Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe (2 total)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nashukuru japo sijaridhishwa hata kidogo na majibu ya Serikali kwa sababu malalamiko ya wananchi kwenye vyama hivi ni makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali la kwanza la nyongeza; kwa kuwa kumekuwa na malalamiko makubwa ya ubadhirifu wa Vyama hivi vya Ushirika, Bodi hizi kuwa wababe, kutoshirikisha wananchi, lakini pia mashamba haya kukodishwa pasipo tija kwa wananchi. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa wa kuunda Tume Maalum itakayoshirikisha vyombo vyote vya dola kwenda kufanya uhakiki wa mashamba haya yote 17?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa tunaona Sheria ya Ushirika ya mwaka 2013 haitoi fursa kwa viongozi wa ngazi ya mkoa kushuka chini kuweza kuona kinachoendelea kwenye vyama hivi vya ushirika. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka wa kufanya mabadiliko ya sheria, ili sasa viongozi wa ngazi ya mkoa waweze kushiriki na kuona nini kinaendelea kwenye vyama hivi vya ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saashisha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna changamoto za baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Ushirika kuhusishwa na ubadhirifu na Serikali imekuwa ikichukua hatua mara kwa mara. Tumeona hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali katika Vyama vya Ushirika vya Tumbaku, tumeona hatua ambazo Serikali imechukua katika Vyama vya Ushirika vya Pamba, tumeona hatua ambayo Serikali imechukua katika Vyama vya Ushirika vya Mkonge.Hatua hizi zote zimechukuliwa na Serikali kuhakikisha kwamba kwanza mali zilizoibiwa za vyama vya ushirika zinarudishwa kwa wanachama, lakini mbili kuwachukulia hatua viongozi wote waliohusika na kuwapeleka katika vyombo vya sheria.

Suala ambalo analisema la uwepo wa Tume, ipo Timu Maalum chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inafanyakazi hii na imekuwa ikiendelea kufanyakazi hii katika maeneo yote yanayohusu vyama vya ushirika na kama kuna specific case inayohusu Wilaya ya Hai namkaribisha Mheshimiwa Mbunge aje atueleze Wizarani na tutashirikiana naye kuhakikisha kwamba ubadhirifu kama upo katika maeneo ya Hai ya Vyama vya Ushirika vya Wilaya ya Hai, au Mkoa wa Kilimanjaro tutaweza kuchukua hatua kama ambavyo tumechukua hatua katika masuala yanayohusu mali za KNCU.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mabadiliko ya sheria kwanza ni vizuri Waheshimiwa Wabunge tukaelewa dhana ya ushirika ni dhana ya hiyari. Ushirika siyo mali ya Serikali ni mali ya washirika, lakini Serikali inaingilia kwenye masuala ya ushirika kwasababu ya public interest kwasababu ile inakuwa ni mali ya umma ndiyo maana tunayo Tume ya Ushirika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la upungufu wa kisheria Wizara ya Kilimo sasa hivi inaipitia sheria na mwaka jana ilikuwa tuilete ndani ya Bunge ili kuweza kuihuisha iweze kuendana na mahitaji ya sasa, badala ya kuwa ushirika wa huduma uwe ushirika wa kibiashara kwa maslahi ya wanaushirika. Kwahiyo suala la kisheria tunaliangalia na ni suala genuine ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema na muda ukifika tutaileta sheria ndani ya Bunge ili iweze kwenda na wakati, lakini siyo kuifanya Serikali i-control ushirika bali tunatengeneza sheria kuufanya ushirika ujiendeshe wenyewe kwa maslahi ya washirika na kutengeneza governing bodies ambazo zitausimamia ushirika kwa maslahi ya wanaushirika.
MHE. SAASISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, majibu ambayo kimsingi yatapunguza maumivu makubwa waliyopata wananchi wa Hai tarehe mbili kutokana na majibu ya swali lao kuhusu suala la ushirika. Niwaambie wananchi wa Hai watulie Serikali yao inawapenda sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niulize swali la nyongeza la kwanza; kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na kwa kuwa wananchi wa Hai tarehe 28 walifanya jambo lao kwa asilimia kubwa sana na kuleta utulivu humu Bungeni na huko nje; je, ni lini sasa Serikali itatekeleza kwa kiwango angalau cha asilimia 50 ya ahadi ya Mheshimiwa Rais?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali italipa madeni ya watumishi wa afya na Walimu ambao ni wastaafu, deni ambalo mimi mwenyewe nimeshaliwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri la milioni 171 ili watumishi wa afya waendelee kufanya kazi yao kwa uaminifu? Ikizingatiwa miongoni...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa umeshauliza swali.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saasisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya kuajiri watumishi wa afya japo kwa asilimia 50. Bunge lako Tukufu na Wabunge wote humu ni mashuhuda wa jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kujenga Hospitali za Wilaya, kuongeza vituo vya afya na zahanati. Hivyo basi, pale ambapo bajeti itaruhusu, tutaendelea kuajiri watumishi katika Idara ya Afya; na hawa 75 wanaokwenda Hai, ni sawa na asilimia 18.6 ya watumishi wote ambao wameajiriwa hivi sasa. Kwa hiyo, kadri uwezo utakavyoruhusu, tutaendelea kuleta watumishi katika Wilaya ya Hai.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili juu ya madeni ya watumishi, Mheshimiwa Mbunge kwanza amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za hawa watumishi na ili jambo amenieleza mimi mwenyewe zaidi ya mara mbili. Tayari tunashughulikia, ukiacha deni ambalo alikuwa analizungumzia la shilingi milioni 171, tayari yalikuja maombi 137 katika Ofisi ya Rais Utumishi yenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 246 ili yaweze kushughulikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa madeni yaliyolipwa ni Sh.50,690,000/= na madeni yenye thamani ya shilingi milioni 148 ambayo ni sawa na watu 88, yamerudishwa kwa mwajiri ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai kwa sababu yalikuwa na dosari mbalimbali. Pale ambapo Mkurugenzi wa Hai atarekebisha dosari zile na kuzileta katika Ofisi ya Rais Utumishi, basi nasi tutazifanyia uhakiki tuweze kulipa madeni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna madeni ya watu 27, sawa na shilingi milioni 33 na kitu hivi, tayari yameshafanyiwa uhakiki na yametolewa katika Ofisi ya Rais, Utumishi na sasa yapo Wizara ya Fedha, tayari kwa malipo muda wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.