Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Justin Lazaro Nyamoga (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, pia nami nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ananiwezesha kwa mara ya kwanza kusimama hapa Bungeni na kuchangia. Nikushukuru wewe, lakini pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Kilolo ambao waliniamini na kunituma niwawakilishe.

Mheshimiwa Spika, nitajielekeza kwenye suala zima la kilimo na mnyororo wa thamani, lakini kabla sijaenda huko, napenda kupongeza na kuunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo ilijaa hekima, busara, mwongozo na maono ambayo naamini katika miaka mitano ijayo tutakuwa na story au hadhithi ya kusimulia ya mabadiliko.

Mheshimiwa Spika, pia niipongeze Tume ya Uchaguzi, kwenye hotuba ilionesha wazi kwamba walifanya matumizi mazuri ya hela hadi kuwa na albaki ya karibu bilioni 69, kiwango cha uadilifu mkubwa ambacho walikionesha.

Mheshimiwa Spika, tukielekeza macho yetu kwenye suala zima la kilimo hasa kwenye suala la uwekezaji, napongeza hotuba hiyo kwa sababu ukurasa wa 29 unataja chai pamoja na mazao mengine kuwa mazao ya kipaumbele. Naomba nijikite kwenye hili suala la chai hasa mawazo na maoni ya wananchi wa Kilolo.

Mheshimiwa Spika, pale Kilolo kuna jumla ya hekta 3,600 ambazo zina rutuba kwa ajili ya kilimo cha chai. Siyo hivyo tu, kuna zaidi ya hekta 184 zimepandwa chai tangu miaka ya 1990 na kuwekewa kiwanda feki. Ile michai hivi tunavyozungumza, ile miti imekuwa inatosha hata kujinyongea. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, tangu miaka ya 1990 imekuwa ni kutafuta mwekezaji. Sasa najiuliza, pamoja na nia na dhamira ya Mheshimiwa Rais, ikiwa tutachukua zaidi ya miaka 30 kutafuta mwekezaji kwa ajili ya shamba na kiwanda cha chai kimoja, tutafika ndani ya miaka mitano?

Mheshimiwa Spika, lazima kuna mahali tunakwama. Nami napenda sana kumwomba kaka yangu, Waziri anayehusika na uwekezaji pamoja na viwanda na biashara ambao wanalijua jambo hili walitilie mkazo kwa sababu uzalishaji wa chai katika Wilaya ya Kilolo ambapo ardhi yake inafanana na Wilaya ya Mufindi yenye zaidi ya viwanda saba, hiyo ingeweza kukuza uchumi kwa kiwango kikubwa na wananchi wale waliopanda ile michai wanataka kuanza kung’oa kubadilisha mazao.

Mheshimiwa Spika, napenda kulizungumzia hili kwa mkazo kwa sababu watu ni lazima wajue kwamba moja ya sababu ya kupanda ile chai ilikuwa ni zao linaloweza kulinda vyanzo vya maji ambayo ndiyo yanayoenda Mtera na hata Kidatu. Kwa hiyo, tutakapobadilisha na kulima zao lingine pia tutavuruga vile vyanzo vya maji ambavyo vinalindwa kutokana na kulima lile zao la chai.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nizungumzie zaidi kuhusu tafiti zinazofanywa na uelekezaji wa mazao. Hivi karibuni nilimwona Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa kule Kigoma akihimiza sana utafiti wa mbegu na uzalishaji wa zao la mchikichi ambalo linalimwa katika mkoa ule.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa taarifa kwamba watu wa Kilolo wanalima maparachichi; na siyo Kilolo tu, ni Mkoa mzima wa Iringa na sehemu ya Mkoa wa Njombe. Changamoto yake ni aina ya miche wanayopanda, hiyo mbegu wanayolima; je, ni ile ambayo itapata soko wakati watakapoanza kuvuna?

Mheshimiwa Spika, hapa napenda kutoa ushauri kwamba ipo hii Taasisi ya Utafiti inayoitwa TARI, napenda waelekeze nguvu kwenye utafiti wa mazao ya matunda na mbogamboga kwa kuweka kituo kabisa katika Mkoa wa Iringa au Njombe kwa ajili ya kuhakikisha haya mazao kama parachichi yanapolimwa, wakulima wanalima mazao sahihi ambayo yatapata soko wakati wa kuvuna utakapofika.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kila mtu anakuza miche, anaokota mbegu huko, wakulima wanauziwa, wakati mwingine wanaambiwa ndani ya miaka mitatu wataanza kuvuna, ikifika miaka mitatu mti unarefuka tu na hakuna mazao kwa sababu hawakujua kama hiyo mbegu wanayotaka kuilima ni bora ama siyo bora. Udhibiti wa mbegu hasa miche, ni changamoto kwenye uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuzungumzia umuhimu wa mnyonyoro wa thamani katika mazao yanayolimwa kwenye maeneo yetu. Kwa sababu tuna nia ya kuwa na nchi ya viwanda, ni lazima kuangalia ni jinsi gani tunaboresha mnyororo wa thamani. Nitatoa mfano wa zao la nyanya ambalo linalimwa sana katika baadhi ya maeneo kwenye Jimbo langu pia. Maeneo hayo ni Ilula na Ruaha Mbuyuni yote ambapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa huwa wanapita na kununua nyanya.

Mheshimiwa Spika, wakati unapita mara ya kwanza unaweza ukanunua tenga moja kwa shilingi 10,000/= lakini upo wakati utakaonunua kwa shilingi 90,000/=. Sababu ni kwamba hakuna namna nzuri ya uongezaji wa thamani kwa mazao yetu. Kwa hiyo, wakati fulani wananchi wanalima kwa gharama kubwa na wanashindwa kuvuna na kuuza kwa bei kubwa kwa sababu thamani yake haijaongezwa.

Mheshimiwa Spika, nafikiri haujafanyika utafiti wa kutosha wa masoko kwa sababu nafahamu ziko nchi ambazo hazilimi nyanya lakini zinauza nje. Wakati mwingine tumesikia baadhi ya mazao yanasafirishwa kwenda nchi nyingine na kule yanapofika ndipo yanapouzwa. Mfano mmojawapo ni parachichi; ukifanya utafiti utakuta bandari zetu bado hazi- pack na kupeleka nje, wala viwanja vyetu vya ndege; lakini zipo nchi ambazo tayari zinafanya hivyo kwa kuchukua mazao hayo kutoka kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hili tusipolifanyia kazi maana yake ni kwamba tunazinufaisha hizo nchi jirani. Pamoja na ujirani mwema, lakini siyo kwa kufikia kiwango cha sisi kulima parachichi, miti ya mbao, zikauzwe kupitia nchi jirani. Napendekeza suala hili lifanyiwe utafiti wa kutosha na Wizara zinazohusika ili mazao yanayolimwa na wakulima kwenye maeneo yetu yaweze kuongezewa thamani na wananchi wale waendelee kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia ukurasa wa 33 unaoelezea kuhusu ubora wa mifugo na vitu vingine mbalimbali. Tukizungumzia mifugo, tunazungumzia uboreshaji wa thamani. Katika hili napenda kupongeza maana ndani ya hotuba hii imetaja baadhi ya machinjio yanayoboreshwa. Katika Mkoa wa Iringa iko machinjio moja ambayo naamini ni mojawapo itakayoboreshwa.

Kwa kuwa machinjio hizi baadhi yake zimechukua muda mrefu; na kwa kuwa baadhi ya watu wanaoishi katika maeneo yetu ya Jimbo la Kilolo na maeneo mengine ya Mkoa wa Iringa ni wafugaji, napendekeza kasi ya uboreshaji wa machinjio hizi iweze kuwa ya kwenda mbele ili wananchi hao waweze kufaidika mapema.

Mheshimiwa Spika, wakati huu ninapozungumzia hili, napenda pia nizungumzie kuhusu vyanzo vya utalii hasa katika Mkoa wa Iringa na hususan Jimbo la Kilolo ambalo natoka. Moja kati ya utalii unaohimizwa ni utalii wa kihistoria. Pale kwenye Jimbo langu la Kilolo, Kihesa Mgagao pale waliishi wapigania uhuru wa maeneo mbalimbali, hata Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Marehemu Nelson Mandela alishafika pale. Pia pana kumbukumbu nyingi za wapigania uhuru hao, kumbukumbu ambazo kwa sasa lile eneo limegeuzwa kuwa gereza.

Mheshimiwa Spika, sisi wananchi wa Kilolo hatusemi kwamba hatufanyi makosa; tunafanya, lakini gereza lile idadi ya wafungwa wake hawafiki 20. Pia pale ni sehemu ya kumbukumbu za kihistoria. Wanafunzi wa Kilolo na maeneo mengine ya Mkoa wa Iringa hawawezi kwenda kujifunza pale kwa sababu ya ulinzi uliowekwa mahali pale.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote, napenda kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii. Nimepitia Mpango huu na ningependa kuchangia kwenye mambo machache kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu mfumo wa kodi hasa kwa wafanyabiashara wa mazao mbalimbali ya misitu na mazao ya mbogamboga. Sheria ya kodi hii inamtaka kila mfanyabiashara mwenye mzunguko unaofikia shilingi milioni 14 basi awe na mashine ya EFD na kwa hiyo, haikuzingatia baadhi ya vitu ambavyo vinawakwaza wafanyabiashara. Nitoe mfano kidogo kwamba, wako watu ambao wanauza mara moja tu, kwa mfano wakulima wa miti ya mbao anachana mbao na anauza anaweza akapata milioni 30 na akapeleka mzigo wake au wafanyabiashara wa mazao wanaonunua kidogokidogo na mzigo unafika kwa kiwango hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna utaratibu wa mageti ambapo yule mwenye mzigo akifika pale, basi anadaiwa risiti ya mahali alikonunua. Hii inatakiwa kurekebishwa kwa sababu kwa kufanya hivyo inawataka watu wengi sana ambao ni wakulima wa kawaida, watu wengi sana ambao ni wafanyabiashara wa mara moja, huo mzunguko wanaupata kwa haraka na sidhani kama tuko tayari kugawa mashine za EFD kwa wakulima, tuko tayari kugawa mashine za EFD kwa mtu anayechana mbao mara moja tu akauza. Irekebishwe ili iseme wafanyabiashara wa maduka au wafanyabiashara wenye sehemu ya kudumu kwa sababu, ndiko ilikolenga, lakini haiku-specify kwa hiyo, wale wa TRA wanapojaribu ku-execute wanasababisha usumbufu kwa baadhi ya wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kuzungumza ni ujenzi wa viwanda vya kimkakati. Juzi hapa nilitembelea kiwanda kimoja cha kutengeneza samani na kimejengwa na VETA kiko hapa Dodoma. Nikajiuliza sababu, iliyofanya VETA kujenga kiwanda hapa kwa sababu, ni cha samani; sikuona kama kuna misitu ya kutosha, kuna miti ya kutosha na hiyo ni taasisi ya umma. Ningeshauri viwanda vya kimkakati kama kile, laiti kama kingejengwa mahali kama Kilolo, Mufindi au Mafinga ambako kuna miti ya kutosha maana yake ni kwamba, hata shida ya madawati ingekuwa historia kwa sababu, kingeweza kufanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba hizi taasisi za umma, taasisi kama VETA na magereza ambao wanataka kuwekeza kwenye viwanda waangalie mazingira, hasa hivi viwanda vya samani. Sasa kwenye huu Mpango iangaliwe, tunaposema viwanda vya kimkakati basi vijengwe kule ambako mazao hayo yanazalishwa badala ya kuweka mahali kwa sababu ambazo huenda haziwezi kuleta tija kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni kuhusu barabara, hasa TARURA, ambalo limezungumzwa na watu wengi. Naunga mkono wale wanaosema kitafutwe chanzo kingine, uundwe Mfuko mwingine wa peke yake na tuangalie kwenye sekta ya mawasiliano, ili tupate fungu la kutosha, tuweze kutatua changamoto ya barabara kwa sababu, baada ya hapo hiyo ndio itakayokuwa mwarobaini wa matatizo tuliyonayo, ili pia TANROADS iweze kubakia na hela za kutosha kwenye Mfuko wake ilionao sasa, kwa sababu, kama tukigawa kwa kiwango kikubwa tutaifilisi TANROADS na itashindwa kufanya kazi tutarudi hapa tena kulalamika. Kwa hiyo, Mfuko mwingine ni muhimu ili kwamba, tusiifilisi TANROADS na TARURA itafutiwe chanzo kingine ambacho kitasababisha pato la Mfuko wa TARURA kuwa stable.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ningependa kuzungumzia suala zima la ajira kwa vijana na kuweka mazingira wezeshi na rafiki. Watu wengi sana wanamaliza form four wanapata division four na wengine wanapata division zero na hao wengi hatujawawekea utaratibu wowote. Tukiendelea hivi ina maana kwenye vijiji vyetu na kwenye maeneo yetu kuna vijana wengi ambao hawajawekewa mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza vyuo hivi vya ufundi vitakapojengwa, vyuo hivi vya kati, viangalie taaluma maalum kwenye haya maeneo. Ikiwa ni maeneo kama kule kwetu basi ufundi wa kutengeneza samani, ufundi wa aina mbalimbali, lakini pia kufundisha masuala mazima ya kilimo na aina mbalimbali za kilimo zinazolimwa kwenye maeneo husika, ili wale vijana wanaopata division four na wanaopata division zero tusiwaache bila kuweka mpango maalum kwamba, maendeleo yao ya maisha yao yatakuwaje kwa sababu ni wengi na hao watakuja kuwa watu ambao hawana kitu chochote wanachoweza kufanya. Hilo ni janga ambalo kama tusipoliangalia si jambo zuri kwa maendeleo ya Watanzania.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imegonga, ahsante sana.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante san ana naunga mkono hoja. (Makofi)