Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Yahya Ally Mhata (8 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Mpango huu, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Nanyumbu kwa kura nyingi walizonipatia katika Uchaguzi Mkuu uliopita. Nami nawaahidi wasiogope, niko hapa kwa ajili yao na nitawawakilisha kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijielekeze moja kwa moja katika kuchangia Mpango huu wa Mwaka Mmoja na wa Miaka Mitano uliowasilishwa jana. Kwanza naomba nijielekeze katika sekta ya afya, jinsi gani itakavyoweza kuongeza mapato yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa medical tourism. Tumeona jinsi gani sekta ya afya ilivyoweza kupiga hatua katika miaka mitano iliyopita. Tumeona zahanati karibu 1,198, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya 99, Hospitali za Rufaa 10 na Hospitali za Kanda tatu. Sasa hospitali hizi zinawezaje kuongeza uchumi wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukulia mfano wa India, wameweza kutumia sekta ya afya kuongeza mapato katika nchi yao. Tunajua wagonjwa wengi walikuwa wanakwenda India. Ni wakati wetu sasa hivi nasi kutumia hospitali zetu kuwavutia wagonjwa kuja katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna balozi zetu katika Afrika. Tutumie balozi zetu kutangaza huduma bora za hospitali zetu. Hawa wakija, watakuja na dola, wataacha katika nchi yetu. Wakija kutibiwa watafanya shopping, wata-stimulate uchumi wetu. Kwa hiyo, ni vizuri balozi zetu zitumike kikamilifu katika kuitangaza nchi yetu hasa huduma za afya ambazo tumeziboresha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba nishawishi, katika zile wilaya ambazo ni pembezoni, mfano Wilaya yangu ya Nanyumbu tumepakana na Msumbiji, nilitarajia kabisa Hospitali yetu ya Wilaya ikapatiwa vitendea kazi vizuri ili wagonjwa wale wa mpakani waje kutibiwa katika nchi yetu. Wakija watakuja na dola, wataziacha ndani ya nchi yetu na halikadhalika uchumi wetu unaweza kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni upande wa madini; tumeona jinsi gani Serikali yetu ilivyofanya katika kuhakikisha kwamba katika miaka mitano ijayo inafufua Shirika letu la STAMICO ili kuwawezesha wachimbaji wadogo waweze kujikwamua kiuchumi. Hili eneo la madini ni zuri sana endapo litatumika katika kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Nanyumbu tunayo madini, lakini nina masikitiko makubwa kwamba yameachwa bila kuendelezwa. Wizara ya Madini imefungua duka la ununuzi wa madini, lakini nikawa najiuliza, duka hili linamnufaisha nani? Kwa sababu madini yapo, lakini kuna mgongano mkubwa kati ya Wizara ya Madini na Maliasili. Vijana wanataka kwenda kuchimba madini, wakienda wanakutana na PFS, wanaambiwa hakuna kuingia msituni. Wakienda wanakutana na TAWA, hakuna kuingia. Sasa kuna contradiction hapo, madini yapo lakini hizi Wizara mbili zinagongana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hizi Wizara mbili zitusaidie vijana wetu ili waweze kufanya shughuli zao, wafuate taratibu gani mahali ambapo pana madini lakini yapo ndani ya msitu? Madini yale lazima yakachimbwe, kwa sababu madini hayapatikani kiholela, hayapatikani barabarani, yapo ndani ya msitu au mbuga. Kwa hiyo, naomba hizi Wizara mbili, nami nawashauri sana, madini haya yasipochimbwa, yatachimbwa kwa njia ya udanganyifu. Kule kwetu mpakani tusipoangalia, wale majirani zetu watakuja kuyachukua na hatutapata chochote. Naomba sana tutumie nafasi hii kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata ajira kwa hizi Wizara mbili kufanya kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kilimo. Kilimo chetu sisi watu wa Kusini hasa Wilaya yangu ya Nanyumbu tunalima sana korosho. Mwaka 2020 tumeathirika sana na uzalishaji wa zao la korosho, lakini Wizara haijaja na majawabu kwa nini zao la korosho halikuzalishwa? Nilitegemea Wizara ya Kilimo itueleze uzalishaji umepungua kwa sababu ya moja, mbili, tatu; vinginevyo tunawavunja nguvu sana wakulima wetu. Wamefuata taratibu zote lakini korosho hazikuzaa na Wizara imekaa kimya. Kwa hiyo, tunategemea Wizara itusaidie.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni ufuta. Tumeuza ufuta kwenye vyama vya msingi, hatujalipwa fedha zetu. Wakulima hawajalipwa. Wizara itusaidie, vyama vya ushirika vinatuangusha. Tunaomba wakulima wale walipwe fedha zao ili iwa-motivate mwakani walime tena.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza sana Waziri wa Fedha na Naibu wake kwa kazi nzuri waliyoifanya kuwasilisha mpango huu wa maendeleo wa miaka mitano, mpango wa tatu. Naomba nijielekeze katika njia gani ambazo nazipendekeza zinaweza zikaongeza mapato katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nchi ya India kabla ya mwaka 2005 ilikumbana na changamoto ya wananchi wake kuhitaji kuwa na uraia pacha. Tatizo hili lilikuwa kubwa, lakini Serikali ya India ilikaa chini na kufikiria jinsi gani inaweza ikatatua tatizo hili na wananchi wake wakaendelea na maisha yao hivyo, wakaanzisha, wakawapatia kitu kinachoitwa Over Seas Citizen of India Card. Kadi ile iliwawezesha raia wote ambao ni wahindi by original kuweza kuingia India kwa wakati wowote na muda wowote wanaotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivi waliweza kutatua matatizo matatu. Kwanza lile takwa la wananchi wa India kuwa na uraia pacha liliondoka kwasababu, lengo lao lilikuwa kuingia India na kushiriki katika shughuli za kiuchumi. Kwa hiyo, kwa kuwapatia hizi kadi za Over Seas Citizen of India raia wa India wanaoishi nchi mbalimbali waliweza kuja India bila matatizo yoyote na ku-maintain uraia wao. Kwa hiyo, Watanzania wengi wenye asili ya India ambao wako hapa Tanzania wanazo kadi hizi Over Seas Citizen of India. Hata raia wanaoishi Uingereza, Marekani, n.k.

Mheshimiwa Naibu Spika, na wahindi hawa wanapofika India wanapata privilege zifuatazo, kwanza wanaweza kushiriki katuika shughuli za uchumi ndani ya nchi ile. Kwa hiyo, wahindi wameweza kuwekeza, wameweza kupeleka uchumi, kupeleka mitaji India kwasababu sasahivi wamekuwa hawana tena pingamizi la kwenda India. Muda wowote na wakati wowote wanaweza kwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili. Raia wa India na huyo ambaye haishi India wana haki sawa. Haki ambazo zinamuwezesha raia wa India, mfano haki za kushiriki katika shughuli za maendeleo, raia wa India na huyo ambaye anakaa nje ya India anafanya wakati mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini waliweka utaratibu wa kuwazuia hawa wenye Over Seas Citizen of India wasifanye mambo yafuatayo; kwanza waliwaambia tunawapatia hizi kadi, hizi sio passport kwa hiyo, wewe sio raia wa India ila tunakutambua kama muhindi mwenzetu. Kwa hiyo, hutaweza kupiga kura katika nchi yetu, hutaweza kushiriki katika shughuli za kiserikali au hautakuwa kiongozi wa kuchaguliwa. Na hautakuwa ukafanya shughuli za kununua ardhi ndani ya India, lakini unaweza ukawekeza katika nchi yetu. Kwa hiyo, India waliweza kuvutia mitaji mingi sana ndani ya nchi yao ndani ya utaratibu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa naomba tujaribu kuiga utaratibu wa India. Tunao Watanzania wengi ambao wako nje ya nchi yetu wana uwezo na wana pesa za kuja kuwekeza ndani ya nchi yetu. Lakini hawataki kuukana uraia wa hizo nchi. Na sisi hatuna utaratibu wa raia pacha, tuwapatie kadi tuwaite Over Seas Citizen of Tanzania. Wakija hapa waje kwenye shughuli za kiuchumi tu, hata ruhusiwa kupiga kura, hata ruhusiwa kuchaguliwa, hata ruhusiwa kununua ardhi, lakini ataweza kuwekeza ndani ya nchi yetu. Nina imani kabisa tutakuwa na uwezo wa kuwavutia wahindi wengi, waingereza wengi, wajerumani wengi, ambao walikuwa raia wa nchi hii, wamarekani wengi wakaja na wakawekeza ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu umewezesha nchi ya India kuinua sana uchumi na vijana wengi wameajiriwa, lakini pamoja na hivyo India waliweza kuvutia teknolojia kwasababu, nchi mbalimbali zilikwenda na wakaweza kuleta teknolojia mbalimbali. Kwa hiyo, halikadhalika kwa nchi yetu nina uhakika kabisa tutakapotumia utaratibu huu tutapata knowledge za mataifa mengine ndani ya nchi yetu; madaktari watakuja kwetu, ma- engineer watakuja kwetu na wataalamu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa pili ambao naupendekeza, sisi nchi yetu ya Tanzania, natoka Wilaya ya Nanyumbu. Wilaya yangu inapakana na nchi ya Msumbiji. Mheshimiwa Mtenga alipokuwa anaelezea daraja la Mtamba Swala liko ndani ya wilaya yangu. Amezungumzia kutokuwa umuhimu wa lile daraja katika maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lile daraja lilijengwa purposely kwa ajili ya kuinua uchumi wa watu wa Kusini, tatizo ambalo lipo upende wa pili wa lile daraja miundombinu ni mibovu. Naomba sana Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje watumie nafasi hii waishauri Serikali ya Msumbiji waweze kuimarisha barabara kutoka Mtamba Swala kwenda mkoa unaofuata ambao hauko kilometa nyingi. Sasa hivi ninavyozungumza mbao zote zinazokuja Dar-es-Salaam, mbao ngumu, zinatoka Msumbiji zinapitia Daraja la Mtamba Swala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunanufaika sana kuwepo kwa lile daraja. Vijana wa Mtwara, vijana wa wilaya yangu wanafanya biashara na mkoa wa jirani wanapeleka mahindi, wanapeleka mchele, wanapeleka samaki, wanapeleka dagaa. Nina imani kabisa endapo miundombinu itaboreshwa upande wa pili wa lile daraja hali ya kiuchumi wa wananchi wetu itaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu naomba sana ndugu zangu viongozi wetu Mawaziri, hawa wawekezaji tulionao tuendelee kuwa-maintain. Kuna tabia ambayo sasa hivi imejengeka, hawa wawekezaji tulionao tunawakatisha tamaa. Tunao wawekezaji wanaofanya biashara ya kuingiza faida, lakini pia tunao wawekezaji wanaotoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu tuna Hospitali ya Ndanda tuna Hospitali ya Nanyangao na majirani zetu pale Tunduru wana Hospitali ya Mbesa. Kuna watu wa foreigners wanaoendesha zile hospitali wanapata tabu sana ku-renew vibali vyao. Unashangaa mtu anamkatalia daktari ku-renew mkataba wake; unajiuliza huyu anatafuta nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nawaomba; hawa watu wanao-renew mikataba ni watalam, na kitendo cha hawa kuwepo wanaongeza utaalam kwa local staffs wetu. Leo unamwambia muda wako umekwisha ondoka aje mwingine. Uapomfukuza yule mtaalam maana yake unaiua ile Hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi ningeomba, Mheshimiwa Waziri, mama yangu, shemeji yangu, Mama Jenista; hawa wataalam wetu wanatuangusha. Haiwezekani leo unamnyima daktari kuongeza mkataba. Daktari anakataa kuongezewa mkataba wanatutakia mema watu hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, unapomkatalia daktari hata wagonjwa hawaendi tena. Kuna watu wanakuja kwa sababu Doctor Yahya yupo pale. Leo unamwambia rudi kwenu halafu ile hospitali unamuachia nani? Ningeomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili, wataalam wetu wanakotupeleka siko, waangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini linguine, kuna baadhi ya missions, mashirika ya dini wanatoa huduma za uchimbaji wa visima. Kuna mashirika kule kwetu wanachimba visima kwenye shule bure. Yule m-mission mkataba umekwisha amekataliwa kuongezwa, anachimbia shule kumi, kumi na tano bure, unamkatalia unapata nini? Amekuja na pesa zake, amekuja na utaalam wake amekuja na vyombo vyake unamwambia muda wako umekwisha rudi kwenu, maana yake wewe hutaki wananchi wetu wapate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana wataam hawa waangaliwe; hasa hawa ambao wanatoa huduma. Mashirika yetu ya dini wana watu wa namna ile wanaanza kufukuzwa eti kwasababu muda umekwisha, jambo hili kwakweli halikubaliki katika uchumi wetu…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, muda umeisha, …

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake kwa bajeti ambayo waliwasilisha jana. Naomba nijiongoze katika maeneo yafuatayo;

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ahadi ambazo viongozi wetu wa juu wanazitoa ambazo kwa kweli zinahitaji kutekelezwa kwa sababu ahadi ya viongozi hao ni maagizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2011 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya nne alitoa ahadi pale Nanyumbu kujenga kituo cha afya katika Kata ya Mkangaula. Ahadi ile imekuja kutekelezwa mwaka jana. Katika utekelezaji wa ahadi ile zilitolewa milioni 200 lakini milioni 200 mpaka sasa hivi hazijatolewa. Kwa hiyo naomba Ofisi ya Waziri Mkuu, jambo hili liangaliwe katika utekelezaji wa ahadi za viongozi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahi kufika Mangaka tarehe 26/2/2018 na akatoa ahadi ya kujenga barabara zetu za lami kilometa tano; mpaka sasa hivi hakuna hata kilometa moja iliyotekelezwa. Kwa kweli naomba sana, ahadi hizi zinapotolewa wananchi wana imani na viongozi wetu, na zisipotekelezwa tunatoa mashaka kwa wananchi wetu kuwaamini viongozi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mama yetu Rais, Samia Suluhu Hassan alipokuja kwenye kampeni pale Nanyumbu alitoa ahadi ambayo ipo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kujenga barabara ya lami itakayounganisha Mkoa wa Mtwara na Morogoro kupitia Seluu; na barabara ile inaanzia ndani ya jimbo langu. Ni matarajio yangu kuwa utekelezaji wa ahadi ile utaanza katika mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba sana niungane na Waheshimiwa Wabunge ambao jana walizungumza, kwamba kuwe na kitengo maalum cha kuratibu ahadi za viongozi wetu. Mheshimiwa Rais wetu mpenzi ambaye ametangulia mbele ya haki kuna ahadi nyingi alizotoa, ni matarijio yangu zitatekelezwa ndani ya awamu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mfuko wa wanawake, vijana, na wenye ulemavu; mfuko huu unategemea mapato ya Halmashauri. Halmashauri nyingi mapato yao ni madogo sana. Wanaonufaika na mfuko huu ni zile Halmashauri ambazo zinauwezo wa kimapato. Lakini mimi concern yangu ipo katika asilimia mbili ya walemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mlemavu na ni Mbunge wa Jimbo, tunazo changamoto kubwa sana sisi walemavu halafu mnatupangia asilimia mbili, jamani hamtuonei huruma. Ninyi wazima mnaweka asilimia nne na sisi walemavu mnatupa asilimia mbili pamoja na changamoto zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba kuishauri Serikali, lazima mfuko huu wa wawalemavu uangaliwe na usitegemewe fedha za Halmashauri. Serikali Kuu itenge fedha kwa kila Halmashauri kuwasaidia hawa walemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, walemavu tuna changamoto kwenye elimu. Tunasoma katika mazingira magumu na baada ya kusoma tunategemea tupate ajira. Ukisoma sheria ya ajira kifungu cha 31 (2) ajira za walemavu imeeleza bayana kila mamlaka itakayoajiri watu kuanzia ishirini na kuendelea asilimia tatu wawe walemavu. Najiuliza sheria hii inatekelezwa? Ni kweli taasisi zetu, Wizara zetu zinaasilimia tatu ya walemavu? Na mimi namshukuru sana Mheshimiwa Rais, ndani ya Wizara hii Naibu Waziri ni mlemavu, naamini ataisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nyingine naomba nijielekeze kwenya afya. Kule Jimboni kwangu kuna mgogoro wa afya. Kuna fedha zilitakiwa ziletwe ndani ya Jimbo langu kujenga kituo cha afya Nanyumbu…

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mhata kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa

T A A R I F A

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimsahihishe tu Mheshimiwa anayeongea pale, asahihishe, watu wenye ulemavu sio walemavu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Khadija

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, Yes.

NAIBU SPIKA: Toa taarifa yako.

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yangu ni kwamba nataka nimsahihishe kwamba ni watu wenye ulemavu na sio walemavu. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Yahya Mhata unaipokea taarifa hiyo.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana mlemavu mwenzangu amenisahihisha, ni watu wenye ulemavu, na ulemavu ni wa aina zote; nashukuru sana kwa masahisho hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nieleze tatizo la Wizara ya Afya katika Jimbo langu. Tuna kituo cha afya ambacho kilitengewa fedha kwenye Hospitali, kwenye Kituo cha Afya Nanyumbu. Fedha zile hazikuja Nanyumbu, fedha zile kuna mahali zimepelekwa. Uthibitisho wa hili vifaa tiba vikaletwa Nanyumbu; sasa tukawa tunajiuliza vifaa hivi vinakuja kwa hospitali gani? tumeshindwa kuelewa. Kwenye hili naomba Ofisi ya Waziri Mkuu itusaidie. Fedha hizi wamezipeleka wapi kujenga kituo cha afya? kwa sababu tumeletewa machine kwa ajili ya kituo cha afya ambacho hakipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo nawaomba sana, wananchi wapale wanamasikito makubwa kwamba kuna fedha Serikali yao ilileta kwa ajili ya kituo cha afya lakini fedha zile hazikufika na badala yake waletewa mitambo (machine) kwa ajili ya kituo cha afya ambacho hakijajengwa. Kwa hiyo mimi nina imani kwamba hizi fedha kuna mahali zimekwenda kimakosa, naomba huko zilikokwenda zijereshwe ili wananchi wa Jimbo langu wanufaike na huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nijielekeze katika suala la ufundi ndani ya wilaya yetu tuna majengo yaliyoachwa na kampuni ya kichina ambayo walikuwa wanajenga barabara ya kwenda mpakani Mtambaswala. Majengo yale ni mengi na yapo pale ndani ya Kijiji cha Maneme ndani ya Tarafa ya Nanyumbu; majengo yale yangeweza kutumika kikamilifu kwa shughuli ya elimu ya ufundi. Naomba niishauri Serikali, majengo yale yapo pale idle na yanazidi kuharibika ni bora yakatumika kwaajili ya elimu ya ufundi. Uwekezaji wake hautakuwa mkubwa kuliko kuuanza upya. Kwa hiyo naomba sana wizara inayohusika tuyatumie majengo yale ili kufufua elimu ya ufundi ndani ya wilaya yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nazungumzia kwenye kilimo. Mheshimiwa Mwambe amezungumza kwamba kilimo chetu kimeathirika sana, uzalishaji wa kilimo wa zao la korosho umeathirika kutoka tani 324 hadi tani mia mbili na kitu, na sababu kubwa zinajulikana na mojawapo ni mbegu bora ambazo tulitegemea wakulima wazitumie hazikutumika. Kwa maana ya Sulphur I mean pembejeo za kilimo na mambo mengine. Wananchi wa jimbo langu walitumia fedha, walitumia nguvu zao kuzalisha mbegu za korosho ambazo miche ile waliwauzia Bodi ya korosho, lakini huu ni mwaka watatu mpaka sasa hivi hawajalipwa pesa zao...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko

MWENYEKITI: Uko tayari, haya karibu.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri na Naibu wake pamoja na watendaji wote walio chini ya Wizara yake kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimwa Mwenyekiti, tarehe 05 Mei, 2021, niliuliza swali la mawasiliano ndani ya Jimbo langu la Nanyumbu, Mheshimiwa Waziri alitoa majibu yenye uhakika kwamba tenda inatangazwa na maeneo yote yenye changamoto yatachukuliwa hatua zinazostahili. Ni matarajio yangu kabla hatujaondoka ndani ya Bunge hili nitapata taarifa sahihi tenda imetangazwa lini na nani anakuja katika jimbo langu kufanya kazi hii ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni changamoto ambayo tumeanza kuishuhudia ndani ya nchi yetu. Wiki mbili zilizopita TRA ilikumbana na changamoto ya mtandao wake wa malipo kutokufanya kazi, karibu siku tatu uchumi wa nchi hii uliyumba, watu hawakulipa na hakuna malipo ya aina yoyote yalifanyika TRA. Siku tatu zilizopita tumeshuhudia Kampuni yetu ya TANESCO imeshindwa kutoa huduma ya kununua LUKU. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni tahadhari, nawaomba sana Wizara, nawaomba sana wataalamu wetu wa TSA wawe waangalifu, dhahama inakuja. Kama hatutakuwa na backup system ya kukabiliana na utaratibu huu iko siku hapa tutakwama kabisa kufanya shughuli zetu. Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up atueleze ni mikakati gani inayofanywa na Wizara yake kukabiliana na hizi changamoto ambazo zimeanza kujitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni minara. Kuna wajanja ambao wapo ndani ya nchi hii wanapata taarifa kwamba kuna Kijiji A kutawekwa mnara, Kijiji B na Kijiji C. Wanakuja kule wananunua maeneo ya wananchi wetu kwa kujua kwamba kesho unakuja kuwekwa mnara, hawa ni matapeli. Namuomba Mheshimiwa Waziri niko tayari kumsaidia wale wote waliokuja ndani ya jimbo langu wakanunua maeneo ya wakulima kumbe lengo lao ni
kuwekwa minara, minara ile walipwe wahusika. Huu ni wizi mkubwa, haiwezekani mtu atoke huko atokako aje kununua eneo ndani ya kijiji chetu kumbe kesho unawekwa mnara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake Serikali ya Vijiji imekosa mapato, wananchi wamekosa mapato na yule mtu kanunua lile eneo na haonekani yuko wapi. Jambo hili kwa kweli linaumiza sana.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti,

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimpe Taarifa mzungumzaji, katika Wilaya yangu ya Liwale kuna Kijiji cha Kibutuka kuna tapeli mmoja ameenda kuchukua eneo la shule, mnara uko kwenye eneo la shule lakini unasoma mtu yuko Arusha.

MWENYEKITI: Taarifa hiyo Mheshimiwa.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa hiyo naipokea. Ndani ya Wilaya yangu kwenye Kata ya Sengenya, kwenye Kijiji cha Mkumbaru, kuna hao matapeli wamekuja na wamechukua hayo maeneo na wameweka minara. Kwenye Kata ya Mkonona, kwenye Vijiji vya Mangara Mbuyuni kuna watu wa aina hiyo. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ihakikishe kwamba jambo hili kwa kweli linakoma na hawa watu warudishe minara hiyo kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Shirika letu la TTCL. Ni jambo la kushangaza sana inakuwaje Serikali inadaiwa na Shirika hili? Ndani ya bajeti tunapitisha hapa bajeti za Wizara, inakuwaje leo wanashindwa kuwalipa? Hhili jambo halikubaliki. TTCL pia mimi naomba niwalaumu inakuwaje unambembeleza mteja? Kama hakulipi si umkatie? Mbona private sector wanafanya hivyo sisi tunashindwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kulialia hapa kumbe power tunazo, tukate. Vinginevyo kama utaratibu huu wa kubembelezana utaendelea mashirika yetu ya umma yatakufa. Tunapitisha bajeti tutalipa umeme, maji, simu, kwa nini wewe Mtendaji Mkuu wa Shirika hukulipa simu TTCL? Unapata huduma bure na unaendelea kuchekewa, hili jambo halikubaliki. Mimi naishauri Serikali, TTCL nendeni mkawakatie wale wote mnaowadai vinginevyo tutakuwa tunakwama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Shirika letu la Taifa (TBC) matangazo yake hayasikiki maeneo mengi ya nchi yetu. Jimbo letu la Nanyumbu TBC haisikiki kabisa. Mfuko huu wa Mawasiliano kwa nini hawawawezeshi TBC wakasikika nchini kwetu? Hili ni eneo ambalo wananchi wetu wanategemea kupata mawasiliano ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuko mpakani na Msumbiji, tunatarajia mawasiliano ya uhakika yapatikane kutoka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, muda wako umekwisha.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja lakini namuomba Mheshimiwa Waziri jioni hapa hapataeleweka kama hakutakuwa na majibu sahihi. Ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, nami naomba nichukue nafasi hii kwanza kuipongeza sana Wizara, kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara kwa kazi kubwa waliyoifanya katika uandaaji wa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nielezee kwa ufupi faida za korosho. Korosho tunapata tunda, katika lile tunda tunaweza tukatengeneza juice na wine. Lile bibo lilikauka unaweza ukatengeneza spirit, viwandani, hospitalini na kwenye maabara tuna shida kubwa ya spirit. Wenzetu wa Naliendele wamekwenda mbali kutengeneza spirit kwa kutumia bibo. Sasa hivi wamefikia asilimia 82 ya spirit kwa tunda lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama hiyo haitoshi, korosho yenyewe unaweza ukala, wengi wenu mnajua kazi yake lakini unaweza ukatengeneza siagi. Wenzetu wa Naliendele wana siagi ya korosho na imekuwa approved na TBS. Pia ile korosho ukisaga, unaweza ukatengeneza chapati. Aidha, korosho ni tui, unaweza ukapika mboga kwa tui la korosho na ukikutana na mwanamke wa Kimakonde hutamuacha. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nutshell ya ile korosho ni mafuta yanayotumika katika dawa. Unaweza ukapaka kwenye mbao kama alivyosema mwenzangu na ile haitaliwa na mdudu yeyote. Lile bibo ukishakamua ni mashudu na ni mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niiulize Wizara, mambo haya walikuwa wanayajua? Viwanda vingeitumia korosho hii leo tungekuwa wapi? Nina uhakika tungetengeneza wine…

T A A R I F A

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mhata.

SPIKA: Ndiyo Mheshimiwa Cecil.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa kwamba pamoja na hayo anayoyasema, Serikali hii ilikamilisha utafiti wa haya yote anayoyasema ambao unapatikana pale Naliendele kinachosubiriwa ni kufanya implementation. Kwa hiyo, sasa awaulize utekelezaji wa haya yote ili kuongezea wakulima mapato kutokana na zao la korosho utaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampa taarifa hiyo.

SPIKA: Taarifa hiyo unaipokea Mheshimiwa Yahya?

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, huko ndiyo nilikokuwa nakwenda, namshukuru sana mwenzangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba wenzetu wa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ule Mfuko wa export levy ndiyo ulitakiwa ufanye kazi hizi. Tuna kazi kubwa ya kufufua viwanda vyetu vya wine, kutengeneza viwanda vya mbolea na juice. Kama tungeutumia Mfuko ule vizuri kwa kuwatumia wataalam wetu wa Naliendele, miaka hii mitatu tuliousimamisha tungekuwa tuko mbali sana. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara tutumie Mfuko ule wa export levy ili kuwezesha wenzetu wa Naliendele wafanya utafiti wao wa dhati kutafuta mazao mbadala ya korosho hatimaye viwanda vingi viweze kutekelezwa ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu la pili, kule Jimboni kwetu kumeingia mtafaruku. Kuna barua iliyoandikwa na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho inayowataka wakulima wote kukatwa Sh.110 kutoka katika mauzo yao ya korosho baada ya kupewa sulphur. Barua ile inachanganya sana. Inasema hata mkulima akipewa mfuko mmoja akienda kuuza tani 20 atakatwa Sh.110 kwa kila kilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mtendaji huyu amekwenda mbali kwa kujiamini kabisa kwa kuwaandikia Wakurugenzi kwamba hayo ni maagizo na lazima yatekelezwe. Hili jambo halikubaliki. Kama mwananchi anakopeshwa mfuko mmoja, kwa nini usimkate kwa mfuko mmoja? Unamkataje kwa idadi ya korosho alizoleta kwa ajili ya kuuza go-down? Hii kitu hakikubaliki.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Mheshimiwa Waziri, ile barua ifutwe. Mtendaji yule anasema baraka hizi amezipata kwa Wabunge, Wabunge wapi? Ni nani aliyempa idhini ya kuandika barua hiyo? Kwa kweli anatuchanganya na anawachanganya wananchi. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri, Mtendaji huyu usipomuangalia ipo siku tutamtoa ofisini kwake kwa nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la minada, Mheshimiwa Waziri amezungumza vizuri sana asubuhi kwamba takriban minada 70 imefanyika ndani ya nchi hii kwa msimu uliopita na minada ile ni mizuri kabisa na mimi naiunga mkono. Hata hivyo, kuna upungufu kwenye minada ile.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Tandahimba imetokana na Wilaya ya Newala lakini utashangaa bei za minada zinatofautiana. Unaambiwa korosho za Tandahimba ni bora kuliko korosho za Newala ambapo jana walikuwa Wilaya moja. Leo kwa kugawanywa tu, bei zinatofautiana. Wilaya ya Nanyumbu, wilaya yangu mimi imetokana na Wilaya ya Masasi. Mwanzo, bei ilikuwa moja kwa kugawanywa tu, bei zinatofautiana, hii ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri uwaangalie watendaji wake kuna hujuma inayofanyika. Haiwezekani korosho za Nanyumbu zikawa na bei ndogo kuliko korosho za Masasi. Wakati tulikuwa wilaya moja bei ilikuwa sawa, leo tunagawanywa, unasema kwamba bei tofauti. Hili jambo halikubaliki. Kwa hiyo, kuna hujuma inayofanyika na haitakubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Wizara, pamoja na mazuri yote wanayoyafanya, naomba muwaangalie watendaji wenu wa chini. Wenzangu wamezungumza kuhusu Bodi ya Korosho, mtendaji amepewa mamlaka makubwa sana kwa sababu hana mtu anayemdhibiti. Naomba huyu mtu aangaliwe kwa macho mawili. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Yahya.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, mwisho naishukuru sana Wizara naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, na mimi naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Balozi Mulamula kwa kuwasilisha vizuri sana na kwa umahiri mkubwa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Lakini pia naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru watumishi wote wa Wizara hii kwa ushirikiano walioutoa katika uandaaji wa bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa maono mazuri aliyonayo juu ya Wizara hii. Kwa mara ya kwanza Wizara hii inaongozwa na wabobezi wa diplomasia, hakuna atakayebisha Waziri wetu ni mbobezi hakuna atakayebisha, Naibu Waziri ni mbobezi hata Katibu Mkuu wa Wizara hii ni mbobezi katika masuala ya diplomasia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi sina mashaka na watu hawa na namshukuru sana, sana, sana Mheshimiwa Rais kwa kuliona hilo. Wakati Rais wetu analihutubia Bunge baadhi ya maneno ambayo aliyazungumza katika Wizara hii ni kama ifuatavyo na naomba ninukuu alisema; “tunafanya uchambuzi utakaobaini nafasi ya kila ofisi ya Ubalozi katika kukuza biashara, uwekezaji na utalii, uchambuzi huo ndio utakaotumika kupanga Maafisa kulingana na uwezo wa kila Balozi.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nakuja kwenye mchango, tunazo changamoto nyingi sana katika balozi zetu,

Mheshimiwa Rais ameeleza hapa. Bahati nzuri mimi nimewahi kufanya kazi katika balozi zetu, nilikuwa Ubalozi wa Tanzania New Delhi, India ni jambo la kushangaza Ubalozi ule una watumishi watatu ambao wanawakilisha ukiondoa India kuna nchi zingine za uwakilishi. Hapa unajiuliza diplomasia ya kiuchumi utaitekeleza vipi kwa idadi hii ya watumishi. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri maelezo yale ya Mheshimiwa Rais ayafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie umuhimu wa India kimkakati katika kukuza biashara, kimkakati katika masuala mazima ya utalii. India ndio makao makuu au ndio soko letu kuu la korosho zote zinazotoka Tanzania. Kuna Jimbo linaitwa Kerera, korosho zote za dunia hii zinakwenda pale, kwa hiyo, lazima tuwe na watumishi wa kuhakikisha wanalikamata soko lile. India ndio makao makuu ya textile industry ukienda Jimbo la Gujarat, ndio pamba yote inayozalishwa duniani inakwenda kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, India ndio makao makuu ya matibabu, ukiwa na tatizo la kiafya usipopona India wewe ujue huponi tena. Kwa hiyo, kuna kila sababu kuhakikisha tunapeleka watumishi wa kutosha wa kuweza kuhakikisha kwamba tunaweza kupata wawekezaji wa kutosha ambao watakuja kuisaidia nchi yetu. Lakini hali ilivyo sasa inatia huzuni sana haiwezekani nchi kama India sub-continent unakuwa na watumishi watatu, ambao unatakiwa utoe huduma Srilanka, utoe huduma Bangladesh na utoe huduma na Napal jambo hili haliwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuna kila sababu ya kujipanga kimkakati katika kuhakikisha kwamba tunawapanga watumishi wetu kwa lengo zima la kukuza biashara zetu, kukuza utalii wetu na kukuza uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna suala la rasilimali watu, nimelizungumza upungufu wa watumishi na jambo hili kwa kila mahali ukienda China, kuna watumishi watatu Balozi na watumishi wawili, mwambata wa jeshi na mwambata wa fedha hauwezi ukafanya kazi kwa kuleta tija katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala la maslahi ya watumishi; unaweza ukawaona watumishi wa Ubalozini wanapata maslahi makubwa kweli jambo hili si sahihi. Bara la Asia watumishi hawa wamegawanywa kimatabaka, mtumishi aliopo New Delhi, India analipwa tofauti na mtumishi aliyopo China. Mtumishi aliyopo China analipwa tofauti na mtumishi aliyopo Malaysia, kwa nini watumishi hawa tunawapa allowance tofauti? Ningeshauri Mheshimiwa Waziri ili kulinda maslahi ya watumishi tuhakikishe watumishi wetu tunawapa maslahi yaliyosahihi na yanayolingana. Haiwezekani Balozi wa India analipwa tofauti na Balozi wa China, analipwa tofauti na Balozi wa Malaysia wakati hawa wote ni Mabalozi, hawa wote ni watumishi walioko katika nchi zetu kwa hiyo, naomba maslahi ya watumishi yaangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kingine watumishi waliopo Ubalozini hawalipwi stahili zao, takribani miaka kumi hakuna mtumishi wa Ubalozini anayelipwa fedha ya likizo, watumishi hawa inabidi wajitegemee wao wenyewe jambo hili kwa kweli linakwamisha sana ustawi wa kazi zao.

Mheshimiwa Spika, lakini imeelezwa hapa changamoto ya makazi ya watumishi, naomba niishauri Wizara naomba tutumie mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii tuliyonayo ikajenge nyumba katika Balozi zetu, kwa kufanya hivi tutakuwa tumefanya mambo mawili, kwanza tutaisaidia Serikali kutoa fedha kwa kujenga nyumba lakini pili, tutarejesha fedha zetu hapa hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama utawaambia National Housing waende Nairobi wakajenge nyumba, nyumba ambazo watumishi wa Ubalozi watakaa, maana yake Wizara ya Fedha itailipa National Housing. Kama utawaambia National Housing wakajenge nyumba India maana yake watumishi wa Ubalozini watakaa katika nyumba za National Housing na Wizara ya Fedha itailipa National Housing, kwa hiyo, tutaacha fedha zetu ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwa kufanya hivi tutajenga nyumba nyingi sana, lakini kama tutaendelea na utaratibu wa kumbana ndugu yangu Mwigulu atoe fedha Hazina, tutakesha hatutamaliza tatizo la nyumba.

Mheshimiwa Spika, kuna mjumbe hapa amezungumzia masuala ya raia pacha, niliwahi kuzungumza ndani ya Bunge hili kwamba tatizo hili liliwakuta wenzetu wa India, lakini walilimaliza kwa utaratibu mzuri sana. Badala ya kutoa uraia pacha, wao waliwatambua raia wao waliopo nje ya nchi kwa kuwapa kadi, wanaitwa Non-residence of India (NRI) na sisi tuwatambue Watanzania waliopo nje ya nchi tuwaachie na uraia wao lakini tuwape kadi Non-residence of Tanzania. (Makofi)

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo…

SPIKA: Nimekuona Mheshimiwa Mbunge wa Longido.

T A A R I F A

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nimpe mzungumzaji taarifa kwamba katika Taifa la Marekani pia wanawapa wageni green card kuwatambua kwamba wanaweza kuishi na kufanya kazi huko.

SPIKA: Unapokea jambo hilo?

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru naipokea taarifa hiyo. Kwa hiyo, ninachojaribu kueleza hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana bahati mbaya na muda wako umeishia hapo hapo.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi hii nami kuweza kuchangia bajeti hii ya Serikali.

Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mama Samia Suluhu kwa maono mazuri aliyonayo juu ya nchi yetu, pili nimshukuru sana Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu wake na wafanyakazi wote wa Wizara ambao kwa namna moja au nyingine wameshiriki kikamilifu katika uandaaji wa bajeti hii. Tatu, naomba niwashukuru sana Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Bajeti, Ndugu yangu Mheshimiwa Daniel Silo, Makamu wake CPA Omar Kigua kwa mchango mzuri walioutoa kwenye Kamati na kuishauri Serikali hatimaye leo hii tunaijadili bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika maeneo yafuatayo, kwanza naipongeza sana Serikali kwa maono yake iliyonayo juu ya kuhakikisha Madiwani wetu wanapata posho moja kwa moja kutoka Serikali Kuu. Tatizo hili lilikuwa tatizo kubwa sana, Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alifanya kama leo Mama yetu anavyofanya, aliamua kuhakikisha Madiwani wote wanalipwa kiinua mgongo kutoka Serikali Kuu, hii ilikuwasuluhisho la matatizo kwenye Halmashauri zetu. Leo hii tunapoamua kuwalipa madiwani posho zao kupitia mfuko mkuu tunahakikisha Halmashauri zote tunazitendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana posho inayopatikana sasa hivi ni ndogo. Mheshimiwa Waziri kwa kuanzia ajaribu kuona alternative way ambayo tunaweza tukainua kidogo posho za Waheshimiwa hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu Mheshimiwa Diwani anahudumia vijiji 12, anatembea ana vijiji 12. Nina Kata mimi inaitwa Kata ya Sengenya Mheshimiwa Diwani ana vijiji 12, posho hii yote anayopata inatumika katika kuhudumia vijiji hivi. Kwa hiyo, badala ya kutumia kidogo kujikimu anajikuta anaitumia kwa ajili ya shughuli za wananchi. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri hili aliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kuamua kuwalipa Maafisa Watendaji wa Kata posho zao, posho za mafuta. Pamoja na kwamba, Maafisa Watendaji hawa hawana vitendea kazi, lakini ninaamini wataitumia posho hii kwa ajili ya kukodi bodaboda, ili kuweza kufanya shughuli za halmashauri. Sisi ni mashahidi, sisi ni Madiwani, tunafahamu Maafisa Watendaji Kata wetu ndiyo wakusanya ushuru wa Halmashauri, ndiyo walinzi wa amani katika Halmashauri zetu kwa hiyo, kwa kweli, hizi 100,000/= watakazopewa zitawasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu hii isiwe hisani, Wakurugenzi wa Halmashauri wasije wakawakopa hawa Watendaji, walipwe kila mwezi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwigulu, Mheshimiwa Waziri, lazima utoe paper itakayowa- instruct hawa Wakurugenzi, hakuna kuwaruka, vinginevyo hawa watakopwa. Sheria ya posho huwezi uka-carry forward, kama hautamlipa ndani ya mwaka wa fedha hautasema hili ni deni. Kwa hiyo, Wakurugenzi wengi wanaweza wakatumia kigezo hiki kutokuwalipa posho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu uamuzi wa kuwalipa Makatibu Tarafa ni wazo la busara sana. Hawa ndiyo viungo muhimu, wanafanya kazi kubwa katika Tarafa zetu kwa kweli, mmewapa vitendeakazi kwa maana ya pikipiki, posho hizi zitawasaidia kwenye mafuta, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuangalia suala la TARURA. TARURA tulizungumza hapa ndani ya Bunge kwamba, wanapata fedha ndogo, tumewaongezea fedha, jambo hili ni heri kabisa. Rai yangu Mheshimiwa Waziri, kuna Sheria ya TARURA ya mwaka 2007, Sheria ya Barabara, inakataza malori yenye zaidi ya tani 10 kwenda vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kijijini kwetu ndiko ambako kuna mazao, wafanyabiashara, hasa kipindi hiki cha mazao mfano kwangu mimi, huu ni msimu wa ufuta halafu utakuja msimu wa korosho, hakuna lori la tani 10 ambalo litatakiwa lipite. Kwa hiyo, nawaomba sana Mheshimiwa kwa kuwa tunaongezewa fedha naomba Mheshimiwa Waziri ije sheria tuibadilishe, hakuna lori la tani 10 kijijini kwetu malori yote ni kuanzia tani 15, tani 30.

Sasa leo unaposema tani 10 yasionekane vijijini maana yake yakae barabara kuu halafu gharama ya kuanza kutoa mazao kutoka vijijini kuleta barabara kuu, tunaongeza gharama ya uendeshaji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana hili mliangalie. Hii kero kubwa sana huko vijijini wananchi wetu wanalia, wafanyabiashara wanalia kwa sababu ya sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Property Tax. Imezungumzwa vizuri, Mheshimiwa Mwigulu nakuunga mkono kwa uamuzi wa kubadilisha njia ya ukusanyaji. Ni kweli 2017/ 2018 Property Tax ilikuwa inakusanywa na Halmashauri kabla ya 2017/2018 ikawa matatizo makubwa. Badaye Serikali Kuu kupitia TRA na sasahivi mmebadilisha utaratibu huu wa ukusanyaji, mimi nauunga mkono. Rai yangu kwao, kupitia LUKU katika wilaya zetu nataka kujua mgawanyo wa mapato utakuwaje? Najua watu watalipa Property Tax kutoka sehemu mbalimbali za nchi hii.

Je, ile Property Tax itakayokusanywa ndani ya wilaya yangu, itabaki ndani ya wilaya yangu au ndio ile asilimia 15 uliyoizungumza kwa utaratibu upi? Lazima tujue mgawanyo halisi wa Property Tax kwenye halmashauri zetu ili halmashauri zetu ziweze kufanya kazi inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Chumi amezungumza, kuna ahadi za viongozi. Viongozi wetu wanatoa ahadi nzuri sana, Mheshimiwa Mwigulu tunakuomba sana hizi ahadi za viongozi muwe mnaratibu na mnaziingiza kwenye bajeti. Isiwe jukumu la sisi Wabunge kuanza kufanya lobbing, kuanza kuwabembeleza kuna ahadi, kuna ahadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Mheshimiwa Rais alipokuja kwangu wakati wa kampeni aliahidi kujenga barabara ya lami kutoka jimboni kwangu kwenda Mkoa wa Morogoro kupitia Selous, ipo ndani ya ilani, lakini kwenye bajeti haipo. Lini itaingizwa ndani ya bajeti? Nilitarajia leo kingekuja kitabu hapa kikaeleza hizi ni ilani za viongozi wetu. Ilani hii itatekelezwa mwaka huu, ilani hii itatekelezwa mwaka huu, badala ya sisi kuanza kuja kuanza kubembeleza kuna ahadi! Waziri Mkuu 2018 aliahidi barabara kilometa tano ndani ya Jimbo langu, haipo popote tangu 2018 mpaka leo. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Mwigulu, tunaomba hizi ahadi za viongozi wetu mziratibu na mziingize ndani ya utaratibu wa bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti ya Serikali Mheshimiwa Mwigulu aliongelea mambo ya msingi mengi, mambo ya kupunguza tozo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wetu. Mimi naunga mkono mia kwa mia.

Rai yangu Mheshimiwa Waziri yale yote ambayo mmeyaeleza yatekelezwe ndani ya mwaka ujao wa fedha ili tutakapokutana tuweze kuisifia bajeti na utekelezaji wake, vinginevyo tutakuwa tunadanganyana. Naomba sana itekelezwe kama tutakavyokubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nichukue nafasi hii kuchangia huu Muswada wa ukusanyaji wa fedha au Finance Bill ambao uliwasilishwa na Mheshimiwa Waziri. Muswada huu ni mzuri na una lengo la kuisaidia Serikali kuweza kukusanya fedha ili yale ambayo tulikubaliana yaweze kutendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali, nampongeza sana Waziri mwenye dhamana na Wizara hii kwa kazi nzuri aliyoifanya kwenye bajeti ya mwaka huu na huu Muswada aliotuletea. Nina uhakika leo hii narudi ndani ya Jimbo langu nikiwa na uhakika wa vyanzo zaidi ya vitano vyenye fedha, zaidi ya shilingi bilioni tatu katika Jimbo langu. Nina uhakika wa kupata shilingi milioni 500, jambo ambalo halijawahi kutokea katika nchi hii. Narudi mwezi huu jimboni kwangu nikiwa nina uhakika wa bilioni 1; narudi nikiwa na uhakika wa shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa shule; na ninarudi ndani ya jimbo langu nikiwa na uhakika wa maboma 10 kwenda kuyatengeneza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, nina uhakika wa mradi wangu wa maji wa kutoka Mto Ruvuma kuja Mangaka utatekelezwa. Kwa kweli nampongeza sana sana sana Mheshimiwa Waziri kwa ubunifu mkubwa aliokuja nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, sasa tunarudi majimboni sisi Waheshimiwa Wabunge, mtuletee fedha hizi haraka. Huu Muswada tuupitishe ndugu zangu ili mwezi huu Julai na Agosti ambapo tutabaki majimboni, tuweze kusimamia fedha hizi zikafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana kulikuwa na issue ya transfer price; labda naomba nichukue nafasi hii kuwaeleze ndugu zangu transfer price ni nini na jinsi gani inatumika kwenye kuiibia Serikali. Transfer price ili iweze kufanyika lazima kuwe na Kampuni mama ambayo kwa lugha ya kigeni parent company na kuwe na subsidiary company. Sasa hii kampuni mama ipo nje ya nchi; hii kampuni nyingine subsidiary inakuja kwenye nchi yetu. Ndio inapokuja kufanyika transfer price na wenzetu Wahasibu walishaligundua hili, ipo standard kabisa International Financial Reporting Standard (FRX kama sikosei 12), inayozungumzia transfer price.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ili wizi huu ufanyike hawa wanatumia njia mbili, ile kampuni mama ambayo iko kule labda nchi yoyote tuseme nchi “A”, inakuja kufungua mradi hapa labda wa uchimbaji wa madini, wizi wake unafanyika katika maeneo mawili. Moja, wana-over invoice, ku-over invoice services huku, ile kampuni mama imekuja kufungua machimbo ya madini kwetu, wale wanapotaka kutoa service katika ile kampuni yao ya huku, wanaichaji bili kubwa, wakiichaji bili kubwa wanapunguza kiwango cha kodi ambacho hii kampuni ambayo imefunguliwa hapa iweze kuilipa Serikali. Hiyo ni sehemu ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili kunakuwa na factitious payment, malipo hewa hewa, wanajifanya hii kampuni ya hapa inailipa ile kampuni mama kule, tumelipa hiki Board of Director, sijui tumelipa nini, anatumwa mtu kuja kutembelea hii kampuni analipwa ili kusafirisha fedha kule. Kwa hiyo ipo financial reporting standard, ambayo inasaidia kugundua mambo haya, wenzetu ma-auditors wakishaligundua hili.

Kwa hiyo inatakiwa kampuni hii inapofunga vitabu vyake i-disclose kama sisi ni subsidiaries company, kampuni mama ipo nchi Fulani. Asipofanya hivyo Auditor anakuwa na two option, moja anarudisha malipo yote yaliyofanyika kwenye ile kampuni mama kwamba sio halali, kwa hiyo yanatozwa kodi. Hata hivyo, kama amefanya inamlazimu sasa Auditor aangalie kwamba malipo haya yana uhaliali kiasigani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naishauri Serikali na naiunga mkono sana kama Mheshimiwa Mwigulu alivyosema, lazima tu-press signal, kwamba signal hii kwamba tunajua huu mchezo. Pili, wataalam wetu watambue kwamba sisi tunafahamu. Kwa hiyo mimi naomba ndugu zangu hii transfer price tuiachie Serikali na ile proposal yao, ili hawa wafadhili waweze kuja, pia tutakuwa na uwezo wa kuwabana. Watakaokuja kufungua makampuni hapa tutakuwa na uwezo wa kuwabana kama tunafahamu na hata wataalam wetu watambue kwamba tunajua kuna mchezo wa transfer price. Hilo la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, Mheshimiwa Waziri alizungumzia masuala ya property tax na jinsi gani inatakavyokusanywa. Naunga mkono kwamba ile asilimia 15 yote ipelekwe TAMISEMI na ikishapelekwa TAMISEMI ndipo pale watakapoanza kuzigawanya kwenye halmashauri zetu. Mpango huu ni mzuri sana kwa sababu kuna baadhi ya miji ina property nyingi na kuna baadhi ya miji haina property za kuchaji hii property tax. Kwa hiyo, wazo la kukusanya na kupeleka TAMISEMI, halafu TAMISEMI wakatugawia kulingana na mazingira yetu, naliunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize mifumo. Hivi karibuni tumegundua matatizo makubwa sana ya mifumo yetu, mifumo mingi imeingiliwa. Sasa kwa kuwa tunaingia katika utaratibu huu kuanzia mwezi ujao, naiomba Wizara iangalie mifumo hii iwe inasomeka. Leo TAMISEMI wana mifumo yao ya ukusanyaji wa mapato, Hazina wana mifumo yao ya ukusanyaji wa mapato na Bandarini wana mifumo yao ya ukusanyaji wa mapato. Sasa naiomba Wizara iisimamie mifumo hii iwe ni ya aina moja na isomeke, vinginevyo kutakuwa na athari ya kuleta hujuma katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja mia kwa mia ili mapato haya yatumike, yaweze kutuletea maendeleo katika Wilaya zetu. Ahsante sana. (Makofi)