Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Alfred James Kimea (2 total)

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya maji ya Busanda inafanana kabisa na changamoto ya maji iliyoko Korogwe Mjini. Nimekuwa nikifuatilia kwa Mheshimiwa Waziri na ameniahidi tatizo la Korogwe litatatuliwa na mradi wa miji 28 ambao Korogwe ni sehemu ya mradi huo.

Je, Serikali inawaahidi vipi wananchi wa Korogwe kwamba lini mradi huu utatekelezwa ili kuweza kutatua changamoto ya maji ambayo inawakabili wananchi wa Korogwe Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa ni mfuatiliaji mzuri na nimeshaweza kuongea naye mara kadhaa na kumhakikishia eneo lake kupata maji na uzuri Korogwe Mjini ipo ndani ya ile miji 28 ambayo fedha tayari zipo na muendelezo wa maandalizi unaendelea na hivi karibuni kuanzia mwezi Aprili miji ile 28 shughuli za kupeleka maji zinakwenda kuanza mara moja.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri na Naibu Waziri, pia tunashukuru kwa ajili ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo madogomadogo lakini matengenezo haya madogomadogo hayakidhi haja ya barabara hii kwani wakati wa mvua inaharibika kabisa na tunakosa mawasiliano kati ya mji mmoja hadi mwingine. Je, Serikali haioni kuna haja ya kutupa commitment ni wakati gani barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami ili tutatue changamoto hii kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara zote za changarawe ama za udongo na hasa maeneo ya mwinuko inaponyesha mvua huwa zinakuwa na changamoto ya kuondoka udongo ama changarawe. Commitment ya Serikali pamoja kutekeleza ahadi ya Rais na Waziri Mkuu tayari Serikali inatafuta fedha ili tuweze kufanya usanifu wa kina ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, Serikali inatafuta fedha na fedha ikipatikana barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.