Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mrisho Mashaka Gambo (14 total)

MHE. MRISHO M. GAMBO Aliuliza: -

Serikali imeongeza viwango vya tozo za utalii kwa Hifadhi zilizo chini ya TANAPA kuanzia mwezi Julai, 2021.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kusitisha tozo hizo ili kutoa fursa kwa Sekta ya Utalii nchini ambayo imeathirika sana na ugonjwa wa Corona?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ongezeko la tozo limelenga Hifadhi za Taifa nne ambazo ni Ziwa Manyara, Serengeti, Tarangire na Arusha. Kiwango cha tozo kilichoongezeka kwa hifadhi husika ikilinganishwa na viwango vya sasa ni kama ifuatavyo: -

HIFADHI ENTRYFEE SEASONAL ANDSPECIALCAMPING FEE CONCESSIONFEE
Tozoya sasa Tozokuanzia 1/7/2021 Tozoyasasa Tozo kuanzia 1/7/2021 Tozoya sasa Tozo kuanzia 1/7/2021
Serengeti 60USD 70USD 50USD 60USD 50USD 60USD
Manyara 45USD 50USD 50USD 60USD 40USD 40USD
Tarangire 45USD 50USD 50USD 60USD 40USD 40USD
Arusha 45USD 50USD 50USD 60USD 40USD 40USD

Mheshimiwa Spika, wakati wafanyabiashara ya utalii wakiishinikiza Serikali kuacha tozo zikiwa za chini sana, wenyewe wamekua wakiwatoza watalii tozo za juu ambazo hawataki kuziweka wazi kwa Serikali. Usiri wa tozo za makampuni binafsi unainyima Serikali taarifa za msingi za kuweza kuona uzito wa hoja yao.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwamba suala la COVID-19 lisitumike kuinyima Serikali mapato ambayo yanasaidia kukuza uchumi wa nchi. Pia, nisisitize kwamba pamoja na shinikizo la kupunguza tozo, sekta binafsi haijawasilisha takwimu zozote Serikalini za kuthibitisha ongezeko la idadi ya wageni waliofuta safari zao kuja nchini kutokana na ongezeko la tozo.

MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga stendi ya kisasa Jijini Arusha ili kukidhi mahitaji ya Wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Jiji la Arusha imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 30 katika eneo la Bondeni City kwa ajili ya ujenzi wa stendi mpya ya kisasa. Stendi mpya itakayojengwa itazingatia pia mahitaji ya wafanyabiashara wadogo kama Machinga, stendi ya teksi, pikipiki, bajaji, Ofisi za Polisi wa Usalama Barabarani na maeneo ya huduma mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayoendelea sasa ni taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu wa mradi huo. Mradi huu wa ujenzi wa Stendi ya Kisasa Jiji la Arusha utajumuishwa kwenye Mradi wa Uboreshaji Miundombinu yaani Tanzania Cities Transforming Infrastructures and Competitiveness - TACTIC utakaotekelezwa kwenye Halmashauri 45 za Majiji, Manispaa na Miji nchini ambapo Serikali inaendelea na majadiliano na Benki ya Dunia.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua Viwanda vya General Tires na Pharmaceutical Industries Ltd. ili kuongeza ajira na upatikanaji wa dawa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Bisahara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na viwanda mbalimbali nchini vikiwemo viwanda vya matairi na dawa ili kuchochea uchumi wa nchi kwa kuzalisha bidhaa na ajira. Kiwanda cha matairi kinachojulikana kama General Tire kilichopo katika Jiji la Arusha ni moja ya kiwanda kikubwa cha matairi katika ukanda wa Afrika Mashariki. Uzalishaji katika kiwanda hicho ulisimama mwezi Agosti, 2007 baada ya kukosa fedha za kujiendesha, husasan fedha za kununua malighafi. Hivyo, Wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukifufua kiwanda hicho ili kufikia malengo ya Serikali kujitosheleza kwa mahitaji ya matairi nchini, kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kuagiza matairi kutoka nje na kuzalisha ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) iliunda Timu ya Wataalam ili kufanya tathmini juu ya njia bora ya kuendesha kiwanda hicho. Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa mitambo na teknolojia iliyopo imepitwa na wakati na hivyo ikashauriwa kuwa mashine na mitambo ya kisasa ifungwe ili kuleta tija na ufanisi katika uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kupitia NDC inaendelea kutafuta mwekezaji mwenye uwezo wa kuwekeza teknolojia mpya katika kiwanda hiki hususan ya kisasa kuendana na mahitaji ya bidhaa za matairi zilizopo sokoni. Tayari utaratibu wa kutangaza zabuni umefanyika ili kumpata mbia wa kufufua Kiwanda cha Matairi Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo na Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda na Mkakati wake, viwanda vya dawa ni moja ya viwanda vya kipaumbele ikizingatiwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika kuagiza dawa kutoka nje ya nchi kwa mwaka, ajira zinazopotea pamoja na umuhimu wa kuzalisha dawa kwa ajili ya usalama wa wananchi wake. Hivyo, Wizara inaona kuna umuhimu mkubwa wa kuharakisha kufikiwa kwa maamuzi ya kesi inayoikabili Kiwanda cha TPI na pia kwa kuzingatia kuwa Serikali inamiliki hisa asilimia 30 katika Kiwanda hicho ili kuruhusu mara moja kuanza kwa uzalishaji wa dawa. Ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Kwa muda mrefu Jimbo la Arusha Mjini limekuwa likisumbuliwa na changamoto ya mafuriko kwenye Kata ya Sembetini, Levolosi, Osunyai, Sekei, Unga Ltd, Sakina, Baraa na Olerian yanayosababishwa na miundombinu mibovu ya barabara ya Sakina – Tengeru na Airport – Soko la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Sakina – Tengeru umehusisha upanuzi wa barabara iliyokuwepo kutoka njia mbili kwenda njia nne na katika mito yote yamejengwa madaraja makubwa yanayopokea maji kutoka mlima Meru na kupeleka katika makorongo makubwa ya asili. Hivyo, mafuriko yanayotokea katika maeneo husika hayasababishwi na miundombinu mibovu ya barabara ya Sakina – Tengeru.

Mheshimiwa Spika, tatizo la mafuriko katika maeneo yaliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge yanasababishwa na sababu zifuatazo: -

(i) Mabadiliko ya kimazingira yanayohusiana na ujenzi uliofanyika katika maeneo ya juu na hivyo kuongeza maji katika maeneo ya juu kuelekea kwenye maeneo ya chini;

(ii) Ujenzi holela katika mikondo asili ya maji na kupunguza upana wa njia ya maji; na

(iii) Utupaji taka ngumu kwenye mitaro ya maji na kusababisha kuziba kwa makalvati na kupelekea maji kupita juu ya barabara na kusambaa katika maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na tatizo la mafuriko, Serikali kupitia Tanzania Strategic Cities Project unaotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha, inafanya utafiti wa kina ili kuona ni jinsi gani mafuriko haya yanaweza kuzuiwa kwa kujenga miundombinu ya kukusanya maji yote yanayotoka Mlima Meru na kuleta madhara ya mafuriko. Mhandisi Mshauri kutoka Kampuni ya Cheil Engineering ya Korea Kusini anaendelea na utafiti huo, ahsante.
MHE. MRISHO S. GAMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanapata malipo kama Madiwani na Wabunge kutokana na majukumu mazito wanayoyafanya ikiwemo ufuatiliaji wa malipo ya Kodi ya Majengo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa kuwa ndio wasimamizi wakuu wa shughuli zote za maendeleo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji na Mitaa za Mwaka 2014 chini ya Tangazo la Serikali Na. 322, miongoni mwa sifa zinazomwezesha mkazi wa Kijiji, Mtaa au Kitongoji kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti ni pamoja na kuwa na shughuli halali inayomwingizia kipato.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa mwongozo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu malipo ya posho ya viongozi hawa kwa kutumia mapato ya ndani kadri ya uwezo wa Halmashauri. Kwa ujumla, uwezo wa Halmashauri zilizo nyingi bado ni mdogo katika kutekeleza jukumu hili. Hivyo, Serikali imeichukua changamoto hii na itaendelea kufanya tathmini. Ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutoa mwongozo wa upandishaji mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mshahara katika sekta binafsi unapanda baada ya Bodi ya Kima cha Chini cha Mishahara katika sekta binafsi ambayo inaundwa kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300 kufanya utafiti na kupanga viwango vya mishahara katika sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Bodi hiyo tayari imekamilisha kazi ya kupanga kima cha chini kipya na kumshauri Waziri mwenye dhamana na masuala ya kazi ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi. Kwa ujumla, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha suala hili na itatangaza rasmi kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi mwezi huu wa Novemba, 2022. Ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, Jiji la Arusha lina wamachinga wangapi, wapo maeneo gani na wangapi wamepatiwa vitambulisho hadi kufikia mwezi Februari, 2022?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Februari, 2022 Jiji la Arusha lilikuwa na wamachinga 5,426 ambao walikuwa wamepangwa katika maeneo mbalimbali kama ifuatavyo; soko la Samunge, Kiwanja Na. 68 Soko la Kilombero, eneo la Ulezi Mianzini, Machame Luxuary na Kilombero eneo la Daladala.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu usajili na utoaji vitambulisho vya wamachinga, ambapo kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha jumla ya wamachinga 1,187 sawa na asilimia 22 wamepatiwa Vitambulisho.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, nini hatma ya madai ya maslahi ya waliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa TanzaniteOne?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Wizara ya Madini imepokea malalamiko ya kutolipwa mishahara ya waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya TanzaniteOne Mining Limited (TML) iliyokuwa ikichimba madini katika eneo la Kitalu ‘C’ Mirerani.

Mheshimiwa Spika, Wizara ilifuatilia suala hili na kubaini kuwa wafanyakazi 540 walifungua shauri katika Tume ya Usuluhishi na Upatanishi (CMA) Arusha na shauri hilo Na. CMA/ARS/ARD/112/2018 ni la madai ya malimbikizo ya mishahara ya miezi 11 na stahiki zao zingine.

Mheshimiwa Waziri, shauri hilo lilisikilizwa na hukumu ilitolewa kuwa TML ilipe wafanyakazi hao jumla ya shilingi 2,529,331,585 kama malimbikizo ya mishahara yao ya miezi 11 na stahiki zao zingine.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hukumu kutolewa hadi sasa wafanyakazi hao hawajalipwa stahiki zao. Hata hivyo, kwa kuwa suala hili limesikilizwa na kutolewa maamuzi na Mahakama, na bado lipo kwenye taratibu za kisheria, Wizara ya Madini inasubiri taratibu za mahakama kukamilika ili kujua hatima ya suala hili, ahsante sana.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-

Je, lini Wananchi wa Kata ya Moshono katika barabara ya mzunguko ya Kona ya Kiserian watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi walioathirika na kupisha ujenzi wa barabara ya mzunguko (Arusha bypass) kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa stendi ya kisasa kwenye eneo la Bondeni City Jijini Arusha kupitia Mradi wa TACTIC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mradi wa kuboresha miundombinu katika Majiji, Manispaa na Miji – TACTIC awamu ya pili, itatekeleza ujenzi wa stendi kuu ya kisasa ya mabasi katika eneo la Bondeni City, masoko mawili pamoja na bustani moja ya mapumziko kwa lengo la kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo jirani.

Mheshimiwa Spika, kazi ya usanifu imekamilika na taratibu za ununuzi kwa ajili ya kumpata mzabuni zinatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2023. Baada ya taratibu hizo kukamilika, utekelezaji wa ujenzi kwenye maeneo yaliyoainishwa utaanza, ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza kuunganisha mita za maji za kulipia kabla ya matumizi kama za TANESCO Arusha Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Arusha (AWSA) imeshaanza kufunga dira za malipo ya kabla kwa taasisi za Serikali na baadhi ya wateja wa kawaida. Mpaka sasa jumla dira 345 zimeshafungwa na zoezi la ufungaji wa dira hizo linaendelea. Baadhi ya Taasisi za Serikali zilizofungwa dira hizo ni pamoja na Jeshi la Polisi, ofisi pamoja na nyumba za watumishi, ofisi za Serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya NIDA, Ofisi za Kata, Ofisi za Magereza na Makumbusho, baadhi ya vituo vya afya na zahanati pamoja na Shule za Msingi na Sekondari zimeshafungiwa dira hizo.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza kuunganisha mita za maji za kulipia kabla ya matumizi kama za TANESCO Arusha Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Arusha (AWSA) imeshaanza kufunga dira za malipo ya kabla kwa taasisi za Serikali na baadhi ya wateja wa kawaida. Mpaka sasa jumla dira 345 zimeshafungwa na zoezi la ufungaji wa dira hizo linaendelea. Baadhi ya Taasisi za Serikali zilizofungwa dira hizo ni pamoja na Jeshi la Polisi, ofisi pamoja na nyumba za watumishi, ofisi za Serikali, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya NIDA, Ofisi za Kata, Ofisi za Magereza na Makumbusho, baadhi ya vituo vya afya na zahanati pamoja na Shule za Msingi na Sekondari zimeshafungiwa dira hizo.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka utaratibu ili bei ya mafuta ya dizeli na petroli iwe moja kwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia EWURA inafanya tathmini ya uwezekano wa kupanga bei moja ya bidhaa za petroli nchi nzima. Utaratibu huu uliokuwa ukitumika miaka ya nyuma, ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo za kisera na kiusimamizi. Hivyo, wafanyabiashara wa mafuta waliruhusiwa kupanga bei za bidhaa za mafuta kuendana na ushindani wa soko. Tathmini hiyo itakapokamilika, Serikali itaweza kujiridhisha iwapo utaratibu huu una tija ikiwa ni pamoja na kujua namna bora ya kuusimamia ili kuhakikisha changamoto zilizojitokeza kipindi cha nyuma hazijirudii. Ahsante.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya malipo ya mkupuo (kikokotoo) ya asilimia 33 kwa wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitangaza matumizi ya Kanuni mpya ya mafao ya pensheni kuanzia tarehe 1 Julai, 2022. Kanuni hiyo iliandaliwa kwa kushirikisha wadau wote (Serikali, wafanyakazi na waajiri) kwa lengo la kufanya maboresho ya pensheni ili kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya mifuko kuwa endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao ya pensheni ikijumuisha malipo ya mkupuo kwa wafanyakazi. Sheria inaitaka Mifuko kufanya tathimini ya kupima uhimilivu kila baada ya miaka mitatu na kutoa ushauri na mapendekezo mbalimbali ikijumuisha maboresho ya mafao ya wanachama na kuifanya Mifuko kuwa endelevu. Kwa kuwa Mifuko itafanya tathmini kwa hesabu zinazoishia mwezi Juni 2023, Serikali itazingatia ushauri wa mtaalam ambaye atafanya tathimini hiyo ili kuongeza Pensheni ya Wastaafu ambayo inajumuisha malipo ya mkupuo wa asilimia 33, ahsante.