Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jafari Chege Wambura (44 total)

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa ziara yake aliyoifanya ndani ya Jimbo langu la Rorya ikiwa ni pamoja na maelekezo ya Mradi wa Kirogo kwamba mkandarasi aliyetekeleza ule mradi kwa kiwango cha chini achukuliwe hatua. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa maamuzi makubwa na mazuri aliyoyafanya kipindi alipofanya ziara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu wa maji unaotoka Ziwa Victoria kwenda Tarime unaanzia ndani ya Jimbo langu la Rorya, zaidi ya Kata 11 na vijiji zaidi ya 28 vinategemea kufaidika na mradi huu. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuanza kutekeleza mradi huu hata kama ni kwa awamu ili kutatua changamoto za mradi huo wa maji ambao kimsingi utashughulika na Jimbo la Rorya, Tarime Vijijini na Tarime Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali tumeweka mikakati kuhakikisha tunaondoa changamoto ya maji kwenye maeneo yote yenye shida hiyo. Kwa Jimbo la Rorya, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge, tayari Wizara iko kwenye michanganuo ya kuleta fedha katika maeneo hayo. Vilevile nimwambie tu kwamba baada ya Bunge hili, fedha awamu hii inayofuata, Jimbo lake pia limezingatiwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na pia kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nataka niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa daraja hili linaunganisha tarafa zaidi ya tatu kwa maana Tarafa ya Suba, Nyancha pamoja na Luo- imbo na ni muhimu sana kwenye uchumi wa muunganiko wa watu wanaoishi ndani ya tarafa hizi.

Je, Mheshimiwa Waziri haoni kuna umuhimu wa kuharakisha daraja hili kwa kuwa si tu linaharakisha uchumi, lakini pia ni sehemu ambayo wananchi wengi wamekuwa wakipoteza maisha wanapovuka kutoka upande mmoja kwenda upande wa pili?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, Mheshimiwa Waziri haoni sasa baada ya Bunge hili, kuna umuhimu sasa wa kuongozana mimi na yeye ili kwenda pamoja kule ndani ya jimbo kuona namna gani tunaweza tukatatua pamoja changamoto hii ili angalau wananchi hawa waweze kupata huduma hii kwa uharaka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba daraja hilo ni muhimu sana kwa kuwa linaunganisha vijiji vingi na tarafa tatu katika Halmashauri ya Rorya na kiungo muhimu sana katika shughuli za kiuchumi na shughuli za kijamii katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoongea katika majibu yangu ya msingi kwamba Serikali inatambua sana umuhimu wa daraja hilo na ndiyo maana katika mwaka wa fedha ujao 2021/2022 Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kufanya tathmini na usanifu ili kutambua shughuli ambayo inahitaji kutekelezwa na gharama za daraja hilo ili kadri ya upatikanaji wa fedha daraja hilo liwezwe kujengwa na kutatua changamoto hizo kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kuambatana na Mheshimiwa Mbunge naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tuko tayari wakati wowote kufika kushirikiana naye Mheshimiwa Mbunge. Baada ya kikao hiki tutapanga tuone ratiba bora zaidi ya kwenda kupita eneo hilo na kuona namna gani tunakwenda kuwahudumia wananchi.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa swali la msingi la Halmashauri ya Rungwe linafanana sana na tatizo la Halmashauri ya Rorya ambayo kwa 2015/ 2020, Serikali ilitupa zaidi ya bilioni 7.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji zaidi ya miradi 12, lakini mpaka sasa ninavyozungumza hakuna mradi ambao umetekelezwa kwa kiwango cha 100% na wakandarasi wameshalipwa fedha na hawapo site.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alifanya ziara mwezi wa kumi na mbili na akatoa maelekezo kwamba wakandarasi hao wakamatwe lakini mpaka leo ninavyozungumza hakuna mkandarasi aliyekamatwa badala yake kuna fedha inatoka kuja kukamilisha miradi ambayo kuna wakandarasi wamekula fedha.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni, je, lini Serikali sasa itaona umuhimu wa kuleta wakaguzi kwenye Halmashauri ile ili kujiridhisha ile fedha bilioni 7.9 kwa miaka ile mitano imetumika vipi na yule ambaye kweli ametumia hizo fedha pasipo kutimiza wajibu wake achukuliwe hatua zinazo stahiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Chege kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilitoa fedha nyingi sana kwa Halmashauri ya Rorya, na swali lake anahitaji kujua lini wakaguzi watapelekwa kuona namna gani wale ambao walikula fedha wanashuhulikiwa. Sisi kama Wizara tayari tumeunda timu yetu ambayo itazunguka majimbo yote kuona kwamba miradi ambayo fedha ilitoka na wakandarasi wakafanya janja janja basi wanakwenda kushughulikiwa na kama kuna mtumishi yeyote wa Serikali aliweza kujihusisha pamoja na hawa wakandarasi na yeye sheria itafuata mkondo wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nipende kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba hivi karibuni watafika Rorya na wote ambao wanastahili kutumikia sheria basi sheria itafuata mkondo wake.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nashukuru.

Niseme tu kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri nirudie kumuomba kama kuna uwezekano angalau wa kufika Rorya kuitambua na kuielewa jiografia ya Rorya ilivyokaa. Nimekuwa nikimuomba hii ni mara ya pili tena narudia kumuomba. Imani yangu akifika atagundua hiki Kituo cha Afya ambacho tumekuwa tukikizungumzia kinahudumia kata zaidi ya tano ikiwemo Kata ya Kyang’ombe, Baraki, Komuge, Kisumwa na Rabol. Inahudumia vijiji zaidi ya 27; population wide ambayo inakwenda kupata huduma pale sio chini ya watu 50,000 kulingana na jiografia ilivyokaa. Umbali wa kutoka kituo hiki cha afya mpaka Hospitali hii ya Wilaya inayojengwa ni zaidi ya kilometa 40 ndiyo maana mara ya kwanza nilikuwa namuomba sana tupate daraja la Mto Moli ili kufupisha safari hii.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu la kwanza la nyongeza; Mheshimiwa Waziri haoni sasa kuna umuhimu wa kupandisha hadhi hizi zahanati ambazo ziko kwenye kata zinazozunguka kata hii ya Kinesi ikiwemo Kata ya Kyang’ombe, Banaki, Komuge na Kisumwa ili zile zahanati ziweze kutoa huduma kama vituo vya afya kukisaidia hiki kituo cha afya cha Kinesi population wide inayokwenda pale?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la nyongeza Mheshimiwa Waziri huoni kuna umuhimu sasa kwa muktadha wa majibu haya hiki Kituo cha Kinesi angalau wpaate ambulance ili iweze kuwasaidia kwa umbali huo wa kilometa 40 wanaosafiri hasa tunapopata wagonjwa wa dharura kama akinamama wajawazito na wagonjwa wengine ambao wako serious kwenye matatizo kama haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Wambura Chege kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatetea wananchi wa Jimbo la Rorya na kuhakikisha wanapata huduma bora za afya ili tuhakikishe kwamba wananchi wale wanaona matunda mazuri ya Serikali yao.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kituo hiki cha afya kinahudumia wananchi wengi katika vijiji takribani 27 na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeeleza namna ambavyo Serikali imeendelea kutoa fedha zaidi ya shilingi milioni 900 katika kituo hicho; kwanza, kuhakikisha majengo yanakamilika lakini pia kuendelea kukipanua kituo kile ili kiendelee kutoa huduma bora kwa hao wananchi wengi ambao kituo kinawahudumia. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba tutaendelea kukiboresha kituo kile cha afya, lakini pia zahanati zinazozunguka kituo cha afya, sera na mpango wa maendeleo ya afya msingi tunahitaji kituo cha afya katika kila kata na kila zahanati katika kila Kijiji. Kwa hiyo, kama kuna zahanati ambazo ziko nje ya kata ilipo Kituo cha Afya cha Kinesi tunaweza kupanddisha hadhi zahanati hizo zikawa Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la ambulance, ni kweli tunahitaji kuwa na magari ya wagonjwa kwa ajili ya dharura na tutakwenda kuweka mpango wa kuhakikisha kituo hiki cha Kinesi kinapata gari la wagonjwa ili kiweze kurahisisha huduma za rufaa.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na nishukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba nipate nafasi sasa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza ambayo kimsingi yanatokana na jibu la swali la msingi.

Swali langu la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba mwaka 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 500 kilichangwa kwa ajili ya kununua vifaa tiba, lakini sasa tumebakiza mwezi mmoja unaokuja wa sita.

Je, ni lini Serikali sasa hii milioni 500 iliyokuwa imetengwa itaweza kufika kwenye hospitali hii ili kuweza kununua vifaa tiba hivi ili kuongeza wigo wa utoaji huduma katika hospitali ile?

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, kwa kuwa Serikali imekiri mwezi Disemba mwaka huu hospitali ile itafunguliwa kwa ajili ya kutoa huduma lakini pia inakiri kwamba hatuna jengo la upasuaji na wala halijaanza kujengwa; je, jengo hili ni lini litaanza kujengwa ili itakapofika mwezi Desemba hospitali ile iweze kutoa huduma inavyotakiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-

Kimsingi tumetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya hospitali zote 67 za Halmashauri za awamu ya kwanza ikiwepo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na fedha hizo tayari zimeshapelekwa Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kwa ajili ya kununua vifaa tiba ambavyo Halmashauri ya Rorya wameainisha kwamba ni mahitaji yao ya kipaumbele.

Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha hizo tayari zimekwishatolewa kwa ajili ya Hospitali ya Rorya ana tayari zimekwishawasilishwa MSD, taratibu za manunuzi ya vifaa tiba zinakamilishwa na vifaa tiba vitaletwa katika Halmashauri ya Rorya.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na jengo la upasuaji; hospitali ile tayari ina majengo saba, tunaendelea na ujenzi wa majengo tisa na kati ya majengo saba ambayo tayari yamekamilika kwa asilimia 98, jengo la akina mama wajawazito linaungana na jengo la upasuaji. Kwa hiyo, tayari tuna jengo la upasuaji la kuanzia katika Hospitali ya Wilaya ya Rorya. Mpango ni kuendelea kujenga majengo mengine ya upasuaji katika mwaka wa fedha ujao, lakini hili halitaathiri kuanza kutoa huduma za upasuaji ifikapo Disemba mwaka huu 2021, ahsante sana.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri majibu ambayo yana matumaini. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nje ya shughuli za kiuchumi na kibiashara ambazo wananchi wa Jimbo la Rorya watafaidika kutokana na urekebishwaji wa bandari hii, lakini pia ni pamoja na shughuli za kiusalama, hasa ukizingatia bandari hii iko mpakani kati ya nchi mbili.

Nilitaka nijue tu, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini sasa bandari hii itaweza kutengewa fedha ili ianze kurekebishwa kama vile ambavyo swali la msingi limekuwa hasa ukizingatia bado hatujafanya hata ule upembuzi yakinifu kujua gharama za ujenzi wa bandari hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jafari Chege Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jibu langu la msingi nilisema kuwa Bandari ya Sota ni kati ya bandari ambazo bado hazijawa rasmi lakini zimetambuliwa na Serikali ili ziweze kurasimishwa. Kwa hiyo isingekuwa rahisi kutenga fedha kupeleka kwenye bandari ambayo bado haijarasimishwa; na ndiyo maana tumesema kwaajili urasimishaji tathmini inafanyika ili hadi mwezi Agosti mwaka huu bandari hizo baada ya kuainishwa na kuona zina sifa zitarasimishwa na baada ya hapo fedha itatengwa kwa ajili ya kuzijenga ili ziweze kuwa rasmi ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini nishukuru pia na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba niulize maswali mawili ya nyogeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ucheleweshaji wa umuhimu wa eneo la mpaka wa Kirongwe si tu ina umuhimu kwa Wilaya na Halmashauri ya Rorya lakini pia ina umuhimu pia kwa Serikali kwa ujumla wake kwa sababu ya sensitivity ya eneo lenyewe lilivyo kati ya mpaka wa Tanzania na Kenya. Lakini mpaka sasa hakuna kifaa chochote vile vifaa tofauti naweza nikasema na counter book na kalamu kwa upande wa Tanzania na Kamba peke yake. Je Serikali haioni kuna umuhimu sasa kipindi ambacho tunakwenda kwenye bajeti ya utekelezaji wa mwaka huu kuweka vifaa vya kisasa ili kuimarisha mpaka ule lakini kudhibiti mapato yanayopotea kwenye eneo lile?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa ucheleweshaji wa eneo hili linaathiri pia mapato ya halmashauri ndani ya Jimbo letu la Rorya. Je Serikali haioni kuna umuhimu, pamoja na maboresho yanayokwenda ya nyumba za watumishi, kuweka soko kubwa la kimataifa ambalo litakuwa ni sehemu ya fursa kati ya wananchi wa Wilaya yangu ya Rorya pamoja na wananchi wa upande wa pili wa Kenya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Chege Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hoja zake zote mbili ni za msingi sana. Hoja ya kuhakikisha kwamba tunatafuta vifaa vya kutosha ili kuwezesha huduma katika mpaka wa Kirongwe pamoja na ujenzi wa soko ni hija za msingi. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge atupe muda Serikali wakati tunakamilisha, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, hatua za ujenzi wa nyumba kwa bajeti ya mwaka huu basi na hili la vifaa tulichukue na hili la soko lenyewe Serikali imelipokea itaangalia pale hali itakaporuhusu ili liweze kufanyiwa kazi.
MHE. JAFARY W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa shughuli hii ya ufugaji wa samaki inafanyika pia katika Jimbo la Rorya, kwa maana ya wilaya nzima, hasa ukizingatia kwamba umbali wa kutoka ziwa kuelekea kwenye maeneo ya wananchi haizidi hata mita tano. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia vijana wa maeneo yale ambao wanaishi karibu na ziwa ili kufanya na kuanzisha ufugaji huu wa samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza, kwamba ufugaji wa samaki, hasa kwenye vizimba, upande wa Ziwa Victoria ndicho kipaumbele chetu cha kule tunakolekea ili kupunguza pressure ya uvuvi ule wa asili. Ili kuweza kufanikiwa katika lengo hili tunahamasisha uundaji wa vikundi, hasa vikundi vya Ushirika, hivyo namwomba Mheshimiwa Chege na Waheshimiwa Wabunge wengine wote wa eneo hili waweze kuwahamasisha vijana wale wajiunge katika vikundi ili tuweze kupata mikopo kupitia Benki yetu ya Kilimo na hatimaye kuweza kuifanya shughuli hii ambayo itawaingizia kipato na kukuza pato la Taifa letu.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Februari 2010 Wizara ya Madini wakati ule wakati akijibu swali hili ambalo liliulizwa na Mbunge wa wakati huo Prof. Sarungi majibu ya Serkali yalikuwa haya haya kuhusiana na utafiti wa eneo lile kwa madini ya Helium, miaka 10 baadae 2021/2022 GST kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kupita na kufanya utafiri lakini bado hawakuwahi kufika eneo lile. Leo ni miaka 12 sasa toka tumepata majibu haya lakini madini haya yameanza kuzungumzwa toka mwaka 1952. Nilitaka nipate comitment ya Sarikali sasa, kwa sababu ni muda mrefu imekuwa ikizungumziwa juu ya kufanya utafiri kwenye ya eneo lile lakini haufanyiki kwa wakati.

Je, kipindi hiki cha mwaka huu wa bajeti kwa mujibu ya Serikali eneo hili litanyiwa utafiti ili kuondokana na haya ambayo yamekuwa yakifanyika huku nyuma na wananchi waweze kunufaika na madini ya eneo lile?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili kwenye tarafa hiyo hiyo tarafa ya Jirango Kijiji cha Upege eneo la form kuna madini pale ya dhahabu na leseni amepewa mtu wa Barec toka mwaka 1997 lakini mpaka sasa zaidi ya miaka 20 na kitu hayajaanza kuchimbwa madini yale. Nataka pia nipate commitment ya Serikali ni lini sasa madini yataanza kuchimbwa kwenye eneo lile Utegi alimaarufu kama farm ili kuongeza mapato lakini kuongeza na kutoa ajira kwa vijana ndani ya Wilaya yetu ya Rorya. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kwanza kumpongeza ndugu yangu Mheshimiwa Wambura Chege kwa jinsi anavyowapambania wapiga kura wake na hususan hawa wachimbaji wa madini na jinsi anavyopigania maslahi ya rasilimali ya hii ya madini iweze kufanyiwa kazi ili nchi yetu iendelee kuneemeka kwa utajiri tulionao wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la kwanza kuhusu ni lini hii gesi asilia ya Helium itaanza kuchimbwa katika eneo la jimbo lake. Napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba tafiti za kutafuta haya madini Helium katika nchi yetu zinaendelea katika sehemu mbali mbali kama nilivyotaja katika kujibu swali lake la msingi, na hata kwa kuongezea katika bonge la Mto Rukwa kuna utafiri mkubwa ambao pia unaendelea na ambao viashiria vimeonyesha kwamba Tanzania huenda ikawa nchi ya kwanza Dunia kwa kuwa na akiba kubwa ya madini hayo kuliko nchi zote duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa hali halisi ilivyo kwa sasa hivi tafiti zinaendelea na mara tafiti hizi zitakavyojiridhisha kwamba tumepata akiba ya kutoka katika maeneo mbali mbali juhudi za kuwapata wawekezaji wa kuchimbua madini haya ya gesi asilia ya Helium yataweza kuendelea. Kwa hiyo, nimuhakikishiue Mbunge kwamba utafiti ambao tumepangia bajeti hii inayokuja uendelee kufanywa kwa kina zaidi utatuletea majibu sahihi kwamba ni lini hayo madini yataanza kuchimbwa katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili anapenda kufahamu kwamba madini ya dhahabu ambayo nayo yamekuwa yakiendelea kufanyiwa utafiti katika Kijiji cha Utegi katika tarafa ya Gilongo katika Jimbo lake yataanza kuchimbwa lini maana tafiti zimeendelea kwa muda mfefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshsimiwa Mbunge kwamba katika eneo hilo maeneo yaliyogundulika kwamba kuna dhahabu ni maeneo ya shamba maalum la Serikali linaitwa farm kwa jina mashuhuri. Lakini utafiti ambao umekuwa ukiendela kwa miaka mingi sasa bado unaendelea, na mara wale watafiti watakapokuwa wamejiridhisha kwamba kuna madini pale taratibu zitafuatwa kulingana na vifungu vya 95 na 96 ya sheria yetu ya madini sura 123 ili waweze sasa kupata vibali vya kuchimba madini hayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na Kata ya Roche pamoja na Ikoma kujumuishwa katika Kata 763 ambazo utekelezaji wake kwa maana ya zabuni kutangazwa mwezi Oktoba, lakini kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa sana wa ujenzi wa minara maeneo mengi nchini hata pale panapokuwa no objection imetoka, lakini bado ujenzi wa minara mingi nchini unakuwa umechelewa.

Nilitaka nipate kauli ya Serikali juu ya hili kwamba ni nini kinasababisha pamoja na kwamba no objection inakuwa imetoka lakini ujenzi wa minara inachukua miaka miwili mpaka mitatu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni mara ya tatu nauliza swali hili Kata ya Bukura, Kata ya Ikoma, Goribe pamoja na Roche ni kata ambazo ziko mpakani, lakini haziwasiliani hakuna mawasiliano ya Kitanzania.

Nilitaka nijue kwa sababu hiyo ya kukosa mapato pamoja na usalama wa Kata zile nini kauli ya Serikali juu ya ujenzi na utekelezaji wa minara maeneo ya mpakani kwa dharura na kwa haraka ili kusaidia maeneo yale ya kimpakani ndani ya nchi yetu? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni kweli kwamba imekuwa inatuchukua miezi tisa mpaka 12 kujenga mnara ambayo ndio ilikuwa hali iliyokuwa imezoeleka na sababu yake ni moja tulikuwa tunatumia miezi sita kutafuta vibali mbalimbali vya kujenga hiyo minara kwenye maeneo husika, lakini tunashukuru Wizara ya Mazingira chini ya kaka yangu Mheshimiwa Jafo sasa wamerahisisha badala ya kutumia kwa miezi sita tumeweza baadhi ya maeneo ikiwemo Zanzibar kupata vibali ambavyo tulikuwa tunatumia miezi sita tumepata kwa mwezi mmoja na hivyo muda wa kujenga minara umepungua sana. Uzoefu uliotokea Zanzibar tumejenga kwa siku 90 kwa hiyo, tunaamini hata eneo hili tutakapopata no objection mradi huu utachukua miezi isiyozidi minne na tuna hakika kwamba utakuwa umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kata husika alizozitaja ni kweli ziko mpakani na yeye na Mkuu wake wa Wilaya wamekuwa wakiwasiliana na sisi mara kwa mara. Changamoto iliyotupata ni kwamba tulipotangaza tender ya kujenga minara kwenye maeneo haya, hawakupatikana wajenzi tukarudia kutangaza mara ya pili na bado mkandarasi hakupatikana.

Tulichoamua tumeamua kuchukua miradi kwenye kata hizi na kuingiza kwenye Tanzania ya Kidigitali ambayo package yake kidogo ni nzuri. Kwa hiyo, wakandarasi watapatikana, nimtoe shaka nia yetu ni kuhakikisha maeneo ya mipakani inapata mawasiliano ya kutosha na hasa kwa sababu biashara ya mpakani ni kubwa na sisi tunapenda kufanya biashara kwenye maeneo hayo. Nimhakikishie kwamba minara hii itajengwa na itajengwa kwa wakati. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Wilaya ya Rory ana Tarime moja ya faida ambayo tunaipata kuwepo mpakani kati ya Tanzania na Kenya ni pamoja na unafuu wa bei ya bidhaa ambazo zinazalishwa maeneo ya mpakani.

Swali la msingi hapa lilikuwa linauliza Wizara haioni kuna umuhimu sasa wa kuwasaidia wale wachuuzi wadogo ambao unakuta bidhaa chache, kwa mfano mifuko miwili ya cement, mifuko mitano ya sukari ambayo wakikamatwa wakati mwingine hupewa kesi za uhujumu uchumi au hunyang’anywa pikipiki zao au kutaifishwa bidhaa zao zile chache. Mheshimiwa Waziri haoni kuna umuhimu wa kuwasaidia hawa wafanyabiashara wadogo ili kutengeneza mazingira rafiki angalau waweze kufanya biashara hizi bila usumbufu wanaopata?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Wilaya ya Rorya tayari tuna eneo ambalo tumelitenga kwa ajili ya kuweka viwanda kwa mahitaji na muktadha wa bidhaa hizo hizo ambazo wananchi wetu wanavuka kwenda kuzifata Kenya.

Je, Wizara ina mpango gani wa kuhakikisha angalau inazungumza na wawekezaji wa bidhaa hizi hizi wanazozalisha Kenya kujenga kiwanda, kuja kuwekeza maeneo ya Rorya ili tuwasaidie hawa wananchi wanaovuka maeneo ya mpaka kwenda nchini Kenya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chege kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli moja ya mikakati ambayo tunayo Serikali ni kuona namna gani tunawasaidia wachuuzi au wafanyabiashara wadogo wadogo, wajasiriamali katika mikoa ya mipakani ambao wanafanya biashara kati ya nchi na nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya maelekezo ambayo tulishawaelekeza maafisa wetu wa taasisi zote zinazohudumia wafanyabiashara mipakani ikiwemo TRA, TBS na nyingine kuhakikisha kwanza wanatoa elimu kwa wachuuzi hawa wajasiriamali namna ya kufanya biashara kati ya nchi moja na nyingine. Lakini zaidi waendelee kuwasaidia kwa maana ya kuwapa muda fulani kama angalizo wakati wanaendelea kujifunza namna ya kufanya biashara kati ya nchi hizi mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la pili nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya mikakati yenu ni kuona tunawavutia wawekezaji katika kujenga viwanda maeneo ya mipakani ikiwemo katika eneo la Rorya. Kwa hiyo, hilo tutalifanya na tutachukua kwa uzito mkubwa nimwakikishie Mbunge tutalifanya hilo tutashirikiana naye, nitawasiliana naye baada ya kikao hiki. Nakushukuru sana.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Utegi-Shirati mpaka Kilongwe ni barabara ya kimkakati inayounganisha nchi mbili kati ya Tanzania pamoja na Kenya kwa kupitia Wilaya ya Rorya. Na kwa kuwa tayari upembuzi yakinifu wa barabara hii umeshakamilika nilitaka nijue ni lini sasa barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii ni muhimu kwa sababu inaunganisha Tanzania na Kenya. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nitakuwa na swali moja dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa Mamlaka ya Mji Mdogo, mamlaka ambayo imeahidiwa kwa muda mrefu kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Mwaka 2009 Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake Mheshimiwa Mizengo Pinda, aliahidi; pia imetajwa kwenye awamu karibu tatu za Ilani ya Uchaguzi ya Chama changu cha Mapinduzi. Mwaka 2020 Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyepo naye aliahidi kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji Mdogo. Nilitaka nijue tu Mheshimiwa Waziri kama yuko tayari sasa kuongozana nami kwenda kujiridhisha sababu hizi zinazosema kwamba uanzishwaji wake unacheleweshwa kwa sababu ya mapato ya ndani. Tuongozane ili twende kujiridhisha kwa kukaa na wataalam na Halmashauri ili tuweze kupata jibu la pamoja la uanzishwaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Shirati.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niko tayari na nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge ndani ya wiki mbili tutakaa na Baraza la Madiwani pamoja na Wakurugenzi katika Halmashauri yake, kuainisha na kutangua vyanzo vyote vya mapato ili tuone kama vinaweza kuhudumia ili mamlaka hii ndogo iweze kuanza.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kituo cha Afya cha Changuge, Tarafa ya Gelango, Wilaya ya Rorya ni moja ya kituo ambacho kimejengwa muda mrefu sana na kwa sasa majengo yake yamechakaa na hata yaliyopo hayatoshelezi kulingana na mahitaji ya tarafa na kata ile. Nataka nijue mpango wa Serikali sasa kuboresha vituo vya afya vile vya zamani ili angalau viendane sasa na kasi na uhitaji wa wananchi wa sasa. Nini mpango wa Serikali katika kuboresha vituo vya afya vya zamani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jafari Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika maeneo mbalimbali kote nchini kuna baadhi ya vituo vya afya na hospitali za halmashauri ambazo ni chakavu, na Serikali imeweka kanzidata kwa kutambua vituo vya afya chakavu na itaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya ukarabati wa vituo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tuichukue hii hoja ya Mheshimiwa Mbunge, tufanye tathmini ya kituo hicho cha afya na kuona uwezekano wa kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya matengenezo. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi: -

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Rorya ni moja ya Wilaya ambazo na sisi tumeanza mchakato wa muda mrefu sana kwa ajili ya maombi ya kupata Chuo cha VETA, na Mheshimiwa Waziri unakumbuka nimekuwa nikikusumbua sana kwa muda mrefu ili angalau na sisi tuweze kupata chuo cha VETA. Nilitaka nijue sasa kwenye mpango wa bajeti ya mwaka huu katika vyuo vya VETA 63 kama na sisi Wilaya ya Rorya tumo katika vyuo hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya zilizobaki ambazo hazina Vyuo vya VETA ni Wilaya 63, tafsiri yake Wilaya ya Rorya nayo imo katika ile orodha. Tafsiri yake tunataka tujenge katika Wilaya zote ambazo hazina vyuo kwa awamu. Kwa hiyo, katika awamu ya kwanza tutaanza kwa Wilaya zote ambazo hazina kwa pamoja katika mwaka huu wa fedha na mwaka unaofuata ina maana tutakuwa na jukumu la kumalizia kazi ile ambayo tutakuwa tumeianza katika mwaka huu wa fedha. Nakushukuru sana.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mpango huu kwa Wilaya ya Rorya kuna vijiji zaidi ya 20 na nimeshamtumia Mheshimiwa Waziri, ambavyo wengi wao wame-raise malalamiko ya kuachwa kwenye mpango wenyewe kipindi unatekelezwa. Nataka nijue nini mkakati wa Wizara kwenye vile vijiji ambavyo hasa watu wanalalamika kwamba waliachwa kipindi cha awali katika mpango wa utekelezaji wa TASAF. Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyokuwa nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, naomba nimjibu Mheshimiwa Chege kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, jibu ni hivyo hivyo kwamba kaya zote ambazo zilikuwa zimeachwa na zinastahili kuingia katika mpango, awamu hii ya pili zinaingizwa zote kwenye mpango huu. Vile vile vijiji vyote ambavyo vilikuwa vimesalia havikuingia kwenye mpango huu wa TASAF, sasa vinaenda kuingia katika mpango huu wa TASAF.

Mheshimiwa Spika, sasa huenda nione ni namna gani nitakutana na Mheshimiwa Chege ili tuweze kupanga, tuone tunasaidiaje hivi vijiji 20 ambavyo anavyo jimboni kwake, kuweza kuona tunakwenda kuziona ama tunawaelekeza wenzetu wa TASAF waweze kufika katika jimbo la Mheshimiwa na kuona tunawasaidiaje walengwa hawa.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Barabara ya Utegi – Kowaki – Kinesi ni barabara iliyoahidiwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli toka akiwa Waziri wa Ujenzi. Nataka nijue ni lini sasa utekelezaji wa ujenzi wa lami wa barabara hii kutoka Kowaki mpaka Kinesi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii iliahidiwa na kiongozi. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeratibu ahadi zote ikiwepo na hii barabara ambayo ameianisha. Nimhakikishie kwamba barabara hii itajengwa kadri Serikali itakapopata fedha. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Bukura kwa maana ya Kirongwe, Roche, Goribe na Ikoma ni Kata zilizoko mpakani na Mheshimiwa Waziri nafikiri unazifahamu hizi, lakini ni Kata ambazo hazina huduma yoyote ya mawasiliano. Pamoja na kwamba, Mkandarasi amepatikana ninataka nijue commitment yenu ni lini Mkandarasi huyu ataanza ujenzi wa minara kwenye maeneo haya ya mpakani kati ya Tanzania na Kenya?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Mheshimiwa Mbunge jana tuliwasiliana na nikamhakikishia ndani ya miezi miwili mitatu tayari ujenzi utaanza. Ahsante sana.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Waziri kwa majibu mazuri pamoja na kwamba hayajaleta sana matumaini kwa wananchi. Pamoja na majibu haya nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza nataka nijue tu kwamba pale utafiti utakapokamilika nini nafasi ya wachimbaji wadogo kupewa nafasi kuchimba madini kwenye eneo lile?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nataka nijue maeneo yanayozunguka eneo la Utegi kama Kowak, Mika na maeneo mengine nini nafasi ya kuanza utafiti kwenye maeneo yale ili eneo litakapokamilika utafiti wa awali kwenye eneo la kwanza iendane sambamba na eneo la pili na haya maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala zima la upatikanaji wa maeneo ya machimbo ya madini kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi hutegemea kukamilika kwa utafiti. Utafiti unapokuwa umekamilika na kwa jinsi ambavyo utafiti huo huchukua gharama kubwa na kampuni zinazofanya utafiti huu ni kampuni kubwa zenye uwezo wa uchimbaji mkubwa, sisi kama Wizara tuna mamlaka ya kumegua eneo ambalo wachimbaji wadogo wanaweza wakakatiwa, waweze nao kupata maeneo yao ya kuchimba kama ambavyo sera yetu inasema kwamba lazima tuwape wachimbaji wadogo maeneo ya kuchimba.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, swali lake hilo la kwanza la wachimbaji wadogo kupatiwa maeneo ya kuchimba linachukuliwa kwa uzito mkubwa na tutawahakikishia kwamba watapewa maeneo.

Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo anayazungumzia kwamba ni lini utafiti huo utakamilika na kuweza kuanza uchimbaji, ni wazi kwamba utafiti ndio utakaotupa jibu kwamba ni lini uchimbaji utaanza katika maeneo hayo.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Moja ya vijiji vilivyoathirika na machafuko ya Mto Mara ni pamoja na Kijiji cha Kwiguse, Marasibola na Kyamwame na Serikali iliahidi kupeleka maji mbadala kwenye vijiji hivi ambavyo havitumii maji haya kwa sasa. Nataka nijue Serikali imefikia wapi kwenye mpango huu wa kuhakikisha wale wananchi wanapata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimepokea, tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Eneo la Mto Mori linalounganisha Kata nne Kata ya Nyabulongo, Nyatorogo, Kigunga na Milale ni eneo ambalo wananchi wamekuwa wakipoteza maisha kwa muda mrefu sana hasa pale wanapojaribu kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine. Hivi ninavyozungumza, wananchi watano wamefariki na mpaka sasa tunaendelea na maombolezo ambapo walijaribu kuvuka kwa kutumia vyombo kwenye eneo lile.

Mheshimiwa Spika, nilitaka nijue Serikali ina mpango gani wa kutengeneza mkataba wa dharura angalau kwa kujengewa daraja kwa kutumia mkataba wa dharura ili kunusuru maisha ya hawa wananchi ambao hawana namna, wanalazimika kuvuka kwenda upande wa pili kutafuta huduma za kijamii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jafari Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri jambo ambalo amelieleza Mheshimiwa Mbunge ninalifahamu. Nasi tumeshamwagiza Mtendaji Mkuu wa TARURA kupeleka timu ya kwenda kufanya tathmini na baada ya hapo, watatuletea taarifa ili sasa tuandae mchoro kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu katika eneo hilo. Tathmini ya awali ambayo tafanyika sasa, itapelekea sasa angalau tuweke kivuko cha muda wa dharura ili wananchi wale waweze kuvuka katika eneo hilo. Ahsante sana.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kata ya Roche, Ikoma, Bukura pamoja na Goribe ni miongoni mwa kata ambazo ziko mpakani kati ya Tanzania na Kenya. Mheshimiwa Waziri nafikiri ulipata ridhaa ya kuzitembelea kata hizi ukaona hazina mnara na hakuna mawasiliano yote katika kata hizi. Nilitaka nijue katika zile minara ambayo umesema wanaitangaza mwezi Juni kama kata hizi nazo zinapata nafasi ya kutangaziwa ili waweze kupata mnara kuboresha na kuweka mawasiliano kwenye maeneo haya ya mpakani na kimkakati?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chege Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana Mheshimiwa Chege kwa sababu tumekuwa tukishirikiana vizuri sana; na maeneo na kata ambazo amezitaja Mheshimiwa chege tulishafika katika maeneo hayo. Vilevile katika mpango wa utekelezaji wa Tanzania Kidigitali tayari maeneo haya tumeyaingiza na Mheshimiwa Chege tayari anafahamu hilo. Kwa hiyo. kilichobaki sasa ni utekelezaji tu na tayari mkandarasi yuko tayari kwa ajili ya kuanza kazi mara moja kwa ajili ya maeneo hayo katika Jimbo la Rorya. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali lanyongeza. Ni kweli, nikiri kwamba mradi huu unaendelea na utakapokamilika, tuweke rekodi sawa, utanufaisha wananchi 4,792 badala ya laki moja na kidogo.

Mheshimiwa Spika, nataka niulize maswali mawili ya nyongeza pamoja na haya, kwamba wananchi wa kata ile wako zaidi ya 12,000, mradi huu ukikamilika unakwenda kuhudumia wananchi 4,700. Nataka nijue mkakati wa Serikali walionao ili kuhakikisha angalau wananchi wote waliosalia kwa zaidi ya elfu kumi na mbili na kidogo wanaweza kupata maji safi na salama?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kuna kituo cha afya ambacho kinajengwa kwenye kata ile, hivi ninavyozungumza wananchi wanatafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya. Nilitaka nijue kama mpango huu wa mradi huu nao pia utahakikisha maji yanafika kwenye eneo la kituo cha afya ambacho kinajengwa kwenye Kata ile ya Rabour?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chege kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vinafikiwa na maji ya bomba yaliyo safi na salama yakiwa ya kutosha. Hivyo niombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana, vijiji hivi vyote vitapata maji.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusiana na kituo cha afya, nimekuwa nikiongea hapa mara nyingi, tumeshaelekeza watendaji wetu kwenye mikoa yote na wilaya zote kuhakikisha maeneo yote yanayotoa huduma za afya, kwa maana ya vituo vya afya, zahanati hospitali yote yanakuwa na mitandao ya maji safi na salama ya kutosha. Lakini vilevile eneo lake Mheshimiwa Chege nalo ni moja ya maeneo ambayo tunakwenda kuyafanyia kazi na kituo cha afya nacho ni miongoni mwa vituo vitakavyoenda kunufaika.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nataka kujua kwa kuwa kasi ya utoaji wa fedha hailingani na uhitaji wa maboma yanayohitajika kwa zahanati kwa vijiji vyote. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu kwa mwaka huu wa bajeti kutenga fedha kukamilisha maboma yote ambayo yanahitajika kwenye vijiji vilivyohitaji ujenzi wa zahanati?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Serikali imekuwa ikitenga fedha shilingi milioni 500 mpaka shilingi milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata 26 kwenye jimbo moja. Je, Serikali haioni sasa badala ya kupeleka fedha hizi kwenye umaliziaji wa kituo cha afya kimoja, fedha hii iende kukamilisha maboma yote yaliyojengwa na nguvu za wananchi kwenye eneo hilo hilo la jimbo ambao wanaweza wakakamilisha maboma 14 badala ya kituo cha afya kimoja kwenye eneo moja la wilaya moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kasi ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati nchini kote kwa kweli ni kubwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka kipaumbele cha hali ya juu sana katika sekta ya afya na ndiyo maana katika kipindi cha miaka hii miwili zaidi ya maboma 1,600 ya zahanati yamekamilishwa na zahanati hizo zimeanza kutoa huduma. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kasi hii ya Serikali itaendelea ili kuhakikisha kwamba maboma hayo ambayo bado hayajakamilishwa yanakamilishwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, pili kuhusiana na kuacha kujenga vituo vya afya na kuweka kipaumbele kwenye zahanati, mfumo wa huduma za afya una utaratibu wa rufaa kwa ngazi. Ngazi za zahanati zina umuhimu wake katika ngazi ya vijiji lakini ngazi ya vituo vya afya ni rufaa ya zahanati na tunafahamu zahanati hazifanyi upasuaji na hazilazi kwa hiyo lazima tuendelee na nguvu za kujenga vituo vya afya sambamba na ujenzi wa zahanati.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi barabara ya Utegi – Shilati – Kilongwe yenye kilomita 56 upembuzi yakinifu umekwisha kamilika Mheshimiwa Waziri ni lini sasa barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jafari Chege Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja nikweli ipo kwenye Ilani na imeahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Naomba nimuombe Mheshimiwa Mbunge asubiri bajeti hii tutakayosoma tutakuwa tumependekeza nini kuhusu barabara hii ya kutoka Mika – Utegi – Ruari hadi Kirongwe, ahsante.
MHE. JAFARI W CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Vituo vya Afya vitatu kwa maana ya Kinesi, Changunge na Kituo cha Nyamagaro havina chumba cha kuhifadhia maiti. Nataka nijue mpango wa Serikali wa ujenzi wa vyumba hivi kwa ajili ya kunusuru na kusaidia wananchi maeneo haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba vituo hivi ambavyo vingine ni vipya havina majengo ya kuhifadhia maiti, lakini mpango wa Serikali ni kuendelea kujenga vituo hivi kwa awamu. Tumejenga majengo awamu ya kwanza, tumejenga awamu ya pili na sasa tunakwenda awamu ya tatu kwa ajili ya kujenga majengo mengine yakiwemo majengo haya ya kuhifadhia miili. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ninataka nijue tu ni lini Serikali itarejesha kituo cha MV Musoma kilichokuwa kinatoa huduma kati ya Kinesi kwa maana ya Rorya na Musoma Mjini hasa ukizingatia kituo kilichopo ni kidogo na hakikidhi mahitaji ya watu lakini pia ni hatari kwa maisha ya wananchi wake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kivuko cha Musoma - Kinesi kiliazimwa kwenda kufanya kazi kati ya Kisolya na Lujezi, Musoma tulipeleka kivuko cha Chato One. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunategemea mwishoni mwa mwezi huu Tarehe 30 Kivuko cha Kisolya- Lugeza ambacho kilikuwa kinatengenezwa kitakamilika na mwanzoni mwa mwezi unaokuja kivuko cha MV Musoma kitarudishwa kwa ajili ya kutoa huduma iliyokuwa imezoeleka kati ya Musoma na Kinesi. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka nijue Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya mkato inayotoka Komaswa – Tarime Vijijini kuja mpaka Rorya kupitia Nyatorogo pamoja na Daraja lake la Nyatorogo kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, kama ina mpango wowote wa ujenzi wa daraja pamoja na barabara hii? (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa unaweza ukataja vizuri hizo barabara zako kutoka wapi mpaka wapi?

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayotoka Komaswa – Tarime Vijijini kuja Rorya kwa kupitia Kata ya Nyatorogo ikiwa ni pamoja na daraja lake linalounganisha Tarime Vijijini pamoja na Rorya. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakaa na Mheshimiwa Mbunge kwanza kuona kwamba barabara hii ni ya TARURA au ya TANROADS halafu kuona ni hatua gani ambazo tunaweza tukazichukua kuweza kufungua Barabara hii ya mkato ya Komaswa hadi Rorya. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mpaka sasa wavuvi wetu wameendelea kupigwa na kunyang’anywa mali zao hasa malighafi ya samaki maeneo ya ziwani. Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuimarisha Jeshi la Marine Sota pale Wilaya ya Rorya ili kuimarisha ulinzi maeneo ya ziwa kwa ajili ya kulinda wavuvi pamoja na malighafi Samaki?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa zoezi hili la uhalifu linafanywa na askari wa nchi jirani. Serikali haioni umuhimu sasa kupitia Wizara kufanya mazungumzo na nchi hizi jirani ambao wanafanya uharibifu na kupiga wavuvi wetu ili waweze kuacha zoezi hili mara moja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uimarishaji wa Kituo cha Marine Sota, nadhani nikubali hiyo ahadi. Mwezi uliopita Waziri wangu alitembelea eneo hilo na ile ilikuwa ni moja ya concern kwamba Kituo cha Marine cha Sota kiko dhaifu. Kwa hiyo kupitia hadhara hii ya Bunge lako tukufu, nimwombe Mkuu wa Jeshi la Polisi azingatie kuimarisha Kituo hiki cha Sota ili kiweze kutimiza wajibu wake ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uhalifu kufanywa na wanaodhaniwa kuwa ni askari wa nchi jirani, Jeshi la Polisi litafanya uchunguzi, pale itakapothibitika tutaimairisha vikao vya ujirani mwema kati ya wakuu wetu wa vyombo kudhibiti suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Halmashaui ya Wilaya ya Rorya ni mwaka wa tatu sasa haijawahi kuajiri watendaji wa vijiji wala wa kata na kwa kuwa sasa tumeomba kibali kwa ajili ya kupata kuajiri watendaji hawa;

Je, Serikali inachelewa nini kutupa kibali na sisi tuweze kuajiri kwenye maeneo ambayo yana upungufu wa watendaji wa vijiji na watendaji wa kata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itatoa vibali hivi vya ajira kadri ya bajeti itakavyoruhusu, na tutaangalia katika bajeti iliyotengwa mwaka 2023/2024, kama kuna nafasi hizi zilizotangazwa basi kule Rorya ambapo kuna upungufu na wameomba kibali, kibali kiweze kutolewa. Kama hakuna iliyotengwa basi tutaipa kipaumbele katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye matumaini kwa wananchi wangu wa Rorya, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa Sheria ya Uthamini inatamka wazi kwamba thamani ya ardhi inapaswa kulipwa ndani ya miezi sita, lakini wananchi hawa wamedai malipo yao toka mwaka 2011 na hawajalipwa. Nataka nipate commitment ya Serikali itakapofika Novemba kama wananchi hawa hawajalipwa uthamini wa ardhi yao, je, Serikali itakuwa tayari sasa kurudia uthamini kwa mujibu wa Sheria inavyotamka kwamba wananchi wale walipwe ardhi kwa mujibu wa Sheria inavyotamka?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa jambo hili limekuwa ni la muda mrefu toka mwaka 2011 na sasa liko ndani ya Ofisi ya Mkurugenzi nataka nipate commitment ya Serikali hasa Ofisi ya Wizara ya TAMISEMI, je, ni lini watalipa fedha ili wathamini warudi site wakamilishe uthamini na upande wa TANESCO waweze kulipa fidia kwa wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Chege, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu kurudia zoezi ikifika Novemba, zoezi hili limeshachukua muda mrefu nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imeshatenga fedha kiasi cha milioni 350 ili wananchi 231 wanaodai fidia walipwe ikifikia Novemba, 2023. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hili tunaenda kulikamilisha na kwa sababu limechukua muda tutafuatilia kwa ukaribu kuhakikisha kwamba linakamilika.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili kuhusiana na kutoa fedha, tayari Serikali kupitia TANESCO imeshatoa fedha kiasi cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya kukamilisha zoezi la uthamini. Tutafuatilia kuhakikisha kwamba Halmashauri ya Rorya inakamilisha taratibu hizi kwa wakati ili zoezi hili liweze kukamilika kwa wakati kwa kadri ambavyo imepangwa, ahsante. (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii tena kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya kuhakikisha kwamba fedha hizi ambazo wenzetu wa TANESCO wameshazipeleka kwenye halmashauri ile ziweze kutumika mara moja na kulipa fida hiyo. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, Kata ya Kirogo wananchi wa Kata hii ili kufanya mawasiliano wakati mwingine huwalazimu kupanda juu ya milima, na kwa kuwa Kata hii ipo kwenye ile miradi ya kidigitali, ninataka nijue commitment ya Serikali, ni lini miradi hii itaanza ya ujenzi wa minara kwenye Kata hii ya Kirogo? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, mradi huu umeshaanza na upo katika hatua mbalimbali. Tunaamini kwamba Jimbo la Rorya watafika kwa ajili ya utekelezaji huo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Barabara ya Utegi – Shirati mpaka Kirongwe kwa kuwa upembuzi yakinifu umekwishakamilika na barabara imeingizwa kwenye bajeti. Nataka nijue nini mpango wa Serikali sasa kuanza ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ndiyo imetengewa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, tunajua upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishakamilika, kwa hiyo taratibu za manunuzi kuanza ujenzi wa barabara hiyo zitaanza mwaka wa fedha wa 2023/2024 kama ilivyopitishwa na Bunge hili kwa maana ya mwaka ujao wa fedha. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nataka nijue ni lini sasa REA Phase Three Round Two ya kusambaza kilometa mbili za ziada kwenye Wilaya ya Rorya utaanza kufanya kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili. Kampuni tanzu ya ETDCo imepewa kazi zaidi ya miaka mitatu sasa kusambaza umeme wilaya ya Rorya, lakini mpaka sasa hawajaanza kufanya kazi.

Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kumfuta mkandarasi huyu ili itangaze upya waombe wakandarasi wengine kwa ajili ya kusambaza umeme Wilaya ya Rorya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, leo tunatarajia wenzetu wa REA watasaini baadhi ya mikataba ya extension ya kilomita mbili kwa kila kitongoji na tunaamini kufikia mwishoni mwa mwezi huu wakandarasi hao watafika site ili kuanza kufanya kazi hizo za kuongeza hizo kilometa mbili kwenye maeneo ambayo mikataba ya vijiji imekamilika na pengine inaendelea.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili, naomba baada ya hapa nikae na Mheshimiwa Chege ili tuone tatizo liko wapi kwa sababu tunafahamu miradi mingi inaendelea kwa hatua mbalimbali katika maeneo yetu, specifically nitakaa ili tubaini changamoto aliyoiona iko wapi na tuweze kueleweshana na kuchukua hatua stahiki.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, pamoja na majibu mazuri na kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii kwa maana ya Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Suba yeye vijiji 20 na sio 17 vijiji vinne kwa maana ya Kijiji cha Ruhu, Muundwe, Kibuyu na Mkengwa ni vijiji ambavyo havina mradi wowote wa maji mpaka sasa. Ninataka nipate kauli ya Serikali juu ya vijiji ni lini sasa vitapata maji safi na salama?

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, pamoja na vijiji 16 kuwa na maji safi na salama lakini vitongoji katika vijiji hivi maji hayajatapakaa kwenye vitongoji. Nayo pia nilitaka nipate kauli ya Serikali, kwamba Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuhakikisha angalau vitongoji kwenye vijiji hivi 16 vinapata maji safi na salama kwa ajili ya huduma ya maji kwa wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chege kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote niseme nimepokea marekebisho ya idadi ya vijiji vyake lakini vilevile katika maeneo haya aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge nipende kumuelekeza Meneja wa Wilaya aendelee kufanya jitihada za kuona anapata visima ili vijiji hivi vipate maji. Mheshimiwa Mbunge eneo lako ni moja ya maeneo yanayonufaika na mradi ya miji 28. Kwa hiyo, wakati miji 28 utekelezaji unaendelea na ni kwa sababu ni mradi wa muda mrefu, jitihada za miradi ya muda mfupi zitaendelea kufanyika na ushirikiano wako namna ambavyo umekuwa ukiufanya, tutahakikisha tunafanya yale tuliokubalina.

Mheshimiwa Spika, katika vijiji hivi 16, vitongoji ambavyo havina maji tutahakikisha tunasambaza maji, Meneja wa Wilaya tayari tumemuelekeza na ninamsisitiza ili ahakikishe maeneo yote yanapata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nataka nijue Serikali ina mpango gani wa kupandisha hadhi Barabara ya Bukama - Nyamagaro mpaka Kiangasaga kuwa hadhi ya barabara ya Mkoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chege kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007, Kifungu cha 11 na Kanuni za Usimamizi wa Barabara ya mwaka 2009 imeelezea wazi namna ya kuomba kupandisha hadhi barabara. Inatakiwa waanze kukaa vikao vyao kule na kupendekeza kwa Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa, Mkoa wao wa Mara. Wakishapendekeza pale, baada ya hapo wanawasilisha maombi yale kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi mwenye dhamana ya ujenzi.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Rorya, ni moja ya wilaya ambayo ipo kwenye kanda maalum kwa maana ya Tarime na Rorya, lakini ni wilaya ambayo haina Kituo cha Polisi cha Kiwilaya, ina Vituo vya Polisi vya Kikanda kwa maana ya Utegi, Kinesi na Shirati. Nataka nijue mpango mkakati wa Serikali wa kujenga Kituo cha Polisi cha Wilaya nzima ya Rorya, itakuwa iko kwenye mpango kule?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chege, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunafahamu kwamba ziko wilaya nyingi hasa hizi wilaya mpya hazina vituo vya wilaya ya Polisi, ikiwemo hii Wilaya ya Rorya. Mpango wa Serikali kama ilivyosemwa wakati Waziri akiwasilisha hotuba yake hapa; tuna mkakati wa kujenga vituo vya Polisi kwenye mikoa ambao hawana vituo vya Polisi kwa ajili ya RPC na vilevile kwenye wilaya ambazo hazina Vituo Vikuu vya Polisi vya Wilaya. Kwa hiyo, mpango huo kadri tutavyokuwa tunapata fedha utaekelezwa, na Wilaya ya Rorya itakuwa ni moja ya wilaya ya vipaumbele kwa sababu iko mpakani.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua mpango na kazi kubwa ya Serikali ni pamoja na kuweka mazingira mazuri na mazingira wezeshi kwa wavuvi hasa kuimarisha masoko kwa sababu baada ya bidhaa kupatikana ndio ukuaji wa viwanda kwenye maeneo mengine.

Nilitaka nijue Mpango Mkakati wa Serikali mlionao kushughulikia na kukimbilia soko la mpakani kati ya Tanzania na Kenya kuweka soko pale la samaki kwa ajili ya maboresho na ukuaji wa viwanda hivyo ambavyo vinazungumzwa vya Musoma. Nataka nijue Mpango Mkakati wa Serikali mlionao. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, nimshukuru sana Mheshimiwa Chege kwa ufuatiliaji wake hasa kuhusiana na masoko ya mazao ya uvuvi kuelekea kwenye nchi jirani ya Kenya. Tumeliona tatizo hilo na tuna mpango sasa wa kuweka utaratibu hasa kwenye mpaka ule wa Sirari ili kwamba wavuvi wanapopeleka mazao yao kwenda nchi ya Kenya au mpakani wasipate usumbufu ambao walikuwa wakiupata huko nyuma. Kwa sasa tutaweka utaratibu ambao utawasaidia wavuvi hawa kulipa tozo mbalimbali ambazo wanatakiwa kulipa za halmashauri lakini pia za Serikali Kuu, kwa urahisi zaidi ili waweze kulipata soko la nchi jirani ya Kenya ambalo mara nyingi kwa kweli linawapa bei iliyo nzuri.

Kwa hiyo, tutashirikiana na wenzetu walioko pale mpakani upande wa Wizara nyingine Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (Uhamiaji) ili kuweka urahisi utakaowafanya wavuvi wetu waweze kulipata soko la nchi jirani kwa urahisi zaidi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Kwa kuwa, barabara ya Utegi – Shirati mpaka Kihongwe Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekwishakamilika na barabara hii tayari imetengewa fedha. Ninataka kujua kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa barabara hii itatangazwa na kuanza ujenzi wa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chege, swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli bahati nzuri barabara hii nimetembelea tukiwa na Mheshimiwa Mbunge na aliahidiwa kwamba barabara hii itaanza kujengwa. Barabara hii ipo kwenye mpango wa kuanza kuijenga kwa kipindi cha bajeti hii ya 2023/2024. Kwa hiyo, taratibu za kuandaa tender document zinaendelea, basi zikikamilika barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza naishukuru Serikali kwa kutupatia gari la ambulance katika Kituo cha Afya cha Kinesi. Kituo cha Afya cha Kinesi kinahudumia tarafa mbili kwa maana ya vijiji zaidi ya 25. Kwa sasa tunapopata maafa Wananchi hutulazimu kusafirisha miili ya ndugu zetu hawa kwenda Musoma Mjini kwa kutumia mtumbwi ama boti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari tuna jengo la mochwari katika kituo hiki, ni nini mpango wa dharura kuhakikisha kwamba mnatupatia jokofu ili kunusuru na kuondoa adha wanayopata Wananchi wakati wanapopata maafa haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilipeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinesi, kimekamilika na kinatoa huduma. Tunafahamu kwamba kituo hiki bado hakijakamilisha ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti na upo katika hatua ya asilimia 85. Tunafahamu pia kwamba jengo hili halijapata mashine kwa maana ya jokofu la kuhifadhia miili ya marehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambaye alishatoa maelekezo hayo, kwamba wahakikishe kupitia mapato ya ndani wanakamilisha asilimia 15 iliyobaki kukamilisha jengo la mochwari. Mheshimiwa Rais ameshapeleka shilingi milioni 400 kwa ajili ya kununua vifaatiba na kati ya fedha hiyo watenge hiyo shilingi milioni 32.5 kwa ajili ya kununua jokofu la kuhifadhia maiti kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kinesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwa ujumla, tumekuwa na hoja nyingi za Waheshimiwa Wabunge kutoka katika Majimbo yote, Mheshimiwa Rais amepeleka fedha shilingi milioni 500, vituo vya afya vimekamilika vimeanza kutoa huduma. Wakurugenzi wa Halmashauri, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wasimamie mapato ya ndani kukamilisha majengo ya kuhifadhia maiti katika vituo vyote ambavyo vimekamilika ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi. Kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshaleta fedha ni kazi ndogo ya shilingi milioni 30 tu kukamilisha yale majengo lakini pia waweke kipaumbele kununua majokofu kwa ajili ya majengo hayo katika vituo hivyo. Ahsante.(Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza naishukuru Serikali kwa kutupatia gari la ambulance katika Kituo cha Afya cha Kinesi. Kituo cha Afya cha Kinesi kinahudumia tarafa mbili kwa maana ya vijiji zaidi ya 25. Kwa sasa tunapopata maafa Wananchi hutulazimu kusafirisha miili ya ndugu zetu hawa kwenda Musoma Mjini kwa kutumia mtumbwi ama boti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari tuna jengo la mochwari katika kituo hiki, ni nini mpango wa dharura kuhakikisha kwamba mnatupatia jokofu ili kunusuru na kuondoa adha wanayopata Wananchi wakati wanapopata maafa haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura Chege, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilipeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinesi, kimekamilika na kinatoa huduma. Tunafahamu kwamba kituo hiki bado hakijakamilisha ujenzi wa jengo la kuhifadhia maiti na upo katika hatua ya asilimia 85. Tunafahamu pia kwamba jengo hili halijapata mashine kwa maana ya jokofu la kuhifadhia miili ya marehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambaye alishatoa maelekezo hayo, kwamba wahakikishe kupitia mapato ya ndani wanakamilisha asilimia 15 iliyobaki kukamilisha jengo la mochwari. Mheshimiwa Rais ameshapeleka shilingi milioni 400 kwa ajili ya kununua vifaatiba na kati ya fedha hiyo watenge hiyo shilingi milioni 32.5 kwa ajili ya kununua jokofu la kuhifadhia maiti kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kinesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwa ujumla, tumekuwa na hoja nyingi za Waheshimiwa Wabunge kutoka katika Majimbo yote, Mheshimiwa Rais amepeleka fedha shilingi milioni 500, vituo vya afya vimekamilika vimeanza kutoa huduma. Wakurugenzi wa Halmashauri, Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya wasimamie mapato ya ndani kukamilisha majengo ya kuhifadhia maiti katika vituo vyote ambavyo vimekamilika ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi. Kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshaleta fedha ni kazi ndogo ya shilingi milioni 30 tu kukamilisha yale majengo lakini pia waweke kipaumbele kununua majokofu kwa ajili ya majengo hayo katika vituo hivyo. Ahsante.(Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuendelea kwa maboresho ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, nataka nijue Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa mtaridhia kama Wizara kuhamisha Mabaraza ya Ardhi kutoka kwenye wizara kwenda kwenye mfumo wa kimahakama? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; ili kuongeza ufanisi na usimamizi katika sekta ya ardhi nchini, je, ni lini Serikali itaridhia na kukubali kuanzisha kwa mamlaka ya maendeleo ya ardhi nchini kama zilivyo mamlaka zingine kwa mfano RUWASA na taasisi nyingine, ili kuendelea kuimarisha usimamizi na uimara katika kutatua migogoro nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jafari Wambura, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja, ni lini Mabaraza ya Ardhi yatahamishiwa kwenye mhimili wa Mahakama. Jambo hili lipo kwenye mchakato na linapitiwa na mamlaka mbalimbali ili kuona uwezekano wa namna ya kuhamisha mabaraza haya kuyarudisha kwenye mhimili wa Mahakama.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuunda chombo maalum cha kuendeleza na kusimamia ardhi nchini, Wizara yetu ipo kwenye mchakato wa kuanzisha kamisheni ya ardhi ambayo itasimamia mamlaka hii ya ardhi kwa maendeleo ya Watanzania hawa.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru, ni lini barabara ya Utegi – Shirati – Kilongwe itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, barabara hii ndiyo kati ya zile barabara za kilometa 27 ambazo zimepewa kibali itangazwe kwa ajili ya kuanza ujenzi. Ahsante.
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kituo cha Afya cha Kinesi ambacho kinahudumu kama hospitali kwa maeneo ya Tarafa ya Suba ni kituo cha afya ambacho hakina gari kwa ajili ya kubebea wagonjwa. Sisi kama halmashauri tulikubaliana tutapeleka gari kupitia yale magari ya UVIKO ambayo Serikali ilituahidi kwamba yatakuja kwenye halmashauri ambazo zilitajwa. Nataka nijue sasa Serikali imefikia wapi kupata yale magari ili yaweze kwenda kwenye Kituo cha Afya cha Kinesi kwa ajili ya kutoa huduma kwenye maeneo yale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jafari Chege, Mbunge wa Jimbo la Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali itapeleka magari ya wagonjwa kwenye halmashauri zote, lakini ni maamuzi ya halmashauri kuamua gari liende hospitali ya halmashauri au Kituo cha Afya ambacho wanaona ni kipaumbele zaidi katika halmashauri husika. Kwa hiyo, ni maamuzi yao katika halmashauri kwa kushirikiana na wataalam wa afya kufanya maamuzi hayo, lakini nimhakikishie kwamba mapema Julai au mwanzoni mwa mwezi wa Agosti, 2022, magari haya yatakuwa yamefika kwenye halmashauri zetu. Ahsante. (Makofi)