Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe (3 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametupa uzima na zawadi ya kuwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Rais ambaye amefanya mengi na ambaye tunategemea ataendelea kuyafanya mengi kwa kipindi cha miaka mitano iliyobaki. Pia nishukuru sana viongozi wenzake Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani za pekee ziende kwa watumishi wa umma Tanzania nzima. Hawa ndiyo wanaotekeleza mipango ambayo sisi tunaipanga hapa na kama ambavyo wamemsikia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba wasiwe na wasiwasi Serikali yao inawapenda na kama alivyosema Mheshimiwa Rais yeye haongezi vibaba vibaba ataongeza mzigo wa kutosha, kwa hiyo, waendelee kushirikiana nasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, lipo jambo nimeliona hapa. Wakati najiandaa kuchangia hapa, nimesoma kwanza Mpango uliopita yale mapendekezo yaliyoletwa humu Bungeni, nikasoma Hansard za Wabunge walivyochangia na nikapitia kwenye changamoto ambazo zimesababisha Mpango ule usitekelezwe kwa asilimia 100, nikajifunza kitu ambacho naomba sasa wakati Waziri anakuja kuhitimisha atuambie hapa ni kwa asilimia ngapi hii michango ya Wabunge hapa inaenda kufanya mabadiliko kwenye rasimu hii tunayoijadili na kuleta Mpango ulio kamili? Tusipopata asilimia ya namna ambavyo michango yetu inaingizwa kwenye Mpango huu na mabadiliko yakatokea tutakuwa tunazungumza hapa halafu hayafanyiwi kazi. Kwa hiyo, niombe sana wakati anakuja kuhitimisha atuambie michango yetu imeingizwa kwenye Mpango huu kwa asilimia ngapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo lingine, wote hapa tunasema, hata dada zangu kule wanakiri kwamba Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri mno ya kutukuka lakini swali langu, hii kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais itakuwa sustainable, itaendelea kuishi? Hii miradi mikubwa inayoanzishwa na Serikali itaendelea hata kama yeye hayupo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachokishauri sasa tuweke mifumo ambayo itasaidia hizi shughuli nzuri zinazofanywa ziendelee kuishi. Hapa kuna wanasheria na Mwanasheria wa Serikali atusaidie, huko kwenye nchi zilizoendelea wana vitu vyao kama interest za Taifa lao, hivi hapa Tanzania hatuwezi kuwa na mambo yetu ambayo ni interest ya Tanzania na yakae kwenye Mpango wa muda mrefu hata kama ni miaka 50 kwa kuanzia baadaye twende miaka 100 ili tuwe na Mipango ya muda mfupi ya mwaka mmoja kama tunavyojadili sasa hivi lakini tuwe na Mipango ya miaka mitano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu tunafahamu namna siasa zetu zinavyoenda. Mara nyingi unakuta viongozi wanacheza beat kulingana na mpigaji anavyopiga ngoma. Sasa tunataka tutengeneze ngoma ya Watanzania ambayo tunaweza kuipiga kwa kipindi cha miaka 50 tuone hayo mambo ambayo yamewekwa yawe ni msingi na yaendelee. Namna ya kuyafanya yawe endelevu ni sisi Wabunge kuweka sheria za kubana lakini pia kuwa na taasisi ambazo ni strong zinazoweza kufanya maamuzi na kuyasimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo tutakuwa tumemfaidi Mheshimiwa Rais tuliyenaye sisi wa kizazi hiki na kizazi kijacho. Tukiacha haya, iko hatari kwamba akiondoka Mheshimiwa Rais na haya yataondoka, atakuja mwingine tutacheza ngoma nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe pia hebu tutazame mfumo wa elimu ya Tanzania, je, unatupa output nzuri kwa watu wetu? Wapo Wabunge wamechangia hapa na utaona kuna kitu ambacho tunakifanya. Sisi tuna-base kwenye kuangalia mazingira zaidi lakini ubora wa elimu bado hatujauweka vizuri. Je, mtaala tulionao una-reflect National objectives maana yake ni kwamba hii Mipango ya Taifa tunayoipanga tukienda kwenye mitaala yetu tunaikuta? Tunataka Serikali ya viwanda, je, mifumo ya elimu inatupeleka huko kuandaa watu waje wafanye kazi kwenye viwanda hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe pia wakati tunapanga Mipango hii tutazame pia suala la mitaala yetu. Kwa sababu moja ya changamoto iliyosababisha Mpango ule usitekelezwe kwa asilimia 100 ni kwamba nchi hii hatuna wataalam wa kuandika maandiko. Hii siyo sawa, watoto wanamaliza vyuo kila siku tunawezaje kuweka challenge kama hii, kwa hiyo, kuna shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine hapa tunaangalia michango yetu na hili siyo zuri sana ninavyolitazama mimi. Nitoe mfano mtoto wangu aliniuliza swali juzi hapa, akaniuliza baba hebu niambie, mle Bungeni kuna Mbunge anaitwa Musukuma na Mbunge mwingine wa Kahama, wanachangia vizuri kweli lakini wao wanasema darasa la saba. Zaidi ya hivyo, tunaambiwa wamefanikiwa kwenye maisha, hivi kuna sababu ya kusoma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili swali ingekuwa ni wewe, ungemjibuje mtoto akikuuliza kitu cha namna hiyo? Iko sababu ya kupita kwenye mfumo wa elimu ili tuweze kuwa na wataalam ambao wana output nzuri. Hata hii tunayosema kuwa sisi tuna sera nzuri, sera nzuri ni ile ambayo ina strong tools of implementation ambazo zinaleta output nzuri. Kwa hiyo na hili pia tunapoangalia tulitazame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nimetaka kuchangia ni kwenye kilimo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda hauko upande wako Mheshimiwa.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kilimo…

MWENYEKITI: Dakika tano tayari zimeisha.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo nilikuwa naanza? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwa dakika moja tu tafadhali sana, kwa kuwa Jimbo la Hai lilifanya kazi kubwa sana, naomba niongezee.

MWENYEKITI: Haya, dakika moja.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwenye eneo la kilimo. Pale Hai tukiamua kuna vyanzo vya maji vya kutosha, kuna ardhi nzuri tuko tayari kufanya kazi. Tukipewa vyanzo hivi vya maji tutalima na tutachangia kwenye Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye Vyama vya Ushirika, kaka yangu Mheshimiwa Nape tumezungumza sana, iko shida. Kule Hai hatuna ardhi ya kutosha lakini tuko tayari kufanya kazi lakini Vyama vya Ushirika vimekumbatia mashamba yetu, wanachokifanya mle ndani hatujui, ukiwaambia ni wataalam wa kufanya lobbying za kutosha. Tafadhali sana ile team niliyoomba iende kule Hai, Mheshimiwa Waziri Mkuu uko hapa, iko shida, uko utajiri mkubwa kule Hai kama tukiamua kufanya kazi. Ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. SAASHISA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Pia kabla ya kusema chochote, nitoe pole sana kwako wewe, kwa Mama Samia Suluhu kwa kuondokewa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, familia ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na Watanzania wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliyetuletea mwenyewe Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Hii kwangu naitafsiri kama ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuja kwa Watanzania. Leo nasimama hapa kushukuru na kurudisha sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ambayo alitupa ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtoa hoja ameeleza mambo makubwa ambayo yamefanywa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, lakini Watanzania kwa hakika wanajua mambo haya makubwa yaliyofanywa na Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Ukiangalia kipindi cha maombolezo, ukianzia safari ya kuaga pale Dar es Salaam, hii ni dhahiri kwamba Watanzania wanajua haya mambo makubwa ambayo Hayati Dkt. Magufuli aliyafanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawakujali ukubwa wa uzito wa uzio ulipo pale Uwanja wa Ndege. Wakatafsiri, ndege ni zetu wenyewe, Rais ni wetu wenyewe na sasa tunaingia wenyewe kwenye uwanja wetu. Waliingia kuonyesha mapenzi yao kwa Rais wao mpendwa wanayempenda. Vile vile kila mahali msafara ulipopita, wananchi walijitokeza kwa wingi. Hii ni ishara kubwa kwamba wananchi walimwelewa, walimpenda na hili ni zao la Watanzania kwa hakika. Naomba nishauri, haya mambo makubwa yaliyofanya tuyaweke kwenye kumbukumbu, niishauri Serikali ikiona inafaa itenge siku maalum iitwe Magufuli Day kwa ajili ya kumuenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Serikali ione namna ya kufanya hapa Dodoma, jiji ambalo mwenzangu aliyepita ameshaeleza namna ambavyo alipambana kuhakikisha linakuwa Makao Makuu ya Nchi; kijengwe kituo maalum kwa ajili ya kutunza kumbukumbu zake. Hii itakuwa ni sehemu kubwa ya kuendelea kuenzi hayo mambo mazuri aliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tayari alikuwa ameshaelekeza namna Wizara ya Elimu itakavyotengeneza mtaala wa kutengeneza historia yetu, basi kwenye mtaala wetu tuweke pamoja na viongozi wengine historia yake ili Watanzania waweze kuisoma vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme, tunalo jambo la kujivunia kwa haya mambo makubwa ambayo wenzangu wameeleza. Leo tunazungumza uwepo wa reli, treni ya umeme; haya ni mapinduzi makubwa ya kihistoria ambayo yamefanyika wakiwa pamoja na Mheshimiwa Mama Samia Suluhu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda moja kwa moja kwenye Azimio la pili. Haya mambo tunayoyataja leo, haya mambo tunayoyaona leo na kuyafurahia, barabara za chini na za juu zimejengwa, Vituo vya Afya vimejengwa, Mahakama wamejengewa ofisi nzuri. Kama wamejengewa Ofisi nzuri, watoto wanasoma kupitia Mfumo wa Elimu Bure, yamefanyika sambamba kwa kushirikiana na aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo ambaye leo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sina mashaka hata kidogo kwamba miradi ile yote ambayo ilikuwa imepangwa itaendelea vizuri kabisa bila wasiwasi wowote. Tumeona katika kipindi cha muda mfupi, ndani ya siku tano, cha uongozi baada ya yeye kuapishwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefanya mambo makubwa ndani ya siku hizo tano. Kule Bandarini tumeona kilichotokea, hii ni ishara kwamba kiatu kilipotoka kimeingia kiatu kingine chenye size ile ile kwa speed nyingine kubwa. Kwa hiyo, tunayo matazamio makubwa sana. Hili lililotokea leo, nadhani wale ambao wanafuatilia kwenye mitandao, hapa kuna watu wamepigwa chenga ya mwili. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walichokuwa wanadhani kwamba sasa tunafika mahali tunaenda kuyumba kama nchi, wamepigwa chenga ya mwili mzima. Leo tumeletewa tena Mtumishi mwingine wa Mungu, mtu ambaye ni mzalendo, amechukua nafasi ya Makamu wa Rais. Nasi hapa bila tashwishi tumempitisha kwa asilimia mia. Nawapongeza sana ndugu zangu upande ule kule kwa namna ambavyo tumeungana kwenye jambo hili. Huu ndiyo msingi wa kuanzia leo, tuendelee kuungana kwenye mambo ambayo ni ya Kitaifa ili hata wale wengine walioko huko, ambao wamebaki na kazi ya kujifungia ndani, kazi yao ni WhatsApp, Twitter, kukashifu, kutukana nchi yetu, wajifunze kuanzia leo kwamba sisi ni Watanzania, tunaenda kusimama kuhakikisha Rais wetu anaenda kutekeleza yale yaliyopo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na vile vile yale yote ambayo waliandika katika hotuba.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakumbuka hapa, Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli alituletea hotuba hapa Bungeni inayoonyesha mwelekeo wa Serikali. Hotuba ile kwa hakika waliandaa pamoja na Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu. Kwa hiyo, haya yote yanaenda kutekelezwa kwa speed ile ile. Kwa hiyo, niwatumie salamu pia wale waliodhani kwamba tunaenda kukwama, Mungu ameshusha tena baraka nyingine na leo tumeshuhudia hapa namna ambavyo tunaenda kukimbia kwa speed. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono na nawaomba sana Watanzania, tumwombee sana Mheshimiwa Rais wetu ili ayafanye yale ambayo ni matarajio yetu. Nasi kama Wabunge tusimame imara kuisaidia Serikali na kumshauri ili yale matarajio ya Watanzania yapate kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja zote. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na ninashukuru sasa umetaja vizuri jina langu ni jepesi tu Saashisha Elinikyo Mafuwe.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ndiyo nimepata nafasi ya kuchangia na kupata fursa ya kuweza kusema neno la shukrani kwa ajili ya wananchi wa Hai walionipa heshima kubwa sana ya kunichagua kuwa Mbunge wa Hai. Pia wametupa heshima kubwa sana kumchagua Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu kwa kura nyingi za kutosha 92%, lakini wametuchagulia madiwani wa kutosha sana. Nawashukuru sana wananchi wa Hai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye Bunge lako Tukufu. Hotuba hii ya Mheshimiwa Rais inatoa mwanga na mwelekeo wa Serikali kwa kipindi cha miaka mitano. Ukisoma kitabu hiki kinajibu matarajio ya wananchi wa Jimbo la Hai na wananchi wa Tanzania. Hii ni ishara kwamba Mheshimiwa Rais ni zawadi ya Watanzania, mambo anayoyafanya kwa nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mambo ambayo katika historia ya nchi hii hayatasahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunayo sababu ya kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetuletea zawadi ya Dkt. John Pombe Magufuli. Miradi mikubwa inayotekelezwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliyopita na hii ambayo tunaandaliwa tena ya miaka mingine mitano inaonyesha kwa kweli Mwenyezi Mungu ametupa zawadi ya Rais mwema. Nichukue nafasi hii kuendelea kumwombea Mungu ampe afya njema ili haya yote yaliyoandikwa na yaliyosomwa kwenye hotuba yake yaweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja ya jambo ambalo limenigusa sana ni habari ya kilimo. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais amesema sasa tutaenda kupandisha thamani ya mazao kwenye kilimo ambacho tunafanya. Kwetu kule Hai 78% tunategemea shughuli za kilimo. Nashukuru sana hotuba hii miongoni mwa mazao ya kimkakati yaliyotajwa, zao la kahawa limetajwa kama zao la taifa la mkakati.

Mheshimiwa Spika, sasa niseme kidogo, kule kwetu Hai zao la kahawa limepunguza tija kidogo kwa sababu ya utitiri wa vyama vingi vilivyopo kabla ya zao hili kufika sokoni. Pia zao hili limepunguza uzalishaji kwa sababu ya kukosekana kwa maji ya kumwagilia.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuunga mkono hoja hii na kuiomba Serikali ihakikishe tunapata maji ya kumwagilia ili tuweze kufufua zao hili la kahawa. Ikumbukwe kwamba mbegu za kahawa au chanzo na utafiti wa kahawa unafanyika ndani ya Jimbo la Hai. Taasisi ya Uchunguzi wa Zao la Kahawa (TaCRI) iko ndani ya Jimbo la Hai. Nashangaa utaona maeneo mengine zao hili linapandwa lakini pale Hai limefifia. Niombe sana Serikali yangu sikivu, tumeomba na nimepeleka ombi maalum la kupatiwa mito ya umwagiliaji mitano inayopatikana ndani ya Jimbo la Hai. Tukipata mifereji hii mitano itatusaidia sana kufufua zao hili la kahawa.

Mheshimiwa Spika, lakini siyo hilo tu, Jimbo la Hai Mungu ametujalia tunavyo vyanzo vikubwa sana vya maji lakini tatizo ni namna ya kuvifikisha kwa wananchi. Tunayo ardhi nzuri ya kilimo lakini tatizo ni namna gani tuitumie.

Mheshimiwa Spika, nilianza kwa kuomba wenzetu wa TARI Mlingano wafanye utafiti wa udongo, kazi ambayo imekwisha kukamilika. Kwa hiyo, kazi iliyobaki ni kuiomba Serikali iweze kutuletea maji kwa ajili ya kumwagilia maeneo haya mazuri.

Mheshimiwa Spika, niseme kilimo cha mazao ya mbogamboga katika Jimbo la Hai ni biashara ambayo Serikali tukiwekeza tutakusanya kodi nyingi sana, tunaweza tukafanana na wanaochimba madini. Sasa hivi ukiangalia mazao mengi yanaenda nchi nyingine sisi Hai tunazalisha lakini wanapeleka nchi nyingine kwa ajili ya kwenda kuongezewa thamani na thamani yanayoongezewa ni kufanyiwa packing tu. Kwa hiyo, naiomba Serikali sasa kule Hai tumekubaliana kuwa na ari mpya ya kilimo na viwanda, tupatiwe msaada wa packing, baada ya wananchi kulima tuweze kuyaongezea thamani kwa kufanya packing. Bahati nzuri tunao uwanja wa ndege tutaweza kusafirisha nje ya nchi ambapo kuna mahitaji makubwa ya chakula cha ziada kinachozalishwa katika Jimbo la Hai.

Mheshimiwa Spika, hotuba hii imezungumza pia habari ya kuendelea kujenga miradi ya maji. Nashukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, namshukuru Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu kwa kutuletea Naibu Waziri wa Maji pale Hai. Tulikuwa na tatizo kubwa sana la maji; moja katika Jimbo letu la Hai huduma ya maji inasimamiwa na Bodi za Maji kulikuwa na shida kubwa sana. Nashukuru Naibu Spika alifika pale dada yangu akafanya kazi kubwa na nzuri ya kurekebisha matatizo yaliyokuwepo kule. Kwenye bodi hizi kulikuwa na shida amezinyoosha vizuri mno.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nasimama hapa kushukuru kwamba tulikuwa na mradi wetu wa Kikafu ambao ulishathaminiwa siku nyingi wa shilingi bilioni 3.6. Nimepewa taarifa tayari Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli imetupelekea shilingi milioni 500 kwa ajili ya mradi huo, nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kule Lundugai tumepata shilingi milioni 200, hii ndiyo raha ya kuchagua CCM. Nataka niwaambie wananchi wa Hai walifanya maamuzi sahihi kabisa ya kuchagua Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kule Romu tumepata shilingi milioni 200. Naomba sana Serikali mradi huu wa Kikafu Chini utatusaidia kuondoa tatizo la maji. Pale Hai tunashida kubwa ya maji ya kunywa ukanda huu wa tambarare. Boma Ng’ombe, Mnadani, Weruweru, KIA hawana maji. Naomba sana Serikali fedha hizi shilingi bilioni 3.6 zikija kwa wingi zitatusaidia kuondoa tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nashukuru sana Serikali kulikuwa na mradi wa visima 18 vilikuwa vinapeleka maji Arusha imesema sasa kwa kuheshimu Sera ya Maji ni vizuri pia Hai baadhi ya maji yakabaki pale. Nashukuru sana kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema mchangiaji mwenzangu mama Anna Kilango Malecela, kwa kweli tunatakiwa kuongezea TARURA fedha ili waweze kufanya kazi. Miundombinu imeelezwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais lakini bado tunayo changamoto na mimi kule kwenye Jimbo la Hai hali si njema kwa habari ya barabara. Bado hatujafikia kiwango cha kukidhi matarajio ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, hapa niombe Mheshimiwa Waziri anayehusika, tunayo barabara moja ambayo inalalamikiwa sana sana na wakati Mheshimiwa Rais ananiombea kura pale aliwaambia nileteeni Saashisha hii barabara nitaitengeneza, ni kilometa 13. Barabara hii iliitwa barabara ya ng’ombe, jambo hili linawachukiza sana wananchi kwamba ile barabara tuliambiwa ni ya ng’ombe. Sasa hii barabara ni ya watu, tunaomba barabara ile iweze kuwekwa lami, ni kilometa 13 tu kuanzia mferejini kupita TaCRI, Lyamungo kwenda kutokea Makoa.

Mheshimiwa Spika, lakini tunayo barabara nyingine ambayo hata ninyi mkishuka kwenye ndege pale KIA mkiwa mnaenda Moshi ni rahisi, inakuwa ni barabara mchepuko inaweza kutumika kilometa 25 tu inaanzia Boma ya Ng’ombe kwenda TPC. Ziko barabara nyingi ambazo kwa kweli kama TARURA itaongezewa uwezo wataweza kufanya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumepeleka maombi maalum ya kupandisha hadhi barabara tano zilizoko ndani ya Jimbo la Hai kutoka TARURA kwenda TANROADS. Nashukuru sana kikao cha RCC kilipitisha barabara hii. Naiomba Serikali iongeze spidi kwenye mchakato huo ili barabara hizi ziweze kuhudumiwa chini ya TANROADS.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limezungumziwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais ni kuhusu umwagiliaji. Naomba sana, kwa kuwa nimeeleza hapo awali Jimbo la Hai linaweza kutumika kukusanya kodi nyingi kwenye mazao haya miradi hii ya umwagiliaji iweze kufanyiwa kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini iko changamoto, niombe sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na TAMISEMI tunayo miradi iliyoko kwenye kata yetu ya Weruweru na pale Kikafu Chini, ni Jumapili tu nimetoka kwenda kutembelea miradi hii, iko shida. Serikali imeleta fedha pale shilingi milioni 91 lakini ule mradi umetulia, hakuna kinachoendelea. Tayari Serikali imeshaweka fedha ziko shilingi milioni 700 kwenye Kata yetu ya Weruweru kule Mijengweni, Serikali imeweka mashine zimefungiwa kule, naomba sana Serikali itoe pesa ili miradi hii iweze kukamilika wananchi waweze kunufaika. Hii ni miradi ya muda mrefu, Kikafu Chini ni miaka nane lakini huu mwingine wa Mijengweni ni miaka 15 mashine zimefungiwa kule na bado zina uwezo wa kufanya kazi. Naomba sana Serikali itusaidie ili kuweza kukidhi matarajio na shauku kubwa aliyonayo Mheshimiwa Rais ya kuweza kuisaidia nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo limezungumzwa kwenye hotuba hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais kupata umeme kwenye vijiji vyote. Wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kwamba maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme wa REA yaweze kufikiwa. Niombe sana kwa kuwa Serikali imeshafanya kwa kiwango cha 84% hii asilimia iliyobaki Mheshimiwa Waziri ni ndogo sana. Wewe unafahamu na asubuhi nimezungumza na wewe kwamba yule mkandarasi pale Hai anatupa shida. Mimi naomba sasa Serikali mfanye maamuzi ili ile ahadi ya Mheshimiwa Rais iweze kutokea.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ni kengele ya kwanza?

SPIKA: Tayari muda wako umeisha.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, haya naomba kuunga mkono hoja.