Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Geoffrey Idelphonce Mwambe (7 total)

MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina maswali mawili nyongeza. Swali la kwanza; ni lini basi Serikali itaona umuhimu katika hivyo vyuo ambavyo imepanga kujenga basi kijengwe pale Masasi kwa sababu tayari kilikuwepo na Serikali ilifanya maamuzi ya kukibadilisha chuo na kuwa shule ya sekondari ili pia ihudumie wananchi wa Masasi na wilaya za jirani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali pia itaona haja ya kufungua matawi vyuo vya elimu ya juu Wilayani Masasi ili kuweza kusaidia watu wa Masasi, lakini pia na watumishi mbalimbali kuweza kujiendeleza kielimu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi kwamba Serikali inamiliki vyuo 35 na katika vyuo hivi tuna mahitaji ya wanafunzi zaidi ya 25,000 lakini wanafunzi waliopo kwa sasa ni 22,000. Tafsiri yake hapa ni kwamba, hata hivi vyuo vilivyopo bado vina upungufu mkubwa wa kupata wanafunzi. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kufanya tathmini ya jambo hili kulingana na mahitaji, kama nilivyozungumza kwenye majibu yangu ya msingi, iwapo kama tutaona kwamba kuna uhitaji wa kujenga chuo, basi Masasi tutaipa kipaumbele katika ujenzi huo.

Mheshimiwa Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba katika Mkoa wa Mtwara, bado tuna vyuo vitatu vya ualimu, tuna Chuo pale Mtwara Mjini, tuna vyuo viwili kimoja cha ufundi na kile cha kawaida. Vilevile katika Wilaya ya Newala tuna chuo pale Kitangale ambavyo wanafunzi hawa wote wanaweza wakatumia vyuo hivi kuweza kupata elimu yao katika maeneo hayo. Kwa hiyo, kama mahitaji yatatokea basi tutaweza kwenda kujenga katika eneo hili Masasi.

Mheshimiwa Spika, katika eneo lake la pili, kuhusiana na masuala ya matawi ya Vyuo Vikuu, naomba nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, hivi sasa Serikali inakwenda kujenga katika maeneo mbalimbali matawi ya Vyuo Vikuu. Naomba tu nitoe taarifa kwenye Bunge lako Tukufu, pale Mtwara tuna matawi ya Chuo Kikuu Huri ana Chuo Kikuu cha Stella Marius, lakini vilevile tuna tawi la Chuo cha TIAA. Vyuo hivi vyote vinaweza vikatumiwa na wenzetu wa Masasi kwa ajili ya kupata mafunzo yao pale. Vilevile Chuo Kikuu chetu cha Dar es Salaam kiko mbioni kufungua tawi katika Mkoa wa Lindi ambapo ni jirani kabisa na Wilaya ya Masasi. Nakushukuru.
MHE. GEOFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa tunashida kubwa ya ajira kwa vijana, lakini pia kwa kuwa tunajua kuna vipaji vingi vya vijana kwenye nchi yetu, lakini pia kwa kuwa tunafahamu ziko nchi zimewekeza vya kutosha kwenye vijana kama vile Brazil, Congo DRC, Senegal, Nigeria, Ghana, naomba sasa niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ningependa kujua kwamba kutokana na umuhimu huu ambao nimeusema, Wizara inaweza ikatengeneza utaratibu kwa kuanza kuweka bajeti kidogo ya kuweza kusaidia Halmashauri za Miji Midogo ambayo haina uwezo wa kibajeti kuweza kuendeleza viwanja ambavyo tayari vipo kwenye maeneo yale? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunafahamu kwamba kuna juhudi kubwa zinafanywa na watu binafsi kwenye kuendeleza vijana kupitia shule mbalimbali za soka. Je, Serikali inaona ni muhimu sasa kuweza kusaidia vituo vya kulelea vijana na hasa ukuzaji wa vipaji vya soka na michezo mingine ili tuweze kupata vijana ambao wameandaliwa vizuri kwa ajili ya timu ya Taifa na kuweza kupata ajira nje ya nchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza alipenda kufahamu kama Serikali tupo tayari ku-support halmashauri ambazo bajeti zao ni chache na wasingeweza kufanya kazi hii.

Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya msingi nimesema kwamba jukumu hili ni la Serikali Kuu, lakini pia Serikali za mitaa. Naomba nipongeze Halmashauri ya Masasi wao wameshaanza kuzungusha uzio katika uwanja ule, lakini pia sisi kwa upande wa Wizara pia tumeanza kujenga baadhi ya viwanja na katika mwaka huu wa bajeti, tulitenga viwanja zaidi ya saba. Pale bajeti ambapo itaruhusu sisi tutaendelea ku-support.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili alitaka kufahamu ni kwa kiasi gani tunaweza tuka-support vituo vya kukuza vipaji (academies).

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara tunaandaa mazingira wezeshi kuhakikisha hizi academy zinafanya vizuri na mpaka sasa tuna academies binafsi zaidi ya 84. Kwa hiyo, sisi Wizara tutaendelea ku-support. (Makofi)
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, ninataka nijue ni lini basi Serikali ina uhakika wa kupata hii (No objection) kutoka kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika ili tujue kwa uhakika kabisa ni lini tutaanza utekelezaji wa mradi huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ninataka kufahamu ni lini Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Temeke itajenga stendi mpya kwa ajili ya mabasi ya kutoka Mtwara, Lindi na Ruvuma yanayoingia Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya Dual Carriage Way ya kutoka Dar es Salaam kwenda Mkuranga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, Mbunge wa Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu za manunuzi zinakwenda vizuri na ni matumaini yetu kwamba kama wenzetu watakwenda kama tulivyopanga tunategemea tutapata (No objection) kwa sababu taratibu zote karibu zimekamilika. Sasa ni lini? Kwa kweli tutanategemea wenzetu wa African Development Bank watakavyokuwa wamefanya kazi yao kwa uharaka na kutoa hiyo (No objection) na sisi tutaanza kutangaza hiyo kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kujenga stendi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama wizara kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI ambao hasa ndio wanaoshughulikia stendi hizi za mijini, tutakaa pamoja tuone uwezekano wa kujenga hiyo stendi na hasa tu nikimhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa upande huo tayari tuna utaratibu wa kuja na mpango wa kujenga dual carriage way ya kutoka Mbagala – Kongowe na ikiwezeka mpaka Vikindu. Ahsante.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyatoa ningependa kujua kwamba Serikali inafikiriaje kwa halmashauri ambazo hazina uwezo mkubwa kimapato wa kuweza kugharamia uwekaji wa taa barabarani kupitia ruzuku inayotolewa na REA kwamba halmashauri hiyo ikapata ruzuku asilimia 75 mpaka 100 ukilinganisha na asilimia 50 ya sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni kwamba, sasa hivi tunajua tunafanya juhudi kubwa ya kujenga barabara za mijini hususani pale Masasi na kwenye majimbo ya wenzangu. Kwa nini TAMISEMI sasa isiamue kufungamanisha fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara na fedha kwa ajili ya uwekaji wa taa ili Mkandarasi anayepewa kujenga zile barabara pale mjini anamalizia na kuweka taa moja kwa moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwambe, la kwanza hizi Halmashauri ambazo haazina uwezo kupata ruzuku ya REA. Hili tunalichukua kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI na tutahakikisha tunakaa taasisi yetu ya TARURA kwa kushirikiana na taasisi ya REA ambayo iko chini ya Wizara ya Nishati kuona ni namna gani tunaweza kufanya kazi ka Pamoja na kutoa hiyo ruzuku iende kwenye barabara hizi kwenye miji ambayo haina uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, kwa sasa barabara zote zinazojengwa na TARURA nchini kote hasa zile zinazopita kwenye Katikati ya miji zinawekewa taa. Pia, kama Masasi kule hawajaanza naamini wakimaliza tu katika ujenzi wa barabara hizi taa zitaanza kufungwa kama nilivyokuwa nimesema kwenye majibu yangu ya msingi.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, tuna Kijiji cha Mlundelunde, Kitongoji cha Mchaka ambacho kina shule ya sekondari ambapo bahati mbaya umeme umepita juu yake na shule ile ya sekondari kama taasisi ya Serikali, haijapata ule umeme: Je, nini maelekezo ya Serikali kwa REA Mtwara ili waweze kufanya haraka kuunganisha umeme katika hiyo shule ya sekondari?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Tumepata changamoto kubwa kwa Jimbo letu la Masasi Mjini ambapo tuna Kata saba za Sururu, Mwengemtapika, Matawale, Chanikanguo, Temeke, Marika pamoja na Mmbaka ambazo ziko vijijini, lakini wanatakiwa kulipa shilingi 320,000/= kama sehemu ya ada ya uunganishaji wa umeme: Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa, wananchi hawa wapate haki kwa maana wapo vijijini, waunganishiwe umeme kwa shilingi 27,000/= kama vijiji vingine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Geoffrey Mwambe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na shule ambayo ameitaja, shule hii ipo katika moja ya kitongoji ambapo utaenda kutekelezwa mradi wa vitongoji 15 ambavyo tayari Serikali imeshatenga fedha kwa mwaka huu wa fedha. Tunaanza kufanya ufuatiliaji ili tuweze kuona ni namna gani tunaanza kutekeleza mradi huu wa vitongoji 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili juu ya maeneo ya vijijini ambayo yanakataliwa kutozwa shilingi 27,000/=, tayari Serikali tumeshaya-identify haya maeneo na tuko katika mchakato wa mwisho ili kuweza kutolea maelekezo kwa maeneo kama haya ambayo yanaleta mkanganyiko wa bei.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mradi huu ni sehemu ya mpango ambao upo kwenye Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya nchi yetu Awamu ya Tatu ambao mwezi Julai unafikia hatua ya miaka mitatu ya utekelezaji. Ni maandalizi gani ya awali ambayo Serikali imeyafanya kuonesha kwamba ina dhamira ya dhati kujenga mradi huu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mradi huu ni sehemu ya mradi funganishi wa Mtwara Development Corridor ambayo makubaliano ya mradi huo ulifanyika Lilongwe - Malawi Novemba, 2004 na marais wanne wa hizi nchi nne.

Je, ni lini Serikali sasa kama mnufaika mkuu utarudisha utaraibu wa marais hao wanne kukutana na kuweza kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huu wa reli pamoja na miradi mingine ndani ya Mtwara Development Corridor? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mbunge wa Masasi Mjini, Mheshimiwa Idelphonce Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa mradi huu na Wabunge wote wa Mkoa wa Mtwara na kwa swali la kwanza anapenda kujua maandalizi ya awali ya mradi huu.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali tumeanza maandilizi ya awali, kwanza tumeanza vikao ndani ya Serikali pamoja na kufanya vikao na wadau mbalimbali na hivi ninavyosema tutakuwa na kikao kingine ambacho kimeitishwa na Mamlaka ya Bandari nchini kitakachofanyika tarehe 22 hadi 23 pale Mtwara na Waheshimiwa Wabunge mnakaribishwa katika mkutano huu kwa sababu ndio unaenda kuifungua Mtwara Corridor yote na wadau wengine ni pamoja na RAS kwa maana ya Mamlaka ya Mkoa wa Lindi, Mtwara yenyewe pamoja na Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi, ni kwamba mradi huu kwa kuwa kwanza kuna makampuni zaidi ya matano kutoka nchi mbalimbali kutoka nchi ya Uingereza, Canada, Marekani, Afrika Kusini, Croatia, Morocco wameonesha nia katika uwekezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR na kwa maana hiyo, changamoto kubwa ilikuwa katika kikwazo ambacho kilichokuwepo kupitia Sheria ya PPP ambayo Bunge lako tukufu wiki iliyopita imepitisha na kufanya mabadiliko madogo kwenye sheria hiyo.

Kwa hiyo, tunaamnini mapatano na mikutano itakayofuata sasa katika makampuni kutoka nchi hizi watakuja moja kwa moja kuwekeza kwa kuwa tayari tulishaanza kufanya nao mikutano hiyo, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwenye Jimbo la Ndanda tuna vituo kwenye Kata ya Ndanda, Kijiji cha Chiroro, Lukuledi, Ngalole, Chikundi pamoja na Namajani. Vituo hivi vimeshakamilika ujenzi wake zaidi ya miaka miwili sasa hivi lakini hata hivyo havijafunguliwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kwa sababu ya mapungufu madogo madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba; je, yuko tayari kutoa maelekezo kwa Halmashauri yetu ya Masasi DC ili vituo hivi vikamilishwe na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kwani zile shilingi milioni 50 zilizoletwa na Serikali hivi sasa majengo haya yameanza kuchakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuwapongeza Wananchi wa Jimbo la Ndanda kwa kujenga kutumia nguvu zao lakini Serikali iliwaunga mkono kuwapelekea shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati hizi na vituo hivi na vimekamilika vitoe huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitumie fursa hii ya Bunge lako tukufu kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwaelekeza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia maelekezo ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba vituo vikikamilika vinabaki hatua ndogo ndogo za ukamilishaji, vifaatiba kwa ajili ya kuanza kutoa huduma. Ni lazima watoe kipaumbele kuhakikisha vinakamilika mapema na vinaanza kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa Wakurugenzi wote nchi nzima, lakini mahususi nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kuhakikisha vituo hivi ambavyo vimetajwa na Mheshimiwa Mbunge wa Ndanda mapema iwezekanavyo ndani ya miezi mitatu tuhakikishe vituo hivi vimekamilishwa na vinaanza kutoa huduma kwa wananchi, ahsante.