Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Tumaini Bryceson Magessa (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kunipa nafasi ya kuweza kuongea mbele ya Bunge hili. Nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Busanda kupitia Chama Cha Mapinduzi walionipatia kura za kutosha na leo nawawakilisha kama Mbunge ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia ya Bunge la Kumi na Moja, lakini katikati kulikuwa na achievement speech, ilikuwa katikati tarehe 16 Juni, kulikuwa na taarifa tena ndani ya Bunge hili ambayo Rais alionesha mambo yaliyofanyika. Mwezi Novemba tumekuwa na hotuba nyingine ambayo tunaizungumzia leo Bunge la Kumi na Mbili, Bunge letu la kwanza la Kumi na Moja lilionesha dira na falsafa ya Mheshimiwa Rais anakotaka kuipeleka nchi hii, lakini tarehe 16 Juni, alionesha yale yaliyofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote ni mashahidi nikiwemo mimi kwenye taarifa hizi na kwa macho yetu, hakuna sekta aliyoizungumzia ambayo haikufanyiwa maboresho. Kama ni barabara, kiwango cha cha lami kimeongezeka, lakini kama ni barabara za TARURA zimeongeza, japokuwa zinaharibika kila mvua inaponyesha. Vituo vya afya vimeongezeka vimejengwa vipya 1,769, katika hivyo zikiwepo hospitali za mkoa, ikiwemo vituo vya afya. Hii inaonesha wazi kwamba dira na falsafa iliyokuwa imetolewa imetekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba hii ya Bunge la Kumi na Mbili ambapo ndipo kuna kazi kubwa tunatakiwa kufanya sisi, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, yapo maono makubwa ambayo nimeyaona kwenye hotuba hiyo na wataalam kazi kubwa tuliyonayo sasa sisi kama Wabunge hasa nikiwemo mimi ni kwenda kuhamasisha yale yaliyoandikwa huko ndani yaweze kutokea. Kwa sababu hotuba ni kitu kimoja lakini utekelezaji ni kitu cha pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya afya page namba 65 wameonyesha wazi kwamba sasa tunakwenda kwenye bima kwa wote. Mtego upo kwa Waziri wa Afya, tunapokwenda kwenye bima kwa wote kipi kilianza kati ya kuku na yai, ni kuku au yai? Inaanza kwanza huduma iwe bora ili watu wahamasike kuingia kwenye Bima ya Afya au bima ya afya kwanza ndiyo huduma iwe bora? Kwa hiyo, kuna kazi fulani wataalam wanatakiwa kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema kwenye ukurasa namba 44, STAMICO itaboreshwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wa madini wanasaidiwa. Kazi kubwa tuliyonayo ambayo naiona Rais ametuwekea mezani hapa, je, huduma hizi tunazotaka kuzifanya wataalam tulionao na sisi wenyewe tunazo service level agreement zetu? Kwa sababu inaonekana mwananchi anaweza kuwa huduma katika level yoyote, service level agreement ni ipi, kiwango gani cha huduma tunatakiwa tumpe, hapo ndiyo kuna changamoto. Tunaye Afisa Kilimo je, anakwenda kwenye shamba darasa na haya mashamba tunayoyazungumza hapa ndani ambayo yanaonekana yatakuwa ni mikataba kati ya wanunuaji na wakulima wenyewe yapo, anaweza kuwa haendi kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatakiwa service level agreement na watu wetu nini wa delivery. Kwa sababu unamuuliza mtu anakwambia nimeingia kwenye OPRAS, nimeingia sijui wapi, anaonekana anafanya vizuri lakini ukimuuliza kuna shamba darasa mahali hakuna. Kwa hiyo, mimi najielekeza kama Mbunge kuingia kwenye maeneo haya kuona namna gani tutafanya ili viongozi sisi pamoja na wataalamu wetu waweze kutoa kile ambacho Mheshimiwa Rais anatarajia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi yaliyozungumzwa hapa ambayo nategemea yakifanyika tutakapokwenda kufunga Bunge hili tutakuta maendeleo yetu yamekwenda kasi. Ninao mfano mmoja mdogo, nilipokuwa natoka kwenye kampeni nafika airport Dar es Salaam nilimwambia mtu mmoja usinipitishe Ubungo kwa sababu tukipita huko wanajenga ile interchange itatuletea shida. Akaniambia wewe inaonekana ni wazamani sana kumbe barabara ilishakamilika, tukapita pale juu na bahati mbaya alikuwa ni mwanangu ananiambia baba wewe umepitwa na wakati, tukapita juu tukashuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, yapo mambo makubwa yamekwishafanyika, tutowe nafasi sasa na akili zetu kuhakikisha kwamba yale yaliyosemwa yanaweza kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisitumie muda mrefu sana, naomba niunge mkono hoja, ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kunipatia nafasi ya kuongea katika Bunge hili kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano na wa Mwaka Mmoja. Ni dhahiri kwamba, ukurasa wa tano umeonesha wazi kwamba, nguzo za Mpango huu wa Maendeleo zimejikita kwenye sehemu tatu; ya kwanza ni utawala bora. Utawala bora sina mashaka kwa namna ambavyo unaendeshwa sasa kwa sababu ya haki na uwajibikaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nguzo ya pili ni ukuaji wa uchumi; ukuaji wa uchumi tumeuona kwamba, uchumi unakua, lakini kuna mambo kadhaa ambayo tunatakiwa tuyapitie. Wabunge wengi wameeleza juu ya kilimo, ni kweli kabisa kwamba, Watanzania zaidi ya asilimia 75 wameajiriwa kwenye kilimo na bajeti tunayoipeleka kwenye kilimo ni ndogo sana. Kama hiyo graph ya ukuaji wa uchumi ni linear maana yake tunapoondoa tu kuwafanya wale wasihusike katika uchangiaji wa pato la Taifa, lazima uchumi wetu utaonekana haukui haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo iko hoja tunataka kuongeza bajeti, lakini sisi tunaotoka vijijini kule watu wamezalisha mchele haujauzwa hadi leo upo, mahindi yapo yamezalishwa hayajauzwa. Maana yake kuna hoja ya masoko hapa haijakaa vizuri ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ndugu zangu wanaitwa TMX, wameshughulika na suala hili, lakini kila mmoja ana mpunga ndani, ana mahindi ndani na biashara haifanyiki. Kwa hiyo, tunapokwenda kwenye hoja hii, lazima tutafiti tujue kwamba, tuna masoko ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna udongo wa kila aina mahali tunapoishi. Hii Wizara ya Kilimo inatakiwa ipewe fedha kwa ajili ya utafiti. Kuna mahali fulani niliwahi kuishi wakaniambia hapa hapahitaji mbolea udongo wake una madini mengi sana, maana yake hawana elimu ya kutosha kujua nini wanatakiwa kufanya kwenye kuzalisha. Kwa hiyo, niseme tu wazi tunahitaji kuchangia kwa kiwango kikubwa kwenye Wizara ya Kilimo, ili tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye ukuaji wa uchumi, ukiangalia vipaumbele kwenye ukurasa wa 101 inasema wazi kwamba, tutachochea uchumi shirikishi na shindani, lakini ukirudi kwenye ukurasa namba 64 kwenye Mpango huu, utagundua kwamba, kuna mahali fulani sekta binafsi haikuhusika vizuri kuna vitu ambavyo vilikwenda vya kichefuchefu. Ukiangalia Clause 3(iii), utagundua kuna habari ya ulipaji wa kodi imeandikwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninakotoka Katoro nina wafanyabiashara zaidi ya 5,000 pale Mjini Katoro, wana ugomvi na TRA kuanzia asubuhi hadi jioni. Nina mashaka sasa kama tunataka kukuza uwekezaji na uchumi, hiyo ni katika kipaumbele cha tatu, inaonekana kuna tatizo kati ya TRA na wafanyabiashara, tutakuzaje sasa uwekezaji na uchumi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima sasa hivi tuanze kutengeneza kama ni ushirikishi na shindani tuhakikishe kwamba, TRA wanafanya urafiki na hawa wafanyabiashara wasiwakadirie vitu ambavyo havipo. TRA wamekuwa wanarudi nyuma miaka mitano halafu wanamwambia mtu sasa unatakiwa kulipa milioni 300; milioni 300 na yeye mtaji wake ni milioni 150, kimsingi huyu amefilisika. Kwa hiyo, niombe sana hoja yetu ya msingi ni kuhakikisha kwamba, sasa uchumi wetu unaweza ukakua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona madini yatakua kutoka asilimia 5.2 kwenda asilimia 10. Tumeona kilimo kinatakiwa kichangie kutoka asilimia 27, bahati mbaya inaonekana mpaka baada ya miaka mitano hakitakuwa kimechangia sana ukiangalia kwenye kumbukumbu ukurasa 104, lakini niseme tu wazi ni lazima tuhakikishe kwamba sasa hivi masoko yapo, lakini tukiendelea kuzalisha na masoko hayapo tutakuwa tumefanya mchezo wa kuigiza na uchumi wetu hautaweza kupanda kwa sababu, wananchi hawatazalisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)