Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Simon Songe Lusengekile (8 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Pia nimshukuru Mungu sana kwa nafasi hii aliyotupatia ya kuwa mahali hapa leo. Kipekee nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi pamoja na wananchi wa Jimbo letu la Busega kwa kuniamini na kunichagua kuwa mwakilishi wao mahali hapa.

Mheshimiwa Spika, 2015 nilibahatika kufuatilia hotuba ya Mheshimiwa Rais wakati akizindua Bunge la Kumi na Moja, tarehe 20 Novemba, 2015. Aliyoyasema nilianza kufikiri kwamba yanaenda kuwezekana vipi, lakini nirudishe shukrani nyingi sana kwa mapinduzi makubwa ya maendeleo aliyotupatia Mheshimiwa Rais kwa kipindi hiki cha miaka mitano iliyopita. Ni Imani yangu kubwa kwamba katika hii miaka mitano kupitia hotuba yake ya tarehe 13 Novemba, 2020 ambayo ilitoa mwelekeo wa nchi yetu yapo maeneo machache naomba nami nichangie.

Mheshimiwa Spika, kuna suala toka asubuhi linaendelea kujadiliwa; habari ya TARURA. TARURA ni pasua kichwa, TARURA ni shida mpaka sasa barabara nyingi vijijini zimekatika. Pia kutokuwepo kwa barabara hizi za vijijini kumesababisha sehemu ya uchumi wa wananchi wetu kushuka kwa sababu hawawezi sasa kupeleka hata mazao yao kwenda kutafuta sehemu ambako kuna masoko, madalali wamekuwa wengi wa bei ya chini kwa sababu ya shida ya barabara ambazo ziko kwenye vijiji ambavyo sisi tunatoka.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano ukiangalia kuna wakati hata hili zao la pamba kwetu kule Usukumani ambapo wananchi wengi wanalima, inafikia sehemu barabara ni ya shida watu wa pikipiki wanakwenda kununua pamba kwa bei ya chini sana, muda mwingine hata nusu ya bei ambayo ni halisia kwa sababu ya kutokuwepo barabara sehemu husika. Tunapotaka sasa kuendeleza uchumi wa wananchi wetu mmoja mmoja lazima tuwatengenezee mazingira mazuri ili wananchi hawa sasa waweze kusafirisha mazao yao ya biashara kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kupata bei iliyo salama.

Mheshimiwa Spika, nataka pia nichangie kidogo eneo la kilimo. Mimi ni muumini sana wa uwekezaji katika sekta ambazo ni productive kwa nchi yetu. Tunapokuwa tunazungumza habari ya ajira milioni nane, ni lazima tufikiri kuelekeza baadhi ya ajira katika sehemu ambazo ni productive kwa nchi yetu ikiwemo na kilimo.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye halmashauri zetu, halmashauri zilizo nyingi zina shida ya watumishi, hasa Maafisa Ugani. Wananchi wetu wengi hawapati fursa ya kufundishwa na hawa Maafisa Ugani kwa sababu hawapo kila sehemu ni shida. Hii ni sekta ambayo tungeweza kuielekezea watumishi wengi wangeweza kuwasaidia wananchi wetu ambao wanalima kwa kutumia akili zao zilezile ambazo Mheshimiwa Mbunge wa Mbogwe alikuwa anajaribu kugusia.

Kwa hiyo, mimi niseme na niombe, tunapokuwa tunaangalia suala la ajira, lazima pia tuangalie eneo hili ili tuweze kuajiri watu wengi waende wakawasaidie wananchi wetu katika suala zima la kilimo na kilimo kiwe chenye tija na tutakapopata malighafi yetu basi itatumika kwa ajili ya viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni viwanda. Eneo hili tukitaka tufanye vizuri ni lazima tuhakikishe kwamba tunapata viwanda vyetu vya ndani ambavyo vinatengeneza bidhaa mpaka mwisho. Kama ni pamba basi tutengeneze bidhaa inayotokana na pamba mpaka mwisho tupate nguo ili tuweze ku-export nguo kwenda nje ya nchi, zao ambalo tayari limekamilika kwa kutumia bidhaa zetu za ndani.

Mheshimiwa Spika, pia nataka kuongelea habari ya uvuvi, Mbunge wa Ukerewe amezungumza kidogo. Eneo hili bado lina shida, tozo ni nyingi sana kwa wananchi wetu ambao wanashughulika katika suala zima la uvuvi. Tozo ni nyingi, kuna leseni ya mtumbwi, TASAC Sh.70,000 wananchi wetu wanalipa lakini pia kuna leseni za halmashauri, kuna leseni ya mtumbwi na kuna shilingi 20,000 leseni ya mvuvi mmoja mmoja. Haya maeneo wananchi wetu wanayalalamikia sana kwa sababu tozo zimekuwa nyingi na wanashindwa kuzimudu kutokana na hali ya uchumi ambao wanao. Kwa hiyo, niombe Wizara husika waje na mpango kuona namna ya kupunguza baadhi ya tozo kwa hawa watu wetu ambao ni wavuvi ili waweze kunufaika na kazi ya uvuvi ambayo wanafanya.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie sekta ya afya. Eneo hili asubuhi limechangiwa katika hoja mbalimbali kupitia maswali. Huduma ya bila malipo kwa akina mama wajawazito, watoto na hata wazee; ni kweli kuna baadhi ya hospitali zinatoa lakini kuna shida kubwa sana ya upatikanaji wa dawa katika sehemu ambazo wananchi hawa wanatibiwa. Ama dawa MSD hazipatikani lakini hata kama zikipatikana basi mpango mzima wa kando unafanyika na kunakuwa na shortage kubwa sana ya dawa.

Mheshimiwa Spika, tumeona hata Mheshimiwa Waziri wa Afya amejaribu kwenda na hoja ya kutaka kuangalia equation tu iliyopo kati ya uwepo wa panadol na mwananchi kukosa dawa na akasema hii siyo simultaneous. Mimi nimpongeze kwa namna ya pekee sana kwa jinsi ambavyo ameamua kuja kwa kasi na kuhakikisha kwamba sehemu zetu dawa zinaendelea kuwepo na wananchi wetu wanapata dawa.

Mheshimiwa Spika, niombe sasa, MSD bado kuna shida. Tunaweza kwenda na order kubwa ya dawa na fedha ambazo tayari ziko MSD lakini MSD inakosa dawa. Niombe sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya kuhakikisha kwamba tunaimarisha MSD ili iweze kuwa na sehemu kubwa ya kupata dawa ili wananchi wetu sasa waweze kupata dawa katika sehemu ambazo wanakuwepo.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nilitaka kuchangia ni maliasili na utalii. Kuna shida kubwa sana ya tembo kusumbua na kuharibu mazao ya wananchi wetu. Nizungumzie kwa mfano kule kwangu Jimboni Busega kuna Kata za Lamadi, Mkula kwa maana ya Kijereshi, kuna shida kubwa ya tembo. Katika mwaka uliopita 2020, zaidi ya wananchi wanne wameuawa na tembo kwa sababu ya kukaa katika kata hizo ambazo nimeweza kuzitaja.

Mheshimiwa Spika, kuna haja kubwa sana ya kuimarisha ulinzi wa wanyamapori kupitia maaskari wetu. Ninajua Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofika pale kwenye jimbo langu aliahidi kutupatia askari 26 ili waongeze kuimarisha ulinzi wa wanyamapori na hii itatusaidia sana wananchi wetu kufanya kazi zao wakiwa na amani. Sasa kwa sababu mazao yao yanaharibiwa tunawapa tena wakati mgumu wa kupata mazao ili waweze kunufaika na mazao yao.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuwa hapa. Lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii nami kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa nchi yetu. Nimpongeze pia Mheshimiwa Vuma kwa kuitambua na kukubali mafanikio ya Timu ya Simba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite katika mambo machache sana kuchangia mpango huu ili kuendelea kuimarisha uchumi wetu. Lakini ijulikane ya kwamba ni lazima sisi kama Wabunge tuendelee kuisimamia Serikali ili tufikie ule mpango ambao unasemwa sasa wa per capita income dola 1,400 katika hii miaka mitano ijayo. Kwasababu sasa ni 1,080 na cut off ni 1,036. Kwa hiyo, bado tuko katika eneo ambalo si salama kwa sababu tofauti yake ni dola 44. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano Nchi ya Algeria mwaka 2019 per capita income ilikuwa 4,060 lakini 2020 ilishuka ikawa 3,970. Kwa hiyo, kushuka pia inawezekana. Kwa hiyo, sisi kama Wabunge lazima tuisimamie Serikali ili uchumi wetu uendelee kupanda kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameeleza katika mambo matano ambayo ameyazungumza yatakayokwenda ku-reflect uchumi wetu. Na ninaomba uchumi huu sasa uende uka-reflect kwa wananchi hawa waliopo huko kwenye majimbo yetu na wananchi kwa ujumla wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa Simiyu ukitafuta identity yetu ni zao la pamba. Lakini wananchi wetu wameshapoteza hope na zao la pamba. Kwa nini; kwasababu ya bei ya zao la pamba. Leo ninataka kuzungumza kidogo kuiomba Serikali kutafuta namna ya kuwezesha Mkoa wa Simiyu kuupelekea kiwanda, hasa cha kuzalisha vifaa tiba vitokanavyo na zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukipata kiwanda hiki maana yake zao la pamba sasa bei yake itaenda kuimarika. Na zao la pamba likiimarika maana yake sasa tutarudisha morali ya wananchi wetu kulipenda na kulima tena zao la pamba ambalo litaongeza uchumi wa wananchi wetu walioko huko kwenye Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kiwanda hiki kitasaidia nchi yetu kwa namna ya pekee sana kwasababu kitazalisha zaidi ya ajira ambazo ni rasmi 600 na ajira ambazo si za moja kwa moja zaidi ya 1,000. Wananchi watapata ajira, watalipa kodi, watapata kipato, na hii sasa itakwenda kuimarisha uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe Wizara ya Uwekezaji iendelee kuhakikisha kwamba inawekeza kiwanda hiki katika Mkoa wa Simiyu ili zao la pamba, kama nilivyosema pale awali, liweze kuimarika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitengeneza vifaa tiba vitokanavyo na pamba maana yake tunakwenda sasa kuimarisha kutokuagiza vifaa hivi nje zaidi ya asilimia 38.3. Asubuhi tumesikia hapa, tunaagiza zaidi ya asilimia 80. Sasa tukiwekeza kwenye kiwanda hiki tunakwenda kupunguza uagizaji kwa asilimia zaidi ya 38.3 ambapo tunatumia zaidi ya bilioni 147 kila mwaka kuagiza vifaa tiba nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba Waziri wa Fedha, Mawaziri wanaohusika, mtatusaidia kuhakikisha kwamba tunapata kiwanda kule Mkoa wetu wa Simiyu ili tuweze kuzalisha vifaa tiba vikiwemo cotton gauze, cotton swab na nguo za madaktari na manesi pamoja na mashuka ambayo yanaweza kutumika katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe Wizara ipunguze tozo mbalimbali kwa ajili ya wawekezaji. Lakini pia mamlaka husika ziwe na lugha moja, hasa mamlaka zinazotoa vibali kwa hawa wanaokwenda kuwekeza kwenye miji yetu. Nilitaka nizungumzie sana hapo kwenye eneo la kilimo ili wananchi wetu sasa wakanufaike. (Makofi)

Kwenye eneo la kilimo bado hatujawekeza mahususi katika kilimo cha umwagiliaji. Bado hatujatumia Ziwa letu Victoria, hasa kwenye Mwambao wa Ziwa Victoria, bado hatujalitumia vizuri katika suala zima la kilimo cha umwagiliaji. Ukianzia kule Rorya, ukija Musoma, ukija Bunda, ukija pale Busega, ukienda Magu, Mwanza, Sengerema, Buschosa na huko mpaka Bukoba, bado hatujatumia ziwa letu katika kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, niombe Wizara ya Maji ijikite kuhakikisha kwamba tunaimarisha miundombinu ili tuwe na kilimo cha umwagiliaji katika sehemu zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapongeza mradi ulioko mkubwa wa kuleta maji hapa; mzuri sana. Lakini pia niseme sisi ambao tunazungukwa na Ziwa Victoria bado tuna shida kubwa ya maji. Mfano kwenye Wilaya ya Busega wanaotumia maji safi na salama ni asilimia 42.9; bado tatizo ni kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunapokuwa tunaangalia suala hili la maji pia tuone kabisa kwamba linaenda ku-reflect kilimo cha umwagiliaji kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo nataka kuchangia hapa ni eneo la asilimia10 ambazo zimepangwa kisera kwenye halmashauri zetu, ambapo asilimia nne ni kwaajili ya vijana, asilimia nne kwaajili ya akina mama na asilimia mbili kwaajili ya walemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ipo kisheria na imepangwa lakini cha kusikitisha ni kwamba haifuatwi na hakuna anayefuatilia. Unakuta Halmashauri imepata mapato ya ndani safi lakini asilimia ambazo zinaenda kwenye group hili hazifiki hata 10, na hamna anayehoji wala anayesimamia. Wakurugenzi hawaojiwi, business as usual.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili lazima tulisimamie. Kama ni asilimia 10 itengwe kweli, kama makusanyo ya ndani ni bilioni moja asilimia 10 ni milioni 100, no discussion kwenye hili, ipelekwe milioni 100 sehemu husika. Lakini sasa hivi inaweza ikawa milioni 100 zikaenda milioni tano, milioni saba, hamna anayehoji, hamna anayechukua hatua, ni lazima eneo hili twende tukachukue hatua ili sasa vijana wetu tuwaimarishe na waweze kupata fedha hizi ili sasa waweze kuzitumia katika kuinua kipato chao pamoja na hawa akina mama na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kidogo kwenye eneo la maliasili na utalii. Nimesikia kengele ya kwanza. Ukitoka Lamadi kuelekea Bunda pale katikati ya Lamadi na Bunda kuna wanyama wa Mbuga ya Serengeti. Ningeishauri Serikali, ili kuinua pia uchumi wa maeneo yale tufungue namna ya wanyama wetu waweze kwenda hadi ziwani, ukienda pale Nyatwali wanyama waende mpaka ziwani. Nasema hivi kwasababu itafungua uwekezaji katika Miji yetu ya Lamadi na Bunda na wananchi wa pale watazidi kunafaika na hali halisi ya uwekezaji ambao utapatikana maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Wizara ya Maliasili iliangalie hili, ni eneo mojawapo ambalo tunaweza kuwekeza na ni eneo mojawapo ambalo linaweza kuipatia fedha Serikali, na hasa hasa katika hizi sehemu ambazo nimezitaja ikiwemo na mji wa Lamadi ambao sasa ni mji mkubwa, pamoja na mji mwingine wa Bunda. Eneo hili lazima tulitazame ili liweze kuingiza kipato katika eneo letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo habari ya TARURA, TARURA lazima tuitafutie fedha; kama TANROADS wanapata asilimia 70 na TARURA asilimia 30 kuna haja ya kuzungumza hapa tena. Kuna haja ya kuendelea kuingalia TARURA kwa jicho la pili, kuna haja ya kuingozea fedha ili maeneo yetu sasa yatengenezwe. Kule vijijini na kwenye majimbo tatizo la TARURA ni kubwa, tatizo la TARURA linalalamikiwa kila mahali. Barabara hazipitikim ukienda pale jimboni kwangu barabara ya kutoka Mwamanyiri kwenda Badugu haipiki, barabara nyingi hazipitiki. Sasa hata kama wazalishaji wa pamba watazalisha hatimaye tutazungumza tena habari ya barabara. Kwamba sasa gari zinaendaje kuchukua pamba huko ambako pamba imezalishwa kuja hapa mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokuwa tunazungumzia kuimarisha uchumi wa watu na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja lazima pia tuziangalie bajeti ya TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Wizara ya TAMISEMI, lazima tuje tuzungumze, na hapa lazima tuje tuone hali halisi ya namna ya kuiwezesha TARURA ili iweze kufanya kazi kubwa kwa ajili ya wananchi wetu. Wapo wengine ambao wamekuwa wakisema irudi TANROAD, Wizara ya Ujenzi lakini hapa issue sio kurudi TANROAD issue ni kuiongezea fedha ili iweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na kazi iendelee. (Makofi).
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia taarifa za Kamati zetu tatu, PAC, LAAC pamoja na PIC. Kwanza nianze kwa kuzipongeza sana Kamati hizi tatu kwa kazi kubwa ambazo wamefanya kuhakikisha kwamba wanapata ripoti iliyo salama na wametuletea hapa leo.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya ya kutafuta fedha, ingawa yapo mambo ambayo yameelezwa kwenye taarifa za Kamati ambayo si mazuri kwa nchi juu ya ubadhirifu wa fedha za Serikali.

Mheshimiwa Spika, katika ripoti hii nitajikita maeneo matatu. Jambo la kwanza ni eneo la Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Pia nitachangia uendeshwaji wa Kiwanja cha Ndege Kilimanjaro (KIA) na la tatu kama muda utakuwa bado unaruhusu nitazungumza kidogo Wakala wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (DART).

Mheshimiwa Spika, CAG amefanya ukaguzi wa ufanisi katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Kuna mambo yamebainika ambayo yanahitaji kupelekewa miongozo ya namna ya uendeshaji wa mifumo ya upatikanaji wa wanafunzi ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa.

Mheshimiwa Spika, jana tumezungumza sana hapa juu ya hoja ambayo ililetwa na Mheshimiwa Ezra juu ya wanafunzi ambao hawajapata mikopo. Katika ukaguzi huu wa ufanisi uliolenga kuangalia ufanisi wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wetu. Vilevile ukaguzi huu ulilenga kuangalia ufanisi wa namna zinavyoshughulikiwa rufaa pale ambapo wanafunzi wanapokuwa wamekata rufaa juu ya upatikanaji wa mikopo yao.

Mheshimiwa Spika, yapo mambo machache ambayo yamebainika. Kwenye taarifa ile alifanya ukaguzi wa miaka mitano, lakini kuna mwaka 2018/2019 mwaka ule ulikuwa na shida kubwa. Ilibainika kwamba wanafunzi 6,182 walipewa mikopo zaidi ya kiwango walichotakiwa kupewa chenye thamani ya 5,670,000,000, kiwango hiki kama wangepewa wanafunzi wengine ambao hawakupata mikopo tungepata wanafunzi wengine 2,835. Tungegawa katika halmashauri zetu 184, kila halmashauri wanafunzi 15 wangenufaika na fedha hizi ambazo walipewa wanafunzi zaidi ya kile walichokuwa wanahitaji.

Mheshimiwa Spika, nikisema hivi naamanisha nini hapa? Namaanisha kwamba mwanafunzi amekubaliwa kupewa kiasi fulani cha mkopo, lakini katika reality wakati anapokuja kupewa mkopo ule anapewa zaidi ya kile kiwango alichokubaliwa, inapelekea wanafunzi wengine kukosa mikopo na huu ulikuwa ni mwaka mmoja wa 2018/2019. Ukiangalia katika miaka yote mitano aliyofanya ukaguzi wa ufanisi CAG 13,000,000,000 zilizidishwa kwa wanafunzi ambao walikuwa wanapewa zaidi ya mikopo husika.

Mheshimiwa Spika, wanafunzi 2,852 walipewa mikopo chini ya kile kiwango walichokuwa wamekubaliwa pale awali. Hii inaamanisha nini? Maana yake mwanafunzi amekubaliwa atapewa asilimia kadhaa, lakini mwisho wa siku anakuja kupewa chini ya kile kiwango ambacho alitakiwa kupewa. Tunamfanya mwanafunzi asimalize masomo yake au tunamfanya mwanafunzi kuhangaika na masomo yake. Nini kilifanyika hapa? Zaidi ya 1,147,000,000 wanafunzi hawakupewa stahiki waliokuwa wanatakiwa kupewa.

Mheshimiwa Spika, wanafunzi 756 walipewa mikopo bila kuwa na sifa za kupewa mikopo, yaani hawana sifa ya kupewa mikopo lakini wakapewa, thamani yake 2,255,000,000. Hapa napo tungepata wanafunzi wengi ambao wangeweza kunufaika na mikopo hii hata pale Mbeya Jiji nao wangepata kupitia fedha ambazo kuna wanafunzi walipewa ambao walikuwa hawahitajiki kupewa mkopo.

Mheshimiwa Spika, nini sasa hapa tafsiri yake? Tafsiri yake katika Bodi yetu ya Mikopo bado kuna shida ya mfumo unaotumika katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu. Kama mwanafunzi alitakiwa kupewa 1,000,000 anapewa 1,200,000 tafsiri yake ufanisi wa ule mfumo siyo salama. Hapa umefanyika ukaguzi wa ufanisi. Sasa ukifanyika ukaguzi wa hesabu itakuwa tatizo zaidi.

Mheshimiwa Spika, nashauri sasa kama inawezekana tufanye ukaguzi wa kina juu ya mfumo unaotumika wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Ukisoma ripoti ya CAG inakupa indication kwamba mfumo siyo salama kwa kutoa mikopo kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile katika ukaguzi huu uangalie hizi 5,670,000,000 za 2018/2019 walipopewa wale wanafunzi zaidi hao wanafunzi walikuwepo kule site au kuna watu walikuwa wanawapa halafu baadaye wanakwenda kuzichukua? Hizo ndio indication za hii. Je, hao wanafunzi waliopewa mkopo wakati hawana sifa hao waliowapa bado wako ofisini? Kwa hiyo ukifanyika ukaguzi wa kina utayabaini haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende eneo la pili, eneo la uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro unaoendeshwa na Kampuni ya KADCO, hapa bado kuna shida. Kampuni ya KADCO iliingia mkataba na Serikali mwaka 1998 ili kuendesha Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro kwa miaka 25. Wakasainishana mkataba, ule mkataba Serikali ikawa na hisa asilimia 24 na kampuni ikawa na hisa asilimia 76. Katika kuendesha ule uwanja inaonekana ufanisi haukuwa mzuri. Serikali 2009 kupitia Baraza la Mawaziri wakakubaliana kununua hisa zote za KADCO kwa asilimia 100. Mwaka 2010 Serikali ilinunua hisa zote za KADCO kwa asilimia 100. TAA ililipa fedha milioni 5.3 fedha za Kimarekani sawa na milioni karibu 12.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2010 baada ya Serikali kununua zile hisa nini kiliendelea? Uendeshwaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro umeendelea kuendeshwa kama private entity. Wameendelea kuwa na mkataba wa concession agreement. Sasa unajiuliza maswali ya kutosha. Swali la kwanza, kama Serikali imenunua hisa zote asilimia 10,0 maana yake Serikali 100% ndio mmiliki wa kiwanja. Kwa tafsiri ya kawaida uendeshwaji wa kiwanja ulitakiwa kuwa chini ya Serikali kupitia TAA. Sasa hii concession agreement iliyopo wanaoendelea kutumia mpaka leo mpaka kesho na jana ni kati ya mkataba wa Serikali na watumishi wa KADCO walioko Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro au ni kati ya KADCO kama private entity na Serikali? Kama ni hili la pili nini maana ya kununua hisa kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Baraza la Mawaziri lilishauri kiwanja kile kiendeshwe na TAA kwa nini hakikuendeshwa mpaka leo? Kwanza cha ajabu zaidi hata fedha wanazokusanya KADCO mpaka leo tunaweza kusema wanazitumia fedha mbichi, kwa nini? Kwa sababu hazipiti Mfuko Mkuu wa Serikali, yaani wao wanakusanya kesho wanapanga matumizi, wanatumia. Wana kipengele kidogo tu wanalipa dividend Serikalini kwa TR hapo tu. Mwaka 2021wame-declare kulipa 350,000,000.

Mheshimiwa Spika, sasa nashauri kwamba, kwa kuwa Serikali ilinunua hisa zote asilimia 100, sasa kiwanja hiki shughuli zote za uendeshaji zirudi TAA. Kwa nini nasema hivyo? tulipohoji kwa Afisa Masuhuli kwa nini wameamua kuendeleza hizi alitujibu jibu simple sana anasema kiwanja hiki kipo kimikakati ya kibiashara. Sasa mimi tu wa la saba wa Busega kule inaniingia kweli kichwani kwamba Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaam hakiko kibiashara eti cha Kilimanjaro kiwe kibiashara zaidi? Kama ingekuwa ni kibiashara basi Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaam ndicho kiko kibiashara zaidi kuliko Kiwanja cha Kilimanjaro. Kwa hiyo, nashauri tufanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili tufanye special audit ili kuangalia mapato yote yaliyopatikana katika miaka 10 hii yote ambapo KADCO walikuwa wanaendesha kiwanja kile kama Serikali, ili tubaini kama fedha hizi zilitumiwa vizuri na sheria za fedha zilifuatwa. Tukifanya yale yote yatatusaidia kujua ni kwa kiwango gani tumepata hasara kule Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho nataka nichangie ni Wakala wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (DART). Tumeona Taarifa ya Kamati imesema hawa DART walilipa 1,700,000,000 kama fidia kwa wananchi kuachia maeneo, lakini CAG anasema fedha hizi zilikuwa nyongeza ya malipo nje ya valuation report iliyokuwepo, yaani Valuation inasema lipa 5,000,000,000 wao wakalipa zaidi 1,700,000,000. Sio hivyo tu, wakalipa na posho za usumbufu 435,000,000. CAG alipoomba kibali, walipata wapi kibali cha kuongeza kulipa fidia hawana. Hivi kweli wanapata wapi ujasiri wa kulipa 1,500,000,000 nje ya valuation report? Wanajibu kirahisi tu waliambiwa na Serikali. CAG anauliza leteni hicho kibali mlichopewa na Serikali, hawana. Hivi tumefika kuendesha taasisi yetu kwa style hiyo?

Mheshimiwa Spika, hapa kuna madudu ya kutosha juu ya malipo ya 1,500,000,000. Vilevile hapa tufanye special audit kuwabaini wale wote waliolipwa 1,500,000,000 kama ilikuwa ni halali. Pia wachukuliwe hatua watumishi ambao wameisababishia hasara Serikali kwa kulipa watu bila kufuata valuation report.

Mheshimiwa Spika, fedha hizi ni fedha za Watanzania na kibaya zaidi miongozo inasema valuation ikifanyika leo baada ya miezi sita, mnaongeza interest kwa wale mliowakadiria. Baada ya miaka miwili, miongozo inasema kurudia valuation. Sasa wale muda umepita miaka 10, hawajafanya tena valuation, wanaibuka tu kulipa zaidi 1,570,000,000. Hili haliwezekani tufanye special audit DART ili tupate taarifa rasmi, fedha hizi wahusika waliolipwa na tuone tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo moja la kumalizia. Ukienda pale Soko la Kariakoo, nafikiri liliungua mwezi Julai mwaka jana, pale napo kuna shida. Tunawaza kwamba, baada ya kufunga mwaka wa fedha 2021 kwa maana Juni, baada ya siku 10 tu soko likaungua, documents zote zikaungua, hamna cha risiti ya mapato, hamna cha risiti ya matumizi. CAG amewapa unqualified report, lakini ni kwa nini? Hapana siyo unqualified report amewapa disclaimer report ameshindwa kutoa maoni kwa sababu hamna document yoyote inayomfanya ku-verify mapato ya 3, 500,000,000 na matumizi ya 3,500,000,000.

Mheshimiwa Spika, sasa hii kwa akili tu ya kawaida inanitafakarisha na kunifanya nione inawezekana Soko la Kariakoo liliungua baada ya documents hizi kutoonekana ofisini. Ni akili tu ya kawaida inanituma hivyo. Kwa nini baada tu ya kufunga mwaka wa fedha Juni, siku 10 tu, halafu mwisho wa siku CAG ameenda pale hamna document yoyote ameshindwa ku-verify matumizi ya 3, 500,000,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa leo nimekuja na special audit tu mwanzo mwisho. Hapa napo ifanyike special audit ya 3,500,000,000 tujue tatizo kubwa lilikuwa ni nini. Sasa sijui watapata wapi document, lakini najua kwa sababu itakuwa ni special na kwa sababu special unaweza ukawahoji watu, CAG atajua namna ya kufanya, lakini mwisho wa siku tupate mbichi na nzuri kwa hapa kwenye Soko la Kariakoo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja za Kamati. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia Wizara ya Maji. Kipekee sana nimpongeze sana rafiki yangu Mheshimiwa Aweso kwa kazi kubwa anayofanya pamoja na Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Wanafanya kazi kubwa, tunaona kazi zao wanazofanya, kweli zimekuwa ni kazi za msingi. Niwaambie tu kwamba wananchi hasa wananchi wa Busega wana imani kubwa nao kwa sababu wameona mageuzi makubwa ambayo wameyafanya kwenye Wizara ya Maji kwa huo muda mfupi ambao wamekuwa kwenye madaraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mageuze hayo ni Pamoja na namna ambayo wamefanya kuhakikisha kwamba wanapunguza gharama za ujenzi wa miundombinu ya maji, kwa sababu tumeona kuna sehemu zingine ambazo wameenda, gharama zimeshuka, unakuta BOQ ilikuwa bilioni mbili lakini kwa sababu wamenda pale mmefanya revision ya budget zimeshuka mpaka kufikia hata bilioni 1.6. Haya ni mageuzi makubwa sana ya kimkakati ambayo wameamua kuyafanya kwenye Wizara yenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee pia nimshukuru sana Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa alipokuja pale kwangu Mkura aliahidi kutupatia mradi wa maji na sasa mradi tayari umeshaanza kazi, tayari wakandarasi wako pale wanafanya kazi. Kwa kweli, tunawapongeza sana na muda ujao naamini kwamba mradi huu utaanza kutoa maji. Nimwombe tu rafiki yangu Waziri, bado kuna shida ya fedha pale. Naomba apeleke fedha ili mradi ule ukamilike kwa wakati na naamini kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri ni msikivu na kwa sababu ni kijana na kwa sababu Wasukuma ni wakarimu aende pale akaangalie namna mradi unavyotekelezwa ili umalizike kwa haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumze suala moja ambalo limekuwa likinipa shida kidogo. Kuna baadhi ya miradi ambayo inaenda kutelekezwa kwenye kata, lakini unakuta kata moja ina vijiji vine, lakini mradi unakuwa wa vijiji vitatu, kijiji kimoja kinabaki. Hili limekuwa ni tatizo na niishauri Wizara, kama wameamua kupeleka mradi kwenye kata, basi ni nzuri kata nzima kumaliza vijiji vyake vyote ili kisibaki kijiji na ikaonekana kama wametengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mfano, kwenye Kata ya Kiloleli yenye vijiji vinne, Kijiji kimoja kimeachwa, Kijiji cha Ilumya, lakini kwenye Kata ya Mwamanyili, Kijiji kimoja cha Milambe ambako Mbunge anatoka kimeachwa. Kwenye Kata ya Mkura, Vijiji viwili kwa maana ya Mwang’ale na Chabutwa vimeachwa. Kwa hiyo, nafikiri kwamba tunapokuwa tunafanya designing ya mradi kwenye kata husika basi ni vizuri kata nzima iweze kuchukuliwa na vijiji vyote viweze kupata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimefurahishwa sana na namna ambavyo wameanza kuleta mkakati wa mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Viktoria kwenda Itilima ambao kwa awamu ya kwanza utaanza na Busega, utaenda Bariadi lakini pia utaenda Itilima. Mradi huu ni mradi mkubwa na ndiyo mradi pekee ambao uta-solve tatizo la maji kwa Wilaya ya Busega, Wilaya ya Bariadi na Wilaya ya Itilima.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwamba, moja ya mradi ambao unatakiwa macho ya Waziri yaende hapo ni huu mradi mkubwa sana, kwa sababu hii miradi mikubwa unapokuwa umemalizika ni mradi ambao utahudumia wananchi wengi. Pale kwangu Jimbo la Busega zaidi ya vijiji 42 vinaenda kupitiwa. Mradi huu kwa Mkoa wa Simiyu utapita kwenye vijiji 256.

Mheshimiwa Naibu Spika,naomba na nimeona Waziri tayari ameweka kwenye Mpango bilioni 19 kwa ajili ya kuanza kati ya bilioni 400. Nimwombe kwamba awekeze sehemu hii ili wananchi wengi, zaidi ya 200,000 wa Wilaya ya Busega waweze kupata maji kupitia mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyokwambia sasa Wilaya ya Busega wananchi wanaopata maji safi na salama ni asilimia 52 wengine bado hawapati maji safi na salama na kijiji cha mwisho ni kijiji chenye kilometa 42, leo tunazungumza kuleta maji Dodoma zaidi ya kilometa 800 tunaomba na sisi utukumbuke kwenye kilometa 42 nao waweze kupata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja. Mheshimiwa Aweso karibu Usukumani, karibu Busega. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kunipa nafasi hii nami nichangie Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi, lakini kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanafanya pamoja na Watendaji Wakuu wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, leo nataka kuchangia tu mambo mawili katika Wizara hii ya Uvuvi. Hapa nyuma kidogo tumekuwa na wimbi kubwa la upungufu au uhaba wa samaki viwandani, leo nataka niishauri Wizara jambo mojawapo ambalo linalosababisha kuwa na uhaba wa samaki katika viwanda vyetu.

Mheshimiwa Spika, ijulikane ya kwamba tuna samaki aina ya sangara hasa kwenye Ziwa letu la Victoria na samaki huyu kwa kilo moja anauzwa shilingi 9,000 mpaka shilingi 10,000 pale Mwaloni. Sasa chukulia samaki wa kilo tano kwa shilingi 9,000 atauzwa shilingi 45,000; lakini ijulikane ya kwamba bondo ndani ya ile samaki ndio lenye samani kubwa kuliko mnofu. Sasa wanapokuwa wanauza pamoja na bondo lake kwa shilingi 9,000 na akipeleka kiwandani atauza kilo moja kwa shilingi 12,000 ina maana kwa samaki mwenye kilo tano atamuuza shilingi 60,000; lakini bondo linauzwa zaidi ya shilingi 60,000 samaki mwenye kilo tano.

Mheshimiwa Spika, sasa mvuvi amekuja na option ambayo ni ya kawaida tu kwamba badala ya kumpeleka yule samaki kiwandani bora mnofu wake awauzie wananchi halafu yeye anufaike na lile bondo. Anajikuta kwa wananchi anaweza kumuuza yule samaki wa kilo tano mpaka shilingi 40,000 mpaka shilingi 50,000 na bondo pia akauza kwa shilingi 50,000.

Mheshimiwa Spika, hapo atajikuta ameingiza shilingi laki moja kwa samaki mwenye kilo tano, lakini atakapompeleka kiwandani atamuuza kwa bondo lake kwa shilingi 60,000 hata ningekuwa mimi nisingeweza kupeleka samaki yule kiwanda.

Sasa mimi niishauri Wizara, waruhusiwe wavuvi au wafanyabishara ambao wanapeleka samaki kiwandani basi kuwepo na thamani ya mnofu na thamani ya bondo liuzwe peke yake, hii itasababisha kunufaisha huyu mvuvi kwa sababu thamani ya samaki itaongezeka, na kama hazitafanya hivi maana yake wataendelea hao wavuvi kutaka samaki vipande vidogo vidogo, wanawauzia wananchi na viwanda nyetu vitaendele kuwa na uhaba kama ambavyo imeonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia ijulikane ya kwamba matumizi ya ndani yameongezeka ya watumia samaki kama kitoweo hata marafiki zangu hapa Wagogo wanataka samaki kutoka Ziwa Victoria kule Usukumani, sasa ni lazima tu viwanda vikose samaki. Kwa hiyo mimi niishauri Wizara kwamba pia lazima tujikite sana kwenye mabwawa ili tuendelee kupata samaki wengi na hawa samaki waweze kutumika katika matumizi yale ya kawaida ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kupunguza ukiritimba hawa wawekezaji wanapokuja kwa ajili ya vizimba, ukija na kizimba utapewa masharti makubwa, tafute eneo kijijini, nenda katafute kibali, lete mtu wa TAFIRI aje apime, huu mlolongo unasababisha wawekezaji wanaondoka; nilitamani sana Wizara iliangalie hili ili mwisho wa siku tuwe na malighafi ya kutosha kwenye viwanda vyetu.

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine ambalo nilitaka kushauri ni tozo kwa wavuvi; kuna tozo nyingi hapa kwa wavuvi kuna tozo inayotozwa na TASAC ambao wanakuja kukagua ubora wa mtumbwi wanatoza shilingi 70,000.

Mheshimiwa Waziri umefika pale kwangu ulikuja wananchi walikulalamikia na ulisema utalishulikia hili lakini bado halijashughulikiwa bado wanatoza shilingi 70,000 kukagua ubora wa mtumbwi. Sasa hapa wananchi wangu wameniuliza swali ndogo sana kama leo mtumbwi ni mpya unakuja kukaguliwa nalipa shilingi 70,000 wakati ni mpya wala haujatumika, sasa wanakagua ubora upi wakati bado ni mpya.

Mheshimiwa Spika, hili swali ni very technque kidogo, mimi niishauri Wizara kwamba wananchi wetu hawajakataa kulipa, lakini wanaona shilingi 70,000 ni kiwango kikubwa sana ukilinganisha na kazi ambayo inakuja kufanyika. Kwa hiyo niiombe Wizara iweze kuliangalia hili.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna tozo kama leseni ya mtumbwi inayotozwa na halmashauri shilingi 30,000 lakini pia kuna leseni kwa mvuvi mmojammoja shilingi 20,000 hapa pia na penyewe nilitamani sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika naunga mkono hoja, lakini tuangalie bei ya samaki ukilinganisha na bondo. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nami nikupongeze kwa kuwa Mwenyekiti. Nakutakia mema sana katika kazi hiyo. Pia nichukue fursa hii adimu sana kumpongeza Waziri, mtani wangu kwa kazi kubwa sana anayoifanya kwa jamii yetu hii ya Tanzania. Kipekee nampongeza Naibu Waziri kwa kazi
kubwa pia anayofanya na kweli ameonesha hekima kubwa sana hata leo asubuhi, ameonesha upendo wa dhati sana kwenye Wizara yake na hiyo ndiyo tumeona faida kubwa sana ya kuzaliwa usukumani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie mambo machache sana kwenye Wizara hii leo. Naishauri sasa Wizara, leo asubuhi hapa Mheshimiwa Mrisho Gambo amesema asilimia 80 ya mapato ya Wizara ya Utalii yanapatikana kule Kanda ya Kaskazini. Hata hivyo, tunaamini kabisa kwamba Kanda ya Ziwa pia tunaweza kuwa na mapato makubwa ya utalii mkitufanyia mambo ya msingi sana ikiwemo na kufungua geti la Ndabaka lililoko pale Lamadi na pia mtufungulie geti la pale Kijereshi. Mageti haya mawili yatakuwa mageti ya msingi sana kwenye pato la Taifa; vile vile yatakuza uchumi wa Kanda yetu ya Ziwa, yatakuza uchumi wa pale Jimbo langu la Busega, hasa pale Lamadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hoteli nzuri sana Speke Bay, tuna hoteli nzuri pale Serenity na pia tuna hoteli nzuri pale Ndabaka, zina uwezo kabisa wa kutunza watalii. Naomba mtufungulie yale mageti ili yaweze kupokea watalii mbalimbali. Watalii siyo lazima waende KIA, wanaweza kushukia pale Mwanza Airport na baadaye wakaenda Lamadi kwa ajili ya kufanya tour pale Serengeti.

Kwa hiyo, nawaomba sana, mkitufungulia haya mageti mawili yatafanya kazi kubwa sana ya kukaribisha wale watalii na hasa mkiyatangaza. Myatangaze ili watalii wetu sasa waweze kupitia pale kwenye geti la Ndabaga lililopo pale Lamadi na geti la Kijereshi lililoko kule Kata ya Mkura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nichangie ni uvamizi wa tembo kwenye makazi ya watu. Pale kwangu kuna Kijiji kinaitwa Kijereshi, kuna Kijiji kinaitwa Lukungu, kuna Kijiji kinaitwa Mwakiroba vijiji hivi vitatu vinaathirika sehemu kubwa sana na uvamizi wa tembo. Naomba sasa mchukulie hatua za dharula ili wananchi wetu sasa waweze kutokutishwa na hawa tembo. Mwaka 2020 tulikuwa na vifo zaidi ya vinne vilivyotokana na uvamizi wa Tembo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, wewe ni msikivu, naomba sana kwa mara nyingine tuweze kuangalia namna ya kuleta askari wa kutosha tuweze kutengeneza Stesheni pale Kijereshi ili maaskari waweze kukaa pale. Ikibidi linapotokea tatizo, basi wapatikane kwa urahisi kwa sababu sasa hivi wanakaa Lamadi na Kijereshi ni mbali kidogo, tembo wanapoingia kule Kijereshi, wao mpaka waje wafike ni zaidi ya nusu saa muda mwingine, mpaka saa nzima au saa 1.30 ndiyo wanafika. Tembo tayari watakuwa wameharibu mazao, tayari watakuwa wamewadhuru wananchi.

Kwa hiyo, naomba sana, mtengeneze Stesheni pale Kijereshi kwa sababu ndiyo sehemu kubwa ya hifadhi. Pia muwape gari pale. Kuna shida ya gari kwa ajili ya usafiri wa kukabili hawa tembo. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie hili ili tuweze kupata gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nililotaka kuzungumzia ni tatizo la TFS. Mheshimiwa Waziri, TFS ni pasua kichwa kwa baadhi ya watumishi; kuna baadhi ya watumishi sio waadilifu. Ukienda pale Magu, kuna TFS ambao wanalinda Hifadhi ya pori la Sayaka. Pale ni pasua kichwa. Wanakamata wafugaji, ni sawa inawezekana wanasimamia sheria, lakini faini ni kubwa sana. Ni shilingi milioni sita, shilingi milioni nne au shilingi milioni nane. Ni tatizo kubwa. Naomba sana tuliangalie hili, mfugaji akiambiwa kulipa shilingi milioni sita leo, haiwezekani. Mfugaji akiambiwa kulipa shilingi milioni nne leo haiwezekani; yaani how much is milioni nne? Yaani ni fedha nyingi kweli kwa mfugaji mdogo. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hawa watumishi kidogo wanapokuwa wanalingalia hili, wawahurumie na wafugaji wetu, wawahurumie na wakulima wetu kwa sababu wanaumizwa sana na faini ambazo wanapigwa. Mheshimiwa Waziri, nimeshazungumza, nawe umeshakubali kuja pale, uje ujionee namna wananchi walivyo na malalamiko juu ya hifadhi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakuomba sana, wananchi wale walikuwa na shida ya eneo la mita 840. Naomba sana utakapofika pale uzungumze na wananchi, usikie kilio chao na kama utaona inafaa Mheshimiwa Waziri, basi muweze kuwarejeshea eneo hili ili watu wa Nyaruande pale Kata ya Nyaruande katika Jimbo langu la Busega na sehemu ya Jimbo la Magu waweze kunufaika pale Sayaka kwa sababu sasa hivi wanapata shida katika namna ya kupata sehemu za kuchungia ng’ombe, lakini pia sehemu kubwa ya kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri; wewe kule ni kwenu, wewe pale ndiyo umezaliwa, hili tatizo unalifahamu, njooni mlitatue ili wananchi wetu sasa waweze kunufaika na hii sehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nskushukuru sana, niseme nawapongeza, nawakaribisha Busega mje mtatue huu mgogoro. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru nami kwa kunipa nafasi kuchangia Mpango wa Bajeti 2022/23.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee sana nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayofanya kwa ajili ya Watanzania. Kipekee pia nimshukuru kwa fedha ambazo ametupatia hivi karibuni kwenye majimbo yetu, trilioni 1.3 katika sekta mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchomekea hapo eneo la elimu. Ni kweli kuna kazi zinafanyika kubwa kwenye Majimbo sasa, madarasa yanajengwa, tunamshukuru sana. Lakini ukweli lazima tukubaliane kujengwa kwa madarasa lazima kuwe directly proportional na upatikanaji wa Walimu. Kwa hiyo mimi niishauri Serikali ije na mpango katika Bajeti ya mwaka 2022/23 wa namna gani tunakwenda kuajiri walimu ili wakabiliane na wanafunzi wengi ambao wanakwenda kutumia madarasa haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunavyokuwa tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia madarasa pia tunamshukuru kwa sababu ni imani yangu kwamba tunakwenda ku-create ajira kwa ajili ya Watanzania na Walimu ambao bado hawajapata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie maeneo machache sana ya mpango huu. Taarifa ya Kamati ya Bajeti pamoja na taarifa ya Mheshimiwa Waziri imeonesha kwamba mwenendo wa Shilingi yetu ya Tanzania unazidi kuimarika. Lakini niseme tu kwamba ili shilingi yetu iendelee kuimarika zaidi ni lazima tufikirie ku-export final product kuliko kuwa na importation kubwa ya raw material kwa ajili ya viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini tunazungumza hivi? Ni lazima tuimarishe viwanda vyetu vya ndani na kuendelea kujenga viwanda mbalimbali ambavyo vitatoa final product kutokana na malighafi ambayo sisi wenyewe tunatengeneza hapa, malighafi nyingi zipo zinatokana na kilimo. Tuchukulie mfano kule kwetu Mkoa wa Simiyu na Mikoa ya Tabora, Mara na Mwanza, tunalima sana pamba, lakini pamba bado haina thamani kwa sababu hatutengenezi final products zinazotokana na pamba, isipokuwa tunafanya exportation ya material ambayo kule wenzetu wanakwenda kutengeneza final product.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeishauri Serikali, kuna andiko lilishaletwa Wizarani, Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda, kujenga kiwanda Mkoa wa Simiyu ili uweze kuhudumia Mikoa ya jirani, na kiwanda hiki kitakuwa cha vifaatiba vitokanavyo na pamba. Tunajua tunaweza tukapata gozi, tunaweza tukapata mashuka. Tutaokoa fedha nyingi za kigeni ambazo tunakwenda kununua vifaa hivi nje, vitaendelea kupatikana kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hiki pia kitatoa ajira kwa Watanzania, zaidi ya Watanzania 1,000 wataajiriwa kupitia viwanda hivi. Kwa hiyo tunapokuwa tunazungumza habari ya viwanda tunazungumza habari ya ku-maintain fedha yetu ili isiendelee kushuka thamani yake bali iendelee kupanda kwa kuwa na products ambazo zinapatikana kwenye nchi yetu. Mfano umeutoa, hata hivi vyuma ambavyo vinatengeneza reli tungekuwa tumetengeneza kupitia Liganga huko wataalam wanasema wala tusingekuwa na haja ya kuagiza. Maana yake fedha yetu ingeendelea kuimarika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye kuimarika kwa fedha mimi huwa najifikiria swali moja, sijui wataalam wanasemaje, lakini huwa nawaza kwa nini mimi niko kwenye nchi yangu Tanzania ninakwenda hotelini naambiwa charge ni dola 200. Sasa nawaza kwa nini naambiwa dola 200 kwenye nchi yangu, si niambiwe tu laki nne ya Tanzania nijue? Kwa nini, kwa sababu demand ya dola itakuwa kubwa kuliko supply na demand ikiwa kubwa maana yake fedha yako ya Tanzania ina-depreciate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najua wataalam haya wanashauri na mimi naomba niseme kama ambavyo amepiga marufuku Mheshimiwa Simbachawene hivi karibuni kutupa pesa chini wakati wa kutunza vikundi mbalimbali, kuna haja sasa Mheshimiwa Waziri kuja na sera ya kukataza charges zozote ambazo wana-charge katika fedha za kigeni. Hakuna sababu ya kwenda kwenye hoteli ukaambiwa dola, maana yake itabidi ukatafute dola ili uende ukalipe hiyo charge ambayo utakuwa umeambiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda siku moja pale…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Kabla ya taarifa, Wasukuma mtaipata, mlizoea kutupatupa hela chini sasa mtakamatwa wote. Taarifa inatokea upande gani? Mheshimiwa Ester.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa Kaka yangu, jirani yangu pale Mbunge wa Busega, kwamba ukienda nchi zingine ukifika airport lazima utabadilisha dola ili uweze kutumia kwa pesa za nchi husika, kwa hiyo ni jambo zuri.

MWENYEKITI: Unapokea taarifa Mheshimiwa Lusengekile.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili kwa sababu nilienda hoteli moja hapa Dar es Salaam nikanywa soda nikaambiwa dola moja, yaani nikawaza kwa nini naambiwa dola moja, si aniambie tu elfu mbili nijue. Lazima tuheshimu fedha yetu, tukiheshimu fedha yetu itakuwa na thamani, hakuna sababu ya ku- undermine fedha yetu. Mheshimiwa Waziri wa Fedha liangalie hili. (Makofi)

MWENYEKITI: Kwa hiyo Musukuma wewe unakwenda kwenye hoteli hujui hata malipo yatakuaje? Endelea mtani. (Kicheko)

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, issue hapa siyo kujua ni shilingi ngapi, issue hapa ni kuniambia anani-charge kwa dola hiyo ndiyo issue yangu. Mimi hata kama angesema 5,000 sina tatizo mtani, lakini shida ni kuni- charge kwa dola. Kwa hiyo, nataka tuimarishe shilingi yetu kwa namna ya pekee sana ya kuiheshimu fedha yetu. Mtu akifika airport pale ana dola zake atafute benki ilipo abadilishe achukue fedha zetu za ndani aende akaanze kutumia, hapo tutaimarisha shilingi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la riba, tumeona kwenye taarifa ya Kamati ya Bajeti. Wastani wa riba za mabenki kwenye kukopesha sekta binafsi tumeona ni asilimia 16.6. Ni kweli riba hizi ni kubwa na tunatamani mabenki yetu yapunguze riba.

MWENYEKITI: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nami niungane na wachangiaji wengine kukupongeza kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana. Naipongeza sana Kamati ya PAC na LAAC kwa taarifa ambayo wametuletea hapa inayoleta taswira kwa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ninaomba niishauri Serikali jambo moja. Serikali inapotaka kuingia kwenye uanzishwaji wa mifumo kwa ajili ya ukusanyaji wa fedha, naomba ifanye upembuzi yakinifu ili mifumo inayotengenezwa ije kuwa na tija kwa ajili ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Bandari mwaka 2010 iliingia mkataba wa miaka minne na Softech, mpaka 2014, kwa ajili ya kutengeneza mfumo wa ukusanyaji wa fedha. Mfumo huu ulikuwa unachukua gharama ya shilingi milioni 694, lakini mpaka kufikia mwaka 2014 mfumo haufanyi kazi na tayari Mkandarasi alikuwa amelipwa shilingi milioni 600 sawa na 87%. Inasikitisha kwa sababu fedha hizi ni za Watanzania, lakini mradi ule haukufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa Softech waliongezwa mkataba wa thamani ya shilingi milioni 55 kwa ajili ya kufundisha watumishi wa TPA ambapo mfumo haukufanya kazi. Pamoja na hayo, walilipwa shilngi milioni 55 zote na katika zile shilingi milioni 55 zilitakiwa kulipwa kwenye mkataba wa awali wa shilingi milioni 694. Serikali ikaingia hasara ya shilingi milioni 600 ya kwanza na ikaingia hasara ya shilingi milioni 55 ya pili. Hizi fedha ni za walipa kodi.

Mheshimiwa Spika, bado haitoshi, mwaka 2015/2016 kampuni ya 23rd Century System iliingia mkataba na Serikali ya kutengeneza mfumo pale TPA ambao ungegharimu shilingi bilioni 14, lakini mpaka mwaka 2019 mfumo huu haufanyi kazi, Serikali imelipa shilingi bilioni tisa; hasara kwa Serikali na hizi ni fedha za walipa kodi. Bado haitoshi fedha zililipwa shilingi bilioni tisa, lakini Mkandarasi hakulipa kodi ya zuio (Withholding Tax), akatoroka na fedha za wananchi sawa na shilingi milioni 874. Ni lazima Serikali ichukue tahadhari inapoanzisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado haikutosha kampuni ya SAP mwaka 2020 ikaajiriwa; kazi yake ni kuangalia kama huyu 23rd Century System Limited alifanya kazi ambayo ilistahili kulipwa zile fedha. Naye akalipwa dola za Kimarekani 433,000 sawa na shilingi milioni 874. Hizi ni fedha za walipa kodi na bado mifumo haikufanya kazi. Tunavyozungumza sasa hivi, ule mfumo haukufanya kazi tena pale TPA na fedha za walipa kodi zililipwa. Katika mifumo hii ni shilingi bilioni 17 zilitumika na mfumo haukufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, siyo TPA peke yake, ukienda pale GPSA wamenunua mfumo wa shilingi bilioni 1,087, sasa wamekuja kugundua ule mfumo hautoi yale mahitaji ambayo walikuwa wanayahitaji. Wamekuja kugundua ule mfumo hautawasaidia tena. Sasa wameshindwa kuutumia ule mfumo na fedha za Serikali zililipwa shilingi bilioni 1,087. Wameandika kibali kwenda Wizara ya Fedha, wabadilishe watumie mfumo mwingine na Wizara ya Fedha imewakubalia na hasara tayari imepatikana katika fedha za walipa kodi. (Makofi)

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mzungumzaji anateremsha taarifa muhimu sana, nilitaka kumpa taarifa kwamba TANESCO mwaka jana 2021 mwishoni wameingia mkataba na kampuni ya kutoka India kwa zaidi ya shilingi bilioni 69 kwa ajili ya mifumo ya TEHAMA na watu wengi tunajiuliza kama uwezo huo wa kampuni kutoka India haupo nchini Tanzania licha ya kwamba mifumo mingine ya Kiserikali inatengenezwa hapa Tanzania?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Simon Lusengekile unapokea taarifa hiyo.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, ninapokea taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tuone ni namna gani Serikali inaingia hasara katika mifumo ambayo haina tija na haileti matokeo chanya kwa Taifa. Wahasibu wanaita this is nugatory expenditure. The Government incur some expense that cannot generate economic benefit. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali kuchukua hatua za haraka kwa wale wote ambao wamesababisha hasara kwa Taifa. Watumishi ambao wapo ofisini wamesababisha hasara kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, tayari ameshaanza kuchukua hatua na kumwelekeza DG wa Bandari kuhakikisha kwamba wafanyakazi waliopo pale waliosababisha hasara hii wanachukuliwa hatua za haraka.

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ichukue hatua kwa makampuni haya ambayo yalilipwa fedha nyingi na Serikali shilingi bilioni 17 na mfumo haukuleta tija ikiwepo na hii 23rd Century System Limited iweze kulipa fedha za TRA ambayo ilikuwa ni Withholding Tax, shilingi milioni 877. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo naomba pia nichangie kidogo kuhusu kiwanda cha sukari pale Mbigiri. Serikali iliingia mkataba wa kusimika kiwanda cha sukari cha kisasa pale Mbigiri, lakini mpaka sasa tunapozungumza, kiwanda kile hakijawahi kusimikwa na Serikali imepata hasara ya fedha kwa sababu walilima miwa wakijua kwamba kiwanda kitawahi kuja, miwa ile imeharibika, tayari Serikali imepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 300. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haitoshi…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nampa taarifa jirani yangu wa Busega kwa mchango wake mzuri. Siyo Serikali tu, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imelazimishwa kuwekezwa hapo, PSSSF miaka mitatu imetengeneza hasara ya shilingi bilioni 11; na ukiuliza sababu, Serikali haijapeleka mashine.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Simon Lusengekile, unapokea taarifa hiyo?

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, pale Mbigiri NSSF ina 96% na Magereza wana 4%, tunazidi kudidimiza taasisi zetu. Waliingia mkataba wa kununua miwa ya outgrowers; wakulima wa mazingira ya pale. Wakulima wamekopa fedha benki kwa ajili ya kuwekeza kwenye kilimo cha miwa wakijua kwamba baada ya kiwanda kuja watauza ile miwa. Kiwanda hakijasimikwa mpaka sasa hivi, wananchi wanateseka, wanashindwa kulipa mikopo kwa sababu kiwanda hakijapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara husika sasa iharakishe kusimika kiwanda hiki ili kiweze kuleta tija kwa Watanzania. Ninaamini kitaleta ajira nyingi kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)