Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khamis Hamza Khamis (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, sasa nichukue fursa hii, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa Mbingu na Ardhi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nichukue fursa hii tena kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako hili Tukufu kwa kuwa wametoa michango mizuri, michango ambayo kitaalam tunaita very constructive ideas, michango ambayo ni michango jengefu. Michango ambayo sisi tutaichukua tunakwenda kuifanyia kazi ili kuona namna ambavyo tunaboresha utoaji wa huduma au tunaboresha Wizara yetu au tunaboresha vyombo vyetu katika kuhudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo sasa nianze kutoa majibu ya baadhi ya michango ambayo Waheshimiwa wameichangia lakini pia wameulizia ndani yake wametaka kujua baadhi ya mambo.

Mheshimiwa Spika, kuna michango mbalimbali ambayo imetolewa, kiujumla ni kwamba kuna Kituo cha Polisi cha Ng’ambo Station Zanzibar kimezungumzwa hiki, kiukweli kituo hiki ni cha zamani maana binafsi ninafungua macho yangu kile kituo nakiona vile vile. Kama Serikali tunao wajibu wa kukifanyia maboresho lakini kwa wanaokifahamu kituo kile hatuwezi kukipanua kwasababu ni kituo ambacho kimezungukwa na barabara. Pande zote ukizitazama kimezungukwa na barabara. Kwa hiyo, kikubwa ambacho tunakifanya ni kwamba kama Serikali tunakwenda kukiboresha zaidi katika utoaji wa huduma ili kiweze kutoa huduma zaidi lakini sio kukitanua na kukijenga upya kwa mazingira kilipo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna hoja nyingine ilikuja hapa Mheshimiwa Omar Ali Omar alizungumzia suala la nyumba za Polisi Finya. Ni kweli nyumba zile nimewahi kufika, nimetembelea pale, nimeona hatua ambayo nyumba zile zimefikia na nimeona waliniambia idadi ya fedha ambazo zinatakiwa ili kumaliza nyumba zile.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee Serikali ilitoa maelekezo na tukalichukua lile jambo na tayari tumeshatoa maelekezo kunakohusika kwamba tuweze kupatiwa zile fedha ili tukamalize kituo kile. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba asiwe na wasiwasi nyumba zile zitamalizwa na askari wa eneo lile na maeneo ya Jirani watapata mahali pazuri pa kuweza kukaa na familia zao.

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Maida Hamad naye ameeleza suala zima la upungufu wa wafanyakazi wa Jeshi la Polisi hasa katika kisiwa cha Pemba. Ni kweli upuingufu upo lakini kama ambavyo mara nyingi huwa nazungumza hasa nikisimama hapa huwa naelekeza kwamba upatikanaji wa ajira una some procedures lazima zifuatwe, sio kwamba tukurupuke tu tuajiri kwasababu tuna uhitaji, kuna mambo lazima tuyafuate, lazima tupate kibali cha kuajiri ambacho tunakiendea mbio sasa hivi kukipata, lazima tuangalie bajeti tuliyonayo, lazima tuangalie uhitaji wa hawa wanaotaka kuajiriwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kikubwa nimuambie Mheshimiwa ndani ya bajeti hii tunategemea kuajiri askari wasiopungua 400 ambao hao sasa wataenda ku-cover hizo nafasi. Mheshimiwa asiwe na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lingine, limezungumzwa suala la OC, amesema kwamba OC ziende moja kwa moja vituoni. Utaratibu umeshawekwa wazi hasa kwenye PGO kwamba fungu alinalo mwenye Fungu ni IGP na RPC. Kwa hiyo, hilo la kusema kwamba ziende vituoni moja kwa moja hapa inabidi tuje tukae tena tujue namna ya kufanya lakini utaratibu uko wazi hivyo kwamba linatoka kwa IGP, linakuja RPC, RPC ana-distribute kwenye OCD’s na vituoni.

Mheshimiwa Spika, kingine Mheshimiwa Ravia Idarus Faina na yeye amezungumzia suala la je, ni lini sasa Serikali itajenga ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Zanzibar? Hili tuseme kwamba tunalichukua kwa umuhimu wa kipekee sana. Ni jambo ambalo tumeliona na limetugusa na tumeona sasa tuna haja ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa asiwe na wasiwasi na hilo, tunakwenda kujenga ofisi nzuri ya kisasa ambayo itakuwa ni Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri akienda atafikia pale, Naibu Waziri na shughuli nyingine za Kiwizara zitafanyika hapo. Hilo asiwe na wasiwasi.

Mheshimiwa Spika, lakini akaja na hoja ya PGO, akasema kuna baadhi ya vipengele vinaepukwa, kuna baadhi ya taratibu hazifuatwi, maeneo hayafuatwi. Ni vyema Mheshimiwa angejaribu kueleza yale maeneo ambayo anahisi kwamba hayakufuatwa na sisi tukajua namna ya kuyaweka sawa kwasababu ukituambia haifuatwi na wakati taratibu zipo, zinafuatwa zote tunakuwa hatujui tufanye nini lakini vizuri tungepata kujua yale maeneo ambayo bwana kwenye maeneo fulani na fulani hapa PGO imekengeuka kidogo haikufuatwa.

Mheshimiwa Spika, kingine kulikuwa kuna jambo la zile tunaita fire clubs. Hapa nataka niseme katika suala hili la zimamoto hatuwezi kuzima moto kwa uzoefu tu kwamba tunauzima moto lazima kuna mambo automatic tuelezane. Kwanza tuwaeleze wananchi kwamba wachukue tahadhari katika suala la ku-control majanga.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, sisi tuna wajibu wa kutoa elimu kwa jamii kitu ambacho tunakifanya mara kwa mara katika Jeshi letu la Zimamoto lakini cha tatu ambacho tunakifanya na tayari tumeshakifanya, hivi karibuni tulifanya makubaliano pale, tulisaini makubaliano baina ya Jeshi hili la Zimamoto na wale watu wa scout ili sasa waweze kutufikishia ujumbe hata mashuleni na maeneo mengine ili hata likitokeza tatizo au janga lolote la moto waweze kuli- save wakati Jeshi la Zimamoto wanakuja kuhami hilo.


Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika hili tumejipanga vizuri na tuwaambie tu wananchi kwamba tutaendeleza kutoa elimu kwasababu kitu kimoja kikubwa ambacho kitawafanya watu waweze ku-control haya majanga ni taaluma ambayo tuanenda kuwapa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna jambo jingine ambalo limeulizwa. Mheshimiwa Faina ameuliza suala zima la Ofisi ya NIDA Wilaya ya Kusini. Ofisi ipo! Tunachokiangalia sisi ni utoaji wa huduma. Hatuangalii kuwepo kwa ofisi kwasababu inawezekana Ofisi ikawa ipo kubwa ya ghorofa lakini huduma zikawa hazipatikani. Lakini sisi huduma inatolewa, ukienda Makunduchi Ofisi ipo pamoja na kwamba ni ndogo lakini huduma zinatolewa na wananchi wanapata huduma kwa wakati uliopangwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kikubwa niwaambie tu kwamba Ofisi zinatoa lakini kikubwa ambacho tumeshakubaliana kwamba tunakwenda kujenga Ofisi ya Kisasa ya NIDA, Serikali itajenga pale Kusini Makunduchi ili wananchi waweze kupata huduma za upatikanaji wa vitambulisho kwa muda ambao umekusudiwa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwaambie tu kwamba wasiwe na wasiwasi tumeshajipanga vizuri, mwanzoni ama mwishoni mwa mwezi wa tano tunategemea maeneo mengi ya Tanzania watu watakuwa tayari wameshapata vitambulisho vya NIDA.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna changamoto nyingine zimeelezwa za magari ya Polisi, wengine hawana, wengine zipo lakini mbovu, wengine hazina maringi, wengine hawana kabisa. Pia kumezungumzwa masuala ya upandishwaji vyeo, hayo yote ni mambo ambayo tuko nayo na tunaenda kuyafanyia kazi. Kikubwa ninachowaomba Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono bajeti hii ili ipite ikatatue changamoto zinazokabili baadhi ya vyombo vyetu ambavyo mmeviorodhesha.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru.