Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rose Vicent Busiga (5 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ni kwa mara yangu ya kwanza kuchangia kwenye Bunge lako tukufu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kuingia kwenye Bunge hili tukufu, ni kwa mara yangu ya kwanza na ninamshukuru Mungu na nawashukuru pia na watumishi wa Mungu walikesha kuomba usiku na mchana ili mimi niweze kuingia kwenye Bunge tukufu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru baba yangu mzazi na familia yangu nzima na mume wangu kwa kunipa ruhusa hii kuja kutumikia Bunge hili tukufu maana si kawaida kwa wanaume kumruhusu mwanamke kuja kwenye Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi ya yote…

SPIKA: Jamani mmesikia Waheshimiwa karuhusiwa huyo. Makofi/Kicheko)

MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nina furaha kubwa sana na nilikuwa natamani nipate nafasi hii ikiwezekana naomba uniongeze dakika mbili tu kwa ajili ya kusema haya. Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwa kuongoza vizuri Chama chetu cha Mapinduzi kwa kuipatia heshima kubwa iliyotukuka katika Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais huyu niwa kuigwa, hajawahitokea toka Tanzania iumbwe, napenda kulisema mbele ya Bunge lako tukufu hili 2015 mara tu baada ya Rais ya Jamhuri ya Muungano kupata nafasi ya kuwa Rais ninaamini kabisa kwa watu ambao wanamtegemea Mungu, Rais huyu aliamua kuichukua Tanzania na kumkabidhi Mungu aliye hai na ndio maana watu wengine wanaweza wakasema uchaguzi ulikuwa hauna haki, lakini kwa mtu ambaye anamtegemea Mungu, Rais aliamua kuichukua Tanzania na kuipeleka kwa Mungu kwa malengo tu, ukimtumikia Mungu utapata hekima, utakuwa na maarifa, utakuwa na busara. Ndio maana leo hii Tanzania sisi ni matajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais nikiamini hata yaliyobakia kwa miaka mitano hii yote yanakwenda kukamilika. Jamani naomba nizungumze hili mwaka 2020 ninaamini kabisa Watendaji wa Kata nchi nzima na mimi nikiwemo niliingia kule Ikulu kwa mara yangu ya kwanza na Bunge hili mimi ni Mtendaji wa Kata na kila Mheshimiwa Mbunge namwambia mimi ni Mtendaji wa Kata najivuna kwa kazi niliyokuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asingekuwa huyu Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli wa wanyonge, mimi ningeingia humu? Jamani lazima tujiulize, na ndio maana jina langu lilipita kwa kila Kamati jina langu lilikuwemo mimi mnyonge na leo hii naunga mkono kwa asilimia mia moja miaka iliyobakia yote ambayo hatujafanikiwa Rais kuyafikia yote yatafika na zaidi nasema nawaunga mkono Mawaziri, baba yangu hapo Waziri Mkuu usiogope, Mungu amekuteua wewe, lakini pia na Mawaziri wote na Naibu Mawaziri wote chapeni kazi mtangulizeni Mungu mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania tumejaliwa kuwa na Rais simba, akiunguruma baba watu ameunguruma na mimi naidhihirisha Tanzania nitamuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano asilimia mia moja, na sitaona haya kusema mazuri yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndio maana nikakwambia naomba dakika mbili ninayo mazuri mengi, ,una daraja la Busisi kule Geita.

SPIKA: Mheshimiwa Rose ngoja, hebu ongezeni dakika mbili hapo. (Kicheko/Makofi)

MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tulivyoenda kule Ikulu, nilipofika Dar es Salaam, nikajua ni Dar es Salaam ya sasa ni kama Marekani kumbe ni Tanzania. Mheshimiwa Rais kwa upendeleo kabisa akatupa na pocket money tukatembee tembee, nani kama Dkt. Magufuli jamani?

WABUNGE FULANI: Hakuna!

MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nazungumza haya kutoka kwenye vilindi vya moyo, nataka niwaambie watanzania mnaweza mkasema wakati tunatafuta kura za Chama cha Mapinduzi, kwa wanawake wa Geita, kwanza ninawashukuru sana wapiga kura wangu wanawake wa Mkoa wa Geita kwa kuniamini kama Mbunge wao na sitawaangusha, wanawake wote yaani ukishataja tu tunaomba kura za Mheshimiwa Rais tulikuwa tunapita wote na Wabunge, na ndio maana hakuna kura iliyoibiwa, hakuna kura iliyoibiwa kwa Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshismiwa Spika, jamani tunaangalia kule Mwanza, daraja la Busisi, tunategemea sisi Wasukuma tutakuwa tunapita pale huku tuna baskeli tumepakiza tunakula na muwa, ilikuwa haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja na nitazidi kuongea kwa kumuunga mkono amefanya mengi, anatupenda Watanzania naombeni tumuelewe, naombeni tumtie moyo pamoja na Serikali yake na Waziri. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia tena kwa mara nyingine. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ametulalia siku ya leo.

Pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwa namna ambavyo ameendelea kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana pamoja na timu yake nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nikikaa kimya nitakuwa sijawatendea haki watendaji wenzangu nchi nzima wa Kata na Vijiji kwa sababu Wizara hii ya TAMISEMI inawagusa wao.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka niliwasilisha wasilisho langu la kuomba Wizara ya TAMISEMI iangalie vizuri namna ambavyo inaweza kuwasaidia Watendaji wa Kata pamoja na Watendaji wa Vijiji kulingana na jinsi ambavyo wanafanya kazi katika mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona wazi kabisa watendaji hawa ndio wanaosimamia maendeleo katika kata zao, katika vijiji vyao, lakini pia nikijikita kwenye suala la ukusanyaji wa mapato, Watendaji hawa wa Kata na Vijiji ndio wanaokusanya mapato na wanakusanya mapato katika mazingira magumu sana. Naweza kutoa mfano mmoja tu, katika ukusanyaji wa mapato wa kodi ya jengo. Kodi ya jengo ilikuwa ni ngumu sana kuikusanya kwa upande wa TRA, lakini Watendaji wa Kata na Vijiji waliweza kukusanya kodi ya jengo vizuri na wakafikia malengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni nini Serikali ifanye; naiomba Serikali yangu kupitia Wizara ya TAMISEMI, namwomba Mheshimiwa Ummy Mwalimu aweze kuwasaidia watendaji wa kata waweze kupatiwa pikipiki kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa maendeleo katika kata zao. Hii itaweza kuwafanya watendaji hawa wafanye kazi kwa kujituma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali yangu iangalie ofisi zao. Ofisi zao zinatia aibu, hazifai. Mimi mwenyewe nikiwa Mtendaji wa Kata siku moja mvua ilinyesha, nilitaka kuangukiwa na lile boma. Kwa hiyo, mimi mwenyewe ni shahidi mkubwa, ofisi zinazotumika na wao ni haya majengo ambayo ni ma-godown. Kwa hiyo niiombe sasa Serikali waweze kuwasaidia Watendaji wa Kata waweze kupata ofisi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia Watendaji wa Kata hawa ndio wakurugenzi kwenye kata zao. Niiombe Serikali iangalie namna ya uendeshaji, watendaji waweze kupata motisha ya kila mwezi kama wanavyopata waratibu wa elimu kata. Ukiangalia mtendaji huyu anafanya kazi katika mazingira magumu. Naiomba Serikali kwa uchungu mkubwa, wawaangalie sekta hii ya utawala.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri, Mheshimiwa Ummy, yeye mwenyewe amekuwa shahidi wa watendaji, wanalia kila siku awatazame. Naamini dada yangu, mtani wangu, Mheshimiwa Ummy, kwa namna anavyojua kuchapa kazi mwaka huu wa 2021 kilio cha watendaji kitakwenda kufutika. Namwomba mtani wangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, asiniangushe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuzungumza kwenye Bunge hili Tukufu. Naomba kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ameendelea kutulinda, lakini pia kulitetea Taifa la Tanzania kutokana na msiba mkubwa wa baba yetu, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Baada ya kupata msiba huo nilikuwa na huzuni kubwa sana na nililia kwa masikitiko makubwa sana kwa sababu baba yetu alitupenda kutoka moyoni. Baba yule alikuwa na upendo usiokuwa na kifani, alikuwa na upendo ambao hauwezi kulinganishwa na mtu yoyote hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumejifunza mambo mengi kutoka kwa baba yetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Moja ambalo nililojifunza kubwa sana, nimejifunza kwa namna alivyoweza kusimama na kutusaidia sisi wanawake kupata nafasi katika Serikali hii ya Tanzania. Nitaendelea kumuenzi baba yetu kwa upendo mkubwa na ndio maana akaamua kumteua mama yetu Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wake kwa mara kwanza Tanzania ikapata Makamu wa Rais mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, safari yake ya miaka mitano ilikuwa ni safari yenye mafanikio sana na hatimaye tukauona uwezo wa mama yetu Samia Suluhu Hassan na mara tu baada ya matatizo kutokea mimi kama Mbunge wa Mkoa wa Geita, nilivyopata tatizo hilo nililia kwa huzuni sana, lakini nikajitia moyo nikasema, Wana wa Israel walipokuwa wakienda wakisafiri kwenye Nchi ya Kanaani, walikuwa na Mussa lakini hawakuweza kuifikia ile Nchi ya Kanaani, hatimaye Joshua ndiye aliyeweza kuwafikisha katika Nchi ya Kanaani. Hivyo nikaamini kabisa kwa matumaini yangu makubwa kuwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan atatufikisha kwenye Nchi ya Kanaani, nchi ya asali na maziwa.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze hili kwa uchungu mkubwa sana. Nasikitika na maumivu makali sana ambapo ninapoona wanambeza baba yetu aliyetusaidia mpaka leo sisi wanawake tunachangia hotuba nikiwa nina imani kabisa ya kuwa ninaweza kutoa mchango wangu na wananchi wangu wakanisikiliza.

Mheshimiwa Spika, naomba niingie kwenye hoja moja kwa moja katika Wizara ya Afya. Tumeona Serikali imeweza kufanya vizuri kwa kujenga Hospitali za Wilaya 99 lakini pia, tumeona imejenga Hospitali za Rufaa 10 na za Kanda tatu sambamba na hivyo imejenga zahanati 1,198 na Vituo vya Afya 487. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweza kufanya vizuri lakini pia, ninaiomba Serikali yangu kwasababu ni sikivu kuna maboma ambayo yapo ambayo wananchi wamechangia fedha zao za mfukoni wakajenga maboma yale na wanaisubiri Serikali iweze kumalizia. Nikitoa mfano, katika Wilaya ya Mbogwe kuna Kituo cha Afya kinaitwa Nghomolwa wananchi wamekijenga kwa muda mrefu sana kituo kile cha afya kimeshafikia hatua ya ukamilishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tunao watendaji wetu wa kata, ndio wanaosimamia miradi hii ya ujenzi wa zahanati, ya ujenzi wa vituo vya afya, lakini watendaji hawa wa kata wanafanya kazi katika mazingira magumu ya kazi. Lakini, watendaji hawa hawa wa kata hata sisi Wabunge tukienda kwenye shughuli zetu za Kibunge, hawa hawa tunafika kwenye ofisi zao, ofisi zao hazifai, ofisi zao haziendani na yale ambayo wanatutendea sisi kama Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali sasa, waone haja ya kuwasaidia watendaji wa kata waweze kupata usafiri wa kufanyia kazi zao ili kuleta maendeleo kwenye kata zao. Lakini pia, niiombe Serikali yangu kwa sababu ni sikivu iweze kuwasaidia watendaji hawa wa kata hata motisha tu inatosha… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Rose Busiga, caucus imeamua iwe dakika tano tano kwa hiyo, sio uamuzi wangu nakushukuru. Imeamua hivyo kwasababu dakika ni chache ili… (Makofi/Kicheko)

MHE. ROSE VICENT BUSIGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja lakini naomba watendaji wa kata wafikiriwe kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi kwa wakati mgumu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ameweza kutupatia zawadi ya uhai, lakini nikushukuru sana wewe kwa kunipa nafasi hii adhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Mama yetu kipenzi kwa namna ambavyo ameendelea kufanya kazi kwa kujituma na naomba tu nizungumze kutoka kwenye vilindi vya moyo wangu kwamba, niwarudishe kidogo nyuma Watanzania wote, ikumbukwe tu Mama alipokea nafasi hii katika mazingira magumu sana, binafsi nilijiuliza hivi itakuwaje na Watanzania wote walijiuliza hivi itakuwaje? Majibu sisi wenyewe tunayaona kwa macho yetu, tunaona Mama ambavyo anaendelea kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nilieleze Bunge hili Tukufu, kuna miradi ya kimikakati ambayo tayari ilikuwa imekwishaanzishwa na Mtangulizi wake na sisi kama Wanageita tuna kauli yetu tunasema hakuna kilichosimama. Uzuri Mkuu wangu wa Mkoa yupo na anaendelea kusisitiza, sisi kama Wanageita hakuna kilichosimama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nieleze tu kwamba mimi binafsi niko kwenye Kamati ya Miundombinu, nimetembea mwenyewe kwa macho yangu bila kusimuliwa na mtu, kwa macho yangu Mradi wa SGR Mama alikabidhiwa ukiwa na kilomita za mraba 700, lakini sasa hivi ni zaidi ya kilomita 2000 nani kama Rais Samia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Binafsi nakumbuka nilichangia hapa Bungeni, nikaomba suala la watendaji wa kata wapewe posho lakini wapewe pikipiki, jamani mimi mwenyewe dada ya Kairuki alinipa mwaliko nilienda kukabidhi pikipiki 916. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kidogo tu, Dada yangu Kairuki ambapo ametoka kupewa sasa donge nono na Mama tayari amekwishakamilisha. Hiyo speed aliyonayo Dada Kairuki nimwombe aendelee na speed hiyo hiyo na kila Mbunge hapa anaenda anamweleza tatizo lake anamsikiliza, Mheshimiwa Kairuki asigeuke nyuma, achape raba aendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba univumilie kidogo, nilisema kwamba leo nikipata nafasi hii lazima niitendee haki. Nikaenda mbele zaidi, sisi watendaji wa Kata tulikuwa tunapita tunachangisha michango ya madarasa. Rais huyu huyu aliweza kutoa fedha za madarasa 23,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watendaji wamefanya kazi katika mazingira mazuri hata likizo walipata, walikuwa hawapati likizo kwa sababu ya kwenda kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Namshukuru sana Rais wangu kwa namna ambavyo anaendelea kuona sekta hii ya elimu, lakini nimwombe sana Waziri wangu Mheshimiwa Kairuki, kuna madarasa ambayo wananchi wamejenga kwa fedha zao za mfukoni, kwenye bajeti hii tunaomba maboma ambayo yako hatua ya upauaji, Serikali waweze kutenga fedha ili kwenda kuzichukua zile nguvu za wananchi waamini Serikali yao iko kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano sisi Mkoa wa Geita, tuna maboma 1,016; ya msingi 713 na ya sekondari 303. Mheshimiwa Kairuki akishuka pale Geita akaja akatembea kidogo na Mkuu wangu wa Mkoa ananisikiliza, atakupokea na utayaona yale maboma.

Mheshimiwa Spika, niende mbele zaidi, narudi kwenye afya. Kule kwetu Geita tuna Hospitali ya Chato ya Kanda, ukifika pale ni kama umefika Dar es Salaam ndogo. Hata hivyo, namwomba Mheshimiwa Kairuki atupe watumishi. Kabla ya hospitali ile tulikuwa tunaenda Mwanza sasa hivi tutakuwa tunaishia Chato.

Mheshimiwa Spika, kuna vituo vya afya, hivyo hivyo na vyenyewe wananchi walijichangisha fedha zao za mifukoni mwao, lakini mpaka sasa hivi vituo vile vya afya vipo. Kwa ridhaa yako nitaje hata vitatu au vinne ili ujue kwamba ninavijua. Kuna Kituo cha Afya cha Buhela, Chikobe, Ng’homolwa, Kafita na Nyijondo. Naomba sana sana kwa ridhaa yako Dada yangu Mheshimiwa Kairuki afike kwenye vituo vya afya na fedha ambazo zimetengwa kati ya hivi vituo nilivyovitaja na vinginevyo aone haja ya kunisaidia hata kwa vituo viwili au vitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimezungumza sana, lakini nisiposema hili nitakuwa sijawatendea haki Waheshimiwa Madiwani. Waheshimiwa Madiwani wanafanya kazi nyingi sana na katika ziara yangu niliyoifanya Mwezi Machi Waheshimiwa Madiwani waliniomba sana, kwa heshima hiyo wakasema Mheshimiwa Mbunge wewe ulienda kuwasemea Watendaji wa Kata, tunaomba tena ukaliseme na hili, ikimpendeza Mheshimiwa Kairuki Dada yangu awasaidie na wao kidogo kaposho kao kale kaongezeke kidogo, wanatusaidia kazi, sisi tuko Bungeni sasa hivi lakini Madiwani wetu wanaendelea kufanya kazi kule. Kwa hiyo, kwa heshima hiyo hiyo Mheshimiwa Waziri anavyoendelea kuchapa raba na aendelee kuchapa mpaka kwa Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nimalize kwa kusema tuna daraja letu la Busisi na lenyewe mambo yanaendelea. Hata hivyo, Mheshimiwa Kairuki, watendaji wa Kata kipindi alipokuwa yupo kaka yangu Bashungwa waliahidiwa watakutana na Mama waje kidogo waangalie Ikulu jinsi inavyojengeka. Kwa heshima hiyo hiyo ya Dada yangu Mheshimiwa Kairuki, namwamini hana choyo, namwomba Watendaji wa Kata waje watembee Ikulu nami niwepo nawaongoza. Waje watembee Ikulu, waone jinsi Rais wao anavyoendelea kuchapa kazi, anavyoendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nimesikia kengele yangu, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu, Mungu akubariki sana. Pia, ninakuombea sana, umekuwa mwema sana, umekuwa ukiendesha shughuli za Bunge kwa uaminifu mkubwa sana. Sisi kama Wabunge tunakuombea katika mchakato wa uchaguzi. Naweza nikasema neno moja, Wamtumainio Bwana ni kama mlima sayuni hawatatikisika milele na milele. Tuna imani kubwa na wewe na tuna mwamini Mwenyezi Mungu atakwenda kutuvusha katika mchakato huo wa uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unanijua vema mdogo wako, kwamba ukinipa nafasi siichezei. Nafasi hii adhimu ninamuomba Mwenyezi Mungu anisaidie niongee ukweli ulioko moyoni. Unanifahamu mdogo wako ni mkweli tupu. Ilikuwa ni juzi, wakati wa wiki ya nishati, nilipata bahati ya kutemebelea mabanda, nikaenda moja kwa moja kwenye mkoa wangu nikiwa na maswali mengi. Nilipofika kwenye mkoa wangu kuna vijana ambao wamepikwa walinipokea vizuri nikaanza kuuliza maswali ya umeme. Katika Mkoa wangu wa Geita nina takribani vijiji 474 lakini viiji vyenye umeme ni 389 na vijiji 85 viko kwenye mpango wa REA mpaka sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba ufikishaji wa umeme kwenye Mkoa wa Geita ni asilimia 82. Kwa hiyo ni asilimia 18 tu ambayo umeme haujafika. Nani kama Mheshimiwa Rais? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naipongeza sana Serikali yangu ya Awamu ya Sita kwa namna ambavyo inaendelea kufanya kazi kwa uaminifu hapa ndipo ninapokuja kusema kazi iendelee; na hapa ndipo ninapokuja kusema tena hakuna kilicho simama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si jambo dogo, naomba niwaambie Watanzania si jambo dogo. Nakupongeza sana kaka yangu Mheshimiwa January Makamba, hongera sana kwa kazi ambayo unaendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais. Mimi ninaona vyema, ni Dhahiri, pamoja na naibu wako na wizara nzima na Katibu Mkuu kwa jinsi ambavyo mmeweza kufanya kazi kwa bidii.

Mheshimiwa Spika, lakini ninarudi kwenye vitongoji, kuna kupeleka umeme katika vitongoji vyetu. Mkoa wangu wa Geita nina takribani ya vitongoji 2,261. Kati ya vitongoji hivyo ambavyo vina umeme ni vitongoji 965, vitongoji 1,296 havijafikiwa na umeme. Kwa heshima hiyo hiyo Kaka yangu January nilipokuwa nimetembelea lile banda, nikafika, wakasema Mheshimiwa Mbunge tunapomaliza kupeleka kwenye vijiji tunashuka mpaka kwenye vitongoji. Ninakuamini kabisa Mheshimiwa January Makamba tunapoenda kumaliza hii bajeti ninaomba vitongoji vya Mkoa wa Geita vikafikiwe na umeme. Sina shaka na wewe, na ninaamini wewe ni mtu mwema sana, ni mtu bingwa sana, hivyo utaenda kufikisha katika vitongoji hivyo 1296 ili wananchi waone Serikali yao jinsi inavyochapa kazi.

Mheshimiwa Spika, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Kiukweli niwadhihirishie Watanzania, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kwa nguvu zote. Ninaomba tumuamini Watanzania wenzangu. Kwa nini nasema hivyo? Ninasema hivyo kwa sababu ladha ya chakula anaijua mpishi, mimi mwenyewe wakati nikiwa kwenye banda lile nilifika Rufiji nikiwa hapahapa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kwa sababu tu Kanuni za Bunge haziruhusu; lakini nilitama niwe humu humu Bungeni na wananchi wananiangalia waone ambavyo nimefika Rufiji. Mambo ambayo niliyoyaona, mafundi wako kazini wanaendeea na kazi, mambo ambayo niliyoyaona nilipofika pale Rufiji ujazo mkubwa wa maji unaendelea. Jamani Watanzania asiyeshukuru kwa kidogo hata kikubwa hawezi kushukuru. Mimi binafsi ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, ninamshukuru sana Kaka yangu Mheshimiwa January Makamba kwa sababu lile bwawa Mama alilipokea likiwa na asilimia takribani 30 leo tunazungumzia asilimia 88, nani kama Samia Suluhu Hassan?

Mheshimiwa Spika, tukienda mbele zaidi utaona upelekaji wa umeme kwenye migodi. Kaka yangu Mheshimiwa January unanisikia; kule kwetu Geita unajua kabisa sisi ni wachimbaji, ninakuomba kwenye migodi ambayo haijafikiwa na umeme kwa heshima hiyo hiyo kaka yangu ninaomba uweze kufikisha umeme kwenye migodi ya Nyakafuru, Mwabomba na migodi mingine ambayo sijaweze kuitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana sana sana kwa nafasi hii ambayo umenipa. Nina imani wananchi wangu wa Mkoa wa Geita hasa akina mama walionichagua, ninawaambia ya kwamba tuwe na imani kubwa na Serikali yetu. Serikali yetu iko kazini, Serikali yetu si ya mchezomchezo, na Mheshimiwa January Makamba kanifikisha Rufiji nikiwa hapa hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninamshukuru sana na kumpongeza Meneja wangu wa TANESCO Mkoa wa Geita pamoja timu yake nzima. Lakini kuna kaka mmoja ambaye sasa alikuwa ananipa hiyo elimu nilipotembelea, anaitwa Engineer Seif Abdul amenielewesha vizuri na ndio maana nimeweza kuchangia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana baada ya kusema haya ninaunga mkono hoja, hongera sana Waziri wangu January Makamba hongera nyingi Naibu Byabato.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)