Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Yahya Ally Mhata (8 total)

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali ila naomba yafanyike masahihisho. Ni Mji wa Mangaka, sio Banyaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yangu mawili ni kama ifuatavyo; la kwanza; kwa kuwa Mradi huu wa kuvuta maji kutoka Mto Ruvuma kwenda Mji wa Mangaka unaanzia Kata ya Masuguru, unapita Nanyumbu, Chipuputa, Kilimanihewa hadi Sengenya ambapo matenki yatajengwa. Swali, je, vijiji vitakavyopitiwa na bomba hili vitanufaika vipi na mradi huu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tunatambua kwamba mradi huu utachukua miaka miwili na wananchi wa Jimbo langu wana shida kubwa ya maji. Serikali ina mpango gani wa dharura wa kuwanusuru wananchi hawa wakati wanasubiri mradi kukamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza, kwa sababu Mradi wa Ruvuma utapita kwenye hizi Kata tano alizozitaja, vijiji vitanufaikaje. Kama tunavyofahamu Sera ya Maji hairuhusu Kijiji cha B kianze kupata maji A kikarukwa. Nipende kusema kwamba vijiji vyote ambavyo mradi huu utavipitia, basi watapata maji kwa sababu lile bomba kuu litaruhusu michepuo kwa vijiji vile vinavyopitiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ameongelea suala la muda mfupi. Mradi huu tunautarajia uchukue miezi 12 na tunatarajia uanze mwezi Mei mwaka huu. Mheshimiwa Mbunge hii kazi itafanyika kwa kasi kwa sababu tayari fedha zipo, hivyo itakuwa ni kazi ya muda mfupi na maji yataweza kuwafikia wananchi wetu kwa wakati. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kutenga fedha za kutosha kuweza kukarabati na kujenga wodi ya akina mama katika hospitali ya Wilaya ya Mangaka. Hospitali ile imekwisha, je, Serikali inatuhakikishia vipi upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali ile wakati kazi imeshakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga bajeti ya kununua vifaa tiba katika hospitali zote mpya za Halmashauri
67. Jumla ya shilingi bilioni 33.5 zimetengwa katika mwaka huu wa fedha na tayari taratibu za mawasiliano kati ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Wizara ya Afya na MSD kuona utaratibu wa kupata vifaa tiba katika hospitali zile mpya unafanyika mapema iwezekanavyo ili vifaa vile viweze kupelekwa katika hospitali zetu mpya za Halmashauri na kuanza kutoa huduma zinazotarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mhata na Waheshimiwa Wabunge kwamba hospitali zetu zote na vituo vya afya zilizojengwa, taratibu za kuhakikisha zinaanza kutoa huduma za afya zinaendelea na Serikali inaendelea kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha, kutenga fedha za kununua vifaa hivyo ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Nanyumbu.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na andiko la huu mradi pamoja na kujenga bwawa, ni kuhakikisha kunakuwa na mtandao wa maji kutoka kwenye bwawa kuelekea Vijiji vya Lipupu, Maratani, Mchangani A na Malema na baadhi ya Vijiji vya Kata ya Mnanje:-

Swali je, ni lini utekelezaji wa uwekaji wa miundombinu ya maji utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ahadi hii ya kujenga bwawa katika Kata ya Mikangaula ilitolewa tarehe 28/07/2011 na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Mrisho Jakaya Kikwete. Swali langu; ni miaka 11 ndiyo mradi huu unatakiwa kutekelezwa:-

Je, Wizara haioni wakati umefika ahadi ya viongozi wa juu hasa Marais wetu ikachukuliwa kama ni agizo na ikatekelezwa haraka iwezekanavyo, badala ya kusubiri miaka 11 ndiyo itekelezwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mtandao wa maji tunaelekea sasa kwenda kuutekeleza. Katika kutengeneza mabwawa, tunaanza kuhakikisha uhakika wa chanzo cha maji ambapo sasa bwawa limeshafika asilimia 95 na sasa hivi kazi zitakazofuata ni kuukamilisha. Hii 5% iliyobaki kufikia mwisho wa mwezi wa Tano au kabla ya kumaliza mwaka huu wa fedha ni kuona kwamba tunakwenda kusambaza mitandao ya mabomba kuelekea kwa watumiaji wetu wote wa Nanyumbu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, amesema mradi umeanza tarehe 28/07/2011. Kama wote tunavyokumbuka, miradi hii kwa kipindi hicho ilikuwa chini ya Halmashauri zetu za Wilaya. Kwa hiyo, wale wenzetu kidogo walishindwa kumaliza miradi hii na ndiyo maana RUWASA ikaanzishwa. Sote tunafahamu RUWASA sasa hivi ina mwaka mmoja na miradi korofi yote kama huu imekuwa ikifanikiwa kwa kuweza kukamilishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge napenda tu kukuhakikishia kwamba tunakwenda kutimiza ahadi hii kwa kutumia RUWASA na wote tunafahamu namna RUWASA ambavyo wamekuwa wakikamilisha miradi chechefu, kwa hiyo, na mabwawa haya pia yanakwenda kukamilika. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba tufanye masahisho katika majina ya vijiji. Kata ya Mkonona ni Nambunda siyo Nambundu na siyo Waniku.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya masahisho hayo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa dhumuni la uanzishaji Mfuko huu pamoja na madhumuni mengine ni kuziwezesha vile vijiji vya mpakani kuweza kupata mawasiliano ya simu hasa kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi yetu unakuwepo. Mfuko huu ulianzishwa mwaka 2007, vijiji vile bado vina matatizo makubwa ya mawasiliano. Hivi ninavyoongea hatuna mawasiliano ya simu ya Airtel wala mitandao mingine. Je, wakati mchakato huu wa kutangaza tenda unaandaliwa ni hatua gani za dharura zinachukuliwa hili kuhakikisha vijiji vile vinapata mawasiliano hasa kwa kipindi hiki kigumu ambacho usalama wetu na nchi ya Msumbiji ni mbaya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tatizo hili la mawasiliano linakwenda sambamba na usikuvu wa redio yetu ya TBC. Katika Wilaya yangu hatuna kabisa mawasiliano ya TBC. Je, ni hatua gani za dharura Mfuko huu unaweza kuisadia TBC ikasikika ndani ya Jimbo langu?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuonyesha ukaribu na Wizara yetu kwa kuhakikisha kwamba anatupatia taarifa sahihi ili na sisi tuweze kuzifanyia kazi kadri inavyowezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameongelea vijiji ambavyo viko mipakani, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tayari imeshafanya utafiti na tathmini ya vijiji vyote Tanzania nzima siyo Nanyumbu peke yake ambapo maeneo yote ya mipakani tunatarajia kuutangaza tenda kwa ajili ya ujenzi na kuhakikisha kwamba tunalinda mipaka yetu yote. Mipaka ya Mtwara, Namanga, Sirari pamoja na maeneo mengine Serikali tunafahamu kabisa kwamba mawasiliano ni jukumu letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilisema katika jibu la msingi maeneo haya ni yale ambayo mara nyingine hayana mvuto wa kibishara. Ndio maana kupitia Mfuko huu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema ulianzishwa mwaka 2007 kazi yake mahsusi ni kuhakikisha tunafikisha mawasiliano katika maeneo ambayo watoa huduma wengine hawawezi kufikisha mawasiliano, hilo ni jukumu la Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu ina vituo vya afya vinne ambavyo vyote havina gari la wagonjwa; je, ni lini Serikali itatuletea magari ya wagonjwa kwa vituo hivyo vya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kujibu katika jibu langu la msingi Serikali kwa kuwa imeendelea kujenga vituo vya afya kwa wingi na Hospitali za Halmashauri automatically tumekuwa na uhitaji mkubwa sana wa magari ya wagonjwa katika vituo vyetu vya afya, lakini pia katika Hospitali za Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, safari ni hatua tumeanza na hatua ya ujenzi wa vituo vya afya sasa tunakwenda na hatua ya kutafuta magari ya wagonjwa. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mhata kwamba tutakwenda kuangalia na kukipa kipaumbele Halmashauri ya Nanyumbu ili magari ya wagonjwa yakipatikana tuweze kupata gari hilo kwa ajili huduma bora za afya katika Halmashauri ya Nanyumbu. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, shamba hili la Nangaramo lilianzishwa mwaka 1986 wakati Wilaya ya Nanyumbu ikiwa chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Ukubwa wa shamba hili ni hekta 5,633; hivi ninavyozungumza kuna ng’ombe 300 tu; vijiji vinavyozunguka shamba hili vina uhaba mkubwa wa mahali pa kulima; vijiji vya Kata ya Kamundi, Mkolamwana, Kamundi na Chekereni vina shida kubwa ya mahali pa kulima hata Kata ya Nangomba, Vijiji vya Nangomba na Mji Mwema vina shida kubwa ya mahali pa kulima.

Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri; je, haoni wakati muafaka umefika maeneo haya ambayo hayatumiki kwa shughuli za mifugo wakaruhusiwa wananchi wanaozunguka vijiji hivi wakalima mazao ya muda mfupi, pale ambapo mtakapokuwa tayari basi mnaweza mkayachukua maeneo yenu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; mwaka 2018 kulikuwa na mgogoro mkubwa kati ya wanakijiji cha Mkolomwana na shamba hili, hali iliyopelekea kijana mmoja kupoteza maisha Bwana Ahmad Swalehe na vijana 36 kupelekwa mahakamani. Kwa kuwa kesi ile imekwisha na vijana wale wameachiwa huru kutokuwa na hatia katika mgogoro huu; nini hatma ya kijana huyu marehemu ambaye amepoteza maisha yake kwenye mgogoro huu, je, Serikali ipo tayari kumlipa fidia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahya Mhata kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, namuelewa Mheshimiwa Mhata na juu ya jambo la mahitaji ya wananchi wa kata na vijiji alivyovitaja vinavyozunguka shamba letu la Nangaramo. Naomba nichukue jambo hili kwa niaba ya Wizara, tutakutana na Mheshimiwa Mhata na tuweze kukubaliana kwenda katika eneo hili la Nangaramo na kuhakikisha tunakwenda kufanya tathmini ya kuona hiki anachokisema na kuzungumza na wananchi na pale itakapoonekana inafaa tunaweza tukaona namna ya kuweza kuwasaidia wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni hili linalohusu marehemu huyu; jambo hili ni kubwa, naomba nilichukue, atueleze vyema na sisi tutafanya mashauriano ya kuona namna iliyo bora ya kuweza kulimaliza suala hili, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALLY Y. MHATA: Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri kuhusiana na swali hili, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Kijiji cha Maneme ambapo ndipo yalipo majengo haya kilishaandika barua kukabidhi majengo haya kwa Serikali. Mimi kama mwakilishi wao niliwasilisha barua yao ya kukabidhi hili eneo kwa Wizara. Kwa hiyo, nataka kupata commitment ya Serikali. Ni lini watendaji hawa wa Serikali watakuja ndani ya wilaya yangu ili kuyahakiki majengo haya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa suala hili la ujenzi wa Vyuo vya VETA liko ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na sisi wananchi wa Jimbo la Nanyumbu tunayo majengo tayari, je, Serikali haioni haja kwa Mwaka ujao wa Fedha majengo haya yakatumika ili wananchi wa jimbo langu wakanufaika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mhata, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba tayari timu yangu ya wataalam kutoka Wizara itakwenda eneo hili. Mheshimiwa Mbunge anataka kujua lini, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwa vile tuko hapa Bungeni na Makao Makuu ya VETA yako hapa Dodoma, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge mara baada ya kipindi hiki tuweze kuonana, twende wote kwa Mkurugenzi wa VETA pale ofisini, twende tukaipange vizuri ili tujue wataalam wetu wale lini watakwenda kwenye eneo hili la kuweza kufanya tathmini ya pamoja na kujua kitu gani cha kufanya kule Nanyumbu.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili, kwamba majengo yapo, kuna baadhi ya miundombinu itahitaji kuongezwa; naomba hili tulichukue tuweze kuangalia katika bajeti ijayo iwapo kama itaturuhusu kuweza kuingiza bajeti ya kuongeza miundombinu katika eneo hili. Wakati tathmini hii ikishafanyika itatupa dira ya wapi tunakoelekea, mahitaji gani yatakayohitajika na ni commitment gani itahitajika ya kifedha kuweza kwenda kuongeza miundombinu kwenye eneo hili. Kwa hiyo hili tunaomba tulichukue tutaenda kulifanyia kazi na baada ya tathmini yetu hiyo tutakutana na Mheshimiwa Mbunge kumwonesha kitu gani tunachoweza kukifanya kwenye eneo hili. Ahsante sana.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, katika harakati za Serikali kuhifadhi mazingira na maliasili yetu ilihamasisha wananchi kufungua mabucha ya wanyamapori. Wananchi wa Jimbo langu walihamasika na walifungua mabucha tatizo ni upatikanaji wa leseni kutoka Wizara husika.

Je, ni lini wananchi wangu watapatiwa leseni ili shughuli hii ya kuuza nyamapori iweze kuanza ndani ya Wilaya yangu?
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imeendelea kutoa leseni za mabucha kwenye maeneo mbalimbali ya hapa nchini na hizi bucha ni kwa ajili ya wanyamapori. Mwaka wa fedha 2020/2021 tuliweza kutoa leseni zaidi ya 46 na tuna masharti ya namna ambavyo wanapaswa kuomba hawa wafanyabiashara wanaofanya biashara hizi za wanyamapori. Lakini kumekuwa na changamoto ya ukosefu wa wanyamapori wenyewe, kwa maana unapowinda kuna- target ambazo wanazifahamu wawindaji. Sasa kumekuwa na malalamiko kwa wale wenye leseni wanakosa nyama na matokeo yake wanarudisha wanashindwa kuendelea na biashara hii.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kama kuna yeyote ambaye anahitaji leseni, Wizara ya Maliasili na Utalii iko tayari wakati wowote kutoa leseni. Lakini changamoto inayojitokeza ni kwamba upatikanaji wa wale wanyama wenyewe ndiyo changamoto halisi inayojitokeza. Kwa sababu, uwindaji kuna maeneo ambayo tunayatenga lakini inapokosekana basi malalamiko yanarudi kwa Serikali, lakini leseni zipo tunawakaribisha wafanyabiashara wote waje. (Makofi)