Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Francis Kumba Ndulane (48 total)

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Kilwa kuna changamoto inayofanana na Wilaya ya Mtwara katika huduma hii ya maji:-

Je, Serikali ni lini itatekeleza mradi wa maji kutoka Mto Rufiji ili kuwaondolea changamoto ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kilwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali ina mipango mikakati ya kuona kwamba Mto Rufiji iwe ni sehemu ya miradi mikubwa ya kutoka maziwa makuu na mito, kuona kwamba maji yale sasa yanakwenda kunufaisha wananchi. Hivyo, kwa watu wa Kilwa pia tunaendelea kuwasihi waendelee kutuvumilia kidogo, huenda mwaka 2021/2022 kadiri tutakavyokuwa tunapata fedha, watu wa Kilwa pia watapata maji kupitia Mto Rufiji. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. Kwa sasa Barabara ya Tingi – Kipatimu ina maeneo mengi ambayo hayapitiki na mengine yanapitika kwa shida sambamba na Barabara ya Nangurukuru – Liwale.

Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuweza kurekebisha barabara hizo mbili ili ziweze kutengenezwa na hatimaye wananchi waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara hizi mbili za Nangurukuru – Liwale kilometa 258 na hiyo ya Tingi – Kipatimu katika miaka ya karibuni zilipanuliwa upana wake, lile eneo la hifadhi ya barabara kutoka mita 30 hadi kufikia mita 45. Na hii Hali ilisababisha wananchi kuweza kuvunjiwa nyumba zao na kuondolewa mazao yao. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa wananchi ambao hawajalipwa hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Tingi – Kipatimu ina vilima, na katika swali lake la msingi nimejibu kwamba, tayari TANROADS Mkoa wa Lindi umeainisha maeneo yote korofi ambayo yana vilima na yatawekewa lami. Na hivi tunavyoongea mwaka huu itawekwa walao mita 500 na mwaka wa fedha kama bajeti itapita pia, maeneo yameainishwa ambayo tunategemea kuongeza kiwango cha lami maeneo ambayo barabara inakuwa ina milima na inateleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Barabara ya Nangurukuru – Liwale, yako maeneo ambayo inapita kwenye bonde na maji huwa yanajaa. Na tunategemea kwenye bajeti ya mwaka huu tunayoiendea kama itapitishwa litajengwa tuta kubwa ambapo maji sasa yatakuwa hayana uwezo wa kufurika na kuziba njia hiyo ya Barabara ya Nangurukuru – Liwale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia, ni kweli kwamba, baada ya sheria kupitishwa barabara zetu zimetanuliwa kutoka mita 30 hadi 45, lakini 45 hadi 60. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mita hizi ambazo zimeongezeka saba na nusu, sab ana nusu kwa upande, pale ambapo ujenzi utaanza basi wananchi hawa ambao watakuwa ni wathirika watapata fidia wakati mradi huu utakapoanza kutekelezwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Hospitali ya Kipatimu ambayo imekuwa ikiendeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi ya Kanisa Katoliki imekuwa na changamoto kubwa ya mtaalam wa mashine ya x-ray. Itakumbukwa kwamba mwaka 2017 Serikali ilitumia jumla ya shilingi milioni 60 kuleta mashine ya x-ray katika hospitali ile lakini mpaka leo hatujawa na mtumishi wa kitengo hicho.

Je, katika hizi ajira chache 2,726 ambazo zimetangazwa hivi karibuni, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kunihakikishia kwamba moja kati ya watumishi hao atapelekwa katika Hospitali ya Kipatimu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri wa TAMISEMI lini atakuwa tayari kutembelea Wilaya ya Kilwa ili kutambua changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa? Ahsante.
(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, mwaka 2017 ilipeleka mashine ya x-ray na mpaka sasa utaratibu wa kumpata mtumishi kwa maana ya mtaalam wa x-ray upo hatua za mwisho na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira hizi ambazo tumezitangaza, tutakwenda kuhakikisha tunapata mtaalam wa x-ray kwa ajili ya kwenda kutoa huduma katika Hospitali ya Kipatimo.

Mheshimiwa Spika, lakini pili niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kufanya ziara katika Jimbo la Kilwa mara baada ya kumaliza session hizi za Bunge Juni 30, 2021. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu namba moja la nyongeza ningependa kufahamu, kwa kuwa katika Mikoa ya Kusini kumekuwa na vyanzo vingi vya maji vinavyotokana na mito mikubwa kama ule wa Rufiji, Ruvuma, Mavuji, Lukuledi, Luhuhu pamoja na Ketewaka kule Njombe. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inamaliza tatizo la maji kwa asilimia 100 kama ilivyofanyika Kanda ya Ziwa kupitia vyanzo hivi vya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Ndulane kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri. Nipende tu kumjibu swali lake la nyongeza la matumizi ya maji yote yanayopatikana kwenye mito na vyanzo vyote vikubwa vyenye uhakika kwa miradi endelevu. Sisi kama Wizara, mikakati yetu katika mwaka ujao wa fedha na kuendelea, ni kujenga miradi mikubwa inayofanana na mradi huu wa Ziwa Viktoria. Mikakati imekamilika na kwa Kusini pia tumepanga kutumia Mto Ruvuma, Mto Rufiji na Ziwa Tanganyika. Hii yote tutakuja kuitekeleza kadri tutakavyokuwa tukipata fedha. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza, napenda kumwuliza Waziri wa Ujenzi kwamba, kwa kuwa katika mwaka 2019, Serikali ilichepusha katika Kijiji cha Njinjo, barabara ya Nangurukuru – Liwale na hivyo ililazimu kulipa fidia kwa baadhi ya wananchi ambao walikuwa na mali zao katika lile eneo ambalo limechepushwa barabara; lakini kuna wananchi wawili hadi kufikia sasa hawajalipwa fidia ya mali zao; nao ni Mama Mary Mahmoud Kiroboto pamoja na Ndugu Said Salum Karanje, ambao wanadai jumla ya shilingi 13,264,180/ =. Napenda kujua: Je, Serikali ni lini itawalipa wananchi hawa wawili haki yao ya fidia kwa ajili ya kuchepusha kipande kile cha barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, napenda kumwuliza Waziri kwamba, kwa kuwa wakati wa maadhimisho ya Kumbukizi za Vita vya Majimaji ilipotimiza miaka 100 mwaka 2010, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati ule, aliwaelekeza Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Lindi…

NAIBU SPIKA: Uliza swali lako, Mheshimiwa Ndulane.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nashukuru. Alitoa maelekezo wafungue barabara kati ya Nandete na Nyamwage: Je, mpango huu umefikia wapi wa kufungua barabara ile ya kipande cha Nyamwage kwenda Nandete? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa, Francis Ndulane Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake amesema kwamba, kulitolewa ahadi na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tatu. Napenda tu nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa hii barabara ilitakiwa ifunguliwe maana yake haipo kwenye mtandao wa barabara za TANROAD wala za TARURA. Hivyo napenda nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imelichukua na tutawasiliana na Meneja wa TANROAD Mkoa wa Lindi ili tuweze kupata taarifa sahihi na ahadi hii ili tuweze kuanza kuitekeleza ama kama ilikwama tujue ni kwa nini ilikwama wakati ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili, kama ulivyotoa maelekezo, ni swali ambalo lipo very specific na kama watu hao wapo ni bora wakaandika barua rasmi kwa TANROAD Mkoa wa Lindi, wakupe copy na sisi watupe copy ili tuweze kuliangalia, kwa sababu ni suala la watu wawili, tuweze kuliangalia kama lina changamoto gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa kwa muda mrefu wavuvi wadogo wadogo kutoka katika Wilaya ya Kilwa na maeneo mengine ya nchi yetu ya Tanzania wamekuwa hawapati mikopo kutoka kwenye mabenki kwa ajili ya kufanyia shughuli zao mbalimbali za kuboresha shughuli za uvuvi.

Je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa kuweza kuwaundia hawa wavuvi wadogo wadogo mfuko maalum ambao wataweza kukopa kwa riba ndogo na hatimae hiyo mikopo iweze kuwanufaisha katika kufanya shughuli zao za uvuvi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Wilaya ya Kilwa kumekuwa na wimbi kubwa la uingiaji wa wafugaji wenye mifugo mingi sana hasa katika Kata za Somanga, Tingi, Kandawale, Njinjo, Mitole, Likawage, Nanjilinji pamoja na Kikole.

Je, Mheshimiwa Waziri ni lini atafika katika Wilaya ya Kilwa ili kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Kilwa kwenda kutatua changamoto mbalimbali zinazotokana na uingiaji wa mifugo mingi katika Wilaya ya Kilwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndulane Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Uvuvi kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo waweze kupata mikopo ya bei nafuu na yenye riba ndogo. Ninaungana na yeye na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya Wabunge wote ambao wanasimamia wavuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa miaka mitano tulionao Wizarani mwaka 2021-2016 wa kuhakikisha tunaupa nguvu uchumi wa blue, jambo hili la kuanzishwa kwa Fisheries Development Fund (Mfuko wa Maendeleo ya Uvuvi) ni miongoni mwa jambo lililopewa kipaumbele. Kwa hivyo, Mheshimiwa Mbunge nikupongeze kwamba umelileta jambo ambalo tayari Serikali imeshaliona na kwa hivyo tunakwenda kulianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili la kuingia kwa mifugo. Tayari tumekwenda kufanya ziara na nimpe pole sana yeye na wananchi wote, lakini tumekwenda na tumezungumza na makundi mbalimbali, katika Wilaya ya Kilwa nilifika katika Kata ya Nanjilinji kwenda kuzungumza na wananchi pale lakini niko tayari kurejea tena ili kusudi tuweze kufika kule kote alipotaja Mitole, Njinjo, Likawage, Kandawale na hata kule Miguruwe na Zinga Kibaoni, ili kuweza kwenda kuzungumza na wananchi kwa niaba ya maombi haya ya Mheshimiwa Mbunge na hatimaye kuweza kupata suluhu ya tatizo hili kubwa ambalo linawasumbua wananchi wa Kilwa Kaskazini. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa nyakati tofauti hapa Bungeni na pia kwenye ziara za viongozi katika Jimbo langu ikiwemo ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mwezi Oktoba mwaka 2021, niliiomba Serikali iweze kujenga barabara njia nne kwenda Kipatimu kwa kiwango cha lami ambayo ina urefu wa kilometa 50.

Mheshimiwa Spika, nashukuru Serikali imeanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami katika kipande cha kilometa 1.4 katika eneo la mteremko mkali wa Kilimangoge pamoja na eneo la Kijiji cha Ngorongoro:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia eneo lililobaki la kilometa 48.6? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kumba Ndulani, Mbunge wa Kilwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika ziara hiyo nami nilikuwepo na Mheshimiwa Waziri Mkuu kweli aliahidi kwamba barabara hiyo itajengwa. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii tumeichukua na tunaiingiza kwenye mpango kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, pia napokea pongezi kwamba tayari tumeshaanza kujenga hizo kilometa chache. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba kadiri Serikali itakavyopata fedha, hizi kilomita 48.6 zilizobaki tutajenga barabara kwa kiwango cha lami kuanzia Njia Nne hadi Kilwa Kipatimu.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kuniona.

Swali langu ni kwamba je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya polisi katika Tarafa za Kipatimu, Njinjo na Mandawa Wilayani Kilwa ili kudhibiti vitendo vya uhalifu katika Wilaya ya Kilwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikiri juu ya changamoto ya upungufu wa vituo vya polisi katika kata za jimbo ambalo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, lakini nizungumze kwa ujumla wake kwamba tuna upungufu wa vituo vya polisi tuna mpango wa kuongeza vituo vya polisi kwa miaka kumi zaidi ya mia tatu na hamsini na kitu ambavyo tunahitaji zaidi shilingi bilioni mia moja sitini na kitu.

Nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mikakati ya kufanikisha mkakati huu wa ujenzi na Wabunge wengine ambao wana shida ya vituo vya polisi katika maeneo yao kwa miaka kumi, mwelekeo wa kuutekeleza mkakati huo katika kipindi kifupi sana upo katika hatua nzuri. Kwa hiyo, wakae mkao wa kula, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine kwamba tuna mkakati kabambe na upo katika hatua nzuri ya kuukamilisha kabla ya muda uliopangwa ambao utatusaidia sana kupunguza changamoto za vituo vya polisi katika nchi hii.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika mgogoro huu wa madai ya fidia, hivi sasa umechukua miaka mitano na jumla ya watu 63 wamehusishwa katika jambo hili: Je, Serikali ipo tayari kulipa fidia ya nyongeza kutokana na ucheleweshaji wa malipo haya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, napenda kutaka kujua: Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuwa na nafasi ya kuweza kuambatana nami twende kwa pamoja tukasuluhishe huu mgogoro? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nianze na la pili, tukimaliza kipindi hiki cha Bunge, tutapanga ratiba vizuri na Mheshimiwa ili tuweze kuona namna ya kumaliza jambo hili kwa pamoja kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la kwanza, Serikali ipo tayari kumlipa mtu fidia kwa kadri anavyostahili kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, kama nilivyosema, tutaenda pamoja na kusaidiana kutatua jambo hili, na lipatakapokwisha wale wanaostahili kulipwa fidia na kwa mazingira tuliyokuwa nayo, aidha ya ucheleweshaji au nyongeza, itafanyika kwa mujibu wa sheria.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza, nina maswali mawili: -

Kwanza, kwa kuwa katika Tarafa mbili zilizobaki ambazo Serikali bado haijawekeza ujenzi wa vituo vya Polisi, kumekuwa na changamoto kubwa ya mapigano kati ya wafugaji na wakulima lakini wakati huo huo Tarafa hizo zipo umbali mrefu sana kutoka kule ambapo vituo vya Polisi vipo hivi sasa: -

Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu katika Tarafa za namna hii zenye changamoto kubwa ya wakulima na wafugaji kuweza kuwekeza kama ilivyowekeza katika sekta nyingine ujenzi wa Vituo vya Afya kwa kuanzia na bajeti ya mwaka huu? (Makofi)

Pili, ningeomba Mheshimiwa Waziri anifahamishe ni lini atakuwa na nafasi ya kuweza kutembelea katika Wilaya ya Kilwa ili tuweze kushirikiana na Wizara yake katika kutatua changamoto ambazo zinakabili upatikanaji wa vituo vya Polisi. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Francis Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza alitaka kujua mpango wa Serikali wa kujenga vituo vya Polisi kama vile ambavyo tunafanya katika vituo vya Afya na shule, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba wazo lake tumeshaanza kulifanyia kazi, tulikuwa na mazungumzo kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Wizara ya TAMISEMI.

Nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwa kulipokea wazo hili na hivi sasa tunavyozungumza wataalam wetu, Makatibu Wakuu wa Wizara hizi mbili na wataalam wetu wanakaa kuangalia uwezekano huo kupitia kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hili ni jambo ambalo tunalichakata na kama litakuwa limekwenda vizuri tunaweza tukaliwasilisha hapa Bungeni kulingana na mapendekezo ambayo wataalam watatupatia.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la mimi kutembelea, hilo halina mjadala. Nimhakikishie Mheshimiwa Francis Ndulane kwamba tutapanga ratiba ili tuweze kwenda katika Jimbo lake kuhamasisha wananchi, kama vile nilivyojibu kwenye swali la msingi kwamba kama wananchi wataweza kufanya utaratibu wa kupata eneo na hata wakianza wa kwa nguvu zao, kama ambavyo kuna maeneo Waheshimiwa Wabunge wamefanya, naye pia alifanya hivyo katika baadhi ya vituo vyake, hata juzi hapa Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula katika Jimbo lake pale, alifanya jitihada za kuhamasisha wananchi kujenga Kituo cha Polisi Ilemela. Kwa hiyo, jitihada kama hizi tutaziunga mkono.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ndulane ninajua jitihada zake katika kupigania wananchi wake na hivyo basi nimhakikishie tutashirikiana kutafuta njia mbadala ya haraka wakati tukisubiri mipango ya muda wa kati na muda mrefu wa Serikali kutatua changamoto hii kwa kudumu.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Katika kipindi cha bajeti niliuliza swali la msingi kuhusiana na utekelezaji wa maji ya kutoka Mto Rufiji, nikaelezwa kwamba katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023, upembuzi yakinifu ungefanyika, sasa napenda kujua Serikali imefikia hatua gani katika upembuzi yakinifu uliotarajiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mto Rufiji ni moja ya mito muhimu sana kwa vyanzo vya maji ambavyo sisi tunavitumia. Tayari wataalam wetu wameshaanza kazi na tunatarajia watakamilisha upembuzi yakinifu kwa namna ambavyo muda umepangwa.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Katika Jimbo la Kilwa Kaskazini Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga minara 37 katika vijiji 37 vya Jimbo letu la Kilwa Kaskazini na hivyo vijiji 16 vimebaki vikiwa havina mawasiliano ya simu za mkononi.

Je, ni lini Serikali itajenga mitandao ya mawasiliano ya simu ya mkononi katika vijiji hivyo 16 vilivyobaki?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika jimbo hili ni zaidi ya asilimia 70 na sasa Wizara yetu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeandaa timu ya kuzunguka nchi nzima na kufanya tathimini na kuangalia maeneo yote ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano ili yaweze kuingizwa kwenye utaratibu wa utekelezaji. Kwa hiyo, naamini kabisa timu hii itakapokamilisha kazi yake, basi tunaamini kwamba bajeti tutakayoileta hapa itakuwa inatazama kwa mapana kulingana na matatizo ya changamoto ambazo zitakuwa zimetokea katika Jimbo la Kilwa Kaskazini. Ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana kwa kuniona. Wizara katika siku za karibuni ilitoa nafasi kwa Vikundi Mbalimbali vya Uvuvi viweze kuomba mikopo katika Wizara hiyo. Swali langu, je, ni lini fedha hizo zitatoka ili ziweze kuwanufaisha wananchi wetu wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa wanufaika wa mikopo ile ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa Wavuvi inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Wavuvi wa Kilwa, watapata boti hizo na tayari taratibu zimekwishakamilika, orodha ya wanufaika iko tayari tuta- share na Waheshimiwa Wabunge wote ili muweze kuona kile mlichokiomba ni hiki kimepatikana na kwa kusudi hilo muweze kuwafikishia walengwa wajipange ili tuweze kutekeleza kazi ya uzalishaji, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunijibu swali langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri; kwamba kutokanana changamoto kuwa kubwa ya migogoro ya wakulima na wafugaji kila kukicha ambayo imesababisha watu mbalimbali kupambana na kufa wengine, wengine wamepata ulemavu.

Je, haioni kwamba kuna uhitaji sasa wa kuharakisha huu mpango wa matumizi bora ya ardhi, ili vijiji bora 34 vilivyobaki viweze kumalizwa kupangwa katika huu mpango wa matumizi bora ya ardhi mwaka 2023/2024?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swalli la pili. Katika kipindi cha miaka 10 Takwimu za Sensa zimeonesha katika Wilaya ya Kilwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi. Mwaka 2012 tulikuwa na wananchi 190,744, mwaka 2022 takwimu za sensa zinaonesha kwamba wananchi wa Wilaya ya Kilwa wameongezeka hadi kufikia 297,676 sawa na ongeezeko la watu 106,932 sawa na asilimia 52 ya ongezeko. Kutokana na ongezeko hili ni wazi kwamba sehemu kubwa ya watu walioongezeka ni jamii ya wafugaji...

MWENYEKITI: Uliza swali.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa kuweza kuwahamisha baadhi ya wafugaji kutoka Wilayani Kilwa kwenda maeneo mengine ya nchi kama ilivyofanya katika Bonde la Ihefu na katika Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna changamoto ya mogogoro kati ya wafugaji na wakulima katika Halmashauri ya Kilwa, lakini pia katika baadhi ya halmashauri hapa nchini. Serikali imeendelea kuchukua hatua, na hatua moja muhimu ni kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji ili kuwa na maeneo mahsusi kwa ajili ya kilimo, pamoja nakuwa na maeneo mahsusi kwa ajili ya ufugaji lakini pia kutunza vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika Halmashauri ya Kilwa kama nilivyotangulia kusema tayari bajeti imeandaliwa ya milioni 60 kwa ajili ya kupitia mipango bora ya ardhi. Zoezi hili ni endelevu mpaka tutakapokamilisha vijiji vingine vilivyobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili kuhusiana na ongezeko la wananchi ni kweli wafugaji wengi wamehamia Kilwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla na baadhi ya mikoa mingine. Serikali inaendelea kufanya tathmini na kuona maeneo yale ambayo yana wafugaji wengi basi tuweze kuweka mgawanyo sahihi ili kulinda mazingira lakini kuepusha migogoro, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Kilwa, katika Vijiji vya Marendego na Kinjumbi kumekuwa na miradi ya maji ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa zaidi ya miaka mitatu hivi sasa.

Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini miradi hii itakamilika ili wananchi wa vijiji hivyo waweze kupata huduma ya maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis, Mbunge wa Kilwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vijiji hivyo ulivyovitaja Mheshimiwa Mbunge ni kweli kazi zimeendelea zikifanyika. Baada ya Bunge hili naomba tuwasiliane ili tuweze kuona tunafika pamoja katika miradi hii.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa wilaya zitakazonufaika na mradi wa ujenzi wa vyuo 63 vya VETA, tumeshaandaa eneo katika Kitongoji cha Matapatapa Kijiji cha Njia Nne na pia tumewekeza shilingi milioni 6.5 kwa ajili ya uandaaji wa hati pamoja na kufanya environmental impact assessment.

Je, ni lini ujenzi wa chuo hicho utaanza?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyozungumza kwenye majibu ya msingi kwamba tutakapokamilisha tu taratibu za manunuzi pamoja na hizi geo-technical, topographical pamoja na environmental impact assessment tunatarajia kuanza. Matarajio yetu kunako kuanzia mwezi wa nne hivi tuweze kuanza ujenzi huu katika maeneo yote nchini. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona; je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya umeme wa REA katika Kijiji cha Tilawandu ambacho kilisahaulika katika awamu zilizopita za utekelezaji wa umeme wa REA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu naomba kujibu naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Ndulane, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vijiji vyote ambavyo vilikuwa havina umeme vipo katika mradi wa REA Awamu ya III Mzunguko wa Pili na kwa sasa tuna takribani vijiji 2,600 tu ambavyo vimebaki havina umeme kabla ya Desemba vitakua vyote vimepata umeme.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo chetu cha Polisi cha Somanga kimechakaa sana.

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo kipya katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ndulane kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba ni kweli kituo cha Somanga ni cha muda mrefu na kimechakaa kama ilivyokuwa vituo vingi maeneo mbalimbali nchini. Tutakachofanya kabla ya kuki-condemn kituo hiki kwamba hakifai kwa matumizi ya binadamu tutaenda kufanya tathmini ya uchakavu wa kituo hiki. Iwapo itaonekana kuwa gharama za ukarabati ni kubwa au zinakaribia kulingana na gharama za ujenzi kitaingizwa kwenye mpango wa ujenzi wa kituo kipya, nashukuru.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika barabara ya Njia Nne hadi Kipatimu tayari Serikali imejenga kilometa 1.9 za lami. Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha kilometa zilizobaki katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuikamilisha hiyo barabara kwa kiwango cha lami, lakini tutakwenda kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Swali langu ni kwamba; je, ni lini Serikali itapeleka fedha Wilayani Kilwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Maafisa Watendaji Kata wa Kata za Somanga, Namayuni, Mitole na Njinjo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaelekeza kutumia fedha za mapato ya ndani kuanza Ujenzi wa Ofisi za Maafisa Watendaji wa Kata. Nitumie fursa hii kusisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa kutenga fedha kwa ajili ya Kata hizi za Somanga na Kata nyingine ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, ili watendaji wetu wapate maeneo mazuri ya kufanyia kazi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Kilwa ina majimbo mawili; je, Serikali ina mpango gani wa kuleta ambulance zaidi ya moja ili kukidhi uhitaji katika Wilaya yetu ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini, kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunapeleka magari ya wagonjwa kwenye kila halmashauri, lakini ndani ya halmashauri kuna vipaumbele vya maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa zaidi wa magari ya wagonjwa. Kwa hiyo, tunapeleka magari mawili katika Halmashauri ya Kilwa, lakini pia kukiwa na uhitaji na vigezo vya kutosha, basi tutaona namna ya kuepeleka gari nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tangu mwanzo wakati Mheshimiwa Waziri, anatoa jibu nimeonyesha masikitiko makubwa sana kwa swali langu kutojibiwa, lakini nimshukuru Mheshimiwa Waziri, katika paragraph ya mwisho ya swali lake ameeleza ukweli kwamba swali hili lilipaswa kujibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, tena ametaja mpaka sheria ambayo inaipa Mamlaka Wizara ya Maliasili na Utalii, kutangaza hizi kumbukumbu za kihistoria kwenye Gazeti la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikiombe kiti chako kwa kuwa swali halikujibiwa. Siku ya Ijumaa tarehe 28, saa tatu asubuhi niiombe Wizara ya Maliasili na Utalii, iweze kuja kujibu swali hili kwa ufasaha. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu mchango wa Mheshimiwa Francis Ndulane, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tunafanya kazi kwa kuwajibika kama Serikali moja na ndiyo maana nimemjibu Mheshimiwa Francis Ndulane kwamba pamoja na swali kuja Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nikaelezea sheria ambayo inatuongoza. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi tutashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, kuhakikisha tunashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kumwongoza na kupitia utaratibu ambao nimeueleza wa kuangalia hiki Kijiji cha Nandete kama kina sifa ya kuingia kwenye kumbukumbu za nchi yetu za maeneo ambayo yalitumika katika vita vya maji maji, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika wilaya ya Kilwa Jeshi letu la Polisi lina gari chakavu sana. Je, ni lini Serikali itapeleka gari jipya kwa ajili ya matumizi ya Jeshi letu la Polisi, Wilayani Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwenye jibu langu la msingi kwamba katika mwaka huu wa bajeti tunaoendelea nao, Serikali imetutengea bilioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa magari na ahadi yetu ni kwamba ma-OCD wote watapata mgao wa magari haya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ndulane kule Kilwa pia watapata mgawo wao, nashukuru.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Katika Kituo chetu cha Polisi kilichopo katika Kata ya Somanga, Wilayani Kilwa chenye watumishi 19, hakina hata nyumba moja ya watumishi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwajengea nyumba watumishi hawa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kujenga kadri ya upatikanaji wa fedha, maadam jengo la polisi lipo. Tutakachoendelea kufanya ni kuhakikisha kwamba eneo linapatikana na sisi tuingize kwenye bajeti kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Ndulane kama eneo limeshapatikana kwenye halmashauri husika, tuko tayari kushirikia nao kuhakikisha nyumba hizo zinajengwa, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Katika Jimbo letu la Kilwa Kaskazini lina mtandao wa barabara za TARURA kilometa 528 ambazo zote ni za vumbi. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TARURA itaanza kujenga barabara za lami katika Jimbo la Kilwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ninarudia tena tayari TARURA imeongezewa bajeti na Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tutaangalia na Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Lindi na Wilaya ya Kilwa kuona katika bajeti ambayo imepitishwa hapa ni kilometa ngapi ya lami ambayo imetengwa ili katika hizi barabara za Kilwa alizotaja Mheshimiwa Ndulane angalau moja ianze kupata lami.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo mwaka 2006 Serikali iliridhia mifugo kuhamishwa kutoka Bonde la Ihefu kupelekwa Mkoani Lindi, hivi ninavyozungumza katika Wilaya za Liwale, Kilwa na Nachingwea kuna mafuriko makubwa ya mifugo na hivyo kusababisha kuwa na uhaba wa malisho, maji pamoja na huduma nyingine za mifugo.

Je, kuna utaratibu gani ambao Serikali imeupanga kwa ajili ya kidhibiti mifugo hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge amelieleza hapa lina ukweli kwa sababu idadi kubwa ya mifugo sasa hivi wamekuwa wakielekea upande wa kusini, ndiyo maana moja ya mipango mikakati ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunayo sasa hivi ni kuongeza maeneo ya malisho, tunapeleka mabwawa ili ku-control sasa ule ufugaji holela. Kwa hiyo, jambo hilo tumelipokea kwa umuhimu mkubwa na tutaleta mpango kazi kwa ajili ya maeneo hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaainisha, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunujibu swali langu kwa ufupi na kwa malengo ambayo niliyakusudia. Ninapenda nishauri barabara hii ianze kujengwa toka Nangurukuru kuelekea Liwale kwa sababu itatengeneza muunganiko wa lami inayotoka Dar es Salaam – Kilwa Masoko pamoja na Mkoani Lindi kuelekea Liwale na kugusa majimbo yote yalipo katika barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kupata kujua;

Je, katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii, itajengwa kilometa ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna barabara ya kutoka Njianne kwenda Kipatimu yenye urefu wa kilometa 50, imekuwa ikijengwa kwa urefu wa mita 700 mwaka 2021, mita 700 2022 na mita 600 2023;

Je, ni lini Serikali itakuja na mradi wa kimkakati ili iweze kujenga kwa urefu mrefu katika barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake wa karibu katika barabara hii. Lakini pia tumeupokea ushauri wake, kwamba ianze kujengwa kutoka Nangurukuru kwenda Liwale, naamini haya tutaweza kuyazungumza. Mkandarasi huyu mmoja anaweza akaanza upande wa Nangurukuru – Liwale ama Liwale – Nangurukuru, yote yanawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake mawili ya nyongeza, la kwanza anataka kujua ni kilometa ngapi katika ujenzi huu utakaoanza Mwaka wa Fedha 2023/2024; ni kilometa 72 kati ya kilometa 230.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anataka kujua barabara hii ya Tinga – Kipatimu, ni kweli kwamba barabara hii tumekuwa tukiijenga sisi kama TANROADS kidogokidogo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuijenga barabara hii hadi ukamilifu wake, na sasa tumetenga jumla ya takribani milioni 281.81 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara hii katika Mwaka wa Fedha ujao, 2023/2024, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika Mkoa wetu wa Lindi barabara zetu kuu na barabara za mikoa zina changamoto hii kubwa ya kuwepo kwa vigingi katikati ya makazi ya wananchi;

Je, ni lini Serikali italipa fidia ili wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, suala hili linafanana sana na suala la msingi na jibu langu litaendelea kubaki kwamba; ndiyo maana katika bajeti hii tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya tathmini, na kama ni maeneo ambayo tunayahitaji kwa sasa tutakuja tuwafidie halafu tuweze kujenga hizo barabara ama kuacha hiyo corridor ikiwa wazi baada ya kuwaondoa wananchi kwa kuwafidia likiwa ni pamoja na hilo la eneo la Mheshimiwa Mbunge ambalo amelisema. Ahsante.
MHE. FRANSIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naona majibu ya Mheshimiwa Waziri yamekuwa mepesi sana. Hii changamoto ya funza mwekundu iligundulika kwenye miaka ya 1940, sasa ni miaka zaidi ya 80 imepita bado hatujapata solution kuhusiana na changamoto hii. Je, Serikali ina mikakati gani madhubuti, ningeomba tuelezwe kwa kutumia teknolojia ya kisasa kuweza kutatua changamoto hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ningependa kujua, kuna mazao mengina ya michungwa, ufuta na minazi ambayo yanalimwa sana katika Wilaya ya Kilwa, ningependa kutaka kujua, je, Serikali imeishirikisha vipi taasisi TARI katika kutatua matatizo ya magonjwa ya mazao haya?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mdudu huyu alitambulika muda mrefu na kama Serikali tumeendelea kuwekeza katika kufanya utafiti kushirikiana na wadau wengi wa kimataifa. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunamtokomeza mdudu huyu ambaye kila muda anaendelea kujipa maumbo tofauti tofauti lakini wataalam wetu wa TARI pamoja na wataalam wengine tunaendelea kuifanya kazi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni kuhakikisha tunamtokomeza mdudu huyu ambaye ana athari kubwa katika uzalishaji wa zao la pamba. Hivyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu hivi sasa Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi kwenye utafiti, tunaamini kupitia fedha hizi wenzetu wa TARI pamoja na mashirika mengine tutafanya kazi hii kwa uaminifu mkubwa kabisa ili mwisho wa siku tupate suluhisho la mdudu huyu na wakulima hao kama ambavyo dhamira yao ya kulima basi tuwe tumemtokomeza mdudu huyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, bajeti yetu ya eneo ya utafiti miaka miwili iliyopita ilikuwa ni shilingi bilioni 11.6. Hivi sasa bajeti yetu ni shilingi bilioni 43 kwenye utafiti. Moja ya maeneo makubwa ambayo tumeyapa kipaumbele ni kuhakikisha pia tunakuja na namna bora ya udhibiti wa magonjwa na wadudu wasumbufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mbunge kwamba, TARI imewezeshwa na hivi sasa inaendelea kufanya tafiti ili kuja na suluhisho la kudumu la magonjwa ambayo yamekuwa yakitatiza sana michungwa na minazi. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, barabara za Jimbo la Kilwa Kaskazini zilizo nyingi zina hali ya miinuko mikali pamoja na udongo korofi na zina hali mbaya sana. Je, Serikali ina mkakati gani wa barabara za aina hii ili kuboresha na kuhakikisha kwamba zinapitika muda wote wa mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya tathmini ya namna ya kufanya allocation ya fedha za barabara kwenye majimbo. Kwa sababu tunafahamu kwamba hali ya hewa inatofautiana, kuna majimbo yenye mvua nyingi kwa mwaka mzima. Kuna majimbo yenye milima na miteremko mikali, lakini kuna majimbo au wilaya ambazo zina udongo korofi kwa ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata ule mgao wa fedha za Bajeti ya TARURA zinakwenda kwa kuzingatia vigezo hivyo, ukiwepo ukubwa lakini na hali ya kijiografia ya maeneo hayo. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali inatambua kwamba Kilwa Kusini na Kilwa kwa ujumla ina changamoto hiyo na ndiyo maana inaendelea kuongeza bajeti na tutaendelea kufanya hivyo kuhakikisha kwamba barabara hizi zinapitika vizuri zaidi. Ahsante. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha afya katika Kata ya kimkakati ya Kandawale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati katika Kata zetu zote nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imefanya tathmini na kuainisha maeneo ambayo yana sifa ya kuwa na vituo vya afya vya kimkakati na tutakwenda kujenga vituo hivi vya afya kwa awamu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nakuhakikishia kwamba itakapofikika awamu hiyo tutawapatia fedha kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha afya, ahsante sana. (Makofi)

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itaanza kujenga minara 15 iliyopangwa kujengwa katika Wilaya ya Kilwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, tayari mradi wa Tanzania ya kidigitali minara 755 kwenda kwenye kata 713, Wilaya 112. Ninakuhakikishia kwamba iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Hivyo ninamuomba Mheshimiwa Mbunge tuwe na subira kwa sababu ujenzi wa minara ni hatua, hatua hizo zikishakamilika kusimamisha mnara wenyewe hauchukui hata miezi miwili. Kwa hiyo, ninamuomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kutoa ushirikiano katika maeneo ambapo wataalamu wetu watakapofika kwa ajili ya kupata maeneo na vibali basi awe sehemu ya ufanikishaji huo. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Katika Tarafa ya Kipatimu Kata ya Chumo tumekamilisha ujenzi wa kituo cha afya mwezi uliopita.

SPIKA: Unataka Serikali ifanye nini?

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali italeta vifaa tiba, dawa pamoja na watumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 7.1 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwenye vituo vya afya mbalimbali hapa nchini, na tutaangalia katika bajeti hii ambayo imetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba hivi; kama Tarafa ya Kipatimu kwenye kituo cha afya alichokitaja Mheshimiwa Ndulane imetengwa na tutapeleka vifaa tiba huko.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Je, ni lini Wananchi wa Kitongoji cha Cheketu, Kijiji cha Somanga Kusini, Wilayani Kilwa watalipwa fidia ya kupisha ujenzi wa miundombinu ya umeme katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la Mheshimiwa Ndulane linahusiana na ujenzi wa mradi wa kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi Megawatt 350 pale Somanga Fungu, na tayari tumepata mfadhili, mwenzetu wa JICA, tunaendelea na kukamilisha mazungumzo. Tutakapokuwa tayari kumaliza mazungumzo na kujenga mradi wananchi wa eneo hilo watapewa fidia yao. Tuombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kutusaidia eneo hilo liendelee kulindwa ili muda wa kulipa fidia utakapofika basi isiwe ni shida kulipa fidia.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Swali langu la kwanza la nyongeza, napenda kujua, ni lini Serikali itakarabati kipande cha barabara toka Somanga hadi Nangurukuru hadi Mbwemkuru ambacho kimechakaa sana?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; miaka ya hivi karibuni Serikali ilitanua barabara za mikoa na barabara kuu katika Mkoa wa Lindi, lakini haijaweza kulipa fidia hadi wakati huu. Ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi walio kando kando ya barabara hizo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii kuu ya Kusini Somanga - Nangurukuru hadi Mbwenkulu hadi Mnazi Mmoja imechoka. Hii barabara sasa hivi inapitisha mizigo mizito sana tofauti na ilivyokuwa awali. Kwa hatua za haraka ni kukarabati yale maeneo yote ambayo yamechakaa sana ili kuhakikisha kwamba hatukwamishi magari. Mpango mkubwa wa sasa hivi, Serikali inatafuta fedha ili kuifanyia ukarabati wa barabara yote kuendana sasa na uzito wa magari ambayo yanapita kwenye hiyo barabara ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kwamba tulibadilisha sheria kwa maana ya kuongeza upana wa barabara. Wizara ya Ujenzi inachofanya sasa hivi ni kufanya tathmini kwa barabara zote. Kwa kuanzia, pale ambapo tunaanza ujenzi, tunalipa, lakini tunataka tupate gharama nzima kwa barabara zote ambazo zimeongezeka kwa ajili ya kutafuta fedha kuwafidia wananchi ambao barabara imewafuata, na siyo kwa Lindi tu, ni kwa sehemu kubwa ya nchi, ahsante. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za CSR katika Vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba la Selous vya Zinga Kibaoni, Mtepela, Namatewa pamoja na Ngarambi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha katika Halmashauri hizo na maeneo aliyoyataja zitafika cha msingi Mheshimiwa Mbunge awe na subira, tutafute hizo fedha ili tuone namna ya kuja kusaidia wananchi katika maeneo hayo na wao waweze kunufaika na uhifadhi, nakushukuru.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Katika Wilaya yetu ya Kilwa zao hili la minazi limekuwa likiabiliwa na changamoto ya magonjwa mbalimbali na hivyo kupelekea uzalishaji kushuka na umaskini kuongezeka kwa wazalishaji wa zao hili la minazi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto ya magonjwa ya minazi katika Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kupitia Kituo cha Utafiti cha Kilimo Mikocheni hivi sasa tunaendelea kufanya utafiti wa kuja na miche bora ambayo itakuwa kinzani ya magonjwa na hasa ugonjwa wa manjano ambao unaathiri sana nazi na kufifisha uzalishaji na kwa hivi sasa tunaendelea na uzalishaji wa mbegu mbili kubwa ya East African Tall pamoja na dwarf ambazo zenyewe zina ukinzani mkubwa wa magonjwa naamini pia wakulima wa Kilwa watanufaika na mbegu hizi na wataongeza uzalishaji kwa sababu kazi ya utafiti imekwisha kufanyika.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, na ahsante sana Serikali kwa kunijibu swali langu vizuri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, napenda kuiuliza Serikali; kwa kuwa biashara ya wazalishaji wetu wa chumvi katika Mkoa wetu wa Lindi imekuwa ikiathiriwa na waagizaji wa chumvi kutoka nje ya nchi.

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia hawa wafanyabiashara wadogo wadogo waanze kufanya biashara ya chumvi kwa ufanisi?

(b) Je, Serikali sasa haioni wakati umefika wa kuweza kuwa na bei elekezi kwa zao hili la madini ya chumvi kwa Mkoa wetu wa Lindi ili kuhakikisha kwamba hawa wafanyabiashara wa chumvi katika Mkoa wetu wananufaika na biashara hii?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto katika sekta hii ya chumvi kwa maana ya baadhi ya viwanda kuagiza malighafi ya chumvi kutoka nje badala ya kuchukua chumvi inayozalishwa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, tulishatoa maelekezo na hili ni agizo la Serikali, kwamba wenye viwanda wote wanaozalisha chumvi hapa nchini watumie malighafi kwa maana ya chumvi inayozalishwa nchini, kwa hiyo tulishatoa marufuku kuagiza chumvi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu bei elekezi, tunashukuru kwa sababu tunadhani biashara zinatakiwa ziende kwa uhuru, kwa maana ya supply and demand, lakini pale inapotokea hoja mahsusi muhimu kama hii tutangalia ikiwa kuna ulazima wa kuweka bei elekezi kwa ajili ya kuona wananchi wa Tanzania, na hasa wanaozalisha chumvi ghafi, waweze kupata bei nzuri inayouzwa kwenye viwanda vya Tanzania, nakushukuru sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nitoe shukrani kwa Serikali ambapo jana tuliweza kusaini Mkataba wa kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Kilwa Masoko wenye thamani ya shilingi bilioni 81. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niulize swali la nyongeza sasa, kumekuwa na hali chechefu katika utekelezaji wa miradi ambayo inahudumiwa na Mfuko wa Maji ikiwemo mradi ambao unatekelezwa katika Kijiji cha Kinjumbi kutokana na mlolongo mrefu wa malipo.

Je, Serikali ina utaratibu gani ambao umeupanga ili kupunguza mlolongo mrefu wa malipo ili miradi hii inayotekelezwa kwa mfuko wa maji iweze kuhudumiwa kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ndulane, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nipende kupokea shukrani kwa uzinduzi wa miradi ya maji ya miji 28, kwenye hili tumpongeze sana Mheshimiwa Rais na tumshukuru na tumuombee kwa sababu kazi aliyoifanya ni kazi iliyotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na malipo ya Mfuko wa Maji kuwa na mlolongo mrefu, Mheshimiwa Mbunge unaelewa hapo nyuma kulikuwa na matumizi mabovu ya fedha katika hali ya udhibiti ilipaswa Wizara kuweka taratibu zote hizo, lakini tunaendelea kuziboresha kuhakikisha kwamba udhibiti utaendelea lakini pia fedha itatoka ndani ya wakati.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Katika Jimbo la Kilwa Kaskazini Serikali ikishirikiana na taasisi ya Pan African ilijenga kituo cha afya katika Kata ya Somanga, lakini kituo kile kimekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa vifaatiba.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka vifaatiba ili huduma bora ya afya iweze kutolewa katika Kata ya Somanga?
NAIBU WA ZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametenga shilingi bilioni 69.95 mwaka ujao wa fedha kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye vituo vya afya na hospitali za halmashauri. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini kwamba kituo hiki cha afya ni miongoni mwa vituo ambavyo vitapelekewa vifaa tiba pamoja na vituo vingine vilivyokamilika ili viweze kuanza kutoa huduma za afya. Ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Katika Jimbo la Kilwa Kaskazini lenye hospitali moja na vituo vya afya vitatu kumekuwa na changamoto kubwa ya uwepo wa gari la wagonjwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka magari ya wagonjwa ya kutosha ili kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya magari hayo 195 plus Halmashauri ya Kilwa ni miongoni mwa halmashauri ambazo zitapata magari hayo na tutafanya tathimini kuangalia umbali wa vituo hivi lakini na idadi ya wananchi wanao hudumiwa ili ikiwezekana tuongeze magari kwenye Wilaya hiyo ya Kilwa. Ahsante.

MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza siku ya leo.

Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba mwaka jana Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembelea katika Jimbo la Kilwa Kaskazini na alifika katika hospitali ya Kipatimu na akakuta kuna changamoto kubwa ya mtumishi wa X-ray baada ya kuwa X-ray ilinunuliwa miaka zaidi ya minne kabla ya mwaka jana ikiwa haitumiki kutokana na kukosa mtumishi wa X-ray.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba mtumishi huyu aliletwa akakaa miezi sita lakini juzi juzi hapa ameondolewa, nataka kujua je, Serikali ina mpango gani wa kumrejesha yule mtumishi ambaye ameondolewa juzi juzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tulipeleka mtumishi Hospitali ya Kipatimu lakini kwa sababu za kiutumishi amehamishwa, lakini kwenye ajira hizi ambazo watumishi watapelekwa mwezi Julai tayari ameshapangwa mtumishi wa X-ray kwenye Hospitali ya Kipatimu, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, katika Jimbo la Kilwa Kaskazini hakuna chuo chochote ambacho kimewahi kujengwa na Serikali. Je, ni lini Serikali itaweka mkakati wa kujenga Chuo cha VETA katika Jimbo la Kilwa Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza katika majibu yaliyopita ni Sera ya Serikali na ipo vilevile kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini ipo vilevile kwenye Dira ya Maendeleo ya Miaka Mitano na Dira ya Maendeleo ya Mwaka Mmoja kuhakikisha kwamba tunafikisha Chuo cha VETA katika kila Wilaya nchini ikiwemo na Wilaya ya hii ya Kilwa. Nimuondoe wasiwasi kaka yangu, ndugu yangu, katika eneo la Kilwa Kaskazini katika mwaka ujao wa fedha tunaamini chuo hiki katika eneo hili tunaweza kuanza ujenzi ili kuhakikisha vijana wetu katika eneo hili wanapata huduma hii ya elimu. Nakushukuru sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Napenda kuiuliza Serikali je, ni lini Serikali itaanza kujenga vituo vya afya katika kata za kimkakati za Kibata, Kandawale na Miguruwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha peke yake Serikali imeendelea kujenga vituo vya afya katika maeneo ya kimkakati na mpaka Juni hii tayari tumeshajenga vituo vya afya 234 nchini kote na mpango huu ni endelevu, tutahakikisha tunaendelea kujenga vituo vya afya ikiwemo katika Jimbo la Kilwa Kaskazini, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba ya Mganga katika Zahanati ya Kijiji cha Mchalambuko Wilayani Kilwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutafanya tathmini ya mahitaji ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya ukamilishaji wa nyumba ya mtumishi. Lakini tutatafuta fedha kwa kupitia mapato ya ndani, lakini pia na Serikali Kuu ili nyumba hiyo ikamilike na watumishi wetu waweze kuishi pale. Ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wananchi wa Kilwa wamekuwa ni wanufaika wakubwa wa umeme wa gesi unaozalishwa katika Kituo cha Somanga.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukiboresha kituo hiki ili kumaliza changamoto kubwa inayokabili wananchi wa Kilwa katika huduma ya umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndulane, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tayari tumeanza mkakati wa kurekebisha kufanya matengenezo kwenye visima vyetu ambavyo vinazalisha gesi na tumeshaanza Mnazi Bay, Songosongo pamoja na Madimba. Kwa Somanga pia tutahakikisha tunaweka kwenye mkakati ili tuweze kukiboresha na wananchi wa Kilwa waweze kupata umeme wa uhakika, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika eneo la Somanga, Serikali iliahidi kwamba italeta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo Polisi chenye hadhi ya Wilaya. Eneo limeshapatikana, fedha kiasi cha shilingi milioni tatu za Mfuko wa Jimbo zimeshakwenda; je, ni lini Serikali italeta fedha hizo ili kituo hicho kiendelee kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Ndulane kwa swali lake na kwa jitihada alizofanya hadi kuniita nikaenda kukagua eneo lile kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hiki cha Polisi. Ni bahati mbaya eneo lililokuwa limetengwa mwanzo lilikuwa dogo, sasa kama wanatuhakikishia kwamba eneo limepatikana, then tutawaelekeza Maafisa wa Jeshi la Polisi wanaohusika na ujenzi, wakakague kwa madhumuni ya kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo hicho, nashukuru. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba, je, ni lini Serikali itamaliza migogoro kati ya wanavijiji wa vijiji vya Nakingombe, Mtepela pamoja na Zinga Kibaoni dhidi ya Pori la Akiba la Selous katika Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Ndulane, Mbunge wa Kilwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli mgogoro huu tunautambua na niliwahi kufanya ziara katika maeneo hayo. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutafika kutatua mgogoro huu ikiwemo kutoa ufafanuzi kwa wananchi, ahsante.