Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Simon Songe Lusengekile (2 total)

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE Aliuliza:-

Je, ni lini Mradi wa Maji wa Nyashimo, Kata ya Nyashimo ambao ulitegemewa kukamilika mwezi Oktoba, 2020 utakamilika ili wananchi waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Nyashimo ulianza kutekelezwa mwezi Julai, 2019 na ulitegemewa kukamilika tarehe Oktoba, 2020 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.58. Wakati utekelezaji wa mradi, Mkandarasi alipata changamoto zilizosababisha kuomba kuongezewa muda na hivyo mradi huu unatekelezwa kufikia mwaka huu 4 Aprili, 2021 ambapo ombi lake lillikubaliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa utekelezaji wa mradi huo upo katika hatua ya majaribio ya kusukuma maji kupeleka kwenye tanki baada ya kufanikiwa kufunga umeme tarehe 9 Januari, 2021. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2021 na kuhudumia wakazi wapatao 12,000. (Makofi)
MHE. ESTHER L. MIDIMU K.n.y. MHE. SIMON S. LUSENGEKILE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa katika Hospitali ya Wilaya ya Busega ili huduma bora za afya ziendelee kutolewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega ni miongoni mwa hospitali 67 za Halmashauri zilizoanza kujengwa mwaka 2018/2019 kwa kupewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ambayo ni jengo la utawala, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la maabara, jengo la mionzi, jengo la wazazi, jengo la kufulia na jengo la kuhifadhia dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali 67 za Halmashauri ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega ambayo imetengewa shilingi milioni 500.

Vilevile katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 33.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba katika hospitali 67 za Halmashauri ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Busega ambayo imetengewa shilingi milioni 500.