Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Geoffrey Idelphonce Mwambe (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kunifanikisha kuwa hapa leo. Pili nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa imani yake kubwa aliyokuwa nayo kwangu kunipa utumishi wa kusimamia jukumu la Wizara yetu ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nisisahau chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa imani kubwa waliyokuwa nayo wajumbe wetu wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Masasi Mjini. Pia niwashukuru wananchi wa Masasi kwa kunipa kura nyingi na kunipa jukumu la kuwawakilisha kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuishukuru sana familia yangu akiwemo mke wangu Tumaini Jasson Kyando na watoto wangu King King, Caren, Catherine kwa imani kubwa waliyokuwa nayo na kunivumilia kwa kipindi kirefu cha utumishi wangu ambapo muda mwingi nakuwa nje ya nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza kabisa tumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Kimamlaka presidential speech is a policy speech. Rais anapata absolute powers kutoka kwenye Katiba, ana mamlaka yote. Mamlaka ya mwananchi mmoja mmoja yote yamekusanywa kupitia kura wakampa yeye. Kwa hiyo, tamko lake ni tamko la wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi watumishi ambao tunatumikia kwa nafasi zetu za kuongoza Wizara kwa niaba yenu, ni maelekezo na ni maagizo. Kwa hiyo, mwanzo kabisa napenda kusema kwamba naunga mkono hoja na sisi tumejipanga kutekeleza. Kazi yetu kubwa ni kutekeleza na tumeshaanza kuifanyia kazi hotuba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri sana napenda nikumbushe kwamba hotuba ya Mheshimiwa Rais zote mbili ikiwemo hii ya terehe 13 Novemba 2020, zinawiana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025. Yote ambayo ameyaongea ni yale ambayo yako kwenye kurasa 303 ya Ilani ya CCM ambayo wengi wetu hapa tulikuwa tunainadi na bahati nzuri pia kila mmoja humu ndani hakuna ambaye amesema kwamba hotuba ile kuna maeneo hakubaliani nayo isipokuwa msisitizo ni namna sisi kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mlituambia wiki ijayo tutakuwa na mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitatu ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Rais inajikita huko pia. Baada ya Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ambao tulikuwa tunajikita kwenye kutengeneza miundombinu ikiwa ni kama capillaries za uchumi, wa pili tukasema tujenge viwanda lakini Mpango wa Tatu tunachukua sasa mafanikio ya kipindi cha kwanza na cha pili tunaunganisha kwenye mpango huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipitia hotuba ile ukurasa wa 10 – 26 kuna maeneo mengi ambayo Mheshimiwa Rais ameyaelekeza ambayo yanagusa kwa namna moja au nyingine maeneo ya viwanda na biashara. Hivyo napenda kupitia hotuba hiyo kuangalia michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge ili tuweze kujua namna ambavyo sisi kama Wizara ya Viwanda na Bishara tumejiandaa. La kwanza, ni utekelezaji wa blue print. Kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walionesha kama vile tunahitaji tuanze kutekeleza lakini naomba niwahakikishie kwamba blue print tumeanza kuitekeleza tangu mwaka juzi na baadhi yenu mnafahamu hata ile iliyokuwa TFDA, sasa hivi inaitwa TMDA kutokana na utekelezaji wa blue print. Kwa hiyo, tutaenda kuhakikisha kwamba ile comprehensive action plan ya blue print tunaitekeleza ipasavyo na kuja na mbinu mpya zaidi ya kuweza kutekeleza vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upande wa masoko imezungumzwa sana hapa kwamba bidhaa nyingi zinakosa masoko. Naomba niwahakikishie tunaenda kuiboresha taasisi/ mamlaka yetu ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE) ambayo kimsingi imebeba jukumu la Board of Internal Trade (BIT) and Board of External Trade (BET). Bodi hizo mbili ziliunganishwa zikatengeneza TANTRADE, lengo lake kubwa au majukumu yake makubwa ni kutafuta masoko ya mazao yetu na bidhaa zetu kwa masoko ya ndani kuunganisha kutoka mkoa mmoja na mwingine, masoko ya kanda na masoko ya Kimataifa kupitia multilateral trading system ambayo sisi ni Wajumbe. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwenye hili tutaenda kupambana kuhakikisha masoko ya bidhaa zetu yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna maboresho ya taasisi zetu. Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kiko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, nimewaambia kwamba tuangalie course content. Tusingependa na kwa kipindi hiki sio vyema kutengeneza business administrators yaani tunatengeneza wasimamizi wa biashara, biashara ya nani? Mimi nimewaambia wakae, waje na mpango mpya tutengeneze course content ambazo zinamjenga asilimia 70 yule mtoto yeye ndiyo akawe mfanyabiashara halafu asilimia 30 iwe ndiyo kusimamia biashara. Unakuwa business administrators wengi wanasimamia biashara ya nani? Kwa hiyo, tunaenda kuiboresha hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama WIzara ya Viwanda na Biashara, tutakuja na Programu ya Miliki Kiwanda ambayo nitaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa sababu Mheshimiwa Rais kwenye hotuba yake ametamani nyie muwe sehemu ya mabilionea mshiriki. Tutakuja na Programu ya Miliki Kiwanda ili kokote ulikokuwa kwenye Jimbo lako, wilaya yako tutengeneze utaratibu wa kuanzisha kiwanda wewe Mbunge ukiwa ni champion kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna masuala ya sekta binafsi. Sekta binafsi yetu ni changa sana tunahitaji kuijenga kwenye maeneo mawili. La kwanza, kuwapa fursa ya kuweza kufanya biashara. Hii tumezungumza mara kwa mara na nashukuru pia Mheshimiwa Waziri Mpango mara baada ya kuapishwa tu alikutana na uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania aliwasisitizia, kufunga biashara au kiwanda cha mtu iwe ni baada ya Commissioner General kutoa kibali. Biashara zote ziko chini ya leseni za viwanda na biashara, napenda kusisitiza sana, tuilee sekta binafsi lakini pia tuwaelimishe kwa upande wa integrity, lazima na wao wawajibike upande wao kuwa na integrity kwa Serikali ili iweze kuwaamini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia siku hii ya leo. Kikubwa zaidi ningependa sana kuwashukuru viongozi wetu wa kitaifa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, lakini pia na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango na Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia na Baraza la Mawaziri lote kwa kuendeleza majukumu ambayo tumekuwa nayo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nisingependa kutoka hivi hivi bila kuzungumza tatizo ambalo limetupata kitaifa, kutoa pole kwako lakini pia na familia ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, lakini pia na Watanzania wote kwa ujumla kwa kuondokewa na kipenzi chetu, jemedari, kiongozi mwenye maono na hatimaye kumfikisha kwenye nyumba yake ya milele kule Chato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa sana kutoa shukrani zangu kwa kamati mbili za Utawala na Serikali za Mitaa, kwa maoni yao ambayo yalikuwa ni mapana, very extensive. Tunashukuru sana na yale maoni tumeyachukua yote na tuwahakikishe kwamba tunakwenda kuyafanyia kazi, kuhusiana na namna ambavyo tutakuza uwekezaji kwenye nchi yetu. Pia Kamati ya Katiba na Sheria ambayo pia imetoa maoni mengi, lakini kipekee Bunge lako Tukufu, Waheshimiwa Wabunge wameweza kutoa maoni mengi, kwa sababu tunafahamu suala la uwekezaji ni suala pana suala kubwa na ndio linajenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, kimsingi hoja kubwa ilikuwa ni kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji. Pia kuwa na mtazamo chanya kuhusu masuala ya uwekezaji kwenye nchi yetu na kwa kutambua kwamba kila taasisi isijiangalie peke yake, lazima itambue kwamba tuna sababu nyingi za kuvutia uwekezaji kwenye nchi yetu. Eneo la kwanza ni ajira kwa vijana wetu, tunafahamu kwamba Ilani ya CCM ya Uchaguzi lakini pia kwenye Mpango wetu wa Maendeleo tumepanga kutengeneza fursa za ajira zaidi ya milioni nane.

Mheshimiwa Spika, pia tunataka ukuaji wa uchumi wetu ambao ni mkusanyiko wa shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zinafanywa na sekta binafsi lakini na Serikali Kuu na Serikali za Mitaa ziweze kufikia angalau asilimia nane kwa kila mwaka. Tafsiri yake ni kwamba uzalishaji wote wa mwaka huu ukitoa uzalishaji wa mwaka jana ukigawanya kwa uzalishaji wa mwaka jana ukizidisha mara 100 basi ikupe asilimia nane ndio tafsiri yake, lakini pia tunafahamu kwamba tumeingia kwenye uchumi wa kati kabla muda wetu ambao tuliupanga mwaka 2025 na hili ni moja ya mafanikio makubwa sana ambayo sijui kwa nini hayazungumzwi kwa uzito.

Mheshimiwa Spika, tumeweza kufanikiwa kuingia kwenye uchumi wa kati mapema zaidi kwa sababu ya juhudi kubwa tulizoziweka kwenye maeneo mbalimbali ya uzalishaji ikiwemo kuvutia uwekezaji. Tafsiri yake labda tuweze kuiweka vizuri tu, kuna kitu tunaita GNI ambayo ni GDP unaiweka kwenye market prices ambayo unapata gross national income, ukigawanya kwa idadi ya watu ndio unapata per capital income ambayo sasa ile ndio imetufikisha pale kwenye 1,080 ambayo ni kiwango cha mwanzo cha kuingilia ngazi ya uchumi wa kati.

Kwa hiyo hata baadhi ya michango tulikuwa tunaisikia hapa tumeingia kwenye uchumi wa kati lakini kule vijijini hatuoni, tafsiri yake sio hiyo.

Mheshimiwa Spika, kule vijijini kimsingi tunaona kwamba badala mtu kutembea kilometa tano kufuata zahanati, basi anatembea kilometa moja au mita 500 kwa sababu zahanati imejengwa kwenye kituo chake cha makazi. Pia huduma nyinginezo za usafiri ambazo zamani ulikuwa uamke saa 10 uweze kupata gari, lakini sasa hivi gari unasimama tu popote unaweza kupata. Vile vile miundombinu yetu imeboreshwa sana. Sasa hivi kila familia ina angalau pikipiki na gari, vitu ambavyo zamani tulikuwa tunasema ni luxury sasa hivi tumevichukua kama ni necessity na ndio maana mahitaji ya maendeleo yetu yanakuwa yanaongezeka kila siku.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa kweli tumepiga hatua kubwa. Haya yote yametokana na uamuzi wa Serikali kuweza kufungua fursa za uwekezaji kwenye nchi yetu, kuruhusu private sector lakini pia kuruhusu Serikali yenyewe kuweza kuwekeza.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba nijielekeze kwenye maeneo ya uwekezaji hususan yake ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge hapa.

Mheshimiwa Spika, la kwanza naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu, kwamba mikakati na mipango ambayo iliwekwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa na msaidizi wake wakati huo, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan walifanya wote, nalichukulia ni kama vile uendeshaji wa ndege, ndege zina Pilot na co-pilot, tuna bahati kwamba sasa hivi aliyekuwa co-pilot wakati ule ambaye alishiriki kwenye program za manifesto kuangalia manifesto ya ndege, kutengeneza mission plan ya kwamba turuke twende destination gani, tupitie route ipi, hali ya hewa ikoje, walipanga wote wawili, ndio maana kuna mwendelezo na pia tumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusema kwamba kazi iendee sio ianze upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale wote wanaojaribu kuutoa ushauri wa hapa na pale kuhusiana na nini akifanye, natamani sana wampe nafasi, afanye kazi yake kwa sababu anaifahamu, alikuwepo kwenye kupanga mipango na yeye ni sehemu ya mipango hii ambayo tunaitekeleza kwa sasa. Ushauri mwingi ambao unatolewa, ningependa sana kuwashukuru lakini tumuache Mheshimiwa Rais, anafahamu wapi ataifikisha nchi yetu kwa sababu tunayo Dira ya Maendeleo ya Taifa, tunayo Ilani ya CCM, tunao Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano awamu ya tatu, ile awamu ya pili yeye mwenyewe alishikiri, lakini hii Ilani ya CCM yeye alishiriki kuipitisha kama Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, lakini pia kama msimamizi wa shughuli za Serikali pia akiwa kama ni Makamu wa Rais, kwa hiyo anafahamu wapi anataka kuipeleka nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie mageuzi makubwa ambayo yamefanywa kwenye nchi yetu kwa upande wa uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuunda Wizara ya Uwekezaji, walifanya wote hayati Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mama Samia Suluhu Hassan kama Makamu wake. Pia na kitendo cha yeye si tu kuamua kuibakiza Wizara ya Uwekezaji, lakini kuipa hata Katibu Mkuu na iwe Wizara Kamili, ni uthibitisho tosha kwamba amedhamiria kukuza mazingira ya uwekezaji nchini, lakini pia kuhakikisha kwamba tunakuza shughuli mbalimbali za uwekezaji kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, la pili, kuna mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji, Sera yetu hii ni ya siku nyingi, ni ya mwaka 1996, kwa hiyo kwa kiasi kikubwa ni kama inahitaji maboresho, inahitaji kuhuishwa ili mambo mapya na changamoto ambazo tumezipata kwenye utekelezaji wa sera ile ya zamani tuweze kuyaingiza kwenye sera mpya na ituongoze vizuri.

Mheshimiwa Spika, pia kuna sheria yenyewe ya uwekezaji, baada ya kupitisha Sera ya Uwekezaji mwaka 1996, mwaka 1997 Bunge lako Tukufu likapitisha Sheria Na. 38 ili iweze kutuongoza sasa katika utekelezaji wa ile sera kwa upande wa sheria. Hiyo tunafanya mapitio na tumefikia hatua ya juu sana.

Mheshimiwa Spika, nafikiri muda siyo mrefu Bunge lako Tukufu litapata nafasi ya kuipitia hiyo sheria ya uwekezaji na ikiwezekana tupate hiyo sheria mpya ya uwekezaji ambayo itabeba mambo mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge wamependekeza. Kwasababu wakati mwingine tulikuwa tunakwazwa na sheria yenyewe huwezi kufanya zaidi ya pale.

Mheshimiwa Spika, pia kuna eneo la maboresho kutokana na taarifa ambazo zinatolewa na International Finance Cooperation (IFC) ambayo ni sehemu ya World Bank Group hii Benki ya Dunia ambayo inatupima sisi Tanzania na nchi zingine 192 duniani namna gani mazingira yetu ni wezeshi kwa upande ufanyaji wa biashara ile easy of doing business ambako tumekuwa rent kwenye numbers ambazo siyo nzuri sana ambazo sisi tungetamani tubadilike kidogo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tangu mwaka 2010 baada ya sisi kuingizwa kwenye huo mpango Serikali imekuwa ikifanya mapitio kupitia mpango wa maboresho ili kuhakikisha kwamba maeneo ambayo yanaainishwa ambayo ni maeneo 11 kuanzia unaposajili kampuni BRELA mpaka unapofunga kampuni BRELA, na hapa katikati kuna vigezo vingi namna ya kupata umeme kupata mikopo na ulipaji wa kodi na mazingira kama hayo kwa hiyo, vigezo vyote vinaangaliwa lakini pia na blue print.

Mheshimiwa Spika, mtakumbuka mwezi Mei 2019 Baraza la Mawaziri lilipitisha blue print ni maarufu kama blue print lakini ni mpango wa maboresho ya mazingira ya ufanyaji biashara kwenye nchi yetu na hii ni mpango wetu sisi is a home grown program ni ya kwetu sisi hakuna Benki ya Dunia, hakuna IMF waliyotuletea ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo Mama Samia Suluhu Hassan kama Makamu wa Rais wa wakati huo naye alikuwa ni sehemu ya huo mpango walipitisha na kuhakikisha kwamba tunaitekeleza ipasavyo na nikuhakikishie sana na Bunge lako Tukufu kwamba tunaenda kuisimamia hilo na tuhakikishe kwamba tunaitekeleza ipasavyo na kujenga mazingira wezeshi kwa upande wa biashara.

Mheshimiwa Spika, lakini pia mabadiliko ya sera na sheria mbalimbali za kifedha na kikodi Bunge lako tukufu limekuwa likipitisha hapa finance act kuangalia maeneo yale ambayo yametajwa kodi tozo mbalimbali ambazo zinachajiwa na taasisi na halmashauri zetu za wilaya au Serikali za Mitaa ili tuhakikishe kwamba tunajenga mazingira wezeshi kwa upande wa maeneo ya biashara na uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, pia yako maboresho ya utendaji wa kituo chetu cha uwekezaji kuna mambo mengi ambayo yamefanyika ingawa majukumu yake ya kisheria yanatakiwa yatimizwe kulingana na sheria inavyotaka. Pale kwenye kituo cha uwekezaji tumetengeneza well stop facilitation center ambako watumishi wa taasisi mbalimbali sasa hivi wako taasisi 14 pale kuna watumishi kama 25 ambao wanakaa pale kuna watumishi wa TRA, kuna watumishi wa BRELA, watumishi wa Uhamiaji, kuna watumishi wa Idara ya Kazi. Lakini pia watumishi wa NEMC, watumishi wa OSHA wa NIDA wako pale wanatimiza majukumu ya taasisi zao katika kufanikisha uwekezaji lakini wakitokea ndani ya kituo cha uwekezaji na hii yote ilikuwa ni katika kujenga mazingira wezeshi na kutoa usumbufu kwa upande wa uwekezaji kuzunguka kwenye hizo na kupata huduma.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa iliyokuwepo ni kwamba kuimarisha na kuhakikisha kwamba tunakuwa na watumishi ambao wanamaamuzi pale ndani ya taasisi hilo tunaenda kulifanya na tunataka hii sheria yetu ikipita mpya tuhakikishe kwamba wanaokaa pale ni watu wenye maamuzi siyo tena watumishi ambao wanatakiwa kila mara kupiga simu kwenye taasisi zao kuandika email au kupeleka mafaili kwa hiyo itachelewesha kwenye biashara zetu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna mfumo tuliuweka wa National Investment Facilitation Committee ambao wakuu wa taasisi zote ambazo kwa namna moja au nyingine huduma zao zinagusa wawekezaji wanakutana chini ya uwenyekiti wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji na kupitia changamoto mbalimbali na naomba nikuhakikishie kupitia Forum hii changamoto 53 zilitatuliwa na mojawapo ilikuwa ni kiwango cha utozaji wa ada wa NEMC pale ambapo mtu anataka au mwekezaji anataka kupata cheti cha NEMC anatakiwa alipie zamani ilikuwa ni asilimia ya mtaji lakini baadaye kupitia kikao hiki tukaja kubaini hapana huwezi kufanya asilimia ya mtaji tafsiri yake mtu kama anawekeza bilioni 100 basi ana 0.03 ya bilioni 100 ni hela nyingi sana kwa hiyo kupitishie EIA ripoti yake apate certificate.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukakubaliana kwamba watengeneze regulation upya na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa wakati huo akaisaini wakatengeneza band ya maeneo kama 14 ambayo yanasema tu kwamba kuanzia mtaji 0 mpaka labda milioni 5 basi utalipia shilingi 50,000 tu. Kwa hiyo, katika milioni 5 mpaka labda milioni 20 utalipia labda 100,000 tu. Tulipata mafanikio sana kupitia huu mfumo na tutaendelea kuboresha ikiwemo mfumo unaotumika kwaajili ya vibali vya kazi ni mfumo ambao umetengenezwa pale TIC kwaajili ya kufanikisha hii na ni imani yetu kwamba tutaendelea kutengeneza mifumo mingi zaidi.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ilikuwa ni uanzishaji na uendelezaji wa land bank au akiba ya ardhi ya uwekezaji. Uwekezaji wote unafanywa kwenye ardhi changamoto kubwa imekuwa ni kupata ardhi kwa wakati. Lakini pia na mchakato wa uhulishaji wa ardhi.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna maeneo mawili moja watu binafsi na Serikali kuhakikisha kwamba ikiwemo Tawala za Mikoa na Halmashauri zetu kupima maeneo ya ardhi na kuhakikisha kwamba ile ardhi tunaileta kwenye kituo cha uwekezaji ili tuweze kuinadi kwa wawekezaji uweze kupata urahisi wa kuipata urahisi wa kuipata ile lakini gharama zote za ulipaji na nini atalipa huyo mwekezaji kikubwa Zaidi ni kwamba asipate muda mrefu wa kuipata hiyo ardhi.

Mheshimiwa Spika, lakini kingine tuna National Land Allocation Committee ambayo inaratibiwa na Wizara ya Ardhi ambayo imekuwa ikigawa hii ardhi kulingana na mahitaji kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuhusu kuondoa urasimu na kufanikisha uwekezaji. Hili Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amezungumza kwa kauli nzito angetamani na angependa tuondoe urasimu kwenye maeneo yetu tutambue wajibu wetu kama watendaji kama watumishi na sisi kama Wizara ya Uwekezaji lakini pia Ofisi ya Waziri Mkuu, tutaenda kufanya, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiyo msimamizi wa shughuli za Serikali tutaendelea kusisitiza hili tuwajibike kwa kujua kwamba tutaisaidia nchi yetu kwenye kufikia kwenye malengo yale yaliyoainishwa kwenye dira ya maendeleo ya miaka 25 lakini pia na mipango yetu ya maendeleo ya miaka mitano mitano ambayo sasa hivi tuko kwenye mwaka wa tatu.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kutambua kwamba tuna ajira kwa vijana lazima tutengeneze ajira kwa vijana lakini pia kuna kutengeneza soko la haraka la wakulima wetu. Kwahiyo tukifanikisha uwekezaji maana yake tunasababisha wakulima hawa wapate soko la haraka kwasababu kutakuwa na wanunuzi hapa ndani. Lakini pia tunahitaji fedha za kigeni ili uchumi wetu uwe imara.

Mheshimiwa Spika, reserve ya fedha za kigeni ni muhimu sana ili iweze kushikilia thamani ya shilingi la sivyo tutakuwa tukihitaji kulipia huko nje kama ni madeni ama au ni uagizaji wa vitu ni lazima tutoe fedha nyingi za Kitanzania tupate dola moja na kufanya sasa ile exchange rate kwenda juu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuwa na pesa ambayo iko tayari kuweza kulipia hizo external obligations kwa hiyo kuna haja sana ya kuvutia uwekezaji tupate fedha za kigeni lakini pia tuweze ku-export hivi vitu vyetu lakini pia kuna masoko ya kikanda na kimataifa ambayo tumesainiwa iko EAC, SADC and International, AGOA ambayo tumesaini kwa hiyo, naomba sana niwahakikishie Bunge lako tukufu kwamba tunaenda kuweka juhudi kubwa sisi kama…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, napenda sana kukushukuru napenda kuunga hoja mkono ahsante sana (Makofi).
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
WAZIRI NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia ningependa kukukumbusha kwamba siku mbili/tatu zilizopita kulikuwa na mechi kule Egypt na hujatuambia matokeo yake. Labda utatupa taarifa ukipata nafasi. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwanza ningependa sana kushukuru michango ya Waheshimiwa Wabunge, kwa kweli ni michango ambayo imesaidia sana kutengeneza Mpango wetu wa Miaka Mitatu ambao ni Mpango wa Tatu wa Maendeleo; na kwa kweli michango yenu tumeichukua na tutahakikisha kwamba tunaifanyia kazi kwenye maeneo yetu ya kisekta, lakini pia kuboresha huu mpango.

Mheshimiwa Spika, kipekee naomba uniruhusu niwataje baadhi ya Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia kwenye eneo la uwekezaji. Kulikuwa na Mheshimiwa Zuberi Kuchauka (Mbunge wa Liwale), Mheshimiwa Tarimba Abbas (Mbunge wa Kinondoni); Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa (Mbunge wa Biharamulo) pamoja na Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani (Mbunge wa Viti Maalum Ruvuma). Pia kuna Mheshimiwa Hassan Mtenga (Mbunge wa Mtwara Mjini); Mheshimiwa Simon Songe na Mheshimiwa Yahya Mhata, huyu wa Nanyumbu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kushukuru kwa michango yao lakini naomba nijielekeze kwenye kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge lakini pia na wananchi kwa ujumla, kwamba Serikali wakati wote imekuwa ikifanyakazi ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara kwenye nchi yetu. Kama ambavyo mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge mwaka 1999 tulikubaliana kwamba tuunde Dira ya Maendeleo ya miaka 25 (2000 – 2025), tunaiita Tanzania Development Division 2025 ambayo ilianza mwaka 2000, mwaka uliofuatia. Tukawa na mipango midogo midogo ya kimkakati sasa kutekeleza ile Dira ya Maendeleo; na ni kwenye ile dira tulijipangia kwamba mpaka kufika mwaka 2025 tuingie kwenye uchumi wa kati, lakini pia tukiongozwa na sekta binafsi, lakini pia na tukiongeza uzalishaji wetu wa mazao kwa ajili ya kupeleka fedha nje, tuwe na fedha za kigeni nyingi. Pia shilingi yetu iweze kuwa imara, tuwe na mfumuko (inflation) ya single digit, ikiwezekana twende kwenye chini ya wenzetu kwenye eneo la Afrika Mashariki na SADC na tukajipangia mipango mingi ikiwemo kukuza ajira kwa vijana; sasa tunakuwa na mkakati midogo midogo ya kuweza kutekeleza hivyo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna reforms ambayo ndiyo nilitaka iwe hoja yangu kubwa. Kwamba tunafanya maboresho kila wakati kama Serikali kwa kupokea mawazo kutoka kwa wadau, lakini pia watekelezaji wa programu mbalimbali za kisekta. Kama mtakumbuka tulikuwa na Public Sector Reform Program ambayo iliunda Idara yetu ya Utumishi kipindi kile, lakini pia kuna Public Finance Reform Program, pia tulikuwa na Local Government Reform Program ambayo tumetengeneza hizi halmashauri kupitia hizo programu. Pia hata Legal Sector Reform Program tuliifanya wakati huo ili kuboresha sheria zetu ziendane na mahitaji yetu sisi ya kuwa na uchumi wa kisasa kuendana na malengo ya kwenye Dira ya Maendeleo.

Mheshimiwa Spika, sasa kwenye kuyafanya hayo tukatengeneza mikakati. Tulikuwa na mkakati mdogo wa miaka mitatu wa kupunguza umaskini lakini tukasema huu mkakati baada ya kupata maoni ya wadau tuupanue zaidi kwa kukuza uchumi na kuupunguza umaskini. Tulikuwa na MKUKUTA, MKUKUTA I na MKUKUTA II wa miaka mitano, mitano kama mtakumbuka. Kwenye MKUKUTA II tukaona sasa tuje na mpango tofauti kidogo, ndipo tukawa na huu Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano ambao Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete alizindua mwaka 2011/2012 mpaka 2015/2016 mpango wa kwanza ukilenga kuibua fursa za kiuwekezaji lakini pia kujenga miundombinu ili tuhakikishe kwamba tunajenga msingi mpana wa kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kutekeleza huo mpango tukaja na mpango wa pili sasa wa miaka mitano mingine ambayo ni 2016/2017, 2020/2021 ambao ndiyo umekamilika, huu tukasema tujikite kwenye ujenzi wa viwanda, na ndiyo maana Serikali inaripoti mara kwa mara kwamba tumejenga viwanda zaidi ya 8,477 ambako vikubwa ambavyo tunaviona ni 210 kwenye nchi yetu, ambavyo vimetoa ajira za kutosha kwa vijana wetu, lakini kutengeneza mafungamano kati ya sekta ya kilimo na masoko kwa kuwa na viwanda katikati ili tuweze kuchakata bidhaa za wakulima, lakini pia kutengeneza immediate market (soko la karibu) la mkulima na kumuhakikishia mkulima soko la mazao yake.

Mheshimiwa Spika, lakini pia sisi kama nchi tukasema baada ya kupata mafanikio kwenye Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Mipango ya Maendeleo kupitia Long Term Perspective Plan sasa twende kwenye Mpango wa Tatu ambao unaishia 2025/2026 na huu mpango umejikita kwenye ku-consolidate na kuchukua yote yale ya nyuma, lakini pia na kuchukua yale ambayo hatukuweza kuyatekeleza au kuyaboresha ili tuweze kwenda mbele. Sasa kwa upande wa uwekezaji kuna mengi ambayo tumeyaona kuna mafanikio makubwa sana ambayo sana tumeyapata kipindi hiki cha miaka iliyopita kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano wa Kwanza na wa Pili.

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye Mpango wa Tatu tumelenga kuongeza; moja, utekelezaji wa mipango ya kuboresha mahusiano yetu sisi na sekta binafsi na tutaongea hizi PPDs (Public Private Sector Dialogue) kwa kuwasikiliza zaidi wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kuweza kuboresha complaints handling; zile kero za wafanyabiashara zile tuwe na masikio mapana zaidi ili tuweze kuzisikia na kuhakikisha kwamba tunatekeleza yale ambayo wafanyabiashara wangetamani, kwa sababu wao ndio wazalishaji na wasambazaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kipindi hiki tunasema blue print ambayo imezungumzwa hapa tunaenda kuitekeleza kwa uhakika labda niseme hivyo. Tangu mwezi Mei, 2018 baada ya Baraza la Mawaziri kuridhia na pia ndani ya Serikali kuweza kuhamasisha wananchi uwepo wa blue print na wafanyabiashara tumeweza kutekeleza mambo mengi ikiwemo kupunguza tozo 273 kwenye eneo letu la kujenga mazingira ya biashara na uchumi. Lakini pia kama mnakumbuka tulikuwa na TFDA ambayo ilikuwa inafanyakazi ambazo zinagongana kidogo na TBS. Kwa hiyo, Serikali baada ya kupata ushauri kutoka kwa wadau ikiwemo Waheshimiwa Wabunge hapa Serikali ikaamua kuchukua eneo la chakula na vipodozi ikapeleka TBS na kuiacha TFDA kushughulika na madawa na vifaa tiba ndiyo maana inaitwa TMDA kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunatekeleza mipango yetu ambayo tumejiwekea kupitia blue print, lakini pia na maboresho mbalimbali ambayo tulianza tangu mwaka 2010 kupitia ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunaita maboresho, ambayo imetokana na kufuatilia na kutafiti juu ya ripoti ya IFC ya Benki ya Dunia ya Easy of Doing Business, kuna indicators kumi na moja ambazo zinatuonesha hatufanyi vizuri kulinganisha na nchi zingine duniani. Kila nchi inapigana na kukimbia kwahiyo tutajitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba tunatekeleza hiyo yale maboresho na kuwa na mazingira wezeshi zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nipende kusema tui le miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo imelengwa kufanywa na Serikali itafanywa ikiwemo Mradi wa Bagamoyo ambao Mheshimiwa Engineer Ezra Chiwelesa ameulizia. Serikali iko wazi kwenye hilo kwamba tulichokataa ni yale masharti tu ambayo hayakuwa mazuri sana kwa nchi yetu, lakini kwa kweli wakija tena wale wawekezaji au wakitokea wengine tukakaa chini tukaongea tukaja na masharti ambayo yana interest kwa nchi, Serikali haitapinga kwa sababu ule mradi ni wa kwetu Serikali, wala si wa wawekezaji ni wa kwetu sisi. Na kwa kweli hayo maeneo mbalimbali tumeshalipia fidia sehemu ya viwanda, sehemu ya logistics lakini pia na sehemu ya bandari tumelipia fidia kabisa yako chini ya mikono ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningependa kuwahakikishia Wabunge na kuwahakikishia wafanyabiashara jumuiya ya wawekezaji kwenye nchi yetu, kwamba Serikali itaongeza usikivu na kuhakikisha kwamba tunafanya kazi pamoja kuweza kuboresha mazingira ya biashara.

Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru sana na naunga mkono hoja.