Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ghati Zephania Chomete (12 total)

MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sera ya Matibabu Bure kwa Wazee wenye umri kuanzia miaka 60 katika Halmashauri za Mkoa wa Mara inatekelezeka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inatekeleza Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, inayoelekeza kutoa matibabu bila malipo kwa wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo kwa kuwatambua na kuwapatia huduma mbalimbali za afya. Hadi Desemba, 2020 jumla ya wazee 2,344,747 wametambuliwa sawa na asimilia ya 87 ya makadirio ya wazee wote nchini. Kati yao wanaume ni 1,092,310 na wanawake 1,252,437. Aidha, wazee wasiokuwa na uwezo 1,087,008 wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bure na wazee 856,052 wamepatiwa kadi za matibabu ya Afya ya Jamii (ICHF).

Mheshimiwa Spika, hadi Februari, 2021 Halmashauri za Mkoa wa Mara zimefanya utambuzi wa wazee 70,170 kati ya lengo la kuwatambua wazee 196,000. Kati ya wazee waliotambuliwa, wanaume ni 32,900 na wanawake ni 37,270. Wazee 39,664 wamepewa vitambulisho vya matibabu kati ya wazee 70,170 waliotambuliwa.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mara na Mikoa mingine inaendelea kufanya utambuzi kwa wazee na kuhakikisha wazee wote wanaotambuliwa wanapewa vitambulisho vya matibabu bila malipo. Aidha, Serikali itaendelea kuwatambua wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasio na uwezo ili waweze kunufaika na Sera ya Matibabu Bila Malipo.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza:-

Je, Serikali ina teknolojia gani mbadala ambayo itaepusha kutumia magogo kama matimba kwenye mashimo ya migodi hasa maeneo ya Nyamongo, Tarime, Buhemba na Butiama?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa wachimbaji wengi wadogo nchini na katika maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji wa dhahabu yakiwemo maeneo ya Nyamongo, Tarime, Buhemba na Butiama wamekuwa wakitumia magogo na kwa lugha yetu ya kichimbaji yanaitwa matimba na yanatumiwa kama mihimili ulalo pamoja na wima kwenye mashimo ya migodi ili kuweka support. Pamoja na teknolojia hiyo kuonekana kuwa ya gharama nafuu, imekuwa ikisababisha uharibifu mkubwa wa mazingira licha ya kuwa si salama na si ya kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, teknolojia mbadala inayotumika kwa sasa ni ujenzi wa mashimo ya migodi kwa kutumia zege pamoja na nondo. Teknolojia hii ni salama na haina athari kubwa za kimazingira ukilinganisha na ile inayotumia magogo. Miongoni mwa sababu zinazopelekea wachimbaji wadogo kutotumia teknolojia hii ni ufinyu wa mitaji, lakini pia, kutokuwa na maeneo ya kudumu ya uchimbaji na baadhi yao kutokuwa na leseni za uchimbaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuwarasimisha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia leseni za madini ili waweze kutambulika kisheria na kwa jinsi hiyo kuwawezesha kuaminika katika taasisi mbalimbali za fedha. Aidha, Serikali kupitia STAMICO inaendelea kutoa elimu kwao kuhusu uchimbaji wa kitaalam na wenye tija unaozingatia masuala ya afya, usalama na utunzaji mazingira.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Tarime hadi Serengeti kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Tarime – Mugumu (Serengeti) ina jumla ya urefu wa kilometa 87.14 ambapo sehemu ya barabara hiyo yenye urefu wa kilometa
10.7 tayari imejengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 76.44 zilizobaki zimejengwa kwa kiwango cha changarawe. Aidha, Serikali imekamilisha ujenzi wa daraja la Mara lililopo katika barabara hii lenye urefu wa meta 94 na barabara za maingiliano za daraja hilo zenye urefu wa kilometa 1.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zabuni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kilometa 25 nje ya kilometa 76.44 zisizokuwa na lami za barabara hiyo imetangazwa tarehe 4 Juni 2021. Taratibu za manunuzi zikikamilika kazi za ujenzi zitaanza mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kwa sehemu itakayobaki kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyopatikana.
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. GHATI Z. CHOMETE Aliuliza: -

Je, ni lini agizo la Mheshimiwa Rais la kuboresha stendi ya Bweri Musoma Mjini litatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali kwa ridhaa yako naomba nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Baraka kwa kutujaalia afya njema sisi sote na kutuwezesha kuendelea na majukumu haya ya kuwatumikia watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyonipa na kuteua kuendelea kuwatumikia watanzania wenzetu katika dhamanahii muhimu ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Naomba kumuahidi Mheshimiwa Rais kwamba nitafanya kazi kwa bidii yangu yote ili kuhakikisha imani yake na maono wake ya kuwatimizia maendeleo watanzania yanatimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo ya utangulizi, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, stendi ya mabasi ya Bweri katika Manispaa ya Musoma ilijengwa mwaka 2007 kwa mapato ya ndani ya halmashari kwa kutumia Mkandarasi CMG Construction Company Ltd aliyeingia mkataba wa shilingi bilioni 1.36 ambapo Mkandarasi huyo alifanya kazi zenye thamani ya shilingi milioni 921.17.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa stendi hiyo yenye uwezo wa kuingiza magari 35 hadi 45 ina miundombinu iliyochakaa hivyo inahitaji kuboreshwa. Kwa kutambua umuhimu wa stendi hiyo, tayari Halmashauri ya Manispaa ya Musoma imeandaa andiko la mradi huo na limewasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya Uchambuzi wa kutengewa fedha kwa ajili ya ujenzi kupitia ufadhili wa Benki ya BADEA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utaratibu wa kupata ufadhili huo ili mradi huo pamoja na miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa kupitia ufadhili huo utekelezaji wake uweze kuanza. Ahsante.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y. MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, ni nini tamko la Serikali kuhusu uchimbaji unaoendelea katika Mto Nyandurumo ambao ni chanzo cha maji kwa wakazi wa Tarime?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha maji cha Nyandurumo ni chanzo ambacho kinatoa huduma ya maji kwa Mji wa Tarime ambapo kina uwezo wa kuzalisha maji lita 6,000,000 kwa siku kwa kipindi cha masika na lita 1,500,000 kwa kipindi cha kiangazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na uharibifu unaojitokeza kwenye chanzo hicho, Serikali kupitia Watalaam wa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Bonde la Ziwa Victoria na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara wamewaondoa wachimbaji waliokuwa wanafanya shughuli za kusafisha madini karibu na chanzo hicho cha maji na kupanda miti 205 ambayo ni rafiki kwa mazingira ikiwa na lengo la kulinda na kuhifadhi chanzo hicho. Umbali wa kutoka maeneo ya uchimbaji hadi kwenye chanzo cha maji ni takribani kilometa tatu.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha huduma za afya zikiwemo dawa muhimu katika hospitali zetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya nchini kwa kuboresha miundombinu ikiwemo kuweka vifaa tiba vya kisasa, kuajiri wataalam wa afya pamoja na kuwapandisha madaraja ili kuongeza morali ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na hadi kufikia tarehe 30 Oktoba, 2022, Serikali imekwisha toa jumla ya shilingi bilioni 74.3 kwa ajili ya manunuzi ya dawa na vifaa tiba ili kuimarisha upatikanaji wake katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya nchini. Ahsante.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo la ukosefu wa maji katika Wilaya za Mkoa wa Mara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mara kwa sasa ni wastani wa asilimia 66 vijijini na asilimia 71 mijini. Katika kuboresha huduma ya maji katika Mkoa wa Mara, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa miwili ya Mugango, Kyabakari hadi Butiama na mradi wa maji Bunda ambayo itanufaisha Wilaya za Butiama, Musoma na Bunda za Mkoa wa Mara. Aidha, utekelezaji wa mradi wa Miji 28 unatarajiwa kuanza katika mwaka huu wa fedha ambapo Wilaya za Serengeti, Tarime na Rorya zitanufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mingine 72 katika Wilaya zote za Mkoa wa Mara. Kukamilika kwa miradi yote kutaboresha huduma ya maji kufikia lengo la asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo 2025.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE K.n.y. MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wakulima wa Tarime wanaolima kahawa aina ya Arabika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Kahawa inaendelea kukiwezesha na kukiongezea uwezo Kituo Kidogo cha Utafiti wa Kahawa (TaCRI) kilichopo eneo la Nyamwaga Tarime ili kuzalisha miche milioni moja kwa mwaka. Miche hiyo inaendelea kuzalishwa na kusambazwa bure kwa wakulima wa Kahawa Wilaya ya Tarime na Wilaya nyingine za Mkoa wa Mara. Kupitia jitihada hizi kuanzia mwezi Septemba, 2022 hadi kufikia mwezi Machi, 2023 jumla ya miche 173,471 imezalishwa na kugawiwa bure kwa wakulima. Aidha, Serikali imeboresha mfumo wa masoko kwa kuwezesha kuanza kufanya kazi kwa mitambo ya kuchakata kahawa katika maeneo ya Muriba na Nyantira.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa tatizo la upungufu wa walimu wa sayansi Mkoani Mara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 Mkoa wa Mara ulipata walimu 531 kwa shule za Msingi na Sekondari. Kati yao walimu wa masomo ya sayansi walikuwa 197. Ni dhamira ya Serikali kuendelea kuajiri na kuongeza idadi ya walimu wa sayansi ili kuendana na malengo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari imetenga nafasi za ajira za walimu na watumishi wa kada ya afya kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo jumla ya nafasi 13,130 ni za kada ya elimu na kipaumbele ni masomo ya sayansi. Waombaji watapangiwa vituo vya kazi kwa kuzingatia maeneo yenye upungufu mkubwa ukiwemo Mkoa wa Mara.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga miundombinu ya maji mashuleni ili kuepusha milipuko ya magonjwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa shule zote za Msingi na Sekondari zinakuwa na miundombinu ya maji safi na salama pamoja na vifaa vya kunawia mikono vikiwemo ndoo, jaba tiririka na miundombinu iliyojengwa kwa pamoja (mass handwashing facilities). Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali kupitia mradi wa usafi na mazingira (SRWSS) imejenga miundombinu bora ya kunawia mikono pamoja na vifaa vya kuhifadhia maji katika shule za msingi 1853.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha usafi mashuleni kupitia vilabu vya uhamasishaji usafi mashuleni (Swash Clubs).
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaboresha Kivuko cha Kinesi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu (jengo la abiria, ofisi, vyoo na uzio) katika Kituo cha Musoma maarufu kama Mwigobero. Mkandarasi amekabidhiwa eneo la ujenzi kwa ajili ya kuanza kazi. Aidha, ujenzi wa miundombinu upande wa Kinesi umepangwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, ahsante.
MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ukarabati wa Stendi Kuu ya Mabasi Bweri iliyopo Manispaa ya Musoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Stendi ya Mabasi ya Bweri katika Manispaa ya Musoma ilijengwa mwaka 2007 kwa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kutumia Mkandarasi CMG Construction Company Limited aliyeingia Mkataba wa shilingi bilioni 1.36 ambapo Mkandarasi huyo alifanya kazi zenye thamani ya shilingi milioni 921.17.

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ilikuwa kujenga stendi hiyo kupitia ufadhili wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Afrika (BADEA). Hata hivyo kutokana na majadiliano kutozaa matunda, Serikali imeiweka stendi hiyo kwenye Mpango wa TACTIC ambapo shilingi bilioni 1.35 zimetengwa.