Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Antipas Zeno Mgungusi (1 total)

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya barabara hiyo kutoka Kijiji cha Misegese kufika Malinyi Mjini huwa haifikiki kipindi chote, hata mvua ikinyesha siku moja tu, tunalazimika kutumia mitumbwi kufika Malinyi Mjini na magari hayafiki kabisa. Mkandarasi ambaye yuko site anaweka calavat moja badala ya yanayotakiwa kama sita au saba. Amepewa kazi ya kuinua tuta mita 200 badala ya kilometa moja ambayo ni uhitaji halisi. Je, Serikali haioni haja ya kumuongezea uwezo kujenga kulingana na uhitaji ambao nimeutaja?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda Malinyi baada ya Bunge hili ili kujionea hali halisi ya miundombinu na kutafuta suluhisho la pamoja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mgungusi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na swali la mwisho, naomba niseme kwamba barabara hii imekuwa inaulizwa sana na Waheshimiwa Wabunge wengi ambao ni wanufaika wa barabara hiyo. Kwa hiyo, niwadhihirishie ama niwaaminishe kwamba mara baada ya kikao hiki nitahakikisha naitembelea barabara hiyo ili niweze kuifahamu vizuri kwa sababu kila mara Wabunge wa eneo hilo wananifuata kwa ajili ya kutafuta utatuzi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili alilouliza kuhusiana na tuta linalojengwa na mkandarasi, naomba Mheshimiwa Mbunge Mgungusi kwa sababu, bahati nzuri mkandarasi yuko site, tutaongea na Meneja wa TANROADS ambaye ndiye anamsimamia mkandarasi huyu ili kama kuna shida ya kitaalamu ama ya uwezo, Serikali tutahakikisha kwamba tunampa maelekezo ya afanye vile inavyotakiwa kama ambavyo ipo kwenye design. Ahsante.