Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Yahya Ally Mhata (16 total)

MHE. YAHYA A. MHATA Aliuliza:-

Je, ni lini utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Ruvuma kwenda Mji wa Manyaka utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ali Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepata mkopo kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim jumla ya Dola za Marekani Milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika miji 28 Tanzania Bara na Zanzibar. Moja ya mji unaonufaika na mkopo huu ni Mji wa Mangaka. Kwa sasa mradi upo katika hatua za manunuzi na wakandarasi wanatarajiwa kuwepo eneo la mradi kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi ifikapo Mei, 2021 na utekelezaji ni muda wa miezi 24.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ya ujenzi wa bwawa la maji katika Kata ya Mikangaula Wilayani Nanyumbu itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali iliahidi kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Nanyumbu kwa kujenga mabwawa katika Vijiji vya Mikangaula, Mchiga, Maratani, Chilunda na Nangova.

Katika kutekeleza ahadi hiyo, Serikali imeanza ujenzi wa bwawa katika Kijiji cha Maratani ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 95 na utakamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2021. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa tuta, spill-way, chemba za kutolea maji na kupokea maji, birika la kunyweshea mifugo na kituo kimoja cha kuchotea maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/ 2022, RUWASA Wilaya ya Nanyumbu imepanga kuanza kazi za ujenzi wa mabwawa ya Mikangaula na Chilunda.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, ni lini changamoto ya mawasiliano ya simu Wilayani Nanyumbu itamalizika katika Kata za Likokona, Mkonona, Nangomba, Nandete, Napacho, Lumesure, Michiga na Chipuputa?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ina jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote ya vijijini na mijini yasiyo na mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa kupitia tumeshafikisha miradi 1,057 ambapo miradi 686 imeshakamilika na miradi 371 inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo za Serikali bado kuna maeneo mengi yakiwemo maeneo ya Jimbo la Nanyumbu ambayo hayana huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, umevifanyia tathmini vijiji vya Kata ya Likokona, Mkonona, Nangomba, Nandete, Napacho, Lumesure, Michiga na Chipuputa katika Jimbo la Nanyumbu. Vijiji vya Kata hizi vimeingizwa katika Mradi wa Mpakani na Kanda Maalum awamu ya sita ambapo zabuni tarajiwa kutangazwa kabla ya kwisha kwa mwaka wa fedha 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Jimbo la Nanyumbu vilivyoingizwa katika zabuni hiyo inayotarajiwa kutangazwa ni kama ifuatavyo:-

1. Kata ya Likokona Vijiji vya Misawaji, Namaka, Msinyasi, na Likokona;

2. Kata ya Mkonona Vijiji vya Nambundu, Waniku and Namaromba;

3. Kata ya Nandete Vijiji vya Chivikikiti na Nakole;

4. Kata ya Lumesure Kijiji cha Lumesure;

5. Kata ya Michiga Kijiji cha Makong’ondera; na

6. Kata ya Chipuputa Vijiji vya Mpwachia, Nakatete na Ngalinje.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Vijiji vya Kata za Nangomba na Napacho vitaingizwa kwenye awamu nyingine ya miradi ya kufikishiwa huduma za mawasiliano kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, wananchi wa Jimbo la Nanyumbu watanufaika vipi na Shamba la Uzalishaji Mifugo Nangaramo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Shamba la Nangaramo ni miongoni mwa mashamba matano ya kuzalisha mitamba chotara wa maziwa na nyama kwa lengo la kusambaza kwa wafugaji.

Mheshimiwa Spika, faida zinazopatikana kwa wananchi wanaozunguka Shamba la Nangaramo ni pamoja na wananchi kupata elimu kupitia mikutano ya ujirani mwema kuhusu fursa za upatikanaji wa mitamba ya maziwa na nyama kwa lengo la kuwahamasisha kufuga ili kuboresha lishe ya familia, kutoa ajira na mbolea kwa uzalishaji wa mazao.

Mheshimiwa Spika, mbili, kutoa mafunzo ya ufugaji bora kwa shule za msingi na sekondari. Aidha, wanafunzi kutoka katika Shule ya Sekondari Mkangaula wamenufaika na mafunzo hayo walipokuwa kwenye mafunzo maalum; na tatu, uongozi wa shamba hushiriki shughuli mbalimbali za kijamii kama vile ujenzi wa shule na utoaji wa ajira za muda mfupi na mrefu kwa wananchi.
MHE. ALLY Y. MHATA aliuliza: -

Je Serikali ina mpango gani wa kuyatumia majengo yaliyoachwa na Kampuni ya Ujenzi ya China yaliyopo Kijiji cha Maneme yatumike kama Chuo cha Ufundi (VETA)?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahaya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika Wilaya zote hapa nchini. Kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 29 ambavyo vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majengo yaliyoachwa na mkandarasi aliyejenga barabara yapo na Wilaya imeona umuhimu wa kuyatumia, Wizara yangu itatuma wataalam kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) washirikiane na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu kufanya tathmini ya majengo hayo iwapo yanakidhi vigezo vya msingi vya kuanzisha mafunzo ya ufundi stadi.

Mheshimiwa Spika, wakati juhudi hizo zikiendelea, nashauri wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu kutumia Vyuo vya Ufundi Stadi vya Mtwara, Lindi na Namtumbo ambavyo vipo jirani na Wilaya hiyo.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -

Je, Serikali ina taarifa juu ya upatikanaji wa madini Nanyumbu na Je, wananchi wananufaikaje?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kwa Niaba ya Waziri wa Madini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), ilifanya utafiti wa awali katika Wilaya ya Nanyumbu iliyopo kwenye Quarter Degree Sheet (QDS) 316 na kubaini uwepo wa madini mbalimbali. Utafiti huo ulionesha kuwepo kwa madini ya dhahabu katika vijiji vya Lukwika, Chungu, Chipuputa na Masuguru. Katika kijiji cha Masuguru utafiti huo ulibaini pia uwepo wa madini ya sapphire, Acquamarine na rhodolite. Aidha, Wilaya ya Nanyumbu imebainika kuwa na madini mengine yakiwemo madini ujenzi.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini katika Wilaya ya Nanyumbu imetoa leseni za uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu 73, madini ya chuma nane, madini ujenzi mbili, madini ya vito 10 na leseni mbili za utafutaji wa madini ambapo moja ni kwa ajili ya utafutaji madini ya nikeli na nyingine ni kwa ajili ya madini ya dhahabu. Aidha, katika maeneo hayo shughuli za utafiti na uzalishaji zinaendelea. Kufuatia shughuli hizo wananchi wamekuwa wakijipatia kipato, ajira na mzunguko wa biashara kuwepo katika vijiji hivyo.

Mheshimwa Spika, ahsante sana.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Mji wa Mangaka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua hitaji la kujengwa Kituo cha Polisi kwenye mji wa Mangaka Wilaya ya Nanyumbu. Tathmini kwa ajili ya ujenzi imeshafanyika na kubaini kuwa kiasi cha shilingi 569,091,050 kinahitajika kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi Daraja B. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kwenye Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2023/2024; nashukuru.
MHE. MAIMUNA S. MTANDA K.n.y. MHE. ALLY Y. MHATA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka magari ya kubebea wagonjwa katika Vituo vitatu vya Afya Wilayani Nanyumbu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahaya Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Nanyumbu ina magari mawili ya kubebea wagonjwa ambayo yanatumika katika Hospitali na Vituo vya Afya. Hata hivyo, magari haya bado ni machache kwa kuzingatia uhitaji uliopo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 itanunua magari 195 ambapo kila Halmashauri itapata gari la kubebea wagonjwa ikiwemo Halmashauri ya Nanyumbu. Ununuzi huu utaboresha huduma za afya za dharura na rufaa. Ahsante.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -

Je, ni wananchi wangapi wa Jimbo la Nanyumbu wamefidiwa kutokana na uharibifu uliofanywa na tembo katika mashamba yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2022/2023, Wizara ilipokea jumla ya maombi nane kutoka kwa wananchi wa Vijiji vya Mchenjeuka, Lukula, Masuguru, Marumba na Mpombe walioathiriwa na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu katika Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu. Baada ya taratibu za malipo kukamilika, mnamo tarehe 21 Machi, 2023, Wizara ilifanya malipo ya kifuta jasho ya jumla ya shilingi 5,160,000 kwa wananchi saba wa Vijiji vya Michenjeuka, Lukula, Masuguru na Mpombe walioharibiwa mazao. Aidha, mwezi Machi mwaka huu, Wizara ilipokea maombi mapya 12 ya wananchi wa Vijiji vya Nanyumbu na Marumba ambayo yanaendelea kushughulikiwa kwa ajili ya kuandaa malipo.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -

Je, lini ujenzi wa barabara ya Mangaka hadi Morogoro kupitia Mbuga ya Selous utaanza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kuunganisha Mikoa ya Mtwara na Morogoro kwa barabara ya kutoka Masasi – Nachingwea – Liwale hadi Mahenge Mkoani Morogoro. Sehemu ya kutoka Masasi – Nachingwea – Liwale yenye urefu wa kilometa
175 itajengwa kwa utaratibu wa EPC + F. Kutoka Liwale – Mahenge kupitia Hifadhi ya Mbuga ya Selous Serikali imepanga kuanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika mwaka wa fedha 2023/2024. Ahsante.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Nangomba hadi Nanyumbu kwa kiwango cha lami?
WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahya Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imekamilisha kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Barabara ya Nangomba – Nanyumbu yenye urefu wa kilometa 28.32 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, lini Benki ya CRDB itafungua tawi katika Mji wa Mangaka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya CRDB imeanza ujenzi wa tawi katika Mji wa Mangaka. Tawi hilo linatarajiwa kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa mji huo kabla ya mwezi Septemba 2023, ahsante.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati katika Kituo cha Afya cha Nanyumbu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahya Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na uchambuzi na mapitio ya vituo chakavu vinavyohitaji ukarabati katika ngazi ya afya ya msingi ili bajeti ya Serikali ikiruhusu vituo hivyo chakavu viweze kufanyiwa ukarabati kikiwepo Kituo cha Afya cha Nanyumbu.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO K.n.y MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga Kituo cha Afya katika Kijiji cha Mikuwa Kata ya Mnanje Wilayani Nanyumbu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepeleka fedha Shilingi Milioni 250 kwenye Kata ya Mnanje kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya ambapo Kijiji cha Mikuwa ni miongoni mwa vijiji vilivyomo kwenye Kata hiyo. Majengo yanayojengwa kwenye Kituo hicho ni jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD), Jengo la maabara na kichomea taka. Majengo hayo yapo katika hatua ya umaliziaji ukiacha kichomea taka ambacho ujenzi wake ndiyo umeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais – TAMISEMI tayari imekwisha wasilisha maombi Wizara ya Fedha na Mipango ya Shilingi Milioni 250 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji na jengo la kufulia.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italeta Sheria ya kuruhusu halmashauri kutumia benki kama wakala wa ukopeshaji na ukusanyaji madeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Yahya Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua ufanisi wa kutumia benki kama wakala wa ukopeshaji na ukusanyaji wa mmadeni kwa kuzingatia kuwa benki zina miundombinu na utaalamu wa kutoa huduma hizo. Hata hivyo, ili kutumia benki katika kutekeleza jukumu la mikopo ya asilimia 10, maandalizi na utafiti unapaswa kufanyika ili kuendana na lengo kusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, iliunda Kamati ya Kitaifa ambayo ilichambua na kuandaa mapendekezo ya uendeshaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri. Aidha, timu imeshakamilisha kazi hiyo na kuwasilisha maoni na mapendekezo ambapo Serikali inaendeleia kuifanyia kazi na baada ya kukamilisha itatoa utaratibu, ahsante.
MHE. YAHYA A. MHATA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya zao la muhogo kuwa moja ya zao la kimkakati katika Mikoa ya Kusini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahya Ally Mhata, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuendeleza zao la muhogo nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na matumizi ya mbegu bora za muhogo zilizogunduliwa na TARI zenye uwezo wa kuzalisha tani 20 hadi 50 kwa ekari. Mbegu hizo zinapatikana kwenye Vituo vya Utafiti wa Kilimo (TARI) na kwa wazalishaji wa mbegu katika madaraja yote.

Mheshimiwa Spika, aidha, mbegu hizo zina sifa za mavuno yenye tija, wanga, kustahimili ukame, wadudu na ukinzani wa magonjwa. Kutokana na matumizi ya mbegu hizo, uzalishaji wa muhogo mkavu umeongezeka kutoka tani 2,486,000 Mwaka wa Fedha 2020/2021, hadi kufikia 2,575,453 Mwaka wa Fedha 2022/2023. Mkoa wa Mtwara upo katika nafasi ya tano ukitanguliwa na Tanga, Kigoma, Pwani na Kagera.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa Mkakati Mahsusi wa Kuendeleza Zao la Muhogo nchini ambao unalenga kuhamasisha uzalishaji wa zao hilo kwa tija, upatikanaji wa masoko ya uhakika ya bidhaa za muhogo, kuhamasisha wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za muhogo zenye thamani kubwa, kama vile viwanda vya kuzalisha wanga utokanao na zao la muhogo, bidhaa ambayo kwa sehemu kubwa huingizwa kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, aidha, kama sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo, Wizara imepanga kufanya Cassava Business Forum ili kujadili biashara ya muhogo nchini utakaofanyika tarehe 15 Aprili, 2024. Kongamano hilo litawezesha kutangaza fursa zilizopo katika Mikoa ya Kusini.