Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jafari Chege Wambura (11 total)

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi. Niseme tu kwa kuwa, hapo nyuma nilishapata nafasi ya kuchangia, hasa kwenye upande wa shughuli za kijamii, kwa maana ya maji, umeme na shughuli nyingine. Leo kwenye mpango nilitamani sana nijikite eneo moja la ardhi pamoja na makazi.

Mheshimiwa Spika, kwenye mpango natambua tumeiweka kwamba, Serikali ina mpango wa kuhakikisha angalao eneo lililosalia ambalo halijapimwa kwa ukubwa wa eneo letu zaidi ya 880,000 kilometa za mraba tumepima eneo zaidi ya asilimia 25 peke yake. Lakini kwenye mpango umetamka namna gani ambavyo kwa miaka hii mitano tunajikita kwa ajili ya kutambua, kupanga pamoja na kupima.

Mheshimiwa Spika, sasa nilitamani nishauri kwasababu, uliwahi kusema hapa ndani na mimi niendelee kuisema kama tukiitumia ardhi yetu vizuri, tukiipima vizuri ardhi yetu naamini kwa sababu, ni mdau wa sekta hii ya ardhi naamini inawezekana ndio kikawa chanzo kikubwa sana cha mapato ndani ya nchi yetu hii Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nishauri? Nini tufanye kutokana na mpango uliopo? Cha kwanza. Ipo idara ambayo inasimamia shughuli za kupanga, kupima pamoja na kurasimisha ardhi ambayo iko chini ya Wizara ya Ardhi. Tulivyokuwa na changamoto ya maji vijijini tulianzisha chombo cha kushughulika na changamoto za maji, RUWASA. Tulivyokuwa na changamoto za barabara vijijini tulianzisha TARURA, tulivyokuwa na changamoto za umeme tulianzisha REA.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri baddala ya kuwa na idara ambayo imejificha ndani ya wizara inayoshughulika na kupanga, kupima na kurasimisha haya maeneo, twende tuone namna gani tunatengeneza agency iwe wakala inayojitegemea ambayo kazi yake kubwa sasa iwe ni kupima na kuendana na mpango wa Serikali huu uliopangwa wa miaka mitano. Tukifanya hivyo, maana yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza itakuwa na wigo mpana wa kushirikiana na sekta na taasisi nyingine. Hii migogoro tunayoizungumza ya ardhi kati ya wananchi na jeshi tukiwa na wakala anayejitanua maeneo yake maana yake atafanya kazi kubwa, lakini ataendana na kasi ya sisi tunayoizungumza kwamba, kwa muda mfupi asilimia 75 ya ardhi iliyosalia iweze kupimwa ndani ya miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili. Mpango ujikite uone namna gani unaweza ukashirikisha halmashauri moja kwa moja. Pamoja na kwamba, halmashauri nyingi zina vyanzo vingi vya mapato ningetemani sana mpango upeleke maelekezo moja kwa moja kwamba, halmashauri zirudi sasa zitambue kupanga na kupima maeneo yao ya ardhi, ili angalau moja kuongeza mapato, lakini mbili kama mnavyotambua tukipanga na tukipima eneo tunapunguza migogoro, kwa kufanya hivyo maana yake tutaipunguzia Wizara mzigo.

Mheshimiwa Spika, wizara sasa inafanya kazi kubwa sana ya kutatua migogoro badala ya kuibadioisha ardhi iwe source au chanzo cha mapato kwenye Serikali yetu. Ningetamani, sasa kwasababu Mheshimiwa Waziri ameshafanya kazi kubwa sana ya kukimbizana na migogoro aende aifanye sasa ardhi iwe ni sehemu ya kuongeza mapato, ili angalau mwisho wa siku tuweze wote kufaidika na sekta hii ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa miezi nane peke yake, kuanzia mwezi wa nane mpaka sasa Wizara imeingiza zaidi ya bilioni 93. Unaweza ukaona asilimia 25 ya ardhi iliyopimwa peke yake tuna bilioni 93, lakini asilimia 77 kati ya 880,000 ya ardhi ambayo haijapimwa tujiulize leo ardhi yote tukiipima kukawa na usimamizi thabiti ambao tukawa na mawakala ambao wanashughulika moja kwa moja na wanawajibika kabisa na upimaji na urasimishaji wa ardhi, Serikali itakusanya kiasi gani cha fedha kupitia sekta ya ardhi peke yake?

Mheshimiwa Spika, lakini la pili. Nizungumzie kuhusiana na hii ni Wizara ya Ardhi pamoja na Makazi, niende sasa kuzungumzia kuhusiana na nyumba. Wabunge wengi tumekuwa tukilalamika hizi real estate developers, National Housing, TBA na watu wengine ambao wamekuwa wakijenga nyumba kwa gharama kubwa. Na wengine tulikuwa tukihoji hapa kwamba, affordability ya nyumba inapatikana wapi?

Mheshimiwa Spika, haya yote tunashindwa kufika mwisho kwasababu, hatuna housing policy. Tunazo sera za misitu na sera za nyuki na sera nyingine, lakini hatuna sera inayotudhibiti na inayotuongoza kwenye nyumba, ili mwisho wa siku National Housing wakijenga nyumba Rorya, tukisema nyumba ni ya bei nafuu iwe angalau tayari ina limit kwa sababu, tukiwa na policy maana yake tutatengeneza sheria. Akijenga Rorya nyumba ya milioni 20 tutakuwa tunajua kabisa hii kweli milioni 20 ni affordable. Akijenga Kongwa nyumba ya milioni 20 tunaweza tukamhoji, hii ni affordable nyumba ya vyumba viwili?

Mheshimiwa Spika, kwasababu, kutakuwa kuna sheria inayomuongoza yeye katika ujenzi, sasahivi hakuna sheria. Anaweza akajenga nyumba akai-term kama affordable, ukimuuliza kwetu sisi, mimi inaweza isiwe affordable milioni 50, lakini kuna mtu mwingine milioni 50 kwake ni affordable. Na kwasababu hakuna policy wala sheria inayomuongoza inakuwa ni wakati mgumu sana kujua sasa wapi Serikali inasimamia kusema affordability ya nyumba ni ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na huu utakuwa ni muongozo mzuri kwa TBA, national Housing na real estate developers wengine wote wanaofanya shughuli za kujenga maeneo. Hata Serikali kwa maana ya kupitia Wizara itakuwa na sehemu ya kujivunia, unapokwenda ukasema unaonesha nyumba za affordability’s unaonesha kulingana na uhalisia uliopo.

Mheshimiwa Spika, sio uwongo gharama za ujenzi wa kila maeneo zinatofautiana. Gharama ya ujenzi wa Rorya haiwezi kuwa sawa na gharama ya ujenzi wa Dar-es-Salaam. Kwa hiyo, maana yake ile ukii-term kwamba, huyu mtu ambaye anajenga nyumba ajenge nyumba ya affordability Rorya ya milioni 30 ukasema sio affordable atakuuliza ni sheria ipi inayomuongoza? Kwa hiyo, ningependa nichukue nafasi hii kuiomba sana Wizara, lakini kupitia Waziri wa mpango, Waziri wa Fedha, ilia one namna gani ile sheria, ile policy inaweza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho ni kwenye RERA, Real Estate Agency. Leo kuna watu sio vizuri kuwasemea, hawa tunaowaita madalali; brokers leo akiuza ardhi akiwa mtu wa kati hata kama ardhi ni ya milioni 500 akichukua commission hakuna kodi anayolipa. Lengo letu ni nini?

Mheshimiwa Spika, nilikuwa natamani sana tutengeneze Real Estate Agency, tutengeneze Real Estate Regulations ambazo zinawa-guide hawa ma-brokers na hawa ma-Real Estate Agency, ili mwisho wa siku moja itasaidia ku-regulate, lakini mbili itasaidia kukusanya kipato ambacho anashiriki kwenye kuuza kama mtu wa kati, lakini tatu itakuwa ni fursa kwao kufanya shughuli za kibiashara kwasababu, sasa watakuwa wanatambulika wako wapi. Leo ni ngumu sana kumtambua broker yupo wapi na anafanya kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Asante sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Leo nitajitahidi kidogo nichangie taratibu ili angalau wote kwa ujumla hasa Wabunge ambao tumeingia ndani ya Bunge hili kwa awamu ya kwanza hasa Wabunge vijana, baada ya hapa ni imani yangu tutakwenda wote sambamba.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nichukue nafasi kukushukuru sana wewe binafsi kwa namna unavyoliongoza hili Bunge. Nachelea kusema maneno haya kabla ukiwa ndani ya Bunge hili na ukiwa ni Spika wetu sisi kama Kiongozi wa Bunge. Ukistaafu ukiwa ndani ya Bunge hili ndiyo nipate ridhaa ya kukushukuru kwa namna unavyotuunganisha sisi Wabunge ndani na nje ya Bunge. Pia namna ambavyo unajitahidi angalau kumpa Mbunge mmoja mmoja nafasi ya kusemea yale ambayo anatakiwa ayasemee kwa mustakabali mzima wa wananchi ndani ya Jimbo lake. Mwenyezi Mungu pekee ndiyo anaweza kukulipa hili, muhimu ni kukuombea uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, nichukue nafasi kumshukuru sana Waziri Mkuu kwa namna anavyotuunganisha sisi Wabunge na Serikali kama Mtendaji Mkuu wa Serikali. Pia nichukue nafasi hii kuwashukuru Mawaziri wote kwa namna ambavyo pamoja na changamoto walizozipitia hapa katikati wiki tatu zilizopita, lakini bado wamebaki imara wanatuongoza na sasa tunakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nichukue nafasi kumshukuru Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan. Namshukuru kwa namna ambavyo ameanza, lakini namshukuru kwa namna ambavyo ameanza na anasema kazi iendelee kutekeleza na kulinda yale yaliyokuwa yanafanywa na pacha wake Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Ametuonesha sote kwamba njia bado iko pale pale. Yale waliyokuwa wanayasimamia juu ya wananchi maskini, miradi ya maendeleo, juu ya utendaji mkubwa wa Serikali kwa ujumla wake, bado ameahidi kuyasimamia na sasa tunaona kazi inakwenda vizuri. Ndugu zangu Wabunge tuendelee kumwombea mama yetu ili aendelee kufanya yale mazuri kwa kadri ambavyo Mungu ataweza kumwongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi sasa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa mujibu wa Taarifa ya Shirika la Kifedha la Kimataifa la IMF mwezi Januari, kutokana na ugonjwa wa corona IMF ilikadiria uchumi wa kidunia utashuka kwa asilimia 3.5 kulinganisha na 2.8 ya mwaka 2019, lakini Serikali yetu juu ya Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakishirikiana na pacha wake, mimi namwita pacha mama yangu, mama Samia Suluhu Hassan kwa sababu hakuna namna unaweza ukazungumza mazuri yaliyokuwa yanafanywa na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli bila kumgusa mama Samia Suluhu Hassan. Hakuna namna unaweza ukazungumza mazuri yaliyokuwa yanafanywa na hawa watu wawili bila kumtaja Waziri Mkuu kama Mtendaji Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo niseme, kwa namna ambavyo walituongoza pamoja na kushuka na kuyumba uchumi wa kidunia pato letu la Kitaifa la ndani ya nchi liliongezeka kwa asilimia 4.7. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana, Wabunge waliokuwa humu wanajua changamoto ilivyokuwa hasa baada ya tikiso hilo la ugonjwa wa corona, walibaki imara wakawasemea wananchi, sasa haya ndiyo matunda yake ambayo wanayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye hotuba hiyo hiyo ya Waziri Mkuu. Taasisi ya Utafiti wa Kilimo kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, imejipanga sasa kufanya utafiti wa kilimo wa kuangalia namna gani sasa tunaanza kubuni mbegu bora na miche bora kwa mustakabali wa wakulima wa nchi yetu. Nina mambo mawili au matatu ya kushauri.

Mheshimiwa Spika, watakapokuwa wanafanya utafiti huu, waende sasa wakatazame namna gani wanafanya utafiti kwa ngazi ya kimkoa, wilaya na halmashauri, washuke chini ngazi ya kata mpaka vijiji ndani ya nchi nzima, ili mwisho wa siku waje kulingana na jiografia ya kila eneo ni zao gani moja linafaa kulimwa kama zao la kibiashara.

Mheshimiwa Spika, pili, utafiti huo ujikite katika maeneo gani ambayo yanaweza yakalimwa na yakafanyika kilimo cha umwagiliaji na yakawanyanyua wananchi kwa ujumla kwenye kipato chao kwenye maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, tatu, waende wakafanye utafiti warudi kushauri ili angalau sasa kwenye kila wilaya tuwe tuna zao moja la kibiashara ambalo wilaya moja ikisimama inasema ndani ya wilaya yangu, zao fulani ndiyo zao la kibiashara ambalo kimsingi kama Mbunge nikitaka kuwashika mkono kuwasaidia wale wananchi mbegu nawasaidia mbegu ambayo wanajua wakiipanda kama zao la kibiashara itainua uchumi wa wananchi kwenye maeneo yao husika.

Ningetamani sana, tafiti hizi ninaporudi ndani ya Jimbo langu kwenye wilaya nione kwamba kweli hapa kwenye kata fulani ndani ya kijiji Fulani, nikiwashauri wananchi kulima pamba inastahimiliki na isiwe kwa ku-guess au kwa kuchukua yale maoni ya wakulima peke yake, badala yake, niweze kuitoa hata kwenye taarifa za utafiti huu utakaokuwa umefanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine, hapo hapo kwenye kilimo ningetamani sana, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Waziri wa Kilimo kwa namna ambavyo amejipanga kupeleka pikipiki kwa Maafisa Kilimo wote ndani ya halmashauri. Wasiishie hapo tu, ningetamani waende moja kwa moja, watengeneze mustakabali mzuri wa kuwasimamia Maafisa Kilimo ili Afisa Kilimo anapoamka asubuhi, ajue ni mashamba mangapi anakagua kwa siku, ametembelea wakulima wangapi, anategemea kupata nini kwa wale wakulima. Mwisho wa siku wampime kwa product inayopatikana kwenye ngazi ya chini kabisa, ngazi ya Kijiji, itakayoleta tija, lakini itaamsha ari mpya ya utendaji wa Maafisa Kilimo kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, natamani sana Wizara ya Kilimo pamoja na kwamba tunawapelekea vitendea kazi, tufike tutengeneze assessment nzuri ya kuwasimamia ili ninaposimama hapa kama Mbunge, yakitajwa maeneo mengine, nami nikitaja kama Rorya nataja mazao fulani ambayo wananchi wangu wameyapata kwa mwaka mmoja kwa kilimo walichokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo nizungumzie kuhusu huduma za kijamii na nitaanza na maji. Nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru sana Waziri wa Maji. Nasema ni katika Wabunge wachache ambao baada ya yeye kupata uteuzi alifanya ziara kwenye jimbo langu. Kulikuwa na Mradi wa pale Shirati, mradi ulikuwa na zaidi ya miaka 10 hautoi maji, lakini alipofika alitoa maneno ndani ya mwezi mmoja, ninavyozungumza chini ya Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi, leo kuna maji yanatoka pale. Unaweza ukaona ni historia gani ndani ya miaka 10, wananchi wale walikuwa wamesahau issue ya maji, leo wanapata maji.

Mheshimiwa Spika, sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri pale imepelea kiasi cha kama milioni 300, najua hili unaliweza, tusaidie ili tuweze sasa isiwe Shirati peke yake badala yake na majirani wote wanaozunguka kata ile waweze kupata maji kwasababu, miundombinu ipo ni kuifufua tu iweze kuwasaidia wananchi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna miradi ya maji ambayo iko ndani ya jimbo. Nichukue nafasi hii kukuomba kuna miradi ya Nyarombo, kuna miradi kwa muge pale Kyang’wame na miradi mingine ambayo kimsingi ukiwekeza fedha pale itawsaidia sana wananchi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri tusiishie mradi mmoja, turudi tuone namna gani ya kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niliwahi kusema na nitarudia tena, ili kutatua changamoto ya maji ndani ya Jimbo ni lazima twende na ule mradi mkubwa wa maji ambao upo kwenye plan ya kutoa maji Rorya kwenda Tarime. Ule mradi tunazungumzia zaidi ya kata 28 zitanufaika na ule mradi na kwa sababu, jimbo langu zaidi ya asilimia 50 changamoto kubwa ni maji ni imani yangu huu mradi ukiingia kwenye pipeline ukaanza kutekelezwa Rorya issue ya maji itakuwa ni historia. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu mkubwa sana na kwa sababu limesemwa na Waziri Mkuu ni imani yangu litafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe, ni imani yangu kipindi mlikuwa mnatunadi sisi Wabunge vijana, Wabunge ambao tumeingia kwa mara ya kwanza, mlikuwa mnazunguka wewe, Spika, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mama yangu Mama Samia Suluhu Hassan. Ulipopita kwenye jimbo langu uliniahidi namna gani tunaweza tukapata ambulance, ili angalau iweze kusaidia wale wananchi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hili tusaidie.

Mheshimiwa Spika, la kumalizia la mwisho nimalizie kuhusiana na issue ya TARURA, tuna daraja pale la Mto Mori, kwa sasa hivi kwasababu nimemuona Waziri wa TAMISEMI amekuja mama na lile daraja tunazungumzia kipenyo ambacho hakizidi hapa na Mheshimiwa Waziri alipo upana wa lile daraja. Ni imani yangu kwasababu limekuwa likizungumzwa zaidi ya miaka 10 huku nyuma sasa amekuja Waziri ambaye ni mama na ninaamini ni mchapakazi mzuri sana wanaoteseka kuvuka kwenda kutafuta huduma za kijamii, huduma za hospitali, huduma za masoko ni akinamama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na niliwahi kusema mto ule watu wamekuwa wakifariki pale. Angalia kipenyo tunachohitaji daraja ambalo tumekuwa tukiliomba kwa miaka 10 ni hapa na pale alipo Mheshimiwa Waziri. Ni imani yangu sasa amekuja mama atawasaidia hawa wamama ili lile daraja sasa badala ya kila mwaka kufanyika upembuzi yakinifu liweze kupata suluhisho la kudumu ili hawa wananchi sasa waweze kuokoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia la mwisho kabisa nizungumzie kwenye sekta ya afya kwenye upande wa Waziri.Ndani ya jimbo langu nina kata 26 ni kata tatu tu ambazo zina vituo vya afya na bahati mbaya sana Kata ya Kinesi ambayo ina Kituo cha Afya cha Kinesi kwa mujibu wa projection ya Wizara ilitakiwa ihudumie vijiji viwili peke yake. Hivi ninavyozungumza kituo kile cha afya kinahudumia zaidi ya vijiji 27 zaidi ya tarafa tatu wanapata huduma tena mpaka Kijiji Jirani cha Butiama, watu wanaokwenda pale projection yake imekuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, na kwasababu kimeshapanuka na Serikali ilitupa fedha tukakipanua zaidi ya milioni 500 hapa kilipofikia nichukue nafasi hii kumuomba sana Waziri tuone namna gani sasa tunakihamisha kwasababu, kimeshatoka kwenye vigezo vya kutoa huduma kama kituo cha afya kiende kiwe hospitali ya wilaya ili angalao tuweze kuwa na hospitali ya wilaya kwa ukanda wa chini upande wa Suba. Na hii hospitali ya wilaya ambayo Serikali ipo kwenye mchakato wa kuifungua upande wa pili maana yake tutakuwa na hospitali mbili, angalau kwa jiografia ya jimbo langu lilivyokaa tunaweza tukawasaidia sana wale wananchi kwenye sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya haya machache nichukue nafasi hii na niseme kwamba, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwanza kwa kunipa nafasi. Nianze tu kusema kwa kuchangia Wizara ambayo binafsi nimeitumikia kwa zaidi ya miaka kumi. Naweza nikasema tu kwa wepesi kwamba nimepata nafasi ya kuchangia Wizara ambayo imenilea kabla ya kuwa mwanasiasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nitumie nafasi hii kuwashukuru; wa kwanza kabisa Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu, mzee wangu, Mheshimiwa William Lukuvi; Naibu Waziri, mama yangu, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula. Pia nitumie nafasi hii kumshukuru Katibu Mkuu wa Wizara hii, dada yangu Mary Makondo na Naibu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru wafanyakazi na watendaji wote wa Wizara hii walioko ndani ya Wizara na wale ambao wanafanya shughuli kama wadau, kwa maana ya private sector. Haya mafanikio ambayo tunayaona ya Wizara hii, mimi kwa sababu nimekuwa kule natambua mchango mkubwa wa watu wote kwa ushiriki wao kwa pamoja ili kuhakikisha angalau tunaisukuma Wizara yetu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa na maeneo matatu, nafasi ikiniruhusu nitakuwa na eneo la nne la kuchangia kwenye Wizara hii. La kwanza niombe nichangie kwenye ushiriki wa private sector kwenye Wizara hii ya Ardhi. Nianze kwa kusema kwamba ili mwananchi aweze kumilikishwa ardhi, maana yake kuna vitu vitatu au vinne vinakuwa vimefanyika; cha kwanza ni lazima ardhi iwe imepangwa; maana yake katika kupangwa ndiyo kutaainisha matumizi bora ya ardhi ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha pili, ardhi lazima iwe imepimwa. Kwenye kupimwa ndiyo tunapata ukubwa wa ardhi na maboresho mengine ili mwishoni mwananchi aweze kumilikishwa ardhi ile. Kwa haya matatu tokea Uhuru, toka mwaka 1961, ardhi ambayo imepangwa mpaka sasa tunavyozungumza ni zaidi ya viwanja milioni sita peke yake. Kati hivyo milioni sita, viwanja ambavyo vimepimwa kwa maana ya kwamba sasa vinakwenda ili viweze kupewa ardhi, ni milioni 2.5. Viwanja ambavyo mpaka sasa tunazungumza kwa maana ya umiliki wa mwananchi mmoja mmoja ni milioni 1.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushiriki wa private sector kwa mwaka 2015 kwenda 2020 ndiyo tumeanza kufanya shughuli ya urasimishaji kwenye maeneo yetu. Hawa watu, hizi private sector unaweza ukaona katika hiyo milioni sita ambayo ni miaka zaidi ya sitini katika kupanga matumizi ya ardhi, wao wameweza katika urasimishaji peke yake, katika milioni sita maana yake kuna viwanja milioni 1.6, hizi private companies, makampuni ya watu binafsi wameweza kuisaidia Serikali, kwa miaka mitano.Kwa miaka mitano wameweza kupima, kupanga ardhi viwanja zaidi ya milioni 1.6. Lakini total zaidi ya miaka sitini ni zaidi ya viwanja milioni 60; hilo ni la kwanza tu peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika kupima peke yake kwa miaka mitano toka 2015 hadi 2020, zaidi ya viwanja 557,000 ambavyo vimepimwa katika kazi ya urasimishaji na hizi private companies.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa kutambua mchango huu pamoja na kwamba amezungumza yapo makampuni ambayo hayafanyi kazi vizuri, tukae nao tuone yale makampuni katika makampuni 163, yale manne ambayo mwanzoni amekuwa akiyasema hayafanyi kazi vizuri, yale 159 twende nayo. Tukiwaweka pembeni hawa tutambue kwamba hawa ndio wana kazi kubwa sana ya kutusaidia sisi. Unaweza kuona kwa miaka mitano namna gani wmaeingia katika shughuli ya kupanga, kupima na mwishoni wakaenda kwenye kurasimisha, namna ambavyo wamefanya kazi kubwa sana. Tusiwahukumu wote kwa pamoja, twende kwenye yale makampuni mengi ambayo yamefanya kazi vizuri tuweze kwenda nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa namsikiliza Mheshimiwa Waziri wa Kenya, siyo vizuri kusema lakini naomba nitoe kama mfano, alikuwa anazungumza kwa miaka mitano (2015-2020) wao kwa kutumia private sector wameweza kupima viwanja zaidi ya milioni tano. Unaweza ukaona wao wamejikita sana kutumia private sector kwa miaka mitano wamepima viwanja milioni tano. Sisi toka Uhuru bado tuna milioni sita peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiziacha hizi private companies zote tukazihukumu katika mfumo huo maana yake ni kwamba Serikali peke yake ndiyo itaingia kufanya hiyo kazi. Sisi wote tunatambua Waheshimiwa Wabunge, watumishi kwenye halmashauri hawatoshi. Kwa mfano Rorya nina mtumishi mmoja tu Afisa Ardhi. Maana yake sina Mpimaji wala sina mtu wa Mipango. Maana yake tukiwaachia wao wafanye kazi hizi hatutaweza kufikisha malengo, lakini pia hatutatimiza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika ukurasa wa 119 ambao umesema kwa muda mchache ili twende na kasi ya kupima maeneo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tutambue kwamba kampuni hizi zimetoa ajira kwa vijana wetu. Kampuni hizi ambazo leo hii tukiziacha pembeni zimekopa mikopo, tukiziacha pembeni zisifanye shughuli hii tutakuwa hatuwatendei haki na yawezekana tukaanzisha mgogoro mkubwa sana kwenye sekta ya ardhi huko mbeleni tunakoelekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni ushiriki wa halmashauri. Kwa mujibu wa sheria mwenye mamlaka ya upangaji nchi hii ni halmashauri. Hata hivyo, twende mbele turudi nyuma, kazi hii tumeona imebaki ikifanywa sana na Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi wakati tunapitisha bajeti ya Wizara ya TAMISEMI tuliona ndani mle, nilikuwa naona moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha ardhi yote inapimwa. Hata hivyo, ulikuwa ukienda kwenye bajeti kuona kwamba namna gani wanakwenda kufanya kazi hiyo kama Wizara ya TAMISEMI, hakuna fedha iliyotengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tukirudisha kwamba halmashauri peke yake kwa sababu kwa mujibu wa sheria ndiyo wana mamlaka ya kupanga na kupima wafanye kazi kwa kupitia mapato yao ya ndani, mathalani mimi Rorya nakusanya milioni 800 tu kwa mwaka. Milioni 800 nichukue asilimia 40 iende kwenye shughuli za maendeleo, bado niitoe iende kwa ajili ya kupima ardhi. Hawatakwenda na kasi tunayoizungumza ya miaka mitano ya utekelezaji wa Mpango na Ilani ya Chama chetu Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aone namna gani anaiongezea fedha Wizara ya Ardhi, hasa kwenye kipengele hiki cha upimaji ili hizi halmashauri huko chini ziingie kwenye uratibu na kutafuta namna ambayo wanaweza wakapima ardhi kuendana na kasi ya Wizara namna inavyotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuomba sana kwa sababu kama kweli dhamira yetu ni ya pamoja, kwamba angalau sasa zaidi ya eneo la kilometa za mraba 883,000 tumepima asilimia 25 peke yake, tukiiachia Wizara peke yake iendelee na huo mfumo na kwa kutoa maelekezo kwa halmashauri zitafute fedha zenyewe ziende kupima, hatutakuwa tumewatendea haki hawa wananchi wetu. Lakini pia hata Serikali bado tutakuwa tunaimba wimbo uleule na inawezekana tusifikishe malengo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni ushiriki wa Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi. Moja ya majukumu ya Tume hii ni kuwezesha mamlaka zote za upangaji wa matumizi ya ardhi katika kutambua mipango ya matumizi ya ardhi, zikiwemo halmashauri zote. Ukienda kwenye bajeti unaweza ukaona tume hii, ndiyo maana miaka yote watu wengine wamekuwa wakisema hatuoni tija ya tume hii, lakini inafanyaje kazi? Unaweza ukaona kwenye fedha ya maendeleo imetengewa bilioni 1.5 peke yake, namna gani itaweza kufanya kazi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nilikwenda mbele nikashauri kwamba kama kweli tuna mpango tumejikita kama Serikali na nchi kwa ujumla tunataka tuhakikishe tunapima ardhi kwa muda mfupi, ni lazima tutengeneze agency. Agencies kama ilivyo TBA, lazima tuwe na wakala ambaye anahusika na shughuli zote za kupanga na kupima ardhi. Ili tunapokwenda kumpangia fedha kwa muda mfupi awe na fedha nyingi lakini utekelezaji wake utakwenda kwa kasi kama ilivyo TBA ambayo ni utekelezaji wa nyumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo agencies, wapo mawakala wengi ambao wanafanya kazi kwenye maeneo mengine. Ili tuondokane na hili na ili tuendane na mpango wa miaka mitano kwa kasi, ni lazima tutafute namna ambayo tutaiongezea fedha Tume ya Taifa ya Mipango, lakini tutengeneze agency, shughuli ya kupanga na kupima ardhi isibaki kwenye kurugenzi moja tu peke yake ndani ya Wizara, tujaribu namna ya kuipanua ili iendane na kasi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba nizungumzie kuhusiana na makazi. Wabunge wengi tumekuwa tukitoa mawazo na michango mingi sana inajikita kwenye ardhi, lakini hatuendi sana kutafuta namna ambavyo tunaweza tukapata suluhu ya upande wa nyumba ili hiyo concept ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi iweze kujaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kushauri na pia niweze kuunga mkono maoni ya Kamati kwamba angalau kwa mwaka huu kama ikipendeza, Wizara iweze kukamilisha Housing Policy, Sera ambayo itaratibu shughuli za ujenzi wa nyumba. Hapa Wabunge wengi tumekuwa tukisema namna ambavyo mashirika, kwa mfano, Shirika la Nyumba na Taasisi nyingine, zinajenga nyumba kwa bei kubwa sana. Hata hivyo, leo tukiulizana humu ndani bei elekezi ya ujenzi wa nyumba, mfano Rorya, hatuitambui. Kama tukiwa na Housing Policy maana yake ni nini? Itakuwa na maelekezo ya ujenzi wa nyumba kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya na maeneo yote ili hawa wanaojenga nyumba watakuwa wanajenga kwa kutambua bei elekezi iliyopangwa kwenye maeneo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa mwaka huu angalau sasa tuwe na policy ambayo itatuongoza sote kama Taifa ili tukizungumza Sera ya Nyumba tuwe na Sera ya Nyumba kama zilivyo sera za nyuki na nyingine. Hili litakuwa ni jambo zuri ambalo kimsingi naamini yale maoni mengi ambayo tumekuwa tukiyasema hapa Bungeni namna ya ku-regulate bei za ujenzi wa nyumba itakuwa vizuri na tutakuwa tumei-control vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tumekuwa tukiongea naye mara kwa mara; kuna wananchi wangu kule walifanyiwa uthamini toka 2011 Rorya, nafikiri hili analifahamu. Niombe atakapokuwa anakuja kufanya majumuisho angalau na wao wapate jibu. Toka 2011 wamefanyiwa uthamini ili kupisha huduma za umeme, lakini mpaka leo ninavyozungumza kama ambavyo huwa nakwambia wale wananchi hawajalipwa fidia. Ni zaidi sasa ya miaka kumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, anajua kwa mujibu wa sheria baada ya miezi sita, valuation ile ilitakiwa ipitwe na wakati. Nitumie nafasi hii kumwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho alizungumzie hili ili na wao waweze kusikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze tu kwa kusema ukisikiliza toka asubuhi mijadala ya Bunge letu hili Tukufu, Bunge la Kumi na Mbili, lakini pia ukisikiliza wadau wanavyozungumzia hasa kwenye wizara na sekta nzima ya elimu; utagundua wote tunajikita kwenye sera ya elimu yetu ilivyo kwa maana sera ya mwaka 2014.

Mheshimiwa Spika, pia tunazungumzia mfumo wa utoaji wa elimu nchini namna ulivyokaa. Ukisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Rais, alivyozungumza juzi kipindi anahutubia Bunge, amezungumzia namna Serikali ilivyojikita kwenda kupitia Sera ya Elimu Nchini. Hata hivyo, sote hapa ni mashahidi huko tunapotoka kwenye majimbo, kwenye maeneo yote ya mijini, namna ambavyo wananchi na wadau mbalimbali wamekuwa wakizungumzia muundo na Sera ya Elimu ilivyokaa na namna gani ambavyo wameshauri jinsi ya kutoka hapa.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye kuchangia. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho yake, kwa sababu leo tunajikita kwenye bajeti, basi kama haitatupendeza, Bunge hili la Kumi na Mbili kwa mikutano inayofuata Mheshimiwa Waziri waende kama Serikali, waende wakaanze mchakato wa kukaa na wadau, kuona namna gani ya kuifumua Sera ya Elimu na mfumo mzima wa elimu namna ulivyokaa ili Bunge linalofuata kwa maana kikao kinachofuata iwe kama section, iwe ni sehemu maalum ya kujadili namna ya mfumo na Sera ya Elimu jinsi ilivyokaa, kwa sababu pale tutakuwa na uwanja mpana wa kujadili elimu yenyewe kama ilivyokaa Nchini Tanzania.

Mheshimiwa Spika, pili, tutakuwa tunazungumzia yale ambayo wao wamekaa na wadau angalau wamepata mawazo yote kwa ujumla ili Bunge lako Tukufu, hili Bunge la Kumi na Mbili, tutoke na maazimio namna gani tunakwenda kufumua mfumo mzima wa elimu ili tutakapokuwa tunazungumza kama Wabunge tuwe angalau tumeshiriki kwenye hili ambalo kimsingi ukitazama kila mtu anayezungumza, anazungumzia namna ya mfumo na sera jinsi ilivyokaa ya utoaji elimu nchini.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Waziri atakapokuja angalau atuahidi hiyo, kwamba angalau baada ya Bunge hili watakapokwenda waweze kuangalia namna gani tunaweza tukarudi mara ya pili kwenye vikao vinavyofuata ili tuweze kulijadili hili kwa upana wake na kwa ujumla ili tutoke na kitu kimoja kama Taifa ambacho kitakuwa na mustakabali mzuri wa kutuongoza kwenye sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maoni hayo, nirudi tu kuzungumzia masuala baadhi ndani ya jimbo langu. Nilikuwa natamani sana Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI wafanye kazi kwa ukaribu sana kwa kushirikiana. Leo ulikuwa unazungumza hapa asubuhi, kuna mahali ukienda ndani ya jimbo langu mathalan, mimi nina shule mbili ambazo moja imejengwa tangu 2005, wamejenga wananchi kuanzia msingi. Wamejichangisha wenyewe wamejenga msingi, wamejenga maboma zaidi ya matano kule, lakini namna ya kupewa idhini sasa ya kufunguliwa iwe shule, kwa maana ya kufanya usajili mpaka leo ninavyoungumza hawajapewa usajili. Kila wakienda kwa hawa mabwana ambao wanajiita watu wa ukaguzi wanawaambia bado ongezeni majengo mawili. Unaweza ukatazama maboma matano na choo na ofisi za Walimu wamejenga wananchi, hapa Wabunge wengi wanatoka maeneo ya vijijini wanajua namna inavyokuwa kwa wananchi wakati mwingine kwenye kuchangishana ili kujenga haya maboma.

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine mtu ana-sacrifice, alikuwa ana shilingi elfu moja, anaacha kwenda kununua mboga yake, kununua mahitaji yake ya ndani anachanga ili aweze kujenga ile shule. Badala yake wanapomaliza bado hatuwezi kuwapa usajili kwenye shule hii. Nini maana yake? Unakuta shule nyingine ambayo mwanafunzi anatakiwa kwenda ipo zaidi ya kilomita tano kutoka maeneo wananchi wanapoishi na wakati mwingine katikati ya maeneo hayo kati ya shule na wananchi wanapoishi kuna majaruba ya maji. Ili mwanafunzi huyu wa miaka saba au nane aweze kufika kule wakati mwingine wakati wa mvua inamlazimu kupita kwenye yale majaruba. Wananchi kwa kutambua umuhimu huo wakaamua kujenga shule yao. Leo ukiwaambia huwezi kuwasajilia na wakati ni suala la kuzungumza kati ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI tukaona namna gani tunawasaidia, tunakuwa hatuwatendei haki wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuwa ku-wind up anisaidie kwenye shule zangu hizi mbili hizi; kuna Shule ya Tacho ipo Kata ya Kirogo na Shule ya Kuruya ipo Kata ya Komuge. Hizi ni shule ambazo zimejengwa na wananchi; hivi ninavyozungumza maana yake Shule ya Kuruya hata wanafunzi hawajakwenda mwaka huu, wameambiwa hatuwezi kuwapa wanafunzi kwa sababu haijasajiliwa, lakini wamejenga wananchi kwa kuepuka huo umbali wa kusafiri muda mrefu. Niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho angalau wananchi nao wapate ahueni kutokana na nguvu zao ili mwisho wa siku wasije kuona nguvu zao zimetumika bila ya kuwa na maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili, naomba sana, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho angalau apitie yale madai mbalimbali ya Walimu. Walimu wamekuwa na manung’uniko mengi sana na naamini kabisa hili lipo ndani ya uwezo wa Waziri. Manung’uniko haya anaweza akayatatua kwa muda mfupi sana. Wananchi wengi, Walimu wengi wamekuwa wakilalamikia miundombinu yao; maeneo wanayofundishia siyo rafiki kwao, lakini wengi wamekuwa wakilalamikia madeni ya likizo na madeni mbalimbali ya malimbikizo ambayo yamelimbikizwa huku nyuma. Naamini kupitia Mheshimiwa Waziri kwa sababu tayari nimeambiwa alikuwa ni Mwalimu na alikuwa Mwalimu mzuri ataweza kuwasaidia katika hili.

Mheshimiwa Spika, pia wana madai ya likizo ambazo walikuwa nazo. Ni imani yangu Mheshimiwa Waziri atawasaidia hili. Pili, tunapofanya mabadiliko ya mtaala, tunapowapelekea Walimu niombe sana tutengeneze fedha angalau za kuwatengezea capacity building, tuwajenge ili waendane na ule mtaala mpya tunaowapelekea. Kwa sababu unapobadilisha mtaala Mwalimu bado alikuwa anajua skills za nyuma zilizopita, ukimbadilishia anapata wakati mgumu sana kuendeana na ule mtaala mpya ambao umeupeleka kipindi hicho. Tuweze kuwapa mafunzo ili waendane na mtaala mpya ambao tumewapelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa, ningependa sana kuzungumzia kuhusiana na ujenzi wa Vyuo vya VETA. Mimi Rorya nimepaka na Tarime, population ya haya majimbo mawili au hizi halmashauri ni zaidi ya watu 600,000. Hata kama bado Serikali inajipanga namna gani ya kupeleka Chuo cha VETA kila halmashauri, tuwekeeni chuo kimoja hata ukiweka pale VETA katikati ya Tarime na Rorya angalau tuweze kuwasaidia wanafunzi wote wanaotoka ndani ya halmashauri zote mbili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Chege.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nami niungane na wenzangu kwanza kabla sijaenda mbele zaidi, kumshukuru na kupongeza kazi kubwa aliyoifanya na Rais wetu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamesimama hasa wazoefu, wengi wamekuwa wakisema hii ni bajeti ya kumi; wengine ni bajeti ya tano kwa kadri ya muda wa miaka aliyokaa ndani ya Bunge. Sisi Wabunge ambao ni awamu yetu ya kwanza tunasema hii ni bajeti yetu ya kwanza. Kipekee kabisa tunakwenda tarehe 29 kwenye Majimbo yetu tukiwa tumetosheka na tumeshiba sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo kimsingi pamoja na miaka yote hii ya nyuma hayakuwa yakifanyika, sisi ndani ya Bunge hili kwa mara ya kwanza tunakwenda kwa wananchi wetu tukiamini na tukiyaona yamefanyika, angalau tunaweza tukasema nini Mheshimiwa Rais wetu ametutendea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumshukuru sana na pia kuwapongeza Mawaziri wote; Waziri Mwigulu Nchemba na Naibu wake pamoja na Wizara nzima, kwa namna ya kipekee walivyokaa humu ndani na kusikiliza maoni ya Wabunge. Leo hii ukiangalia upande wa TARURA, ni historia, haijawahi kutokea kutengwa fedha zaidi ya shilingi milioni 500 kurudi kwenye Majimbo, halafu Mbunge ukashirikishwa namna ya utendaji wa fedha ile. Haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi tangu nimeingia hapa na nimekuwa nikilia sana juu ya daraja langu la mto Mori, na nimekuwa nikisema lile daraja linaunganisha tarafa tatu kati ya tarafa nne ndani ya Jimbo, hata tarafa ya nne nayo inaingia. Leo hii ninavyochangia hapa, nakwenda tarehe 29 ndani ya Jimbo nimepewa zaidi ya shilingi milioni 950, kwa ajili ya utekelezaji wa daraja lile. Nikiongeza na shilingi milioni 500 maana yake nina 1.4 billion, ambayo inakwenda kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Jimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema inawezekana ikawa ni bajeti ya kwanza kwa awamu hii, lakini kwetu sisi Wabunge wa mara ya kwanza kiukweli imetutendea haki na imetunyanyua sana. Pia amekwenda maeneo mengi; maeneo ya maji imegusa, maeneo ya afya imegusa, kiukweli sina namna ya kusema zaidi ya kuwapongeza Mawaziri na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha muhimu ambacho nataka nichangie leo ni kumwomba Mheshimiwa Waziri, mimi napenda sana kushauri kuliko kusifia, kwa sababu naamini nikishauri vizuri ndiyo ataendelea kufanya kazi sawa sawa na ataendelea kuwepo kwenye Wizara hii na mwishoni atatengeneza historia ndani ya nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba niende ndani ya vipengele vya kumshauri ili aendelee kufanya kazi vizuri kuliko kumsifia zaidi. Naamini ameshafanya mengi mazuri, Wabunge wameshamsifia na anastahili sifa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ili kuhakikisha fedha zote za miradi ya maendeleo, tengeneza historia kuhakikisha fedha zote zilizotengwa zinakwenda kwenye majimbo na kwenye Halmashauri. Ukifanya hivi utakuwa umetengeneza historia ya miaka yote ambayo tunasema zinakwenda asilimia 10 na asilimia kadhaa kwenye bajeti za kisekta. Peleka fedha zote kwenye miradi ya kimaendeleo. Amini ninachokwambia Mheshimiwa Waziri, tukirudi hapa mwakani utakuwa umetengeneza historia nzuri sana, kwa sababu miradi mingi itakwenda kutekelezwa na mwishoni wewe ndiye utakayepata sifa hizi kwa wananchi wetu ndani ya maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, napenda sana kuchangia kwenye Property Tax (Kodi ya Majengo). Nishawahi kusema nachangia kama mdau. Ningependa nichangie maeneo matatu na ninaamini kwamba Mheshimiwa Waziri utalichukua hili, utakuja kulitolea ufafanuzi. Unakuta kwenye kiwanja kimoja, mimi mmiliki wa nyumba nimejenga nyumba tatu kwenye kile kiwanja au nyumba nne ndani ya kiwanja; nimeweka Luku moja peke yake. Maana yake mwishoni nikilipa Luku, nalipia nyumba moja. Sheria inavyosema, ni kila property; nyumba iliyopo kwenye kiwanja kimoja, kama ni property Na. 5 zile nyumba tatu zote kwa sasa zinalipia kodi ya jengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ikiwa Luku ni moja kwenye eneo lile, lazima angalau utakapokuja Mheshimiwa Waziri utuambie, zile nyumba mbili zinazosalia katika tatu kwenye kiwanja kimoja, ni mpango gani mkakati uliopagwa ili angalau zote ziwe accommodated kwenye Luku moja ya ukusanyaji wa eneo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye Property Tax kuna haya majengo, tuchukulie nyumba za ibada ambazo kimsingi kwenye sheria ya sasa hazikuwa zinalipa kodi. Kuna wazee wa miaka 65 na kuendelea, umri wao umezidi walikuwa hawalipo hii Property Tax. Namna gani sasa unaenda kuwa-accommodate? Kwa mfano, majengo haya ya ibada yana Luku: Je, hawatahusika kwenye Luku zao kulipia Property Tax? Nafikiri hii na yenyewe kwenye mkanganyiko Mheshimiwa Waziri utaiweka sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna majengo ambayo yanalipiwa na wapangaji. Mwenye nyumba amejenga, Luku inalipiwa na mpangaji: Je ni namna gani ambavyo tutawa- accommodate wale wapangaji ambao wananunua Luku kwenye majengo waliyopanga, wakati Property Tax inatakakiwa kulipiwa na mmiliki wa eneo lile (owners)? Haya mambo matatu Mheshimiwa Waziri naamini ukiyaweka sawa sawa hakuna kinachoshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nichangie sana kulingana na Mahusiano ya Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo ya Taifa, Mheshimiwa Waziri tutakubaliana, ili maeneo yote kuwe kuna uchumi imara kwa wananchi, cha kwanza kabisa, lazima kuwe na stability, lazima kuwe na usalama wa wale wananchi ili kufanya biashara vizuri. Nitatolea mfano ndani ya eneo langu mimi la Rorya. Mimi shughuli zangu za kiuchumi ni tatu; moja, ni kilimo; pili ni uvuvi na tatu ni ufugaji. Kilimo sina shida kwa sababu naamini kwenye bajeti ya kisekta Waziri amenitengea fedha na nitakwenda kutekeleza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zinabaki shughuli mbili za kiuchumi ili wananchi wale ndani ya Jimbo waweze kwendana na kasi ya mpango wa Taifa ndani wa miaka mitano. Tuchukulie mfano suala la uvuvi. Mheshimiwa Waziri mimi kule, napenda nilizungumze kwa Waziri wa Bajeti, Waziri wa Fedha na pia Waziri wa Mambo ya Ndani na ikibidi Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kuna wizi mkubwa sana unafanyika kwenye maeneo ya maziwani. Wavuvi wanapokwenda kuvua na ndiyo shughuli kubwa ya kiuchumi. Ndani ya Jimbo langu Mheshimiwa Waziri, asilimia 77 nimezungukwa na ziwa. Unaweza kuona, ili uchumi wa wananchi wangu uweze kuendelea, ni lazima wafanye shughuli ya uvuvi, lakini haufanyiki sawa sawa. Wanapokwenda kuvua, wanakutana na shughuli kubwa sana ya kupigwa na kunyang’anywa zana zao za uvuvi. Nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ikibidi Waziri Mkuu atusaidie sana kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya shughuli mbili hizo nilizosema, ya tatu ni ya ufugaji. Mheshimiwa Waziri, leo ufugaji haupo stable. Kule ndani ya Jimbo langu, kila siku ndani ya Halmashauri ya Rorya isipopita siku mbili, siku tatu lazima utakuta wananchi wameibiwa mifugo; na lengo kubwa la uanzishwaji wa Halmashauri zile mbili, mpaka ikafikia sehemu ikatengenezwa Polisi ili kuhudumia maeneo haya yote mawili, haipo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninavyozungumza, jana wananchi toka asubuhi mpaka saa 8.00 wanazunguka kutafuta mifugo yao ambayo imeibiwa. Uanzishwaji wa kanda maalum ndani ya ile Halmashauri kwa maana ya Tarime na Rorya, ilikuwa ni kuhakikisha angalau kuna usalama kwanza wa hizi Halmashauri mbili, lakini nisikufiche ningetamani sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alichukulie serious suala hili, kwa sababu kule imekuwa ni kero kubwa sana. Leo Mheshimiwa Rais akienda au Waziri Mkuu, amini ninachokwambia, bango la kwanza atakalokutana nalo ni suala la wizi wa mfugo. Imekuwa ni suala la kihistoria, limekuwa la miaka mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa unyenyekevu mkubwa, watafute mbinu za kukomesha hili suala ili angalau wale wakazi wa Rorya ambao kimsingi wameamua kuhamasika kwenye kuingia kwenye shughuli za ufugaji, wafuge mifugo yao, kama ni ng’ombe ikiwa ni salama kabisa bila kuingiliana na huu msuguano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwa sababu bila ya kufanyika, haya ndiyo yana mahusiano na mwingiliano wa ukuaji wa kiuchumi wa wananchi wangu. Kama utakutana na disturbance kwa maeneo haya mawili, maana yake kila mwaka watakuwa wanakwenda na bado watakuwa wanarudishwa nyuma, kwa sababu mtu anajikakamua, anaanza kufuga ng’ombe wawilia au watatu; na mwingine wale ng’ombe ndiyo anaotumia kulipa ada ya watoto wake. Mwingine wale ndiyo wanazitumia angalau akipata shida kuuza na kuingia kwenye shughuli zake za kiuchumi na kujiendesha katika maisha yake. Halafu haifiki mwisho, wale ng’ombe wanakuja kukwapuliwa, anaanza upya yule mwananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana sana, Wizara ya Mambo ya Ndani, kwa sababu nimeshafuatilia kwa muda mrefu, walichukue walione ni namna gani angalau wanalitatua ili wananchi nao waweze kujikwamua kwenye suala hilo la kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nami niungane na mchangiaji aliyetoka kuchangia, kwanza kukushukuru wewe binafsi kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili na ni mara yangu ya kwanza wananchi wamenipa ridhaa ya kuongoza ndani ya Jimbo la Rorya, Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe binafsi kwa namna ambavyo, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza nimeona namna unavyoliongoza Bunge, lakini imetupa faraja hasa Wabunge wengi wapya; kwa namna ambavyo tulikuwa tunakuona nje na hakika wewe ni kiongozi bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kabla sijasahau Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja hotuba zote mbili za Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; hotuba ya kwanza ilikuwa ya kufunga Bunge na ile aliyoitoa Novemba ya kufungua Bunge. Naunga mkono hoja hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, nami niseme tu kwamba hotuba ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilikuwa na mwelekeo chanya, ni hotuba ambayo ina matumaini mazuri kuanzia ngazi zote na sekta zote za kibiashara na kiuchumi na shughuli nyingi za ukuaji na ustawi wa jamii kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaenda kuchangia kwenye baadhi ya maeneo ambayo nimeona angalau niweze kuchangia katika kuboresha na katika utekelezaji wake utakavyokuwa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu katika hotuba yake ukurasa wa 34 na 35 amezungumzia namna ambavyo Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano chini ya Chama chetu Cha Mapinduzi, ilifanya kazi kubwa sana katika uboreshaji na uinuaji wa sekta ya maji. Nichukue nafasi hii kwa moyo wa dhati sana kumshukuru Waziri mhusika wa Wizara hii. Naweza kusema, kwa muda mfupi wa miezi hii mitatu, mimi nimepata ridhaa ya kutembelewa na Waziri wa Maji. Kwa kweli nichukue nafasi hii kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya. Ni imani yangu alikuwa anatekeleza yale ambayo Mheshimiwa Rais amemwagiza na ndiyo haya ambayo wananchi wetu wanatarajia kuyaona.

Mheshimiwa Spika, jimbo langu kwa asilimia 77 limezungukwa na maji; asilimia 23 peke yake ndiyo eneo la nchi kavu ambalo wananchi wanalima na kufanya shughuli nyingine za kiuchumi. Kwa miaka yetu mitano kwa chama chetu na Mheshimiwa Rais wetu, alituletea zaidi ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji. Nilikuwa naiona hapa kwenye hotuba yake hapa ameisema, hizi shilingi trilioni 2.2 ambazo zimeletwa kuinua na kuboresha sekta ya maji, sisi katika Jimbo letu ni miongoni mwa Majimbo ambayo yamepokea fedha hizi, lakini niseme tu kwamba haikutumika vizuri.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alipokuja kufanya ziara yake, ndiyo maana nimesema nianze kumpongeza, kuna maelekezo aliyatoa kutokana na namna fedha hizi zilivyotumika. Niendelee tu kumwomba Mheshimiwa Waziri aendelee kukazia hapo, kwa sababu ndani ya Jimbo langu, nina changamoto kubwa sana ya maji. Unaweza kuona hiyo asilima 77 ambayo inazungukwa na maji, lakini hatuna mradi mkubwa unaotokana na Ziwa Victoria, asilimia iliyobaki 23 ndiyo maeneo ya nchi kavu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitupa fedha ili angalau fedha hizi ziweze kuinua na kuwasaidia wananchi wanyonge hasa akina mama lakini haijatumika sawasawa. Nachukua nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri aendelee kukazia wakandarasi wote ambao walichukua hizi fedha za umma ili angalau waweze kurudi sasa kuweza kutimiza na kumalizia hii miradi.

Mheshimiwa Spika, unaweza ukakuta mkandarasi ametekeleza mradi kwa asilimia sitini lakini amelipwa asilimia mia moja na ameuacha ule mradi hauna maji. Amelipwa zaidi ya shilingi bilioni moja na ushee. Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kukazia ili tuweze kulipata hili.

Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake amezungumza namna tulivyofanya kwa miaka yetu mitano na matarajio yake ya miaka mitano kwenye sekta ya afya. Mimi nishauri kidogo kwenye Wizara yetu hii ya Afya, ndani ya jimbo langu mimi nina vituo vinne tu vya afya lakini kiukweli kwa population na wingi wa watu ulivyo, vituo vya afya hivi havitoshi na unaweza ukakuta kituo kimoja cha afya kinahudumia zaidi ya vijiji 27. Kwa malengo mazuri ya Mheshimiwa Rais na naamini namna Waziri wa Afya anavyofanya kazi kwa muda toka amechaguliwa namwomba aitazame Rorya katika kipengele hiki cha upande wa sekta ya afya.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu unaweza ukakuta kituo kimoja cha afya kinahudumia zaidi ya vijiji 27, kina kata zaidi ya nane lakini ndani ya hicho kituo cha afya unakuta bado hakijapata huduma ya ambulance, wakati mwingine kuna changamoto kubwa sana kunapokuwa na wagonjwa kumtoa kwenye kata moja kumpeleka kwenye hospitali ya wilaya au kumsafirisha kwenda kwenye hospitali ya mkoa. Kwa hiyo, naomba na lenyewe hili ili kuendana na yale mazuri ambayo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameyazungumza kwenye hotuba yake tuyaboreshe sasa tuendane na kasi hiyo katika sekta hii ya afya.

Mheshimiwa Spika, la tatu, Mheshimiwa Rais amegusia vizuri sana upande wa barabara na sisi wote ni mashahidi kwa kazi kubwa iliyofanyika miaka mitano iliyopita. Tuna barabara ambayo imezungumzwa kwenye Ilani toka mwaka 2010, 2015, 2020, barabara ya kutoka Mika - Shirati, lakini inanyooka mpaka Kilongo kule mpakani. Barabara hii ina umuhimu wa aina mbili, moja ni barabara ambayo inainua uchumi ndani ya Jimbo letu la Rorya, lakini ni barabara ambayo kiusalama kwa sababu sisi tuko mpakani inaweza ikarahisisha shughuli za kiusalama ndani ya Jimbo kwa sababu ni sehemu ambayo tunapatikana kwenye mpaka wetu wa Kenya, Uganda pamoja na Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumuomba Mheshimiwa Waziri husika, hii barabara kwa kipindi hiki ambacho imetajwa kwenye Ilani iingizwe kwenye utekelezaji angalau wa kupatiwa lami ili wananchi wa maeneo yale tuweze kuinua uchumi wao. Pili kama nilivyosema itakuwa ni sehemu nzuri sasa pia ya kuboresha upande wa ulinzi na usalama ndani ya jimbo.

Mheshimiwa Spika, nne, nizungumzie kidogo kuhusiana na TARURA. Pamoja na mambo mazuri na makubwa aliyofanya Mheshimiwa Rais, ndani ya Jimbo langu mimi la Rorya kuna shida kubwa sana ya barabara, hizi barabara za kuunganisha kata na kata na tarafa na tarafa ambapo ziko chini ya TARURA. Hivi navyozungumza kuna baadhi ya maeneo hayapitiki. Bado naamini kwa sababu ni mwanzo mzuri ambapo Serikali yetu ndiyo imeanza kufanya kazi chini ya Waziri Jafo, aone namna anavyoweza kutusaidia kwenye hii sekta hii ili angalau sasa tuendane na yale mazuri yaliyotajwa kwenye Ilani yetu hii na kwenye hotuba yetu ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Spika, mwisho nizungumzie kuhusiana na wavuvi. Kwenye ukurasa wa 19, Mheshimiwa Rais amezungumza vizuri sana juu ya maboresho ya kodi na tozo mbalimbali zinazotolewa upande wa wenzetu wavuvi. Wabunge wote ambao wanatoka Kanda ya Ziwa watakuwa mashahidi, ilikuwa ni kazi kubwa sana kwa mwaka jana 2020 kupata kura kutoka kwa wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa sababu Mheshimiwa Rais ametoa mwongozo mzuri sana kuhusiana na kupitia tozo zote ambazo zinawagusa wavuvi, Wizara kwanza ikae na hawa wavuvi wawape elimu na ipitie tozo hizo. Mimi nadhani si busara nzuri sana unapomkuta mvuvi anafanya biashara haramu ukamchomea mtumbwi wake kwa sababu wakati mwingine unakuta ule mtumbwi yeye mwenyewe siyo wa kwake, ameazima au amekodisha kutoka kwa mtu mwingine. Kwa hiyo, si tu kumrudisha yule mvuvi nyuma bali unamuathiri hata yule mmiliki halali wa ule mtumbwi.

Mheshimiwa Spika, wale wavuvi ndani ya jimbo na Kanda ya Ziwa wamekuwa wanalalamika kwa muda mrefu sana. Naiomba Wizara kipindi hiki turudi sasa tuone namna gani tunaweza tukapitia tozo lakini hata maboresho ya sheria ili angalau wale wenzetu wanaofanya shughuli za uvuvi wasiendelee kila siku kulalamika kwamba wanaonewa.

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba inawezekana wapo kweli wanaofanya biashara haramu na hawa sina maana kwamba tunatakiwa tuwatetee lakini wako ambao wananunua na wanapewa risiti halali kutoka kwenye maduka halali na wanakwenda kufanya biashara ile ya uvuvi. Mvuvi anakutwa ziwani ana risiti zote, ana mtego au ana nyenzo ile ile aliyonunua lakini wale watu wanamwambia kwamba wewe mtumbwi wako hauna uhalali wowote.

Mheshimiwa Spika, natamani sana Mheshimiwa Waziri kwenye kipengele hiki, maeneo yote ya Kanda ya Ziwa wakae wazungumze na hawa wavuvi na cha kwanza kabisa tutoe elimu. Kabla ya kumkamata uvuvi na kumpa kesi ya uhujumu uchumi, ningetamani sana tukae nao tuwaelimishe kwa sababu naamini mlinzi na mtetezi wa kwanza wa hizo maliasili ni mvuvi mwenyewe. Sisi Wabunge ambao tunatoka maeneo ya uvuvi, tuko tayari kutoa ushirikiano, wapewe elimu ili tuone namna gani tunanusuru hayo maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nizungumze kidogo kuhusiana na rasilimali zetu. Moja kati ya kazi ya Mbunge ni pamoja na kutetea na kulinda maslahi ya wananchi na Serikali yetu kwa ujumla wake. Nilisema hili kwa sababu naamini Mheshimiwa Jafo ni mtendaji mzuri na anafanya kazi na anafuatilia sana utendaji na kulinda rasilimali za nchi.

Mheshimiwa Spika, kuna gari letu sisi ndani ya Halmashauri ya Rorya. Tulipewa gari hili na Serikali yetu kwa upendo kabisa toka mwaka 2009 lakini leo limekuwa na mkanganyiko mkubwa sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Jafari, Mbunge wa Rorya.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza kupitia kitabu cha Mpango tunaojadili wa mwaka mmoja na miaka mitano ukurasa wa 13; nipende tu kusema ndugu zangu Wabunge wote twende pamoja, pamoja na kwamba tunajadili Mpango ambao uko mbele yetu, tujaribu kukumbushana tu kupitia ukurasa wa 13 yale mazuri ambayo ameyafanya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ili tunapokwenda kujadili twende sambamba pasipo kupotosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, baadhi tu peke yake idadi ya kaya imeongezeka, zilizounganishiwa umeme zaidi ya 14.9% ndani ya miaka mitano (2015 mpaka 2020 Desemba). Vijiji vilivyounganishiwa umeme kutoka vijiji 2000 mpaka vijiji 10,000. Kuongezeka kwa kiwango cha uandikishaji, juzi Waheshimiwa Wabunge tulikuwa tunajadili hapa namna idadi ya wanafunzi walivyoongezeka mpaka madarasa yamepungua na mengine mengi ambayo ameyafanya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kwa hiyo tunapokwenda kujadili Mpango uliopo mbele yetu tunatakiwa tujadili yale mazuri ambayo yako mbele, lakini tujaribu kuainisha changamoto, namna gani sasa Waziri wa Mipango, Waziri aliyewasilisha Mpango huu aone namna gani sasa anatoka hapa ili kwenda mbele kuyafanyia kazi yale mawazo yote ya Waheshimiwa Wabunge bila kubagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia hilo niende kujadili Jimbo langu la Rorya. Leo asubuhi tulikuwa tunajadili hapa Mheshimiwa Waziri alikuwa anajibu kuhusiana na hoja ya maji. Ndani ya Jimbo la Rorya, zaidi ya 77% imezungukwa na maji maana yake shughuli kubwa ya kiuchumi ukiacha shughuli ya kijamii ya maji, ni uvuvi. Mpango unasema kuna mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa zaidi ya dola milioni 500 ambao unatoka kwenye Jimbo la Rorya unakwenda Tarime, lakini kijiji ambacho unatoka jimbo ambalo unatoka huo mradi halijawekwa kwenye mpango wa utekelezaji wa hayo maji. Kwa hiyo, naomba sana, tunapojadili na tunapopanga mipango tuangalie namna gani inagusa wananchi kwenye maeneo ambao mradi unatoka ili kwenda maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ushauri wangu kwenye upande wa viwanda, natamani sana nimshauri Mheshimiwa Waziri upande wa viwanda, viwanda hivi ninavyovizungumza yawezekana visiwe vina mashiko sana hasa maeneo ya vijijini. Ningetamani sana Serikali ije na mpango wa namna gani ambayo itaanzisha viwanda ambavyo zinashiriki moja kwa moja kwenye shughuli za maendeleo za kiuchumi za kule ndani ya halmashauri, ikibidi waainishe mazao ya kibiashara ambayo yanatolewa kwenye halmashauri husika ili Serikali iwe na mpango wa kiwanda kulingana na zao la kibiashara linalozalishwa kwenye halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu ukitoa tathmini ongezeko la viwanda, leo tunasema kuna ongezeko la viwanda zaidi ya 8,400, yawezekana kwenye maeneo mengine hicho kiwanda hakipo. Kwa hiyo, yawezekana ukisema kuna ongezeko la viwanda kuna baadhi ya maeneo haliwagusi moja kwa moja wale wananchi, maana yake watakuwa wanashabikia ule mpango, lakini hauwagusi wale wananchi wa chini kabisa ambao tunawawakilisha. Ningetamani kwenye hii mipango Serikali izingatie sana unapopanga mipango ya kuongezeka viwanda, basi viwanda viwe moja kwa moja kwenye maeneo ambako kuna uzalishaji kwa wananchi hasa ukizingatia yale mazao wanayozalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nizungumzie sana upande wa uvuvi, mimi kama nilivyosema 77% ya jimbo langu inazungukwa na maji, shughuli kubwa inayofanyika kule ni uvuvi, lakini ndani ya miaka hii mitano iliyopita nyinyi wote mtakuwa mashahidi, wavuvi hawa hawana furaha kwenye maeneo yao. Ningetamani sana kama nilivyosema mara ya kwanza, Serikali ije na mpango wa namna gani itakaa na hawa wavuvi, ianishe na ione ni changamoto gani kubwa inawasumbua, kama shida ni nyenzo zile za uvuvi, wenyewe wanasema wanaponunua hakuna shida, ikija huku inakuwa na shida, Serikali ione namna gani inavyowasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningeomba Serikali kupitia Ofisi ya DPP iende ikaone wale wavuvi wadogo wadogo waliokamatwa kwa miaka mitano kwa makosa ya uhujumu uchumi ili iweze kuona namna gani inaweza ikawasaidia ili kuwaondoa, kwa sababu kuna wengine kimsingi mwingine hana hata fedha, lakini amekamatwa kwa makosa ya uhujumu uchumi. Kwa hiyo tuone namna gani kupitia Ofisi ya DPP inaweza ikawaona hawa watu na ikawasaidia kwa maana hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda umeisha Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa maoni yangu kwenye mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali na hatimae mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa wa mwaka 2023/2024. Kwa sababu ya muda tu na kwa sababu ninayo mengi ambayo ningetamani na mimi nishauri ili yaweze kuingizwa kwenye utekelezaji wa mpango na hatimaye yaingizwe kwenye bajeti ili tutakapokuwa tunajadili mwakani basi mengi ambayo yanawagusa wananchi kwa ujumla wake Waziri wa Fedha pamoja na Serikali kwa ujumla wake, wawe wameyaweka kwenye bajeti ili angalao yalete ahueni kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu nichukue nafasi hii kwanza kupitia kidogo taarifa ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na mtikisiko wa uchumi wa kidunia. Pamoja na mambo mengine ametaja sababu mbili ambazo ndiyo zinasababisha sasa mtikisiko wa kiuchumi kidunia, moja ni vita inayoendelea Ukraine, lakini la pili amezungumzia mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka tu nishauri kwenye hili la mabadiliko ya tabianchi ukisoma vizuri taarifa ya Mheshimiwa Waziri, niombe tu alipe mkazo kwa sababu, mabadiliko ya tabianchi sit u kwamba, yanakwenda kuathiri uchumi wa nchi, lakini pia yana madhara katika afya ya kibinadamu kwa ujumla wake. Kwa hiyo, nilikuwa natamani sana lipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanadamu tunaishi kutokana na ikolojia inayotuzunguka, lakini sote tunakubaliana kwamba, ikolojia ile imeanza kuathirika kutokana na shughili nyingi za kibinadamu, miti imeanza kukatwa na maeneo mengi sana yameanza kuathirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, hivi ninavyozungumza nchi wanachama wa Jumuiya ya Dunia wako Misri wanajadili juu ya mabadiliko ya tabianchi. Ningeomba sana Mheshimiwa Waziri uone namna ya kulijazilisha vizuri, namna ambavyo Serikali tumejipanga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kabla ya mwaka 2030 na kuendelea ili angalao isije ikafika huko tukakutana na changamozo hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema ya kwangu yatakuwa yale ambayo yanawagusa wananchi ambayo ningetamani yaingizwe kwenye bajeti. Kwanza, Mheshimiwa Waziri ningetamani sana bajeti ya mwakani pamoja na mpango wa bajeti hiyo ambao unakuja mwakani ili angalau tuweze kuujadili na kuupitisha, ni vema Wizara yako ingejipanga namna ya kuboresha na kuongeza mapato ya Halmashauri, hasa Halmashauri ambazo ziko pembezoni mwa mipaka ya nchi, lakini Halmashauri ambazo mapato yake yako chini ya bilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani mpango wako na bajeti ujikite sana tutakapokuja kujadili uone namna ambavyo unakwenda kuzisaidia hizi Halmashauri ili angalao zisiendelee kutegemea vyanzo vilevile kila mwaka. Mfano nitatoa, zipo Halmashauri ambazo zinategemea vyanzo viwili tu vya mapato. Ningeshauri sana kwenye Wizara yako kwa sababu huwa mnatenga fedha za miradi ya kimkakati na nimekuwa nilisema sana hili kwa Mheshimiwa Waziri. Muone hizi fedha za miradi ya kimkakati mpeleke kwenye Halmashauri ambazo mapato yake yako chini ya bilioni moja, lakini mapato yake hayako stable. Tungetamani kwenye bajeti ya mwakani inayokuja tupate angalao kujua fedha za miradi ya kimkakati zinazokwenda kwenye Halmashauri ambazo mapato yake hayako stable mnakwenda kuzisaidiaje? Kwa sababu, huko mbele haya mapato mwisho wake utafika yatakwisha, maana yake hizi Halmashauri hazitaweza kujiendesha. Kwa hiyo, ningetamani kwenye mpango na bajeti yako Mheshimiwa Waziri uone namna ya kulifanya hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye mpango na bajeti tutakayokuja kuijadili mwakani, Mheshimiwa Waziri kwa sababu tunaishi na watu, ipo fedha ambayo inatolewa na Halmashauri ya asilimia 10 kwa ajili ya akinamama, vijana na watoto. Fedha hizi zinatolewa kulingana na kiasi ambacho Halmashauri zinakusanya. Zipo Halmashauri ambazo kiwango cha fedha wanachokusanya ni kidogo sana kiasi kwamba, kinachokwenda kwa vijana kwa ajili ya mikopo na akinamama hakitoshelezi. Ningetamani kupitia mpango wako uje utuambie nini mnajiandaa, hasa Halmashauri ambazo zinakusanya fedha kidogo kwa ujumla kwa vijana wa watu 10 unakuta mfano fedha wanayopewa ni Milioni Moja au Milioni Mbili ambayo haitoshi hata kujiendesha kwenye kikundi hicho ambacho kipo. Mnao mpango gani kama Wizara na Serikali kusaidia hizi Halmashauri ili fedha inayokwenda angalao kikundi kimoja kikipata fedha kiweze ku-sustain?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika hilo ningetamani kwenye mpango na bajeti yako Mheshimiwa Waziri, ni vyema ukaona namna ya kupitia utaratibu na sheria za mfumo huu wote ambao unatoa fedha zinazokwenda kwenye miradi kwenye hivi vikundi vya vijana, akinamama na walemavu. Ningetamani mpango wako na bajeti hiyo ije iseme namna mlivyojipanga kama Serikali kupitia upya namna ya utoaji wa fedha, namna ya kupata vile vikundi, namna ya pesa zinavyopata kwa sababu, hawa ndiyo wananchi ambao wametuzunguka huko, hawa ndiyo wangetamani kwenye bajeti ya mwakani waone namna ambavyo inakwenda kushughulika na changamoto zao kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika hilo ningetamani kwenye mpango na bajeti yako Mheshimiwa Waziri utuambie ni namna gani mnakwenda kujenga kama Serikali, barabara za lami kwenye maeneo ambayo yanaunganisha kati ya nchi na nchi, kwenye maeneo ya miradi ya kimkakati ambayo kimsingi yanaweza yakainua uchumi wa nchi, pia kwenye Mkoa na Mkoa? Ningetamani kwenye bajeti yako pamoja na mapendekezo utakayokujanayo mwakani ili mtuambie kwenye Halmashuri ambazo kimsingi zinagusana nchi na nchi angalao wapate kidogo barabara za lami ili ku- sustain na kuibua uchumi wa nchi ile pamoja na zile Halmashauri na hatimaye ninyi kama Serikali naamini mtakuwa mmepata mapato mengi sana, ningetamani hilo pia Mheshimiwa Waziri uje utwambie ni namna gani ambavyo mmejipanga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri katika hilo, uone namna ambavyo unaweza ukapitia Sheria za Manunuzi na utekelezaji wa maeneo mbalimbali. Sheria za Manunuzi ambazo ziko TARURA, RUWASA na maeneo mengine kwa sababu, naweza nikakutolea mfano Mheshimiwa Waziri; tumepitisha bajeti mwezi wa Saba, leo tunazungumza ni mwezi wa Novemba tunakwenda mwezi wa Disemba, bajeti ya fedha, fedha za mipango tulizopitisha kutekelezwa kuanzia mwezi wa Saba mpaka leo hakuna Mkandarasi site, hakuna kazi, maana yake ni nini? Hizi Taasisi zote bado zipo kwenye utaratibu wa kimanunuzi. Ningetamani kupitia ofisi yako upande wa fiscal policy au upande ambao wanahusika na mambo nya sera na sheria uone ni wapi ambapo tunakwama? Ni kwa nini tunapitisha bajeti mwezi Julai, lakini utekelezaji wake unakwenda zaidi ya miezi Minne katika utekelezaji wake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni kwamba, hata unaposema umeona kwenye bajeti yako wanasema angalao mwakani kuanzia Januari mpaka Juni, tunategemea uchumi wetu ukue kwa asilimia 5.3. Unaweza usikue kwa sababu, inawezekana mvua hizi zinazokuja barabara nyingi zitakuwa hazijatengenezwa. Hivi ninavyozungumza na wewe maeneo mengi umeme bado haujafika sawasawa, ninavyozungumza na wewe maeneo mengi bado miradi ya maji tuliyopitisha bajeti haijaanza kutekelezwa, hawa wote ukiwauliza ni utaratibu wa kimanunuzi ambao kimsingi ndiyo unasababisha hizi shughuli ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani kwenye mpango na bajeti ili mje muone namna gani ambavyo mnaweza mkapitia, ili fedha inapotoka ya Serikali inakwenda moja kwa moja kwa mwananchi na isichukue muda mrefu na ikaleta maswali mengi sana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningetamani nilizungumze na tulilisema hapa Mheshimiwa Waziri na umelisema kwenye hotuba yako ni pamoja na usimamizi wa fedha mnazopeleka. Umesema kwenye hotuba yako kwamba, utaimarisha na kupeleka fedha kuimarisha simamizi hizi, ofisi ndogondogo za Ukaguzi za CAG ambazo ziko kwenye Halmashauri. Mimi nikuongezee lingine, pamoja na mipango yako na bajeti tafuta namna ambavyo utaongeza usimamizi kwa kuwalipa fedha Wasimamizi Wakuu wa fedha za miradi huko ni Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye mpango na bajeti inayokuja mwakani ningetamani na penyewe uone namna hawa wasimamizi wa kwanza ambao leo unapeleka zaidi ya Bilioni Mbili kwenye Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, msimamizi wa kwanza wa kuhakikisha fedha inatumika ni Diwani. Sasa lazima angalao kwa kuwa unaandaa fedha za kwenda kulipa namna ya usimamizi - CAG, angalia namna ambavyo unaweza ukaweka mpango mkakati mzuri wa kuwalipa wale Madiwani ili kazi zao ziweze kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri ni kuhusiana na ulinzi na usalama. Mimi niko kule Rorya na maeneo mengine, ningetamani sana kwenye mpango wa Serikali pamoja na bajeti muone namna ambavyo mnaweza mkapeleka fedha kwenye maeneo ya Maziwa na Bahari Kuu kuimarisha ulinzi na usalama wa maeneo yale. Niliwahi kutoa mfano hapa tunalinda sana maeneo ya maliasili na ndiyo maana tumeweka Jeshi Usu, ukienda kwenye madini kule wanalinda, lakini ukienda maeneo ya Maziwa na Baharini huku hakuna ulinzi wa rasilimali samaki na hakuna ulinzi wa wavuvi wanaovua maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano na niliwahi kusema hapa, ukienda Rorya leo wavuvi kila siku wanalia kupigwa na kunyang’anywa nyavu zao, kupigwa na kunyang’anywa samaki, hakuna ulinzi. Kinachohitajika kule ni feasibility ya ulinzi angalao Askari waweze kuonekana, lakini hawapo. Nini ambacho ningeshauri katika hili kwenye maeneo ya Maziwa na Bahari, kwenye mpango wako na kwenye bajeti Mheshimiwa Waziri, uone namna unaweza kupeleka fedha kwa mfano maeneo ya Kanda ya Ziwa yote na Mkoa wa Mara ambao wanaathirika na hii shughuli ya kupigwa na kunyang’anywa samaki. Peleka fedha watu hawa waweze kununua mashine, ipo mashine pale Rorya ambayo ukubwa wake na utumiaji wa mafuta ni mkubwa sana kwa siku wanatumia zaidi ya lita 600 hawawezi Askari wale kuimarisha ulinzi maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa wakiiomba Serikali iweze kuwasaidia kupata mashine ndogo za watt power 40 mpaka 50 ili waweze kuratibu ulinzi wa maeneo yale ya Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Spika, wavuvi wanapigwa sana, watu wanafilisika kule. Ningetamani kwenye ulinzi na usalama wa maeneo ya bahari Mheshimiwa Waziri nione namna mlivyojipanga kuimarisha rasilimali samaki kwenye maeneo ya maziwa ili angalao kuondokana na hili ambalo limekuwa likienda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningelisema hapa ni kuhusiana na kilimo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa namna anavyokwenda, lakini ningetamani pia hii block farming ambayo inaendelea ingeenda na kasi kwenye maeneo mengi ya nchi, pia iende sambamba na hili suala linalokwenda la utambuzi wa udongo ambao unafaa kwa aina fulani ya zao, hasa kwa Mikoa ambayo haina mazao ya kimkakati na mazao ya kibiashara, ikiwemo na Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili likienda haraka litatusaidia sisi kulingana na yale mabadiliko ya tabianchi ambayo kimsingi yanatuathiri maeneo mengi na ndiyo yanatusababishia baadae ukame na njaa, kutakuwa hakuna chakula. Block farming inaweza ikatusaidia hasa tukiendana na kilimo cha irrigation kwenye maeneo mengi kwa kutambua mazao ya kibiashara kwenye Mikoa ambayo haina, ili kukingana na kuepukana na hili linalokwenda. Ningetamani sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha mtakapokuja kutenga fedha muendane kwanza na haya yote mliyoyapamga, lakini mwakani muende mtenge fedha kwenye Mikoa ambayo haina mazao ya miradi ya kimkakati ili kuweza kuimarisha na kuwapa fedha ili waweze kubuni, hasa Mkoa wa Mara ambao kimsingi umekuwa ukiathirika kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie moja kama muda utakuwa unaniruhusu. Lipo suala la utekelezaji wa umeme wa REA na hapa tumekuwa tukijibiwa sana, mimi ningetamani sana kwa baadae kuna umuhimu wa kuja kupitia kanuni ya majibu ambayo kimsingi huwa yanatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa umeme wa REA leo ninavyozungumza ambao kimsingi unakwamisha shughuli na bajeti tuliyopitisha, tusipolisema leo maana yake hata mwakani litakwamisha shughuli na bajeti tunayopitisha. Wakandarasi maeneo mengi hawako site au hawatekelezi, lakini Serikali imekuwa ikisema kufikia mwezi wa 12 tutamalizana na hili zoezi, haliwezekani Mheshimiwa Waziri. Mimi ningetamani kama linawezekana adhabu yoyote itolewe kwangu mimi itakapofika mwezi wa 12 kama Wakandarasi watakuwa wamemaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano, Vijiji 13 Mkandarasi ametekeleza Kijiji kimoja tu ndiyo umeme unawaka, ana mwaka mmoja na nusu. Leo tumebakiza mwezi mmoja ukisimama ndani ya Bunge ukasema ndani ya mwezi mmoja utamaliza Vijiji 11 haileti maana. Mimi ninaomba sana fedha hizi za miradi, hizi ambazo zinachochea ukuaji wa uchumi kwenye umeme na maji zitoke kwa wakati, lakini usimamizi wake uweze kuwa imara sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukuwe nafasi hii kwanza kukushukuru wewe mwenyewe binafsi na niseme tu niendelee kukutia moyo niseme uendelee kufanya kazi ukiamini Wabunge wengi wako nyumba yako wala usiwe na hofu na yoyote yanayoendelea mtaani au kwenye mitandao ya kijamii, tuko nyuma yako na tunaelewa nini unafanya kwa wakati huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuchangia wizara hii nichukuwe nafasi kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji Wizara nzima pamoja na wadendaji wa RUWASA, mheshimiwa Waziri pongezi zote tunazokupa tunakupa kwasababu unatimu nzuri kwa maana ya wizara nzima yenyewe namna ilivyofanya kuanzia Katibu Mkuu na watumishi wote, lakini na RUWASA kwa utekelezaji mzuri wanaoufanya hasa pale unapokuwa unapokuwa umetoa maagizo.

Mheshimiwa Spika, nichukuwe nafasi hii kukushukuru binafsi kwa miradi mbalimbali ambayo umenisaidia, mradi wa Shilati niliwahi kusema ulikuwa na Zaidi ya miaka 15 hauna maji, umefanya Ziara ya siku moja ukatamka neno hivi ninavyozungumza tayari wananchi wale wana maji, nikuombe sasa kwa sehemu iliyosalia ulimalizie fedha walioomba milioni 300 ili angalau maji yaweze kusambaa ndani ya kata yote, lakini ikibidi na kata vijiji jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ukuhishia hapo uliweza kunisaidia pia kwenye vijiji vingine kwa mfano kijiji cha Mwame, Kata ya Komuge, umenisaidia Nyarombo, umenisaidia Sudi, umenisaidia Nyehara na vijiji vingine, niendelee kusema kwa namna unavyokwenda sisi vijana tunafarijika sana. Sasa niseme tu usife moyo, ninachoweza kushauri kwa miaka hii inayokwenda ili angalau tuendelee sisi kukuunga mkono na kwenda na wewe sambamba nitakuwa na ushauri kwa maeneo matatu.

Mheshimiwa Spika, moja nikuombe sana Mheshimiwa Waziri jitahidi sana kuboresha RUWASA kwa maana wakala ya maji vijijini, na katika kuboresha huko wajengee uwezo ili waweze kupata watumishi wa kutosha kwa sababu nilikuwa najaribu kuangalia hotuba yako, kwenye fedha za maelendeleo peke yake maji vijijini Tanzania nzima umetenga Zaidi ya bilioni 360, kwa Mkoa wangu wa Mara umeniwekea Zaidi ya bilioni 21, tazama halmashauri peke yangu Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini yako umenipa Zaidi ya bilioni
5.3 ambayo inatakiwa itekelezwe kwa mwaka mmoja wa bajeti.

Mheshimiwa Spika, lakini fedha yote hii kama kuna mtumishi mmoja tu ndani ya halmshauri kwa maana ndiyo engineer utaona namna gani fedha bilioni 35.3 inakwenda kusimamiwa na mtumishi mmoja ambaye inakwenda kusimamiwa na mtumishi mmoja ambaye unaweza kusema ni engineer wa wilaya. Kesho yake naamini, Mheshimiwa Waziri kama usipo wapa uwezo hawa watu wakuongeza watumishi utapita kwenye ziara yawezekana huyu asiwe na wakati mzuri. Niombe sana tuwajengee uwezo watu wa RUWASA ili waweze kuongeza watumishi wa kutosha waweze kukusaidia kusimamia fedha hizi nyingi ambazo mmezitenga kwa ajili kwenye upande wa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili nikuombe sana fedha hizi ambazo zimetengwa ziende kwa wakati kwasababu leo nitaondoka naenda kusema na ninasema kwa uwazi kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri kupitia Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan wilaya yangu imepata bilioni 5.3 kwa ajili ya miradi ya maji, ikienda kwa wakati na ikafika sahihi hautakuwa na ugomvi wowote na Mamlaka za usimamizi wa Maji kote hata hao watu wa RUWASA, kwasababu zitakuwa zinakwenda kwa wakati na wanatimiza yale ambayo wananchi wanahitaji haya mawili, Mheshimiwa Waziri ukiyasimamia vizuri ni Imani yangu, pongezi zote wanazozitoa ndani ya Bunge hili utaendelea kupata kwa miaka yote, kwasababu utawajengea uwezo miradi itakwenda kwa usahihi na kwa muda ambao umepangwa, niamini sana niendelee kukuomba sana fedha hizi ambazo zimetenga, hasa Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, niombe sana Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Maji fedha hizi mtusaidie sana ambazo zimetengwa kwenye bajeti hii tutengeneze historia kwa mara ya kwanza kwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maji kwenda yote kwa asilimia 100 hasa kwenye miradi ya maji hasa mkizingatia Rais Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ni mama ambaye kimsingi na yeye angetamani wamama wote ndani na vijiji vyote ambao kimsingi wanateseka sana na kero ya maji kwa miaka hii michache waweze kuondokana na kero hii ningeshukuru sana kama haya na hii bajeti tuliyoitenga itakwenda kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, nizungumzie sana hii miji 28. Mheshimiwa Waziri nikupongeza sana mwanzoni ilikuwa inazungumzwa 16 lakini leo ndani ya Bunge hili unazungumzia miji 28. Nikuombe usipunguze hata mji mmoja, nenda nayo miji 28 kama ilivyosema kwa sababu tayari ndani ya Bunge hili tunaondoka tukijua miji 28 inakwenda kupata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndani ya jimbo langu nina vijiji 87 lakini vijiji vyenye maji ni 12 peke yake. Vijiji ambavyo vina miradi ni 23; vijiji 52 ndani ya jimbo langu havina mradi wowote wa maji safi na salama. Kwa hiyo, mradi huu wa miji 28 leo hii ukipitisha bomba lile linalotoka Rorya kwenda Tarime maana yake zaidi ya kata 11 zinakwenda kunufanika na mradi huu. Ndiyo mradi ambao sisi watu wa Rorya tunategemea kwa muda mfupi utakuwa umetatua kero kubwa na kwa eneo kubwa. Coverage ya mradi huu ni kubwa sana kuliko hata ukichimba kisima kimoja kimoja kwenye kila Kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye huu mradi wa miji hii, naomba Waziri uipe kipaumbele sana hasa Rorya na Tarime. Watu wa Tarime hawana ziwa, ili wapate maji wanategemea maji ya Ziwa Victoria ambayo kimsingi yanatokea Rorya, Kijiji cha Nyamagaro. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ukisimamia hili ni imani yangu kwa muda mfupi ndani ya miji hii miradi ya maji itakuwa mizuri na utakuwa umetatua kero kwa asilimia kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, Waziri amesema kuna watu wanapita kukagua miradi iliyotekelezewa na Serikali kwa miaka mitano iliyopita kwa kutumia wakandarasi na inawezekana wasiwe wakandarasi lakini fedha zilizokwenda kwa ajili ya miradi ya maji haikutumika sawasawa. Naomba Waziri atilie mkazo suala hili kwa sababu kama fedha zinaendelea kwenda kulekule ambako hakujatengenezwa mfumo mzuri wa kusimamia miradi hii na kuna fedha ilikwenda haikutumika inavyotakiwa maana yake hata hii inayopelekwa yawezekana isitumike vizuri. Naomba sana ukamilishe suala hili ili kila kitu kiende sawasawa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru nichukue nafasi hii kukushukuru kabisa kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara hii nyeti. Lakini pia nachukua nafasi hii kumshukuru Waziri, Naibu Waziri Pamoja na watendaji wote wa Wizara wakitambua kwamba wanaongoza Wizara ambayo ni mtambuka ni Wizara ambayo katika sekta ni Wizara toka tunapata uhuru tunazungumzia Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni Wizara ambayo ukitaja sekta zingine zote unaweza ukasema zimeanza baada ya Wizara hii ya Kilimo. Lakini nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya changamoto ni nyingi wakati mwingine kuzimaliza kwa muda mfupi yawezekana isiwe kazi ya rahisi lakini tuna imani kwa sababu sasa tumempata Waziri kijana ambaye ni Professor, tumempaka Naibu Waziri kijana ni imani yangu sasa mtakwenda kubadilisha kilimo kutoka kwenye nadharia sasa iende kwenye vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba kwa miaka yote toka uhuru hakuna ambacho hakijawahi kuandikwa kwa maana ya research kama utafiti kwenye zao lolote la kilimo nchi hii. Kazi kwenu sasa kwenda kutumia research zilizoandikwa na wataalamu hao ili sasa kutumia nafasi zenu za vijana muiondoe nadhania hii ya kilimo ambayo imekuwa ikizungumzwa na wananchi na Pamoja na Waheshimiwa Wabunge iende kuwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, lakini Wizara hii haiwezi kufanya mazuri kama haina fedha angalia tazama bajeti tunayoijadili sasa ni bilioni 2.9 kama haitaenda yote maana yake haya tunayozungumza ukiacha nje ya mifumo hii ambayo Wabunge wamekuwa wakilalamikia, maana yake bado haiwezi kufanya vizuri vile ambavyo wananchi wanahitaji. Nichukue nafasi hii kuiomba sana Serikali hii bilioni 2.9 iliyoombwa na Wizara hii wapeni yote ili angalau tunaporudi bajeti ya mwakani tuweze sasa kushikana mashati sawasawa tukiwa tumewapa fedha sasa za utekelezaji na uendelezaji wa utekelezaji wa Wizaa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie maeneo yangu mawili ndani ya jimbo langu eneo la kwanza ni eneo la kilimo cha umwagiliaji mradi wa Chereche nilikuwa naangalia taarifa ya Mheshimiwa Waziri hotuba yake na randama sijaona ikitajwa. Chereche ni mradi ambao wa umwagiliaji una heka Zaidi ya 350 unahudumia zaidi ya wananchi ambao walikuwa wakifanya shughuli pale Zaidi ya watu 300 na kitu.

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa umwagiliaji umeanza toka mwaka 2002, lakini toka mwaka 2018 umesimama una miaka minne tunakwenda miaka mitano umesimama na haufanyikazi yoyote unaweza ukaona wananchi waliokuwa wanafanya shughuli za kiuchumi pale mpaka leo wanaenda wapi. Lakini nimeangalia kwenye bajeti humu nilikuwa naangalia kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri haupo tuna mradi wa umwagiliaji upo Kijiji cha Rabol Kata ya Rabol, Tarafa ya Loimbo una zaidi ya heka 250 kwa mara ya kwanza Serikali iliamua kufufua mwaka 2012 kwenda mwaka 2013 wakaitengea bajeti 2016 kwamba sasa tunakwenda kuufufua huu mradi ili uwanufaishe wananchi wa maeneo yale Kijiji cha Loimbo. Hivi ninavyozungumza mpaka leo ile bajeti 2016 haikwenda kwenye utekelezaji nimeangalia kwenye bajeti ya Serikali bajeti ya Mheshimiwa Waziri haimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna mradi wa umwagiliaji Ochuna wananchi wanalima mpunga kule ni mradi wa umwagiliaji ambao wananchi masikini ya Mungu wanahangaika lakini wanachangamoto zao za miundombinu ndani ya ule mradi haipo ni imani yangu Mheshimiwa Waziri atakapokuwa amesimama kesho kufanya majumuisho aniambie na kwa sababu nimekwisha zungumza naye kabla ya hapa haina haja ya sisi tena kurudi kule na wakati ninaye Waziri ndani ya Bunge hili. Atoe tamko na atoe maelekezo wale watendaji wote ambao wamesahau kuingiza kwenye bajeti ili angalau sasa nitakaporudi na mimi Jimboni nirudi nikijua hawa wananchi wanatokaje hapa na wanakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushuru kwa kunipa nafasi. Kabla sijasahau kwanza nianze kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya.

Mheshimiwa Spika, nami niendelee kusisitiza kwamba Giza Cable Industry huyu mkandarasi ambaye amepewa kazi katika Wilaya nne za Tarime, Serengeti, Butiama pamoja na Rorya, mkandarasi huyu kama alivyosema Mheshimiwa Sagini hapatikani kwenye simu. Sisi kama wakazi wa Mkoa wa Mara kwenye hizi wilaya nne tunapata wasiwasi kwa sababu kama wakandarasi wengine wamekwishaanza kufanya survey lakini yeye mpaka sasa hapatikani. Leo asubuhi nilikuwa naogea na Injini wa Wilaya yangu Rorya anasema hajaona mkandarasi yeyote maeneno yale. Kwa hiyo, kama Bwana Giza ananisikia popote alipo basi ni vema tukafanya mawasiliano ili angalau atuondoe kwenye adha hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba nishauri mambo mawili ambayo yako ndani ya jimbo langu. La kwanza ni kushukuru kwa kazi kubwa iliyofanyika katika Jimbo langu la Rorya, ndani ya vijiji 87 vijiji 73 vyote tayari vina umeme wa REA. Ni imani yangu kwa Vijiji 14 vilivyobaki vya Kanyamsana, Kabache, Nyamusi, Masike, Nyabikondo, Burere, Wamaya, Nyabihwe, Nyihara, Bugendi, Busanga, Ulio, Tai pamoja na Lalanya navyo vitapata umeme. Ni imani yangu utekelezaji wa REA awamu hii vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme.

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu Mheshimiwa Waziri atatusaidia pia kutatua kero kwenye maeneo ambayo tayari ndani ya vijiji 73 hivi ambavyo umeme umefika ili angalau maeneo mengine waweze kupata umeme. Kwa sababu hiyo Mheshimiwa Waziri nishauari maeneo mawili, ni kweli umeme umefika kwenye vijiji 73, lakini kwenye kijiji kuna kaya au wakazi wako 20 kwenye center ya Kijiji, unaweza ukaona kwamba kama wako watu 20 ni nyumba tano tu ndizo zinazopata umeme lakini nyumba 15 hazina umeme. Sasa kwa status ya Rorya jinsi ilivyo katika hizo 15 bado unakuta watu 10 tayari wamelipia umeme zaidi ya mwaka mmoja lakini hawajaunganishiwa umeme. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba wananchi wengi pamoja na kwamba tunawaambiwa ndani ya kijiji chenu wana umeme hawaoni tija ya umeme ule.

Mheshimiwa Spika, atakuambia tu Mheshimiwa Mbunge ninachoona ni nguzo mimi nimelipia nina miaka miwili au mwaka mmoja sijapata huo umeme. Zile kaya tano zilizosalia wanashindwa kulipia kwa sababu wanaona wenzao mpaka sasa hawajatatuliwa tatizo lolote la umeme. Nikuombe Mheshimiwa Waziri kipindi unakimbizana na namna ya kutatua changamoto ya vijiji vilivyosalia nchi nzima tupeleke fedha TANESCO ili wakimbizane kumalizi hivi vijiji vilivyosalia ili hawa watu 15 waliosalia na waweze kupata umeme katikati ya kijiji kwenye maeneo ya centre. Kwa kufanya hivyo utakuwa umetatua tatizo zima la eneo lile.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili nizungumzie kuhusu kukatikakatika kwa umeme. Mimi kwangu ni changamoto kubwa sana, naweza nikawa naongoza kwenye Mkoa wa Mara kwa Jimbo la Rorya kukatika umeme. Changamoto kubwa ni ukubwa wa kilometa za mraba ambazo TANESCO Halmashauri ya Wilaya ya Rorya wanazohudumia. Watu hawa wanahudumia zaidi ya kilometa 344, kutokea Nyamongo mpaka ndani ya jimbo zima ni zaidi ya kilometa 344.

Mheshimiwa Spika, lakini ukifuatilia historia ya umeme ule nguzo zina zaidi ya miaka 40 kwa hiyo zimechoka na kuchakaa. Pamoja na kwamba utakuja kutoa majumuisho na kutoa mwelekeo wa nchi nzima ni kwa nini umeme unakatikatika lakini solution kubwa ni kupeleka fedha za kuboresha miundombinu kwenye maeneo haya. Hizi nguzo za umeme zina miaka 40 sasa kwenye maeneo ambayo kuna chemchem zinaoza halafu zinadondoka ndiyo maana mpaka leo ninavyozungumza kuna maeneo ndani ya jimbo langu watu wana siku tatu hawana umeme. Hivi ninavyozungumza kuna Kijiji cha Chabakenye toka jana mchana hakuna umeme wowote lakini ukifuatilia unakuta miundombinu hii imechakaa.

Mheshimiwa Spika, kwa namna yoyote hata kama Mheshimiwa Waziri atafanya marekebisho ya watendaji mimi niseme kwamba inawezekana hawana wakawa hawana kosa. Kikubwa ambacho anaweza kufanya ni kupeleka fedha ya miundombinu hasa fedha maintenance kwenye maeneo haya ambayo umeme unakatika mara kwa mara. Pamoja na kwamba atakuja na suluhisho lingine lakini aamini nachosema umeme huu kwa maeneo haya nguzo zina muda mrefu sana toka zimeoteshwa. Akitatua hilo pamoja na mengine atakayokuja nao naamini kwenye halmashauri hizi ambazo ziko pembezoni atakuwa amewaokoa kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)