Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Iddi Kassim Iddi (49 total)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya wananchi wa Msalala, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara hii imekuwa kero kubwa sana kwa wananchi, hususan wa Kata za Segese, Shilela, Ngaya na Bugarama. Barabara hii imeahidiwa kiasi cha dola milioni 40 kwa ajili ya kutengenezwa na Mgodo wa Barrick na imekuwa ni kero kubwa sana kwani inasababisha wakazi wa maeneo haya ambayo nimeyataja kuhama makazi yao asubuhi na kurudi jioni kutokana na vumbi kali kwa sababu inatumiwa na magari makubwa. Je, ni lini sasa Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Madini watakwenda kwa Waziri wa Fedha ili wamwambie Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kutekeleza mkataba na makubaliano walioingia baina ya Serikali na Mgodi ili Mgodi uanze kutengeneza barabara hii mara moja? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini sasa Serikali itaanza kufikiria ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara inayotoka Kahama kupita Kata ya Busangi kwenda Nyang’hwale na kutokea Busisi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kassim Iddi Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Msalala kwamba katika jibu langu la msingi nimesema Mgodi wa Barrick wameonesha nia maana yake ni kwamba tayari timu ya majadiliano imeundwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wizara ya Madini, lakini kwa sababu tunayojadili ni masuala ya fedha timu hiyo imejuimuisha pia Wizara yenyewe ya Fedha. Kwa hiyo, once majadiliano yatakapokuwa yamekamilika na kupata utaratibu sahihi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo itaanza kujengwa ili kuwapunguzia adha wananchi wake wa Lunguya, Segese, Ntobo hadi Bukoli na Geita ambao wako Mkoa wa Geita. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge aamini kwamba Serikali itafanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Nyang’hwale kwenda Busisi, naomba pia nimhakikishie kwamba ipo kwenye mipango, ipo kwenye Ilani na tuna mpango wa miaka mitano ambao nina hakika katika kipindi hiki barabara hiyo pia itajengwa kadiri fedha zitakavyopatikana. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nilitaka niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kumekuwa na malalamiko juu ya ongezeko la bili za maji katika Kata ya Isaka, Kata ya Bugarama; je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuunda tume na niombe au Waziri mwenyewe husika uweze kufika katika Kata ya Bugarama na Kata ya Isaka, ili kuweza kubaini nini chanzo cha ongezeko la gharama za maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kuna fedha iliyobaki katika mradi ambao unatoka Kagongwa – Isaka; je, Serikali ina mpango gani wa kutumia fedha hizo kuweza kuanza kusambaza maji katika Kata ya Mwakata? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Iddi kwa kazi kubwa, nzuri anayoifanya katika Jimbo lake la Msalala, lakini kubwa ambalo nataka kulisisitiza ni haki ya mwananchi wa Tanzania kupatiwa maji na mwananchi naye asisahau kwamba ana wajibu wa kulipia bili za maji. Sisi kama Wizara ya Maji tutasimamia bili hizo zisiwe bambikizi. Tumetoa maelekezo mahususi kwa Taasisi ya EWURA yenye jukumu la kuidhinisha bili za maji na ripoti wamenikabidhi hivi karibuni, tutaifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu swali lake la pili, tunakiri kuna fedha ambazo zimebaki katika mradi wa Isaka – Kagongwa. Tumetoa maelekezo mahususi kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira - Kahama, kufanya kazi ile kwa force account kuhakikisha vijiji vyote ambavyo vimebaki vipatiwe huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza, ahsante sana.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Kwa kuwa tatizo lililopo Kyela ni sawasawa na tatizo lililopo katika Wilaya ya Halmashauri ya Msalala. Je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara inayotoka Busisi – Ngoma, Ngoma – Nyang’hwale, Nyang’hwale – Chela, Chela – Busangi – Kahama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara anayoisema ya kutoka Busisi – Nyang’hwale na kupita kwenye Jimbo lake ni barabara ambayo tayari imeshafanyiwa usanifu na kinachosubiri ni upatikanaji wa fedha ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi kwa kipindi cha miaka mitano nina uhakika zitajengwa kwa kiwango cha lami kadri fedha itakavyoendelea kupatikana. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala yapo katika Kata ya Ntobo na ukizingatia Kata zake zilivyokuwa mbalimbali hususan Kata za Isaka, Mwalugulu, Jana na Mwakata kupata taabu sana kupata huduma za ki- Halmashauri. Sasa nini mpango wa Serikali wa kuanzisha Mamlaka ya Mji mdogo katika Kata ya Isaka ili kuwawezesha wana Isaka nao sasa waweze kupata huduma kwa urahisi. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kassim Iddi Iddi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba tu kwamba kwa nini sasa Serikali isianzishe Mamlaka ya Mji Mdogo katika eneo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala kwenye Kata ya Ntobo kama alivyoeleza. Kwa hiyo, ametaka kujua ni lini lakini jibu langu la msingi utaratibu ni uleule kwamba mkitaka tuanzishe haya Mamlaka maana yake mfuate taratibu hizi ambazo tumezianisha, mlete maoni yapitie katika ngazi zote na sisi tutafanya tafakuri na tathmini na baadae tukishajiridhisha basi maomba hayo tutayapeleka kwa Mheshimiwa Rais ambaye ndiye ana mamlaka ya mwisho kabisa ya kutangaza maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo ndilo jibu la Serikali anzisheni mchakato nasi tutakuja tufanye tathmini. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Nataka kuiuliza Wizara kwamba ni lini sasa Serikali ina mkakati wa kusambaza maji katika Kata ya Mwaluguru, Kata ya Jana, na Kata ya Ikinda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la usambazaji maji ni suala ambalo litafanyika mara baada ya kukamilika kwa miundombinu yote kwa sababu lengo ni kuona baada ya uchimbaji wa visima, usambazaji uweze kufuata na akinamama waweze kutuliwa ndoo kichwani.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kumekuwa na changamoto ya watu wenye bima wanapokwenda kwenye kituo cha afya ama zahanati kukosa dawa. Sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inaziunganisha bima zao za afya na maduka ya private ama maduka yaliyomo ndani ya hospitali za Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tumekuwa na changamoto pia ya upatikanaji wa dawa kwa wakati na Halmashauri ya Msalala tulitenga milioni 30 kununua dawa na tulipoomba dawa kutoka MSD waliweza ku-supply dawa kiasi cha shilingi milioni 17 tu na wakakosa dawa na fedha zipo. Kwa maelezo ya Wizara ni kwamba, wanapokosa dawa kuna yule mshitiri ambaye amechaguliwa kwa ajili ya ku- supply dawa. Washitiri hawa wana-supply mkoa mzima na mikoa mingi; sasa Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inaanzisha washitiri hawa, hawa watu wanao- supply dawa kwenye kila wilaya ili kuondoa gharama kwanza za usafirishaji wa dawa, lakini pia kupatikana kwa dawa kwa wakati? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya baadhi ya wateja wa bima kukosa dawa kwenye baadhi ya vituo vyetu ni kweli imekuwepo, lakini kwa taarifa ambazo tumeendelea kuzifanyia kazi, kasi ya ukosefu wa dawa kwenye vituo vyetu imeendelea kupungua. Hata hivyo, maelekezo ya Serikali yaliyotolewa ni kwamba, lazima vituo vyetu vyote na hospitali zetu zote na zahanati ziwe na dawa za kutosha kwa angalau asilimia 95 ya dawa zote muhimu. Hivyo, wateja hao wa bima wataendelea kuboreshewa upatikanaji wa dawa katika vituo vyetu ili kuepusha na changamoto ya kukosa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wazo la kuwaunganisha na maduka ya binafsi; Serikali yenyewe tumeweka mkakati kwamba hatuna sababu ya kuweka kigezo cha kuongeza maduka binafsi wakati vituo vyetu vina uwezo na vinalazimika kuweza kuwa na dawa za kutosha. Kwa hiyo njia sahihi sisi ni kuimarisha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyetu badala ya kupeleka kwa maduka binafsi kwa sababu kwa kuimarisha dawa hizo katika vituo, hata wale ambao hawana bima pia watanufaika na utaratibu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili kuhusiana na changamoto za upatikanaji wa dawa za wakati na hasa kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD); ni kweli kumekuwa na changamoto hiyo na Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo wiki iliyopita kwamba MSD lazima wajipange kuhakikisha dawa zote zinapatikana kwa wakati na kuhakikisha kwamba vituo vyetu vinapata dawa kupitia MSD. Kwa hiyo suala hilo tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mshitiri, ni kweli tulikuwa na mshitiri mmoja katika mkoa, lakini tulishatoa maelekezo kwenye mikoa yote kuongeza idadi ya washitiri, kuwa na angalau washitiri wawili, lakini hatua ya kwenda washitiri ngazi ya halmashauri bado tunaona haitakuwa na tija sana. tukishakuwa na washitiri ngazi ya mkoa ambao wana-supply vizuri, uzoefu unatuonesha tutakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante; tatizo lililopo Mpanda ni sawa sawa na tatizo lililopo kwenye Wilaya ya Kahama, Halmashauri ya Msalala Jimbo la Msalala; barabara inayotoka Bulyanhulu kwenda Kahama; barabara hii imekuwa ni mbovu sana mwaka jana imetengewa shilingi bilioni 3...

SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, swali langu ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii inayotoka Bulyanhulu kwenda Kahama kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Mbunge wa Msalala kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Bulyanhulu – Segesi – Kahama ni sehemu tu ya barabara inayoanzia Geita – Bukoli
– Bulyanhulu – Segesi - Kahama na kama alivyosema barabara hii imetengewa fedha, lakini niliwahi kujibu kwenye jibu la msingi swali lililopita kwamba kuna mazungumzo ambayo wenzetu wa Barrick wameonesha utayari wa kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami na mazungumzo bado yanaendelea. Kama watakwama basi Serikali itachukua hatua ya kuijenga barabara hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mradi wa Maji wa Izuga ni mradi wa muda mrefu, na kwa kuwa fedha iliyobaki ili mradi ukamilike ni milioni 76 tu. Kwa kuwa Mkandarasi yuko tayari walau apewe milioni 15 ili mradi ule ukamilike. Sasa, upo tayari baada ya Bunge hili mimi na wewe tuongozane mpaka Wizarani kuhakikisha kwamba Mkandarasi analipwa walau hiyo milioni 15 wananchi wapate maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mkandarasi atalipwa, nami niko tayari kwenda naye site.
MHE. IDDI KASSIM IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara inayotoka Solwa kuja Moktolio – Bulige - Ngaya mpaka Kahama ni barabara iliyoko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi na inatakiwa ijengwe kwa muda mrefu sasa. Sasa swali langu ni lini fedha hizi zitatengwa ili barabara hii ianze ujenzi mara moja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara niliyoitaja ipo kwenye mpango na ipo kwenye Ilani, kwa hiyo, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili ijenge kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa kumekuwa na ucheleweshwaji mkubwa wa utoaji wa tax exemption kwa wakandarasi, sasa ni lini Wizara ya Ujenzi watakaa chini na Wizara ya Fedha ili waweke mfumo mzuri utakaorahisisha wakandarasi hawa kupewa tax exemption mapema ili waweze kujenga barabara mapema ikiwemo Barabara ya Bulyanhulu mpaka Kahama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na maboresho mengi ya kuhakikisha kwamba malipo ya wakandarasi yanalipwa haraka na sasa hivi TRA hata mikoani wana uwezo wa kuchakata na kuharakisha malipo ya hawa wakandarasi. Hata hivyo, bado Serikali inaendelea kuboresha ili kuona namna bora zaidi ya kukamilisha malipo haya ya wakandarasi kwa muda. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Naibu Waziri alifanya ziara jimboni Kata ya Jana na alipokuwa pale aliahidi ujenzi wa minara sita ambayo itajengwa Kata ya Mwakata, Kata ya Mwaluguru, Kata ya Chela, Kata ya Mega na Kata ya Runguya, Kijiji cha Nyangarata.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu ni lini utekelezaji huu utaanza?
Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika kata hizo tuliahidi na tayari zimeingizwa katika mpango wa utekelezaji wa miradi hiyo, na katika miradi ambayo inaongozwa na Mradi wa Tanzania Kidigitali ambao ni miradi 763 na katika minara hiyo 763 na maeneo ya Mheshimiwa Kassim Iddi yatakuwemo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aendelee kusubiri ilimradi tu mchakato wa utangazaji wa tender utakapokamilika, ujenzi wa minara utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, maswali yangu mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza: Mchakato wa ununuzi wa mabomba ambao ulikuwa unasimamiwa na Wizara na baadaye kurudishwa mkoani, sasa ni lini Serikali itaharakisha mchakato huo wa manunuzi ili wakazi wa Busangi waweze kutumia maji katika eneo hilo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili: Mkandarasi anayejenga mradi unaotoka Mangu – Ilogi bado ameendelea kuchelewesha malipo ya wafanyakazi: Ni lini Serikali itamhimiza mkandarasi huyo ili aweze kuwalipa watumishi wake fedha hizo?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji imeangalia namna ya kutatua tatizo la maji hasa maeneo ya vijijini. Tumeanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) na Bunge lako Tukufu tunalishukuru. Tunapoanzisha taasisi yoyote tunakuwa na mikakati. Tumeweka kwa ajili ya manunuzi wizarani, sasa yameshuka mikoani. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wizara yetu itaendelea kufanya marekebisho ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maji inafanyika kwa urahisi zaidi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, malipo ambayo mkandarasi amekuwa akichelewesha kulipa watumishi wanaofanya kazi, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa baadaye saa 7.00 Bunge litakuwa limeasitishwa, tukutane ili tuzungumze na Mkandarasi moja kwa moja kwa ajili ya malipo ya watumishi wake. Ahsante sana.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nataka kuuliza ni lini sasa Serikali itajenga daraja linalounganisha Halmashauri ya Msalala, Kijiji cha Namba Tisa na Halmashauri ya Nyang’hwale? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja ya kazi kubwa ambayo sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumekubaliana kuifanya sasa ni pamoja na kutambua madaraja korofi yote ambayo tunahitaji kuyahudumia sasa ili tuunganishe moja na eneo lingine. Kwa hiyo, hata hili daraja alilotaja Mheshimiwa Mbunge la kuunganisha Halmashauri ya Msalala na Halmashauri ya Nyang’hwale liko katika mpango wetu, hivyo, nimuondoe hofu katika hilo.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nilitaka kuuliza, kwa kuwa mchakato wa ujenzi wa barabara inayotoka Kakola kwenda Kahama umekalimika. Sasa ni lini na nini kimekwamisha Wizara kutangaza barabara hiyo ili ianze ujenzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge tumekutana naye sisi na Wizara lakini pia na watendaji wa TANROADS. Ni barabara ambayo kweli fedha imeshapatikana, taratibu zinaandaliwa ili kuitangaza barabara hiyo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo mwaka huu wa fedha itaanza kujengwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami barabara inayotoka Kahama - Geita? Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anipe majibu ya kweli, barabara hii imekuwa ni kero ya muda mrefu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kahama – Ilogi kwenda Geita ni barabara ambayo inauganisha mikoa miwili; Mkoa wa Shinyanga na Mkoa wa Geita kupitia kwenye Jimbo la Mheshimiwa Iddi ambao ni Jimbo la Msalala.

Mheshimiwa Spika, ni kweli hii ni barabara ya kiuchumi na Serikali tumefanya majadiliano na wenzetu wa Barrick, lakini imeonekana bado wanasitasita kuanza kujenga hii barabara.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii sasa Serikali itaichukua ili ione namna ya kuifanya na pengine katika bajeti tunayoendelea kuiendea pengine tutaona nini cha kufanya ili tuanze kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na ukosefu wa amani katika baadhi ya maeneo hasa katika Kata ya Ngaya na kata ya Buriye na kupelekea wananchi sasa kuweza ku-share na Mbunge wao ambaye ni mimi kujenga Kituo cha Polisi na sasa kimefikia kwenye hatua ya lenta. Sasa swali langu ni lini Mheshimiwa Waziri atafika kuja kuweka jiwe la msingi sambamba na kutenga fedha kuja kumalizia Kituo hicho cha Polisi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake kujitolea kujenga kituo hiki na kama ambavyo nilivyokuwa nimejibu jana kwa zile jitihada ambazo zimeanzishwa na wananchi, tumeshajitahidi kuziendeleza. Tuna mfuko wetu wa tozo na tozo, japokuwa hauwezi kukidhi maeneo yote, lakini tutajitahidi kuangalia tutakachoweza kufanya ili tuongeze jitihada hizo ambazo Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake wamezifikia. Nitakuwa tayari kwenda kuweka jiwe la msingi wakati wowote ambapo Mheshimiwa Mbunge mimi na yeye tutashauriana yaani muda muafaka wa kuweza kufanya kazi hiyo.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Msalala ni miongoni mwa Halmashauri ambazo hazina Vyuo Vikuu na tayari kupitia mapato ya ndani tumetenga fedha kiasi cha Shilingi Milioni 212 kuanza ujenzi wa Chuo cha VETA. Sasa ni Serikali itatuongezea fedha ili tuweze kumaliza chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali katika sera yetu tunahakikisha kwamba tunakwenda kuwa na Vyuo vya VETA katika kila Wilaya nchini, kwa kuanzia tulianza na Wilaya 29 na hivi sasa vyuo hivyo vinakwenda kumalizika pamoja na Mikoa Minne ambayo haikuwa na Vyuo vya VETA. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha ujao, mambo mengi sana kulingana na upatikanaji wa bajeti vyuo hivi tutakwenda kujenga kwenye maeneo ambayo bado ujenzi haujafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni lini sasa Serikali itaanzisha ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya katika Halmashauri ya Msalala?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Msalala ni Wilaya mpya kama ilivyo Wilaya nyingine, tumeanzisha mpango wa ujenzi wa Vituo vya Polisi kwenye maeneo mapya ambayo hayakuwahi kuwa nayo, ni matarajio yetu kulingana na upatikanaji wa fedha Wilaya ya Msalala pia itafikiwa muda siyo mrefu ujao. Nashukuru. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Msalala hasa Kata ya Ngaya na kata ya Isaka tayari wana eneo na tayari tumeshajenga vituo vya polisi viko kwenye hatua ya renta; sasa ni lini Serikali itatenga fedha ili ije imalizie vituo hivi viwili ili wananchi waweze kupata huduma hiyo haraka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi anazofanya za kuhamasisha wananchi wake kuchangia ujenzi wa vituo hivi ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Msalala. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri hali ya fedha itakavyoruhusu vituo hivi vya kata mbili ambavyo vimeshajengwa kiwango cha renta tutaviunga mkono kwa kumalizia baadhi ya vifaa vinavyopatikana madukani/viwandani sorry ili ujenzi wake uweze kukamilishwa, nakushukuru.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza niipongeze Serikali kwa kutenga fedha kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ukarabati wa majosho matano. Nilitaka kuuliza swali langu la kwanza, kama Serikali ilitenga fedha kukarabati majosho haya Matano;

Je, fedha zilizotengwa kwenda kukarabati majosho Kata ya Ngaya na Ntobo zilikwendwa wapi na kama zipo Wizarani, ni lini sasa fedha hizo zitakuja kukarabati majosho hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa tulipokea barua iliyotuonesha kwamba tutaletewa majosho Matano, na Mkeka uliotoka, kwa maana ya idadi ya majosho ya mwaka huu haijaonyesha Msalala kuwemo.

Je, ni lini sasa Wizara itatuletea majosho hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza; majosho mawili pesa zake hazifahamiki zilipo na kwa hivyo ninaomba nimueleze tu kwa mujibu wa utaratibu wa ujenzi wa majosho haya. Utaratibu wote wa manunuzi hufanywa na halmashauri ya wilaya. Baada ya kuwa wamekamilisha taratibu zote za manunuzi hutuletea Wizarani ambapo Katibu Mkuu wa Mifugo huenda kuziombea pesa zile Hazina. Ikiwa kama katika kata alizozitaja na hivyo vijiji alivyovitaja liko hilo tatizo, niko tayari mimi kumpa ushirikiano Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, kufanya uchunguzi kwa kutumia wataalam wetu ili tuweze kubaini wapi mkwamo huu ulikotokea na baadaye kuweza kuwanusuru wananchi wa pale Msalala.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni hili la kata alizozitaja ambazo zilikuwepo lakini sasa anaona katika mkeka huu wa mwaka huu hazipo. Naomba nimuhakikishie, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetenga pesa za kutosha na mpaka sasa tumeshapeleka kiasi cha shilingi bilioni 5.4. Naomba nimuhakikishie tena kwa mara nyingine Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi hivi vijiji vinavyohitaji na anavyosema vilikuwepo katika mkeka nivipate tena ili tuweze kufanya ufuatiliaji wa pamoja wa kuona wapi palikosewa tuparekebishe na hatimaye wananchi wale waweze kupata ile huduma ya josho na hatimaye kuhudumia mifugo ile. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa Serikali imetuletea mahindi kwenye vituo viwili kwa maana ya Segese na Isaka na kuacha kata zingine 16 ambazo ziko umbali mrefu kutoka kwenye kata zile.

Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni lini Serikali itawatuma NFRA kuja kuongeza idadi ya vituo kwenye kata ambazo ziko mbali na maeneo hayo husika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa chakula cha bei nafuu Halmashauri husika huwa wanatuambia eneo ambalo limeteuliwa, lakini kutokana na changamoto za wananchi wetu wanatoka maeneo ya mbali tumeishatoa maelekezo kwa NFRA kuhakikisha kwamba wanaongeza vituo zaidi ili wananchi wengi waweze kuhudumiwa kwa ukaribu. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba katika Jimbo la Msalala tutazingatia pia hiyo ili wananchi wake wasitembee umbali mrefu kufuata chakula hiki cha bei nafuu.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nilikuwa nataka kufahamu ni lini Serikali itaweza kusimamia malipo ya wahanga wa kesi ya mwaka 1994 katika kata ya Bulyanhlu?Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Madini, siku zote iko tayari kusikiliza kero za wadau wake wa sekta ya madini na kama malalamiko haya yakifikia Wizarani, sisi tutalifanyia kazi bila kusita.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kumuuliza Naibu Waziri kumekuwa na RL nyingi kwa maana ya leseni zilizoshikiliwa na Serikali katika Halmashauri ya Msalala Kata ya Ntobo. Sasa ni lini Serikali itaachia maeneo haya ili wachimbaji wadogo wadogo wa Jimbo la Msalala waweze kutumia haki yao ya msingi kuchimba katika maeneo yale?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote yaliyoshikiliwa na Serikali au maeneo yote ambayo yameshikiliwa na kampuni kubwa za utafiti wa madini ambayo anaomba au anadai ni lini watarudishiwa wananchi. Watarudishiwa wananchi pale ambapo utafiti utakamilika au sisi tumebaini kama Wizara kwamba watumiaji wake hawana mpango wa kuyatumia na hivyo tutaweza kukaa nao na kuyarejesha Serikalini tuweze kuwekea utaratibu wa kupewa wadau au wawekezaji ambao wako tayari kuwekeza.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria unaotoka Mangu kwenda Ilogi ni mradi uliochukuwa muda mrefu sana kutoka 2016. Mwaka 2021 niliuza swali la msingi juu ya mradi huo wa maji. Waziri akaniambia Juni mwaka 2021 mradi ule ungezinduliwa. Sasa ni lini Serikali itazindua mradi wa maji unaotoka Mangu mpaka Ilogi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Iddi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, miradi hii ya Ziwa Victoria tunaendelea kuitekeleza. Ipo katika hatua mbalimbali kwa kila eneo, lakini maji ya Ziwa Victoria yataendelea kutumika vizuri, kuhakikisha huduma ya maji safi na salama itapatikana.

Mheshimiwa Spika, ni hivi karibuni uendelezaji na utekelezaji wa mradi huu unaendelea kufanyiwa kazi.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, mradi wa Mhangu - Ilogi ni mradi uliochukua muda mrefu sana na mwaka jana niliuliza swali la msingi na Mheshimiwa Waziri alinipa majibu kwamba mwezi wa sita mwaka jana mradi ule ungezinduliwa. Sasa nataka kufahamu majibu ya ukweli ni lini sasa mradi huo wa Mhangu - Ilogi utakamilika?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukimwona mtu mzima analia ujue kuna jambo. (Makofi/Kicheko)

Nimwombe Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi cha maswali baada ya saa saba tukutane ofisini ili kuhakikisha kwamba hili jambo tunalikamilisha na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. IDDI KASSIM IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kumuuliza Naibu Waziri; Kata ya Mwanase, Mradi wa Maji wa Izuga umechukua muda mrefu sana. Sasa ni lini Serikali itapeleka fedha ya kuwalipa wakandarasi ili waweze kumaliza mradi huo wa maji wa Izuga?
MHE. NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kupeleka fedha; tayari wakandarasi wanaendelea kulipwa, hivyo ninaamini hata mkandarasi huyu naye yupo kwenye foleni ya kulipwa. Tayari Katibu Mkuu pamoja na timu nzima inayohusika inaendelea kufanyia kazi suala hili la malipo.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nasikitika kwa kupata majibu ambayo sio; niseme tu kwa lugha nyepesi kwamba siyo ya ukweli. Barabara haziwezi zikakosa wakandarasi.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kumekuwa na kucheleweshwa kwa mikataba hiyo juu ya kuwepo taratibu nyingi za manunuzi: Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kupunguza milolongo hiyo ya manunuzi ili mikataba hii iweze kusainiwa kwa wakati? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini sasa Serikali itaanzisha au itarudisha mfumo wa kila Halmashauri kuwa na Meneja wa TARURA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tu nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu za manunuzi kwenye kandarasi zozote tunazozifanya ni lazima zifuatwe. Nasi hatutaruhusu mtu yeyote kukiuka hizi taratibu za kimanunuzi. Kikubwa tu ni kwamba tunaendelea kuboresha mifumo ili kuhakikisha kwamba tenda zote zinazotangazwa ziweze kupatikana kwa muda ili kazi ambazo zimekusudiwa zifanyike kwa haraka. Kwa hiyo, tumekuwa tukiboresha na ndiyo maana sasa hivi watu wote wanaomba kupitia mfumo.

Mheshimiwa Spika, la pili, utaratibu uliopo sasa ni kwamba kila Halmashauri tumeweka Meneja wa TARURA ambaye anasimamia barabara katika eneo lake. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa spika, ahasante sana, kwa kuwa marudio ya upembuzi yakinifu wa barabara inayotoka Bulyanhulu kwenda Kahama umekamilika, vikao vya tathimini vimekamilika, vikao vya Kata zote vimekamilika, fedha zipo cash.

Ni lini sasa Wizara itaanza ujenzi wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Idd Kassim Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Bulyanhulu kwenda Kahama kama alivyosema nikweli usanifu ulishakamilika na fedha ipo sasa hivi kinachoandaliwa ni makabrasha tu kwa ajili ya kuanza kuitangaza hiyo barabara ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami ikiwa ni pamoja na kusaidiana na wenzetu wa Twiga kwa maana ya Barrick, ahsante.
MHE. IDD K. IDD: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Kwanza kabisa tunaipongeza Serikali kwa majibu mazuri haya na kwa kuwa mradi huu tayari umekamilika, sasa ni lini Wizara itatenga fedha ili kupeleka maji katika Kata ya Shabaka, Kata ya Kaboha, Kata ya Busolwa na Kata ya Mwingiro?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili la nyongeza; kwa kuwa Mradi huu wa Mangu – Ilogi umeshakamilika, je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kupeleka maji katika Kata ya Runguya na Kata ya Segese? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Idd kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa tunaendelea na mpango na bajeti wa mwaka huu unaokuja wa 2023/2024, maombi yake tutayaingiza katika bajeti hiyo ili wananchi wa maeneo husika waweze kufaidika na huduma bora ya maji. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nilitaka kufahamu ni lini sasa Serikali italeta watumishi wa afya katika Jimbo la Msalala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, watumishi wa afya kwenda Msalala naamini katika hizi ajira zilizotangazwa sasa ambazo Mheshimiwa Rais ametoa kibali cha kuweza kuajiri watumishi wa afya wa kutosha na Msalala vile vile nanyi mtapata watumishi wa afya.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Waziri mradi wa Nduku - Msangi – Ntobo ni mradi ambao umechukua muda mrefu sana, kwa hatua iliyofikiwa sasa wameweza kukosa kiasi cha Shilingi Milioni 50 tu kwa ajili ya Mkandarasi kuchimba mtaro, kuchelewa kwa mradi huu kumesababisha sasa Hospitalli ya Wilaya ya Ntobo kukosa maji na hivyo kupelekea mlipuko wa magonjwa mbalimbali kwenye hospitali ile ya Wilaya.

Je, ni lini sasa Wizara itatoa kiasi hiki kwa dharura ili ipeleke fedha hizo hospitali ya Wilaya iweze kupatiwa maji?

Swali langu la pili, Kata niliyoitaja hapa kwa maana ya Mwakata imepitiwa na bomba kuu linalotoka Kagongo kwenda Isaka na Kata hii haina maji. Je, ni nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba Kata hii na yenyewe inanufaika na maji hayo kwa sababu bomba hilo limepita maeneo hayo? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Kaka yangu wa Msalala kwamba Wizara ya Maji mwezi huu tumepokea Bilioni 67 kwa ajili ya malipo ya Wakandarasi. Kwa hiyo, moja ya maeneo ambayo tutayapa kipaumbele cha haraka ni eneo la Msalala kuhakikisha mradi huu unakamilika na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni juu ya mradi ambapo bomba kuu linapita. Sera inasema bomba kuu linapopita vijiji ambavyo vipo karibu na kilomita 12 kulia na kushoto mwa bomba kuu, vinahakikishiwa kwamba vinapata huduma. Nataka nimhakikishie hili tumelipokea na tunaenda kulifanya kazi kuhakikisha kwamba Kata hiyo nayo inapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano kwenye Kata ya Jana, Mwalugulu, Kashishi, Chela na maeneo mengine je, ni lini sasa Serikali itaanza rasmi ujenzi wa minara hii katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshmiwa Naibu Spika, kwa Kata ya Jana tayari tumepata mtoa huduma Vodacom, Kata ya Mwalugulu tumepa mtoa huduma tigo na kata zingine na uhakika kwamba Mheshimiwa Mbunge akishatoka hapa tutawasiliana ili ajue watoa huduma gani wanaenda kutoa huduma katika maeneo hayo.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya vivuko ambavyo vinasababisha mkwamo wa kutoka kitongoji kimoja kwenda kingine. Kuna changamoto kubwa sana kutoka Kijiji cha Itogwamolo kwenda Kijiji cha Bandari, lakini hivyo hivyo kutoka kitongoji cha Shilabela kwenda Isaka Stesheni na hivyo hivyo kutoka kwenye Kata ya Isaka kwenda ya Jana. Sasa swali langu la kwanza; ni lini Serikali itaweza kutenga fedha ili iweze kujenga vivuko vitakavyowawezesha wananchi kufika kwenye maeneo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa katika eneo la Isaka hasa kwenye suala la bandari.

Je, ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakuja kwenye Kata ya Isaka ili aweze kufanya mkutano wa hadhara awasikilize wananchi wa Isaka kero kubwa ambayo inayozuka katika maeneo haya ya bandari, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa karibu sana masuala ya kivuko katika eneo hili. Serikali itaanza ujenzi katika vijiji hivyo alivyovitamka vyote, hususan katika Kijiji cha Isaka na Isakajana, Isaka Stesheni na Kitongoji cha Shilabela na Kijiji cha Itogwa hadi Kijiji cha Bandari. Tutaanza ujenzi wa kuunganisha vijiji hivi tarehe 27 ya mwezi huu wa tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwenda kukagua, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na yeye, mara baada ya kuanza ujenzi tutaenda kukagua eneo hili pamoja na eneo la Stesheni ya Kisaka, ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Wilaya ya Kahama haijanufaika na mradi wa BBT; na kwa kuwa Halmashauri ya Msalala sasa tuko tayari kupokea mradi huu kwa vijana wetu: Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri utafika katika Halmashauri ya Msalala ili tuweze kuanzisha mradi huu? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Iddi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza Wizara iko tayari kushirikiana na Halmashauri yoyote katika nchi yetu ambayo iko tayari kutenga eneo la kilimo kwa ajili ya mfumo wa block farm na kwa ajili ya mfumo wa BBT. Mfano mzuri ni Halmashauri ya Makete ambao wameamua kutenga ten percent yao kuwakopesha vijana, na sisi Wizara tukawapatia pembejeo kwa maana ya mbegu za bure kwa ajili ya kilimo cha ngano. Kwa hiyo, nihamasishe Waheshimiwa Wabunge ninyi ni wajumbe wa Baraza la Madiwani, ni wajumbe wa Kamati za Fedha tengeni maeneo na kuwa tayari kutenga sehemu ya asilimia kumi za Halmashauri kuwasaidia vijana katika maeneo yenu, na Wizara tuko tayari kuja ku-support initiatives za namna hiyo. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nataka kufahamu ni upi sasa mkakati wa Serikali wa kutenga fedha kuweza kwenda kurekebisha shule chakavu kwenye Halmashauri ya Msalala, ikiwemo Shule ya Msingi Isaka, Kata ya Isaka, Shule ya Msingi Kilimbu, Kata ya Mwaruguru na Shule ya Msingi Butegwa, Kata ya Ngaya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hizi za kule Jimbo la Msalala alizozitaja Mheshimiwa Iddi Kassim zitakarabatiwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Tayari Halmashauri ya Msalala pia imepokea fedha ya kukarabati shule kongwe na chakavu na kujenga shule nyingine kutokana na Mradi wa BOOST ambao fedha zimekwenda. Ni zaidi ya bilioni 230 ambayo Serikali hii ya Awamu ya Sita imetoa kwa kila halmashauri hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kuwaelekeza Wakurugenzi wote wa Halmashauri Nchini, kuhakikisha wanatenga fedha na kuanza ukarabati wa shule chakavu katika maeneo yao ya halmashauri zao kwa sababu, tayari Serikali hii imeshasaidia sana katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali kwa kutafuta fedha kutoka Serikali Kuu na wao sasa waanze kutenga kutoka kwenye mapato yao ya ndani.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kiwango cha lami barabara inayotoka Kahama – Busangi – Chela – Nyang’wale mpaka Busisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja tunakamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa maana ya kutoka Kahama kwenda Busisi. Pia, baada ya hapo ndiyo tutaanza kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wilaya ya Kahama ina Halmashauri tatu na hivyo kusababisha changamoto ya kupata huduma kwa wakati. Lini sasa Serikali inampango wa kuanzisha Mkoa wa ki-TANESCO katika wilaya ya Kahama ili isaidie kutoa huduma kwenye maeneo yale? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kweli Wilaya ya Kahama inazo Halmashauri tatu na sisi tunayo Ofisi ya Kiwilaya ya TANESCO kama zilivyokuwa ofisi nyingine za Serikali na tunachokifanya ni kuendelea kupeleka huduma kwa wananchi kwa kufungua ofisi ndogo au viunga kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, jambo la kufungua Ofisi ya Kimkoa ya Ki-TANESCO tunaendelea kulitizama kwa sababu zinazo viwango na grade mbalimbali na zitakapokuwa zimekamilika tutakamilisha jambo hilo kwa ajili ya huduma kwa wananchi.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Je, Serikali haioni haja ya kupeleka Ofisi za NIDA kwenye kila Halmashauri badala ya kwenye kila Wilaya ili kusiogeza huduma za wananchi hususani katika Halmashauri ya Msalala?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba inaweza ikaonekana umuhimu wa kuzipeleka ofisi hizi kwenye ngazi ya Halmashauri, lakini shughuli za NIDA ziko sehemu ya Serikali Kuu, na kama sehemu ya Serikali Kuu iko chini ya Mkuu wa Wilaya, ndiyo maana tumeanzia pale. Pale ambapo kutakuwa na haja, kwa mfano Wilaya yenye majimbo zaidi ya moja, tutaona uwezekano wa kuimarisha huduma hizo kwenye majimbo ya mbali na makao makuu ya wilaya, ili wananchi hawa waweze kupata hizo huduma stahiki.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Halmashauri ya Msalala tumekamirisha ujenzi wa vituo vya afya viwili na zahanati 24: Nini mkakati wa dharura wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanapeleka vifaa tiba ili zahanati hizi na vituo vya afya vianze kufanya kazi haraka iwezekanavyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi na Mheshimiwa Mbunge, tumetembelea vituo hivyo na nimeona kweli kuna tatizo hilo. Namwomba Mheshimiwa Mbunge aje tukae pamoja, tumpigie DMO wake ili aweze kutuma list ya vifaa ambavyo tulikuwa tumeona havipo tupeleke MSD ili aweze kupata vifaa. (Makofi)
MHE. IDD K. IDD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa Halmashauri ya Msalala imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa mnada wa Kata ya Burige, sasa ni lini Serikali italeta fedha kukamilisha ujenzi wa miundombinu katika mnada huo wa Burige?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwanza tuipongeze Halmashauri ya Msalala kwa kutenga fedha kwa ajili ya uzio wa mnada ambao Mheshimiwa Mbunge ameuainisha. Serikali tulishaweka commitment yetu kwa ajili ya kumalizia mnada huo, commitment yetu iko pale pale isipokuwa kwa sasa hivi tunaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha mnada huo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Serikali imeweka utaratibu wa kutangaza ajira ambazo zinatoka TAMISEMI na hivyo kukadiria watumishi kupelekwa TARURA: Kwa nini sasa Serikali isiruhusu TARURA wenyewe waweze kuajiri wakandarasi au wahandisi?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Kwa kuwa, Jimbo la Msalala liko katika mazingira magumu sana kwenye maeneo hayo kwa maana ardhi yake ni mbuga: Sasa Serikali haioni haja ya kuongeza bajeti ili iendane na uhalisia wa maeneo hayo kwenye Jimbo la Msalala? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Iddi Kassim, la kwanza hili la kwa nini TARURA wasipewe vibali vya kuajiri wenyewe, ni kwamba ajira katika utumishi wa umma hutolewa kulingana na ukomo wa bajeti ambayo imepitishwa na Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. TARURA wenyewe wanaomba vibali kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Utumishi na tutaendelea kutoa kipaumbele ajira za ma-engineer kwenye taasisi hii ya TARURA kadiri ya fedha ambavyo inapatikana na bajeti ya Serikali inaruhusu.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la mgawanyo wa fedha, hasa kule Msalala kwa sababu ya mazingira magumu, kwa sasa tayari kuna review inayofanyika chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki, kuangalia ni namna gani mgawanyo wa fedha unakwenda katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo kule Msalala. Naomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira na muda siyo mrefu timu hii itawasilisha taarifa yake mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na baada ya timu hiyo kuwasilisha taarifa hiyo, tutaangalia upya formula inayotumika kwa ajili ya kupeleka fedha maeneo mbalimbali nchini.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa tayari Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Nduku Busangi Ntobo na mradi wa Mwarugulu tayari amesha supply vifaa na hajalipwa fedha. Kufanya hivyo, umesababisha mradi kusimama. Ni lini sasa Wizara itaenda kumlipa fedha mkandarasi ili aweze kutekeleza miradi hiyo miwili ya Mwarugulu na mradi wa Busangi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii yote uliyoitaja ni kweli utekelezaji unaendelea na ulipwaji wa madeni kwa wakandarasi tayari tumeanza kama Wizara. Fedha tunavyozipata tunaendelea kupunguza madeni na kuhakikisha wakandarasi wote walipwe ili waweze kuendelea na miradi hii.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Msalala, Halmashauri ya Msalala ina Kituo cha Wilaya na haina gari la Polisi. Kama unavyofahamu kwenye maeneo yetu ya uchimbaji usalama ni hatari sana ukizingatia kwamba kwa sasa kumeanza kuibuka makundi mbalimbali. Sasa ni lini Serikali itachukua hatua za dharura wakati ikisubiria mpango wa kuleta magari yale mengine, ichukue hatua ya dharura ili kuhakikisha kwamba wanatupatia gari la Polisi tuweze kukabiliana na uhalifu katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua ni kweli kwamba maeneo ya migodi ni maeneo yanayovutia pia matendo ya uhalifu. Kwa hiyo tutakaa na Mheshimiwa Mbunge ili tukae na RPC wa Mkoa wa Shinyanga kuona kama pana magari ya ziada basi sehemu ya magari yale yahamishiwe kwenye Wilaya hii ya Kahama ili kuimarisha usafiri kwenye eneo hilo. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante; Wilaya ya Kahama ina Halmashauri tatu ambapo kila Halmashauri mmeanzisha vituo vya Wilaya lakini vituo hivyo vya wilaya havina vituo vya polisi.

Sasa nataka kufahamu ni lini Serikali itaanzisha ujenzi wa kituo cha polisi nakwakuzingatia kwamba mimi Mbunge wao nipo tayari sasa kutoa tofali 4000 ili tuanze ujenzi huo haraka iwezekanavyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim, Mbunge wa Kahama kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tumpongeze kwa juhudi zake za kusaidia sekta ya usalama wa raia na mali zao kwa kuchangia idadi hii ya 4,000 ya matofali lakini mpango wetu ni kujenga vituo vya polisi vya Wilaya zile halmashauri ni kuimarisha tu kwa kuweka vituo vingine kwa hivyo kipaumbele kitakuwa kujenga kituo kikuu cha Wilaya ya Kahama na zile Halmashauri zitaendelea kuwekewa vituo visaidizi kwa ngazi ya tarafa na kata kama ambavyo sera yetu ya usalama wa raia inavyoelekeza. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, tatizo lililoko Tarime Mjini ni sawasawa na tatizo lililoko kwenye Halmashauri ya Msalala. Kwa kuwa Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kupeleka umeme kwenye makao makuu ya vijiji na hivyo kupelekea baadhi ya mitaa kukosa huduma ya umeme. Ni lini Serikali itaanza umeme kwenye mitaa ya Kata ya Bulyamuru, Segese, Isaka na Burige?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema kwenye jibu la msingi mitaa yote ambayo haijafikiwa na umeme katika mwaka wa fedha unaokuja, tunayo program yetu ya Densification 2B na 2C itahakikisha inafikisha umeme katika maeneo hayo kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba sijaridhika na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwa sababu hata maeneo ambayo ameyataja hapa kwamba yamejengewa ofisi kwa mfano mimi kwenye Jimbo langu hakuna kata inayoitwa Bulungwa wala Chambo.

Sasa Mheshimiwa Waziri niseme kwamba ni lini sasa mtaanzisha ofisi hizo ambazo wewe umezitaja hapa ikiwemo Kata ya Isaka, Kata ya Segese, Kata ya Bulige na Kata ya Jana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la nyongeza wakati mnaendelea kufanya upembuzi yakinifu au tathmini, Mheshimiwa Waziri alifanya ziara kwenye Halmashauri ya Msalala na tukampatia kiwanja na tofali 1000 na akaahidi kujenga ofisi kwenye Halmashauri ya Msalala.

Sasa ni lini Serikali mtaanza ujenzi wa ofisi ya Wilaya kwenye Halmashauri ya Msalala? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la pili la ni lini Serikali itaanza kujenga ofisi; kama tulivyoeleza kwenye jibu la msingi TANESCO inaendelea na tathmini mahitaji ya vigezo kwa ajili ya kufungua ofisi hiyo, kwa hiyo tathmini itakapokamilika mara moja mahitaji yakabainika ni kwa kiasi gani basi itaamuliwa ijengwe hiyo ofisi kwa mazingira yatakayo kuwepo.

Mheshimiwa Spika, lakini kweli swali la kwanza kwamba ofisi hazijafunguliwa; kwa sababu ya uhaba wa watumishi tuliokuwa nao na kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ya kujenga majengo yetu katika maeneo yote wenzetu wa TANESCO walianzisha utaratibu wa kufanya visiting offices ambazo ni katika haya maeneo ya hizo ofisi ndogo tukiazima maeneo ya ofisi za kata. Kwa hiyo, maeneo haya hautaenda na kukuta jengo limejengwa lakini tunapata vyumba kwenye ofisi za watendaji wa Kata na tunaanza kuhudumia watu kutokea kwenye maeneo hayo, wakati Serikali ikiwa inajihimu kuongeza bajeti kwa ajili ya kuweza kujenga majengo hayo kwenye maeneo yote yanayohitajika. (Makofi)
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililoko Manyara ni sawasawa na Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama. Kwa kuwa Kata ya Isaka kumekuwa na ongezeko la wageni mbalimbali na ukizingatia uwepo wa bandari na uendelezaji wa ujenzi wa bandari mpya, hivyo kuongeza idadi ya watu katika Kata ya Isaka. Sasa Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kituo cha uhamiaji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua uwepo wa muingiliano mkubwa wa wananchi pamoja na wageni kwenye eneo lake hasa kutokana na shughuli kubwa za kiuchumi za uchimbaji wa madini na kwa mtaji huo ni halali Wilaya yake kupata ofisi ya uhamiaji. Na sera ya Wizara ni kuhakikisha kwamba kila ilipo wilaya siyo halmashauri na pale Wilaya ya Kahama ipo ofisi yetu ya Uhamiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba watu wote wanaokwenda Msalala waendelee kutumia huduma zinazotolewa katika ofisi ya wilaya ambayo iko pale Kahama. Lakini patakapotokea umuhimu wa kupanua zile huduma kuzipeleka kule, tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kupata majengo kule ili yaweze kutumika kutoka huduma hiyo. Nashukuru.
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; barabara inayotoka Ntobo - Busangi mpaka Didia kwa muda mrefu imekuwa haina matengenezo. Sasa nilitaka kufahamu ni lini Serikali itaweza kuweka matengenezo ya kudumu kwenye barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Kassim, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja imetengewa fedha kwa mwaka wa fedha unaokuja kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo kwa mwaka huo unaokuja. Kwa hiyo, nina hakika katika mwaka unaokuja barabara hiyo itatengenezwa na tutahakikisha kwamba pengine yale maeneo yote ambayo hayapitiki ndio yanayopewa kipaumbele katika matengenezo hayo. Ahsante.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana matumizi ya zebaki kwenye maeneo yetu wachimbaji wadogo wadogo hasa Jimbo la Msalala yamekuwa na athari kwa wachimbaji wenyewe, lakini pia kwenye mazingira yanayozunguka pale. Sasa kabla Serikali haijaenda kuzuia matumizi ya zebaki ni teknolojia ipi ambayo mmeianzisha kama mbadala wa matumizi ya zebaki?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kuna teknolojia mbadala ambayo inaendelea kutumika katika uchenjuaji wa madini ya dhahabu na teknolojia hiyo inaitwa ni cyanide na matumizi ya cyanide ni aina ya utaalam ambao ile kemikali yenyewe inapokuwa imetumika kuchenjua na kukamatwa kwenye mabwawa ya kuchenjulia madini huyeyuka na kupotea hewani bila kuacha madhara yoyote na hiyo ndiyo teknolojia ya kisasa ambayo tunaendelea kutumia na kuendelea kuitambulisha kwa wachimbaji wadogo.