Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Salim Mussa Omar (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu Azzawajal kwa kutujalia siku ya leo sote tukiwa wazima na akili timamu. Pili, nikishukuru chama changu cha Mapinduzi kwa kunichagua miongoni mwa vijana ambao wameaminika kupeperusha bendera katika nafasi hii ya Ubunge katika Jimbo ambalo kwa mara ya kwanza linaongozwa na Chama cha Mapinduzi toka 1995. Nawaahidi wananchi wa Jimbo langu la Gando Pemba Kaskazini kwamba sitowaangusha. Naamini huko wanakonisikia sasa hivi au watakaponisikia wataamini kwa yale ambayo yameshaanza kutendwa na Mbunge huyu ndani ya miezi hii miwili mitatu ambayo tumeanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika mchango wangu kidogo kwa kutumia dakika chache kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Magufuli kwa yafuatayo. Kwanza, namshukuru sana katika hotuba yake aliposema kwamba ataleta meli nane Tanzania, nne zitaelekezwa upande wa Zanzibar na nne zitabaki upande wa Tanzania Bara. Hii imeonesha wazi kwamba Mheshimiwa Rais wetu kumbe anafahamu kwamba sisi Wazanzibar hatuna madini, madini yetu yako katika bahari. Ndiyo maana licha ya utofauti wa ukubwa uliopo baina ya Tanzania Bara na Zanzibar aliweka uwiano sawa wa mgawanyo wa meli zile, ahsante sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, papo hapo niiombe Serikali yangu ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Bunge hili Tukufu kwa kupitia Waziri wetu wa Muungano mama yetu Mheshimiwa Ummy Mwalimu afanye juhudi za kuweza kushauri na kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanza sasa mchakato mzima wa kutoa mafunzo katika suala zima la bahari kuu. Kwa sababu licha ya kwamba meli hizo zitakuja, tunahitaji utaalam kutoka kwenye kidau au viboti vidogo tulivyovizoea mpaka kwenda kuyazoea mameli haya yanayokuja kunahitaji taaluma kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kujikita katika suala la utoaji wa elimu kwenye hilo. Naamini ushirikiano ambao Mheshimiwa Rais aliaahidi katika hotuba yake yataenda kuifanya Zanzibar kuwa kama Brunei In shaa Allah. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake hakusita kuzungumzia suala la ushirikiano wa dhati kabisa na Rais wa Zanzibar kwenye suala la amani na utulivu sambamba na kuulinda Muungano na Mapinduzi Matukufu. Nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Mkuchika na Waziri wa Mambo ya Ndani wasitoe fursa na mwanya hata kidogo kwa wale watu wachache wa Zanzibar ambao wanatumia platform za kidini lakini pia na za kisiasa kutaka kuchokonoa amani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nimwombe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu aliahidi kwamba atatoa ushirikiano kwa Rais wa Zanzibar basi afanye hivyo. Nakumbuka alipomtuma Mheshimiwa Waziri Mkuu kuja Pemba katika kampeni yake kumwakilisha alipopiga simu pale alisema atakuja Pemba. Tunamuomba basi Mheshimiwa Rais aje Pemba tupitie katika yale maeneo ambayo ni kero ili aweze kutoa msukumo wa hali ya juu na kumshawishi Mheshimiwa Rais wa Zanzibar. Kwa nguvu yake mimi naamini mambo yataenda kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, namwomba Mheshimiwa Rais pia katika suala la business dispute ambalo alilizungumzia kwenye hotuba yake lipewe kipaumbele kwa sababu yapo makampuni yana shida nyingi sana. Sisi vijana ambao tulimaliza vyuo tukaamua kujiajiri mwanzo tumekumbana na mambo mengi ambayo mwisho wa siku hujui uende ukalalamike wapi. Unakuta muda mwingine unafanya kazi na taasisi ya Serikali wana-freeze pesa, wanashindwa kuzirejesha Serikalini, wanazibakisha ndani ya akaunti ya kampuni yako, kushtakiwa hushtakiwi, pesa ukiangalia ipo lakini kukopesheka hukopesheki na mwisho wa siku unaua mpaka ile taaluma ndani ya kampuni yako. Kwa hiyo, naiomba hii business dispute hii ifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo ili sisi tulioelekea kujiajiri na wenzetu ambao wanamaliza shule sasa hivi wanaofikiria kujiajiri waweze kujua wapi wanaelekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia machache katika Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu wa Azza wa Jalla, kwa kutukutanisha leo hapa tukiwa wazima na tukiwa na akili timamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nakishukuru chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini na kuniteua na leo ni Mbunge wa Jimbo la Gando ndani ya Bunge hili Tukufu. Kipekee nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru wananchi wa Jimbo la Gando walionichagua kwa kishindo kunileta katika mjengo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua tu fursa hii kuwaambia kwamba sitawaangusha na kama ilivyo sasa hivi mambo yanarindima, Suluhu Cup inaendelea Jimbo la Gando, karibuni sana. Mimi nina mambo matatu ambayo nataka nichangie katika hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, kama walivyotangulia Wabunge wengi ndani ya Bunge hili kumshauri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Wizara yake kuhusiana na Bureau De Change; mimi ni Mbunge kutokea Pemba. Wafanyabiashara wengi waliopo Dar es Salaam ni wapiga kura wetu au ni ahali, au ni ndugu wa wapiga kura wetu. Sasa nisipolizungumza suala hili, kidogo nitakuwa sijawatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kutokea Pemba tumejikita sana kwenye biashara. Unapofunga moja kati ya component za biashara, unatuua kiuchumi. Unapoweka kizingiti katika biashara kama ya Bureau De Change unaua kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hainiingii akilini mwangu hata kidogo kuwekwa kwa shilingi milioni 300 mtaji wa kufungua Bureau De Change. Binafsi kama Salim, naiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliangalie tena jambo hili…(Makofi)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Omar Salim kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jesca Msambatavangu.

T A A R I F A

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumpa taarifa mzungumzaji. Capital requirement ya kuanzisha bureau kwa mujibu wa regulation ya 2019 ni shilingi bilioni moja na siyo milioni 300 kama alivyosema. Hiyo ilifutwa. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Omar Salim, unaipokea taarifa hiyo.

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, hicho ni kichakaa. Kule kwetu tunaita kichakaa, yaani balaa. Hilo ni balaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi, mpaka namaliza Chuo Kikuu pale UCC kuchukua Diploma yangu ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano sikuwahi kufikiria kuajiriwa na Serikali; na huu Ubunge haikuwa ndogo yangu kabla, umekuja tu kwa sababu nilihisi ninao uwezo wa kuwasemea wananchi wa Gando Bungeni baada ya kumaliza chuo. Nilikuwa nategemea sana kujiajiri, lakini sasa kama kutakuwa kuna vingiziti kama hivyo, sidhani kama wale ambao hawajabahatika kuwa Wabunge kama Salim watakuwa na uwezo wa kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lipo serious ndani ya Dar es Salaam. Mimi binafsi nilikuwa na rafiki zangu ambao waliokuwa na Bureau De Change wanafika hata 125 kwa ambao ninawafahamu, leo hii wamekaa dormant. Sio hao tu, hata wale ambao walikuwa ni wafanyakazi wao, wamerudi Pemba wengine na ndio hao wanaoshika mabango kuitukana Serikali pale wanapoambiwa waandamane na wale watu ambao hawaitakii mema Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoke huko nielekee katika dirisha la kupeleka claims kwenye masuala ya business dispute. Narudia tena kama nilivyoungumza siku ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Wako vijana ambao wamepewa nafasi kubwa, nami leo ni-declare interest, nilikuwa ni mfanyabiashara na ni mmiliki wa Kampuni kubwa ndani ya Taifa hili katika wamiliki wa kampuni hiyo (shareholder). Unafanya kazi na Serikali lakini mwisho wa siku anatokea mtu, kwa sababu tu ya cheo chake na nafasi yake, anatengeneza mazingira ya kuwakwamisha bila kujali kama akikuangusha wewe…; na inawezekana tu ana personal conflicts na mmoja wa director katika Kampuni, anatengeneza namna ya kuizuia kampuni hiyo kutokuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hii inawezekana ina wafanyakazi zaidi ya 300; ni familia 300 hizo ambazo ni nyingi katika Taifa letu hili; lakini anatengeneza mazingira, anaikwamisha, inashindwa kufanya progress zake za utendaji na mwisho wa siku kampuni ile ina-collapse na inaanguka. Sijui sasa anamlaani nani? Mwisho wa siku ukiwa unamiliki kampuni kama hii na mtu anakutengenezea mazingira kama hayo kwa sababu ya nafasi yake kubwa, unashindwa kuamua: Je, umshitaki au uende wapi? Maana yake unaenda kumshaki sehemu ambayo wewe ndipo unapatia riziki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mimi nafanya kazi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Kampuni yangu. Akinitengenezea mtu mazingira, nashindwa kulishtaki Bunge kwa sababu nafikiria kesho itakuweje? Inawezekana lile tatizo likatatuliwa lakini kwa sababu nililipeleka Mahakamani Bunge lako, litashindwa kuweza kuniamini kwamba labda nitakuwa sina imani nalo. Kwa hiyo, unakuta makampuni yanafanya kazi na baadhi ya taasisi za Serikali, lakini mkandarasi yule anashindwa kwenda Mahakamani kuishtaki taasisi ya Serikali na mwisho wa siku anajikuta anarudi mtaani.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri atutengenezee dawati la Claim la chini kwa chini…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Salim, unaweza kusimama kawaida, bado utasikika. Maana mpaka ukimaliza kuchangia unaweza ukawa unaumwa mgongo. Kwa hiyo, utaweza kuchangia ukiwa umesimama na bado utasikika. (Kicheko)

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, usijali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri Mheshimiwa Waziri atutengenezee dirisha la kutusikiliza chini kwa chini kwanza. Kuna baadhi ya Kampuni zinaonewa na hili liko wazi. Ukweli tuuseme. Hata mimi ndani ya Chama changu cha Mapinduzi niliapa kwamba nitasema ukweli daima, fitina kwangu mwiko. Sasa kama niliapa hivyo na nimeapa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni lazima ukweli tuuseme. A spade, call it a spade, not a big spoon. Pauro libaki kuitwa pauro, tusiliite kijiko kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kutakuwa na window ya kupeleka claims zetu ndani ya Wizara ya Fedha, basi itatusaidia wafanyabiashara wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoke hapo, niseme tu, maana yake imefikia mahali mfanyabiashara anatega teuzi zinazokuja za Rais atachaguliwa Waziri gani? Je, namjua? Sasa ole wako achaguliwe mtu ambaye alikupigia simu hujapokea. Unaanza kufikiria, eeh, nirudishe tena ile missed call yake ya jana. Yaani tunaenda katika mazingira ya kumtegemea mtu kwa sababu ya nafasi yake sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui nafahamika! Yaani akiteuliwa mtu, unafikiria huyu nitamfikiaje? Hakuna ule mfumo uliowekwa kwamba hapa mimi nitafanya biashara zangu na nitakuwa salama na sitoathiriwa na awamu itakayokuja. Hili lipo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na crew yako tafadhalini sana tuokoeni kwenye hili, mambo ni mengi na wafanyabiashara tunaumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema pia nichangie katika suala la special number/plate number. Ni kweli, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na crew yako kwa kupunguza kiwango kile cha shilingi milioni 10 mpaka kikaja kuwa milioni tano. Bado tunaomba hebu tupunguzieni kidogo hadi ifikie shilingi milioni tatu. Vijana wengi wataweka majina yao ndani ya plate number, itatusaidia kuweza kufanya accumulation ya hizo fedha nyingi sana watakazolipa na pia itasaidia katika vyombo vya usalama kuweza kugundua kwa haraka zaidi pale ambapo tunamtafuta mtu ambaye ana gari ambalo limeandikwa jina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nielekee katika kuchangia kidogo kwenye masuala ya utalii. Next year, inshallah tutakapofika hapa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na crew yako pamoja na Waziri wa Utalii hebu tutengenezeeni kifungu cha kutafuta fedha kwa namna ya kuwekeza katika digital tourism. Tuwe na fedha ambazo zitatuwezesha kumpata mkandarasi duniani atuwekee digital tourism ambayo itaweza ku-display hata katika slogans za kule kwenye airport. Mfano Dubai pale, tuweze kuona swala wetu wa Tanzania, Mlima Kilimanjaro, popo wetu wa Pemba ambao hawawezi kupatikana sehemu yeyote duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyo vivutio vya Utalii ambavyo haviwezi kuonekana sehemu nyingine yoyote isipokuwa Zanzibar au Tanzania Bara. Tunao Kima Punju, tuweze kuwa na display kule katika airport; watu wanaposubiri ku-connect ndege kutoka sehemu moja kwenda nyingine waweze kuona Zanzibar kuna nini? Tanzania Bara kuna nini? Tuweze kuongeza wigo mpana wa kupata watalii na kupata fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache niliyochangia, naomba niunge mkono hoja, niwaombee kila la heri Mheshimiwa Rais pamoja na watendaji wote, Ishallah tutafika. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi kuweka baraka yangu katika mpango huu wa Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

Kwanza kabisa na mimi kwa niaba ya wananchi wa Gando natoa zangu pole kwa wote wahanga waliofikwa na issue hii ya Precision Air, lakini kwa wale waliotangulia mbele ya haki tunasema Allahumma ghufilahum warhamni maskanahum fil Jannah (Mwenyezi Mungu aende awape pepo na mapumziko mema na sisi atujalie hatima njema).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nitachangia mambo matatu katika mpango huu ambayo naona kidogo hayakuzunguziwa sana kwa mujibu wa nilivyosoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukuza uchumi wa nchi ni lazima tuweze kukuza teknolojia ndani ya nchi yetu. Nimeangalia miongoni mwa means ya kukusanya kodi ni pamoja na kuliongezea Jeshi la Polisi uwezo wa kiteknolojia. Leo Mheshimiwa Bonnah alisimama hapa kazungumzia suala la kamera za barabarani, jambo hili ni la msingi sana. Wengi ambao hawana taaluma na masuala ya kamera wanaona kwamba labda ni kumulika tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamera hizi zitakapowekwa barabarani zinauwezo wa kuwa integrated na system za kileo ambazo zina uwezo wa kuweza ku-capture plate numbers na kuweza kupiga automatic fine na mwisho wa siku Taifa hili likakusanya fedha nyingi kuliko traffic kutembea na gadgets ambazo traffic unaweza uka- bargain naye barabarani, bwana nipige faini ama la na akakuacha, lakini teknolojia haina bargaining.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeshauri katika Mpango huu Mheshimiwa Waziri wa Fedha uchukue suala hili la CCTV camera tuweze kuweka walau kwa kuanzia first phase tuweke katika junctions za barabara zetu. Wapo wanaopita taa nyekundu, wanao overtake hovyo, wako wanaofanya mambo ya hovyo kabisa barabarani ili wakumbane na system hii mwisho wa siku tuweze kuweka nidhamu bora barabarani na kukusanya mapato kwa kutumia digitali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda mbali zaidi teknolojia hii hii iende i-apply katika kulinda heshima, mali na utu wa Mtanzania na kwa wale wenzetu wanaotoka nje ya Tanzania wanaokuja hapa Tanzania. Nasema hivi kwa sababu lipo janga kubwa ndani ya Taifa letu sasa hivi na mimi naliona na tiba yake inaendeshwa lakini kidogo kidogo sana likisimamiwa na Jeshi la Polisi, suala la kuchafuliwa majina ya watu kupitia mtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwapatia uwezo askari polisi na tukawajengea unit maalum ya cybercrime iliyo ya kweli kabisa kwa kila kituo cha mkoa, tukawapa na equipment na skills ili waweze kuwakamata hawa watu ambao wanachafua watu ambao wamejenga heshima zao kwa miaka mingi, basi Taifa hili tutaweza kwenda mbali zaidi. Lakini sio tu kuchafuliwa majina, lakini pia mtandao unatumika kwa ajili ya kufanya fraud ya kuwaibia watu fedha. Wapo watu wanatapeliwa wengi, kuna zile namba utasikia tuma kwa namba hii. Kuna watu wanasikiliza information za watu halafu mara tu wana-dump in na wanakuja kuchukua fedha pasipo na kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Wizara ya Fedha walichukue hili tuliwezeshe Jeshi letu la Polisi kwa skills pamoja na equipments, kwa kila mkoa iwepo kweli cybercrime na sio tu maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika kituo cha mkoa wetu Wete pale simuoni askari hata mmoja ambaye ana iPad ya inayoshughulika na masuala ya kwenda ku-extract information kwa ajili ya kuweza kutupa majibu haya. Jambo hili linapelekea polisi kuweza kupewa lawama kubwa. Kesi ni nyingi lakini watuhumiwa hawakamatwi mpaka polisi waende wakaangukie taasisi nyingine, wakapigie watu magoti sjui TCRA, mobile providers hao. Polisi wenyewe waweze kutengenezewa unit na waweze ku-extract information kiukweli hasa ili tuweze kuendelea zaidi ndani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kabisa ningependa pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie suala la kuongezea nguvu Jeshi letu la Uokozi (Fire). Kwa mfano wa Jiji la Dar es salaam, juzi hata mimi nilipata kadhia ya kuunguliwa gari langu moto, lakini gari la zimamoto mpaka lisukumwe au liwe boosted. Sasa hadi liwe boosted tayari watu watakuwa wamefariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliunguliwa na soko letu la Kariakoo, hivi ukiangalia distance ya kutoka kwenye Ofisi ya Fire pale hadi Kariakoo, soko lile ni la kufikia mpaka likaangamia namna ile? Ipo haja ya Serikali kuongeza magari ya kisasa, yaliyopo ni chakavu, yana umri sawa na Salim miaka 34 na kwenda mbele. Ukiangalia matukio yanatokea frequently, lakini kubadilisha equipment hizi imekuwa ngumu ndani ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi nitoe mchango wangu huo In Sha Allah uende ukatekelezeke. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi na vilivyomo kwa kutujaalia tumefika hapa tukiwa hai na wazima. Pili, ninakushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee leo nitajikita katika suala zima la maafa katika ukurasa 69 na ukurasa wa 70 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi mwaka 2019 nilipata fursa ya kwenda kutembelea museum tatu nchini Marekani, ikiwemo ya Titanic Museum iliyoko pale Branson, pamoja na World Trade Centre iliyoko pale New York pia JF Kennedy iliyoko Texas.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio haya yalinipa msisimuo wenye mfanano sawa na baadhi ya matukio yaliyotokea ndani ya nchi yangu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na janga la Titanic lilotokea na kupelekea kufariki kwa watu takribani 1,500. Tukio hili linafanana na ajali ya boti yetu ya MV Spice iliyotokea Zanzibar na kuondoka kwa Wazanzibari wasiopungua 1,370. Hali kadhalika tukio hili la Titanic linafanana sana na ajali iliyotokea ya MV Bukoba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kama Mbunge, napenda kuishauri Ofisi ya Waziri Mkuu ni wakati sasa wakutengeneza museum za digital ambazo zitapelekea kizazi kijacho kuweza kuwa na kumbukizi na Taifa kuweza kujipatia kipato katika museum kama hizi, haswa nilipoona kwamba kiingilio katika museum ile ya Titanic ilikuwa ni takribani Shilingi Laki Moja sawa na Dola ya Kimarekani 49.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kama tutakwenda katika muundo kama huu yanapotokea maafa makubwa kama haya na kuweza kuyawekea museum maalum, tunaweza hata kukusanya kipato ambacho kinaweza kikasaidia hata angalau kuwasomesha wahanga wale ambao wazee wao waliathirika kwa kiasi kikubwa, katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na majanga kama haya pia yaliyojitokeza nilijionea pia mfanano mkubwa sana niliyoiona katika museum ya JF Kennedy na tukio lilotokea pale Zanzibar tarehe 7 Aprili, 1972 la kupigwa risasi hadharani Rais wetu wa kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Karume.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo bado halijatengenezewa museum hasa yakuweza kutueleza ilikuwaje na unaweza ukakuta hata mwanafunzi wa Chuo Kikuu sasa hivi asiwe na picha halisi ya kukueleza namna gani lile tukio lilitokea siku ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu ofisi yako iweze kutengeneza museum mahsusi ya kuweza ku-display hasa historia muhimu kama hizi. Ukienda Zanzibar leo pale ofisi kuu utamkuta Mzee Baraka Shamte atakuelezea ilikuwaje lakini Mzee Baraka Shamte hataishi milele, tutengeneze digital museum ambayo itaweza ku-display matukio muhimu ya kihistoria kama haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo hata ile museum yetu iko pale kwa Mwalimu Nyerere Butiama pia tuangalie namna gani ya kuweza kuitengeneza iwe katika hali ya kidigitali zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema mchango wangu uende katika masuala hayo ya maafa ili tuweze kuwa na rekodi ambazo zitakuwa kumbukizi ya muda mrefu ili na watoto wetu, wajukuu zetu waweze kuja kujionea hasa nini nchi imepitia, athari zilizojitokeza zilisababishwa na nini ili kuweza ku-overcome hizo situation zisiweze kujirudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)