Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ghati Zephania Chomete (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyeweza kunipa uhai leo nimesimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Kipekee zaidi naomba niwashukuru wanawake wa Mkoa wa Mara walioweza kunichagua mimi kuwa mwakilishi wao katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuweza kuniteua mimi kuwa Mbunge. Pia nakushuru wewe kwa kunipa nafasi leo nimesimama kwa mara ya kwanza katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba nimpongeze Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020. Mheshimiwa Rais wetu mpendwa amefanya kazi kubwa sana katika nchi yetu. Kikubwa zaidi Mheshimiwa Rais wetu katika Mkoa wangu wa Mara amejikita kufanya mambo mengi makubwa sana ambayo yamesababisha nchi yetu imepiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika suala la afya. Mheshimiwa Rais wetu wetu mpendwa katika Mkoa wangu wa Mara amefanya mambo makubwa katika Sekta ya Afya hasa upande wa hospitali, amejenga zahanati takriban 45 mpya, lakini pia vituo vya afya 13 vipya, amejenga hospitali za wilaya saba mpya. Kipekee kabisa Rais wetu ameweza kutupatia takriban zaidi ya bilioni 15 kuhakikisha tunajenga hospitali ya rufaa maarufu kwa jina la Kwangwa iliyokuwa imekaa zaidi ya miaka 40 sasa inafanya kazi katika kitengo cha mama na mtoto. Mheshimiwa Magufuli apewe sifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi naomba niende kuchangia katika hotuba aliyoitoa ya ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili. Mheshimiwa Rais wetu aliongea hotuba ambayo ilisababisha sisi kutupa dira, maono na mikakati mikubwa ya mstakabali wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba Mheshimiwa Rais wetu kwa hotuba hii ambayo Rais aliitoa imegusa kila eneo la Taifa hili ambayo naomba nielekee katika kundi la wanawake, lipewe fursa kubwa kwenye taasisi za kifedha kama mabenki. Nina Imani ili akinamama hao ambao wamekuwa ni sehemu kubwa mama zetu hawa ambao wamekuwa ni sehemu kubwa katika kulijenga Taifa letu waweze kupata fursa kubwa katika kupunguziwa masharti ya kupewa mikopo ya nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uhakika nilionao niwaombe masuala ya kuhakikisha wanawake wanapata fursa ya kukopeshwa, naamini watakaoweza kukopeshwa wataweza kuonekana katika ujenzi wa Taifa hasa katika suala la Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua mama zangu wana changamoto kubwa hasa katika masuala ya kiafya. Nijikite kwenye kusema kwamba masuala ya tatizo la kiafya hasa ugonjwa wa akinamama wa kansa ya matiti na ya kizazi, hawa akinamama wanapata tabu sana hapo bada ya kuwa wanakosa huduma pale ambapo Madaktari wanakuwa hawapo pale. Sasa naomba niishauri Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sekta ya kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa letu basi Serikali ilipe kipaumbele suala hili la bajeti ili kukidhi mahitaji ya Maafisa Ugani, mbegu, mbolea bora na pembejeo kwa ajili ya kuchochea hali ya wakulima na hivyo kuchochea uzalishaji bora wa mazao ya chakula na biashara.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali izamilie kuwasaidia wakulima wetu kuuza mazao kwa bei yenye tija na kupata masoko ya uhakika hasa kwa mazao ya kahawa, pamba na kadhalika ili kuwezesha mkulima kunufaika ipasavyo na kilimo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na ukosefu wa mbolea umewafanya wakulima wetu hasa waliopo karibu na mipaka mfano Wilaya ya Tarime wakulima wamekuwa wakinunua mbolea Kenya ili kukidhi mahitaji ya kilimo hii pia ni kwa kuwa mbolea yetu haiwafikii kwa wakati lakini pia ikiwepo huuzwa kwa bei ya juu zaidi.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ifanye haraka upatikanaji wa mbolea katika mipaka hiyo ili pia kuzuia magendo ya mbolea, kwa sababu wakulima wanafuatwa mpaka mashambani na TRA kuwakamatia mbolea hizo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Maji. Kwanza kabisa nampongeza Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hotuba nzuri aliyoitoa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia ninampongeza kwa juhudi anazoendelea kuzifanya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali kwa kuhakikisha inaboresha miradi ya maji nchi. Nampongeza sana Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso, nampongeza Naibu Waziri wa Maji Maryprisca kwa kazi nzuri wanazozifanya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na wafanyakazi wote wa Wizara hiyo. Wamefanya kazi nzuri katika Manispaa ya Musoma kwani hivi sasa wananchi wanapata maji mazuri ya bomba kwa kiwango cha kuridhisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizo, Mkoa wa Mara ambao una wilaya nyingi sasa maji ni pungufu sana.

Naomba mradi wa kutoka Ziwa Victoria, ule ambao unaanzia Wilaya ya Rorya uhakikishe Wilaya ile ya Rorya pamoja na vijiji vyake vinapata maji. Hivyo hivyo, Wilaya ya Tarime pamoja na Vijiji vya Nyamwaga mpaka Nyamongo wahakikishe vinapata maji. Niombe Serikali ihakikishe mradi huo wa kutoka Ziwa Victoria unawasaidia wananchi wa Wilaya ya Tarime kwa sababu mpaka sasa wanateseka sana hawana maji. (Makofi)

Mheshimiiwa Spika, vilevile Musoma Vijijini, Butiama pamoja na vijiji vyote vinavyozunguka zile wilaya havina maji. Bunda kuna miradi ya maji mpaka sasa miradi ile inasuasua, niombe Serikali kupitia Wizara hii ya Maji iangalie miradi yote iliyoko Bunda inatekelezeka. Mfano Mwibara kuna mradi wa maji ulipelekewa shilingi milioni 510 wa kutoka Namuhura kuelekea Kwibara lakini unasuasua. Kuna mradi wa kutoka Buramba, Kibara mpaka Kisorya mpaka sasa miradi ile inasuasau. Niombe Serikali yangu sikivu kupitia Wizara hii ya Maji ihakikishe miradi ile inatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya Serengeti kuna mradi wa chujio la maji katika bwawa Manchira. Mradi ule ukitekelezeka unasaidia sana Mji wa Mugumu pamoja na vijiji vile vinavyozunguka pale ili wananchi wa maeneo yale waweze kuondokana na kero hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna sera ya kusema kwamba tunamtua mama ndoo kichwani, niwaombe sana Wizara ya Maji wahakikishe wanatua ndoo kichwani wale wanawake wa Mkoa wa Mara maana wanateseka sana. Akina mama wa Mkoa wa Mara ni wachapa kazi, wanaamka asubuhi kwenda kutafuta maji. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu sikivu iuangalie kwa jicho la pili Mkoa wa Mara ili kusudi tuweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Rorya, Kata ya Komuge kuna mradi wa maji. Mradi ule ulishatengewa shilingi bilioni 1.3 lakini sasa toka umetengewa fedha hiyo ni miaka mitano sasa umepelekewa shilingi milioni 300 tu. Niombe Serikali ihakikishe mradi ule unatekelezeka. Nasisitiza Serikali ihakikishe inapeleka pesa hizi kwa wakati lakini ihakikishe pia inatekeleza miradi yote iliyowekwa katika Mkoa wa Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete. Nilikuwa sijamfahamu, sasa sijui ni katika Waanchari au Wanyichoka au Mkurya au Mjaluo au Mngorebe au Msweta au… Kuna makabila bwana. (Kicheko)

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Spika, mimi ni Mtimbaru. Mkurya Mtimbaru.

SPIKA: Naam.

MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mimi ni Mkurya Mtimbaru. (Makofi)