalamika, kila Wizara kwa asilimia kubwa tunakuja kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Bunge lako, Bunge lichukue nafasi yake ya kupitisha lakini kusimamia ili miaka ijayo au mwaka mwingine wa fedha tusije kumlaumu mtu, kwa sababu kazi yetu kubwa hapa tumeambiwa sisi kama Bunge ni kuisimamia Serikali na kuishauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama hoja ni hiyo, ombi langu na ushauri wangu kwa mujibu wa kifungu hiki cha 63 (2) naomba basi kushauri kwamba Bunge hili sasa likubali kutunga au kuandaa Kamati ambayo itafanya kazi ili Wizara ya Fedha pamoja na mambo mengine, kazi zake kubwa ziwe mbili: kwanza, kutengeneza sera na ya pili iwe ni kukusanya, period. Hii ni ili Bunge hili lije lifanye kazi ya kusimamia fedha zilizokusanywa na kuzipeleka kunakohusika ili tuje tujiulize wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nilishauri Bunge lako lifanye kazi ya kuunda Kamati ambayo ndiyo itafanya kazi ya uhakika kuhakikisha kwamba kile ambacho tumekipitisha kama Bunge, basi kinapelekwa kwenye Wizara zote na taasisi zote ili baadaye tuje tujitathmini wenyewe na wala siyo Serikali kuja kutuambia hiki sikupeleka. Maana yake kwa taratibu hizi tumewaachia Wizara ya Fedha mamlaka ya kujiamulia nani wampe? wampe nini? Kwa wakati gani? Kwa kiasi gani? Hii siyo kazi ya Wizara ya Fedha, ni kazi ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maneno haya mafupi, naomba kuchangia hoja. Ahsante sana. (Makofi)
The Fire and Rescue Force (Amendment) Bill, 2021
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba kwanza kuishukuru Serikali na pia kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa aliyoifanya na kubwa kuliko yote kuweza kufanya kazi kwa karibu sana na Kamati yetu, jambo ambalo limetufanya kuwa kitu kimoja kwa lengo na maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye Muswada na nitazungumzia mambo matatu. La kwanza, tumekubaliana kwamba kwa mujibu wa Muswada huu, Jeshi la Zimamoto sasa linakuwa jeshi kamili, kwa maana ya kwamba litaingia katika mlolongo wa kijeshi; litafuata kanuni na taratibu zote za kijeshi, wala siyo jeshi kwa maana ya jina. Kwa hiyo, wenzetu wataalamu wafanye kazi zao, wali-train jeshi hili liwe kama jeshi kamili na siyo kwa maana ya kuzima moto tu, lakini kwa maana ya kuwa Jeshi la Akiba wakati wote likihitajika litaendelea kuwa jeshi. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo hiyo, kwa sababu, tumeliita “jeshi,” maana yake ni kwamba, litatakiwa kufuata taratibu zote zikiwemo za mafunzo pamoja na kumiliki silaha. Kumiliki silaha ni kwa sababu, hatuwezi tukawa na jeshi ambalo linamiliki maji, lakini halimiliki silaha. Wenzetu hawa wanafanya kazi kubwa katika maeneo mbalimbali na mara nyingi changamoto zinatokea kwa sababu kwenye moto wako wanaoathirika, lakini wako wanaopenda athari itokee ili wao waweze kufanya uhalifu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Bunge lako kwenye hili lione kwamba tumekubaliana kama Kamati na Serikali kwamba tuliwezeshe jeshi hili ili pamoja na kufanya kazi yao ya msingi ya kuhakikisha wanazuia moto, wanahakikisha wanatoa taaluma ya moto na pia waweze kufanya kazi ya kulinda mali wakati ambapo pia wanazima moto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo kulinda mali tu, kuhakikisha kwamba wanazuia uhalifu, lakini nao wenyewe wanajilinda, kwa sababu mara nyingi askari wetu hawa wanashambuliwa na wanaposhambuliwa wanakuwa hawana uwezo wa kujikinga wao wenyewe kama askari. Kwa hiyo, nashauri Bunge lako lisaidie hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo hiyo, naomba sana; na hili naomba wenzetu wa Jeshi la Polisi, tumekubaliana sasa vyombo vyote hivi vinafanya kazi kwa pamoja kwa maana ya Polisi, kwa maana ya Uhamiaji, kwa maana ya wenzetu hawa wa Jeshi la Zimamoto, wote wanakuwa kwenye umbrella moja. Ombi langu, waendelee kufanya kazi kwa pamoja kwa sababu moja ya msingi, mara nyingi linapotokea tukio la moto wanaowahi kwenye tukio hili ni wenzetu wa Jeshi la Zimamoto, lakini mara nyingi inatokea kwamba, wenzetu wa Jeshi la Polisi wanachelewa ama kupata taarifa ama kufika kwenye eneo la tukio. Kwa hiyo, madhara yake yanakuwa makubwa kwa sababu watu wanavamia; wako watu wabaya na wako watu wema. Kwa hiyo, tatizo letu ni watu wabaya.

Mheshimiwa Spika, ombi langu sasa, mtandao wa mawasiliano kati ya Jeshi la Zimamoto na Jeshi la Polisi kwa sababu, wako chini ya umbrella moja, wawe kitu kimoja ili wapeane taarifa kwa pamoja. Anapotokea fire kama ni advance na mwenzetu wa polisi awe pale ili kusaidia kazi hii ya kulinda watu na mali zao. Tusiwaachie wenzetu wa Jeshi la Zimamoto tu kazi ile kwa sababu kazi yao kubwa na ya msingi ni kuhakikisha kwamba, wanazuia moto usitokee au wanazima moto pale maeneo ambayo janga limetokea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ombi langu na ushauri wangu kwa wenzetu wa Jeshi la Polisi, wawe faster au wawe na haraka kwenye kutafuta taarifa au kuzipokea, kuzichakata na kuhakikisha kwamba wanafika kwenye eneo la tukio kama ambavyo wenzetu wa Jeshi la Kuzima Moto wamefika. Naomba sana hilo.

Mheshimiwa Spika, mwisho kuliko yote, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, kama alivyosema Mwenyekiti wetu, kwamba tuliwezeshe jeshi letu hili liweze kufanya kazi zake kama inavyotakiwa ili tuweze kufanya kazi kubwa ya Serikali, kulinda raia wake, kulinda na mali zao na kuhakikisha kwamba wanaendelea kuishi kwa usalama na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)