Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maimuna Ahmad Pathan (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha siku ya leo kwa kunipia pumzi ya uhai na pia kupata nafasi hii ya Ubunge. Pia nawashukuru akina mama wa Mkoa wa Lindi kwa kuniamini na kunipa nafasi hii ya Ubunge ili niweze kuwatumikia miaka hii mitano. Vilevile nakishukuru chama change, Chama cha Mapinduzi na shukrani za pekee pia ziende kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa alitekeleza vizuri Ilani ya chama chetu kuanzia mwaka 2015 mpaka 2020 jambo lililotopelekea kutubeba Wabunge wengi wa CCM kuingia humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia sana kwenye suala la maji. Ukurasa wa 34 Mheshimiwa Rais alisema kwamba atalipa kipaumbele sana suala la maji na pia alisema sehemu nyingi alipokuwa anazunguka kwenye kampeni wananchi wengi sana walikuwa wanalalamika kuhusu maji hasa maeneo ya vijijini. Kwa kweli tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, amejitahidi sana kutekeleza suala la maji katika maeneo mengi. Kwa Mkoa wangu wa Lindi tunamshukuru sana ametusaidia akina mama kututua ndoo kwa asilimia kubwa sana. Sehemu zilizobakia na changamoto ya maji ni chache sana. Tunaomba Waziri wa Maji na viongozi wengine mnaohusika na suala hilo la maji mjitahidi sehemu zile chache ambazo zimebakia ili nao wanachi wa vijijini waweze kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo napenda kuchangia ni huduma ya afya. Tunashukuru sana Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi imejitahidi sana kuboresha huduma ya mama na motto. Kwa kweli imejitahidi sana ukiangalia kwenye Wilaya ya Nachingwea wamefanya maboresho kwenye jengo la akina mama na watoto, wodi ya wazazi imekuwa nzuri na inahuduma nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambao napenda kuchangia ni kilimo, ukurasa wa 19. Pia nako kwenye suala la kilimo Rais wetu mpendwa amejitahidi sana kutekeleza Ilani hiyo ila kuna changamoto chache tu ambazo tunaomba na zenyewe zitiliwe mkazo ili wananchi wafaidike na Serilikali yao ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Lindi wanalima sana mbaazi, lakini bahati mbaya kidogo mwaka huu na mwaka jana bei ya mbaazi imeshuka sana na Akinamama wengi wameanzisha vikundi, wameungana na biashara yao kubwa ni kulima mbaazi kwa ajili ya biashara.

Tukifuata kwenye ukurasa wa 19, Mheshimiwa Rais amesema tufanye kilimo kiwe biashara, na akinamama wale walijitahidi sana kulima mbaazi lakini bahati mbaya soko kidogo limeshuka. Ninachoomba, Mawaziri husika wajitahidi kutafutia akinamama wa Mkoa wa Lindi masoko ya mbaazi ili na sisi tuinuke katika maisha yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi hii ya kuchangia hoja. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai wake na leo hii tunaweza kuhudhuria Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Spika, pia namshukuru sana Rais wetu kipenzi, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi yake kubwa anayoifanya kwa awamu hii. Mama huyu ametoa fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali katika Halmashauri zetu. Ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya, ametoa fedha nyingi kwa ajili ya umaliziaji wa maboma mbalimbali, kwa ajili ya ujenzi wa shule, madarasa na mambo mengineyo. Mwenyezi Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali kwa Halmashauri. Tumebaini udhaifu mwingi sana kwenye ripoti ya CAG kwenye halmashauri zetu. Kwanza kuna udhaifu mkubwa katika usimamizi wa maeneo ya ununuzi na mikataba. Kama tunavyofahamu kwamba eneo la manunuzi linatumia fedha nyingi sana za Serikali, ni zaidi ya asilimia 70 ya pesa zote za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo basi, ndiyo maana Serikali ikaona ni vyema Bunge litunge sheria kwa ajili ya matumizi ya fedha hizi za manunuzi. Kuna Public Procurement Act ya 2011 pamoja na Regulation yake ya mwaka 2013. Lengo kubwa ilikuwa ni kudhibiti fedha hizi za Serikali ili zitumike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kitu cha kusikitisha na kushangaza sana kwenye halmashauri zetu hili eneo limekuwa ni bovu kweli kweli. Kuna fedha nyingi za Serikali zimetumika isivyo. Inaonekana kuna halmashauri 42 zilitumia fedha zenye thamani ya Shilingi bilioni 7.93 bila idhini ya Bodi ya Zabuni. Kwa kweli hapa nashindwa kuelewa. Hivi unafanyaje manunuzi bila kupitisha kwenye Bodi ya Zabuni? Hapa kuna question mark, huu unawezekana ukawa ni mpango wa makusudi wa kutaka kutumia vibaya na kutumia tofauti fedha ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna halmashauri 24 zilifanya ununuzi wa Shilingi bilioni 3.84 bila kuzingatia Mpango wa Manunuzi ya Mwaka. Kwenye Taasisi zote za Serikali ikiwemo halmashauri, huwa tunakaa, tunaandaa procurement plan ya mwaka husika. Unapoona kuna matumizi ya dharura yamekuja, labda kuna fedha zimekuja, mnatakiwa mwombe kibali maalum kwa matumizi hayo, na pia mnatakiwa muweke kwenye nyongeza ya mpango wenu wa manunuzi. Unapoona haya hayafanyiki, tunaanza pia kuwa na question mark kwamba fedha hizi hazikutumika kihalali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna Halmashauri 39 zilifanya ununuzi wenye thamani ya Shilingi bilioni 5.37 bila kuitisha nukuu za bei (competitive tendering/competitive quotation). Ni kitu cha kushangaza kama hujaitisha nukuu za bei, umempataje huyo mzabuni kwenda kuleta bidhaa katika halmashauri? Hapo panaonesha kuna upendeleo, rushwa na ubadhilifu wa fedha za Umma. Haiwezekani mimi kama procurement officer nimekaa ofisini kwangu nikaamua kampuni ‘X’ ije ifanye kazi ya Ujenzi, au Kampuni ‘Y’ ije ifanye kazi ya kuleta bidhaa fulani, hiyo siyo sahihi na haikubaliki. Moja kwa moja inaonesha kwamba kuna rushwa ndani yake, kuna upendeleo na ubadhirifu wa mali za Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna baadhi ya halmashauri 21 zilinunua bidhaa ya Shilingi bilioni mbili, lakini cha ajabu ziliingizwa kwenye ledger bila Kamati ya Mapokezi kuzikagua bidhaa hizo. Pia hapa kuna ukakasi ndani yake. Sheria inatutaka tunaponunua bidhaa zozote au huduma yoyote accounting officer aunde Kamati Maalum kwa ajili ya Ukaguzi na mapokezi ya bidhaa hizo. Ni ajabu, inaonekana baadhi ya halmashauri wanapokea kinyemela hivyo vitu, mtu wa procurement ameagiza yeye na anapokea yeye na anaingiza kwenye ledger yeye na ana-issue yeye. Hii haikubaliki. kwanza tuna wasiwasi, inawezekana hizo bidhaa hazikufika ipasavyo au hazikufika kabisa au hizo huduma hazikufanyika na ndiyo maana Kamati ya Mapokezi na Ukaguzi haikufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna halmashauri wanafanya ununzi wa bidhaa mbalimbali au huduma mbalimbali kwa kuwatumiua wazabuni ambao hawajasajiliwa GPSA. Hili ni kosa kubwa kwa Sheria za Manunuzi. Ina maana mtu anaamka tu nyumbani kwake asubuhi anaenda kupanga, leo nitachukua Kampuni ‘Z’ ilete bidhaa fulani. Hiyo siyo sahihi, kwa sababu manunuzi haya ni ya Serikali, yana sheria na taratibu zake, siyo kama manunuzi ambayo tunayafanya majumbani kwetu.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache tu kwanza Kamati ilibaini kwamba kuna upendeleo, udanganyifu na ubadhirifu wa mali za Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inashangaza pia kuna halmashauri nyingine ilionekana imenunua vitu lakini haijaingiza kwenye ledger na wala hawaja mu-issue local fundi. Kuna mizania ambayo iko tofauti kwenye hizi force account, watu wanataka kuzitumia vibaya hizi force account. Haiwezekani mimi nimenunua labda mchanga au nimenunua matofali halafu fundi anayajengea bila mimi kumkabidhi. Sidhani kama hiyo ni sahihi. Hapa pia kuna ukakasi, inaonekana kuna mambo yanaenda ndivyo sivyo kwa dhamira ya makusudi, kwa nia potofu na nia ovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachoomba Wabunge, ushauri wetu, watu wanaofanya haya mambo, wachukuliwe hatua kali kwa haraka. Tatizo linaonekana kwamba, kama mtu amefanya kosa mwaka 2022, inafika mwaka 2023, 2024, 2025 issue ni ile ile moja haijachukuliwa hatua, kwa kweli hii haikubaliki na ndiyo maana watu wengi wanaendelea kufanya mambo haya wanaona kwamba zile sheria za kinidhamu hazichukuliwi kwa haraka. Vilevile tunapendekeza kwamba ifanyike hivyo, haya mambo yatapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna uteketezaji wa dawa za binadamu katika vituo vinavyotoa huduma ya afya. Hii inasikitisha sana. Kuna vituo vya afya, zahanati na hospitali hazina dawa. Hivi inakuwaje mpaka dawa zinafikia wakati wa kuteketezwa? Kuna sheria inaruhusu, kama mimi kituo ‘X’ nina dawa za ziada/za nyongeza, nimeona labda baada ya miezi mitatu zinaweza ku- expire au miezi minne, ninaruhusiwa kuwapa zahanati ‘Y’ hizo dawa. Kwa nini wasipeane hivyo? Kwa nini kama unajua kwenye eneo fulani hayo magonjwa siyo mengi, upeleke dawa ziwe nyingi?

Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana kwa sababu inaonekana kuna fedha nyingi zimetumika kununulia dawa hizo ambazo wananchi wetu wanazihitaji, lakini baadaye zinakwenda kuteketeza. Hiki nacho ni kichaka kingine, tunatakiwa tukiangalie sana, haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna maeneo manne ambayo Kamati imeyabaini ambayo ni mianya ya upotevu wa mapato ya halmashauri. Vilevile kuna ushuru wa huduma (service levy), inakusanywa bila uthibitisho wa mapato halisi ya kampuni ya mwaka (turnover). Hiki kitu siyo halali, inabidi kifuatiliwe. Kuna halmashauri nyingine zinafanya malipo bila kukata kodi la zuio (withholding tax five percent).

Mheshimiwa Spika, hii ni fedha ya Serikali ambayo inatakiwa itumike kwa ajili ya Serikali, lakini cha kushangaza, mzabuni analipwa fedha yake kama kawaida, inakuwaje halmashauri usikate hii kodi ya zuio ukairudisha TRA ili iweze kutumika na Taifa letu? Huu ni mwanya mwingine wa matumizi mabaya ya fedha ya Serikali. Pia tumebaini kuwa kuna halmashauri nyingine zinafanya malipo bila kutumia risiti ya electronic. Hiyo ni kosa kisheria.

Mheshimiwa Spika, pia inaonekana kuna halmashauri nyingine zinaendelea kutoa leseni mbalimbali za biashara nje ya mfumo. Pia hicho ni kichaka kingine. Vile vile kuna baadhi ya stahiki za watumishi kutolipwa ipasavyo. Rasilimali watu ndiyo msingi wa utendaji wa mafanikio ya taasisi yoyote, lakini rasilimali watu usipoitendea haki kuna matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inaonekana kuna watumishi wengi wa halmashauri wanadai stahiki zao; wengine wanadai malimbikizo ya mshahara baada ya kupanda cheo, lakini hawapati kwa muda mrefu. Hiyo ipo sana, na mimi mwenyewe ni mfano halisi nikiwa mtumishi wa Serikali, nilipokuwa Serikalini, nilifanya kazi, nikapanda cheo, lakini nilikaa zaidi ya miaka sita bila kulipwa arrears. Hiyo inashusha morali na ari ya kufanya kazi. Kwa sababu hiyo ni haki yao, tunaomba TAMISEMI na Serikaki kiujumla iangalie eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kuna wafanyakazi wengine wanahamishwa; kwa mfano, anahamishwa kutoka Wilaya ya Buchosha unampelewa Wilaya nyingine. Mtumishi huyu ana familia na mizigo yake, anatakiwa alipwe stahiki yake, lakini unamwambia aripoti ndani ya siku saba au siku 14 aende pale lakini fedha yake haumlipi, anaendaje kule? Hii nayo inashusha morali ya kufanya kazi vizuri. Tunaomba wafanyakazi hawa walipwe stahiki zao vizuri ili waweze kufanya kazi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi kuchangia hoja katika Serikali za Mitaa, sehemu ya kwanza napenda kuchangia ni uhamisho wa watumishi wa Serikali za Mitaa kumekuwa na matatizo sana la watumishi wa Serikali za Mitaa kuhama kwa suala kubwa hili la kubadilishana hilo suala limekuwa kizungumkuti.

Mheshimiwa Spika, kuna mtu ambaye nilikuwa namshughulikia kabisa mwenyewe aliniomba document zake nizishughulikie nimeangaika nazo muda mrefu karibu miaka miwili bila mafanikio na huyo mtu alishapata mtu wa kubadilishana naye na kulikuwa na nyaraka zote ambazo zilikuwa zinatakiwa kwa ajili yakubadilishana.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa kila siku naenda Mtumba kila baada ya siku mbili tatu lakini nikifika kule naambiwa document hazipo natoa kopi zingine naacha, nikika siku mbili nikienda tena naambiwa hizo document hazipo natoa copy nyingine naziacha pale, nimefuatilia hiyo issue karibu miaka miwili mpaka ilipofika kipindi cha kwenda kwenye kampeni nikaacha nikamwambia yule binti aje mwenyewe kibaya zaidi alivyokuja mwenyewe ndio yalitokea mambo ya ajabu sana.

Mheshimiwa Spika, baada ya kufuatilia pale aliandikiwa barua feki ya uhamisho yule binti yangu alitaka kufukuzwa kazi alipokwenda kuripoti sehemu ambayo anatakiwa kwenda kuripoti walipofuatilia ile barua ilionekana ni feki. Kwa kweli matatizo yalikuwa makubwa sana, ikabidi niingilie kati yale mambo yakaisha akarudi kwenye kituo chake kilekile cha kwanza. Kwa hiyo, tunaomba TAMISEMI iangalie kitengo hicho cha uhamisho mambo yanayofanyika ni mabaya naya aibu sana tunaomba kuwaomba mjitahidi kurekebisha hapo Serikali yetu Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni eneo la watumishi wa afya na walimu kuna maeneo mengi katika mkoa wetu ya Lindi ni sehemu ambazo sio rafiki sana kwa kuishi, ni sehemu zenye mazingira magumu. Watumishi wanakwenda pale kwenda kuchukuwa cheki namba baada ya muda wanatafuta uhamisho kuhama kwenda sehemu nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba kuna watumishi vijana ambao wamemaliza chuo wako kwenye maeneo yale wameomba nafasi za kazi naomba wapewe kipaumbele wale vijana kuliko mkiwachukuwa watu ambao wanatoka maeneo ya mbali wanafika pale kuchukuwa cheki namba wanaondoka mfano halisi ni Wilaya ya Liwale, Nachingwea huko Kilimarondo kuna shida sana za watumishi na sehemu nyingi.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya tunacho kikubwa kizuri cha Kilimarondo lakini inakatisha tamaa watumishi wako 12 pale wanafanya operation zote wana huduma nyingi zote afya lakini hali ni ngumu. Kwanza hata jokofu lile la theatre hawana, hawana vifaa tiba, watumishi ni wachache. Na pia kuna hospitali zetu za wilaya kuna Hospitali ya Wilaya Nachingwea, ina hali mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hospitali ile ya Nachingwea haina vifaa tiba muhimu kwa mfano kuna wodi ya wazazi iliyopo pale haina kifaa hata kimoja ni jengo tu lipo pale mapambo lakini hakuna kifaa tiba kwenye ile theatre na theatre kubwa iliyopo katika Wilaya ile ya Nachingwea haina hata zile taa hakuna hata washing machine vitanda ni vya kizamani vimechakaa sana, tunaomba Waziri husika atupie macho hospitali za Mkoa wa Lindi zaidi zile zilizopo pembezoni na Vituo vya Afya ili waweze kusaidia wananchi wa kule wapate huduma stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo tunaliomba kwako kwa hawa watumishi ambao wanakwenda kwenye sehemu mazingira magumu tunaomba iweke posho kwa watu wale ahsante naomba kuchangia hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi kwanza napenda Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na sisi wote kuwa hai kwa siku hii ya leo. (Makofi)

Napenda pia kumpaongeza Rais wetu mpenzi Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na timu yake yote. Pia napongeza Waziri wa Ulinzi kwa hotuba yake nzuri ambayo ametusomea leo asubuhi, kwa kweli imeshiba, inapendeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mwenyeji wa Mkoa wa Lindi, kule kwetu Lindi na Mtwara tupo mpakani kabisa, mwaka jana kuanzia mwezi wa sita/wa saba mpaka kumi kidogo tuliishi kwa mashaka. Watu walikuwa hawawzi kufanya kazi zao, kazi kubwa ambayo inafanywa na wakazi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara ni uvuvi na kilimo. Kipindi kile watu walikuwa wanashindwa kwenda mashambani kwao kwa sababu kuna watu waliingia ambao sio watu wazuri kutoka kwenye nchi za wenzetu japokuwa siwezi nikasema ni nchi gani, lakini inaonekana kuna watu waliingia wakawa wanafanya matendo ambayo hayafurahishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nashukuru sana nilipongeze Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania walichukua jitihada za haraka wakatuma vikosi vya Jeshi kwenye mipaka ile na ulinzi uliimarishwa, hatimaye hali ikarejea vizuri sana kwa kweli tunawapongeza sana tunasema ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Lindi na Mtwara kwa sasa wanaamani wanaendelea na kufanya kazi zao na tunaona bajeti iliyowekwa hapa tunaomba ipitishwe tu kwakweli tusishike shilingi ipitishwe vizuri kwa sababu wanaonesha wanania ya kulinda mipaka na walilinda mipaka ipasavyo, tunaomba bajeti yao iende vizuri ili kazi iendelee kusiwe na mkwamo wowote wa ulinzi na usalama wa mipaka yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuliongelea ni suala la nyumba za wanajeshi, katika Wilaya ya Nachingwea kuna kikosi cha Jeshi kinaitwa Majimaji na Old Camp, nyumba zilizopo pale ukiziona kwa kweli zinakatisha tamaa na ukiambiwa wanaishi watu/wanajeshi kwa kweli inatisha. Ombi langu kwa Serikali kwa Wizara ya Ulinzi mfanye marekebisho ya zile nyumba ili watu wanaoishi mle wajisikie ni watu kama watu wengine wanaishi vizuri, zile nyumba zimechoka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lingine nililonalo kwa Wizara ya Ulinzi ni ofisi zao, nimeshaingia kwenye ofisi zao mara nyingi hata pale Kikosi cha Mgulani ofisi zao kwa kweli haziko vizuri. Tunaomba Waziri wa Ulinzi ulichukuwe hilo ujaribu kuangalia kuboresha ofisi za jeshi kwa sababu zile ni ofisi kama zilivyo ofisi nyingine, tunaomba uboreshe ziwe vizuri ili na wao wafanye kazi vizuri, wajisikie wanapotimiza majukumu yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine napenda kuliongelea ni kuhusu barabara za mipakani. Wabunge wengi wameongelea hizo barabara, tunashukuru Serikali yetu kupitia Wizara ya Ujenzi wamejitahidi kutengeneza barabara hizo. Ila tunaomba tunatia msisistizo kwamba barabara zile ziendelee kuimarishwa ili ziwe vizuri hata kama kukitokea suala lolote kusiwe na tatizo jinsi ya kupita kwenye zile barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina mengi ya kuongea kwenye Wizara hii ila ombi langu naomba tusishike shilingi tuwaache Wizara hii wapewe pesa zao vizuri ili waweze kufanya majukumu yao vizuri, kwa kweli wanajitahidi, wanafanya kazi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara hii nyeti sana ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza, napenda kutoa shukrani zangu za dhati na pongezi nyingi sana kwa Kamati ya Nishati na Madini kwa kazi yao nzuri ambayo wameifanya kupitia kwa Mwenyekiti wake na wajumbe wote kwa kuishauri vizuri Wizara hii ya Nishati na mpaka inaendelea kufanya vizuri kwa sasa. Pia napenda kumpa pongezi nyingi sana Mheshimiwa Kalemani, Msaidizi wake na Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kalemani kwa kweli ni mtu ambaye ni msikivu, anajitahidi sana kutusikiliza. Mimi nimemsumbua mara nyingi sana lakini namshukuru Mungu kila napomuendea kwa suala linalohusu TANESCO na mambo mengine ya Wizara yake, huwa ananijali na huwa tunampigia simu Meneja wa TANESCO na matatizo yote tunayaongelea vizuri. Kwa kweli, Mungu akubariki Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati kwenye eneo la umeme ni Wizara nyeti sana. Umeme ni kitu cha msingi sana kwenye maendeleo kwenye nchi yoyote. Tunashukuru mmeweka umeme wa REA sehemu nyingi sana kwenye vijiji vyetu. Ombi langu ambalo bado liko kwenu umeme wa Mkoa wa Lindi haueleweki au hauaminiki kwani unakatika sana mara kwa mara. Ndani ya dakika 20 au 10 umeme lazima ukatike, hauwezi ukanunua vitu ukaweka kwenye friji vikakaa salama, itakuwa ni uongo vile vitu vinaharibika. Kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa mmesema kukuza ushiriki wa sekta binafsi kwenye maendeleo ya kiuchumi kwa kweli tunatakiwa tujitahidi kwa sababu kuna watu wengi wamejiajiri kupitia kazi hizi za umeme lakini wanashindwa kufanya kazi zao vizuri kwa kuwa umeme huu hauko stable. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru Mheshimiwa Kalemani amesaidia sana kwenye Mkoa wa Lindi hususani Wilaya ya Liwale, Nachingwea na Ruangwa. Inaonekana kweli kuna mafanikio lakini naomba uongeze nguvu kwa sababu ile kasi ya kuzimika sana imepungua lakini bado unaendelea kuzimikazimika. Naomba Waziri atusaidie ili wananchi wale waweze kufaidi huduma hii ya umeme na wao wajisikie vizuri waone kama vile walivyo watu wa Dodoma wanavyofaidi umeme wao. Sisi wananchi wa Lindi tungefurahi sana tupate umeme kama huu wa Dodoma ili tuweze kujisikia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo napenda kulichangia kwenye Wizara ya Nishati ni kuhusu gesi asilia. Gesi asilia ni muhimu sana kwa sisi wananchi wa Tanzania hasa wenye kipato cha chini ili iweze kutusaidia. Tunaomba sana hii gesi asilia ingeanza kutumika vizuri na pia isambazwe sehemu zote vizuri sana ili iweze kusaidia. Matumizi ya gesi asilia ukiangalia gharama zake ni nafuu sana kuliko vitu vingine.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna magari yanayotumia gesi asilia sasa hivi, matumizi ya yale magari nimejaribu kuongea na wale wataalam yako chini sana karibu nusu ya gharama ya mafuta ya petroli tunayotumia sasa hivi. Kilo moja ya gesi asilia ni Sh.1500 ambayo inaweza kutumika kwa zaidi ya kilomita, samahani kidogo nimesahau lakini gharama yake ni chini zaidi ukilinganisha na petroli lita moja. Tunaomba Wizara hii ya Nishati ijitahidi sana kusambaza hizo gesi asilia na pia iweze kutoa elimu kuhusu matumizi ya gesi asilia ili Watanzania tuweze kufaidika na gesi yetu ambayo iko katika nchi yetu ya Tanzania zaidi Mikoa ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa karibuni kulitokea tatizo la LUKU kwenye ununuzi wa umeme. Tunashukuru Waziri wetu alifanya jitihada na tuliona juhudi alizokuwa amefanya hali ikarejea. Hata hivyo, siku mbili, tatu za juzi mpaka jana ile hali imerudi tena kwa Mkoa wa Dodoma. Watu wengi wamejaribu kununua umeme wameshindwa lakini sasa hivi kuna watu nimewasiliana nao wanasema sasa hivi ile hali imeanza kurudi umeme umeanza kupatikana lakini kulikuwa na kama siku mbili tatizo lilirudia tena. Tunaomba Waziri wetu ambaye anajituma sana Mheshimiwa Kalemani ajaribu kuliangalia tena tatizo hili ili wananchi wako tuweze kuwa vizuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai wa kuweza kuchangia siku hii ya leo. Pia, namshukuru sana Rais wetu kipenzi mama Samia Hassan Suluhu kwa kazi yake nzuri aliyoifanya. Amemwaga fedha nyingi sana kwenye sehemu zetu za kazi kwa ajili ya afya na elimu. Tunamshukuru sana Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali zetu za Mkoa wa Lindi zimechakaa sana na zinakatisha tamaa. Kuna hospitali za wilaya ukifika pale huwezi ukaamini kama ni hospitali ya wilaya, hospitali zile ni kongwe na zimechakaa sana. Hospitali hizo zina matatizo mengi, kwanza hazina vifaa tiba, zina matatizo ya watumishi, wataalam mbalimbali hakuna. Kuna tatizo lingine la kukosekana kwa umeme, unazimika mara kwa mara. Tunaomba wapatiwe hata solar kwenye zile sehemu muhimu katika Hospitali hizo. Zaidi kwa mfano kuna Hospitali ya Nachingwea tunahitaji kupatiwa solar kwenye jengo la mama na mtoto, pia kuna tatizo la taa ile kubwa ya theatre hakuna kabisa kwenye hospitali ile. Ni Hospitali ya Wilaya lakini haina hicho kitu, taa ile kubwa ya theatre hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la ambulance, Wilaya nzima kuna ambulance moja ambayo iko kwenye Kituo cha Afya Kilimalondo, ni mbali sana kutoka pale Wilayani Nachingwea. Tunaomba sana sana tupate ambulance kwa sababu, kuna Ambulance ambayo ni mbovu zaidi ya miezi sita na haitengenezeki. Tunaomba sana watuangalie kwa jicho la pili tupate ambulance kwenye hospitali hiyo. Hakuna ukumbi wa mikutano, asubuhi kunakuwa na ile morning report, hakuna ukumbi wa kufanyia kile kitu, wanasimama tu wanapeana ripoti. Tunaomba watusaidie tupate ule ukumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wodi ya wanaume imechakaa sana, inakatisha tamaa. Hakuna kichomea taka kulingana na uwezo wa hospitali ile. Incinerator iliyopo ni ndogo sana tunaomba watusaidie tupate hiyo incinerator. Uzio wa Hospitali ya Nachingwea ule unakatisha tamaa, ni mbovu mbovu, mbovu mno. Tunaomba watusaidie tupate matengenezo ya hospitali hiyo. Pia, hakuna dental chair kwenye hospitali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna Hospitali ya Liwale, katika hospitali hiyo tunashukuru wametuletea X-Ray, lakini X-Ray hiyo kuna mtaalam mmoja tu, akiumwa au akiwa na dharura yoyote au akienda likizo, hakuna huduma inayoendelea pale. Tunaomba tuongezewe wataalam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, kuna hizi barabara. Barabara zinakatisha tamaa sana, kuna barabara ya kutoka Lupota kwenda Chingunduli, huwezi kupita imekufa ile barabara, inakatisha tamaa. Tunaomba watusaidie tutengenezewe hizi barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi niliuliza swali kuhusu barabara ya Nanganga – Nachingwea – Masasi – Liwale, lakini bahati mbaya nimejibiwa jibu la Mkoa wa Mtwara barabara tofauti kabisa. Naomba sana tupate jibu la msingi baadaye kabla hawaja-wind up Wizara husika, hizo barabara tupate majibu ya msingi ili tujijue na sisi tuko katika sehemu gani. Wananchi wa kule tangu tumezaliwa na wengine mpaka wamekufa, hatuijui lami jamani, hatuijui lami, inasikitisha na barabara hizo ni za mkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana watuangalie kwa jicho lingine, kwa jicho la huruma, barabara zinakatisha tamaa. Akinamama wajawazito wanajifungua njiani kwa kukosa barabara. Barabara na madaraja hakuna, tunaomba sana watusaidie, tunaomba sana TAMISEMI waangalie hilo suala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la watumishi naomba niongee kidogo nieleweke. Watumishi wengi wanaoajiriwa wanaopelekwa Mkoa wa Lindi, wanakwenda kuchukua check number, then wanaomba uhamisho wanageuza. Matokeo yake kule kwetu kunakaa hakuna watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa hivi, kuna vijana wengi wanajitolea, kuna wanaojitolea nafasi za ualimu na nafasi zingine. Tunaomba sana wapewe kipaumbele wazawa wa kule kwa sababu wamezoea mazingira ya kule. Wakiajiriwa watu wa kule watakaa. Inasikitisha sana wanapoajiriwa watu wengi tunasema tuna watumishi, lakini baada ya muda mfupi watumishi wote wanakuwa wameshaondoka. Sijui ni kwa nini, sijui kunaonekana vipi kule kwetu. Tunaomba sana hili suala lipewe kipaumbele. Watumishi wakiajiriwa waanze kuajiriwa wazawa wa kule. Kwanza wana uchungu na kwao; pili wamezoea mazingira magumu watakaa. Naomba sana, haya masuala yaangaliwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nalirudia ni barabara, jamani barabara, barabara jamani, barabara za kwetu zinasikitisha. Tunaomba jamani watufikirie kwa barabara za kwetu na sisi wenzao ni binadamu pia, tunaomba. Barabara za kwetu ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini nasisitiza kuhusu suala la barabara. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuongelea Bajeti ya Waziri Mkuu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia uhai wake na pia tunamshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu kwa miradi ambayo ametuletea pesa nyingi katika nchi yetu na miradi hiyo inaendelea. Tunampongeza sana na tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Waziri Mkuu, tumeiona iko vizuri sana. Tunashukuru imekwenda vizuri na waliofanya kazi, kwa kweli wamechakata wamefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina nyongeza ya mambo ya msingi sana yanayoendelea, lakini hayana matokeo mazuri. Naongea kwa masikitiko makubwa sana na maumivu makubwa sana kutoka moyoni mwangu. Wananchi wa Mkoa wa Lindi Wilaya ya Liwale na Wilaya ya Nachingwea wanavyouawa na wanyama tembo. Ukienda kwenye mashamba ya wananchi wale utatoa machozi, utalia njaa itakayotokea sasa hivi ni kubwa mno. Tuna vijiji vingi ukienda maeneo yanaitwa Nditi, Namapwiya, Ngumichile, Mbute, Nyambi, Mwandila, Matekwe, Majonanga na ukienda Liwale; Kibutuka, Mkutano, Lilombe na Kilangala inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya wamepelekwa Askari Wanyamapori wachache. Hivi kwa hali ya kawaida kwenye shamba wakiingia tembo hamsini kwa mara moja hawa askari wetu wawili, watatu wataweza kufanya ile kazi kweli? Wataweza kweli? Hali ni mbaya. Mwisho juzi kuamkia jana kuna kijana amefariki ameuawa na tembo mchana kweupe katika maeneo ya Mwinyichile saa tisa mchana, amejitoa nyumbani akasema akaangalie shamba lake kama limebakia mahindi kidogo au alizeti, amefika kule yeye ndiye wamemfanya chakula inasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea ingetokea hali ya dharura, ya tahadhari ya haraka ya kupeleka helikopta, lakini tumelizungumzia sana. Haijapelekwa helikopta kufukuza wanyama wale mpaka leo lakini angeuawa ndovu mmoja ingeenda helikopta na maaskari pale kwenda kuwaletea vurugu wananchi, inasikitisha sana hii hali, inasikitisha mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza na wananchi wa kule wanajiuliza ndovu na binadamu nani ni muhimu? Inafikia wakati wanasema mtapigiwa kura na ndovu, siyo kwamba wanaongea vile kwa kutulaghai ni hatua na uchungu waliokuwa nao. (Makofi)

MHE. YAHYA A. MHATA: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya Mhata, taarifa.

TAARIFA

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la tembo kwa kweli ni la hatari sana. Hata Jimboni kwangu tembo ni tatizo, kwa hiyo namuunga mkono kabisa mzungumzaji. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Maimuna taarifa unaipokea?

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Hali ni mbaya. (Makofi)

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, nimeona kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Pallangyo.

TAARIFA

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji pia kwamba kule kwetu Arumeru Mashariki, Kijiji cha Kilinga, tembo wamehamia kwenye nyumba za wananchi. Hali ni mbaya sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea sisi wananchi wa Mkoa wa Lindi hali ya dharura ingetokea, kwa sababu ndovu wanaoingia kwenye shamba moja ni zaidi ya Hamsini, wanapelekwa askari wawili, watatu wanashindwa wanakimbia na wao wanaondoka. Wabunge wenzangu na viongozi mbalimbali wameripoti hicho kitu mara chungu nzima, tulitegemea wangeleta helikopta kufukuza wale wanyama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali iko tofauti. Tunajiuliza wangeuawa ndovu wawili pale pangetulia vile, wananchi wetu wangepona kweli? Inasikitisha sana. Tunaomba…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine, kuna wahanga wananchi wetu wa Wilaya ya Kilwa Masoko na wa Nachingwea kulikuwa na upanuzi wa viwanja vya ndege, walitwaliwa maeneo yao, ni siku nyingi, lakini mpaka sasa hivi hawajawapa pesa zao. Hiyo hali inakatisha tamaa na inarudisha maendeleo. Pia kuna barabara hii ya Masasi – Nachingwea – Liwale. Hii Barabara tangu 2015 kila siku tunaambiwa ipo kwenye upembuzi yakinifu, kila siku tuaambiwa inajengwa, kwani hii keki ya Taifa na sisi pia hatuitaki? Tugawane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba na sisi barabara ile ni ya muhimu ni ya kimkakati ile barabara itengenezwe. Jamani ikinyesha mvua dakika kumi tu, huwezi kupita ile barabara.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Maimuna, endelea na mchango wako.

MHE MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mtuangalie kwa jicho la huruma. Kuna akinamama, kuna vitu vingi, kilimo kikubwa kule kinaendelea, lakini hatuna barabara, lami hatuijui kule kwetu. Watu wanazaliwa mpaka wanakufa. Tunaomba watusaidie tuwekewe lami barabara ile, kila siku tunapigwa danadana na maelekezo, lakini ilani haitekelezeki, ni kwa nini hii huku tu? Tunaomba watusaidie barabara itengenezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna migogoro ya wafugaji na wakulima. Hali ni mbaya, kuna watu wanauawa, tuna uhakika na tuna uthibitisho watu wameuawa na wafugaji. Tunaomba watusaidie, hali ni mbaya ni mbaya sana, kwa hiyo hakuna amani, hakujatulia watusaidie wenzao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba malambo kwa ajili ya mifugo, Mheshimiwa Dkt. Samia, aliahidi yafufuliwe yatengenezwe tunaomba tusaidiwe kwa Mkoa wa Lindi, hakuna kabisa malambo hali ni mbaya. Pia tunaomba na scheme za umwagiliaji kwa sababu kilimo cha sasa hivi mvua haziaminiki. Mabadiliko ya hali ya hewa ni kila siku, tunaomba tusaidiwe tupate na scheme za umwagiliaji ili vijana wetu waweze kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mikoa ya Kusini karanga na alizeti zinastawi sana lakini wananchi wa kule wanashindwa kulima vizuri kwa sababu hawana mbegu nzuri. Tunaomba Serikali sikivu ilete mbegu na wataalam kule wa kuweza kuwaelewesha wale ndugu zetu kilimo cha karanga na alizeti. Pale Nachingwea kuna maeneo yalikuwa yanaitwa farm one mpaka farm 17, yale maeneo yalikuwa maeneo mazuri sana kwa ukulima wa karanga. Zilikuwa zinatoka karanga nzuri sana lakini sasa hivi watu wakilima hakuna, tunaomba Serikali yetu sikivu itusaidie tupate mbegu nzuri na tupate na Wagani waweze kuwaelimisha watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)