Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Simon Songe Lusengekile (2 total)

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali na niipongeze Serikali kwa namna inavyochukua hatua juu ya mradi ule. Pamoja na hayo mradi ule katika Kijiji cha Mwagulanja umeacha sehemu kubwa sana ya wananchi wa Isuka takriban kilometa nne kufikia point ambapo maji yamewekwa.

SPIKA: Mheshimiwa swali lako ni Nyashimo…

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, ni Kata ya Nyashimo sasa hicho Kijiji nilichokisema. Naomba tu kuuliza Serikali nini mpango sasa wa kufanya extension kutoka kwenye ule mradi kwenda kwenye Kijiji cha Mwagulanje kule Isuka ili wananchi wa kule nao waweze kupata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Simon Lusengekile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, huu mradi unaendelea kutekelezwa. Extension ni kazi ambayo hata yule Meneja aliyeko pale anaweza kufanya, kwa hiyo nimwaminishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kufika mwezi Machi, tutaanza kuzitekeleza extension, lakini kwa kutumia wataalam wetu ambao wako kule.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kuniona na mimi niulize swali la nyongeza kwa Wizara hii yetu ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Mahakama ya Wilaya ya Uyui ni sawasawa na tatizo lililoko pale kwetu Wilaya ya Busega na kesi za Mahakama ya Wilaya zimekuwa zikienda kusikilizwa Wilaya jirani ya Bariadi.

Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kutumia jengo lililopo la Mahakama ya Mwanzo ili litumike kusikiliza kesi za Mahakama ya Wilaya, lakini hivyo hivyo ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa…

NAIBU SPIKA: Swali ni moja Mheshimiwa, swali la nyongeza ni moja.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba Waziri wa Katiba na Sheria nipende kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutumia jengo la Mahakama ya Mwanzo inategemea sana sifa ya hilo jengo kwa sababu vingine ni vyumba vidogo ambavyo haviwezi kuhimili huduma ambazo zinatakiwa kutolewa kwenye ngazi ya Wilaya, lakini tutalichukua na kulifanyia utafiti ili kuona kama hiyo Mahakama ya Mwanzo ina sifa zinazostahili kuwa kwenye kiwango cha matumizi ya Wilaya na tukijiridhisha huduma itaanzishwa mara moja kwenye eneo husika, ahsante.