Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Iddi Kassim Iddi (13 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na afya iliyo bora, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii leo ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu nianze kwa kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Msalala kwa kunipatia imani kubwa hii ya kuweza kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunajadili hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, niseme sisi kama Wanajimbo la Msalala, hotuba hii imeleta mapinduzi makubwa sana katika Jimbo langu la Msalala. Niliarifu Bunge lako Tukufu hili kwenye ukurasa wa 37, lakini pia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais ya 2020, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika Jimbo la Msalala ameweza kutupatia miradi mikubwa kabisa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ametupatia mradi mkubwa wenye zaidi ya bilioni 13 ambao ni mradi wa maji unaotoka Magu kuja Ilogi. Hata hivyo, hajaishia hapo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ametupatia mradi mkubwa kabisa wa maji unaotoka Kagongwa kwenda Isaka unaogharimu kiasi cha bilioni 23. Pia hajaishia hapo, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameweza kutupatia mradi mwingine wa maji ambao unatoka Nduku Mtobo kwenda Busangi, ambao unagharimu kiasi cha shilingi bilioni nne nani kama Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tumeona azma yake ya kuunganisha mikoa kwa mikoa, wilaya kwa wilaya. Katika Jimbo langu la Msalala, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameweza kutupatia barabara mbili zenye kiwango cha Lami, barabara hizi ni barabara inayotoka Solwa kuja kupita Kata ya Ngaya na Kata ya Bulinge kuja Kahama lakini pia ametupatia barabara nyingine inayotoka Bulyanhulu kuja Segese mpaka Kahama. Naiomba Wizara ya Ujenzi iweze kuona namna gani inaweza kuanza utekelezaji wa barabara hizi mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala nzima la afya, niseme tu mbele yako Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa sisi Wanabulyanhulu alianza kupambana juu ya kupitia mikataba upya ya madini na mikataba hiyo sisi kama Wanamsalala tumeweza kunufaika pakubwa sana na mikataba hii. Leo hii ninapozungumza tunapokea fedha za CSR. Nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Doto Biteko, Waziri wa Madini aweze kufanya ziara na kuona namna gani sasa Wanamsalala tunaweza kunufaika na fedha hizi za CSR.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ucheleweshwaji wa miradi mbalimbali inayopangwa kwa ajili ya kutekelezwa na watu hawa wa mgodi zinazotolewa na fedha za CSR. Nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Doto aweze kufika katika Jimbo langu la Msalala ili tuweze kufanya kikao na watu hawa tuone namna gani wanaweza kutekeleza miradi hii ya CSR ili iweze kuleta tija kwa wananchi wa Jimbo la Msalala.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli imeweza kutufanya Jimbo la Msalala kuhama kutoka uchumi wa chini na kuhamia uchumi wa kati. Ninavyozungumza hapa tuna vituo vinne vya afya katika Jimbo langu la Msalala, lakini pia tunaenda kujenga kituo kingine kwa fedha zetu za ndani za jimbo, tunaenda kujenga kituo cha afya katika Kata ya Isaka. Niiombe TAMISEMI na Waziri Mheshimiwa Jafo, kaka yangu aweze kutusaidia kutupatia vifaa tiba ili kituo cha afya kinachokamilika kiweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu sio hilo tu, lakini tumekuwa na uhaba wa watumishi katika sekta ya afya katika Jimbo la Msalala; nimwombe Mheshimiwa Jafo aweze kutuangalia kwa jicho la huruma Wanamsalala, tuna uhaba wa Walimu pia, naomba ndugu yangu atusaidie katika suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu juu ya kauli yake ya kuhakikisha kwamba tunaenda kuongeza madarasa katika nchi nzima. Katika Jimbo langu la Msalala napenda nimhakikishie Mheshimiwa Waziri Mkuu tulilipokea wazo lake hilo na maagizo yake hayo kwa kutekeleza ujenzi wa madarasa na tumeweza kuongeza madarasa katika kila kata mawili. nami kama Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie Mheshimiwa Waziri Mkuu nilitoa lori la cement kuhakikisha kwamba naunga juhudi za ujenzi wa madarasa hayo. Kwa sasa tunavyozungumza tuko katika hatua nzuri na baadhi ya shule tayari madarasa hayo yameanza kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la ajira..

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda umeisha Mheshimiwa.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia fursa hii ili kuchangia leo Mpango wa Tatu. Kwanza kabisa nianze kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Msalala. Lakini pia leo nitachangia katika maeneo matatu; eneo la kwanza nitachangia eneo la kilimo, na eneo la pili nitachangia eneo la madini na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya katika Taifa hili. Kila mmoja ni shahidi wa mambo ambayo kimsingi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ametufanyia sisi Watanzania. Tuna haja kubwa ya kumpongeza Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Msalala limegawanyika katika maeneo mawili; eneo la kwanza ni kilimo. Asilimia 50 ya jimbo langu ni kata ambazo kimsingi zinafanya shughuli za kilimo, lakini kumekuwa na tatizo katika suala zima la utoaji wa vibali ambacho kitawaruhusu wakulima hawa baada ya kupata mazao mengi waweze kusafirisha kwenda kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uliowekwa na Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha kwamba wakulima hawa wanaweza kuomba kibali kwa kutumia njia ya mtandao. Ni ukweli usiopingika kwamba katika maeneo yetu, hasa ukizingatia maeneo ya Kata za Mwaluguru na Mwanase, ni maeneo ambayo hayana mawasiliano. Nimwombe Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na Waziri wa Kilimo waweze kuona namna gani wanakwenda kushirikiana na Waziri wa Mawasiliano ili kuweza kuhamisha mawasiliano ambayo yatawafanya basi sasa wananchi hawa, wakulima hawa, waweze kupata huduma ya mtandao ili waweze ku-apply kibali hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe sasa Wizara iweze kubadilisha utaratibu huu wa wananchi kuomba kibali kwa kupitia njia ya mtandao, kwani tunaamini kuwa wananchi wengi hawawezi kuingia kwenye mtandao na kujaza taarifa za kuomba kibali hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba kwa sasa kumeibuka tabia ya kwamba kila maeneo wanaweza kuanzisha mazao mbalimbali ikiwemo korosho na mengine. Niseme tu kwamba sisi wananchi wa Shinyanga ni wakulima wa zao la pamba, lakini kumeibuka tabia ya sasa hawa Maafisa Kilimo kuanza kutuletea mazao mapya. Niombe Waziri wa Kilimo yuko hapo, Naibu Waziri wa Kilimo yuko hapo, waone namna gani sasa wanaweza wakahakikisha kwamba wanatu-support ili tuweze kwenda kwenye kilimo cha pamba kwa kutupatia fedha na mitaji na matrekta yetu yaingie kwenye zao la kilimo cha pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima la madini. Jimbo langu la Msalala ni jimbo ambalo kimsingi lina Mgodi mkubwa wa Bulyanhulu. Nimwombe Waziri wa Madini yuko hapo, Mheshimiwa Doto Biteko, kwanza niwapongeze kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuhakikisha ya kwamba wameweka makubaliano na Kampuni ya Twiga. Ni ukweli usiopingika kwamba wanasimamia vizuri shughuli hizi za madini na usimamiaji wa utoroshaji wa madini. Hata hivyo, nimwambie tu Mheshimiwa Waziri kwamba kampuni hii kwa sasa nadhani imeanza kuja na mfumo mwingine ambao kimsingi kama Taifa tunakosa mapato lakini kama halmashauri tunapoteza fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hii imeanzisha kampuni mbili ambayo moja iko Marekani inaitwa TSL. Uwepo wa kampuni hii Marekani kama Taifa tunapoteza mapato. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, kampuni hii ipo USA maana yake kazi kubwa ya kampuni hii ni kutangaza tenda tu na zabuni mbalimbali katika makampuni makubwa makubwa. Kwa nini kampuni hii isweze kurudi hapa nchini, Makao Makuu yake yakawa Dar es Salaam ili kama nchi tuweze kupata mapato?

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Kampuni hii imeanzisha mtoto wa kampuni ambayo inaitwa TSR Service, iko Dar es Salaam. Uwepo wa Kampuni hii Dar es Salaam inatufanya Halmashauri kupoteza zaidi ya shilingi bilioni 20 fedha za Service Levy. Namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kushirikiana yeye na Waziri wa Viwanda waone ni namna gani sasa wanaweza kuzishauri kampuni hizi ziweze kuja kuwekeza na kuanzisha ofisi zao katika maeneo ya kazi hususan Bulyanhulu. Uwepo wa kampuni hii Dar es Salaam unasababisha ukosefu wa ajira kwa wananchi wetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MBUNGE FULANI: Unga mkono hoja.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. IDDI KASSIM IDDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipatia leo nafasi hii ya kuchangia. Kwa niaba ya wanananchi wa Jimbo la Msalala naomba niipongeze Serikali kwa mambo makubwa na mazito kabisa ambayo yamefanyika ndani ya miaka mitano iliyopita na ambayo kwa sasa yanaendelea kufanyika kwa Awamu hii ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tumesomewa mpango hapa na hotuba ya Waziri Mkuu kwa ajili ya bajeti ya Waziri Mkuu. Hotuba hii ya bajeti ya Waziri Mkuu ni hotuba iliyoshiba kweli kweli; imeeleza wapi tumetoka na inatuelekeza wapi tunaenda. Niseme kwamba katika hotuba hii ya bajeti Waziri Mkuu ameelezea mambo mengi na nijikite kuelezea mambo machache.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuelezea mradi wa Julius Nyerere. Mradi huu wa Julius Nyerere ni mradi muhimu sana na niseme tu kwa niaba ya wananchi wa Msalala, tunaunga mkono Serikali ili mradi huu uende ukatekelezwe na ukamilike. Kwa hiyo, tunafahamu the cheapest source of energy kwenye nchi hii ni umeme unaotokana na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia gharama ya sasa ya umeme, wananchi wetu wanalia huko; unit moja kwa sasa ni shilingi 100/=, lakini ukiangalia manufaa ya mradi huu utakapokamilika, uzalishaji wa unit moja katika mradi huu wanaenda kutumia kiasi cha shilingi 36 kuzalisha unit moja. Maana yake nini? Ni kwamba itaenda kushusha gharama ya uzalishaji kwenye viwanda na pia itashusha gharama ya unit kwa wanananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme, japo mradi huu utaenda kukamilika, niipongeze Wizara ya Nishati, inafanya kazi kubwa. Katika Jimbo langu la Msalala ni ukweli usiopingika kwamba watu wa Nishati wanafanya kazi kubwa, lakini kuna baadhi ya maeneo umeme huu haujafika. Wananchi wa Msalala tunapoona mtu anasimama na kuupinga mradi huu, tunashikwa na hasira kwa sababu Jimbo la Msalala lina Kata 18 na Kata zaidi ya 12 hazina umeme. Kwa hiyo, matarajio yetu ni kwamba mradi huu wa REA III ambao kimsingi utaenda kukamilika, ni kwamba baada ya mradi huu wa Mwalimu Nyerere kukamilika tutakuwa na umeme wa uhakika lakini pia nasi wananchi wa Jimbo la Msalala tutanufaika na nishati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la kilimo. Katika Kata 10 katika Jimbo langu la Msalala ni wakulima wa mpunga. Kuwepo na ukamilishaji wa mradi huu na uwekwaji wa umeme katika Kata zetu hizi utachochea uchumi kwa wakulima. Maana yake nini? Wakulima wataweza sasa kuchakata na kuongeza dhamani ya mazao hayo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la madini. Nimeona hapa imeelezewa na ninaipongeza Wizara imefanya kazi nzuri sana kwenye Sekta ya Madini. Namwomba Mheshimiwa Waziri Dotto hapa, sisi tunaotoka katika maeneo ya migodi, Mheshimiwa Bonnah Kaluwa amezungumza hapa, kuna masuala ya fidia ambayo kimsingi imekuwa ni tatizo katika maeneo yetu haya.

SPIKA: Mheshimiwa, anaitwa Bonnah Kamoli.

MHE. IDDI KASSIM IDDI: Mheshimiwa Bonnah Kamoli.

SPIKA: Eeeh! (Makofi/Kicheko)

MHE. IDDI KASSIM IDDI: Mheshimiwa Spika, kuna tatizo la fidia kwenye eneo langu. Tunatambua ya kwamba kuna mgodi umeanzishwa pale katika eneo letu Kata ya Bulyanhulu ambao ni mgodi wa Bulyanhulu. Baada ya hao watu kuanzisha mradi pale kuna watu mpaka leo toka mwaka 1966 hawajalipwa fidia ya ardhi yao. Naiomba Wizara na Serikali kuhakikisha ya kwamba tunamaliza tatizo hili, kwani ni la muda mrefu sana. Tatizo hili limedumu toka Mheshimiwa Rais Mwinyi akiwa bado ni Rais.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara kwamba sasa tuhakikishe tunatatua tatizo hili la mgogoro na fidia kwa wananchi hao wa Kata ya Bulyanhulu.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo, maslahi ya wafanyakazi. Bado kuna wafanyakazi wanadai. Naomba sasa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wameshaanza kulifanyia kazi, waharakishe kuhakikisha kwamba wafanyakazi wale wanapata stahiki zao mapema ili waweze kujikita kwenye shughuli za uchumi na kutumia fedha hizo katika mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la maji. Tuna miradi ya maji katika Jimbo langu la Msalala. Ni kazi nzuri inafanywa na kaka yangu Aweso, lakini namwomba Mheshimiwa Aweso aweze kuharakisha mradi wa maji unaotoka Mangu mpaka Ilogi uweze kukamilika. Baada kukamilika sasa waanze usambazaji wa maji mara moja katika Kata ya Ikinda, Kata ya Runguya na Kata ya Segese ili wananchi wale nao waweze kufaidika na huduma hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la barabara limekuwa ni mtihani. Wabunge wengi wanalia hapa kuhusu suala la TARURA, lakini mimi naweza nikasema ni jimbo langu la Msalala ni jimbo ambalo lina miundombinu mibovu sana katika. Leo hii tunapozungumza hapa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kampeni, tuliahidiwa kupata barabara mbili zenye kiwango cha lami. Kuna barabara inayotoka Geita - Bukori -Kata ya Bulyanhulu – Kahama. Barabara hii tuliahidiwa kujengwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba niikumbushe Wizara kwamba wakati Serikali inaingia makubaliano na mgodi huu wa Twiga, moja ya makubaliono ambayo walikaa wakakubaliana ni kuhakikisha kwamba wanatenga kiasi cha dola milioni 40 ili waweze kukamilisha barabara hii kwa kiwango cha lami. Fedha hizi zipo, naiomba Wizara husika iweze kuona ni namna gani sasa wanaenda kukaa na kuzungumza fedha hizi zipelekwe ujenzi ili barabara hii ianze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo, tuna barabara nyingine ambayo inatoka Solwa inakuja Bulige inaenda Ngaya na Kahama. Barabara hii pia imeahidiwa kwa kiwango cha lami. Naendelea kuomba Wizara ione namna gani basi inaweza kuanza ujenzi wa barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna barabara moja ambayo ni ndefu sana ina zaidi ya kilometa 85. Barabara hii inaunganisha Makao Makuu na Jimbo la Solwa. Naomba Wizara ya Ujenzi waone namna gani basi wanaweza kuanza mchakato wa kuihamisha barabara hii kutoka TARURA iende TANROADS ili ingie kwenye matengenezo ya kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuishia hapo, niseme kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala, naomba na mimi nichangie katika hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa kazi kubwa inayoendelea kuifanya, lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba tunaona kabisa Wizara ya Madini inavyofanya kazi kubwa katika kuhakikisha kwamba inachangia pato la uchumi wa nchi yetu katika kuimarisha mambo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara ya Madini kwa kuanzisha masoko mbalimbali na hasa katika Jimbo langu la Msalala, tumeona Waziri wa Madini ameweza kutoa maelekezo na Serikali imeweza kuanzisha masoko ya madini katika Kata za Bulyanhulu na Segese. Niombe tu Mheshimiwa Waziri baada ya kikao hiki cha Bunge basi uweze kutembelea ili kusikiliza changamoto za wachimbaji wadogo katika maeneo hayo, hususan Kakola, Bulyanhulu na Kata ya Segese.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hotuba ya bajeti ilivyoelezea juu ya namna gani Wizara imejipanga katika kuhakikisha kwamba inakwenda kuwawezesha wachimbaji wadogowadogo. Niipongeze Wizara inafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha kwamba inawawezesha wachimbaji wadogowadogo, lakini ni ukweli usiopingika kwamba bado kuna changamoto ndogondogo ambazo kimsingi niombe Wizara iweze kuzishughulikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii STAMICO wameonesha mkakati wao kwamba wanakwenda kujipanga katika kusimamia na kuwawezesha wachimbaji wadogo. Hata hivyo, katika maeneo yetu wachimbaji hawa wamekuwa wakinyanyasika sana kwa kukosa mitaji au mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali. Niiombe Wizara iweze kufikiria sasa namna gani wanaweza kuanza kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo ambao ndiyo shokomzoba ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ametueleza hapa mchango wa wachimbaji wadogowadogo katika kuchangia uchumi wa pato la Taifa. Ni ukweli usiopingika kuwa hawa watu wanafanya kazi ngumu sana. Naomba nishauri twende tukaweke mkakati kuhakikisha kwamba tunakabiliana na matapeli kwa sababu wamekuwa wengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri ametueleza hapa namna gani wamefanya jitihada kuwapatia wachimbaji wetu wadogo leseni, niipongeze Wizara katika baadhi ya maeneo yangu hususan Nyangarata na maeneo mengine katika Jimbo la Msalala, Wizara wamefanya hivyo lakini namna gani wanakwenda kutoa leseni hizi lazima tukueleze leo na tutoe ushauri, kwamba watu wanaokwenda kupata leseni katika maeneo haya ni watu ambao kimsingi sio original katika maeneo yale na wengi wao ukiwatafuta unakuta ni madalali. Leo hii unakuta mtu anamiliki shamba, lakini siyo shamba tu ameanzisha uchimbaji na akagundua madini katika maeneo yale, anatoka mtu anakotoka anakuja na leseni kujitambulisha pale na anasema yeye ndiyo mmiliki halali wa maeneo yale. Hii inamnyima haki mchimbaji wetu na tunampa kazi ngumu katika kuhakikisha kwamba anachangia pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe Waziri wa Madini wakae kama Wizara waone namna gani wanaweza wakauboresha huu mfumo wa kuomba kwa mtandao (portal). Watu wetu huko vijijini network hakuna Mheshimiwa Waziri inawanyima haki ya wao kumiliki leseni hizi. Niiombe Wizara iweze kuona namna gani wanaweza wakaweka mfumo mzuri ili iweze kuwarahisishia wachimbaji wetu wadogo, hususan wakazi wa Bulyanhulu, Nyangarata, Segese na maeneo mengine katika Jimbo langu la Msalala kuwa na haki hii ya kuweza kupata leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali, imefanya kazi kubwa kuhakikisha wanaunda ubia kati ya Twiga na Serikali na nipongeze jitihada ambazo zimesemwa. Mimi nizungumzie suala hili katika maeneo mawili; katika local content na fedha za CSR.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Musukuma amesema hapa katika Jimbo lake la Geita wanapewa fedha za CSR kiasi cha shilingi takribani bilioni 10, lakini inasikitisha kuona Jimbo langu la Msalala ambalo tunamiliki Mgodi wa Bulyanhulu, tunapokea fedha za CSR bilioni 2.5 tu na wakati migodi yote ipo Tanzania. Kwa nini Geita wapokee bilioni 10 na sisi tupokee bilioni mbili? Namwomba Mheshimiwa Waziri akimaliza hapa tufanye ziara tuone ni kwa nini kuna tofauti hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yote tunayojadili hapa ni ukweli usiopingika kwamba watumishi wa kwenye Tume ya Madini ni wengi lakini bajeti yao ni ndogo. Ukiangalia watumishi katika Wizara ni wachache lakini bajeti kubwa inakwenda Wizarani na hii inasababisha Tume ya Madini isifanye kazi zake kiuhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, makampuni haya; GGM na makampuni mengine yote, hususan nizungumzie katika Jimbo langu la Msalala, Bulyanhulu pale, kumekuwa na uvunjaji mkubwa wa sheria ya local content. Leo hii tunazungumzia namna gani ya kuwakuza wachimbaji wadogo kutoka katika ngazi ya chini kwenda ngazi ya kati na tuwafanye wachimbaji hao wawe wakubwa lakini ni ukweli usiopingika tunaona kabisa migodi hii wanachangia kwa kiasi kikubwa kuvunja Sheria ya Local Content. Tuna wafanyabiashara wana uwezo wa ku-supply katika migodi yetu hii hawana kazi, kumekuwa na matapeli katikati hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikiwa bado M-NEC nilimsikia Mheshimiwa Waziri akitoa maelekezo katika Mgodi wa GGM waweze kutekeleza sheria hiyo ya local content kuhakikisha kwamba wazawa wanapewa nafasi lakini watu hawa wana kiburi, hawajatekeleza yale aliyowaambia. Watu hawa wana dharau kubwa, nenda kawaeleze kwamba sisi kama wananchi tunaoishi katika maeneo yale ya mgodi tuna-play part kubwa ya kuhakikisha usalama wao na mali zao na ni lazima sasa wakazi tunaoishi katika maeneo yale hususan Bulyanhulu na meneo mengine kama ya Bugarama tunanufaika na migodi hiyo. Kama leo hii hawataweza kutekeleza sheria hii ya local content…

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kassim, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Musukuma.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nampa taarifa mzungumzaji kwamba baada ya tamko la Mheshimiwa Naibu Waziri kule GGM kwamba GGM watekeleze local content, walitekeleza kwa kutoa zile kazi kama ku-supply nyanya na vitunguu, zile kazi zenye maslahi zote wanafanya Wazulu.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Musukuma kwa mikono miwili na sisi Wanamsalala tulishafikisha kilio chetu …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kassim, inabidi usubiri kwanza nikuite tena ndiyo uzungumze. (Kicheko)

Mheshimiwa Kassim Iddi Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupokea taarifa hii kwa mikono miwili, lakini unisamehe kwa sababu ya unjuka, nitazoea. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana asilimia 100 na Mheshimiwa Musukuma. Leo hii makampuni haya ni ukweli usiopingika Mheshimiwa Waziri anafahamu, baada ya kuona Wizara imeweka mifumo ya kudhibiti utoroshaji wa madini sasa wameamua kuja na mfumo mpya kuhakikisha wanatupiga sisi Serikali lakini pia Halmashauri yangu ya Msalala.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili nimeshalifikisha kwa Waziri na naomba alishughulikie haraka iwezekanavyo. Tumekuwa wavumilivu sana wananchi wa Bulyankhulu na Msalala. Tunatamani mgodi huu uendelee kuwepo, leo hii tulikuwa tunazungumza kwamba kampuni hizi zimeanzisha kampuni ndogo pale Dar es Salaam, TCL Mheshimiwa Waziri, tumeshalizungumza hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mama anayelima nyanya katika Jimbo langu hawezi ku-supply nyanya kwenye mgodi mpaka aende Dar es Salaam. Hivyo mnatutoreshea mapato katika Halmashauri yetu. Naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri suala la barabara, fedha nendeni mkatekeleze haya barabara ianze kupitika. Mimi na wananchi wangu tumekubaliana ikifika mwezi wa Saba barabara haijatengenezwa, fedha hazijatoka, Mheshimiwa Waziri sisi tutaziba barabara, kwa sababu wananchi wangu wanahangaika mno. Tunanufaika vipi na madini haya kama wananchi wetu wanakula vumbi? Kwa hiyo, naomba Wizara ya itekeleze haya ili wananchi wetu waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja asilimia mia moja na mbili. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii nami kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala kuchangia juu ya bajeti hii ya Wizara ya Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika maeneo matatu kama muda utaniruhusu, na nianze moja kwa moja kwa kujikita katika suala zima eneo la madini. Lakini nianze kwa kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitachukua nafasi hii kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa ajili ya kuniamini mimi na kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Msalala lakini pia kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya. Tumeona Katibu Mkuu na Sekretarieti nzima ikizunguka kwa ajili ya kuinadi na kuisimamia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii pia kuwapongeza Mawaziri na wafanyakazi wote wa Wizara ya Madini. Pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia fedha kiasi cha shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa kilometa Moja barabara ya lami katika Kata ya Bulyanhulu. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona namna gani sasa wananchi wa Bulyanhulu wanasumbuliwa na vumbi na kutupatia kiasi cha shilingi 500,000,000 walau tuweke kilometa moja ya lami katika eneo lile ili tuweze kupunguza vumbi lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Lakini pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutupatia shule moja ya sekondari ambayo tunaenda kuijenga katika Kata ya Ikinda ambayo itapunguza adha ya ukosefu wa shule katika Kata ile ya Ikinda. Lakini niendelee kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais na Wizara kwa kutupatia kiasi cha shilingi 1,000,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali yetu ya wilaya. Hivyo hivyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais tena kwa kutupatia kiasi cha shilingi 750,000,000 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la utawala katika Wilaya yangu ya Msalala. Nimpongeze pia kwa kutupatia kiasi cha shilingi 500,000,000 katika ujenzi wa kituo cha afya kinachoendelea katika Kata ya Isaka. Mambo mengi Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametutendea katika jimbo langu la Msalala. Hivyo, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala ninamshukuru na tunamshukuru kwa dhati Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kututendea wema huu katika Jimbo langu la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa moja kwa moja kuchangia katika Sekta hii ya Madini. Sekta ya Madini kama mnavyofahamu imetembea katika misuko suko mikubwa sana mpaka hapa ilipofikia. Sekta ya Madini imekabiliwa na changamoto nyingi, nimshukuru Waziri wa Madini kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kuhakikisha kwamba sekta hii ya Madini inasimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kuchangia nimeona hapa kwenye bajeti hii kuna tozo ambayo inaenda kuanzishwa kwa wachimbaji wa madini wadogo wadogo na hii Mheshimiwa Waziri nikuambie ukweli, hii tunayoenda nayo kwa sasa ambayo inawataka wachimbaji wadogo wadogo wenye makusanyo yasiyozidi milioni mia moja kwenda kulipa tozo ambazo zimeorodheshwa hapa. Hii kiukweli tunaenda kuua Sekta hii ya Madini. Sekta ya Madini Mheshimiwa Waziri nikuambie ukweli, Sekta ya Madini kwa sasa tunaona kabisa kwamba Wizara zingine zote, Sekta ya Madini wameiona sasa kama ni Sekta ambayo ya kwenda kukusanya fedha. Sekta ya Madini tunakabiliwa na changamoto nyingi sana hasa za kikodi. Kuna kodi nyingi sana katika Sekta ya Madini na ili Sekta hii iende ikasimame ni lazima tuone namna gani tunaenda kuisaidia sekta hii katika kupunguza gharama na tozo mbalimbali zilizoko hapa.

Mheshimiwa Waziri, leo hii tunakwenda kumwambia mchimbaji mdogo mdogo anapokwenda kuuza madini yake katika soko la dhahabu aende akakatwe tozo ya zuio la ajira. Leo hii tutambue Mheshimiwa Waziri, huyu mchimbaji mdogo mdogo kwanza hana maeneo ya kuchimba ambayo ni rasmi na utaratibu unaotumika kule ni kwamba mtu anayemiliki leseni ni tofauti kabisa na mchimbaji mdogo mdogo anayechimba katika leseni ile. Sasa, baada tu ya huyu mchimbaji mdogo mdogo kuchimba madini yake kunakuwa na migao mingi ambayo kimsingi inaenda kufanyika pale kabla hata ya kwenda sokoni kuuza dhahabu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wachimbaji wadogo wadogo hawajaajiri watu, wanapochimba mathalani mchimbaji ametoa mifuko 100 kwenye shimo lake, hapo hapo anakatwa mifuko kwa ajili ya mmiliki wa leseni mifuko ishirini na zaidi. Hapo hapo anakatwa kwa ajili ya ulinzi, hapo hapo anakatwa kwa ajili ya wafanyakazi, hapo hapo wanamalizana. Maana yake ni kwamba mtu anapotoka na dhahabu yake mchimbaji mdogo mdogo huyu kwenda sokoni ameshamalizana na mambo mengine yote huku. Unaendaje kumkata tena fedha pale kwenye soko la dhahabu anapouza kwa ajili ya kulipa zuio la ajira? Mheshimiwa Waziri nikuombe hebu nendeni makapitie upya mapendekezo haya mliyoyaleta yanaenda kuua Sekta ya Madini. Sisi kama wachimbaji wadogo wadogo tuko radhi kuhakikisha ya kwamba tunalipa kodi. Lengo la kuanzishwa masoko haya ni kudhibiti utoroshwaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kodi hizi zinazoendelea kuwekwa hapa inaenda kufungua tena milango ya kuhakikisha kwamba utoroshaji wa dhahabu unaendelea. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, nenda kapitie upya. Hili suala haliwezekani, wachimbaji wadogo wadogo hawa wasiopitia mauzo ya chini ya milioni 100 hawawezi wakalipa mambo yote hapa, hapa yamewekwa kuna kodi inakatwa asilimia tatu ambayo kodi hii tayari ameshailipa kule mifuko. Imewekwa hapa anatakiwa akatwe kodi ya mapato ya ajira, huyu anamuajiri nani mchimbaji mdogo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe chonde chonde twendeni tuhakikishe ya kwamba tunaenda kuondoa kodi hizi ili kumrahisishia mchimbaji mdogo mdogo. Lakini pia niiombe Wizara badala ya kujikita kuongeza kodi hizi tujikite katika kuhakikisha ya kwamba tunaenda kuwajengea uwezo wachimbaji wetu hawa wadogo wadogo. Leo wachimbaji wadogo wadogo wanahangaika na ukosefu wa mitaji, wanahangaika na ukosefu wa maeneo sahihi ya uchimbaji, tafiti hazitolewi kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo hawa ili waweze kuchimba maeneo sahihi, hazitolewi. Leo hii tunaenda kuongeza kodi tena. Mheshimiwa Waziri nikuombe, kuna maeneo mengi ya kwenda kukusanya kodi na siyo maeneo haya. Mheshimiwa Waziri, ukipiria ripoti ya CAG imeonesha kuna kampuni kubwa zipo ambazo kimsingi zinaweza zikachangia ongezeko la kodi na mapato katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ripoti ya CAG imejieleza hapo. Imetueleza kuna kampuni za Kimataifa zinafanya kazi hapa na kampuni hizi kwa sasa ukiangalia uwezo wake ukisoma Ripoti ya CAG kuna kampuni zaidi ya 504 ambazo zipo na kampuni hizo ni zaidi ya 116 mpaka 154 hazijafanyiwa ukaguzi. Hebu twendeni tukajikite katika kuhakikisha ya kwamba kampuni hizi zinazoanzisha shughuli hizi za utoroshaji wa mapato twende tukatafute fedha kule tuwaache wachimbaji wadogo wadogo waweze kunufaika na rasilimali za nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe angalieni namna gani mnaenda kutupatia mitaji. Leo hii tunazungumzia habari ya mitaji kuna fedha zinatolewa asilimia 10, asilimia Nne zinaenda kwa vijana, asilimia Nne zinaenda kwa akina mama. Leo hii mchimbaji mdogo mdogo anayekopeshwa fedha hii anaenda kuchimba, bado hujajua kwamba ametumia gharama kiasi gani katika ku-invest, wewe unaenda kukaa katika soko kusubiri sasa umkate tozo ya ajira, umkate kodi mbalimbali bila kuangalia ametumia gharama kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe hebu twende tukapitie upya mapendekezo haya. Mimi siyaungi mkono mapendekezo haya Mheshimiwa Waziri na nitashika shilingi. Nendeni, ukija hapa Mheshimiwa Waziri njoo na majibu ya namna gani unaenda kutusaidia wachimbaji waodgo wadogo na mkaondoe tozo hizi. Haya masharti ni magumu mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapozungumza Mheshimiwa Waziri mimi jimbo langu lina mgodi wa Bulyanhulu pale na Bulyanhulu kuna kampuni ambayo imeanzishwa Mheshimiwa Waziri iko pale. Wamezanzisha kampuni mbili kwa ajili, naweza kusema utoroshaji wa fedha. Kuna kampuni moja imeanzishwa ya TSL ambayo iko nje huko. Lengo la kampuni hii ni kupata purchasing activities ambazo zinaendelea. Lakini pia kuna kampuni nyingine TSL imeanzishwa Dar es Salaam hapa, leo hii mama ambaye analima nyanya Bulyanhulu hawezi akauza nyanya zake pale mgodini inatakiwa aende Dar es Salaam kwenye kampuni hiyo iliyoko kule na nyanya anapouza wale kazi yao ni ku- maximize profit tu kuongeza bei na kuhakikisha kwamba wanatorosha fedha katika maeneo yale. Nikuombe Mheshimiwa Waziri chonde chonde, sisi kama wachimbaji Mheshimiwa Waziri tuko tayari kulipa kodi lakini hatuko tayari kulipa kodi za namna hii. Nikuombe, sheria hii na mapendekezo haya yaende yakafutwe, yanaenda kuua Sekta ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mheshimiwa Waziri amenielewa katika Sekta ya Madini. Sasa niende katika kuzungumzia suala zima la biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Tanzania ukiiangalia hapa tumezungukwa na nchi jirani. Mimi nilipata bahati ya kutembea kwenda Dubai nikaona namna gani wanafanya. Kuna maeneo mengi Mheshimiwa Waziri nikuombe, leo hii hapa unaona watu wa kutoka Uganda, Rwanda, kutoka maeneo mbalimbali wanaenda Dubai kwenda kununua magari wanayaleta yanapita hapa na yanaondoka. Hivi, kwanini kama Serikali Tusianzishe utaratibu wa kuwaruhusu watu hawa wanaoingiza magari wafungue yards kubwa hapa wasitozwe ushuru kwanza, watozwe tui le kodi ambayo kimsingi mteja akienda kununua gari lake ndiyo atozwe kodi. Maana yake ni kwamba tutawarahisishia watu wanaotoka Uganda, wanaotoka Burundi na maeneo mengine kuishia hapa nchini kwetu Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuambie watu wakazi wa Isaka tuko tayari kutoa eneo tuwaite hawa watu ondoeni kodi za magari watu walete hapa magari yao waweke. Mteja akienda pale anaponunua gari lake basi aweze kutozwa kodi na wale wanaotoka nchi jirani wanapokuja kununua magari hapa wasitozwe kodi wapeleke huko, hii itasaidia kuongeza mapato katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niende kwenye suala zima la kilimo. Tumeona mnajitahidi na nipongeze wakati tunajadili bajeti ya kilimo hapa watu wengi wamezungumzia walikuwa wanalia kilimo, kilimo, kilimo, lakini mimi nizungumze mambo mawili tu; katika kilimo hapa ni lazima tuone namna gani tunaenda kutengeneza masoko, issue sio mbegu, mbegu wananchi tunaweza tukanunua, lakini issue ni masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo ninapozungumza hapa kwenye Jimbo langu la Msalala wengi ni wakulima wa mpunga. Ukiangalia Kata ya Mwaruguru, Kata ya Jana, Kata ya Mwananse, Kata ya Kashishi, wote ni wakulima wa mpunga na tunavyozungumza hivi bado wana stock ya mwaka jana na bado wana stock ya mwaka huu na wameamua baadhi yao kutelekeza mpunga wao mashambani kwa sababu hawana sehemu ya kuupeleka na bei bado iko chini. Kwa hiyo, niwaombe namna gani Wizara inaweza kujikita katika kuhakikisha ya kwamba mnaenda kututafutia soko la kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali imekuwa inakuja pale ambapo wananchi wanavuna ndio inaingia, lakini ni namna gani inamsaidia huyu kutafuta soko na kuhakikisha ya kwamba inamsaidia kwenye kumkopesha ili aweze kufanikiwa, hakuna. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri na niwaombe Wizara ya Kilimo hebu njooni sasa mfanye walau research katika Jimbo langu la Msalala ili muwasaidie wananchi hawa muone namna gani wanaweza wakauza mpunga wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu leo gunia la mpunga mwananchi anauza kwa shilingi 36,000 lakini bado kuna matapeli wameibuka humo humo. Leo Serikali imepiga marufuku lumbesa, lakini viwanda vimeibuka sasa kuanza kutengeneza mifuko ambayo inabeba madebe kuanzia nane, wanaenda kumdhulumu mkulima. Niwaombe Wizara na wanaohusika njooni basi katika Jimbo langu la Msalala muone namna gani wakulima hawa tunaweza kuwasaidia ili waweze kuuza mazao yao kwa bei iliyokuwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine niseme tu kuna matapeli wamo katika Wizara ya Kilimo na maeneo mengine. Ili tuweze kufanikiwa katika sekta ya kilimo; moja ni tunaweza kutafuta masoko nje ya nchi. Leo hii watu wanatoka nje kuja kufanya biashara ya mazao, kuna watu wanakuja kuwatapeli, ku-destroy image ya nchi; Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo uko hapo unanisikia, leo hii kuna watu wamekuja hapa kufanya biashara ya ufuta, Mheshimiwa Naibu Waziri ananisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa wamekuja kutuamini hawa wakatoa fedha zao hapa na wametapeliwa, chukueni hatua kwa watu hawa. Kesi hii Mheshimiwa Waziri bado inasumbuliwa, watu hawa wamedhulumiwa zaidi ya dola laki nne watu wamedhulumiwa na wafanyakazi hao wapo kwenye ma-go down wanawaleta watu kutoka nje, wanawaleta kuwaonesha kwenye ma-go down ya ufuta yale na wanawaambia ufuta huu sisi ndio tunaweza kuuza, wanapewa advance, kufanya hivyo ni ku-destroy image ya nchi na masoko katika nchi yetu hii Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo uko hapo, hebu ninaomba hili suala lichukulie hatua, limeenda TAKUKURU, limeenda wapi, lakini hakuna majibu watu wanalia kutafuta fedha zao. Huyo aliyechukua fedha hizo Mheshimiwa Waziri mchukulieni hatua arudishe fedha, anaharibu taswira ya nchi Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu kipenzi, mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Kwa ridhaa yako naomba basi nitumie style ya Mayele kumshangilia Mama Samia Suluhu Hassan kwani anaupiga mwingi sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ninavyochangia hapa nina furaha sana baada ya kumwona Mwenyekiti wa Yanga Bunge, Mheshimiwa Gulamali baada ya kunikabidhi kadi yangu sasa ya Yanga kwanza. Sasa najijua ni mwanachama halisi wa Yanga. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika maeneo matatu na moja nianze na suala zima la nishati. Nianze kuipongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kuifanya, chini ya Waziri wake Mheshimiwa January Makamba na msaidizi wake Mheshimiwa Byabato. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nimempongeza mwanachama wa Yanga kwa kuonyesha kadi yake na sio kadi tu, ni kadi ya viwango ya timu ya wananchi. (Makofi/Vigelegele/Vicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Kassim Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ninapokea taarifa hiyo na ninaomba nimshangilie na yeye kwa style ya Mayele. (Makofi/Kicheko)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba Yanga wanajitahidi kuigaiga ila tunawaomba waje na kadi za viwango. Simba ya Kimataifa tuna mpaka VISA Card, tuna kadi ya wanachama ya kiwango, ukiangalia kadi yao, yaani hadi wanatia huruma. Kwa hiyo, naomba mchangiaje aje achukue hizi kadi za Simba ili wakaboreshe za kwao zaidi kupitia Mwenyekiti wake wa Tawi. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo siipokei kwani Mheshimiwa Nicholaus Ngasa, Mbunge wa Igunga, ameniambia kuwa na kadi ya Yanga pia nimeanza kukopesheka kuwa na sifa. (Makofi/Kicheko)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba tu kumpa taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Iddi kwamba, wananchi wanamsikiliza na hayo sio waliyomtuma, kwa hiyo aongee masuala ya wananchi. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo siipokei kwani waliyonituma hapa ni wananchi na nazungumzia wananchi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, basi naomba niende moja kwa moja kwenye mchango wangu. Kwanza nianze kwa kuwapongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya na hapa niwe mkweli kwamba, suala zima linaloendelea kwa sasa na hasa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya wachangiaji jana juu ya upandaji wa bei za mafuta katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kwamba katika mfumo huu ambao umeanzishwa na upo, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Msalala, naendelea kuwaomba waendelee kuuboresha mfumo huu wa uagizaji wa mafuta. Kwani ni mfumo ambao ni bora sana na hata nchi zingine za jirani wanakuja kuiga mfumo huu hapa Tanzania. Ukiangalia Nchi za Malawi, Zambia tayari wamekuja kujifunza namna bora ya Serikali ya Tanzania tunavyofanya katika uingizaji wa mafuta ya pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hoja ambazo zimeibuka kwamba soko la mafuta liwekwe huria na wapewe wawekezaji binafsi waweze kuingiza mafuta. Nataka tu niuambie umma wa Watanzania kwamba, suala zima la uingizaji mafuta kwa pamoja lina faida zake katika nchi yetu hii ya Tanzania. Moja ya faida ya uingizaji wa mafuta kwa pamoja ni national security. Leo hii tunaangalia Nchi za Rusia na Ukraine vita inayoendelea kule, leo kama nchi tukiiachia soko huria la mafuta, upi sasa uhai na usalama wa nchi yetu hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba watu tunaochangia katika suala zima hili la mafuta tuweke uzalendo mbele, kuhakikisha , kwamba tunachangia ili kuleta manufaa ya nchi yetu. Nimeona wengi katika suala hili la mafuta wanachangia kuangalia masilahi yao binafsi. Niseme tu kuanzia leo utaratibu huu uendelee kwa sababu, ni utaratibu ambao unalinda uhai na usalama wa nchi yetu. Pia, leo kama mafuta yataachiwa liwe soko huria, sisi kama wafanyabiashara… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kassim Iddi ngoja kwanza ni kazi yangu kuwalinda Wabunge humu ndani. Wale wenye mawazo tofauti na ya kwako umewasema hapo kwa ujumla kwamba wanachangia kwa masilahi yao binafsi; na Kanuni zetu zinasema mtu akiwa na masilahi lazima ataje na maslahi yake ya kifedha.

Sasa nataka kukurahisishia una njia mbili; moja, ni ya kusisitiza kwamba wana maslahi, kwa hiyo, sisi tutawataka wao walete hayo maslahi ambayo na wewe unayajua. Au ni kuondoa hiyo kauli ili kila Mbunge humu ndani awe huru kutoa mawazo yake, lakini kama unao uhakika huo, basi utalisema kwa namna hiyo. (Makofi)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, naomba kuondoa kauli hiyo, lakini niendelee kusisitiza kwamba, tunapokwenda kuchangia ni lazima tuangalie maslahi ya wananchi wetu ambao wametutuma.

Mheshimiwa Spika, niendelee kwa kusema kwamba upatikanaji wa mafuta kwa bei ambayo iliyopo sasa ni utaratibu ambao ni wa Serikali umeendelea kudhibiti mfumuko wa bei kupanda na kushuka na kuhakikisha kwamba, hao waagizaji wa mafuta wanaagiza kwa pamoja, sambamba na kutangazwa tender ya pamoja ili kuweza ku- control bei ya soko la Kimataifa. Kwani tunafahamu kwamba hata visima vya mafuta vinavyouza mafuta haviuzi moja kwa moja kwa muuzaji wa mafuta ama kampuni yoyote, isipokuwa wameteua ma-agent kwenye nchi zao huko ambao wanauza mafuta kwenye nchi nyingine hizi za jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kusisitiza kwamba utaratibu huu Serikali iendelee kuuboresha vizuri, lakini niishauri tu kwamba hapa suala ni kuhakikisha ya kwamba wanajitahidi sasa, kuangalia zile gharama na kodi mbalimbali ambazo zimewekwa waweze kuzifanyia kazi, waziondoe ili kupunguza gharama ya mafuta. Tukumbuke sakata hili linafanana moja kwa moja na sakata la vinasaba. Wapo waliokuja hapa wakasema Kampuni ya GFI haifai inatunyonya na Serikali ilisikia ushauri huo ikaenda kuondoa na kuwapa TBS. Hata hivyo, baada ya siku tu kupita wale wale waliokuwa wanaipiga vita GFI walirudi wakaanza kusema kwamba sasa TBS haina uwezo, baada ya kuona sasa mianya ya mafuta yameanza kuingia ambayo yanachakachuliwa. Kwa hiyo, niombe tunapokwenda kujadili hili suala hasa katika kuzingatia usalama wa nchi yetu tuweke uzalendo mbele.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuchangia sasa upande wa TAMISEMI. Hali ya barabara katika maeneo yetu ni mbaya sana na hasa nizungumzie sasa kwenye Jimbo langu la Msalala. Barabara ni mbovu sana. Leo hii tunazungumzia ukuaji wa kilimo kwenye maeneo yetu, leo hii tunazungumzia ukuaji wa viwanda kwenye maeneo yetu, lakini vyote hivi haviwezi vikaenda sambamba kama miundombinu ya barabara haitarekebishwa. Niombe Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Naibu Waziri nadhani yupo hapo ananisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto kubwa sana kwenye maeneo yetu haya, hasa katika usimamizi wa fedha ambazo zinakwenda kwenye kukarabati barabara. Leo hii utaona tender nyingi za barabara zinatangazwa wakati wa mvua. Niendelee kuwaomba Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa pamoja waweke mkakati sasa wa fedha hizi ambazo tutakuwa tumezipitisha kwenye bajeti, ziende zikaendelee kukaa pale hata wakati wa mvua zisiende zikachukuliwa tena huko mbele. Pia, waweke usimamizi madhubuti katika kuhakikisha kwamba wakandarasi wanaopatikana kwenye maeneo yale ni wakandarasi ambao moja, wana sifa za kuhakikisha ya kwamba wanatekeleza miradi ile kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, wakandarasi hao wawe financially fit kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miradi ile wanakwenda kuitekeleza bila kusuasua na wala kutegemea mikopo kwenye mabenki. Kwani kuwapa wakandarasi ambao hawana uwezo kwenye maeneo yetu ndio kunapelekea kucheleweshwa kwa barabara nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, leo hii nitazungumzia miradi katika eneo langu la Kata ya Jana, Kata ya Mwaruguru, Kata ya Mwanase, maeneo haya ni wakulima wa mpunga. Nimpongeze Mheshimiwa Bashe kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kugawa vitendea kazi kama pikipiki na kuendelea kuthibitisha kwamba mama yetu Samia Suluhu ametoa fedha nyingi kwenye kilimo. Matunda hayo hayawezi yakaenda kuleta matokeo kama barabara zetu kwenye maeneo ya uzalishaji zitakuwa ni mbovu. Leo hii tunaongea barabara hizo hazipitiki. Niiombe Wizara wajaribu kuangalia namna gani na njia bora ya kuhakikisha kwamba barabara hizi zinaanza kutengenezwa mapema kabla ya mvua, ili wananchi sasa wa kwenye maeneo yale waendelee na uzalishaji katika maeneo hayo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Msalala ili nichangie hotuba ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja nianze kwa kuipongeza Wizara ya Maji kwa kazi kubwa inayoendelea kuifanya. Pia niishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa sasa wa wananchi wa Jimbo la Msalala kupata maji safi na salama. Pia tutakuwa wachoyo wadhila kuishukuru Serikali kwa fedha nyingi ambazo wametutengea sisi Jimbo la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetutengea kiasi cha Sh.4,600,000,000.00 kwa ajili ya miradi mbalimbali katika Jimbo langu la Msalala. Kwa kweli kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, tunaishukuru sana Serikali lakini pia tunamshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweza kutengea kiasi cha shilingi milioni 558 katika mradi wa maji ambao utahudumia Vijiji vya Nduku, Ntobo, Busangi. Niombe baada ya fedha hizi kutoka basi ziende haraka iwezekanavyo ili kukamilisha mradi huu ambao ni changu na utaweza kupunguza tatizo la maji katika Kata hii ya Busangi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri na Serikali haijaishia hapo tu, wameenda kutupatia kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya extension katika mradi mkubwa wa maji. Hata hivyo, kuna mradi mkubwa ambao unaitwa Manguirogi ambao ni joint venture kati ya Serikali na Mgodi, hii ni fedha ya CSR. Namwomba Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili akubali kuambatana nami ili twende kule tukaangalie ili tuweze kufahamu ni kiasi gani Serikali imeweza kuchangia katika mradi huu lakini pia mgodi umechangia kiasi gani? Fedha hizi ni za CSR na tunatamani sana tuone ili tujue chenji yetu imebaki kiasi gani ili kusaidia kusambaza maji katika Kata za Runguya, Ipinda, Segese na maeneo mengine. Mradi huu unatoka Mangu unaishia Irogi, niiombe Serikali bsi iweze kutenga fedha tena kwa ajili ya kufanya extension katika maeneo ya Ikinda Kata za Lunguya, Nyangarata, lakini na maeneo mengine ili kuweza kusaidia na kupunguza tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Segese inakua kwa kasi sana kwa sasa na matarijio yetu ni kuhakikisha kwamba tunapata maji ya ziwa ili watu waweze kunufaika. Pia tuna Makao Makuu ya Ntobo ambayo kimsingi tunaenda kuyazindua muda si mrefu, niombe mradi huu unaotoka Nduku kuja Ntobo lakini pia mradi huu unaotoka Mangu kuja Irogi extension iweze kufanyika pia maji haya yaweze kusogea katika Makao Makuu ili ituwezeshe kuwafikishia wananchi miundombinu hii ya maji na tuweze kuwahimiza sasa waweze kuwekeza kwa kiwango cha juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna mradi mkubwa ambao umeshakamilika wa Kagongwa – Isaka. Mheshimiwa Waziri kama anakumbuka alikuja kuzindua na Mheshimiwa Rais alikuja pale na alitaja mbele ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwamba kuna chenji imebaki. Pia mradi huu unapita katika Kata ya Mwakata ambayo haina maji. Naomba Waziri aone ni namna gani chenji iliyobaki katika mradi unaotoka Kagongwa kwenda Isaka mnaweza kuzipeleka katika Kata ya Mwakata ili sasa na wakazi wa Kata ile waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Serikali na Mheshimiwa Waziri kwa kututengea kiasi cha shilingi 1,500,000,000 katika Kata za Jana na Mwalugulu. Ni matumaini yangu kama fedha hizi zitaenda haraka na kufanya uzinduzi wa mradi huu utasaidia sana wakazi wa Kata hizi ili na wao waweze kunufaika na mradi huu wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba kumekuwa na changamoto ya bili za maji, nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kutembelea mradi huu Mangu - Irogi tupate fursa ya kutembelea wananchi na kusikiliza kilio chao juu ya ongezeko la bili za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Wizara ione namna gani wanaweza wakaja na solution ya kuhakikisha kwamba wanatengeneza mfumo mpya ambao utasaidia kupunguza adha ya ongezeko la bili la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, niiombe Wizara iweze kuwapatia mafunzo maalum wale wasimamizi kule chini. Hii itawasaidia kutumia miradi hii ya maji ambayo inapelekwa kule na inatumia gharama kubwa ili waone namna gani sasa wanaweza kuanza kusambaza katika miji ya watu na ili wakazi wa maeneo yale waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapo, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipatia nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala. Nami naomba nichangie hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niende moja kwa moja kwa kuipongeza Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya katika Taifa letu hili la Tanzania. Pia, niende moja kwa moja kuipongeza Serikali kwa kufikiria na kuanza ujenzi wa standard gauge kwa maana ya kwamba reli ya kati na kufikiria kujenga bandari kavu katika Kata ya Isaka ambayo matumaini yetu kama wana Msalala ni kuhakikisha ya kwamba bandari hii itakapokamilika itaenda kukuza uchumi wa Jimbo la Msalala katika kata ya Isaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwa kuipongeza Wizara na hasa bandari kwa kutupatia mabati 300ya CSR kwa ajili ya ukamilishaji wa kituo cha afya katika Kata ya Isaka. Ahsanteni sana, kwa niaba ya wana Msalala tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja nizungumzie suala la barabara katika Jimbo langu la Msalala. Hali za barabara katika Jimbo langu la Msalala ni mbaya sana. Nimekuwa nikipiga kelele hapa suala la barabara inayotoka Bulyanhulu – Kahama. Barabara hii ni muhimu sana katika uchumi wa Tanzania kwani wote ni mashahidi ya kwamba Serikali yetu inapokea fedha nyingi sana kutoka katika Mgodi ule wa Bulyanhulu lakini barabara hii inahudumia wakazi wengi sana wa Jimbo la Msalala lakini pia wa Mkoa wa jirani wa Geita. Lakini, ndiyo shortcut
ambayo mtu anaenda Geita, ni rahisi kwake kupita pale katika Jimbo la Msalala kuelekea maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kama nilivyosema hapo mwanzoni kwamba kuna fedha imetengwa na nikaomba Wizara ya Ujenzi, Madini na nikamuomba Waziri wa fedha wakae kwa pamoja waone namna gani fedha hizi zinaweza zikatoka kwenda kukamilisha barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona hapa kama Wabunge wenzangu walivyochangia kwamba ni ukweli usiopingika kwamba tunaona kabisa kama Mbunge mwenzangu Kunambi amesema kwamba anashangaa ni vigezo gani vinatumika Wizarani katika kugawa fedha hizi. Nimeona hapa barabara hii Geita – Bukoli – Kahama imetengwa kwenye route tatu na route tatu hizi ukiangalia Geita kwa maana ya kwamba Bulyanhulu junction road wametenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 lakini hivyo hivyo junction road to kahama wametenga bilioni 1.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia hapa barabara nyingine ambayo inaenda Uyoga – Nyamilangano, barabara ile ile route ile ile, wametenga kiasi cha shilingi bilioni 3, usawa uko wapi? Mmetenga kiasi cha shilingi bilioni 6 kwa maana ya kwamba mmetenga route tatu. Kwanini route ya kwanza mmempa bilioni 1.5, route ya pili mmetupa bilioni 1.5, halafu route ya tatu mkampa bilioni 3? Basi toeni hiyo bilioni 1 mtugawanyishe huku milioni 500, 500 ili wote twende sawa bilioni 2, 2 Mheshimiwa Waziri, nadhani unanisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Waziri, barabara hii japo ina urefu wa kilometa 160 lakini kilometa zilizotengwa hapa ukiangalia ni jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 6 ambayo ni kilometa 6 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niendelee kuwapongeza na kuwaomba barabara muhimu naona hapa tumetengewa barabara ambayo inatoka Ntobo – Busangi – Ngaya – Buluma – Jana mpaka Didia mmeitengea kiasi cha shilingi milioni 170 kwa kutengenezwa kiasi cha kilometa 4.8 lakini mmeenda tena mnatutengea kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya kilometa 2.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina urefu wa kilometa 85 lakini ukiangalia hapa ni kilometa kama saba ndiyo mmetutengea hapa. Barabara hii ni muhimu katikauchumi wetu huu wa Jimbo la Msalala. Barabara hii inahudumia Kata ya Ngaya, Kata ya Jana, Kata ya Kashishi na maeneo yote haya ni wazuri wa kuzalisha mpunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha mpunga, unapozungumzia mpunga asilimia 85 ya mpunga unaopatikana Kahama unatoka katika Jimbo la Msalala kwenye kata hizi. Matumaini yangu ni kwamba barabara hii ikienda kuimarika itainua uchumi wa Jimbo langu la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri, barabara hii muendelee muichukue moja kwa moja. Muimiliki, namaanisha kwamba muiingize kwenye matengenezo ya kila mwaka ili wananchi…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Kengele imegonga Mheshimiwa.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ninaomba niunge mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala, ninaomba nichangie kwenye hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Mawasiliabo. Kwanza kabisa, naomba nijielekeze kwenye suala zima la usalama wa fedha za mtu anaye-transfer fedha kutoka kwenye mtandao mmoja kwenda kwenye mtandao wa pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa kwa watumiaji wa mitandao wanaofanya transfer kutoka mtandao mmoja kwenda mtandao wa pili juu ya usalama wao wa fedha mahali ambapo wanakosema kutuma fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano na mwenyewe ni muathirika, mimi ni mtumiaji wa mtandao wa Airtel na inapotokea bahati mbaya ninatuma fedha kwenda kwenye mtandao mathalani wa Vodacom, inapotokea nimekosea usalama wa fedha unakuwa ni mdogo. Kwa hiyo, naomba nishauri Wizara iweze kuona namna gani basi sasa ianze kushauri kampuni hizi zijikite katika kuhakikisha kwamba wanaweka coordination ili ku-secure zile fedha za mtumiaji anayetuma mtandao mmoja kwenda mtandao wa pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze moja kwa moja kwenye Jimbo langu sasa la Msalala. Jimbo langu la Msalala lina kata 18 na lina vijiji 92 lakini katika Kata zaidi ya 12 hatuna mawasiliano. Kumekuwa na changamoto nyingi sana juu ya ukosefu wa mawasiliano katika Jimbo langu la Msalala na hasa katika Kata ya Jana, Mwaruguru, Mwanase, Kashishi, Lunguya, Ntobo, Shilela, Mega na kata nyingine nyingi. Matatizo haya yanasababisha sasa ndoa kuvunjika. Leo hii katika maeneo mbalimbali katika Jimbo langu la Msalala ukitaka kupiga simu mpaka utafuta mti au mbuyu mrefu ili uende ukapige simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo haya nimeshawasilisha kwa Waziri na nimemuomba Waziri kwamba aone namna gani anaweza kutusaidia sisi wa Jimbo la Msalala ili tuondokane na adha hii. Ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu ya kisingizio cha mtu kwenda kwenye mlima fulani kupiga simu, unakuta ameshaandaa mchepuko hukohuko. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosekanaji wa mawasiliano haya unahatarisha sasa ndoa za wananchi wangu wa Jimbo la Msalala. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, chondechonde, makao makuu ya wilaya hatuna mtandao. Wanapotaka kuchapisha document za halmashauri ni mpaka wasafiri waende Kahama Mjini, Mheshimiwa Waziri hebu tuangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hilo tu, tuna maeneo mengi ya machimbo katika Jimbo langu la Msalala. Kama mnavyofahamu suala zima la biashara ya madini na biashara nyingine linaenda kimtandao, lakini suala la applications mbalimbali linaenda kimtandao, ukosekanaji wa mawasiliano katika Jimbo langu la Msalala, hasa katika Kata ya Segese, Kata ya Bulyanhulu, Kijiji cha Nyangalata, Kata ya Jana na maeneo mengine, unasababisha kuwanyima haki wananchi juu ya kufanya application ya kuomba leseni za madini na kibali cha mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyofahamu wananchi wetu ili kupata kibali cha kusafirisha mazao unatakiwa u-apply kwa mtandao na maeneo yale hayana mtandao. Mheshimiwa Waziri ukosefu wa mawasiliano katika Jimbo la Msalala unasababisha anguko kubwa la kiuchumi. Tunakuomba chondechonde katika kata hizi ambazo nimezitaja angalia namna gani basi unaweza kutupatia mawasiliano, ili wananchi wetu waweze kuondokana na adha hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo. Naunga mkono hoja, naomba Mheshimiwa Waziri chondechonde akina mama na akina baba wanalalamika ndoa zao ziko hatihati, tuangalie kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipatia nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu Rais wetu wa Jamhuri ya Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya na niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa heshima na taadhima kabisa kwa kutoa heshima kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tugonge meza mara mbili ili tuonyeshe heshma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ninaomba nimpongeze Jenerali Mabeyo kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya ya kudumisha amani katika nchi yetu hii ya Tanzania. Lakini pia niipongeze Wizara na Waziri Mheshimwia Elias Kwandikwa, jirani yangu, kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika Wizara hii ya Ulinzi lakini mwisho kabisa niwapongeze majenerali na mabregedia wote walioko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa na mimi nianze kuchangia katika hotuba ya bajeti hii. Moja kabisa tunafahamu ya kwamba JKT kwa sasa wameingia katika ushindani wa kuwekeza lakini wameenda mbali Zaidi katika kuhakikisha ya kwamba wana-compete zabuni mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia kwa maana ya kuiomba Wizara hasa JKT kumekuwa na ucheleweshaji wa miradi inayotekelezwa na jeshi letu la JKT. Nimuombe Waziri Mheshimiwa Waziri utakuwa ni shahidi katika Jimbo langu la Msalala tunao mradi mkubwa wa ujenzi wa jengo la Utawala katika Halmashauri ya Msalala ambayo inatekelezwa na JKT na Mheshimiwa Waziri niseme tu kwamba ukiangalia fedha iliyotengwa walitoa certificate ya kiasi cha shilingi milioni 515 kwa ajili ya hatua za awali za ujenzi wa jengo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo ucheleweshaji umeendelea kuimarika jengo hilo mpaka tunapozungumza sasa bado halijakamilika japo kuna jitihada ambazo zinaendelea. Niombe Wizara Mheshimiwa Waziri unanisikia upo hapo ndugu yangu, jirani yangu, tunapata tabu sana wananchi wa jimbo la Msalala Halmashauri yetu tumekaa katika sehemu ya kupanga tumebanana tunahitaji sasa tuhamie kwenye jengo hilo, niiombe Wizara, niwaombe JKT kumaliza mradi huu kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko juu ya wastaafu wetu, juu ya namna gani kuiomba Wizara na Serikali waweze kuwaongezea pension. Kama unavyofahamu wastaafu hawa baada ya kustaafu wanarudi vijijini kuja kujumuika na wananchi, kumekuwa na changamoto nyingi juu ya changamoto za kimaisha katika wastaafu hawa. Niiombe Wizara iweze kuona ninamna gani basi wanaweza kuongeza walau pension kidogo ili wasaidie wastaafu wetu hawa kuendesha maisha yao huko walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa kuwa Jeshi linatoa mafunzo mbalimbali, nikuombe kabla wastaafu wetu hawa hawajastaafu basi ni vyema Wizara ikae na kupanga waone namna gani basi wanaweza wakaanzisha short course ya kuwaandaa wastaafu wetu hawa wanapostaafu waende wakakabiliane na maisha ya huko vijijini. (Makofi)

Kwa hiyo, ni ukweli usiopingika kwamba wazee hawa, wastaafu hawa wanapokuja kule ni kweli usiopingika kwamba wanazalilika sana maisha ni magumu mno, wanapokuja kuanza ku-adopt mazingira ya kule vijijini wanapata taabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kwamba kumekuwa na malalamiko kwamba Mbunge mwenzangu amechangia hapa juu ya namna gani askari wetu wanajeshi wetu hawa wanapatiwa mavazi pair chache na ameshauri kwamba ikiwezekana walau waweze kupatiwa pair tatu. Lakini ni ukweli usiopingika kwamba Jeshi lina taratibu zake na taratibu za namna gani kuweza kutoa mavazi haya unaona kabisa hapa wanatakiwa wapewe mavazi mapya ya ndani ya miezi sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa ninavyozungumza bado baadhi ya wanajeshi hawa hawajapatiwa mavazi hayo mapya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri, vijana wetu hawa wanafanya kazi kubwa sana, lakini pia na wao wanahitaji wapate mavazi haya ili waonekane smart kama watu wengine, niiombe Wizara kama kunauwezekano basi Wizara ione namna gani inaenda kuwapa mtaji Jeshi la JKT, ili wafungue kiwanda cha kushona mavazi hawa wanajeshi wetu. Kwa kufanya hivyo tutasaidia kutengeneza ajira, lakini tutakuwa tumewajengea vijana wetu ili tuweze kuondokana na adha ya upungufu wa mavazi na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nimalizie kusema kwamba kumekuwa hakuna usawa juu ya usaili wa vijana wetu huko chini katika ngazi za chini katika kujiunga na Jeshi letu. Taarifa katika baadhi ya maeneo zinakuja leo kesho usaili umekwisha, kwa hiyo, niiombe Wizara ione namna gani inapotoa taarifa za usaili za vijana wetu hawa wapeleke mapema kule, lakini kumekuwa kuna urasimu pale mikoani, vijana wetu hawa baadhi wanaobahatika kuingia katika nafasi hizo wanapofika mkoani wanapewa vikwazo vingi vingi na wengine wanatolewa majina yanakuwa yameandaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri, sisi wana Mkoa wa Shinyanga ni waathirika wa hilo, hebu tuangalie tuone namna gani sasa Wizara inaenda kujipanga kuonesha ya kwamba inaondoa urasimu huo ili vijana na wao wapate sifa ya kujiunga na Jeshi letu hili la wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia naomba niendele kuwapongeza na ninaunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Kwa niaba ya wananchi wa Msalala naomba nichangie hotuba ya bajeti hii ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja nianze kwa kumpongeza Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika Taifa letu hili la Tanzania. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Waziri Kalemani kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika nchi hii ya Tanzania na Deputy wake kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Nitakuwa mchoyo wa fadhila bila kuwashukuru watumishi wote wa Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kuchangia katika maeneo matatu. Nianze kuchangia katika suala nzima la REA. Mheshimiwa Waziri nikuombe suala la REA hili katka Jimbo langu la Msalala na Mheshimiwa Mbunge mwenzangu leo yule wa Zanzibar ametutania hapa kwamba mradi wa REA katika Jimbo langu la Msalala Mheshimiwa Waziri bado na wewe mwenyewe ni shahidi. Pia sijui ni kwa nini Jimbo langu la Msalala na Mkoa mzima wa Shinyanga tumekuwa na bahati mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mbunge mwenzangu hapa tuna vijiji 92 katika Jimbo la Msalala lakini vijiji 63 bado havijapatiwa umeme. Siyo hilo tu hata mradi wa umeme jazilishi kwa maana ya desentification katika baadhi ya maeneo bado haujasambaa kwa uhakika. Nimuombe Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili tuweze kuambatana kwenda katika Jimbo la Msalala tuweze kuzindua miradi mbalimbali inayoendelea, lakini pia tufike katika maeneo yenye changamoto za umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu na maeneo mengine ya Mkoa wetu wa Shinyanga ukosekanaji wa umeme unapelekea kuhatarisha ndoa za kina mama. Akina mama wanajitahidi sana kupika wali na kuhakikisha umenyooka lakini unakuwa ni bokoboko kwa sababu wanatumia mbinu ya kutwanga badala ya mashine za kisasa za umeme ambazo zitachambua mchele vizuri na kuwapelekea kupika wali ambao utapelekea kudumisha mapenzi ndani ya ndoa. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri chondechonde fika Jimbo la Msalala tuone namna gani tunaenda kuanzisha umeme katika Kata za Jana, Mwalugulu, Mwakata na kata zingine zote zilizoko katika Jimbo la Msalala. Kwa kufanya hivi utanusuru ndoa za kina mama. Nikuombe baada hapa twende tukanusuru ndoa hizo za kina mama wa Jimbo la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie changamoto ya umeme katika uwekezaji. Katika Jimbo la Msalala wengi wetu ni wawekezaji katika sekta ya madini, tunategemea umeme ili shughuli hizi za uchimbaji ziweze kufanikiwa. Waziri alitoa maelekezo kwamba katika Kata ya Lunguya, Kijiji cha Nyangarata maeneo yote yenye machimbo wapeleke umeme. Nashukuru Mheshimiwa Waziri tayari umeme unaelekea katika Kijiji cha Nyangarata, lakini bado Ntambarare umeme haujafika. Haya maelekezo unayatoa huku Mheshimiwa Waziri watendaji wako hebu jaribu kuyafatilia wanayapuuza, ulisema utakapotoka waanze kupeleka umeme mara moja katika Kijiji cha Ntambarare Segese katika Kata ya Segese. Mheshimiwa Waziri hebu tusaidie kwa sababu ukuaji wa sekta ya madini katika Jimbo langu la Msalala tunategemea nishati ya umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kumekuwa na changamoto ya gharama. Wawekezaji wengi wanalia kwa sababu ya changamoto ya gharama na gharama hiyo ni KVA charges kama penalty. Unapoenda kuwekeza hao wateja wakubwa kuna gharama ambayo huwa inatozwa kama penalty kwa wawekezaji hawa na gharama hiyo inapelekea kuleta changamoto kubwa katika uwekezaji. Leo hii mtu analipa gharama ya umeme mathalani shilingi milioni 40, lakini hapo anapigwa penalty kwa ajili ya matumizi ya umeme wa ziada ambao yeye hautumii. Niiombe Wizara hebu jaribuni kuona ni namna gani sasa mnaenda kutupunguzia charges hizi na ikiwezekana mziondoe ili ilete unafuu kwa wawekezaji wetu katika maeneo hayo ya migodi na viwanda vikubwa katika Jimbo la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia ni namna gani mnaweza kuimarisha ugawaji wa transformer katika maeneo mbalimbali katika Jimbo langu la Msalala lakini pia katika maeneo mengi nchini kote. Nimekuletea concern za wafanyabiashara wengi ambao mpaka sasa viwanda vimesimama kwa sababu ya ukosefu wa transformer. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri bajeti hii itakapoenda kupita uone namna gani unaenda kuimarisha suala zima la usambazaji wa transformer kwa wafanyabishara wetu hawa katika maeneo yale ili na wao waweze kuendeleza viwanda vyao hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi hii, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi ya kuchangia. Pia namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuwakilisha vyema nje ya nchi na kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kwa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Mheshimiwa Waziri wa Madini, kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja niende kuchangia kwenye sekta ya madini. Tumeona, na ninawapongeza sana Wizara kwa kuhuisha Shirika letu la STAMICO. STAMICO wanafanya kazi kubwa sana. Ukilinganisha STAMICO ilipokuwa na sasa, unaona maendeleo makubwa sana; na tunaona uendelezaji wa ununuzi wa mitambo kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo wadogo umeshika kasi kubwa sana kwa sasa. Niendelee kuwaomba STAMICO pia waendelee kuondoka sasa kwenye maeneo ya uwekezaji mkubwa, waje sasa moja kwa moja kwenye uwekezaji wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona sekta ya madini wachimbaji wengi katika nchi hii hawana lesseni. Naomba Wizara, sisi tunaishi katika maeneo ambayo yana wachimbaji, maeneo mengi yamekamatwa na wachimbaji wenye PL na leseni kubwa. Leseni hizi ukiziangalia, bado watu hawazifanyii kazi. Kwa hiyo, naiomba Wizara kwamba wahakikishe wanaenda kuzipitia upya leseni hizi zote na ikiwezekana waweze kuzifuta wazirejeshe kwa wachimbaji wadogo wadogo ili wachimbaji wadogo wadogo waweze kupata leseni za uchimbaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitarudia aliyosema Mheshimiwa Musukuma kwenye Nishati; sisi tunaotoka kwenye majimbo ya vijijini tumeona kata zetu nyingi na vijiji vyetu vingi bado havina umeme na mabadiliko ya bei yaliyotoka ya shilingi 27; katika maeneo yetu huko kwenye ngazi za mkoa kuna maelekezo yametoka ambapo yanataka maeneo ya vijijini ambapo kuna vituo vya afya, sekondari na shule, basi bei ile ya shilingi 27 inaenda kuondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kazi anayoifanya Mama Samia Suluhu Hassan katika maeneo yetu haya ni kuweka miundombinu ya vituo vya afya hasa vijijini. Sasa unapochukua kituo cha afya kama kigezo cha kubadilisha bei ya shilingi 27,000/= kwa wananchi wale, maana yake ni kwamba unaenda kuwaumiza wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri yuko hapa, naomba alichukue hili, aende akapitie upya maelekezo hayo, aondoe; kwa sababu vijiji vyetu ukiangalia, center zake zina umbali mrefu wa kilometa moja. Unapochukua kigezo cha pekee kuwa na kituo cha afya ndiyo kigezo cha kuchajiwa 320 siyo sawa. Wananchi wetu bado wanahitaji umeme. Namwomba Mheshimiwa Waziri afute kauli hii, wananchi wetu waweze kupata haki ya umeme katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niende kwenye suala nzima la barabara na sisi wanashinyanga hasa Mkoa wa Shinyanga tunahitaji huduma ya usafiri wa ndege. Tuna kiwanja chetu Mkoa wa Shinyanga, tumepata ufadhili kati ya Serikali na Benki ya European Investment Bank ya European Investment ambayo imetoa kiasi cha shilingi bilioni tatu na Serikali imetoa shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege Mkoa wa Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka ninavyozungumza hivi, Wizara imeshindwa kutoa shilingi milioni 500 tu kwa ajili ya kulipa fidia ili ujenzi uanze. Naomba Wizara, toeni fedha hii shilingi milioni 500 iende ikalipe fidia kwenye eneo lile ili uwanja wa ndege uanze kujengwa na wananchi wa Shinyanga nao wapate huduma ya ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Leo ningependa kutoa mapendekezo yangu katika mpango huu wa Mwaka Mmoja wa 2023/2024 kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu kwamba Wizara na Serikali imetueleza hapa, kwamba imejipanga kuhakikisha kwamba inaboresha mazingira mazuri kwa wafanyabiashara hata hivyo pia mazingira mazuri katika ufanyaji biashara na uwekezaji katika nchi yetu hii ya Tanzania.

Leo mchango wangu na ushauri wangu utajielekeza kuielekeza Serikali kuongeza bajeti na kutenga bajeti na fedha katika kuhakikisha kwamba ina invest kwenye Jeshi letu la Polisi hasa katika kuwekekeza zana za kisasa katika kuweza kupunguza matumizi ya Askari Polisi barabarani. Ni ukweli usiopingika kwamba tunapozungumzia ukuaji wa uchumi na tunapozungumzia mazingira mazuri ya uwekezaji inaonesha ya kwamba ni lazima tutengeneze mazingira yanayoenda na uhalisia wa kumwezesha mfanyabiashara kutekeleza majumu yake kwa wakati au biashara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii utaona Jeshi letu la Polisi katika nchi yetu hii ya Tanzania imekuwa ni obstacle, imekuwa ni kikwazo kikubwa katika kuhakikisha ya kwamba inamwezesha mfanyabiashara kutimiza majukumu yake na kumwezesha kutimiza majukumu yake kwa wakati. Leo hii utaona unapozungumzia habari nzima ya uwekezaji ni lazima uzungumzie habari ya miundoimbinu. Serikali yetu nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuweka fedha kuimarisha miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii utaona barabara ambayo Serikali ime- invest fedha nyingi ili kumwezesha mfanyabiashara huyu aweze kutimiza majukumu yake ya kwa wakati, Jeshi la Polisi na hususan Usalama wa Barabarani wanasimama barabarani kuhakikisha ya kwamba ukaguzi wa magari yale, pia mara zote kuhakikisha ya kwamba huyu mfanyabiashara anaweza kutoka hapa kwa namna moja ama nyingine wanaweza kumzuia mfanyabiashara huyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejenga barabara ya njia Nane kutoka Dar-es-Salaam kuja mpaka Chalinze lakini utaona kila baada ya mita tano Askari Polisi hasa traffic hawa wamejaa barabarani, lengo ni ukaguzi ambao ukaguzi huu unamchelewesha mfanyabiashara kwenda kutimiza majukumu yake kwa wakati. Sasa niiombe Serikali iweze kuona namna gani inaweza ku- invest fedha ili iweze ku-invest kwenye Jeshi la Polisi kuwa na mitambo ya kisasa kuhakikisha kwamba inafanya kaguzi mbalimbali kwenye maeneo ya barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala zima la Madini. Niipongeze sana Wizara, mimpongeze Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba anaweka jicho lake kumsaidia mchimbaji mdogo mdogo katika maeneo yale. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika sekta ya madini. Ninaomba na ninashauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha upo hapa, leo hii mchimbaji mdogomdogo hasa sekta ya madini na Mheshimiwa Rais alitoa maealekezo kwamba anahitaji Wizara ya Madini, iweze kuchangia Pato la Taifa sasa ili Wizara ya Madini, iweze kuchangia Pato la Taifa lazima Serikali iweke mkakati na bajeti kubwa kuhakikisha ya kwamba inamwezesha huyu mchimbaji mdogomdogo. Kwa hiyo, naomba nishauri Wizara na Serikali iweze kutenga fedha ili iweze kuwakopesha hawa wachimbaji wadogowadogo katika kwenda kufanya uwekezaji kwenye maeneo yao ili waweze kuzalisha kwa wingi na kuweza kuchangia Pato hili la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nizungumzie suala zima la barabara. Leo miundombinu ya barabara yetu katika maeneo yetu haya niipongeze Serikali na nimpongeze Mheshimiwa Rais kwenye Jimbo langu la Msalala, ametoa maelekezo kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye kiwango cha lami kutoka Bulyanhulu kwenda mpaka Kahama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na urasimu katika utekelezaji wa miundombinu hii kwa wakati. Sasa niiombe Wizara kwamba ihakikishe pale ambapo tunatenga fedha na bajeti kwenda kujenga barabara wapitie upya mambo ambayo yanakwamisha utekelezaji wa miundombinu hii ya barabara ili kuwezesha barabara hizi ziweze kutekeleza kwa wakati na kumwezesha mfanyabiashara kutumia barabara hizi katika kutekeleza majukumu yake kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara yangu ambayo tayari Mgodi wa Bulyanhulu umetenga fedha kiasi cha Dola Million 40 kwa ajili ya utekelezaji wa barabara. Barabara hii kwa muda mrefu sana tumeweza kuipambania Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni shahidi, mpaka dakika ya mwisho Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, ametoa tamko kwamba barabara ile sasa fedha ipo tayari na barabara ile ianze kujengwa maana ya kutoka Bulyanhulu mpaka Kahama, lakini leo hii utaona Wizara ya Miundombinu na Ujenzi kutoa tu kibali cha kuweza kuitangaza barabara hii ianze kujengwa mpaka leo bado hakijatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe ili mpango huu ambao tunaujadili hapa uweze kutekelezeka kwa wakati ni lazima tupunguze urasimu ndani ya Serikali. Tunapanga mpango huu sisi wenyewe lakini sisi wenyewe hawa hawa tunaukwamisha huu mpango. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, aweze kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais ya kuanza kutangaza barabara hii na ianze kujengwa kwa wakati, barabara yenye kilometa 77 ambapo fedha zake anayelipa ni mgodi na mgodi upo tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana leo hii tunaona fedha zile tumepewa na Mhisani hivi ikitokea leo madini yamepotea fedha zile tutazitoa wapi? Mlipaji yupo tayari na anataka kujenga barabara ile kwa wakati lakini Katibu Mkuu kutoa tu kibali barabara ile ianze kujengwa hajatoa mpaka leo ilkitokea leo madini yale yamepotea tunafanya nini? Ahsante sana. (Makofi)