Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Francis Kumba Ndulane (14 total)

MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Tingi – Kipatimu yenye urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha lami hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo inapita katika maeneo yenye kumbukumbu za Vita vya Majimaji na vivutio muhimu vya Utalii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa barabara ya Tingi – Kipatimu yenye urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha lami. Hata hivyo, mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuunganisha makao makuu ya mikoa kwa barabara za lami zilizoainishwa kwenye shoroba za maendeleo (development corridor). Serikali itakapokamilisha mpango huu barabara nyingine za mikoa zitafuata ikiwemo barabara ya Tingi – Kipatimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda maalum ili kuifanya barabara hii kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 496.569 zimetengwa kwa ajili ya kuifanyia matengenezo barabara hii. Aidha, Serikali imepanga kuimarisha baadhi ya sehemu korofi kwa kuziwekea lami. Ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kupeleka watumishi wa Idara ya Afya katika Jimbo la Kilwa Kaskazini ambalo lina uhaba mkubwa wa watumishi kiasi cha kufanya baadhi ya zahanati kutoa huduma duni na nyingine kuchelewa kufunguliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 60 zikiwemo hospitali mbili, vituo vya afya vitano na zahanati 53. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2017 hadi Desemba, 2020, Serikali imeajiri na kuwapanga watumishi 108 wa kada mbalimbali za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa. Aidha, mwezi Mei, 2021 Ofisi ya Rais-TAMISEMI imetangaza nafasi 2,726 za ajira za kada mbalimbali za afya. Watumishi hao watapangwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini kwa kutoa kipaumbele kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vyenye upungufu mkubwa wa watumishi ikiwemo baadhi ya vituo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya na kuwapangia katika vituo Wilayani Kilwa na kote nchini kwa ujumla, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafikisha huduma ya Maji kwa Wananchi wa Kata za Kipatimu, Kibata, Chumo, Kandawale, Namayuni, Miguruwe, Njinjo, Mitole na Kinjimbi katika Jimbo la Kilwa Kaskazini ili kuwaondolea adha ya maji inayowakabili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis K. Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 Serikali imeendelea kuboresha huduma ya maji kwa kutekeleza miradi Wilayani Kilwa ambayo imehusisha uchimbaji wa visima virefu nane, ukarabati wa tanki la maji la lita 45,000 katika Kijiji cha Kipatimu, ukarabati wa mradi wa maji Mtubei Mpopera katika Kata ya Kandawale na ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji. Kukamilika kwa kazi hizo kumeboresha upatikanaji wa huduma ya maji kufikia asilimia 68.5.

Mheshimiwa Naibu Spika katika Mwaka wa Fedha 2021/2022, Serikali itaendelea kuboresha huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza katika Wilaya ya Kilwa kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ikiwemo uchimbaji wa visima virefu sita katika Vijiji vya Mitole Kata ya Mitole, Zinga kibaoni Kata ya Miguruwe, Namayuni Kata ya Namayuni, Kisima-Mkika Kata ya Njinjo, Kibata Kata ya Kibata na Ruhatwe Kata ya Kikore. Pia, ujenzi wa miradi mitano ya mitandao ya mabomba ya matanki ya kuhifadhia maji katika Vijiji vya Kinjimbi Kata ya Kinjimbi, Chapita Kata ya Migumbi, Chumo Kata Chumo, Marendego Kata ya Somanga na Kipindimbi Kata ya Njinjo. Aidha, katika vijiji hivyo kutajengwa vituo 50 vya kuchotea maji.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Je, ni lini barabara ya Nangurukuru – Liwale yenye kilometa 258 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 25 inavyoelekeza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa, Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa zabuni wa kumpata Mhandisi Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, kwa ajili ya kuijenga Barabara ya Nangurukuru – Liwale yenye urefu wa kilometa 258 kwa kiwango cha lami umeshakamilika na mkataba wa kazi hii unatarajiwa kusainiwa mwishoni mwa mwezi Juni, 2021. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni
548.603 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Kazi ya usanifu itakapokamilika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga masoko ya kisasa ya kuuzia samaki hasa katika Kata ya Somanga na Kivinje ambazo upatikanaji wa samaki ni mkubwa ili kuboresha maisha ya wavuvi wa Wilaya ya Kilwa kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kasmazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa Kata ya Somanga na Kata ya Kivinje ni miongoni mwa maeneo yenye samaki wengi katika Wilaya ya Kilwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 kupitia mradi wa IFAD imetenga fedha kiasi cha shilingi 211,698,940 kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha barafu. Wilaya ya Kilwa ni moja ya maeneo ambayo mitambo ya kuzalisha barafu itajengwa ili kusaidia kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutekeleza mipango ya kuboresha miundombinu ya uvuvi, ikiwemo masoko ya kisasa ya uvuvi katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na Kata ya Somanga na Kivinje katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kadri fedha zinavyopatikana. Ahsante. (Makofi)
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Kitongoji cha Cheketu Somanga Kusini watalipwa fidia kupisha ujenzi wa miundombinu ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO inatarajia kujenga njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 190 ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Kinyerezi hadi Somanga.

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imelipa jumla ya Shilingi milioni 37.5 kwa wahanga 11 kati ya 13 wanaoathiriwa na mradi huu. Wahanga wawili waliobaki walitathminiwa kuwa maeneo ya Serikali ya Kijiji cha Cheketu, lakini kumekuwepo na mgogoro baina yake na wananchi. Serikali italipa malipo hayo baada ya utatuzi wa mgogoro huo.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -


Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Vituo vya Polisi katika Tarafa za Kipatimu, Njinjo na Nanjilinji Wilayani Kilwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga vituo vya Polisi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhudumia wananchi katika kudhibiti uhalifu. Katika Tarafa ya Nanjilinji kinajengwa kituo cha Polisi kitakachogharimu shilingi 67,700,000. Kituo hiki kiko kwenye hatua ya umaliziaji ambapo jumla ya shilingi 62,000,000 zimetumika. Wizara kupitia Jeshi la Polisi itatenga kiasi cha shilingi 5,700,000 ili kukamilisha ujenzi huo kama njia ya kuunga mkono juhudi za wananchi waliochangia ujenzi huo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inashauri wananchi wa Tarafa za Kipatimu na Njinjo kutenga maeneo ya kujenga vituo vya polisi na kuanza ujenzi na Serikali itaunga mkono kama ilivyofanya katika Tarafa ya Nanjilinji.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ili kuondoa migogoro ya Wakulima na Wafugaji katika Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa ina jumla ya vijiji 90 na kati ya vijiji hivi, vijiji 56 vina Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi mpaka kufikia mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa na kumaliza kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara, Serikali imejipanga kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji sita kwa kila mwaka. Aidha, kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 60 kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji vitatu vya Nandete, Kiranjeranje na Ruhatwe na kufanya urejeaji wa mipango ya matumizi ya ardhi iliyokwisha muda wake katika Vijiji vya Kandawale, Likawage na Nanjilinji B.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na changamoto hizo, halmashauri zote za wilaya nchini zimeelekezwa kutenga fedha kila mwaka katika bajeti zao kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo yote ya vijiji ikiwa ni pamoja na kuweka alama zinazoonekana kwa urahisi ili kuwezesha maeneo hayo kulindwa na kuzuia mwingiliano wa kimatumizi unaofanywa na wananchi. Hatua hii itawezesha kumaliza migogoro ya ardhi inayohusisha wakulima na wafugaji, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatangaza kumbukizi za Vita vya Majimaji vilivyoanzia Kijiji cha Nandete katika Gazeti la Serikali?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vita ya Maji Maji ilipiganwa kuanzia Mwaka 1905 hadi 1907, kusini mwa nchi yetu katika baadhi ya Mikoa ya Lindi, Iringa, Morogoro na Ruvuma, ikiwa
na lengo la kupinga utawala na ukandamizaji wa ukoloni wa Mjerumani. Mwaka 2006, Makumbusho ya Taifa ilianza kuadhimisha kumbukizi ya miaka 100 ya Vita ya Maji Maji na inaendelea kuadhimishwa tarehe 26 Februari kila mwaka, katika Manispaa ya Songea kwenye eneo la Makumbusho ya Vita vya Maji Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, huadhimisha siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa tarehe 25 Julai kila mwaka, ili kuwaenzi mashujaa wetu waliopoteza maisha katika vita na operesheni mbalimbali za ukombozi wa nchi yetu na Bara la Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya kutangaza eneo lolote au lengo la kihistoria iko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Mambo ya Kale, chini ya Kifungu cha Sheria ya Mambo ya Kale, Sura ya 333 ya Mwaka 2002, kifungu cha 3(1) na (2). Sheria hiyo inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Malikale kutangaza eneo lenye sifa ya Urithi wa Taifa kwenye Gazeti la Serikali. Endapo Mheshimiwa Mbunge ana nia ya Kijiji cha Nandete kutangazwa katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya Kumbikizi ya Vita vya Maji Maji, basi namshauri awasilishe ombi hilo Wizara husika ili liweze kufanyiwa kazi, ahsante sana.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Nangurukuru - Liwale?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea na kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Nangurukuru hadi Liwale yenye urefu wa kilometa 230. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ipo katika hatua za mwisho. Katika mwaka wa fedha wa 2023/24, Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu ya kwanza, kuanzia Liwale.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Je, lini Serikali itafufua kilimo cha pamba katika Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa maeneo yaliyo chini ya karantini ya pamba katika eneo la kusini mwa Tanzania kutokana na uwepo au kupakana na nchi zilizoathiriwa na funza mwekundu (diparopsis castenea) ambaye ni mdudu hatari wa zao la pamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2020/2021 Serikali ilifanya tathmini ya hali ya funza mwekundu na kubaini kuwa mdudu huyo bado yupo katika maeneo ya karantini. Aidha, Wizara itaendelea kufanya utafiti kwa kushirikiana na Taasisi za Kimataifa kuhusu namna bora ya kudhibiti mdudu huyo.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa njia nne kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Kilwa kipande cha Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kuanza ujenzi wa kipande cha barabara kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe, kilometa 3.8 katika mwaka wa fedha 2023/2024, ahsante.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuvutia Wawekezaji wa Viwanda vya kuchakata Madini ya chumvi Wilayani Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Serikali kuvutia wawekezaji katika sekta ya Chumvi unaendelea ikiwa ni pamoja na kutenga eneo lenye ukubwa wa hekta 168 katika Wilaya ya Kilwa kwa ajili ya wawekezaji wenye nia ya kuchakata madini ya chumvi.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali imeendelea kutoa vivutio mbalimbali vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa uratibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Taasisi husika ili kufanikisha azma ya kuwekeza katika sekta husika kwa maana ya sekta ya madini.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -

Mheshimiwa Spika, je, ni lini mradi mkubwa wa maji toka Mto Rufiji utaanza kutekelezwa ili kuwaondolea wananchi wa Kata 23 za Wilaya ya Kilwa tatizo la ukosefu wa maji safi na salama ambalo limekuwa likiwakabili kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji huduma ya maji katika Wilaya ya Kilwa ni wastani wa asilimia 64. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi tisa ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi wa Julai, 2022 na kuboresha huduma ya maji kufikia asilimia 86.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itaajiri Mtaalam Mshauri na kufanya usanifu wa mradi wa kimkakati na kwa kutumia chanzo cha maji cha Mto Rufiji ikiwa ni mpango wa muda mrefu wa kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Kilwa na maeneo mengine ya Mkoa wa Lindi.