Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mrisho Mashaka Gambo (5 total)

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imefanya kazi nzuri ya kujenga barabara kwenye Jiji la Arusha na hasa ukizingatia kwamba, barabara ya mzunguko ya bypass ambayo imesaidia sana kwa watalii na wananchi wa Jiji la Arusha, lakini bado kuna kipande cha Kata ya Moshono ambacho kinatoka eneo la kona ya Kiseliani kuunganisha barabara ya bypass maarufu kama barabara ya T Packers Osunyai kama kilometa saba. Je, Wizara ya Ujenzi haioni sasa ni wakati sahihi wa kumalizia kipande hiki ili kupunguza msongamano na kuweka mazingira mazuri zaidi ya utalii pamoja na wananchi wa Kata ya Moshono?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye ukurasa wa 77 barabara za bypass kwa ajili ya kupunguza msongamano zimeainishwa zikiwemo Miji ya Dar-Es-Salaam, Mbeya na Arusha ni kati ya miji ambayo zitanufaika na barabara hizi za mizunguko kwa ajili ya kupunguza misongamano. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha kwamba, barabara hii aliyoitaja ni moja ya barabara ambazo zitatekelezwa katika kipindi hiki tutakachoanza bajeti katika kipindi hiki cha miaka mitano. Ahsante. (Makofi)
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, naomba niweke wazi tu kwanza kwamba sijaridhika na majibu ya Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake sekta ya utalii kwa Mkoa wa Arusha na nchi nzima imeathirika sana. Wananchi wengi sana wamekosa ajira, madereva wamekosa ajira kwa sababu magari hayatembei kutokana na uchache wa watalii, guides wamekosa ajira, wafanyakazi wa mahoteli wamepunguzwa kwenye maeneo yao, magari ambayo yangetembea, yangeweka mafuta shell zingeweza kufanya biashara zao.

Mheshimiwa Spika, tukiangalia kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, karibu nchi nyingi zimeweza kupunguza tozo kipindi hiki. Mfano, Kenya, Nairobi National Park wamepunguza tozo kutoka Dola 43,000 mpaka 35,000. Ukienda Rwanda kwenye masuala ya gorilla wamepunguza kutoka Dola 1,500 mpaka Dola 500. Ukienda Uganda kwenye masuala pia ya gorilla wamepunguza kutoka Dola 700 mpaka 500. Naomba Wizara ya Maliasili na Utalii iangalie athari za ugonjwa wa Corona kwenye masuala ya ajira na masuala mengine.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza, Wizara ya Maliasili na Utalii ina mpango gani wa kuipa ahueni sekta ya utalii ili kuweza kunusuru changamoto kubwa ya ajira ambayo imewaathiri wananchi wa Mkoa wa Arusha pamoja na Tanzania kwa ujumla?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Gambo ametoa takwimu, wenzetu wamepunguza kutoka Dola 1,500 mpaka 1,000, kutoka Dola 700 mpaka 500; hizo ndiyo takwimu zake. Viwango vya kuingia katika hifadhi zetu bado viko chini sana ukilinganisha na ubora wa hifadhi tulizonazo. Ukisema Serengeti hulinganishi na hifadhi yoyote iliyoko katika Afrika Mashariki; kule Rwanda unaona gorilla tu. Serengeti is a jewel, bado ni Dola 60. Kwa hiyo, viwango bado viko chini sana. Nilitaka kwanza hilo niliweke sawa.

Mheshimiwa Spika, la pili, Serikali inatoa tahafifu gani hasa kwa kipindi hiki? Wizara imegawa suala la utalii katika misimu miwili; high season na low season. Ongezeko hilo ambalo tunalisema litagusa kwenye high season tu; low season bado rates zitabaki pale pale.

Mheshimiwa Spika, hii ni kwa nini? Katika high season, sehemu kama Ngorongoro kwa siku moja yanaingia magari 400 ambayo yanaathari kubwa kiikolojia wakati kwenye low season yanaingia magari 70. Tunataka tu-balance sasa, hawa wafanyabiashara wetu ambao tutawapa tahafifu, waende sasa kwenye low season ili tutunze pia na ikolojia iliyopo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, AJIRA, KAZI, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, pamoja na kuunga mkono majibu mazuri yaliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini swali la msingi na maswali ya nyongeza yamegusa pia sekta ya ajira katika sekta hiyo ya maliasili.

Mheshimiwa Spika, naomba kuliambia Bunge lako Tukufu, wakati wa Covid, hata sasa na hata baadaye, kama kunatokea tatizo lolote linalohusiana na suala la wafanyakazi, tunaomba wafanyakazi, waajiri watumie platform yao ambayo ni ya dhana ya utatu ambayo tumekuwa tukiitumia mara nyingi kuamsha mijadala na kutafuta solution katika mazingira ya mawanda hayo ya sekta ya kazi, ajira na Serikali. Kwa hiyo, nawashauri watumie platform hiyo.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, Mkoani Arusha kuna shule ya St. Jude, ni shule ambayo inasomesha watoto wenye mazingira magumu na kwa kupitia misaada ya watu mbalimbali huko duniani. Siku za karibuni TRA imeenda kwenye account ya shule hiyo imechukua fedha na kusababisha shule hiyo kupata misukosuko na kufungwa kiasi ambacho watoto wenye mazingira magumu wamekosa nafasi ya kwenda kusoma pamoja. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ahueni kwa shule hii ili suala la elimu ambayo ni kipaumbele chetu liweze kupewa mstari wa mbele?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama alivyobainisha uwepo wa shule hiyo na changamoto zilizotokea kuhusiana na wenzetu wa TRA, suala hili naomba tulichukue twende tukalifanyie kazi na badaye tutaweza kutoa majibu muafaka kwa Mheshimiwa Mbunge na Mkoa wa Arusha kwa ujumla. Ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa changamoto ya umeme wa Jimbo la Handeni inafanana kabisa na Jimbo la Arusha Mjini, napenda kuuliza maswali ya nyongeza yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba Jiji la Arusha ni jiji la kitalii, lakini bado kuna kata ambazo zinachangamoto kubwa sana ya umeme Kata kama za Telati, Kata ya Olasiti, Olmoti, Moshono, Mulieti kule maeneo ya Losoito, Sokoni 1 na Sinoni. Ningependa kufahamu, je, Wizara ina mpango gani kupitia Mradi wa Peri-urban ili kuhakikisha kwamba wananchi hawa ambao wapo kwenye Jiji la Kimataifa, Jiji la Utalii wanaondokana na changamoto ya umeme katika jimbo letu?

Mheshimiwa Naibu Spika, la piliā€¦.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa moja tu, hilo ni la nyongeza.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gambo, Mbunge wa Arusha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inapeleka umeme katika maeneo mbalimbali kwa programmes tofauti. Ziko awamu za REA ambazo zimeendelea, ziko programme ya densification, lakini ipo programu peri-urban ambayo inapeleka umeme kwenye maeneo ambayo yana asili ya ukijiji lakini yako mjini. Mkoa wa Arusha tayari umeshanufaika na awamu ya kwanza ya densification, peri-urban kupeleka umeme katika baadhi ya maeneo na iko awamu ya pili ya peri-urban ambayo itakuja, inaanza mwezi wa Saba.

Katika maeneo ambayo hayajapata Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza na Tanga yatapelekewa umeme katika Mradi huo wa pili wa peri-urban. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba awamu hiyo ya pili ikianza basi na yeye maeneo yake yatapatiwa umeme katika awamu hiyo.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri na Waziri lakini tumeona kwamba pamoja na faini ya bodaboda kuwa kubwa, lakini bado matukio ya uhalifu yameongezeka kwa hiyo ni ishara kwamba faini haiwezi kuzuia uhalifu, lakini ukiangalia pia katika utaratibu wa kawaida sasa hivi tuna changamoto kubwa ya ajira katika nchi yetu na Serikali yetu imeahidi kutoa ajira milioni nane na miongoni mwa watu ambao wanajiajiri sehemu yao ni bodaboda.

Mheshimiwa Spika, nadhani ni vizuri sasa Wizara ya Mambo ya Ndani ikaleta utaratibu hapa ili tuweze kupitia upya mchakato wa faini hizi kwa sababu tunafahamu mtu leo ukiua una adhabu yake, lakini pia leo mtu ukiiba kuku una adhabu yake, haiwezekani gari ambalo ni milioni mia tatu faini yake elfu thelathini na pikipiki ya milioni mbili faini yake elfu thelathini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa tunasema elfu thelathini kama ni kosa ni moja, bodaboda anaweza kupigwa makosa manne kwa siku akalipa laki na ishirini na pikipiki ile sio ya kwake, inabidi pia apekeleke hela kwa mwenye pikipiki na yeye pia aweze ku-survive. Nadhani Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma watu hawa wa bodaboda ili changamoto iweze kuondoka.

Mheshimiwa Spika, swali langu katika eneo hili tumeona watu wa traffic wamekuwa kwa kiwango kikubwa wanawakamata sana bodaboda pamoja na watu wa bajaji. Je, Wizara ya Mambo ya Ndani ina mpango gani wa kutoa maelekezo mahususi kwa watu wa traffic ili sio kila kosa analokamatwa nalo mtu lazima apigwe faini waweze kutoa onyo pamoja na utaratibu mwingine?

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kumekuwa kukijitokeza baadhi ya askari wetu kutokuwa waungwana. Unajua shughuli hizi huwezi ukazi-control kwa sheria per se a hundred percent. Kwa hiyo, hekima, busara na hasa unapokuwa mtumishi wa Umma unayewatumikia watu lazima utumie hekima na busara. Enforcement a hundred percent na yenyewe huwa kidogo ina shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge, lakini pia na Waheshimiwa Wabunge mtusaidie, baadhi ya vijana wetu wanafanya kusudi na ninyi wenyewe mashuhuda, mnaendeshewa vibaya sana bodaboda hata hapa mjini, tukiacha hii hali na yenyewe ni shida pia. Mimi niseme tu, sote tutekeleze wajibu wetu na kwa upande wa askari polisi, hasa wa usalama barabarani wajitahidi kuwa wanatumia busara katika kuhakikisha kwamba wanasimamia sheria siyo kukomoa.