Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Alfred James Kimea (4 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii uliyonipatia ili niweze kuchangia kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuongea mbele ya Bunge lako Tukufu, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii kuwa kati ya wawakilishi wa wananchi kwenye Bunge hili la Kumi na Mbili. Nafahamu umuhimu na ukubwa wa nafasi hii, hivyo, namuomba Mwenyezi Mungu akapate kunipa busara na hekima hasa kwa hiki kipindi changu cha miaka mitano ili niweze kuwaongoza watu wake kwa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata fursa ya kuusoma vizuri Mpango huu lakini kutokana na muda nimeamua ushauri wangu wote wa kitaalam niuweke kwenye maandishi hivyo baada ya hapa nitakabidhi meza yao ushauri wangu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa hizi dakika chache ulizonipatia, naomba niongee mambo machache hasa yanayohusiana na Jimbo langu la Korogwe Mjini. Nafahamu Mpango huu hasa umejikita kuimarisha uchumi kwenye Sekta ya Viwanda na Biashara. Hata hivyo, ili tuweze kufikia malengo hayo, naomba tuzingatie ushiriki wa wanawake katika uchumi wa viwanda na biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu umuhimu wa wanawake katika kukuza uchumi. Hii hata kwenye Biblia inadhihirishwa, inasema wanawake ni Jeshi kubwa. Hata hivyo, ushiriki wa wanawake kwenye sekta ya uchumi umeathiriwa sana na changamoto mbalimbali kwenye jamii zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini, ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za uchumi na biashara pamoja na viwanda umeathiriwa sana na tatizo la maji. Wamama wa Korogwe badala ya kujihusisha kwenye shughuli za kiuchumi wamekuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji kwa ajili ya kuhudumia familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yamekuwa changamoto kubwa ambayo imewapotezea focus wamama wa Korogwe hivyo kupunguza kasi ya uchumi na maendeleo ya Jimbo letu la Korogwe Mjini. Hivyo nimuombe kaka yangu Mheshimiwa Aweso aone namna gani tunatatua tatizo hili ili akina mama wa Korogwe wakape fursa ya kushiriki kwenye uchumi badala ya kuhudumia familia zao kutafuta maji usiku mzima. Kwa wastani kwenye Jimbo langu tunapata maji mara moja kwa wiki, hivyo tunaomba tuangaliwe kwa jicho la kipekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu pasipo afya bora ni vigumu kuweza kufikia haya maendeleo tuliyoyaainisha kwenye Mpango huu. Hivyo, kwenye sekta ya afya kwenye Jimbo langu la Korogwe pia ni changamoto kubwa. Tuna hospitali yetu moja ya wilaya ambayo tunaitegemea kwenye Jimbo letu la Korogwe, lakini sio Korogwe tu pamoja na wilaya nyingine za jirani; hospitali hii ni chakavu sana imejengwa tangu mwaka 1952 hivyo haiwezi kukidhi mahitaji ya huduma za afya kwenye jimbo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba Wizara husika ione namna gani inatutatulia changamoto hii. Aidha, tukarabatiwe hospitali ile kwa viwango vikubwa au kujengewa hospitali nyingine, ili watu wapate afya bora tuweze kukimbizana na shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba niweze kuungana na watu wengine wengi waliochangia, umuhimu wa miundombinu ya barabara katika kukuza uchumi na kuweza kufikia Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini tuna barabara muhimu sana, barabara hiyo inatuunganisha watu wa Korogwe Mjini, watu wa Korogwe Vijijini, pamoja na Mkinga. Barabara ambayo inatokea Korogwe – Kwa Mndolwa – Magoma, tuliahidiwa na Rais pamoja na Waziri Mkuu tutatengenezewa barabara hii, hivyo namwomba Waziri mhusika wa Wizara hii aweze kutujengea barabara hiyo ili kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nichangie kwenye hii bajeti ya Wizara ya Elimu. Nina mambo machache sana ya kuchangia kwenye Wizara hii na napenda nijikite hasa kwenye elimu ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya changamoto ambazo zimetolewa imeonekana tuna upungufu wa Wakufunzi au Wahadhiri katika vyuo vyetu, lakini tuangalie ni nini kinasababisha kitu hiki? Kama tunafahamu vyuo vyetu vina tendency ya ku-retain wanafunzi waliofanya vizuri wabaki kufundisha wanafnzi wetu, lakini pia kufanya research ambazo zinasaidia kutatua changamoto zinazopatikana kwenye jamii zetu. Ili mwanafunzi awe retained pale chuoni ni lazima wawe ni wanafunzi wanaofanya vizuri, First Classes ndio zinabakizwa vyuoni. First Class hizi hazihitajiki chuoni tu peke yake, pia mashirika mbalimbali yanatafuta watu hawa. Kwa hiyo, maslahi ya wanaobakishwa pale chuoni ndio yanayosababisha aidha mwanafunzi huyo au wanafunzi hao wazuri wakubali kubaki chuoni au waende sehemu nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa niishauri Serikali, ione namna ya kuboresha maslahi kwa wataalam wetu hawa ambao wana kazi kubwa ya kufanya research, wana kazi kubwa ya kufundisha wanafunzi wetu vyuoni, ili waweze kuwa na morali ya kubaki vyuoni kuliko kwenda kuajiriwa sehemu nyingine. Huo ndio mchango wangu wa kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, naongea hili kwa kuwa nina uzoefu na nilikuwa miongoni mwa watu hao, labda kwanza naomba ku-declare interest. Nadhani unafahamu ugumu wa kupanda madaraja kwenye vyuo vyetu, tunaajiriwa mara nyingi kutoka vyuoni kama Tutorial Assistant, baada ya kupata Masters tunaenda kuwa Assistant Lecturer na baada ya hapo tunakuwa ma-lecturer aidha kwa ku-publish baada ya kukaa miaka mitatu au kupata Ph.D.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo,watu hawa wanaweza wa-qualify. Mtu amehangaika sana aka-publish au kapata Ph.D anapanda cheo kwa kuandikiwa tu barua umepanda, lakini wanasema tunasubiri Serikali itoe idhini ya kupandishwa vyeo ili mpewe maslahi yenu. Hii inakatisha moyo wakufunzi wetu, inasababisha watu waondoke vyuoni; tunasema Wahadhiri ni wachache, lakini Serikali ndio inasababisha. Kwa kweli, hii ni sehemu nyeti sana, tunaomba maslahi ya watu hao yaangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ni wa kwangu mimi mwenyewe, kabla ya kwenda kufanya PhD nili-publish ili niweze kupanda kuwa Lecturer kabla ya kwenda PhD. Nilipewa tu barua ya pongezi kwamba, nime-qualify kuwa Lecturer, lakini hadi leo sijawahi kupata mshahara wa mtu kama Lecturer. Kwa hiyo, nasema wapo wenzangu wengi huko vyuoni wana changamoto kama ya kwangu, naomba tuangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, tunajua mazingira ya kusoma hapa Tanzania. Najua unaweza kuwa unafahamu watu ambao wamefanya Ph.D zao hapa Tanzania, kuna changamoto kubwa, lakini changamoto hii inasababishwa na maslahi mabovu ya wasimamizi wa Ph.D zile. Lecturer hana kipato kizuri, inasababisha aanze kutafuta shughuli nyingine za kumuingizia kipato. Utakuta lecturer anafundisha part time vyuo vinne, utakuta lecturer anafuga kuku ili kujiongezea kipato, anaacha kusimamia dissertation za wanafunzi. Kwa hiyo, kama tunataka kupandisha elimu ya vyuo vyetu, basi tuangalie maslahi ya watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hilo tu, pia vyuo vyetu havina fund kwa ajili ya kuendesha research. Sio research tu, ili uweze kutoa watu wa masters na PhD lazima vyuo viwe vime-subscribe kwenye journal nzuri za kimataifa, viwe vina software kwa ajili ya data analysis, lakini vyuo havipatiwi fedha hizi. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ivipatie fedha vyuo vyetu ili elimu iweze kukua, hasa research ambazo zinahitajika kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha mwisho, naomba Wizara ya Elimu inisikilize kwa makini; kulikuwa kuna institute hapa Tanzania inaitwa African Institute for Mathematical Science. Institute hii ipo South Afrika, Ghana, Tanzania na Rwanda, lakini institute hii inafadhiliwa na wafadhili (Donors) kwa asilimia kubwa na nchi ambayo hii institute ipo nchi hiyo inatoa kiasi kidogo kwa ajili ya uendeshaji wa chuo hicho, lakini Serikali yetu imeshindwa kulipia fedha kidogo kwa ajili ya kuendesha institute hiyo na institute hiyo imekufa. Namwomba Waziri kwenye majumuisho yake aje aniambie kimetokea kitu gani kwa institute hii mpaka kufa?

Mheshimiwa Naibu Spika, institute hii inasaidia researcher wetu, institute hii inasaidia wataalam wetu kuweza kufundishwa jinsi ya ku-apply mathematics kwenye kutatua matatizo kwenye jamii zetu. Imefanya vizuri sana Rwanda na inaendelea kufanya vizuri, imefanya vizuri Ghana na inaendelea kufanya vizuri, Tanzania kuna nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Huo ndio ulikuwa mchango wangu. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini napenda tuweke taarifa sahihi, jina langu ni Alfred Kimea na sio Kimei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi, wenzangu wameongea mengi. Ukianza kufuatilia utaona kila mchango ambao unatakiwa kwenda kwa Wizara hii kwenye hii Bajeti Kuu ya Serikali, imeshaongelewa. Napenda tu niongezee machache na sehemu nyingine niongezee ambapo palishaongelewa kwa sababu mengi yameshaongelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza napenda kumshukuru Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya. Tusiposhukuru kwa kazi kubwa anayoifanya, tutakuwa hatumtendei haki mama huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi kichache tangu tuwepo Bungeni mambo makubwa, aidha yameshafanyika au tumepewa ahadi kubwa kwa ajili ya kuendeleza majimbo yetu. Mfano tu kwenye jimbo langu la Korogwe Mjini, kwa kipindi hiki kidogo tumeshaandaliwa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya sekta ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu ni la Korogwe Mjini, kwa kipindi hiki kidogo tumekwisha kuandaliwa zaidi ya bilioni mbili kwa ajili ya sekta ya maji. Sekta ya barabara ikiwemo TARURA tuna bajeti ya karibu 1,300,000,000 kwa hiyo, hii ni kitu kikubwa ni lazima tumshukuru Mama kwa kazi kubwa anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye bajeti sasa, mchango wangu utakuwa wa sehemu mbili, moja nitapongeza lakini sehemu ya pili nitashauri sehemu chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa pongezi kwa kweli tunamshukuru na tunampongeza kweli Waziri, wetu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu pamoja na kaka Mheshimiwa Engineer Masauni kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kutuletea hii bajeti nzuri. Kwa kweli ni bajeti nzuri ambayo inatakiwa kupongezwa na ninazo sababu ya kupongeza hii bajeti siyo tu kama nafuata mkumbo wa watu wameipongeza bajeti na mimi nipongeze lakini ninazo sababu kabisa za msingi kwa ajili gani naipongeza hii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza ni kweli hii bajeti imekwenda kumgusa kila mtanzania. Kila Mtanzania ameguswa kwenye hii bajeti kuanzia wafanyakazi tumeona wanakwenda kupandishwa vyeo na hii tuliipigia kelele sana mimi nilikuwa mmoja wapo nilisema walimu hasa wa vyeo vikuu ambao mimi nilitoka huko nilikuwa mmoja wao walikuwa wanastahili kupandishwa madaraja lakini kwa muda mrefu hawakuwa wanapandishwa madaraja. Lakini hii bajeti sasa imekuja na dawa hiyo; walimu wa Vyuo Vikuu wanakwenda kupandishwa madaraja. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa ajili ya kuona hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia bajeti hii imegusa au imezingatia maoni ya Wabunge na Wadau wengine wengi. Hajakaa tu chini kuandaa bajeti, hajachukua template za bajeti zilizopita, amekaa chini kuangalia Wabunge waliongea kitu gani, alikaa chini kuangaliwa wadau wanazungumza kitu gani akaja na bajeti nzuri ambayo imezingatia maoni ya watu hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauri juu ya TARURA kuongezewa bajeti na kweli TARURA imekwenda kuongezewa bajeti. Tulishauri Wizara ya Afya iongezewe bajeti na wamefanya hivyo. Tulishauri miradi mikubwa iende kufanyika na kweli wanakwenda kuiendeleza ile miradi mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndugu yangu Mheshimiwa Waziri kwa kuwa umesema unakwenda kufanya vitu hivyo, kweli tunataka hivyo vitu vikafanyike. Mfano mmojawapo; tunakwenda kushika kodi kwenye line za simu na tunakwenda kuchukua kodi kwenye mafuta na alisema specific kwenye mafuta shilingi 100 inakwenda TATURA na kwenye line inakwenda kwenye huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania siyo watu wajinga, wanakwenda kuhesabu kitu gani kinakwenda kupatikana na kitu gani kinakwenda kufanyika. Kwa kuwa ulisema specifically hii inakwenda kwenye afya kweli tunataka iende kwenye afya. Tumesema hii inakwenda TARURA kweli tunataka hii iende TARURA. Kwa hiyo, tunakupongeza lakini tunataka kweli ahadi yako uende kuitimiza kwa ajili tuna mwaka mmoja tu, mwakani siku kama hizi tutarudi tena tukikupitishia bajeti nyingine tunataona hiki kitu umekifanya kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sehemu nyingine ya mwisho, kwa ajili gani naipongeza hii bajeti kama kauli mbiu ya nchi yetu ni kuinua uchumi wa viwanda ni kweli bajeti hii imeonesha dhamira yake ya kwenda kuinua uchumi wa viwanda. Tumeona wakipunguza baadhi ya ushuru wa forodha kwa bidhaa ambazo zinakwenda kutumika kwenye viwanda vyetu. Lakini pia wameongeza ushuru wa forodha kwenye bidhaa ambazo zinatengenezwa Tanzania ili kuweza kuinua sekta ya viwanda kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, tunaipongeza bejeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mchango wangu utakuwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni pongezi ambayo nimekwisha kutoa lakini sehemu ya pili ni maoni yangu kwenye baadhi ya maeneo machache ambayo naona yanahitaji kufanyiwa marekebisho. Ya kwanza, nitoe maoni yangu kwenye hii sheria ya kodi ya majengo. Kweli Mheshimiwa Waziri nakupongeza kwa hii kodi mpya au namna ya utozaji wa hii kodi mpya. Kama tunavyofahamu ni kweli kodi yoyote ambayo inaanzishwa ni lazima iwe nyepesi kukusanya. Kweli nakupongeza hii kodi ambayo umeianzisha itakwenda kuwa rahidi kukusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kodi mpya inayoanzishwa ni lazima iwe na urahisi wa kulipa. Ni kweli walipo kodi wetu itakuwa rahisi kuilipia hii kodi ya majengo kuliko mwanzo ilivyokuwa. Lakini kuna principle nyingine ya kodi inaitwa principle diversity kwamba mtu yoyote ambaye anakusudia kulipa hii kodi kweli anatakiwa kulipa hiyo kodi na kweli kodi hii itakuwa vigumu sana kwa mtu yoyote ambaye kakusudia kulipa kukwepa kodi hii. Kwa hiyo napongeza kwa jitihada hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti kodi hii inachangamoto kidogo ambazo kidogo ambazo lazima Mheshimiwa Waziri waweze kuzi-address. Ya kwanza tunafahamu kodi yoyote kuna principle muhimu sana ambayo hii kodi inakwenda kinyume na principle hiyo. Principle ya Equity, kwamba watu wenye kipato sawa waweze kulipa kodi sawa; lakini watu wenye vipato tofauti basi kodi iwe tofauti, mwenye kipato kikubwa alipe kodi kubwa na mwenye kipato kidogo alipe kodi ndogo. Lakini Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kabisa kwamba kodi jinsi ilivyo wewe Mheshimiwa Waziri utakwenda kulipa shilingi 1,000 kwa mwezi, na yule bibi yetu kule nyumbani kwetu kwa Mndolwa, kule nyumbani kwetu Old Korogwe naye atakwenda kulipa sawasawa na wewe ulivyolipa. Hii siyo sawa kabisa Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, lazima hii kodi ije itengenezwe namna kwamba mwenye kipato kikubwa atalipa kodi kubwa na mwenye kipato kidogo atalipa kodi ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara ya hiki, moja itawadhulumu wale watu wanyonge; lakini namba mbili Serikali haitakusanya mapato yake sahihi kwa ajili mtu mwenye kipato kikubwa atalipa sawa na yule mwenye kipato kidogo. Nini kifanyike; maoni yangu, nadhani haya yataondoa ile shida ambayo Wabunge wengi wameiongea. Maoni yangu ni kwamba kwanza assumption zangu ni kwamba mtu ambaye anatumia unit nyingi atakuwa na kipato kikubwa kuliko mtu anayetumia unit ndogo. Sasa kwa namna gani mtu mwenye kipato kidogo atalipa kidogo na mwenye kipato kikubwa atalipa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kusema unashika kodi shilingi 1,000 kwenye Luku achana na hiyo, shika kutokana na matumizi ya Unit, badala ya Luku shika hiyo kodi kwenye unit mtu anazotumia. Ukifanya hivyo Mheshimiwa Waziri; moja mtu mwenye kipato kidogo atalipa stahiki yake, mwenye kipato kikubwa atalipa stahiki yake. Namba mbili, ile issue ya maghorofa mtu ana ghorofa ngapi? Mtu ana apartment ngani, hiyo hutaizingatia tena kwa ajili mtu mwenye kikubwa atatumia sana na alipa kodi kubwa na mtu mwenye kanyumba kadogo atalipa kidogo. Kwa hiyo nashauri badala ya kukatwa hiyo kodi kwenye mita ikatwe kwa Unit jinsi mtu anavyotumia. Huo ndio ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kodi nyingine ambayo napenda kushauri kidogo ni tozo kwenye line za simu. Kengele ya kwanza naamini. Tozo kwenye line ya simu. Mheshimiwa Waziri, hapa tozo kwenye line ya simu lazima uwe clear hii kodi inakwenda kushikwa kwenye nini; kwa ajili kila kodi mpya inayoanzishwa lazima tujue base ya hiyo kodi ni kitu gani? Aidha, unakwenda kushika kodi kwenye line ambayo siamini kwamba umiliki wa line unaweza kumshika mtu kodi au unakwenda kushika kodi kwenye matumizi ya muda wa maongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama ni kwenye matumizi muda wa maongezi ile item uliyoisema kwa siku itakuwa siyo muhimu. Kama unakwenda shika hii kodi kwenye muda wa maongezi kuna mtu anaweza akaongeza muda wa maongezi mara kwa wiki, mwingine akawa anamiliki line tu lakini haongezi muda wa maongezi. Kwa hiyo ukisema unamshika ile kodi kila siku hutakuwa umemtendea haki. Kwa hiyo, naamini watakaoshika hii kodi per muda wa maongezi na pia inatakiwa um-charge mtu kwa jinsi anavyoongeza muda wa maongezi. Kwa hiyo, hayo ndio maoni yangu, naomba kodi hizo zifanyiwe kazi ili kodi zetu ziweze kuleta tija zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha mwisho kama muda upo, naomba nishauri kwenye ushuru wa forodha kwenye mafuta. Kweli Mheshimiwa Waziri naamini kabisa kodi hii ni kwa ajili ya kulinda viwanda vyetu lakini sasa hivi Tanzania bado tuna deficit ya mafuta. Kwa hiyo, kodi ni nzuri lakini ninachoona timing bado. Tuhimize watu wetu wazalishe mbegu za alizeti pale tutakapokuwa tuna-produce zaidi hapo ndio tuanze ku-protect hatuwezi kuanza ku-protect kitu ambacho hatunacho bado. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kodi hii ni nzuri na ninaiunga mkono lakini nahisi timing bado sasa hivi mahitaji ya nchi yetu ni karibu tani za ujazo 500,000, zaidi ya 500,000 lakini tuna produce 200,000 tu. Kwa hiyo, tukienda ku-protect sasa hivi kitu ambacho hakipo bado haiingia akilini kwa hiyo naomba tuwahimize watu wetu na tutakapokuwa tunazalisha zaidi hapo ndipo tutakapokuwa na nafasi ya kuweza kulinda viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa muda huu, naunga mkono hoja, mungu awabariki sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa
Spika,nakushukuru kwa nafasi hii. Pili, nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Maji, kwa namna wanavyopambana kuona namna gani wanatatua changamoto ya maji kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu umuhimu wa maji kwenye jamii zetu. Tunafahamu kwamba kama tunataka jamii au nchi yenye watu wenye afya nzuri tunahitaji maji safi. Kama tunahitaji kuinua kiwango cha elimu wanafunzi wote wa kike na wakiume waweze kwenda kuhudhuria masomo vizuri tunahitaji maji.

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa tunahitaji kuinua kiwango cha uchumi wa nchi yetu, kuzuia magonjwa yasiwasumbue watu na tukapoteza fedha nyingi kwenye kutibu magonjwa, tunahitaji maji safi.

Mheshimiwa Spika, nafahamu juhudi kubwa ambazo Serikali inazifanya kutatua changamoto ya maji na zipo takwimu zinazoonyesha kiwango gani cha maji kinapatikana sasa hivi, lakini kwa uhalisia zaidi ya asilimia 50 bado watu hawana access ya maji safi na salama. Ushauri wangu ni nini? Serikali inabidi sasa itoe kipaumbele kikubwa kwenye Sekta ya Maji.

Mheshimiwa Spika, research zinaonyesha kwamba kutatua changamoto ya maji, kuleta maji safi na salama si kwamba tu muhimu kwa afya, lakini pia tunaona zitanyanyua kiwango cha uchumi kama nilivyosema hapo mwanzo. Pia itasabisha kuwe na Taifa la watu wenye furaha kwa ajili tunapata maji safi, watu wanaoga vizuri kabla ya kwenda kazini asubuhi, kwa hiyo maji ni muhimu sana.


Mheshimiwa Spika, statistics zinasema tuki-invest shilingi moja kwenye Sekta ya Maji pamoja na Usafi wa Mazingira inaweza kuiletea ongezeko la uchumi kwa shilingi 12. Investment ya shilingi moja inaweza kuletea pato la Taifa ongezeko la shilingi 12. Kwa hiyo naomba tujitajidi kuongeza investment kwenye sekta ya maji.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni huu; kama tulivyofanya investment kubwa kwenye standard gauge, tulivyofanya investment kubwa kwenye umeme, tunaona tunajenga bwawa la umeme, kwa nini sasa tusiwe na mradi mkubwa wa kimkakati nchi hii ili kutatua tatizo la Maji Tanzania nzima.

Mheshimiwa Spika, tunaweza tusiwe na fedha za kufanya hivyo, lakini tunaweza tukakopa fedha nje ya nchi au ndani ya nchi kwenye vyanzo mbalimbali kama vile Government Bond tuka-invest kwenye changamoto ya maji ili tuweze kutatua tatizo la maji kwa sasa hivi na hata miaka hamsini ijayo. Halafu tutaendelea kulipa deni hilo pole pole lakini tukiwa na uhakika kwamba changamoto ya maji imekwisha kabisa kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Spika, mradi mkubwa ambao uta- identify tatizo la maji lipo kiasi gani nchi nzima. Mradi mkubwa ambao uta-identify vyanzo vya maji, tumetajiwa Ziwa Victoria, Tanganyika na Maziwa mengine, Mito na kila mahali. Mradi ambao utasambaza maji nchi nzima, tuji-commit sehemu hii tutaendelea kulipa deni lakini tukiwa tunajua kabisa changamoto ya maji imeisha kwenye nchi hii.

Mheshimiwa Spika, naomba nirudi Jimboni kwangu Korogwe. Nashukuru Mheshimiwa Waziri kaka yangu Aweso kwa commitment yake kubwa kuhakikisha anatusaidia kutatua changamoto ya maji pale Korogwe. Korogwe ina changamoto moja, changamoto iliyokuwepo Korogwe kwanza kuna mradi unaoitwa HTM, huu ni mradi wa miaka mingi, mradi huu unasabisha wakati wowote tunapoomba fedha kwa ajili ya maendeleo ya maji, kutatua changamoto ya maji, tunaambiwa mna Mradi wa HTM. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe anatuleta maji kwenye Mji wa Korogwe bila kuangalia hii HTM. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Waziri kwa sababu kwenye bajeti hii angalau tumepewa hela kidogo, lakini tunaona itatatua angalau changamoto ya maji Korogwe. Nilimwomba milioni 700 kwa ajili ya Kata ya Bagamoyo lakini kwa mwanzo ameniletea milioni 200. Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kutumalizia hizo milioni zilizobaki ili kuweza kutatua changamoto ya Maji Korogwe. Tuna imani sana na Mheshimiwa Waziri, tunamwamini na tunajua atatatua changamoto ya maji Korogwe na Tanzania nzima. Mungu ambariki sana.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii na naunga mkono hoja. (Makofi)