Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Priscus Jacob Tarimo (16 total)

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Kumekuwa na wimbi la kukosa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri waliomaliza kidato cha sita kwenye shule binafsi kwa madai kuwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi wazazi au walezi wao wana uwezo wa kuwalipia ada ya chuo.

Je, Serikali katika kuleta usawa kwenye fursa hii ya mikopo ya elimu ya juu haioni haja ya kutoa mikopo hiyo kwa kuzingatia ufaulu wa wanafunzi wote?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele kwenye Bunge lako tukufu, nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniona na kuniamini kwamba na mimi naweza nikawa miongoni wa watu wa kuweza kumsaidia.

Mheshimiwa Spika,baada ya hayo sasa, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge Moshi Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawalenga vijana wenye sifa za kitaaluma za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za elimu. Upangaji na utoaji mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura 178) ambayo inabainisha sifa za msingi za mnufaika ambazo zinajumuisha.Awe Mtanzania; awe amedahiliwa kwenye chuo kinachotambulika; awe ameomba mkopo, asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake. Aidha, kusoma shule binafsi za sekondari siyo kigezo cha mwanafunzi mwombaji kunyimwa mkopo wa kugharamia elimu ya juu. Wapo wanafunzi waliosoma shule binafsi na wanapata mkopo baada ya kuthibitisha uhitaji wao kwa mujibu wa vigezo vya utoaji mikopo.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa mujibu wa sheria tajwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ina mamlaka ya kuweka utaratibu wa kubaini wahitaji. Kwa sababu hiyo, Bodi huandaa mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika. Sifa za ziada zinazoainishwa kwa waombaji ni pamoja na; uyatima, ulemavu au wazazi wenye ulemavu na wale ambao masomo yao ya sekondari au stashahada yalifadhiliwa ambapo katika kundi hili wapo waombaji wengi waliosoma katika shule za sekondari za kulipia.

Mheshimiwa Spika, nashauri Waheshimiwa watusaidie kutoa elimu ili kuwezesha jamii kubadili mtazamo huu. Aidha, wawashauri waombaji wajaze kikamilifu fomu za maombi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Bodi wakati wa uombaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na kuambatanisha nyaraka zote muhimu ili kuepuka uwezekano wa mwanafunzi mwenye sifa stahiki kukosa mkopo kutokana na kutojaza kwa usahihi fomu ya maombi ya mkopo.
MHE. PRISCUS J. TARIMO Aliuliza:-

Kumekuwa na wimbi la kukosa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri waliomaliza kidato cha sita kwenye shule binafsi kwa madai kuwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi wazazi au walezi wao wana uwezo wa kuwalipia ada ya chuo.

Je, Serikali katika kuleta usawa kwenye fursa hii ya mikopo ya elimu ya juu haioni haja ya kutoa mikopo hiyo kwa kuzingatia ufaulu wa wanafunzi wote?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele kwenye Bunge lako tukufu, nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniona na kuniamini kwamba na mimi naweza nikawa miongoni wa watu wa kuweza kumsaidia.

Mheshimiwa Spika,baada ya hayo sasa, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge Moshi Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawalenga vijana wenye sifa za kitaaluma za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za elimu. Upangaji na utoaji mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura 178) ambayo inabainisha sifa za msingi za mnufaika ambazo zinajumuisha.Awe Mtanzania; awe amedahiliwa kwenye chuo kinachotambulika; awe ameomba mkopo, asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake. Aidha, kusoma shule binafsi za sekondari siyo kigezo cha mwanafunzi mwombaji kunyimwa mkopo wa kugharamia elimu ya juu. Wapo wanafunzi waliosoma shule binafsi na wanapata mkopo baada ya kuthibitisha uhitaji wao kwa mujibu wa vigezo vya utoaji mikopo.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa mujibu wa sheria tajwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ina mamlaka ya kuweka utaratibu wa kubaini wahitaji. Kwa sababu hiyo, Bodi huandaa mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika. Sifa za ziada zinazoainishwa kwa waombaji ni pamoja na; uyatima, ulemavu au wazazi wenye ulemavu na wale ambao masomo yao ya sekondari au stashahada yalifadhiliwa ambapo katika kundi hili wapo waombaji wengi waliosoma katika shule za sekondari za kulipia.

Mheshimiwa Spika, nashauri Waheshimiwa watusaidie kutoa elimu ili kuwezesha jamii kubadili mtazamo huu. Aidha, wawashauri waombaji wajaze kikamilifu fomu za maombi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Bodi wakati wa uombaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na kuambatanisha nyaraka zote muhimu ili kuepuka uwezekano wa mwanafunzi mwenye sifa stahiki kukosa mkopo kutokana na kutojaza kwa usahihi fomu ya maombi ya mkopo.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali wa kupima na kurasimisha maeneo yanayozunguka Mamlaka za Miji ili kuepuka kuendelea kuwa na makazi holela pamoja na kuweza kupeleka huduma za dharura kama ambulance na zimamoto?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Sura ya 355 Fungu la 7(1), mamlaka za upangaji ambazo ni Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri za Wilaya nchini zina wajibu wa kupanga, kupima na kurasimisha maeneo yote yaliyo chini ya mamlaka zao. Pamoja na wajibu huo wa kisheria kwa mamlaka za upangaji, bado kasi ya upangaji na upimaji ardhi nchini imekuwa sio ya kuridhisha. Hivyo, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na mamlaka za upangaji pamoja na taasisi binafsi katika utekelezaji wa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kasi ndogo ya upangaji na upimaji, katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/2021 Wizara yangu imeziwezesha mamlaka za upangaji 21 nchini kupanga na kupima viwanja vipatavyo 56,792 kwa gharama ya shilingi billioni 3.5. Lengo la kutoa fedha hizo ni kuziwezesha mamlaka za upangaji kuongeza wigo wa upatikanaji wa viwanja vilivyopangwa na kupimwa katika maeneo yao na kurasimisha makazi mijini. Pamoja na kupatiwa fedha hizo, jumla ya makazi yapatayo 735,047 yamerasimishwa nchini katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Machi, 2021 katika Halmashauri 104 nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo yote yaliyopangwa, kupimwa na kurasimishwa, utengaji wa maeneo kwa ajili ya matumizi ya umma umezingatiwa ili kuruhusu utoaji wa huduma za kijamii. Natoa rai kwa mamlaka za upangaji nchini kuhakikisha zinatenga fedha katika bajeti zao kila mwaka ili kuharakisha upangaji, upimaji ardhi na urasimishaji wa makazi katika maeneo yao. Ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, ni nini mpango wa Serikali kuwawezesha akina baba kiuchumi baada ya mpango wa Halmashauri wa kuwawezesha akina mama, vijana na watu wenye ulemavu kuwa na mafanikio makubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea kuwezesha wananchi kiuchumi kwa kutoa mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Mikopo hiyo hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 kifungu cha 37A inayoelekeza kutenga 10% ya mapato yanayokusanywa na Halmashauri kwa ajili ya mikopo ya 4% kwa wanawake, 4% kwa vijana na 2% kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, lengo la mikopo hii ni kusaidia makundi maalum katika jamii ambayo hayawezi kupata mikopo katika mabenki ya biashara na taasisi za fedha kwa sababu ya masharti magumu ikiwemo dhamana na riba kubwa. Hivyo, Serikali ilitoa kipaumbele kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa kuwa wengi wao hawakopesheki katika mabenki na taasisi za fedha. Kwa sasa Serikali haikusudii kuanzisha mpango wa kuwawezesha wanaume au akina baba katika mikopo hii.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, ni nini mpango wa Serikali wa kukamilisha Mradi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi ambao umeanza tangu mwaka 2008/2009 bila kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo la kuwahudumia mama na mtoto katika Hospitali ya Mawenzi umekamilika kwa asilimia 70. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetolewa na kutumika.

Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 5.2 kimetengwa kwa mwaka 2021/2022 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 3.6 zitatumika kukamilisha ujenzi na kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kitatumika kununulia vifaa tiba na ujenzi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Januari, 2022.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, ni nini hatma ya biashara ya maduka ya kubadilisha fedha (Bureau de Change) yaliyofungwa na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ukaguzi ambao umefanyika mwaka 2018/2019 ulisababisha maduka mengi ya kubadilisha fedha za kigeni kufungwa kutokana na kubainika kuendesha biashara bila kuzingatia sheria na kanuni husika. Baada ya kufungwa kwa maduka hayo, benki za biashara nchini zilihamasishwa kuendelea kutoa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni katika matawi yake yote nchini. Kwa sasa benki zote za biashara zinatoa huduma hizo nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, pia maduka ambayo hayakufungwa yameendelea kufungua matawi na kutoa huduma hizo katika miji mbalimbali nchini. Kwa ujumla hali ya upatikanaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ni ya kuridhisha. Aidha, maduka yaliyofungwa pamoja na kampuni nyingi ambayo yanayotaka kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni nchini, yanaruhusiwa kuomba leseni Benki Kuu kwa kuzingatia matakwa ya Sheria za Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 pamoja na Kanuni za Biashara ya Kubadilisha Fedha za Kigeni ya mwaka 2019. Hadi kufikia tarehe 30 Julai 2021, Benki Kuu ilikuwa imepokea maombi mapya manne ya leseni ya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ambazo yanafanyiwa uchambuzi na wahusika watapewa leseni iwapo watakuwa wamekidhi vigezo.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali kuwasikiliza na kufanyia kazi hoja za wamachinga, hasa baada ya zoezi la kuwapanga?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inafanyia kazi hoja za wamachinga, hasa baada ya zoezi la kuwapanga kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ambapo Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hukukutana nao mara kwa mara kwenye vikao na kujadiliana nao kupitia viongozi wao kwa lengo la kushughulikia hoja na kero zao.

Mheshimiwa Spika, katika ngazi ya Taifa, Serikali inasikiliza hoja zao kupitia viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Taifa. Kutokana na vikao vinavyofanyika, Serikali imeweza kuwajengea uwezo katika masuala ya uongozi na utatuzi wa changamoto zao. Pia watendaji wa kata sehemu mbalimbali nchini ikiwemo kwenye masoko wamekuwa na mchango mkubwa katika kuwasikiliza na kufanyia kazi hoja na kero zao kwa kadri zinavyojitokeza. Ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, ni nini mpango wa Serikali wa kupambana na majanga ya moto yanayotokea mara kwa mara kwenye masoko nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na mikakati ya kuzuia majanga ya moto kwa kufanya ukaguzi wa masoko, kutoa ushauri wa kitaalam na utoaji wa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto. Jeshi pia linasisitiza kuwepo kwa vifaa vya awali vya kuzima moto (fire extinguishers) na ving’amuzi vya moto (fire detectors) na uwepo wa walinzi katika maeneo yote ya masoko.

Mheshimiwa Spika, napenda kuitumia fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba masoko yote nchini yamekaguliwa na wahusika kupewa ushauri stahiki. Jeshi pia linafanya ufuatiliaji ili kujiridhisha kama ushauri uliotolewa unafanyiwa kazi.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kusaidia Halmashauri zinazozunguka Mbuga na Hifadhi kwa kutoa CSR kwenye mapato ya utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kupitia utekelezaji wa Sera ya Uwajibikaji Kijamii (Community Social Responsibility - CSR), Serikali inatekeleza miradi ya ujirani mwema kwa jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa zikiwemo Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Wanyamapori za Jamii (WMAs). Katika kutekeleza Sera hiyo, Halmashauri za Wilaya pamoja na jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa, zinanufaika na mapato yanayotokana na utalii ikiwemo kupatiwa miradi mbalimbali ya kijamii inayoibuliwa na wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya, Sekta ya elimu, Sekta ya Maji na Sekta ya Ujenzi. Miradi hii hutekelezwa na Taasisi za Uhifadhi nchini ambazo ni TANAPA, TAWA na NCAA.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Uwindaji wa Kitalii, Serikali pia imekuwa ikitekeleza Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na.5 ya 2009 ambayo inaelekeza kuwa asilimia 25 ya fedha zinazotokana na ada za wanyamapori waliowindwa katika vitalu vya uwindaji wa kitalii zirudishwe kwenye halmashauri zinazopakana na maeneo ya uwindaji. Aidha, katika maeneo ya WMAs, Kanuni za WMAs za mwaka 2018 zinaelekeza kuwa asilimia 75 ya ada ya kitalu, asilimia 55 ya ada ya wanyamapori wanaowindwa na asilimia 45 ya gharama za uhifadhi zinazotokana na uwindaji wa kitalii zirudishwe kwa jamii inayomiliki maeneo husika. Wizara imekuwa ikitekeleza matakwa haya kupitia TAWA. Ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itahuisha mpango wa upanuzi wa Manispaa ya Moshi kutoka kilometa 58 hadi 146 pamoja na kuwa Jiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tarehe 25 novemba, 2015 ilipokea ombi la uendelezaji wa Manispaa ya Moshi kuwa Jiji kwa kuongeza ukubwa wa mipaka ya kiutawala kutoka kilomita za mraba 58 hadi kilomita za mraba 142 kwa kuongeza vijiji kutoka Halmashauri za Wilaya za Moshi na Hai.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mwongozo wa Uanzishaji wa Maeneo ya Utawala wa mwaka 2014, kigezo cha ukubwa wa kuanzisha halmashauri ya jiji ni kilometa za mraba 1,000 na Halmashauri ya Wilaya ni kilometa za mraba 5,000.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mamlaka nyingi zilizoanzishwa bado zinaupungufu wa miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya utawala na huduma za kijamii, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu katika maeneo ya utawala yaliyopo.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali kuhusu malalamiko ya wastaafu juu ya kikokotoo kinachotumika kupiga mahesabu na kulipa mafao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitangaza matumizi ya kanuni mpya ya mafao (kikokotoo) ya pensheni kuanzia tarehe 1 Julai, 2022 kupitia Gazeti la Serikali Na. 357 Toleo la tarehe 20 Mei, 2022. Kanuni hiyo iliandaliwa kwa kuzingatia haja ya kuboresha na kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya Mifuko ya Pensheni kuwa endelevu.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuwaelimisha wananchi hususani waajiri na wanachama wa Mifuko ya Pensheni wakiwemo wastaafu kuhusu faida ya kanuni mpya ya mafao ya pensheni. Hivyo, Serikali kupitia Mifuko ya Pensheni na kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) imejipanga na inaendelea kutoa elimu ya Kanuni hiyo. Hadi kufikia Tarehe 30 Juni, 2023, Mifuko iliweza kutoa elimu kwa jumla ya waajiri 5,580 kati ya waajiri 6,200 waliopangwa kufikiwa kipindi hicho. Aidha, wanachama 131,497 walifikiwa na mafunzo hayo. Mifuko itaendelea kutoa elimu kama sehemu ya majukumu yao ya kila siku, ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kusimamia ubora wa nguo na viatu vya mtumba vinavyotoka nje ya nchi ambavyo havina ubora na bei ni kubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania inatekeleza majukumu ya udhibiti wa ubora na usalama wa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini kupitia Kitengo cha Udhibiti wa Ubora wa Bidhaa zinazoingia na kutoka nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bidhaa zote zinazotoka nje ya nchi zilizoainishwa kwa vigezo mbalimbali zikiwemo nguo na viatu vya mtumba hukaguliwa chini ya mfumo wa ukaguzi wa shehena kabla ya kuingia nchini (Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards), ukaguzi ambao unafanywa na mawakala waliopewa dhamana na shirika. Pamoja na kukagua ubora, vilevile usalama wa nguo na viatu vya mitumba hukaguliwa kwa vigezo vya kiafya na kutoa cheti cha afya (Fumigation Certificate). Endapo bidhaa hizo zitakidhi vigezo vilivyowekwa na kuhakikiwa na Maafisa Afya, pale shehena husika inapofika bandarini Dar es Salaam au katika mpaka wowote, nashukuru.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwezesha Shule za Kata kuwa pia za Kidato cha Tano na Sita kutokana na kuongezeka kwa ufaulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiongeza shule za Kidato cha Tano na Sita kulingana na uhitaji. Kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali ilisajili jumla ya shule 23 ambazo zilikuwa Shule za Kata kuwa Shule za Kidato cha Tano na Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza shule za Kidato cha Tano na Sita katika Halmashauri zote nchini kwa kuongeza miundombinu ya mabweni, madarasa mabwalo kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha na uhitaji.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani kusaidia Halmashauri zinazozunguka Mbuga/Hifadhi za Taifa kupitia CSR kutoka kwenye mapato ya utalii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia utekelezaji wa Sera ya Uwajibikaji Kijamii (Community Social Responsibility - CSR) Serikali inatekeleza miradi ya ujirani mwema kwa jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Hifadhi za Wanyamapori za Jamii. Katika kutekeleza Sera hiyo, Halmashauri za Wilaya pamoja na jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa, zinanufaika na mapato yanayotokana na utalii ikiwemo kupatiwa miradi mbalimbali ya kijamii inayoibuliwa na wananchi kwenye sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhakikisha Halmashauri za Wilaya pamoja na wananchi wanaopakana na maeneo yaliyohifadhiwa wananufaika kutokana na mapato ya utalii kupitia utekelezaji wa Sera ya Uwajibikaji Kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, Mwaka 2021 – Januari, 2022 Sekta ya Mifugo imeuza nyama nje ya nchi kwa asilimia ngapi na upi mkakati wa kuimarisha Sekta hii?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya tani 10,415 za nyama zimeuzwa nje ya nchi zenye thamani ya dola za Kimarekani 42,500,994.90 ikilinganishwa na tani 1,774.29 za nyama zenye thamani ya dola za Kimarekani 4,290,000 zilizouzwa katika mwaka wa fedha 2020/2021. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 492.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuimarisha tasnia ya nyama ikiwemo; kuvutia uwekezaji katika ujenzi wa machinjio za kisasa zinazokidhi viwango vya kimataifa ambapo hadi sasa, zipo machinjio sita tu zenye ithibati ya kuuza nyama nje ya nchi; kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara katika tasnia ya nyama kwa kupunguza tozo na kodi za usafirishaji wa nyama nje ya nchi; kuwajengea uwezo vijana waliohitimu vyuo vya mifugo kupitia vituo atamizi ili waweze kufuga kisasa na kuzalisha malighafi ya kutosha kwa ajili ya viwanda vya kuchakata nyama na kuboresha mbari za mifugo kupitia uhimilishaji, ugawaji wa madume bora na usambazaji wa mitamba ya ng’ombe wa nyama.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI K.n.y. MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali wa kuimarisha Jeshi la Zimamoto hasa katika maeneo ya miji yenye hatari kubwa ya majanga ya moto?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika mpango wa kuimarisha huduma za zimamoto na uokoaji nchini kwa kuimarisha na kuongeza vifaa vya kisasa. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 vitajengwa jumla ya vituo saba vya zimamoto na uokoaji kwa kuanza na mikoa isiyokuwa na vituo hivyo. Mikoa hiyo ni pamoja na Songwe, Simiyu, Kagera, Njombe, Manyara, Katavi na Geita. Aidha, kwa kuzingatia ukuaji wa haraka wa Jiji la Dodoma ambalo ni Makao Makuu ya nchi, ujenzi wa vituo viwili Chamwino na Nzuguni utakamilika hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa ajira mpya ya askari 400 ambao kwa sasa wapo mafunzoni. Vilevile Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu kinga dhidi ya majanga ya moto kuanzia shuleni, maeneo ya biashara na yale yenye mikusanyiko mikubwa ya watu. Nashukuru.