Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Iddi Kassim Iddi (13 total)

MHE. IDD K. IDDI aliuliza:-

Je, nili ni Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Geita – Bukoli hadi Kahama kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasimu Iddi Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na maandalizi ya makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Geita – Bukoli hadi Kahama yenye urefu wa kilomita 139 inayounganisha mikoa ya Geita na Shinyanga.

Mheshimiwa Spika, kazi hii ilifanywa na Mhandisi Mshauri ENV Consult (T) Ltd kwa gharama ya Shilingi milioni
440. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Aidha, Kampuni ya Uchimbaji Madini BARRICK imeonyesha nia ya kufadhili ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya Kahama – Bulyanhkulu – Geita yenye urefu wa kilometa 120.2. Kwa sasa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Wizara ya Madini zinaendelea na mazungumzo na Kampuni ya BARRICK Kuhusu utaratibu wa ujenzi wa barabara hii.

Mheshimiwa Spika, wakati ujenzi wa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha Wizara yangu inaendelea kuihudumia barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika mwaka wa fedha huu wa 2020/2021, jumla ya shilingi milioni 872.966 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hiyo.

Aidha, ninapenda kulifahamisha Bunge lako tukufuku kuwa ili ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ufanyike, hatua mbalimbali hufuatwa ambazo ni pamoja na upembuzi yakinifu, usanifu wa kina. Utayarishaji wa Nyaraka za zabuni na taratibu za ununuzi za kumpata mkandarasi wa ujenzi. Hivyo, kukamilika kwa hatua tajwa, maana yake nikuanza kwa mradi husika. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kusambaza maji kutoka Mradi wa Maji Mhangu – Ilogi katika Kata za Lunguya, Ikinda, Shilela, Sogese na Mega katika Halmashauri ya Msalala?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Msalala, Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imeendelea na utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Mhangu – Ilogi awamu ya kwanza ambayo ilihusisha ujenzi wa bomba kuu kutoka Mhangu hadi Ilogi umbali wa kilometa 56 kwa gharama ya shilingi bilioni 13.86 na kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi huu kwa awamu ya pili ambayo itahusisha usanifu wa miundombinu ya usambazaji maji na ujenzi wa miundombinu hiyo katika kata zote tano ambapo mradi unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka 2022.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -

Je, lini Serikali sasa itaipandisha Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kuwa Wilaya kamili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassim Iddi Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kuanzisha Mkoa na Wilaya mpya umebainishwa kupitia Sheria ya Uanzishwaji wa Mikoa na Wilaya. Kwa mujibu wa Sheria hii, utaratibu wa kuanzisha Wilaya mpya huanzia kwenye Serikali za Vijiji/Mitaa ili kupata ridhaa ya wananchi kisha hupelekwa kwenye Mabaraza ya Madiwani ya Halmashauri, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC). Baada ya hatua hiyo, maombi hayo huwasilishwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa ajili ya uhakiki na kujiridhisha na baadaye kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili akiridhia atoe kibali cha kuanzishwa kwa Wilaya husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala iko katika Wilaya ya Kahama ambayo ni moja kati ya Wilaya tano zinazounda Mkoa wa Shinyanga. Halmashauri ya Wilaya ya Msalala bado haijaanza mchakato wa kuomba kuwa Wilaya kwa kadri ya matakwa ya sheria.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa vifaa tiba na dawa za kutosha kwenye vituo vya afya na zahanati zote katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaatiba, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali ilitenga shilingi bilioni 11.3 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaatiba ambapo Halmashauri ya Msalala imetengewa shilingi milioni 376 kati ya fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022, imetenga bajeti ya dawa na vifaatiba kiasi cha shilingi bilioni 1.5 ambapo hadi kufikia Desemba, 2021 kiasi cha shilingi milioni 403.2, sawa na asilimia 38.1 kimetolewa.

Aidha, Kituo cha Afya Isaka na Mwalugulu vimetengewa vifaa vya jumla ya shilingi milioni 600 na Zahanati za Matinje, Mwakima na Kabondo zimetengewa jumla ya shilingi milioni 150 kwa ajili ya vifaa na vifaatiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Serikali Kuu, halmashauri zimeelekezwa kuimarisha na kudhibiti makusanyo ya fedha za uchangiaji wa huduma za afya ili kuhakikisha vifaatiba na dawa vinapatikana ipasavyo. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -

Je, ni lini Miradi ya maji Halmashauri ya Msalala itaanza kutekelezwa baada ya Serikali kutenga Shilingi bilioni 4.8 kwa ajili ya miradi hiyo?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri ya Msalala. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya miradi mitano ilikamilika. Katika mwaka 2022/2023, Serikali inaendelea na ujenzi wa miradi 12 ambapo miradi miwili imekamilika na miradi 10 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, aidha, utekelezaji wa mradi wa maji wa Mhangu – Ilogi awamu ya kwanza umekamilika na tayari unatoa huduma katika Kijiji cha Ilogi. Utekelezaji wa awamu ya pili unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba, 2022. Mradi huu ukikamilika utakuwa na bomba lenye urefu wa kilomita 37.5, matenki manne yenye jumla ya ujazo wa lita 440,000 na vituo 32 na kunufaisha wananchi wapatao 24,436.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga majosho ya kuogesha mifugo katika Halmashauri ya Msalala?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, (Mb), kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali ilifanya ukarabati wa majosho matano (5) katika kata za Burige, Lunguya, Mega, Ntobo na Ngaya zilizoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala. Aidha, Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majosho katika halmashauri mbalimbali nchini; ikiwemo Halmashauri ya Msalala. Pia Serikali inaendelea kuhamasisha wafugaji kuchangia ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo ujenzi wa majosho. Ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -

Je, Serikali inaichukulia hatua gani TARURA Msalala kwa kuchelewesha mikataba na kuwapa kazi wakandarasi wasio na uwezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, jumla ya mikataba 11 inatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala yenye jumla ya Shilingi bilioni 2.66. Kati ya Mikataba hiyo 11 Mikataba minane ilisainiwa mwezi Agosti, 2021 na Novemba, 2021 ambayo yote inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2022.

Mheshimiwa Spika, mikataba mitatu haikufikia hatua ya kusainiwa kutokana na kutopatikana kwa Makandarasi kwa wakati baada ya kushindwa kukidhi vigezo vilivyowekwa kwenye zabuni. Hivyo, Mikataba hiyo mitatu imesainiwa mwezi Februari na Machi, 2022 baada ya kuwapata Makandarasi waliopata zabuni.

Mheshimiwa Spika, kutokana maelezo hayo, Makandarasi wanaotekeleza mikataba minane imesainiwa kwa wakati kwa mujibu wa taratibu za ununuzi na mikataba mitatu ilichelewa kusainiwa kutokana na kushindwa kupatikana Makandarasi na zabuni kutangazwa upya.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Kata za Ikunda, Mwakata, Menga, Shilela na Lunguya - Msalala?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa upanuzi wa miradi ya maji ya Mhangu - Ilogi na Nduku - Busangi itakayohudumia Kata za Ikunda, Mwakata, Menga, Shilela na Lunguya zilizopo Wilayani Msalala. Kwa sasa taratibu za kumpata Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi zinaendelea na ujenzi utaanza katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga vivuko ili kuweza kupita magari, pikipiki na baiskeli katika Reli ya Bandari Isaka - Msalala?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kuimarisha usalama katika maeneo yote ya makutano ya reli na barabara kuu kwa kujenga madaraja au kuweka mageti ya kisasa yanayojifungua na kujifunga yenyewe ili kuzuia watumiaji wa barabara kupita pale treni inapopita kwenye makutano.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuweka mageti hayo katika makutano yote ya reli na barabara yaliyopo kwenye barabara kuu yakiwemo makutano ya Isaka. Kwa sasa Serikali imeweka walinzi eneo hilo kwa saa 24 ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara hiyo, ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:-

Je, lini Sheria italetwa kupunguza michakato ya utangazaji wa Miradi ya TARURA na fedha kusimamiwa na Mameneja wa Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kassim Iddi Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ununuzi wa Umma imetungwa ili kuweka uwiano mzuri wa haki na ushindani katika Ununuzi wa Umma na hutumika kwa Taasisi zote za Serikali na siyo TARURA pekee. Kwa mujibu wa muundo wa TARURA, fedha zote za miradi na utekelezaji wake umekasimiwa kwa Mameneja wa Wilaya. Malipo yote huandaliwa na Meneja wa Wilaya na kutumwa kwa Meneja wa Mkoa kwa ajili ya uidhinishwaji na ulipwaji kupitia mfumo wa Malipo Serikalini (MUSE). Aidha, Ofisi ya Mkoa kwa kushirikiana na Ofisi ya Meneja wa Wilaya, itaendelea kufanya tathmini kuhakikisha miradi inafanyika kwa kuzingatia thamani ya fedha ili iweze kukidhi uhitaji wake.
MHE. MIRAJI J. MTATURU K.n.y. MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga mitaro ya kuchepushia maji katika Kata za Bulyanhulu, Segese, Ngaya na Bulige?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Idd Kassim Idd, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kata za Bulyanhulu na Segese zinapitiwa na Barabara ya Kahama hadi Kakola ambayo ipo kwenye mpango wa kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2023/2024. Taratibu za manunuzi kwa ajili ya ujenzi zinaendelea na ujenzi wa mitaro utafanyika wakati wa utekelezaji wa mradi huo. Aidha, Mji Mdogo wa Bulige unapitiwa na Barabara ya Kahama – Solwa ambapo ujenzi kwa kiwango cha lami unaendelea na utahusisha ujenzi wa mitaro. Vilevile, mitaro iliyopo katika Kata ya Ngaya inakidhi mahitaji ya barabara hiyo na itaendelea kufanyiwa matengenezo, ahsante.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanzisha Mkoa wa TANESCO katika Wilaya ya Kahama na kujenga Ofisi ya TANESCO Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, TANESCO imekuwa ikifungua Ofisi za Mikoa na Wilaya katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuzingatia mahitaji na vigezo muhimu ikiwa ni pamoja na Wilaya, ongezeko la wateja, ukubwa wa mtandao na miundombinu ya umeme katika maeneo husika. Katika Halmashauri ya Mji wa Kahama ipo Ofisi ya TANESCO ya Wilaya ya Kahama inayotoa huduma kwa wananchi wa Mji wa Kahama pamoja na Halmashauri za Msalala na Ushetu.

Mheshimiwa Spika, katika hatua ya kusogeza huduma zaidi kwa wananchi, TANESCO imefungua Ofisi ndogo yaani Sub Offices katika maeneo ya Nyamilangano, Ilogi na Isaka. TANESCO inaendelea kuongeza Ofisi ndogo nyingine katika maeneo ya Segese, Bulungwa, Bulige na Chambo pamoja na kuongeza watumishi, magari na majengo. TANESCO inaendelea na tathmini ya mahitaji na vigezo kwa ajili ya kufungua Ofisi ngazi ya Mkoa katika Mji wa Kahama.
MHE. IDDI K. IDDI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga minara ya simu katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala?
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, Mbunge wa Jimbo la Msalala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imepata mtoa huduma wa kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata ya Ntobo yalipo Makao Makuu ya Halmashauri ya Msalala. Kampuni ya Simu ya Vodacom ndiyo ilishinda zabuni ya kujenga mnara huo kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Vodacom inaendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji wa ujenzi wa mnara huo.