Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Alfred James Kimea (7 total)

MHE. ALFRED J. KIMEA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Old Korogwe kwenda Kwamndolwa - Magoma - Mashewa - Bombomtoni - Maramba hadi Mabokweni yenye urefu wa kilomita 127.54 kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu kwa wananchi wa Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Old Korogwe – Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bongomtoni – Maramba hadi Mabokweni yenye urefu wa kilometa 127.69 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo inayopita barabara kama ilivyotajwa hapo juu. Ili kuweza kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 1,450.78 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA K.n.y. MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga bandari kavu eneo la Old Korogwe katika Halmashauri ya Mji Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa bandari kavu hufanyika ili kuongeza ufanisi wa bandari zilizopo mwambao wa bahari na maziwa. Ujenzi wa bandari kavu huzingatia vigezo maalum ikiwa ni pamoja na kuondoa msongamano katika bandari iliyo karibu na bandari kavu na kusogeza huduma karibu na watumiaji wa mwisho. Aidha, kigezo kingine ni uwepo wa upembuzi yakinifu unaobainisha mahitaji ya bandari kavu husika ili kuwa na msingi wa kufanya maamuzi sahihi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo hayo, eneo la Old Korogwe halijabainishwa kwa sasa kwamba linafaa kujengwa bandari kavu. Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari itafanya tathmini kuona umuhimu wa uwepo wa bandari kavu katika eneo la Old Korogwe. Ahsante.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA aliuliza: -

Je, ni lini Mahakama ya Wilaya ya Korogwe itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania inaendelea kutekeleza mpango wake wa miaka mitano wa Ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali. Kutokana na mpango huo wa Mahakama, jengo la Mahakama ya Wilaya ya Korogwe, limepangwa kujengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Mahakama ya Tanzania ipo katika mpango wake wa ujenzi na ukarabati wa Mahakama zake hapa nchini. Hivyo basi, ujenzi wa Mahakama za Makao Makuu ya Tarafa zote nchini utakamilika ifikapo 2025.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa wa Hospitali Kongwe ya Magunga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 17.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali 19. Aidha, hadi kufikia mwezi Februari, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 12.95 zimekwishatolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya hospitali Kongwe kumi na nne (14).

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itatenga shilingi bilioni 27.9 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe 31 ikiwepo Hospitali ya Mji wa Korogwe ya Magunga ambayo imetengewa shilingi milioni 900.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde ya mpunga ya Mahenge, Goo na Kwamngumi - Korogwe Mjini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mabonde ya umwagiliaji ya Mahenge, Goo na Kwamngumi ni miongoni mwa maeneo ya uzalishaji wa mpunga katika Halmashauri ya Mji Korogwe. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilitenga fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde hayo. Mwezi Aprili, 2023 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilisaini mkataba wenye jumla ya Shilingi bilioni 1.85 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu katika Bonde la Mahenge na Bonde la Goo.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Mpango na Bajeti ya mwaka 2023/2024 imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kupata gharama halisi ya kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji katika Bonde la Kwamngumi.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde ya mpunga ya Kwamgumi na Kwamsisi - Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa Niaba ya Waziri wa Kilimo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Korogwe ina zaidi ya skimu 64 zilizoendelezwa na ambazo hazijaendelezwa ikiwemo Skimu ya Kwamgumi inayokadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 210 na Kwamsisi yenye ukubwa unaokadiriwa kufika hekta 1,500.

Mheshimiwa Spika, katika skimu ya Kwamgumi Serikali imefanya uwekezaji wa awali kwa kufanya ujenzi wa mfereji mkuu wenye urefu wa kilomita tatu. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imefanya ukaguzi na tathmini ya awali kwa ajili ya kufanya ukarabati na uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu hii, ikiwemo usakafiaji wa mifereji ya kupitisha maji kwa ajili ya umwagiliaji. Hivyo basi, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Skimu ya Kwamgumi utaingizwa katika mpango na bajeti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ina mpango wa kujenga miundombinu katika Skimu ya Kwamsisi. Aidha, mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa kufanya ujenzi katika skimu hii umeanza.
MHE. COSATO D. CHUMI K.n.y. MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Kibo – Mgombezi – Bagamoyo na NMB Benki hadi Magunga hospitali zilizo kwenye mradi wa TACTIC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za Kibo - Mgombezi - Bagamoyo na NMB Benki hadi Hospitali ya Magunga zipo kwenye utekelezaji wa mradi wa TACTIC kundi la pili (Tier 2). Kundi hili linatekelezwa kwenye Miji 15 ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Korogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa kazi ya usanifu wa miradi ya ujenzi wa barabara kupitia kundi la pili (Tier 2) unaendelea kutekelezwa na Wahandisi Washauri ambapo tayari walisaini mikataba tarehe 15 Disemba, 2023 na itafanyika kwa kipindi cha miezi nane ambapo kitakamilika mwezi Agosti, 2024. Aidha, usanifu wa miradi hiyo utakapokamilika Agosti, 2024 kazi ya kutangaza zabuni itaanza Septemba, 2024.