Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Fredrick Edwad Lowassa (1 total)

MHE. FREDRICK E. LOWASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yako mazuri. Ni kweli kwamba Wananchi wa Jimbo la Monduli wanamwamini sana Mheshimiwa Rais na wanaimani kubwa sana na ahadi yake, lakini ni kweli pia tunaamini uongozi wa Wizara ya Maji ukiongozwa na ndugu yangu Mheshimiwa Juma Awesso, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; tayari Monduli kuna miradi ambayo ipo ya maji lakini inasuasua, tunaomba kauli ya Serikali kuhusu mradi na mpango ambao mmejipanga nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunaomba kuhakikishiwa usimamizi mzuri juu ya ahadi hii ya Mheshimiwa Rais. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Lowassa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miradi ambayo inasuasua mpango wa Wizara ni kuhakikisha kwamba miradi yote inakamilika kufikia wiki ya maji mwaka huu mwezi Machi na tayari wataalam wetu wanaendelea kufanyia kazi kwa maana ya miradi ambayo imetekelezwa kwa kutengeneza miundombinu lakini maji hayako bombani, tunatarajia kufikia mwezi Machi, Wiki ya Maji miradi hiyo itaanza kutoa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu usimamizi wa ahadi ya Mheshimiwa Rais, wote tunafahamu ahadi ni deni na ahadi hii ni ya Mheshimiwa Rais, naomba nimpe amani Mheshimiwa Mbunge kwamba miradi hii tutakwenda kusimamia na nafahamu alikuwa na ahadi na Mheshimiwa Waziri kwenda jimboni kesho lakini ile safari imeahirishwa kwa sababu ya msiba mkubwa uliotokea pale ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kwa hiyo hali itakapotulia kwenye Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Waziri atakwenda na kuhakikisha usimamizi unafanyika vizuri. (Makofi)