Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon Omary Juma Kipanga (123 total)

MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Kumekuwa na wimbi la kukosa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri waliomaliza kidato cha sita kwenye shule binafsi kwa madai kuwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi wazazi au walezi wao wana uwezo wa kuwalipia ada ya chuo.

Je, Serikali katika kuleta usawa kwenye fursa hii ya mikopo ya elimu ya juu haioni haja ya kutoa mikopo hiyo kwa kuzingatia ufaulu wa wanafunzi wote?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele kwenye Bunge lako tukufu, nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniona na kuniamini kwamba na mimi naweza nikawa miongoni wa watu wa kuweza kumsaidia.

Mheshimiwa Spika,baada ya hayo sasa, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge Moshi Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawalenga vijana wenye sifa za kitaaluma za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za elimu. Upangaji na utoaji mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura 178) ambayo inabainisha sifa za msingi za mnufaika ambazo zinajumuisha.Awe Mtanzania; awe amedahiliwa kwenye chuo kinachotambulika; awe ameomba mkopo, asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake. Aidha, kusoma shule binafsi za sekondari siyo kigezo cha mwanafunzi mwombaji kunyimwa mkopo wa kugharamia elimu ya juu. Wapo wanafunzi waliosoma shule binafsi na wanapata mkopo baada ya kuthibitisha uhitaji wao kwa mujibu wa vigezo vya utoaji mikopo.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa mujibu wa sheria tajwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ina mamlaka ya kuweka utaratibu wa kubaini wahitaji. Kwa sababu hiyo, Bodi huandaa mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika. Sifa za ziada zinazoainishwa kwa waombaji ni pamoja na; uyatima, ulemavu au wazazi wenye ulemavu na wale ambao masomo yao ya sekondari au stashahada yalifadhiliwa ambapo katika kundi hili wapo waombaji wengi waliosoma katika shule za sekondari za kulipia.

Mheshimiwa Spika, nashauri Waheshimiwa watusaidie kutoa elimu ili kuwezesha jamii kubadili mtazamo huu. Aidha, wawashauri waombaji wajaze kikamilifu fomu za maombi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Bodi wakati wa uombaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na kuambatanisha nyaraka zote muhimu ili kuepuka uwezekano wa mwanafunzi mwenye sifa stahiki kukosa mkopo kutokana na kutojaza kwa usahihi fomu ya maombi ya mkopo.
MHE. PRISCUS J. TARIMO Aliuliza:-

Kumekuwa na wimbi la kukosa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri waliomaliza kidato cha sita kwenye shule binafsi kwa madai kuwa wanafunzi wanaosoma shule binafsi wazazi au walezi wao wana uwezo wa kuwalipia ada ya chuo.

Je, Serikali katika kuleta usawa kwenye fursa hii ya mikopo ya elimu ya juu haioni haja ya kutoa mikopo hiyo kwa kuzingatia ufaulu wa wanafunzi wote?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele kwenye Bunge lako tukufu, nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniona na kuniamini kwamba na mimi naweza nikawa miongoni wa watu wa kuweza kumsaidia.

Mheshimiwa Spika,baada ya hayo sasa, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge Moshi Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawalenga vijana wenye sifa za kitaaluma za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za elimu. Upangaji na utoaji mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura 178) ambayo inabainisha sifa za msingi za mnufaika ambazo zinajumuisha.Awe Mtanzania; awe amedahiliwa kwenye chuo kinachotambulika; awe ameomba mkopo, asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake. Aidha, kusoma shule binafsi za sekondari siyo kigezo cha mwanafunzi mwombaji kunyimwa mkopo wa kugharamia elimu ya juu. Wapo wanafunzi waliosoma shule binafsi na wanapata mkopo baada ya kuthibitisha uhitaji wao kwa mujibu wa vigezo vya utoaji mikopo.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa mujibu wa sheria tajwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, ina mamlaka ya kuweka utaratibu wa kubaini wahitaji. Kwa sababu hiyo, Bodi huandaa mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika. Sifa za ziada zinazoainishwa kwa waombaji ni pamoja na; uyatima, ulemavu au wazazi wenye ulemavu na wale ambao masomo yao ya sekondari au stashahada yalifadhiliwa ambapo katika kundi hili wapo waombaji wengi waliosoma katika shule za sekondari za kulipia.

Mheshimiwa Spika, nashauri Waheshimiwa watusaidie kutoa elimu ili kuwezesha jamii kubadili mtazamo huu. Aidha, wawashauri waombaji wajaze kikamilifu fomu za maombi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Bodi wakati wa uombaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na kuambatanisha nyaraka zote muhimu ili kuepuka uwezekano wa mwanafunzi mwenye sifa stahiki kukosa mkopo kutokana na kutojaza kwa usahihi fomu ya maombi ya mkopo.
MHE. REGINA N. QWARAY Aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza bajeti ya kuboresha elimu katika Vyuo vya Ufundi (VETA) Mkoani Manyara ili kuboresha utoaji wa elimu ya ufundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiongeza wigo wa bajeti kwa ajili ya kutekeleza mipango mbalimbali ya kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi nchini. Mkoa wa Manyara ni moja kati ya mikoa inayonufaika na ongezeko hilo la bajeti. Katika kipindi cha mwaka 2018 – 2020, Serikali imetumia kiasi cha shilingi 1,925,438,420.13; kati ya fedha hizo shilingi 600,000,000 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na shilingi 505,159,420.00 zimetumika kununua nyumba za watumishi katika chuo cha VETA Manyara kutoka Shirika la Nyumba la Taifa.

Mheshimiwa Spika, katika Chuo cha VETA Gorowa, kiasi cha shilingi 337,081,677.13 kimetumika kwa ajili ya ujenzi wa karakana, ofisi ya utawala na madarasa. Vilevile, katika Chuo cha VETA Simanjiro Serikali imetumia kiasi cha shilingi 223,981,323.00 kwa ajili ya kununulia vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kujenga bweni la wasichana. Aidha, shilingi 259,279,000.00 zimetumika kugharamia mafunzo ya muda mfupi katika Vyuo vya VETA Manyara na Gorowa.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuongeza bajeti kwa ajili ya kuboresha utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi katika mkoa wa Manyara na mikoa mingine kwa ujumla kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE Aliuliza:-

Miradi mikubwa ya ujenzi nchini inafanywa na kampuni kutoka Bara la Asia wakati wahandisi nchini wanasoma uhandisi kwa mitaala ya Uingereza na Marekani.

(a) Je, Serikali haioni haja ya kuongeza mitaala ya Asia katika mitaala ya Vyuo vya Uhandisi ili Wahandisi wetu wapate utaalam katika miradi ya ujenzi?

(b) Je, suala la kubadilishana weledi limepewa kipaumbele gani katika miradi inayoendelea kujengwa hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Uhandisi ni fani ya Kimataifa ambayo mitaala yake haitofautiani kijiografia. Kwa muktadha huo mitaala ya shahada za uhandisi katika vyuo vyetu nchini nayo ni ya viwango vya kimataifa. Hata hivyo, ni kawaida kuhuisha mitaala mara kwa mara ili kuingiza utaalam mpya kwenye fani. Hivyo basi ni nia ya Serikali yetu kuhuisha (review and update) ya mitaala ya kihandisi na fani nyingine za kipaumbele kwenye Tanzania ya viwanda kama tunavyoongozwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025, Ibara ya 80 Ukurasa 130 Kipengele (c) ambayo inaagiza “kuhuisha Mitaala (curriculum review) na kuanzisha programu kulingana na mahitaji ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili wahitimu wawe na stadi stahiki za kumudu kufanya kazi mbalimbali za kuajiriwa na kujiajiri na hasa kwa kuzingatia Mapinduzi ya Nne ya Viwanda”.

(b) Mheshimiwa Spika, suala la kubadilishana uweledi wa kihandisi kati ya miradi mikubwa inayoendelea tayari linatekelezwa ambapo wahitimu wetu wa uhandisi hupata nafasi za utarajali katika miradi yetu mikubwa ya Kitaifa ili kupata weledi. Kwa mfano, kupitia Bodi ya Usajili wa Wahandisi (Engineers Registration Board) wapo wahandisi wahitimu 197 ambao wanashiriki kwa sasa katika miradi mikubwa mbalimbali mfano Mradi Umeme wa Mwalimu Nyerere na Mradi wa Reli ya Mwendo Kasi. Hivyo, Serikali itaendelea kuweka mfumo wa kuhakikisha kuwa katika miradi mikubwa inayotekelezwa nchini suala la kubadilishana uweledi linaendelea kupewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha dhana ya elimu bure kwa kutoa elimu bure kuanzia Shule ya Msingi hadi Kidato cha Tano na cha Sita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, dhana ya utoaji Elimu Msingi Bila Malipo inamaanisha kuwa mwanafunzi atasoma bila mzazi au mlezi kulipa ada wala michango ya fedha iliyokuwa inatozwa shuleni kabla ya kutolewa kwa Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka 2015. Gharama hizo zote ambazo mzazi au mlezi alitakiwa kutoa kwa sasa hulipwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, dhana ya Elimu Bila Malipo inalenga elimu msingi. Elimu hii inaanzia Elimu ya Awali hadi Elimu ya Sekondari, Kidato cha Nne ili kuwajengea watoto wa Kitanzania misingi imara ya masomo ngazi zinazofuata na ustawi wa maisha yao kwa ujumla. Elimu ya kidato cha tano na sita nchini hutolewa kwa ushirikiano kati ya wazazi/ walezi na Serikali. Wazazi au walezi hutakiwa kuchangia ada ya shilingi 70,000 kwa wanafunzi wa shule za bweni na shilingi 20,000 kwa wanafunzi wa shule za kutwa kwa mwaka. Serikali hugharamia gharama nyingine zilizobaki kama vile mishahara ya walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa mfano vitabu na vifaa vya maabara pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kwa vijana wanaoshindwa mitihani kwenye ngazi mbalimbali za elimu nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwaendeleza vijana wakiwemo wale ambao hawakubahatika kuendelea na ngazi ya elimu inayofuata ya masomo baada ya kuhitimu. Hii ni kwa sababu vijana hawa ndiyo rasilimaliwatu ya Taifa inayotegemewa katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mipango mbalimbali ya kuwaendeleza vijana hao. Mipango hiyo ni pamoja na ujenzi wa Vyuo vya VETA katika ngazi za Mikoa na Wilaya pamoja na ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 2020/ 2021, Serikali imeendelea na ujenzi wa vyuo vipya vya VETA 29 katika ngazi ya Wilaya ambavyo vinatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali imeendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 kwa lengo la kuwezesha wananchi na vijana kupata ujuzi mbalimbali. Aidha, vipo vyuo 34 vya Wilaya na 22 vya Mikoa ambavyo vinadahili wanafunzi katika fani mbalimbali na hivyo kutoa fursa kwa vijana hao kujiendeleza na kupata ujuzi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaomba wazazi na Watanzania kwa ujumla kutumia vyuo hivyo ili kuwawezesha vijana na wananchi wengine kujiendeleza na kupata ujuzi katika fani mbalimbali. Ahsante.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE Aliuliza: -

Je, ni kwa kiwango gani Serikali inajiridhisha kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu imetolewa kwa wanafunzi walengwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Atupele Fredy Mwakibete, Mbunge wa Busekelo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajiridhisha kuwa inatoa mikopo kwa wanafunzi walengwa, kupitia vigezo vilivyowekwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura178) ambayo inawalenga wanafunzi wa Kitanzania wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu, lakini kutokana na hali ya kiuchumi hawana uwezo wa kumudu gharama. Vigezo hivyo ni mwombaji anatakiwa awe Mtanzania mhitaji; awe amepata udahili katika taasisi inayotambulika; asiwe na ufadhili wa masomo yake ya elimu ya juu kutoka taasisi nyingine; na awe ameomba mkopo kwa usahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha ili kuwafikia wahitaji wengi zaidi Sheria ya Bodi ya Mikopo imetoa mamlaka kwa Bodi kuweka vigezo vya ziada ambapo katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ilitangaza Mwongozo wa Utoaji wa Mikopo uliotaja sifa na vigezo vya ziada kama ifuatavyo: Yatima; mwombaji au mzazi mwenye ulemavu; mwombaji aliyefadhiliwa katika masomo yake ya sekondari au stashahada; na mwombaji aliyetoka katika familia ya kipato cha chini au kaya maskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia sifa na vigezo hivi, katika mwaka wa masomo 2020/2021, jumla ya waombaji wapya 66,374 wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu waliomba mkopo na kati ya hao waombaji 55,318 sawa na 83% walipangiwa mkopo kwa mchanganuo ufuatao: Yatima walikuwa 1,137 sawa na 2.06%; waliofiwa na mzazi mmoja walikuwa 8,683 sawa na 15.7%; waombaji wasiofahamu wazazi au waliolelewa katika Vituo vya Ustawi wa Jamii walikuwa ni 71 sawa na 0.17%; waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye ulemavu walikuwa ni 92 sawa na 0.13%; waombaji waliofadhiliwa na taasisi zinazotambulika walikuwa 1,992 sawa na 3.6%); na waombaji kutoka kaya maskini walikuwa 43,343 sawa na 78.35%. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO K.n.y. MHE. RASHID A. SHANGAZI Aliuliza:-

Je, ni vigezo gani hutumika kushindanisha ufaulu kwa shule za msingi na sekondari kwa Halmashauri na Mikoa hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu kwanza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu toka uteuzi ulipofanyika, basi nichukue fursa hii adhimu na adimu kwanza kabisa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mungu ambaye ametuumba na akatujalia uhai, lakini shukrani ya pili kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuamini katika Wizara hii kuendelea kuhudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kigezo kinachotumika katika kuzipanga shule kwa ubora wa ufaulu katika Halmashauri na Mikoa kwenye mitihani ya kitaifa ni wastani wa alama kwa shule za msingi na ufaulu wa watahiniwa kimadaraja na kimasomo kwa shule za sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mpangilio wa ubora wa ufaulu kwa Halmashauri na Mikoa hutegemea wastani wa ufaulu wa shule zilizopo katika Halmashauri au Mkoa husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule za msingi hupangwa katika mpangilio wa ubora wa ufaulu kwa kuzingatia kigezo cha wastani wa alama walizozipata watahiniwa wote wa shule husika katika masomo yote waliyoyafanya. Wastani huo hupatikana kwa kufuata hatua zifuatazo; kukokotoa jumla ya alama walizopata watahiniwa wote wa shule husika kwenye masomo yote waliyoyafanywa; na kukokotoa wastani wa alama wa shule kwa kugawanya jumla ya alama walizopata watahiniwa wote wa shule kwa idadi ya watahiniwa wa shule husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa shule za sekondari mpangilio wa ubora wa ufaulu huzingatia kigezo cha wastani wa ufaulu (Grade Point Average-GPA) wa watahiniwa kimadaraja na kimasomo. Wastani huo hupatikana kwa kukokotoa wastani wa ufaulu wa watahiniwa wa shule husika kimadaraja na kimasomo. Jumla ya wastani huo wa ufaulu wa shule wa kimasomo na kimadaraja hukokotolewa tena ili kupata ubora wa ufaulu kwa kila shule. Ahsante!
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo Kikuu katika Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benardetha Kasabago Mushashu Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na gharama kubwa za uwekezaji unaohitajika katika kuanzisha Vyuo Vikuu, ni vigumu kwa Serikali kuanzisha Chuo Kikuu katika kila Mkoa. Vyuo Vikuu vya Serikali na Binafsi vilivyopo nchini vinapokea wanafunzi kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na vilevile kutoka nje ya nchi ambapo ndiyo utamaduni wa Vyuo Vikuu Duniani.

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Kagera kuna tawi la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilichopo katika Makao Makuu ya Mkoa ambacho ni cha Serikali. Kwa sasa Serikali inaendelea na mpango wa kuboresha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza nafasi ya udahili na kuongeza ubora wa elimu ya juu itolewayo ili kukidhi mahitaji ya nchi. Ahsante.
MHE. ASIA A. HALAMGA K.n.y. MHE. NG’WASI D. KAMANI Aliuliza:-

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka sasa wa kufanya masomo ya Ujasiriamalai na Usimamizi wa Fedha kuwa masomo ya lazima kwa kila mwanafunzi nchini kwa kuwa Elimu ya Ujasiriamali ni mbadala wa changamoto ya ajira kwa vijana?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufundisha masomo ya ujasiriamali na usimamizi wa fedha ili kuwajengea wanafunzi stadi na ujuzi utakaowasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali katika jamii ikiwemo suala la ajira.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa masomo hayo yanafundishwa kuanzia ngazi ya elimu msingi na sekondari kama ifuatavyo: Shule za Msingi, Ujasiriamali na Usimamizi wa Fedha hufundishwa katika masomo ya stadi za kazi, maarifa ya jamii na hisabati. Katika ngazi za Shule ya Sekondari, masomo haya hufundishwa katika masomo ya Civics na General Studies ambayo husomwa na wanafuzni wote. Aidha, masomo hayo hufundishwa katika masomo chaguzi kama vile Book Keeping, Commerce, Economics, Accountancy, Home Economics, Mathematics na Agriculture.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na zoezi la kuboresha mitaala na mihtasari ya masomo katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kwa lengo la kuandaa mitaala itakayokidhi mahitaji na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kijamii katika ulimwengu wa sasa.

Mheshimiwa Spika, katika hatua hii, Serikali itatilia mkazo mbinu tete na stadi za maisha hususan stadi za karne ya 21 ambazo ni fikra tunduizi, ubunifu, ushirikiano, uongozi na stadi za teknolojia habari na mawasiliano ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kukabiliana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika jamii yetu na dunia kwa ujumla likiwemo suala la ajira. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaendeleza kimasomo watoto wa kike waliokatisha masomo kwa kupata ujauzito?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwaendeleza wanafunzi wanaoacha masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo wasichana waliopata ujauzito. Mikakati hiyo ni pamoja na Mpango wa Elimu Nje ya Mfumo Rasmi. Katika mpango huu wanafunzi wanaruhusiwa kufanya mitihani ya Kidato IV na cha VI. Kwa sasa kuna Vituo 753 vya Elimu nje ya mfumo rasmi vilivyosambaa katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hiyo, Serikali imeendelea kutoa fursa za wanafunzi kujiendeleza wakiwemo wale waliopata ujauzito. Fursa hizo ni pamoja na:- Mpango wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA), mpango wa elimu kwa vijana uitwao Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (Integrated Program for Out of School Adolescents - IPOSA). Serikali pia inatoa fursa za kujiendeleza kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) ambapo maeneo Manne ambayo ni; Taaluma (Academic skills), Stadi za Ufundi wa awali (pre-vocational skills), Ujasiriamali na Stadi za maisha (Generic Skills) kusisitizwa katika ujifunzaji. Ahsante.
MHE. USSI SALUM PONDEZA Aliuliza:-

(a) Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati wa wanafunzi wote kunufaika kwa 100% bila kujali shule walizosoma?

(b) Je, Serikali inawasaidiaje wazazi waliostaafu ambao wameshindwa kuchangia gharama za elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Jimbo la Chumbuni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178) ambayo inaelekeza kuwa walengwa wa mikopo hiyo ni wahitaji (needy).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa uhitaji wa mwanafunzi hupimwa kwa kuchambua taarifa zilizowasilishwa wakati wa maombi ya mkopo, zikiwemo gharama za masomo ya sekondari au stashahada. Uchambuzi huu hutumia king’amua uwezo (means testing tool) ambacho hubaini kiwango cha uhitaji cha mwombaji mmoja mmoja ukilinganisha na wengine.

Aidha, uhitaji wa mnufaika unatumika kuamua kiasi anachopangiwa kulingana na gharama ya shahada aliyodahiliwa. Baada ya uchambuzi linganishi, waombaji hupangiwa mikopo kulingana na uhitaji wao. Katika mwongozo, vigezo na sifa za kunufaika na mikopo ya elimu ya juu, hakuna kigezo mahususi cha shule aliyosoma mwombaji na mnufaika.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu waombaji wa mikopo ambao wazazi wao wamestaafu katika utumishi, Serikali inaamini utaratibu wa sasa wa kutambua na kuwapangia mikopo wahitaji wanaotoka katika familia zisizo na uwezo wa kumudu gharama za elimu ya juu kwa watoto wao unajitosheleza. Hata hivyo, Serikali ipo tayari kuendelea kupokea maoni ya namna ya kuboresha zaidi utaratibu huu.
MHE. MARYAM AZAN MWINYI Aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuwa na Mtaala mmoja kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne kati ya Tanzania Bara na Zanzibar? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Azan Mwinyi Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana vizuri na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika masuala mbalimbali ikiwemo suala la elimu hususan katika utekelezaji wa mitaala na kutoa elimu bora kwa watoto wa kitanzania.

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mitaala ya elimu kati ya Tanzania Bara na Visiwani, pande zote mbili hutumia mtaala mmoja kuanzia Kidato cha Kwanza hadi Kidato cha Sita. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:-

Uziwi ni moja ya aina ya ulemavu ambao una lugha yake ya ishara (signal language).

(a) Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kufundisha Lugha ya Ishara kama moja ya masomo ya lazima Shuleni kwa wanafunzi wote kuanzia Elimu ya Awali ili kuondoa kikwazo cha mawasiliano kati ya wenye uziwi na wale wanaosikia?

(b) Je, Tanzania tuna vitabu vya kufundishia Lugha ya Ishara katika lugha ipi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Stephen Lemomo Kiruswa Mbunge Longido, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Lugha ya alama katika kuondoa kikwazo cha mawasiliano kati ya wenye uziwi na wale wasio na uziwi. Aidha, ili kufikia lengo la kufundisha lugha ya alama kama somo katika ngazi zote za elimu, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuboresha ufundishaji wa lugha hiyo. Hatua hizo ni pamoja na kukamilika kwa usanifishaji wa Kamusi ya Lugha ya Alama ya Tanzania pamoja na uandaaji wa Mwongozo wa Utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Sekondari kwa wanafunzi viziwi Kidato cha kwanza mpaka cha nne chini ya Taasisi ya Elimu Tanzania.

Mheshimiwa Spika, vile vile, kupitia Chuo cha Ualimu Patandi na Chuo Kikuu cha Dodoma walimu wenye taaluma ya Elimu Maalumu katika fani ya ukiziwi na lugha ya alama wanaandaliwa.

Mheshimiwa Spika, vitabu vinavyotumika kufundishia lugha ya Ishara vimeandikwa katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili ili kukidhi mahitaji ya ufundishaji na ujifunzaji. Ahsante.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya Chuo Kikuu cha Afya Mbeya pamoja na Ndaki ya Afya na Sayansi Shirikishi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Ndaki ya Afya ya Sayansi Shirikishi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilihamia Mbeya mwezi Desemba, 2017 ili kupata hospitali kubwa ya kufundishia. Ndaki ilipewa nafasi katika majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, baadhi ya majengo yaliendelea kutumika kama yalivyokuwa na baadhi yalihitaji ukarabati.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, imefanya upanuzi na ukarabati mkubwa wa bwalo la chakula na ukarabati wa madarasa na maabara. Pia Chuo kilinunua na kufunga jenereta la dharura kwenye maabara. Kutokana na ufinyu wa nafasi ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, kama mkakati wa muda mfupi, majengo matatu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyopo eneo la Uzunguni yamekarabatiwa na kuwekewa samani ili yaweze kutumika. Pia Serikali imefunga vifaa vya TEHAMA katika majengo mbalimbali ya Chuo na kuweka mtandao wa internet kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali wa muda mrefu ni kupata ardhi Jijini Mbeya ili kuanza ujenzi wa majengo ya Ndaki ya Afya na Sayansi Shirikishi. Mkakati huo utatoa fursa ya kuongeza miundombinu ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia na kuongeza udahili wa wanafunzi wa shahada mbalimbali za Afya na Sayansi Shirikishi. Maombi ya ardhi yameshawasilishwa na ufuatiliaji unaendelea. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutenganisha fedha za maendeleo ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Fedha za Bodi ya Mikopo kwa kuzitengea Vote tofauti fedha hizi za mikopo ili kuleta tija ya miradi ya maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo yenye dhamana ya kuendeleza mtaji watu kwa ajili ya mipango na maendeleo ya Taifa letu. Aidha, lengo la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, ni kuongeza mtaji watu katika nchi yetu. Hivyo, utengaji wa fedha za mikopo ya elimu ya juu chini ya Fungu 46, ulizingatia majukumu ya Fungu husika ambayo ni kuandaa na kuendeleza mtaji watu kwa ajili ya maendeleo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza rasilimali fedha katika Sekta ya Elimu kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizopo. Hivyo, Serikali itaendelea kutafuta fedha zaidi ili kuendeleza hatua zake za kutatua changamoto zilizopo. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja kukipandisha hadhi Chuo cha Ualimu Nachingwea kuwa Chuo Kikuu cha Ualimu kutokana na mahitaji ya Walimu kuwa makubwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha vyuo vya ualimu hapa nchini, kikiwemo Chuo cha Ualimu Nachingwea, ni kuhakikisha kuwepo kwa walimu mahiri na wanaotosheleza mahitaji ya walimu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya watu wazima. Vilevile, Vyuo hivi vina jukumu kubwa la kuwezesha mafunzo ya walimu kazini ambapo walimu walio karibu na vyuo hivyo hupata nyenzo mbalimbali za kitaalamu ili kuboresha ujifunzaji na ufundishaji shuleni.

Mheshimiwa Spika, ongezeko kubwa la wanafunzi na shule katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kutokana na Sera ya Elimu Bila Malipo, limesababisha kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa walimu katika ngazi hizo. Ili kukidhi mahitaji ya walimu katika ngazi hizo, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya vyuo vya ualimu, uwekaji wa samani pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Chuo cha Ualimu Nachingwea ni miongoni mwa vyuo vilivyofanyiwa ukarabati na ujenzi kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mahitaji ya walimu, hususan katika ngazi ya elimu ya awali na msingi ni makubwa kutokana na ongezeko kubwa la shule na wanafunzi katika ngazi hiyo, Chuo cha Ualimu Nachingwea bado kinahitajika katika kuandaa walimu wa stashahada na astashahada.

Mheshimiwa Spika, hivyo, wanafunzi wa shahada wanaweza kuendelea kudahiliwa na vyuo vikuu vilivyopo nchini kwa kuwa, bado vina uwezo wa kufanya hivyo. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA katika Jimbo la Mbulu Vijijini ili vijana wapate ujuzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwa na lengo la kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya. Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitenga jumla ya shilingi bilioni 48.6 kwa ajili ya kujenga vyuo 29 vya VETA katika ngazi ya Wilaya ambavyo kwa sasa vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Mbulu kuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tango ambacho pia hutoa mafunzo ya ufundi stadi. Chuo hiki kinaendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu utakaogharimu jumla ya shilingi milioni 605.2 ambao unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA wilayani humo, nashauri wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kuendelea kutumia vyuo vilivyopo maeneo yote nchini, ikiwa ni pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi - Tango na Chuo cha VETA Manyara. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha Ujenzi wa Chuo cha VETA Shaurimoyo – Ludewa ili kuzalisha Wataalam watakaosaidia kutekeleza mradi wa Liganga na Mchuchuma utakapoanza?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Njombe kinachojengwa katika Wilaya ya Ludewa ni miongoni mwa vyuo vilivyokuwa vinajengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Elimu ya Ualimu (STVET – TE). Mradi huu ulikuwa unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambapo mkataba kati ya Serikali na Benki hiyo uliisha muda wake tarehe 31 Desemba, 2019, kabla mradi haujakamilika.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa kukamilika kwa mradi huu, utekelezaji wa mradi huu utaendelea kupitia Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ) kwa utaratibu wa “Force account”. Tathmini ya gharama imeshafanyika ambapo jumla ya shilingi 4,342,678,784.32 zitatumika katika kukamilisha ujenzi huu. Ujenzi wa Chuo hiki unatarajiwa kuanza tena katika Mwaka wa Fedha 2020/2021. Ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:-

Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kurekebisha mfumo wa elimu na kuingiza mbinu tete na stadi za maisha ili kuwajengea uwezo wa kiushindani vijana wanaohitimu na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; kwa niaba ya Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwawezesha wanafunzi kupata stadi mbalimbali zikiwemo stadi za maisha na mbinu tete ili kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo suala la ajira na kiteknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itafanya mapitio ya mitaala ya shule za msingi na sekondari ili kuingiza stadi mbalimbali kama vile stadi za maisha hususan stadi za karne ya 21 na mbinu tete. Stadi za karne ya 21 ni pamoja na fikra tunduizi, ubunifu, ushirikiano, uongozi na stadi za teknolojia ya habari na mawasiliano. Stadi na mbinu hizi zitasaidia kuwajengea vijana uwezo wa kiushindani katika soko la ajira. Ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na Sera na Mitaala shirikishi ili kuwa na msingi wa aina moja kuanzia elimu ya maandalizi, elimu msingi na sekondari kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuongeza ufaulu zaidi kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Mbunge, naomba kuchukua fursa hii kuwatakia heri wanafunzi wetu wote wa kidato cha sita walioanza mitihani yao siku ya jana ambayo itaendelea mpaka tarehe 25. Tuna watahiniwa wa kidato cha sita 81,343 katika vituo 808 kote nchini. Sambamba na hao vilevile tuna watahiniwa 6,973 wa vyuo vya ualimu ambao nao vilevile wanafanya mitihani yao katika vyuo 75 nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana vizuri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala mbalimbali ikiwemo suala la elimu hususan katika utekelezaji wa mitaala na kutoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Sera na Mitaala shirikishi baina ya pande mbili za Muungano, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) hushirikiana na Taasisi ya Elimu Zanzibar (TEZ) katika masuala mbalimbali yahusuyo utekelezaji wa mitaala. Ushirikiano huu hutoa fursa mbalimbali ikiwemo mijadala kuhusu utekelezaji wa mitaala na jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zitokanazo na ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi. Aidha, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya mapitio ya Sera ya Elimu ili kuweka uwiano wa miaka kwa Elimu ya Msingi baina ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara. Hivyo, nitoe rai kwa Watanzania wote kutumia nafasi hii ili kutoa maoni yao kuhusu mfumo huo. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo Kikuu cha Taifa Kusini mwa Tanzania na Kanda nyingine ambazo hazina Vyuo Vikuu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea M. Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, taratibu za uanzishwaji wa Vyuo Vikuu vya Umma hazilengi kuanzisha Vyuo Vikuu vya Kikanda, Kimkoa au Kiwilaya. Vyuo Vikuu vilivyopo nchini, vikiwemo vya Serikali na Binafsi, vinapokea wanafunzi kutoka Kanda zote za Tanzania Bara na Visiwani; na kutoka nje ya nchi. Huu ndio utaratibu wa Vyuo Vikuu Duniani kote. Katika Kanda ya Kusini kuna vituo vitatu vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) vilivyopo katika Makao Makuu ya Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Aidha, kipo Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris STeMMUCO kilichopo Mkoa wa Mtwara na Taasisi ya Uhasibu Tanzania TIA Kampasi ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mpango wa Serikali ni kuboresha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia. Tunafanya hivyo ili kuongeza nafasi za udahili na ubora wa elimu itolewayo na hivyo kukidhi mahitaji ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Mkopo wa Elimu ya Juu ili kuwapunguzia mzigo mkubwa wa malipo wanufaika wa mkopo huo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge Mtambwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya mapitio katika tozo na makato yanayohusu mikopo ya elimu ya juu ili kuwapunguzia mzigo wa tozo na makato wanufaika wa mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuanzia tarehe 01 Julai, 2021 Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, itafuta Tozo ya Asilimia Sita (6%) ya kulinda thamani ya fedha inayotozwa kwa wanufaika wa mikopo hiyo. Vilevile, Bodi ya Mikopo itatekeleza maelekezo yangu ya kuondoa tozo ya asilimia kumi (10%) ya wanufaika wanaochelewa kurejesha mkopo baada ya muda wa miezi 24 kupita baada ya kuhitimu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kupunguzwa kwa mzigo wa makato na tozo, nitoe wito kwa wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu ambao hawajajitokeza, kuanza kurejesha mikopo hiyo ili fedha hizo ziwasomeshe Watanzania wengine wahitaji.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa Mikopo ya Elimu ya Juu kwa Watu wenye Ulemavu kama ruzuku badala ya mikopo kama ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (SURA 178) ambayo inabainisha kuwa fedha na mikopo hiyo ni kwa ajili ya wanafunzi wahitaji (needy) wenye sifa za kujiunga na taasisi za elimu ya juu (eligible). Lengo la matakwa haya ya kisheria ni kuwawezesha wanafunzi wote wahitaji, wenye ulemavu na wasio na ulemavu, wanaotoka kwenye familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi kufikia ndoto zao za kupata elimu ya juu.

Mheshimiwa Spika, sheria pia inaipa Bodi mamlaka ya kuweka vigezo vya ziada ambapo katika mwaka wa masomo 2020/2021, Mwongozo wa Utoaji Mikopo ulitoa kipaumbele kwa makundi maalum wakiwemo wenye ulemavu au waombaji mkopo wenye wazazi wenye ulemavu. Kwa kutumia kigezo hiki, katika mwaka wa masomo 2020/ 2021, jumla ya wanafunzi 92 wenye ulemavu au wazazi wenye ulemavu walipangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 350.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kutoa ruzuku badala ya mikopo, Serikali italifanyia kazi kwa kuzingatia dhana nzima ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji na kuwa na mfuko endelevu wa mikopo ya elimu ya juu nchini.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafanya marekebisho ya malengo ya Mtaala wa Elimu ya Msingi na Sekondari nchini ili kuendana na uhitaji wa sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufanyia marekebisho mitaala ya elimu ya msingi na sekondari ili kuwawezesha wanafunzi kupata stadi mbalimbali zinazoendana na mahitaji ya wakati. Kwa sababu hiyo, Serikali imekuwa ikiboresha mitaala hiyo kila kunapokuwa na hitaji la kisayansi, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kiteknolojia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imepanga kufanya mjadala mpana kuhusu mfumo wa Elimu nchini ambao utahusisha Sera ya Elimu na Mitaala kwa ujumla ili iendane na wakati na ikidhi mahitaji ya sasa na baadaye. Ahsante.
MHE. ZUBERI M. KACHAUKA K.n.y. MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza:-

Je, Serikali iko tayari kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kata ya Makata - Liwale ambao wameanzisha ujenzi wa Chuo cha VETA na madarasa mawili yamekamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kachauka, Mbunge Liwale kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na wananchi za kuona umuhimu wa kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi katika maeneo yao wakiwemo wananchi wa Kata ya Makata - Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Wilaya nchini. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 29 nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaendelea na mpango huu kwa awamu, nashauri wananchi wa Kata ya Makata waendelee na juhudi hizo wakati Serikali inaendelea kutafuta fedha. Aidha, niombe uongozi wa Wilaya ya Liwale uwasiliane na uongozi wa VETA kuweza kuona namna ya kupata msaada wa kitaalam kuhusu ujenzi wa majengo ya Vyuo vya Ufundi Stadi. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kusomesha Wahadhiri wengi zaidi katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu (Ph.D) kwani waliopo sasa ni wachache?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao mpango mkakati wa kuongeza rasilimaliwatu katika taasisi za elimu ya juu ikijumuisha wahadhiri, wakutubi na wataalamu wa maabara na karakana ili kukidhi mahitaji ya viwango na ubora wa Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwezi Julai, 2021 Serikali kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) ina mpango wa kusomesha jumla ya wahadhiri 430 katika kipindi cha miaka mitano (2021-2026) ili kukabiliana na upungufu huu katika fani za kipaumbele (Priority Programs) katika vyuo vikuu vya Serikali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na mpango huo mahsusi, vyuo vikuu navyo vinaendelea kusomesha wahadhiri wao kupitia vyanzo vingine, ikiwemo mikataba ya kitaalam ya utafiti (collaborative research projects) na scholarship mbalimbali tunazopokea kutoka nchi rafiki ambapo wahadhiri hupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mipango hiyo, Jumla ya wahadhiri 621 katika ngazi ya shahada ya Uzamivu (PhD) na 241 katika Shahada ya Umahiri wanaendelea na masomo. Aidha kwa mwaka wa masomo 2021/2022 jumla ya wahadhiri 48 wanaendelea na masomo katika nchi mbalimbali. Kwa mfano katika nchi ya China wapo wanafunzi au wahadhiri 30, Uingereza 12 na Hangaria wahadhiri sita. Ahsante sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA Igunga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Igunga kama ifuatavyo: -

Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Igunga ni miongoni mwa vyuo 29 ambavyo vinaendelea kujengwa. Ujenzi wa Chuo hiki unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2021. Aidha, mchakato wa ununuzi wa mitambo na zana za kufundishia unaendelea sambamba na ukamilishwaji wa chuo hiki. Ujenzi wa chuo hiki utakapokamilika udahili wa wanafunzi wa kozi fupi utaanza mara moja wakati ule wa kozi ndefu unatarajia kutafanyika ifikapo Januari, 2022. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuleta Sera ya Ubunifu (Innovation Policy) ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jidith Salvio Kapinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango wa ubunifu na teknolojia kama nyenzo muhimu katika kurahisisha maisha yetu kwa kuokoa muda katika utendaji kazi, kuongeza tija na ubora katika uzalishaji wa bidhaa na hata utoaji huduma.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa ubunifu, mwaka 2012 hadi 2014 Serikali ilifanya mapitio ya Mfumo wa Ubunifu nchini ili kuutambua na kuainisha upungufu uliopo. Mapitio hayo yalitoa mapendekezo ya namna ya kuboresha mfumo huo ili kuleta tija katika shughuli za kijamii na kiuchumi. Aidha, moja ya mapendekezo hayo ni kuwa na sera yenye kuchochea ukuaji wa ubunifu nchini kwa maendeleo ya nchi.

Mheshimiwa Spika, hatukuwa na Sera maalum ya Ubunifu nchini na kwa kuwa, masuala ya ubunifu yanaenda sambamba na sayansi na teknolojia, kwa sasa Serikali inafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996 kwa lengo la kuiboresha ili ijumuishe masuala ya ubunifu. Aidha, maboresho hayo yanalenga kuifanya sera iendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia nchini, kikanda na kimataifa. Hivyo, katika mapitio hayo sehemu ya ubunifu itapewa uzito unaostahili. Ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha somo maalum la maadili kuanzia shule za msingi sambamba na somo la afya kwa mtoto ili kukabiliana na mabadiliko ya maumbile ya hisia za mwili pindi mtoto anapoanza kukua ikiwa ni njia ya kukabiliana na tatizo la watoto kuanza kushiriki mapenzi mapema?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatambua umuhimu wa kufundisha maadili kwa mtoto ili kukabiliana na mabadiliko ya maumbile ya hisia za mwili kama njia ya kukabiliana na tatizo la watoto kuanza kushiriki mapenzi mapema.

Mheshimiwa Naibu Spika, mitaala ya elimu inayotumika kwa sasa imetilia msisitizo kuhusu masuala ya maadili katika ngazi zote za elimu. Katika ngazi ya elimu ya msingi kuna Somo la Uraia na Maadili ambalo ni somo la lazima kwa wanafunzi wote kuanzia darasa la tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, suala la mabadiliko ya maumbile ya mtoto hufundishwa katika Somo la Sayansi na Teknolojia, Stadi za Kazi, na Uraia na Maadili. Katika ngazi ya sekondari masuala ya maadili hufundishwa katika Somo la Civics Kidato cha kwanza mpaka cha nne na katika Somo la General Studies Kidato cha tano na cha sita. Masomo haya ni ya lazima kwa wanafunzi wote wa sekondari. Aidha, masuala ya afya hufundishwa katika Somo la Biologia ambalo pia ni somo la lazima kwa wanafunzi wote wa Kidato cha kwanza mpaka cha nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na zoezi la kuboresha mitaala kwa ngazi za elimu ya awali, msingi na sekondari. Zoezi hilo linahusisha kupokea maoni ya wadau ambayo yatazingatiwa katika maboresho ili kuhakikisha mitaala yetu inakidhi mahitaji na inawajengea wanafunzi maadili ya Kitanzania. Ahsante sana.
MHE. ALLY Y. MHATA aliuliza: -

Je Serikali ina mpango gani wa kuyatumia majengo yaliyoachwa na Kampuni ya Ujenzi ya China yaliyopo Kijiji cha Maneme yatumike kama Chuo cha Ufundi (VETA)?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahaya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika Wilaya zote hapa nchini. Kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 29 ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majengo yaliyoachwa na mkandarasi aliyejenga barabara yapo na Wilaya imeona umuhimu wa kuyatumia, Wizara yangu itatuma wataalam kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) washirikiane na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu kufanya tathmini ya majengo hayo iwapo yanakidhi vigezo vya msingi vya kuanzisha mafunzo ya ufundi stadi.

Mheshimiwa Spika, wakati juhudi hizo zikiendelea, nashauri wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu kutumia Vyuo vya Ufundi Stadi vya Mtwara, Lindi na Namtumbo ambavyo vipo jirani na Wilaya hiyo.
MHE. JUMANNE A. SAGINI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Teknolojia na Kilimo, Butiama?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Jumanne Abdallah Sagini Mbunge wa Butiama kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza mchakato wa kukijenga Chuo Kikuu cha Teknolojia ya Kilimo cha Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Butiama. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imetenga Dola za Kimarekani Millioni 44.5, sawa na Shilingi za Kitanzania Bilioni 103 kupitia mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa ajili ya Elimu ya Juu uitwao Higher Education for Economic Transformation-HEET. Mradi wa HEET unatekelezwa kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikishirikiana na Benki ya Dunia kuanzia mwaka huu 2021 mwezi Septemba.

Mheshimiwa Spika, yapo baadhi ya maandalizi muhimu yaliyokamilika ambayo ni pamoja na: kupatikana kwa hati miliki ya eneo lenye ukubwa wa ekari 573.5; uandaaji wa mpango kabambe (master plan); tathmini ya athari ya mazingira (Environmental and Social Impact Assessment); na usanifu wa majengo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa taratibu zinazofuata ni kumtafuta mshauri mwelekezi, na atakapopatikana atafanya kazi ya mapitio ya michoro na kuandaa hadidu za rejea na makabrasha ya zabuni ili kutangaza na kumpata mkandarasi. Michakato hiyo itakapokamilika ujenzi huo utaanza rasmi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kulifanya somo la kilimo kuwa la lazima kuanzia ngazi ya elimu msingi mpaka chuo kikuu kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu na mchango mkubwa wa Kilimo katika maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, somo la kilimo linafundishwa katika ngazi zote za elimu hapa nchini. Kwa mfano, katika ngazi ya mtaala wa ngazi ya elimu ya msingi maarifa na stadi za kilimo zinafundishwa katika somo la stadi za kazi. Kwa upande wa Sekondari, somo la kilimo ni somo chaguzi na linasomwa na wanafunzi kuanzia kidato cha Kwanza hadi cha Sita.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inahuisha miongozo ya eimu ya kujitegemea kuanzia shule za msingi hadi vyuo vya ualimu. Miongozo hiyo imelenga kuziwezesha shule na vyuo vya ualimu kuanzisha na kusimamia kwa ufanisi miradi ya uzalishaji mali ikiwemo shughuli za kilimo na biashara. Elimu hiyo itamsaidia mwanafunzi kujifunza kwa vitendo stadi mbalimbali za maisha ikiwa ni pamoja na kilimo kwa lengo la kuwajengea misingi imara ya kujitegemea na kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa Wizara kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania inafanya mapitio ya mitaala ya ngazi zote za elimu msingi, suala hili litajadiliwa na kufanyiwa maamuzi stahiki. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -

Je, ni kwa nini Serikali isiingie makubaliano na Chuo cha Ufundi Lugarawa kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe kwa kupeleka Walimu, vifaa na fedha za ruzuku ili Wanaludewa na Wananjombe wapate mafunzo wakati ujenzi wa Chuo cha VETA Shaurimoyo ukisubiriwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Eilimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa haina utaratibu wa kushirikiana katika kutoa mafunzo kwa pamoja na taasisi binafsi. Hata hivyo, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na sekta binafsi, zikiwemo taasisi za dini katika utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha taasisi zake za elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kujenga vyuo katika ngazi za Wilaya na Mkoa na kuvipatia vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa lengo la kuhakikisha kwamba watanzania wanapata elimu bora ya ufundi karibu na maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Njombe, Serikali inamiliki Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Makete chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 160 kwa mwaka. Kwa sasa Serikali inaendelea kupanua Chuo hicho kwa kuongeza madarasa matano yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 100 kwa wakati mmoja, mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 72 kwa kila moja na nyumba mbili za watumishi, kila moja ikiwa na uwezo wa kubeba familia mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inaendelea na matayarisho kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Njombe kitakachojengwa katika Wilaya ya Ludewa kupitia fedha za IMF. Aidha, ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kuanza mwezi huu wa Novemba, 2021. Ahsante. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Handeni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwa na lengo la kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi katika kila ngazi ya Mkoa na Wilaya. Tangu mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga zaidi ya shilingi bilioni 76 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi 33, ambapo vyuo 29 ni vya ngazi ya Wilaya na vyuo vinne ni vya ngazi ya Mkoa. Mpaka sasa vyuo hivyo viko katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Handeni kuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Handeni ambacho pia kinatoa mafunzo ya ufundi stadi. Katika chuo hiki Serikali ilifanya ukarabati na ujenzi wa miundombinu uliogharimu jumla ya shilingi milioni 599.6 na kwa sasa Chuo kinaendelea kutoa mafunzo ya ufundi stadi.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA wilayani humo, nashauri wananchi wa Handeni kuendelea kutumia vyuo vilivyopo nchini, ikiwa ni pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi wa Handeni. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, ni upi mgawanyo wa vitabu 812 vya nukta nundu vilivyotolewa katika Mpango wa Fedha za Mapambano dhidi ya UVIKO 19?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nichukue fursa hii adhimu na adimu kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu alitupa kibali cha kukutana katika eneo hili kwa siku ya leo. Shukrani ya pili nimpelekee Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu, Mama Samia Suluhu Hasan kwa kuendelea kuniamini na kutuamini sisi, mimi na Profesa Mkenda kuweza kumsaidia katika eneo la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayasi na Teknolojia, kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vitabu vya Nukta Nundu kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wasioona kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi wasioona wapatao 514 wanaosoma katika shule za sekondari nchini, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ilitenga shilingi milioni 704 kwa ajili ya kuchapa jumla ya nakala 18,200 za vitabu kwa ajili ya wanafunzi wasioona vya masomo yote ya sekondari, ambapo nakala 9,100 ni vitabu vya nukta nundu na nakala 9,100 ni vitabu vya michoro.

Mheshimiwa Spika, uchapaji wa vitabu hivyo upo katika hatua za mwisho na utakapokamilika vitasambazwa katika mikoa yote kulingana na mahitaji. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika mikoa yote wakiwemo wanafunzi wasioona. Nakushukuru.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Stella Alex Ikupa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Lugha ya Alama katika kuondoa kikwazo cha mawasiliano kati ya wenye uziwi na wale wasio na uziwi. Katika kufikia lengo la kuingiza Lugha ya Alama kwenye Mitaala ya Elimu nchini, Serikali imekamilisha usanifishaji Kamusi ya Lugha ya Alama ya Tanzania ya mwaka 2020 na kurahisiha ufundishaji na ujifunzaji pamoja na mawasiliano. Vilevile, Serikali imekamilisha uandaaji wa Mwongozo wa Utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Sekondari kwa wanafunzi viziwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuandaa walimu wenye taaluma ya Elimu Maalum katika fani ya Uziwi na Lugha ya Alama kila mwaka. Aidha, Serikali inaendelea kupokea maoni ya wadau kuhusu uboreshaji wa mitaala ya elimu na mafunzo nchini ambapo suala la matumizi ya Lugha ya Alama katika mitaala hii litazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kuhakikisha vijana wote wanaoomba mikopo ya Elimu ya Juu wanapata mikopo hiyo kama walivyoomba?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kugharamia utoaji wa mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi wa Elimu ya Juu mhitaji anapata mkopo kwa ajili ya kugharamia masomo yake. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imekua ikiongeza fedha za bajeti ya mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kila mwaka. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu ikiwa ni ongezeko la bilioni 106 kutoka bilioni 464 ya mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ongezeko hilo la fedha za bajeti, wanufaika wa mikopo ya Elimu ya Juu wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo katika mwaka 2021/2022 wanafunzi wanufaika wa mikopo ya Elimu ya Juu walikua 176,617 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 27,228 kutoka wanafunzi 149,389 wa mwaka 2020/ 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuongeza fedha za mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kulingana na ongezeko la fedha katika bajeti yake ili kuhakikisha vijana wote wanaoomba mikopo ya Elimu ya Juu wanapata mikopo hiyo kama walivyoomba. Ahsante sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Vyuo Vikuu katika Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali huanzisha Vyuo Vikuu na kutoa vibali kwa watu na taasisi binafsi kuanzisha Vyuo Vikuu kwa lengo la kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kupata fursa ya kusoma Elimu ya Juu. Vyuo Vikuu vilivyopo hupokea wanafunzi kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara, Visiwani pamoja na wanafunzi kutoka nje ya nchi. Huo ndiyo utamaduni wa Vyuo Vikuu duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Songwe kuna Kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kilichopo katika Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe. Pia, kuna Kampasi ya Myunga ambayo ni Tawi la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) iliyopo katika Wilaya ya Momba. Hivyo, wananchi wanashauriwa kuendelea kuvitumia Vyuo hivyo na vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea na mpango wa kuboresha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia kwa lengo la kuongeza nafasi za udahili na ubora wa Elimu ili kukidhi mahitaji Kitaifa, Kikanda na Kimataifa. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudisha masomo ya ziada ya kazi za mikono kama vile useremala, upishi, ushonaji, kilimo na ujenzi katika shule za msingi na sekondari ili kupunguza changamoto ya ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufundisha masomo ya kazi za mikono kama vile Useremala, Upishi, Ushonaji, Kilimo na Ujenzi ili kuwajengea wanafunzi stadi mbalimbali za maisha zitakazowasaidia kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutilia mkazo masomo ya ziada ya kazi za mikono katika ngazi mbalimbali za elimu. Kwa mfano, katika ngazi ya Elimu ya Msingi, Stadi za Useremala, Upishi, Ushonaji, Kilimo na Ujenzi hufundishwa katika somo la Stadi za Kazi kuanzia Darasa la Tano. Pia, masomo ya ziada ya kazi za mikono yamekuwa yakifundishwa kama masuala mtambuka kupitia vilabu vya masomo. Katika ngazi ya sekondari, stadi na maarifa haya hufundishwa katika somo la Home Economics pamoja na masomo ya ufundi yakiwemo ya useremala na ujenzi. Vilevile, somo la Kilimo hufundishwa ngazi ya sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na mapitio ya mitaala ya elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali kwa lengo la kuboresha elimu na mafunzo yatolewayo ili yaweze kutoa stadi mbalimbali na kukidhi mahitaji ya jamii kwa maendeleo ya Taifa letu. Hivyo, nawaomba wadau mbalimbali wa elimu kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato huu kwa kutoa maoni na ushauri utakaosaidia kuboresha elimu yetu. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. JUDITH S. KAPINGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha COSTECH inapata fedha za kutosha kwa ajili ya kuwekeza katika STARTUP programu za vijana?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA aliuliza: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango wa STARTUP programu za vijana katika ubunifu na teknolojia kama nyenzo muhimu katika kuongeza tija na ubora katika uzalishaji wa bidhaa, utoaji wa huduma na kuzalisha ajira mpya kwa ajili ya vijana nchini.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inapata fedha za kutosha kwa ajili kuendeleza ubunifu na ubiasharishaji wa teknolojia ikiwemo kupitia STARTUP programu, mwaka 1995 Serikali ilianzisha Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia (MTUSATE).

Mheshimiwa Spika, kupitia Mfuko wa MTUSATE, kila mwaka Serikali hutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza ubunifu na matokeo ya utafiti unaofanywa nchini kwa lengo la kutatua changamoto zinazoikabili jamii. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi bilioni 3.5 zimetengwa kupitia mfuko huo. Vilevile kupitia utekelezaji wa Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu kwa ajili ya Mageuzi ya Kiuchumi COSTECH imetengewa shilingi bilioni 2.13 kwa ajili ya kutekeleza shughuli zake ikiwemo kujenga Mfumo wa Kielektroniki wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambao utawezesha kusajili watafiti, wabunifu, vifaa na miradi ya utafiti na ubunifu pamoja na teknolojia zinazozalishwa hapa nchini na zinazoingia kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, Serikali pia inashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha kwamba COSTECH inawezesha miundombinu ya ukuzaji ubunifu na ubiasharishaji wa teknolojia ikiwemo uanzishaji wa STARTUP za ubunifu na teknolojia. (Makofi)

Mheshsimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali isiweke utaratibu wa mafunzo ambao utahakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapangiwa moja kwa moja maeneo ya kwenda kujifunza badala ya utaratibu wa sasa wa mwanafunzi kutafuta mwenyewe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mitaala ya vyuo vikuu huwataka wanafunzi kukamilisha masomo kwa kufanya mafunzo kwa vitendo katika taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi. Utaratibu uliopo ni kwamba vyuo vikuu vinaainisha maeneo wanayokusudia kupeleka wanafunzi na kuomba nafasi za kufanyia mazoezi kwa vitendo. Baada ya maeneo ya kufanya mazoezi kwa vitendo kupatikana, vyuo huwapatia wanafunzi barua za kuwatambulisha kwenye taasisi husika ili waweze kupokelewa.

Mheshimiwa Spika, wanafunzi wana uhuru pia wa kutafuta maeneo ya kufanyia mafunzo kwa vitendo na kukijulisha chuo kwa taarifa rasmi. Baada ya wanafunzi kupata nafasi katika Taasisi husika vyuo huwapa barua za utambulisho ili waweze kupokelewa na kuendelea kufanya mafunzo kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa vyuo vikuu nchini kudumisha mahusiano na taasisi mbalimbali vikiwemo viwanda na kuwa na mikataba ya makubaliano ya kupeleka na kupokea wanafunzi kwenye mafunzo kwa vitendo. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Njika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kujenga Vyuo vya VETA katika Mikoa na Wilaya mbalimbali kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini. Kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 25 na Mikoa 4 ukiwemo Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Meatu na maeneo mengine, wananchi wa Meatu wanashauriwa kutumia Vyuo vya VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo jirani kwa ajili ya kupata elimu na mafunzo ya ufundi. Nakushukuru.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Malinyi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi n a Teknolojia naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Jimbo la Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa vyuo vya mafunzo na ufundi stadi katika Mikoa na Wilaya kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa sasa Serikali inakamilisha ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 25 na Mikoa minne nchini kwa lengo la kuwapatia vijana ujuzi katika fani mbalimbali utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Malinyi na maeneo mengine, wananchi wa Malinyi wanashauriwa kutumia Vyuo vya VETA vilivyopo katika Mkoa wa Morogoro ambavyo ni Mikumi, Dakawa, Kihonda, Ulanga pamoja na vyuo vingine vya VETA vilivyopo nchini kwa ajili ya kupata elimu na mafunzo ya ufundi. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE aliuliza: -

Je, tangu kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kuna changamoto gani katika kukuza na kuendeleza Mfuko wa Elimu ya Bodi ya Mikopo ili kukopesha wanafunzi wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kukuza na kuendeleza Mfuko wa Elimu ya Bodi ya Mikopo ili kukopesha wanafunzi wengi zaidi. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imekuwa ikiongeza fedha za bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kila mwaka. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 570 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 106 kutoka shilingi bilioni 464 ya mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo za Serikali, kumekuwepo na changamoto kadhaa katika kukuza na kuendeleza Mfuko wa Elimu ya Bodi ya Mikopo ambazo zinazotokana na mambo yafuatayo; jambo la kwanza baadhi ya wanufaika wa mikopo iliyoiva kutojitokeza na kurejesha kwa hiari mara baada ya kumaliza masomo. Lakini kambo la pili baadhi ya waajiri kutowasilisha kwa wakati orodha ya waajiriwa wapya ambao ni wanufaika wa mikopo na wengine kuchelewa kuwasilisha makato ya fedha kwa wakati kutokana na wanufaika ambao ni waajiriwa wao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo imeendelea kutoa elimu kwa wanufaika na waajiri ili kuhamasisha urejeshaji wa mikopo kwa hiari na kwa kuzingatia matakwa ya kisheria. Vilevile imeendelea kuimarisha kaguzi kwa waajiri pamoja na kuwashirikisha wadau wa kimkakati kama BRELA na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kubaini wanufaika wapya na kuongeza kasi ya urejeshaji mikopo iliyoiva kwa lengo la kukuza na kuendeleza Mfuko wa Elimu ya Bodi ya Mikopo ili kukopesha wanafunzi wengi zaidi. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa Chuo cha VETA unaoendelea Wilayani Mkinga utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kukamilika kwa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Mkinga pamoja na vyuo vingine ili viweze kutoa mafunzo yatakayowawezesha vijana wetu kujiajiri na kuajiriwa. Kwa sasa ujenzi wa Chuo hiki upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji ambapo ujenzi umefikia asilimia 95. Ujenzi wa Chuo hiki unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Disemba, 2022. Hivyo, Chuo hiki kinatarajiwa kuanza kutoa mafunzo ya muda mfupi kuanzia mwezi Oktoba, 2022 na mafunzo ya muda mrefu mwezi Januari, 2023. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaifanya elimu ya sekondari kuwa ya lazima?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 kwa lengo la kuiboresha elimu yetu ili iweze kukidhi mahitaji ya sasa na baadaye.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali ipo katika hatua ya kupokea na kuchambua maoni ya wadau kuhusu Sera ya Elimu, hivyo suala la elimu ya sekondari kuwa ya lazima itategemea maoni ya wadau na mahitaji ya wakati. Rasimu ya kwanza ya Sera ya Elimu inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2022. Nakushukuru.
MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza: -

Je, kwa takwimu ni wahitimu wangapi wa kada ya Ualimu wa masomo ya sayansi na hesabu hawajaajiriwa tangu mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Esther Nicholaus Matiko, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 2015 hadi 2022 jumla ya wahitimu 33,492 wa kada ya Ualimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati wamehitimu mafunzo katika Vyuo mbalimbali vya Ualimu na Vyuo Vikuu. Kati yao wahitimu 13,383 wameajiriwa katika shule mbalimbali nchini tangu mwaka 2015. Aidha, wahitimu 20,109 hawajaajiriwa katika shule za Serikali.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuajiri ili kukidhi mahitaji ya Walimu katika shule za umma. Nakushukuru sana.
MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK aliuliza: -

Je, kuna Wavumbuzi wangapi na wa teknolojia gani kwani Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa una lengo la kuchochea uvumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Amour Khamis Mbarouk, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mchango wa uvumbuzi na ubunifu kama nyenzo muhimu katika kuchochea ushindani na uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya watu kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuibua, kutambua na kuendeleza uvumbuzi, ubunifu na maarifa asili ya Tanzania kupitia mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) na programu ya kutambua teknolojia zinazozalishwa ndani ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Serikali imetambua wavumbuzi na wabunifu wapatao 2,735 katika sekta za Afya, Viwanda, Elimu, Kilimo, TEHAMA, Usafirishaji, Nishati, Madini, Mazingira, na Uvuvi. Aidha, Teknolojia 479 zimeweza kuibuliwa, kutambuliwa na kuhakikiwa. Wabunifu 376 wanaendelezwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Kati ya bunifu zilizoendelezwa, 35 zimefikia hatua za ubiasharishaji. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI aliuliza: -

Je, kwa nini darasa la saba wanafanya mtihani wa Taifa mwezi Septemba, wakati mtaala unaelekeza masomo yakamilike mwisho wa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala wa elimu unaelekeza mwanafunzi kutumia siku 194 za mwaka kwa masomo. Aidha, mtaala wa elimu pamoja na masuala mengine umezingatia muda wa kufanyika kwa mitihani ya ndani na ile ya Kitaifa. Hivyo, kukamilika kwa ufundishaji na ujifunzaji wa maudhui ya muhtasari kwa darasa la saba hutegemea zaidi mpango kazi wa Mwalimu. Kwa msingi huo, hadi kufika mwezi wa Septemba walimu wa darasa la saba hupaswa kuwa wamekamilisha kufundisha mada zilizobainishwa katika muhtasari ili kutoa nafasi ya ufanyikaji wa mitihani ya Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanyikaji wa mitihani ya kitaifa ya darasa la saba mwezi Septemba unasaidia kutoa nafasi kwa zoezi la usahihishaji na utoaji wa matokeo kwa wakati ili kutoa nafasi kwa wazazi na walezi kufanya maandalizi ya kuwawezesha watoto wao kujiunga na masomo ya ngazi nyingine za elimu ambapo masomo yanaanza Januari mwaka unaofuata. Ninakushukuru.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali kueneza matumizi ya TEHAMA katika kufundisha ili kuwaokoa walimu na matatizo ya mgongo na shingo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji kuanzia mwaka 2019/2020, Serikali kupitia Programu ya Kuimarisha Mafunzo ya Elimu ya Ualimu (TESP) imeendelea kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa Vyuo vya Ualimu kuhusu matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika mwaka 2021/2022 Serikali kupitia Programu ya Mafunzo Endelevu kwa Walimu Kazini (MEWAKA) imewezesha mafunzo kwa walimu wa Shule za Msingi 30,400 yanayohusu matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kugawa vishikwambi vilivyotumika katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi mwezi Agosti, 2022 kwa walimu wote nchini kwa lengo la kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji. Nakushukuru sana.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -

Je, wanafunzi wangapi kutoka Zanzibar wamepata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2020/2021?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Omar Ali Omar, Mbunge wa Wete kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wote wa Kitanzania wenye uhitaji bila kuangalia mwombaji anatoka upande upi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, takwimu za mwaka 2020/2021 zinaonesha kuwa wanafunzi Watanzania wapatao 1,492 wanaosoma katika taasisi sita za elimu ya juu zilizopo Zanzibar walipangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 5.3. Aidha, kwa mwaka 2021/2022 jumla ya wanafunzi wa Tanzania 1,929 wanaosoma katika taasisi za elimu ya juu Zanzibar walipangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 5.8. Nakushukuru.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilayani Kalambo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Jimbo la Kalambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo, kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, Kalambo ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi katika mwaka huu wa fedha. Nakushukuru sana.
MHE. GEOFFREY I. MWAMBE aliuliza: -

Je ni lini serikali itajenga Chuo cha Ualimu Masasi baada ya Chuo cha Ualimu Ndwika kuwa shule ya Sekondari ya Wasichana?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Geoffrey Idelphonce Mwambe, Mbunge Jimbo la Masasi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilibadili Chuo cha Ualimu Ndwika kuwa Shule ya Sekondari ya Wasichana kutokana na mahitaji ya wakati huo. Kwa sasa Serikali ina vyuo 35 vya Ualimu vyenye uwezo wa kudahili wanachuo 25,054 ambapo hadi sasa jumla ya wanachuo 22,085 wamesajiliwa. Idadi hii ni chini ya uwezo wa vyuo hivyo katika udahili kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeelekeza nguvu katika ukarabati wa vyuo hivyo ili kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji na ujifunzaji. Aidha, Serikali itaendelea kujenga Vyuo vya Ualimu katika maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji na rasilimali.
MHE. ESTHER L. MIDIMU K.n.y. MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilayani Busega?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo, kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, Busega ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa vyuo vya ufundi stadi katika mwaka huu wa fedha. Nakushukuru sana.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilayani Tunduru?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo, kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, Tunduru ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa vyuo vya ufundi stadi katika mwaka huu wa fedha. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa vibali kwa Vyuo Vikuu vyenye upungufu wa Wahadhiri ili viweze kuajiri Wahadhiri wapya?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Paulina Daniel Nahato Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya upungufu wa Wahadhiri katika Vyuo Vikuu vya Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekua ikitoa vibali vya ajira kila mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2018/ 2019 hadi 2020/2021, Serikali ilitoa vibali vya nafasi za ajira mpya za Wakufunzi na Wahadhiri Wasaidizi 333 katika Vyuo Vikuu vya Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa Wahadhiri Vyuoni, Wizara yangu inaendelea na jitihada za kuomba vibali vya ajira za Wahadhiri kutoka Wizara yenye dhamana na Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Sambamba na hilo, pia upo utaratibu wa kuwahamisha watumishi wenye sifa kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali kwenda Vyuo Vikuu na kuwajengea uwezo ikiwa ni pamoja na kuwasomesha kozi za muda mfupi na mrefu. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, ni Vyuo Vikuu vingapi vimepewa fursa ya kuajiri watumishi wake?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Vyuo Vikuu kama zilivyo taasisi nyingine za Umma huajiri watumishi baada ya kupata vibali vya ajira kutoka Wizara yenye dhamana na Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jumla ya Vyuo Vikuu vya Umma 13 kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2018-2019 mpaka 2020/2021) vilipata vibali vya kuajiri watumishi 618 ambapo wanataaluma ni 333 na waendeshaji ni 285.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na fursa hizo za kuajiri watumishi zilizotolewa, bado Serikali inaendelea na taratibu za kuwahamisha watumishi wenye sifa kutoka sehemu mbalimbali kujiunga na utumishi katika Vyuo Vikuu. Aidha, Serikali itaendelea kutoa vibali vya ajira katika Vyuo Vikuu kwa lengo la kuviongezea fursa ya kuajiri watumishi kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani Vyuo vya Serikali vimejiandaa kupokea wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatanyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) inatarajia kuongeza fursa za wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi katika Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu kwa kujenga na kukaratabati miundombinu kama ifuatavyo: ujenzi wa maabara na karakana za kufundishia 108; vyumba vya mihadhara na madarasa 130; kumbi za mikutano ya kisayansi 23; mabweni 34; miundombinu ya shambani na vituo atamizi 10 kwa ajili ya kuendeleza ubunifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma programu za Sayansi kutoka wanafunzi 40,000 kwa mwaka 2020 hadi kufikia 106,000 mwaka 2026. Aidha, mradi huu pamoja na kuboresha mitaala zaidi ya 290 pia utasomesha wahadhiri 831 katika programu za kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, kwa mwaka wa masomo 2022/2023, Serikali kupitia Samia Scholarship imetoa ufadhili wa asilimia 100 kwa wanafunzi 640 wenye ufaulu wa juu waliodahiliwa katika Vyuo Vikuu kusoma Programu za Sayansi, Teknolojia, Hisabati na Tiba.

Mheshimiwa Saibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawalipa Wahadhiri wote nchini malimbikizo yao ya miaka ya nyuma?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Paulina Daniel Nahato, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali hulipa malimbikizo ya watumishi wote wa Serikali wakiwemo Wahadhiri baada ya kujaza fomu za malimbikizo (arrears clearance forms). Mara baada ya mtumishi kukamilisha kujaza fomu hizo na kuwasilishwa, madai yao hupelekwa Ofisi ya Rais, Management ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na baadaye Hazina kwa ajili ya malipo.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Septemba, 2022, Serikali imelipa jumla ya Sh.1,172,429,710 kwa ajili ya malimbikizo ya Wahadhiri. Serikali itaendelea kulipa malimbikizo ya Wahadhiri kulingana na bajeti ya fedha kwa mwezi na mwaka husika.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Ndaki ya Sayansi ya Afya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mamlaka ya Mji wa Mbalizi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali na Mheshimiwa Oran Manase Njeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanza hatua za awali kwa kuwasilisha kwa Msajili wa Hazina maombi ya kupewa ardhi yenye ukubwa wa hekari 2000 kwenye eneo lililokuwa shamba la Tanganyika Packers kwa ajili ya ujenzi. Kwa sasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaendelea kufuatilia maombi haya kwa Msajili wa Hazina.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Ndaki ya Sayansi ya Afya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam - Mbalizi utaanza mara moja pale upatikanaji wa ardhi utakapokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. HUSSEIN N. AMAR aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Nyangh’wale?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Nassor Amar, Mbunge wa Jimbo la Nyangh’wale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo. Kiasi hiki kitatumika pia katika ujenzi wa Chuo cha VETA katika Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nyangh’wale ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi kwa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafungua tawi la Chuo Kikuu cha Sokoine Wilayani Tunduru kwani majengo yamekamilika kwa asilimia 65?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, kilikabidhiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru majengo na ardhi kwenye eneo lililokuwa Kambi ya Mkandarasi wa ujenzi wa barabara katika Kijiji cha Darajambili tarehe 17 Agosti, 2018.

Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilianza kutumia majengo ya kampasi ya Tunduru kama kituo cha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Usimamizi wa Wanyamapori na Wanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Misitu mwaka, 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na mpango wa kufanya ukarabati wa miundombinu na kuanzisha shughuli mbalimbali za kitaaluma, utafiti na ushauri wa kitaalam kwa lengo la kuiwezesha kampasi hiyo kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.(Makofi)
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza: -

Je, ni wanafunzi wangapi waliokuwa wajawazito na wangapi wamerejeshwa shuleni baada ya agizo la Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2021/2022 wanafunzi wa shule za msingi waliopata ujauzito ni 1,554 na sekondari ni 7,457.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Januari, 2023 wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu ya ujauzito na kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari ni 1,692. Aidha, kwa upande wa shule za msingi Serikali inaendelea kukusanya taarifa za wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu ya ujauzito. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kusaidia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Uvuvi na Usafiri Baharini Lindi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimwa Hamida Mohamed Abdhallah, Mbunge wa Lindi Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuongeza idadi ya vyuo vikuu kulingana na uhitaji na upatikanaji wa rasilimali fedha. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) imetenga shilingi bilioni 5.8 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kampasi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mkoa wa Lindi. Kampasi hiyo itakuwa mahususi kwa ajili ya kozi za Ufugaji wa Nyuki, Kilimo-Uchumi na Biashara, Sayansi na Teknolojia ya Chakula, na Uhandisi Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tayari kinatoa kozi za Uvuvi katika Shule Kuu ya Akua na Teknolojia ya Uvuvi - Kunduchi na kozi za Sayansi ya Bahari katika Taasisi ya Sayansi ya Bahari Zanzibar, Serikali itafanya tathmini ili kuona kama kuna uhitaji wa kuongeza kozi za Uvuvi na Usafiri wa Baharini katika kampasi mpya ya Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwajengea uwezo Wahitimu wa Vyuo nchini ili waweze kushindana katika soko la ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ujulikanao kama, Higher Education for Economic Transformation (HEET), inaendelea na maandalizi ya uboreshaji wa mitaala iliyopo na uandaaji wa mitaala mipya zaidi ya 290 katika programu za kipaumbele cha Taifa ili kuwajengea uwezo wahitimu kuhimili ushidani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua inayoendelea ni ukusanyaji wa maoni (tracer study and needs assessment) kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kubaini mahitaji halisi. Mitaala hiyo iliyoboreshwa inatarajiwa kuanza kutumika katika mwaka wa masomo 2023/2024, nakushukuru.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya masomo ya dini kutokuwa principal pass ya kujiunga na Stashahada na Shahada?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu wa uendeshaji wa elimu ya Chuo Kikuu hapa nchini na katika nchi nyingine duniani, Mabaraza ya Vyuo Vikuu (Seneti) yamepewa mamlaka ya kisheria kuweka vigezo mahsusi vya udahili kwa kila programu ya masomo kwa ngazi husika (Specific Program Requirements).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hapa nchini, principal passes za masomo ya dini zinatambuliwa kama vigezo mahsusi vya kujiunga na baadhi ya program za masomo kwa ngazi ya Stashahada na Shahada ya kwanza. Mfano, baadhi ya Vyuo Vikuu ambavyo vimekuwa vikitumia masomo ya dini kama kigezo kimojawapo cha kujiunga na program za masomo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro; Chuo Kikuu cha Zanzibar; Chuo Kikuu cha Arusha; Chuo Kikuu cha Mt. Yohana cha Tanzania; Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi; Chuo Kikuu Huria cha Tanzania; Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo. Kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kahama ni miongoni mwa Wilaya zitakazojengewa Vyuo vya VETA ambapo kwa sasa Serikali ipo katika hatua za maandalizi ya ujenzi. Hivyo wananchi wa Jimbo la Ushetu watanufaika na Chuo cha VETA cha Wilaya ya Kahama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI aliuliza: -

Je, ni lini Chuo cha VETA Ukerewe kitaanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi, Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA Ukerewe ili kiweze kutoa mafunzo yatakayowezesha vijana kujiajiri na kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa chuo hiki upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji ambapo ujenzi umefikia asilimia 97. Aidha, tayari Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hiki ili kianze kutoa mafunzo ya muda mfupi ifikapo mwezi Aprili, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza: -

Je, ni chombo gani kinadhibiti vyuo binafsi vinavyodahili walimu nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule ndiyo yenye jukumu la kuthibiti ubora wa elimu inayotolewa katika vyuo vya ualimu vya binafsi nchini. Mamlaka haya ni kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 kifungu cha 25 na marekebisho yake kifungu cha 10 cha mwaka 1995.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vyuo vikuu binafsi vinavyodahili walimu nchini, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ndio chombo chenye mamlaka ya kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa katika vyuo hivyo. Mamlaka haya ni kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura Na. 346 ya Sheria za Tanzania, nakushukuru.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA Wilayani Serengeti ili vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari wapate ujuzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo. Kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe. Serengeti ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeshakamilisha maandalizi ya awali ikiwemo upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi pamoja na kuandaa michoro na makadirio ya gharama za ujenzi kwa kila chuo na ujenzi huo unatarajiwa kuanza mara tu taratibu za manunuzi zitakapokamilika, nashukuru sana.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Chuo cha VETA katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo, kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe. Busega ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeshakamilisha maandalizi ya awali ikiwemo upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi pamoja na kuandaa michoro na makadirio ya gharama za ujenzi kwa kila chuo na ujenzi huo unatarajiwa kuanza mara tu taratibu za manunuzi zitakapokamilika, nakushukuru sana.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri haya majibu yanataja Mkoa wa Songwe na lile lililopita pia Mkoa wa Songwe una kitu special huu Mkoa wa Songwe?

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, katika mikoa 26 ya Tanzania Bara ni Mkoa wa Songwe peke yake ndio ambao haujajengewa Chuo cha VETA cha mkoa. Kwa hiyo ni lazima tuutaje kwa sababu ni mkoa pekee ambao hauna na katika mwaka huu wa fedha tumeuweka kwenye mpango na tutakwenda kujenga katika Mkoa wa Songwe. (Makofi)
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga majengo ya Wizara ya Elimu Zanzibar ili kutoa huduma kwa wakati na kupunguza gharama za kukodi Ofisi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge Chumbuni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Zanzibar kuna Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, yenye majengo yake, ambayo ina Idara ya Elimu ya Juu inayoongozwa na Mkurugenzi kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanafunzi wa elimu ya juu wanapata huduma. Vilevile, zipo Taasisi za Elimu ya Juu zinazotoa huduma kwa wanafunzi kama vile; Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume, Taasisi ya Sayansi ya Bahari (IMS) na Tume ya Taifa Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga ofisi katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa kila Taasisi ya Umma inakuwa na majengo yake kwa lengo la kupunguza gharama za kukodi ofisi. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA K.n.y. MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, lini Serikali itafupisha muda wa miaka saba kwa elimu ya msingi na sita ya sekondari ili kupunguza muda kwa wanafunzi wenye uwezo mkubwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la miaka inayotumika kumuandaa mhitimu wa elimu ya msingi na sekondari hutegemea kiasi cha maudhui yanayotakiwa kujengwa ili kumuwezesha mhitimu kupata stadi na ujuzi unaohitajika kulingana na mahitaji ya wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua uwepo wa wanafunzi wenye uwezo tofauti katika kujifunza mwaka 2019 ilitoa mwongozo kuhusu utaratibu wa kurusha darasa wanafunzi wa elimu ya msingi. Mwongozo huo unatoa utaratibu unaopaswa kufuatwa na uongozi wa shule kwa kushirikiana na mzazi wa mtoto husika katika kumrusha darasa mwanafunzi anayeonekana kuwa na uwezo mkubwa darasani. Aidha, baada ya kufanyika kwa tathmini ya utekelezaji wa mwongozo huo Serikali itaona namna ya kuendelea na utaratibu huo kwa ngazi nyingine za elimu. Nakushukuru sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA - K.n.y MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Magu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Bonivetura Destery Kiswaga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuwezesha upatikanaji wa fursa za ujuzi na stadi mbalimbali za maisha kupitia elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi katika Mikoa na Wilaya zote nchini. Kutokana na nia hiyo, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi wa Vyuo vya VETA kwa awamu katika Mikoa na Wilaya mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Magu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Magu na maeneo mengine, wananchi wa Magu wanashauriwa kutumia Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Mwanza pamoja na Vyuo vingine vya VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo jirani kwa ajili ya kupata elimu na mafunzo ya ufundi. Ninakushukuru sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je ni lini Serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo vya Kati nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu Swali la Mheshiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa elimu ya kati katika maendeleo ya nchi, Serikali imeendelea kugharamia uendeshaji wa vyuo vya kati kupitia ruzuku ambapo kwa mwaka 2022/2023, imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 41.47 kwa wanafunzi 2,435 waliopo katika vyuo vya kati wanaosoma fani za sayansi na ufundi. Aidha, Serikali inakamilisha taratibu za kuwezesha mikopo kutolewa kwa ajili ya elimu ya kati.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, hali ya upatikanaji wa vitabu vya kufundishia na kujifunza katika shule za msingi na sekondari ipoje?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge Wa Newala Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha uandishi, uchapaji na usambazaji wa vitabu vya kiada na viongozi vya mwalimu kwa masomo yote ya elimu ya awali na msingi darasa la I – VII. Vitabu hivyo ni pamoja na vitabu vya kiada vilivyotafsiriwa kwa ajili ya shule zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia. Vitabu vya kiada vya wanafunzi walio nje ya mfumo rasmi (Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa – MEMKWA), vitabu vya kiada vya breli kwa wanafunzi wasioona na vitabu vilivyokuzwa maandishi kwa ajili ya wanafunzi wenye uoni hafifu. Aidha, imekamilisha kuandika, kuchapa na kusambaza jumla ya vitabu vya kiada vya masomo 171 kati ya 183 ya sekondari ikiwemo vitabu vya masomo ya sayansi, hisabati, sanaa, lugha, biashara, kilimo, michezo, muziki na vitabu vya ufundi ambavyo vipo hatua ya uchapaji. Vitabu 12 vilivyobaki ni vya masomo chaguzi (optional subjects) ikiwemo Kichina ambavyo vinatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2023.

Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada hizo, hali ya upatikanaji wa vitabu, kwa shule za msingi na sekondari imefikia uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani kukomesha kuvuja kwa mitihani nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kwa lengo la kukomesha tabia ya udanganyifu katika mitihani ya Taifa ikiwemo mitihani ya kumaliza elimu ya msingi, sekondari na vyuo. Hatua hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa walimu, wasimamizi wa mitihani na wadau wote wa elimu kuhusu athari za udanganyifu katika mitihani ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza jukumu la usimamizi wa mitihani hiyo kwa uadilifu na kwa kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa kwa ajili ya uendeshaji wa mitihani.

Mheshimiwa Spika, hatua nyingine zilizochukuliwa kutokana na udanganyifu katika mitihani ni hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria za nchi. Hatua hizi zimekuwa zikichukuliwa kwa Walimu, wasimamizi na wadau wote wanaohusika katika kusimamia mitihani pale ambapo ilibainika pasina shaka kuwa walishiriki katika kosa hilo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria wahusika wote wanaojihusisha na udanganyifu wa mitihani ili kuhakikisha kuwa nchi inapata wataalam wenye sifa stahiki. Nakushukuru sana.
MHE. ROBERT C. MABOTO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Halmashauri ya Mji Bunda?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Robert Chacha Maboto, Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi za Kitanzania Bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Bunda ni miongoni mwa Wilaya 64 ambazo zipo katika mpango wa kuanza kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi katika mwaka huu wa fedha ambapo tayari kiasi cha Shilingi Milioni 45 kimetolewa mwezi Machi, 2023 kwa ajili ya shughuli za awali ikiwemo upimaji wa udongo kwa ajili ya uhimilivu pamoja na tathmini ya athari za mazingira na jamii wakati wa ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. SYLVIA F. SIGULA aliuliza: -

Je, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mahitaji ya sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sylvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea na mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, sambamba na mapitio ya Mitaala ya Elimu katika ngazi zote.

Mabadiliko haya ya Sera na Mitaala yamelenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za kazi, stadi za maisha za karne ya 21 ambazo ni fikra tunduizi, ubunifu, ushirikiano, uongozi pamoja na stadi za mawasiliano na teknolojia ya habari kwa lengo la kuwajengea uwezo wahitimu kukabiliana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali upande wa Vyuo vya Kati na Vyuo vya Ufundi Stadi, Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTVET) linaendelea na maandalizi ya Occupational/Professional Standards ambazo zitatoa mwogozo katika mabadiliko na maandalizi ya mitaala inayokidhi mahitaji ya sasa na baadae. Vilevile, kwa upande wa Elimu ya Juu tayari Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) inaendelea kukusanya maoni ya wadau kuhusu ubora wa elimu inayotolewa na Vyuo Vikuu pamoja na kutoa mafunzo kwa Wahadhiri katika maandalizi ya mitaala inayozingatia mahitaji ya ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA K.n.y. MHE. KABULA E. SHITOBELA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti matukio ya ubakaji na ulawiti katika shule za bweni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Kabula Enock Shitobela Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sehemu ya kudhibiti matukio ya ubakaji na ulawiti kwa wanafunzi, Serikali imetoa Waraka wa Elimu namba 11 wa mwaka 2002 kuhusu malezi, unasihi na ulinzi wa mtoto ambapo Waraka unaelekeza kila shule na chuo cha ualimu kuanzisha huduma za malezi na ushauri nasaha kwa wanafunzi. Katika utekelezaji wa Waraka huo Serikali imewezesha mafunzo kwa walimu wawili wa ushauri na unasihi kwa kila shule pamoja na kuanzisha dawati la ulinzi na usalama wa mtoto shuleni kwa lengo la kutoa fursa kwa wanafunzi kuzungumza na kuripoti vitendo vya unyanyasaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia imetoa Waraka wa Elimu namba mbili wa mwaka 2023 kuhusu utoaji wa huduma ya bweni kwa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi ambapo waraka huu unaelekeza kuwa huduma ya bweni itolewe kwa wanafunzi kuanzia darasa la tano na kuendelea. Hatua hii imezingatia ukweli kuwa wanafunzi wa umri huo walau wana upeo wa kutambua baya na zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ni kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa mtoto dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wawapo shuleni na majumbani pia.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuwa na Chuo cha VETA katika kila Jimbo ili kuwakomboa vijana na tatizo la ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, azma ya Serikali ni kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo. Kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe ambao hauna chuo cha ngazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, Serikali inaendelea kutekeleza azma hiyo na ikishakamilisha ujenzi wa VETA katika kila Wilaya itaangalia uwezekano wa kuanza kujenga vyuo hivyo katika Majimbo kulingana na uhitaji na upatikanaji wa fedha. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA K.n.y. MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuondoa tofauti ya Viwango vya Ufaulu kwa Mitihani ya Kidato cha Nne na Sita Kati ya Bara na Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Said Issa, Mbunge wa Konde kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchambuzi wa jumla wa matokeo ya mitihani ya Kidato cha Nne na Sita uliofanywa na Baraza la Mitihani la Tanzania katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2022 ulibainisha kuwa Zanzibar ilikuwa na ufaulu wa juu zaidi kwa kidato cha nne na sita kuliko Tanzania Bara katika mwaka 2013, 2015 na 2016. Aidha, Tanzania Bara ilikuwa na ufaulu wa juu zaidi ya Zanzibar kwa mwaka 2014 na mwaka 2017 hadi 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi na uendeshaji wa elimu ya msingi (awali, msingi na sekondari) siyo suala la Muungano, ingawa kwa Kidato cha Nne na cha Sita wote wanafanya mtihani mmoja wa Baraza la Mitihani la Tanzania. Kwa msingi huo, kila upande wa Muungano una mikakati yake ya namna ya kuongeza kiwango cha ufaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea na mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu. Zoezi hili linafanyika kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha kuwa tunakuwa na Sera na Mitaala inayolenga kutoa ujuzi zaidi kwa wahitimu na pia tunaoanisha kwa kiwango kikubwa elimu inayotolewa Tanzania Bara na ile inakayotolewa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA K.n.y. MHE. SHANIF J. MANSOOR aliuliza: -

Je, ni lini Chuo cha VETA Ngudu Kwimba kitakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shanif Jamal Mansoor, Mbunge wa Jimbo la Kwimba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa vyuo vya VETA Nchini. Kwa sasa inakamilisha hatua ya uwekaji wa samani pamoja na kuandaa rasilimaliwatu kwa lengo la kuviwezesha vyuo vya VETA ikiwemo Chuo cha Ngudu kuanza kutoa mafunzo kwa mwaka wa masomo 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Chuo cha VETA Ngudu upo katika hatua ya ukamilishaji na umefikia asilimia 97. Aidha, Wizara kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeshapeleka kiasi cha shilingi 189,607,486.00 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa chuo hicho, nakushukuru.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali isiagize kuwe na madereva na kondakta wa jinsia zote kwenye mabasi ya shule ili kudhibiti vitendo vya ubakaji?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Waraka wa Elimu Na. 1 wa Mwaka 2023 imetoa maelekezo kwa wamiliki wote wa shule zinazotoa huduma ya usafiri kwa wanafunzi kuhakikisha kuwa wanakuwa na mhudumu wa kike na wa kiume katika kila basi au gari linalosafirisha wanafunzi kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Waraka huo, Wizara ilikutana na wadau wa elimu kujadiliana namna bora ya kutekeleza Waraka tajwa na tulikubaliana kwamba deadline ya kutekelezwa imefutwa. Hivyo, wadau wote wanatakiwa kujitahidi kutekeleza Waraka huo na kabla ya kupanga deadline nyingine tutapanga kikao na wadau wote kujadiliana namna ya utekelezaji. Kwa sasa tunahimiza kwamba, mabasi yote ya wanafunzi yawe na watumishi au wahudumu wa jinsia zote. Ninakushukuru sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilayani Kilombero baada ya wanachi kutenga eneo la hekari 30?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Ni azma ya Serikali kujenga chuo cha ufundi stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2203, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kilombero eneo lililotengwa kujengwa chuo cha ufundi stadi ni katika Kijiji cha Nakaguru Kata ya Mchombe. Aidha, tayari kiasi cha shilingi million 45 kimetolewa mwezi Machi, 2023 kwa ajili ya shughuli za awali za ujenzi wa chuo hicho.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza: -

Je lini Serikali itaanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya kada ya kati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na taratibu za maandalizi ya kuwezesha utoaji wa mikopo kwa elimu ya kati ikiwemo utafutaji wa vyanzo endelevu vya ugharamiaji wa elimu na mafunzo nchini. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa elimu ya kati katika maendeleo ya nchi, Serikali imeendelea kugharamia uendeshaji wa vyuo vya kati kupitia ruzuku ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 41.47 kwa wanafunzi 2,435 waliopo katika vyuo vya kati wanaosoma fani za sayansi na ufundi.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa vyuo vikuu vyenye taaluma ya sayansi na tiba vinakuwa na hospitali za kufundishia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKINOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara Mbunge wa Viti Maalaum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaala ya Mafunzo ya Sayansi ya Utabibu (Medical and Health Training) vyuoni hutekelezwa kwa mafunzo ya nadharia na vitendo ambavyo hufanyika katika hospitali zenye wagonjwa halisi. Kwa vyuo ambavyo havina hospitali za mafunzo kwa vitendo, upo utaratibu wa makubaliano kati ya vyuo na hospitali za rufaa, mikoa, wilaya pamoja hospitali za watu binafsi zenye kukidhi vigezo kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wanaosoma katika vyuo hivyo kufanya mafunzo kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vikuu vyenye taaluma ya sayansi na tiba kuwa na hospitali za kufundishia; ambapo kwa sasa inaendelea na ujenzi wa Hosipitali ya Mloganzila kama hospitali ya kufundishia ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili. Aidha, Serikali itaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha kwa ajili ya kujenga hospitali za kufundishia katika vyuo vikuu vingine vyenye taaluma ya sayansi na tiba ambavyo havina hospitali hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA K.n.y. MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga chuo cha VETA Wilaya ya Buchosa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Sengerema eneo lililotengwa kujengwa Chuo cha Ufundi Stadi ni katika Kijiji cha Kayenze Kata ya Nyehunge na tayari kiasi cha shilingi million 45 kimetolewa mwezi Machi, 2023 kwa ajili ya shughuli za awali za ujenzi wa chuo hicho, nashukuru.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge Viti Maalum kutoka Iringa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga chuo cha ufundi stadi katika kila mkoa na wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga vyuo vya ufundi stadi katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Kilolo eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha ufundi stadi ni katika Kijiji cha Luhindo Kata ya Mtitu. Aidha, pamoja na kiasi cha shilingi milioni 45 kilichotolewa awali kwa ajili ya shughuli za maandalizi, tayari Serikali imetuma kiasi cha shilingi milioni 228 kwa kila chuo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ESTHER E. MALLEKO aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha Uwanja wa Ushirika Moshi ili kukuza utalii wa michezo nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Maleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kinamiliki viwanja mbalimbali vya michezo ambavyo ni uwanja wa mpira wa miguu, pete, wavu, kikapu na riadha. Viwanja hivyo ni miongoni mwa miundombinu iliyojengwa na Serikali ili kuendeleza michezo na burudani kwa jumuiya ya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na wadau wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa viwanja hivyo vipo katika hali nzuri na vinaendelea kutumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa. Aidha, Chuo kina utaratibu wa kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa viwanja hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: -

Je, ni lini majengo yataongezwa katika Chuo cha VETA Urambo ili kuongeza fani ambazo hazitolewi kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza baadhi ya majengo yanayokosekana katika Chuo cha VETA cha Urambo ili kuimarisha uwezo na ufanisi wa kutoa mafunzo kwa wananchi wa Urambo yatakayowawezesha kupata ujuzi na kutekeleza shughuli zao za kiuchumi kwa weledi na viwango stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetenga fedha kiasi cha shilingi 880,719,315.39 kwa ajili ya kukiimarisha Chuo cha VETA cha Wilaya ya Urambo. Fedha hizi zitatumika katika ujenzi wa miundombinu ya jiko, bwalo la chakula, madarasa na majengo mawili ya karakana. Aidha, ujenzi wa majengo hayo umeanza mwezi Mei, 2023.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha masomo yatakayoibua vipaji vya watoto kuanzia shule za msingi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa masomo yanayoibua vipaji vya watoto kuanzia ngazi ya elimu ya msingi. Kwa kuliona hilo Wizara ilianzisha somo la sayansi na teknolojia kuanzia darasa la tatu; stadi za kazi pamoja na sanaa na michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masomo hayo mada mbalimbali zinazochochea vipaji zinafundishwa. Kwa mfano katika somo la stadi za kazi wanafunzi hujifunza muziki, uigizaji, ufinyanzi na ususi. Katika somo la michezo na sanaa wanafunzi hujifunza michezo sahili, michezo ya jadi, riadha na mpira. Aidha kwa upande wa somo la sayansi na teknolojia wanafunzi hujifunza matumizi ya nishati, majaribio ya kisayansi, mashine na kazi na kuelea na kuzama kwa vitu.

Aidha, Wizara imetoa mwongozo wa ubainishaji na utambuzi wa wanafunzi wenye vipawa na vipaji wa mwaka 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali kwa sasa inaendelea na mapitio ya mitaala ikiwemo Mtaala wa Elimu ya Msingi ambapo ushauri wa Mheshimiwa Mbunge utazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga campus ya Chuo Kikuu Mzumbe katika Mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wa kupeleka huduma ya elimu ya juu katika mikoa isiyokuwa na Chuo Kikuu au Taasisi ya Elimu ya Juu ukiwemo Mkoa wa Singida. Kwa sasa Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economics Transformation (HEET) imetenga jumla ya Dola za Kimarekani milioni nane kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Kampasi ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) katika Mkoa wa Singida. Maandalizi ya shughuli za ujenzi yameshaanza ambapo hadidu za rejea za kumpata Mshauri Elekezi na Mkandarasi, Michoro na Mpango kabambe wa Ripoti ya Tathmini ya mazingira na Jamii (Environmental and Social Impact Assessment) vimeshaanza kuandaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada hizo za kusogeza elimu ya juu kwenda mikoa ambayo haina taasisi hizo, Chuo Kikuu cha Mzumbe pia kupitia mradi wa HEET kimepangiwa kujenga kampasi mpya katika Mkoa wa Tanga katika Wilaya ya Mkinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Aliuliza: -

Je, kwa nini kumekuwa na ugumu wa upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi waliosoma shule binafsi wanapojiunga na elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Spika, mikopo inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inawalenga vijana wenye sifa za kitaaluma za kujiunga na taasisi za elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kumudu gharama za elimu.

Mheshimwa Spika, aidha, upangaji na utoaji mikopo unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo Sura 178 kwa kuzingatia sifa za msingi ambazo ni: awe Mtanzania; awe amepata udahili wa masomo ya shahada au stashahada katika taasisi inayotambuliwa na Serikali; asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake; na kwa wanaoendelea na masomo ya mwaka wa pili, watatu na kuendelea, wawe wamefaulu kuendelea na masomo yao katika mwaka unaofuata.

Mheshimwa Spika, Kila mwaka bodi huandaa mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika. Pamoja na vigezo vilivyotajwa, mwongozo hueleza taratibu za kufuata wakati wa kuomba mkopo pasipo kuangalia mwanafunzi kasoma shule ya binafsi au ya umma.

Mheshimiwa Spika, iwapo muomboji atafuata maelezo yote kama yalivyo katika mwongozo wa mwaka husika na akawa ana vigezo vyote, hatutegemei pawepo na ugumu wowote katika kupata mkopo hata kama alisoma shule binafsi. Nashukuru.
MHE. NORAH W. MZERU sliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la uhaba wa Hosteli kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu wanaosoma katika Vyuo vya Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA, Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inafanya juhudi mbalimbali katika kutatua tatizo la uhaba wa hosteli kwa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu hapa nchini vikiwemo Vyuo vya Mkoa wa Morogoro. Kwa sasa hosteli zilizopo katika vyuo vikuu vya Mzumbe na Sokoine zina uwezo wa kulaza jumla ya wanafunzi 7571. Ikiwa Mzumbe ni wanafunzi 3742 na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ni wanafunzi 3829.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo wanafunzi ambao hawapati nafasi za malazi katika hosteli za vyuo wamekuwa wakipata malazi katika hosteli zinazomilikiwa na watu binafsi katika maeneo yaliyokaribu na vyuo.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua ongezeko la uhitaji wa malazi kwa wanafunzi katika vyuo vikuu vya serikali vikiwemo vyuo vya Mkoa wa Morogoro, Serikali imekamilisha ujenzi wa hosteli 4 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1024 katika Chuo Kikuu cha Mzumbe na zimeanza kutumika kuanzia mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, aidha kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation yaani HEET imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli moja yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 600 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Kampasi ya Mazimbu Morogoro. Nashukuru.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Nyamongo Wilayani Tarime?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita, Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Tarime Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Tarime eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi ni katika Kijiji cha Nyabichune, Kitongoji cha Komoware, Kata ya Matongo. Aidha, pamoja na kiasi cha shilingi milioni 45 kilichotolewa awali kwa ajili ya shughuli za maandalizi, tayari Serikali imetuma kiasi cha shilingi milioni 228 kwa kila Chuo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. JUDITH S. KAPINGA K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaboresha Mitaala ya Elimu ili mafunzo ya biashara yatolewe kuanzia shule za Msingi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara iko katika hatua za ukamilishaji wa mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na Mitaala katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Mafunzo ya Ualimu. Aidha, Wizara imevielekeza Vyuo Vikuu kuhuisha na kufanya maboresho ya mitaala yote ili iendane na Dira na Mipango ya Maendeleo ya Taifa katika kutoa elimu itakayompa kijana wa Kitanzania ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatambua umuhimu wa Somo la Biashara na hivyo somo hili limepangwa kuwa ni somo la lazima kwa wanafunzi wote kuanzia Kidato cha kwanza hadi cha nne kwa mikondo yote miwili ya elimu ya jumla na elimu ya amali. Aidha, kwa ngazi ya elimu ya msingi darasa la I - VI mitaala imetilia mkazo elimu ya fedha pamoja na elimu ya ujasiriamali ambapo elimu ya fedha imechopekwa kwenye somo la Hisabati na elimu ya ujasiriamali imechopekwa kwenye somo la sanaa na michezo, lugha, jiografia na mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vyuo Vikuu vya Serikali na Binafsi kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation – HEET) vimepata mafunzo mbalimbali ya kuandaa programu zinazoendana na vipaumbele vya nchi na mahitaji ya soko la ajira. Kupitia utaratibu huu, zaidi ya programu 300 zitaanzishwa na kuhuishwa ikiwemo somo la biashara ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na soko la ajira. (Makofi)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya za Liwale, Nachingwea, Ruangwa na Lindi Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Liwale na Nachingwea ni miongoni mwa Wilaya 64 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi kwa mwaka huu wa fedha. Tayari kiasi cha shilingi 228,942,380 kimeshatolewa kwa kila chuo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Ruangwa umeshakamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 2.3 na mafunzo yameshaanza kutolewa. Aidha, kwa Wilaya ya Lindi tayari kipo chuo cha mkoa kinachoweza kutumiwa na wananchi wa Halmashauri ya Lindi Vijijini, nakushukuru.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza:-

Je, ni maprofesa wangapi wanaozalishwa kila mwaka na ni wangapi wanastaafu kwa kipindi hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa ni ngazi ya kitaaluma ambapo Mhadhiri au Mtumishi wa Taasisi za Elimu ya Juu hufikia baada ya matokeo ya kazi za kitaaluma ikiwemo kufanya machapisho na ufundishaji. Hivyo, kupanda cheo cha mwanataaluma kunatokana na jitihada za mhusika katika ufundishaji, kufanya tafiti na kuchapisha maandiko yake katika majarida yanayotambulika Kitaifa na Kimataifa. Hivyo, kuongezeka kwa idadi yao kunategemea zaidi jitihadi za mtu binafsi katika utekelezaji wa majukumu yake na kukubalika kwa jitihada hizo kwa wanataaluma wenziwe kwa kuzingatia miongozo waliyojiwekea. Hadi kufikia Mwaka 2022 tulikuwa na jumla ya Maprofesa 226 kati yao 163 wakiwa ni Maprofesa Washiriki (Associate Professors) na 63 ni Maprofesa Kamili (Full Professors).

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kustaafu linahusu zaidi Vyuo Vikuu vya Umma ambao umri wa kustaafu ni miaka 65. Kwa takwimu za mwaka 2022 idadi ya maprofesa kamili waliostaafu ni wanne na wanaotarajia kustaafu kwa mwaka 2023 ni watano, kwa mwaka 2024 ni Wawili, na mwaka 2025 ni sita. Maprofesa Washiriki waliostaafu kwa mwaka 2022 ni mmoja na wanaotarajiwa kustaafu kwa mwaka 2023 ni 18, mwaka 2024 ni wanne, na mwaka 2025 ni sita. Ninakushukuru.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha maslahi ya Wathibiti Ubora wa Walimu nchini ili kuinua ubora wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza Muundo mpya wa Utumishi wa Maafisa Udhibiti Ubora wa Shule kuanzia Julai, 2023 ambao unatoa maslahi na motisha kwa Maafisa Udhibiti Ubora wa Shule kwa kuwaongezea Mishahara na kuwabadilishia ngazi ya mishahara kutoka TGTS kuwa TGQS. Hii ina maana kuwa kwa sasa mwalimu atakayeteuliwa kuwa Mdhibiti Ubora lazima awe amefikia ngazi ya mshahara ya TGTS G pamoja na sifa nyingine za uteuzi wa viongozi wa elimu kwa kuzingatia mwongozo wa uteuzi. Aidha, maslahi mengine ni kuongeza ukomo wa ngazi ya mshahara toka TGTS I hadi TGQS J yenye maslahi makubwa kuliko awali. Muundo huo umetambua majukumu makubwa ya Wadhibiti Ubora wa Shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi ya Wadhibiti Ubora wa Shule, Serikali imefanikiwa kutoa vifaa mbalimbali vya TEHAMA kwa Wadhibiti Ubora wa Shule Tanzania Bara, ambapo vishikwambi 1,680 vilitolewa kwa Maafisa Udhibiti Ubora wa Shule, photocopia 234, kompyuta za mezani 769, printer 450 na kompyuta mpakato (laptops) 1,002.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imefanikiwa kujenga ofisi tano za Wadhibiti Ubora wa Shule katika Halmashauri za Wilaya ya Njombe, Tarime, Bunda, Ubungo, na Nyasa na hivyo kufanya au kuwezesha halmashauri 181 kuwa na ofisi. Lengo ni kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi, nakushukuru.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Jimbo la Igalula?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa vyuo vya ufundi stadi katika kuwasaidia wananchi kupata ujuzi utakao wasaidia kutekeleza kazi zao za kiuchumi. Kwa sasa Serikali inatekeleza azma ya kujenga chuo cha ufundi stadi katika kila mkoa na wilaya nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Igalula lipo katika Wilaya ya Uyui na kwa sasa Serikali inakamilisha ujenzi wa Chuo cha Wilaya ya Uyui. Ujenzi huo umefikia asilimia 97 na chuo hiki kimeshaanza kutoa mafunzo ya muda mfupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya zote nchini, Serikali itaangalia uwezekano wa kujenga vyuo vya VETA katika ngazi za majimbo na ngazi zingine za chini kadri ya upatikanaji wa fedha na uhitaji, nakushukuru.
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha matawi ya Vyuo Vikuu vya Umma katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita imelenga kupanua na kuboresha huduma za jamii ikiwemo Elimu ya Juu ili kufikia maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kutokana na azma hiyo, Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation – HEET wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021-2026 inatarajia kujenga kampasi mpya 14 za Vyuo Vikuu katika mikoa ambayo haina Taasisi ya Elimu ya Juu ukiwemo Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Spika, Kupitia Mradi wa HEET, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetengewa jumla ya shilingi bilioni 18.4 kwa ajili ya ujenzi wa kampasi mpya katika Mkoa wa Katavi Wilaya ya Mlele, Halmashauri ya Mpimbwe. Kwa sasa kazi zinazoendelea katika kampasi hiyo ni tathmini ya athari za kimazingira na Jamii yaani environmental and social impact assessment na mchakato wa kumpata mshauri elekezi unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni 2023 na baadaye mkandarasi wa ujenzi, nakushukuru.
MHE. OMAR ALI OMAR aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali haipangi kusahihishia mitihani ya kidato cha nne Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Ali Omari, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2021 na 2022 Serikali ilisahihisha mitihani ya Taifa, kidato cha nne (CSEE) katika kituo cha Shule ya Sekondari Hasnuu Makame, Kusini Unguja. Aidha, Serikali itaendelea kusahihisha mitihani Zanzibar kwa vituo vya mitihani vyenye sifa za kulaza watahini wasiopungua 500 kwa wakati mmoja, kuwa na vyumba visivyopungua ishirini vya kazi, na miundombinu ya maji na umeme kwa wakati wote wa kazi ya kusahihisha, nakushukuru sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wanafunzi wote waliomaliza kidato cha sita wanapata mkopo wa elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka hadi mwaka ili kuongeza wigo wa wanufaika. Bajeti ya mikopo iliongezeka kutoka shilingi bilioni 570 mwaka 2021/2022 hadi shilingi bilioni 654 mwaka 2022/2023. Pia mwaka 2022/2023 shilingi bilioni tatu zilitengwa kwa ajili ya Samia Scholarship iliyonufaisha wanafunzi 593 waliohitimu kidato cha sita wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kupanua fursa za mikopo kwa wahitimu wa kidato cha sita, Serikali imeingia mkataba wa mahusiano na Benki ya NMB ili kutoa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia tisa kwa wazazi/walezi kwa ajili ya kugharamia elimu ya watoto wao katika ngazi ya elimu ya juu na kati. Aidha, Serikali itaendelea kutafuta fursa za mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila mhitimu wa kidato cha sita mwenye sifa anapata mkopo kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu, nakushukuru.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanzisha Tawi la Chuo Kikuu Huria katika Halmashauri ya Ifakara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali haina mkakati wa kuanzisha Tawi la Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania katika Halmashauri ya Ifakara. Aidha, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimefungua matawi yake katika Makao Makuu ya Mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Mkoa wa Morogoro ambapo wananchi wa Halmashauri ya Ifakara wanapata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania pia kina vituo vya mitihani kwenye ngazi ya wilaya kwa pale ambapo idadi ya wanachuo ni 50 na kuendelea. Nakushukuru.
MHE. LUCY J. SABU K.n.y. MHE. JUDITHI S. KAPINGA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti watoto chini ya miaka saba kusoma shule za bweni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliandaa Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule uliotolewa mwezi Novemba, 2020. Mwongozo huo umeelekeza bayana kuwa kibali cha kutoa huduma ya kulaza wanafunzi wa bweni kitatolewa kuanzia darasa la tano na kuendelea. Aidha, huduma ya bweni itatolewa kwa kibali maalum kwa wanafunzi wanaosoma chini ya darasa la tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutolewa kwa mwongozo huo, pia, Serikali imetoa Waraka wa Elimu Na. 2 wa Mwaka 2023 unaowaelekeza wamiliki wa shule wasiokuwa na kibali maalum cha kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi waliochini ya darasa la tano wasiendelee kutoa huduma hiyo. Aidha, kwa kushirikiana na wadau wa elimu, Wizara inakamilisha kuandaa vigezo vitakavyotumiwa na Kamishna wa Elimu katika kutoa kibali maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kudhibiti tatizo la watoto chini ya darasa la tano kusoma shule za bweni kwa kuhakikisha kuwa inafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara na shule itakayobainika kukiuka maelekezo hayo itachukuliwa hatua za kinidhamu, na kisheria ikiwemo kufutiwa usajili, nakushukuru.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza:-

Je, ni wanafunzi wangapi wamerejea shuleni tangu waraka wa kuwaruhusu utolewe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpaka kufikia mwezi Januari, 2023 wanafunzi waliorejea shuleni kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari ni 1,907 ambapo waliorudi katika mfumo rasmi ni 562 na waliorejea nje ya mfumo rasmi wa elimu kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ni 1,345.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa wanafunzi wa elimu ya msingi; Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI inaendelea kukusanya taarifa za wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaboresha miundombinu ya Chuo cha VETA Kitangari?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza baadhi ya majengo yanayokosekana katika Chuo cha VETA cha Kitangari ili kuimarisha uwezo na ufanisi katika kutoa mafunzo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetenga fedha kiasi cha shilingi 666,904,745.01 kwa ajili ya kukiimarisha Chuo cha VETA Kitangari ikiwemo ujenzi wa mabweni, jiko, bwalo la chakula, madarasa na nyumba za watumishi. Ujenzi wa majengo hayo umeanza mwezi Mei, 2023, ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Busanda ili kiweze kutoa elimu ya uchimbaji madini na hatimaye kuongeza tija kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tumaini Bryceson Magessa, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Vyuo vya Ufundi Stadi nchini ili kuwapatia ujuzi wananchi utakaowawezesha kutekeleza shughuli za kiuchumi katika maeneo yao. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilipeleka fedha kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 4.2 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Geita kilichojengwa katika Halmashauri ya Mji wa Geita. Ujenzi wa Chuo hiki upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa ujenzi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Busanda ipo katika Wilaya ya Geita, Serikali inaomba wananchi wa Busanda kutumia chuo hicho cha Mkoa kilichojengwa katika Wilaya ya Geita ambapo elimu ya uchimbaji wa madini itatolewa.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuwaendeleza vijana wanaomaliza kidato cha nne na kupata daraja la nne au sifuri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa fursa kwa vijana wote hata wale waliomaliza darasa la saba kujiunga na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyo karibu na maeneo wanayoishi kwa lengo la kujiendeleza katika ujuzi na stadi mbalimbali za maisha. Vile vile vijana hao wanaweza kurudia mitihani yao kama watahiniwa wa kujitegemea iwapo wanahitaji kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi kwa kuwapatia vijana mafunzo ya uanagenzi na utambuzi wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, nani anahusika kukamilisha ujenzi wa viwanja vya michezo Nelson Mandela University ili shughuli za michezo ziendelee?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa viwanja vya michezo katika Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia umefanywa na Mkandarasi Elerai Construction Company Ltd. chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Ardhi. Hata hivyo, wakati ujenzi unaendelea kulijitokeza dosari na hivyo ujenzi haukukamilika na kusimama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu ndiyo inayohusika na ukamilishaji wa ujenzi huo. Hivyo mwezi Machi, 2021 Wizara iliitisha kikao cha wahusika wote wa mradi huo ambao ni Wizara ya Fedha na Mipango, Pension Property Ltd., Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia, Mshauri Elekezi na Mkandarasi kujadili suala hili. Katika kikao hicho ilikubalika kuwa Chuo Kikuu cha Ardhi kiendelee kumsimamia mkandarasi Elerai na kuhakikisha anakamilisha kazi ya ujenzi wa viwanja hivyo. Nakushukuru sana.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali juu ya kuvuja kwa mitihani inayosimamiwa na vyuo vya afya mwaka 2021?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Husna Juma Sekiboko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakiri kutokea kwa changamoto ya kuvuja kwa mitihani inayosimamiwa na vyuo vya afya mwezi Agosti, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua zifuatazo ili kuhakikisha kuwa tatizo hili halijitokezi tena kwa kufanya mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza; ni kuboresha mfumo wa utungaji, uchapishaji na ufungaji wa mitihani kwa kushirikiana na Mpiga Chapa wa Serikali.

Jambo la pili ni kufanya mapitio ya Mwongozo wa Mitihani iliyo chini ya Wizara ya Afya ili kuendana na mahitaji ya kiulinzi na kiusalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni kuongeza kasi ya kuanzishwa Mamlaka itakayosimamia mafunzo ya vyuo vya afya ngazi ya kati pamoja na uendeshaji wa mitihani.

Jambo la nne ni kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kwenye ulinzi wa mitihani katika hatua zote kuanzia utungaji, usambazaji hadi utoaji wa matokeo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, Serikali imetekeleza kwa kiwango gani Mkakati wa Afrika wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STISA – 2024) kufuatia maendeleo makubwa ya sayansi, teknolojia na ubunifu duniani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA, alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza kutekeleza Mkakati wa Afrika wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu uitwao STISA 2024 mwaka 2015 kwa kuandaa mpango wa utekelezaji wa mkakati husika. Utekelezaji umejikita katika maeneo yafuatayo; eneo la kwanza ni kuweka mazingira wezeshi ya watafiti na wabunifu kwa ujumla kwa kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya utafiti na ubunifu kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia yaani MTUSATE; eneo la pili ni kuimarisha miundombinu ya utafiti na ubunifu kwa kuongeza idadi na kuwajengea uwezo watafiti na wabunifu kupitia miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Vituo vya Umahiri yaani ACE-II; Mradi wa Kukuza na Kuendeleza Ujuzi (ESPJ); Mradi wa Afrika Mashariki wa Kuboresha Mafunzo ya Ufundi (EASTRIP) na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Uchumi (HEET); na eneo la tatu ni kuimarisha mahusiano kati ya Taasisi za ubunifu /utafiti na sekta za viwanda, nakushukuru sana.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza miundombinu ya Vyuo Vikuu nchini kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Paulina Daniel Nahato, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) itajenga Chuo Kikuu kipya cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Butiama chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 5,620. Vilevile Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Mkoa wa Lindi kitakachokuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 360, Kampasi mpya ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili wanafunzi 11,000, Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo cha Mizengo Pinda Mkoa wa Katavi wanafunzi 2,500, Kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya Kampasi ya Rukwa wanafunzi 3,000. Vilevile, mradi wa HEET utafanya ujenzi wa Kampasi mpya za Vyuo Vikuu katika Mikoa ya pembezoni ikiwemo Mikoa ya Kagera, Tanga, Kigoma, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Ruvuma, Manyara na Singida.

Mheshimiwa Spika, mradi huo kwa ujumla unatarajia kuboresha Taasisi za Elimu ya Juu 19 kwa kujenga Hosteli 34 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 9,042, vyumba vya mihadhara 130 vitakavyokuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 27,254, maabara na karakana zitakazokuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 7,850, kumbi za mikutano ya Kisayansi 23, miundombinu ya mashambani pamoja na Vituo Atamizi 10. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa Chuo cha VETA Burugo – Nyakato katika Jimbo la Bukoba Vijijini utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera ambacho ujenzi wake ulianza mwaka 2019. Utekelezaji wa mradi huo unafanywa kupitia ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China wenye thamani ya shilingi bilioni 22.4 na mradi umefikia asilimia 96 na unategemea kukamilika mwezi Juni, 2022.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mradi huo kutatoa fursa ya utoaji wa mafunzo kwa wananchi wa Jimbo la Bukoba Vijijini na Mkoa wa Kagera kwa ujumla. Nakushukuru.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga mabweni pamoja na miundombinu mingine katika Chuo cha VETA Kitangali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Salum Mtanda, Mbunge wa Newala Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Naibu Spika, Serikali inatambua mahitaji ya miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo mabweni katika Chuo cha VETA Kitangali ambapo mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali ilitoa Sh.299,267,002.00 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, jengo la utawala na vyoo na ukarabati wa karakana ya ushonaji, umeme pamoja na uwekaji wa samani na vifaa.

Mheshimwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya miundombinu ikiwemo mabweni, bwalo, nyumba za Walimu na uzio katika Chuo cha VETA Kitangali.

Mheshimwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -

Je, ni vijana wangapi wamepata nafasi za masomo nje ya nchi kwa mwaka 2015 - 2020 na kati yao ni wangapi wanatoka Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Naibu Spika, kwa mwaka 2015 - 2021, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar iliratibu ufadhili wa masomo katika Nchi za Uingereza, Hangaria, China, Morocco, Misri, Algeria, Urusi, Ujerumani, Msumbiji, Thailand, Mauritius, Iran na Indonesia. Watanzania walionufaika na ufadhili huo ni 856 ambapo kati yao wanaume ni 609 sawa na 71.1% na wanawake 247 sawa na 28.9%.

Mheshimwa Naibu Spika, nafasi za ufadhili wa masomo nje ya nchi hutolewa pasipo kujali mwombaji anatoka upande upi wa Muungano.

Mheshimwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Bodi ya Mitaji kwa wahitimu wa elimu ya juu kama ilivyo kwa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilianzishwa mwaka 2004 ili kuweka utaratibu wa kisheria unaowawezesha wanafunzi wahitaji wenye sifa ya kujiunga na vyuo vikuu kumudu gharama za elimu ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeupokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge, hata hivyo, Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa vijana kupitia halmashauri kwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani. Nashauri wahitimu wa elimu ya juu kutumia fursa hiyo kupata mitaji. Nakushukuru sana.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA katika Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe?

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge Vwawa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo mbioni kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Songwe ambapo tayari eneo lenye ukubwa wa ekari 50 limetengwa. Chuo hicho kinatarajiwa kujengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.99 kupitia mapato ya ndani ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Ujenzi huo unatarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2022/2023. Nakushukuru sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-

Je, kwa nini ukumbi wa VETA Nyasa haujawekwa vipooza joto?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshafanya makadirio ya gharama za kufunga vipooza joto katika Chuo cha VETA cha Wilaya ya Nyasa ambapo katika Mwaka huu wa Fedha 2023/2024, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 20 kwa majengo yote. Kati ya fedha hizo shilingi milioni 7.5 zimetengwa kwa ajili ya kuwezesha kununua vifaa vitakavyofungwa katika ukumbi huo ili kuondoa changamoto ya joto kali, nakushukuru.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza

Je Serikali inampango gani wa kupandisha Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa kuwa Chuo Kikuu kamili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu vya Tanzania na Mwongozo kuhusu Vyuo Vikuu Tanzania uliotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania mwaka 2019.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea kukiimarisha Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa kama Taasisi ya Elimu ya Juu chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kukifanya kuwa Chuo Kikuu kinachojitegemea. Serikali itakipandisha hadhi kitakapokidhi taratibu tulizojiwekea kama nchi na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Ujenzi wa Vyuo vya VETA kwa awamu katika mikoa na wilaya mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Meatu, wananchi wa Meatu wanashauriwa kutumia Vyuo vingine vya VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo kwa ajili ya kupata elimu ya mafunzo ya ufundi, nakushukuru sana.