Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Tumaini Bryceson Magessa (1 total)

MHE. BRYCESON T. MAGESSA Aliuliza:-

STAMICO inamiliki maeneo yenye dhahabu lakini haiyatumii huku wachimbaji wadogo wakiwa hawana maeneo ya kuchimba.

Je, kwa nini Serikali isiwapatie wachimbaji wadogo maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bryceson Tumaini Magessa, Mbunge wa Jimbo la Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa majukumu ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ni kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini. Katika kufanya hivyo Shirika limekuwa likifanya kazi kwa karibu sana na wachimbaji hao katika kuhakikisha kwamba wanaongeza uzalishaji katika maeneo wanayochimba. Kupitia mkakati huo, Shirika pia limekuwa likitoa maeneo yake kuwapatia wachimbaji wadogo kwa lengo la kuwaendeleza.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2018, Shirika lilitoa maeneo ya uchimbaji kwa vikundi 15 vya wachimbaji wadogo vilivyoundwa katika eneo la Lwamgasa (Geita) kwa usimamizi wa viongozi wa Kijiji na Afisa Ushirika yenye ukubwa wa kilomita za mraba 0.08. Vilevile, mwaka 2019, Shirika liligawa pia eneo la leseni ya Buhemba kwa vikundi vya wachimbaji wadogo waliopo Ilasaniro Mkoani Mara lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1.2 na jumla ya leseni ndogo za uchimbaji 15 ziligawiwa. Aidha, kwa kushirikiana na mbia Shirika lilitoa leseni tatu katika eneo lake la mradi wa Buckreef (Geita) kwa wachimbaji wadogo wa maeneo hayo yenye jumla ya kilomita za mraba 7.2.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo kwa sasa hakuna maeneo ambayo yanamilikiwa na STAMICO bila kuendelezwa. Shirika linaendelea kuendeleza maeneo yake kwa kufanya utafiti ili kujua kiwango cha mbale kilichopo kabla ya kuanza uchimbaji. Pia Shirika limeanza kuendeleza leseni yake ya dhahabu ya Buhemba kwa kushirikiana na mbia na uzalishaji unatarajiwa kuanza Septemba mwaka huu 2021. Ahsante.