Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Maimuna Ahmad Pathan (10 total)

MHE. MAIMUNA A. PATHAN Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza Ujenzi wa barabara ya Masasi hadi Liwale kupitia Nachingwea kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GEOFREY K. MSONGWE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Masasi hadi Liwale kupitia Nachingwea kwa kiwango cha lami ambapo kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa sehemu ya Masasi – Nachingwea – Nanganga yenye urefu wa kilometa 90 ilikamilika mwaka 2014 na sehemu ya Liwale – Nachingwea yenye urefu wa kilometa 130 imekamilika mwezi Juni, 2021. Katika mwaka huu wa fedha 2021/2022, jumla ya shilingi milioni 1,500 yaani sawa na shilingi bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami sehemu ya Masasi – Nachingwea.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili kuhakikisha inaendelea kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha wa 2021/2022, jumla ya shilingi milioni 634 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itabadili utaratibu kuwataka wavuvi wanaotumia ring net kutoruhusiwa kuvua mchana na kuvua chini ya mita 50?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya wavu wa ring net wakati wa usiku yanawezesha kuvua samaki wanaolengwa yaani dagaa pekee na kupunguza uwezekano wa kukamata samaki wasiolengwa yaani by-catch. Aidha, matumizi ya wavu wa ring net kwenye kina cha mita 50 wakati wa maji kupwa kwa upande wa baharini na katika umbali wa mita 1,000 kutoka ufukweni kwenye visiwa na rasi kwa upande wa Ziwa Tanganyika yanawezesha kuwa na uvuvi endelevu kwa kutovua samaki wachanga na kutosababisha uharibifu wa maeneo ya mazalia, makulia na malisho ya samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wavuvi pamoja na wadau wa uvuvi kudhibiti matumizi ya zana haramu katika shughuli za uvuvi ikiwemo matumizi ya ring net kwenye kina cha maji chini ya mita 50 na wakati wa mchana ili kuwa na uvuvi endelevu. Hivyo, kupitia Bunge lako tukufu; Serikali inatoa wito kwa jamii za wavuvi kuendelea kuzingatia sheria za nchi katika kulinda rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya sasa na ya kizazi kijacho.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaunda tena Bodi ya Wataalam wa Ugavi na Ununuzi (PSPTB) baada ya kuvunjwa kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kufuatia uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi uliofanywa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara iliteua Wajumbe wa Bodi ambapo uteuzi wao ulianza Desemba 19, 2021. Ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya Wafugaji na Wakulima katika Wilaya za Liwale, Nachingwea na Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa Niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kumjibu swali lake Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Mkoa wa Lindi Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya ardhi katika Wilaya zote zilizotajwa ikiwemo Liwale, Nachingwea na Kilwa, lakini pia ni pamoja na maeneo ya Lindi Vijijini. Migogoro hii inatokana na kuongezeka kwa mifugo katika maeneo hayo, changamoto ya tafsiri ya mipaka ya ardhi katika vijiji hivyo, usimamizi mbovu wa mipango ya matumizi ya ardhi. Kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo kimsingi ndiyo suluhisho la migogoro ya mwingiliano baina ya watumiaji wa ardhi. Hadi sasa jumla ya vijiji 114 katika Wilaya ya Kilwa, Nachingwea na Liwale vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2204, Serikali imepanga kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 40 ikiwemo Liwale (17), Nachingwea (12) na Kilwa (11) katika Mkoani wa Lindi, ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga uwanja wa Ndege Lindi kwa kiwango cha lami pamoja na kukarabati Uwanja wa Ndege Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ,napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kazi ya kufanya marejeo ya usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Lindi kwa kiwango cha lami. Marejeo ya usanifu wa kina yalifanyika ili kuzingatia mahitaji ya sasa ya kiwanja, ikiwemo kuwezesha utekelezaji wa Mradi wa Gesi katika maeneo hayo. Kwa sasa, Serikali inakamilisha maandalizi ya makabrasha ya zabuni hiyo ili iweze kutangazwa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kiwanja cha Ndege cha Nachingwea, Serikali imekuwa ikifanya matengenezo ya miundombinu ya kiwanja hicho ili kiendelee kutumika ambapo mwaka 2020 ilikamilisha ukarabati mkubwa wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa Kiwanja cha Ndege Nachingwea, Serikali inaendelea na utwaaji wa eneo la ziada ili kujenga kiwanja hicho kwa kiwango cha lami. Aidha, mnamo mwezi Machi, 2023 wataalam wa Wizara walifanya uhakiki wa daftari la fidia na kuwasilishwa kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa idhini, ahsante.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya za Liwale, Nachingwea, Ruangwa na Lindi Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale na Nachingwea ni miongoni mwa Wilaya 64 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi kwa mwaka huu wa fedha. Tayari kiasi cha shilingi 228,942,380 kimeshatolewa kwa kila chuo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ruangwa umeshakamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 2.3 na mafunzo yameshaanza kutolewa. Aidha, kwa Wilaya ya Lindi tayari kipo chuo cha mkoa kinachoweza kutumiwa na wananchi wa Halmashauri ya Lindi Vijijini, nakushukuru.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya marekebisho ya sheria zisizo rafiki kwa wavuvi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/2024 Serikali imepanga kuendelea kupitia na kufanya marekebisho ya Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 ili kukidhi mahitaji ya hali halisi ya sasa ya shughuli za uvuvi. Aidha, Serikali ina utaratibu wa kufanya maboresho ya kanuni mbalimbali za uvuvi mara kwa mara ili kuondoa kero na kuboresha mazingira ya biashara kwa wadau wa uvuvi. Kwa mfano, katika mwaka 2019 Serikali ilirekebisha kanuni kuruhusu leseni ya uvuvi iliyokatwa kwenye Wilaya moja kutumika katika Wilaya zote katika ziwa husika au ukanda wote wa bahari. Pia mwaka 2020 Serikali ilirejelea kanuni za uvuvi kuruhusu ongezeko la kina cha nyavu za makila katika Ziwa Victoria kutoka macho 26 mpaka macho 78 kwa uvuvi wa samaki aina ya sangara.

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na tathmini ya sheria, kanuni, na miongozo iliyopo katika sekta ya uvuvi ili kubaini sheria zisizo rafiki kwa wavuvi nchini na kuzifuta au kuzirekebisha. Aidha, Wizara yangu iko tayari kupokea maoni na ushauri wa wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge juu ya sheria zetu zinazohitaji kufanyiwa maboresho, naomba kuwasilisha.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:-

Je, ni lini tatizo la kukatika umeme mara kwa mara Mkoani Lindi litakwisha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi unapata umeme kutoka katika vyanzo viwili ambavyo ni mitambo ya kufua umeme wa gesi iliyopo Mtwara na Lindi (Somanga).

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kifupi (siku 90), Serikali imeandaa mkakati wa kuongeza upatikanaji wa umeme mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kupeleka jenereta ya megawati 20, kufanya ukarabati wa miundombinu ya kusambaza umeme na kufunga vifaa vinne vya kuzima na kuwasha umeme (Autoclosers) kwenye njia mchepuko. Utekelezaji wa Mipango hii ulianza mwezi Mei, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mitatu ya muda mrefu ni kujenga njia yenye msongo wa kilovoti 220 Songea – Tunduma (mradi huu ulianza mwezi Machi, 2023 na utachukua miezi 18). Kujenga njia yenye msongo wa kilovoti 220 Tunduru – Masasi, Mkandarasi atakabidhiwa eneo la mradi mwezi Juni, 2023. Ujenzi wa njia yenye msongo wa kilovoti 220 Masasi - Mahumbika ambayo upembuzi utaanza mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua nyingine kubwa, Serikali inaendelea na mazungumzo na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) juu ya ujenzi wa kituo kikubwa kitakachozalisha Megawati 300 Mkoani Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii itakapokamilika, hali ya umeme katika mikoa ya Mtwara na Lindi itaimarika sana.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kwa uvamizi wa tembo kwa wananchi na mashamba katika Wilaya za Liwale na Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kuwepo na changamoto ya wanyama wakali na waharibifu wakiwemo tembo. Kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wa mwaka 2020 – 2024. Wizara inaendelea kufanya yafuatayo; kutoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu; kujenga vituo vya askari wanyamapori ili kusogeza huduma karibu na wananchi; kuwafunga mikanda tembo na kuanzisha timu maalum (rapid response teams).

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuwashirikisha wananchi kwa kutoa mafunzo kwa Askari wa Vijiji (VGS) ili kuongeza nguvu ya kudhibiti tembo katika maeneo ya wananchi. (Makofi)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi waliopisha upanuzi wa maeneo ya Jeshi 843 KJ Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kikosi cha Jeshi cha 843 JKT Nachingwea, kilichopo Mkoani Lindi kilianzishwa mwaka 1964. Kumbukumbu zinaonesha eneo husika lilikuwa ni moja ya mashamba ya karanga yaliyokuwa yanamilikiwa na Mzungu aliefahamika kwa majina ya John Molam. Shamba hilo baadae lilitaifishwa na Serikali na kutumika kwa matumizi ya Kijeshi kwa ajili ya kuimarisha Ulinzi katika mipaka ya Kusini mwa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1964 wakati Jeshi wanakabidhiwa eneo hilo, upande wa mpaka wa Mashariki kikosi kilipakana na Kijiji cha Naipingo, baadaye eneo la Jeshi katika mpaka wa upande huo lilikatwa na kuanzishwa Kijiji cha Mkukwe ambacho kilisajiliwa Mwaka 1999. Kwa sasa kikosi kinapakana na Kijiji cha Mkukwe katika upande huo wa Mashariki. Upimaji mpya wa kurekebisha mipaka uliofanyika mwaka 2021 na Hatimiliki yake imetolewa 2023.

Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo hakuna upanuzi uliofanywa wa kuongeza eneo la kikosi, bali eneo la Jeshi ndilo lilipunguzwa na kuanzisha kijiji cha Mkukwe Mwaka 1999. Nashukuru.