Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jacquline Andrew Kainja (6 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JACKLINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru kwa kunipatia nafasi hii niweze kuchangia Bunge lako tukufu Bunge la Kumi na Mbili. Awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia kuwepo humu kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Napenda niweze kushukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini na kunipa nafasi yakuwa mwakilishi wa wanawake kutoka Tabora, pia niweze kuwashukuru akinamama wa Mkoa wa Tabora kwa kuniamini kuwa mwakilishi wao na mimi nawahahidi sitawahangusha. (Makofi)

Vilevile naomba nitowe shukrani zangu za dhati kwa familia yangu mume wangu mpenzi Mr. Seleman Sungi pamoja na watoto wangu watatu Tarik Seleman Sungi, Lion Seleman Sungi na Cairo Selemani Sungi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa shukrani hizo naomba name nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais. Hotuba nzuri nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri iliyojaa matumaini kwa wananchi watanzania wote lakini niende moja kwa moja eneo la afya, niipongeze wizara ya afya kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuboresha sekta ya afya, tukiangalia miundombinu wachangiaji wa mwanzo waliona hilo na mimi pia naona nigusie hapo.

Mheshimiwa Spika, kuboresha miundombinu katika zahanati na vituo vya afya kutoka zahanati 1,198 na vituo 487; tunaona hayo ni maendeleo ndani ya miaka mitano iliyopita. Lakini vilevile niipongeze wizara ya afya na Serikali kwa kuweza kupunguza vifo vya akinamama wajawazito wakati wa kujifungua kutoka 11,000 kwa mwaka 2015 na mpaka kufikia 3,000 tunaona kwa miaka mitano tayari tumeokoa wa mama idadi 8,000 kwa mwaka. Kwa hiyo niombe Serikali kwa idadi hii iliyobaki Mungu akitujalia Inshallah hotuba ijayo tuweze kupata asilimia sifuri ya vifo vya akinamama wajawazito wakati wa kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naipongeza Wizara ya Afya kwa namna ambavyo wameweza kuboresha na kuweza Hospitali za Kanda za Rufaa kama Bugando, KCMC, Muhimbili, Benjamin Mkapa pamoja na Mbeya Refferal Hospital.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naiomba Serikali iweze kuangalia kanda ya Magharibi yenye Mikoa ya Katavi, Kigoma pomoja na Tabora. Jambo najuwa mpango upo basi Serikali iweze kutusaidia kwa haraka ili wananchi hawa wa Kanda hii ya Magharibi waweze kunufaika na wao kutokana na adha wanaoyopata ya hospitali ya rufaa kutoka Mkoa wa Katavi aende Mwanza basi iwepo kwenye Kanda yao ya Magharibi.

Naomba niongelee suala la maji napenda niipongeze Serikali na Wizara ya Maji kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kumtua ndoo mwanamke wa kitandania na nimpongeze Mheshimiwa Rais tarehe 30 Januari, 2021 ameweza kuzindua Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria, Mkoa wa Tabora. Lakini nilikuwa naiomba Wizara husika iweze kuangalia kwenye Wilaya na maeneo ambayo bado maji ya mradi huu wa Ziwa Victoria haujafika kama Urambo, Sikonge, Kaliua, Jimbo la Igalula ili wanawake hawa/akinamama wa Kinyamwezi waweze kupumzika na ndoo kichwani.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo naomba niunge mkono hoja naunga asilimia zote nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi ili niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa. Kwa kuanza kuchangia moja kwa moja niende kugusia upande wa upatikanaji na uongezaji wa uchumi katika Taifa letu kutokana na mpango huu na hatutoweza kukwepa suala la kuongeza uchumi wetu bila kuongelea wafanyabiashara. Suala la wafanyabiashara na Serikali, kuweka mahusiano mazuri kati ya mfanyabiashara na Serikali, lakini vile vile kuna malalamiko kati ya wafanyabiashara, haya tuweze kuyaangalia kama Serikali, kwamba mfanyabiashara anakuwa na kodi nyingi, lakini vilevile makadirio yake ni makubwa sana ambayo wakati mwingine hayana uhalisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nitaenda kuongelea kwamba tunafanyeje, kwa hiyo naanza kwamba na hizo ambazo ni kama changamoto. Pamoja na hayo lakini mfanyabiashara huyu anapata changamoto nyingize za wachuuzi ambao wanafanya ujasiriamali au tunaita Machinga’s mbele ya maeneo ya wafanyabiashara hawa. Simaanishi kwamba Wamachinga au wachuuzi watolewe, lakini kuwepo na utaratibu mzuri kama Serikali kuweza kuwezesha hawa vijana ambao ni wengi wanajikita kuweka biashara barabarani kuna wengine ni akinamama wana-risk hata maisha yao kwa kukaa karibu kabisa na barabara, wakati mwingine magari yanapita na vijana wetu ambao ni wengi wameenda kujiajiri kwenye kazi ya uchuuzi ambayo ukiiangalia haina tija kwenye Taifa kwa namna nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nishauri Serikali iweze kuangalia ni namna gani tunaweza tukaboresha upande wa kilimo kama ambavyo Wabunge wengine waliopita wameongelea suala la kilimo kwa aina mbalimbali ili tuweze kuwa na kilimo ambacho kina tija na kinamnyanyua mwananchi mkulima wa chini kabisa huyu aweze kuwa na maisha mazuri. Hawa vijana wote na akinamama watatoka huku kwenye kuchuuza hizi biashara ambazo hazina tija kwa Taifa na kwenda kuwekeza kwenye kilimo ambacho kitakuwa na maslahi katika maisha hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna suala la hizi kodi zinakuwa ni nyingi; kuna biashara inaweza ikawa biashara moja lakini mtu ana kodi kama kumi. Ukiziangalia zile kodi zinalandana, kuna kodi ya mabango, biashara bila matangazo ambayo tunataka huyu mfanyabiashara tupate kodi kutoka kwake ni sawasawa na bure. Naongelea mabango yale mfanyabiashara anaweka kwenye duka lake au kwenye jengo lake. Yale mabango yapo upande wa TRA, kwa hilo bango mfanyabiashara anatakiwa achajiwe, bado napata shida kidogo, kama mfanyabiashara huyu anatangaza tu biashara yake labda Neema Saluni ili mtu aweze kujua mle ndani kunatolewa hiyo huduma, aingie ili kupata ile huduma nayo anatakiwa akatwe kodi. Sasa tunategemea huyu mfanyabiashara atangaze vipi ile biashara yake ili aweze kutuletea sisi kodi. Kwa hiyo kama Serikali, naomba iweze kuangalia upande huu, kuna vitu vingine ni vya kuondoa tu ili sasa huyu mfanyabiashara ajitangaze vizuri na aweze kufanya biashara yake na kodi ije kama kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Serikali iweze kuangalia sheria za kodi ambazo pengine inakuwa ni changamoto kubwa sana kwa wafanyabishara hawa. Hata Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, shemeji yangu, naomba aweze kufuatilia Bodi ya Rufaa za Kodi ambako kule kuna malalamiko mengi ya wafanyabaishara hawa, wakiwa wanalalamika ili wakate rufaa kwa ajili ya zile kodi zimekuwa tofauti na jinsi ambavyo walitakiwa kukadiriwa. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kwenda kuiangalia bodi hii ili aweze kujua malalamiko haya ya wafanyabiashara ni yepi ili tuone je, tunayaboresha kwa namna gani ili sasa kama Taifa tuweze kuangalia upande huo wa wafanyabiashara tunaweza tukapata vipi kuinua uchumi wetu na pato la Taifa, maana wafanyabiashara bado ni kiini kizuri katika ukuaji wa uchumi wetu. Vilevile naomba pia Serikali iweze kuangalia investors ambao ni wa nje na wa ndani, waweze kukaa kuangalia ni namna gani wataweza kuweka mazingira mazuri ili watu waweze ku-invest, watu waweze kuwekeza katika nchi yetu, kuangalia sheria kanuni na taratibu ambazo zingine zinaweza zikawa zinamfunga sana investor ambaye anashindwa ku- invest kwa kadri ambavyo alikuwa anategemea na akaamua kuondoka na tukakwama kwenye kuingiza mapato kwa ajili ya kuinua uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo kama tutaweza kuruhusu wawekezaji wa nje na wa ndani tunaangalia kabisa tunaweza tukainua pato la vijana pamoja na akinamama, wakapata ajira katika makampuni ambayo yatakuwa yamefunguliwa na viwanda mbalimbali, akinamama hawa ambao wengi wanajitoa kufanya biashara za uchuuzi, wakati mwingine zinahatarisha maisha yao barabarani. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Fedha aweze kuliangalia kwa upana huo kwa ajili ya kuweza kuinua uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia katika hotuba hii nzuri ya bajeti. Naipongeza Wizara kwa kazi nzuri ya kutuletea bajeti nzuri. Nampongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara. Ni bajeti ambayo ina matumaini kwa wananchi, bajeti ambayo imesikiliza mawazo asilimia 80 ya Wabunge na inaonyesha kwamba ile moja ya kazi ya Wabunge kuishauri Serikali, basi hapa katika bajeti hii inaonekana Serikali imesikiliza mawazo ya Wabunge nao wameenda kuyafanyia kazi na wametuletea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kuchangia moja kwa moja kwenye upande wa afya. Naipongeza Wizara kwa kazi nzuri ya kutuletea bajeti ya shilingi bilioni 265.8 kwa ajili ya afya, dawa vifaatiba na kumalizia miundombinu iliyojengwa na wananchi kwa nguvu zao wenyewe ikiwepo zahanati 8,004, pamoja na Vituo vya Afya 1,500. Namwomba Waziri wa Fedha, bajeti hii kwa upande wangu naiona bado ni ndogo kwa afya, lakini pamoja na udogo wake tuweze kuipokea hivyo ilivyo ila iende ikatekeleze kama inavyosomeka hapa, kama mpango ulivyo. Hii bajeti iende kama ilivyo, itekelezeke kule, tuisaidie MSD.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kabisa ni jambo ambalo liko wazi kwamba MSD inafanya kazi katika hali ya uhafifu. Tunajua kabisa ina madeni nje na ndani ya nchi, lakini kama bajeti hii ambayo inaonekana hapa itapelekwa fedha hizi kwa ajili ya kuwezesha dawa na vifaatiba kama ambavyo imeelezewa, tunaona kabisa changamoto ya ukosefu wa dawa na vifaatiba itaenda kupungua. Kama Wabunge wengine ambavyo wameweza kusema na kumsifia Waziri wa Fedha, itakuwa ni Waziri wa kiwango cha juu kwa bajeti hii iliyokuja hapa. Naomba niseme, atakuwa ni Waziri wa Fedha wa kiwango cha juu sana kama bajeti hii itatekelezeka kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo atakuwa ameweza kututolea changamoto kubwa tunayopata akina mama na watoto mahospitalini kwa ukosefu wa dawa; na hasa kina mama zile changamoto za kupoteza uhai wakati wa kujifungua ambapo hata Mheshimiwa Rais wakati wa hotuba yake aliongea akasema katika moja ya vita atakayoenda kuipiga ni kuhakikisha vifo vya mama mjamzito wakati wa kujifunga vinaisha. Sasa vitaisha kama bajeti hii itatekelezeka kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, namwomba sana Waziri wa Fedha, bajeti hii ipeleke pesa zinakohitajika. Kama ni MSD tuisaidie iweze kuhudumia wananchi, waweze kupata dawa na vifaatiba kama inavyotakikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala zima la Bima ya Afya. Ilani ya Chama cha Mapinduzi tuliyoinadi mwaka 2020, tuliwaomba wananchi kwamba wachague chama chetu, tutakuja na Bima ya Afya kwa kila mwananchi. Bajeti hii imeeleza na inaonyesha kwamba kwa mchakato wa mwazoni tunahitaji shilingi bilioni 145 kwa mwanzo wa fedha. Hata hivyo, naiomba Wizara, nilikuwa natamani Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-finalize aweze kutuelezea, hii pesa ambayo ameona kwamba ni shilingi bilioni 145: Je, ni pesa ambayo imekaa kwa bima ya mfumo upi? Ni Bima ya NHIF au ni CHF?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotegemea ni wananchi wapate bima yenye tija, isiwe bima ile ambayo mgonjwa anaenda kutibiwa hospitali ya Serikali tu, hana option ya kwenda kwenye private hospital. Hii itatusaidia kuweka mahusiano mazuri kati ya Serikali pamoja na private sector. Ile sera yetu ya PPP itaweza ku-apply vizuri zaidi maana mgonjwa au mtu anayehitaji matibabu atakuwa na option ya kwenda sehemu yoyote aidha ni private au aende Serikalini na kote atapata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Waziri wa Fedha, huu mchakato wa shilingi bilioni 145 wa Bima ya Afya uwe ni wa bima ambayo ni kama ya NHIF ambapo mgonjwa anaenda sehemu yoyote anapata ile huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nimeona hapa, inaonyesha bajeti yam waka 2034/2035 ndiyo tutakuwa tumeweza kumaliza suala hili zima la Bima ya Afya kwa kila mwananchi. Kwa hiyo, nikiangalia hapa naona kama tuna miaka 14 ya kuweza kukamilisha hili. Natambua kabisa universal health coverage siyo suala dogo la miaka miwili mitatu minne, iwe imeisha.

Naomba Waziri wa Fedha arudishe nyuma kidogo kwa sababu mwaka 2020 tumewaomba wananchi kwamba tutawaletea Bima ya Afya; mwaka 2025 tena tutaenda kuwaambia tena tunawaletea Bima ya Afya, wakati huo bado tuko kwenye process. Kuna wengine wamepata kuna wengine awajapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, inavyoonekana, tena mpaka 2030 bado tutakuja kuwaambia wananchi tunawaleteeni Bima ya Afya kwa kila mwananchi. Bado naona ni muda mrefu sana, naomba tu apunguze. Japokuwa ni jambo kubwa, sawa, lakini hebu irudi nyuma kidogo tusiwe tuna muda mrefu wa kupeleka hii Bima ya Afya kwa kila mwananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la kilimo. Natambua tuna benki ya kilimo, tuna Tanzania Investimate Bank ambazo zina riba kubwa. Nampongeza Mheshimiwa Rais ameweza kuona riba hizi ambazo ni kubwa na zinawakandamiza wananchi ambao wanashindwa kuweka maendeleo zaidi. Namwomba Waziri tuwe na mfuko wa kuchochea maendeleo ya kilimo na viwanda kwa sababu tunaelewa tuna Sera ya Awamu ya Tano na Awamu ya Sita ya Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika hizi sera tukiwa na mfuko wa kuchochea maendeleo, tunaona kabisa ni namna gani wananchi wataenda kukopa pesa kwa riba nafuu kwenye mifuko ya kuchochea maendeleo. Wakati huo huo, tunajua kabisa kilimo kinatupatia asilimia ya 65 ya ajira, asilimia 66 tunapata malighafi, asilimia 100 chakula tunachotumia sisi Watanzania kinatokana na kilimo.

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, sorry ni kengele ya kwanza au ya pili?

NAIBU SPIKA: Ya kwanza.

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 100 tunapata chakula kwa Watanzania na vilevile asilimia 30 ni kwa ajili ya kuingiza pesa za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwenye viwanda tunakuza thamani ya malighafi ya bidhaa zetu, tunaongeza ajira, tunakuza wigo wa kuongeza kodi. Kwa hiyo, tuliangalie eneo hili la kilimo na viwanda, ni namna gani tutachochea ili wananchi waweze kupata mikopo ya bei nafuu, huku tukiwa tumewaambia vijana wajiajiri? Anajiajiri vipi kama bado hawezi kujisimamia mwenyewe na akienda kwenye benki za kilimo riba ni kubwa ambayo mama amesema itakuja kupunguzwa? Kwa hiyo, tunaomba Waziri wa Fedha aliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Wizara na bajeti nzuri ambayo imesikiliza mawazo ya Wabunge wote. Wabunge walisimama katika Wizara ya TAMISEMI ilipokuwa inawasilisha bajeti yake, wakawa wanatetea sana suala la Madiwani. Limechukuliwa vizuri sana, wameleta hapa ufumbuzi kuhusu posho za Madiwani. Mama amelipokea, amelielewa na atatekeleza kwa mujibu wa taarifa hii ya bajeti iliyosomwa. Ameelekeza kwamba Waziri wa Fedha na Waziri wa TAMISEMI wataenda wakakae.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe tu Waziri wa Fedha na Waziri wa TAMISEMI wanapokuja kukaa pamoja kuangalia Madiwani hawa wanaangaliwaje, waweze kuangalia na lile jambo ambalo kuna Madiwani wanalipwa, ni posho tu inalipwa lakini hawawekewi nauli. Unakuta kuna mtu anatoka kwenye kata yake mpaka anakoenda kwenye Halmshauri ambapo kikao kipo ni kilometa 30, lakini mtu anayetoka kilometa 60 atapewa nauli, sawa; atapewa na pesa ya kulala sawa; sasa huyu mtu ambaye hata kama atatembea kilometa tano, analipwa nini? Waweze kukaa wawapatie pesa hizo za nauli hawa Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwa hali ilivyo sasa hivi, watu kutembea kwa muda hata wa nusu saa ni kama unapoteza muda. Mambo ni mengi. Kwa hiyo, tujaribu kuwa tunarudisha nauli za hawa Madiwani ambao wanatoka kilometa 20 kilometa tano waweze kurudishiwa. Kwa hiyo, namwomba Waziri wa Fedha na Waziri wa TAMISEMI ambao wameagizwa na mama yetu kipenzi, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakakae pamoja, waweze kuangalia suala hilo la nauli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara ya maji, awali ya yote nipende kuishukuru Wizara na kumshukuru Waziri wa Maji kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha kwamba wananchi tunapata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kijikite moja kwa moja kwenye suala zima la kupata maji kwa njia ya uvunaji wa maji ya mvua kutengeneza mabwawa. Nasema hivyo kwa maana ya kwamba katika hotuba ya Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan ukurasa wa 29 aliweza kuongelea kuweza kulinda miundombinu ya maji na vyanzo vya maji. Lakini vile vile hakuacha mbali suala zima la kuhakikisha tutatengeneza mabwawa ya kuvunia maji hasa kwa sehemu ambazo hazina vyanzo vya maji vya kutosha zenye ukame. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoka Mkoa wa Tabora Mkoa wetu hauna vyanzo vya maji vya kutosha na sehemu ambazo ziko pembezoni akinamama wanateseka sana kupata maji ya kutumia. Lakini niipongeze Wizara kwa Mradi wa Maji wa ziwa Victoria ambao mpaka hivi sasa umefika Tabora Mjini na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba wana mpango wa kupeleka maji katika Wilaya ya Urambo, Kaliua Sikonge. Kwa hiyo, nilikuwa ninaiomba Wizara katika huu mradi wa maji wa Ziwa Victoria mradi ambao umetengewa fedha shilingi bilioni 11 kutoka maji Tabora Mjini mpaka kwenda Jimbo la Igalula Kata ya Kigwa nilikuwa ninaomba Wizara iweze kuangalia hii National Water Fund iweze kuwa inaongeza fedha mradi ni bilioni 11 lakini katika mradi huo wa bilioni 11 mpaka sasa hivi imetoa bilioni mbili kasoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unajaribu kuangalia kama kilometa 30 kutoka Tabora kwenda Kigwa na Mradi ni gharama kubwa za bilioni 11 unaanza kuona je, kama hawatoweza kuongeza fedha hawa National Water Fund je, huu mradi unaweza ukaisha kwa muda gani? Lakini vile vile niiombe Wizara iangalie kwamba kwa namna nzuri tukiweza kuwekeza kwenye uvunaji wa maji ya mvua maeneo ya pembezoni inamaana hata gharama ya kutandika mabomba ya maji ya ziwa Victoria kwenda maeneo kama Tarafa ya Kiwele, Wilaya ya Sikonge ambapo kutoka Sikonge kwenda hadi Kiwele ni kilometa 200.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna maeneo ya pembezoni kutoka labda Bukene Mambali kupeleka maji yale kule kama vile maeneo ya pembezoni tukiwawekea mabwawa wananchi wakaweza kuvuna maji ya mvua yale wakatoa maeneo itakuwa imewasaidia akinamama kuhakikisha kwamba tunakwenda na Sera ya kumtua mwanamke ndoo kichwani kwenye uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niweze kuipongeza sekta ya maji ya Mkoa wa Tabora ambayo inafanya kazi vizuri kupitia RUWASA kwa jinsi ambavyo kuna mradi ambao ni wa Benki ya Dunia payment for results ambao mara ya kwanza walipewa bilioni 8.5 wakaifanyika kazi vizuri wakachimba visima vya maji lakini hivi sasa tunaona tunaletewa fedha bilioni 21 hii ni kazi nzuri sana inayofanya na sekta ya maji katika Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuangalie tunapokwenda kwenye Mkoa watu wa Tabora fedha zile tunazopeleka kwenye visima ardhi yetu ni kavu mkandarasi anakwenda pale anachimba kisima kwa gharama kisima kimoja ni milioni 25 lakini akifika chini maji hakuna. Kwa hiyo, tukiangalia namna gani nzuri katika aina mbili ya mradi huu wa Maji wa Ziwa Victoria lakini vile vile tuwekeze kwenye uvunaji wa maji ya mvua ili tuhakikishe mwanamke wa Mkoa wa Tabora tunamtua ndoo kichwani inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kuishukuru Serikali iweze kuangalia Wizara kuhakikisha mradi ambao umeshatengea fedha wa Bukene maji kwenda ya bilioni sita na mradi wa Nsimbo wa bilioni nne tuhakikishe basi hizi fedha zinakwenda kwa wakati, ili akina mama hao wa Nsimbo kwa Jimbo la Manonga na akinamama hawa wa Jimbo la Bukene na kata zote za mbali Kamangaranga na kwingine kote huko waweze kupata nafuu ya upatikanaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja mchango wangu niuelekeze kwenye Universal Health Coverage kwa maana ya Bima ya Afya kwa Wananchi Wote, ambayo tuliinadi katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kwamba Watanzania wote wapatiwe bima ya afya. Hata hivyo, tukiambatanisha na Sera yetu ya PPP - Public Private Partnership ili kuweza kuondoa changamoto na matatizo ambayo yanalikumba Taifa letu la upungufu wa dawa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaifafanua hiyo bima ya afya pamoja na Sera yetu ya PPP, naomba niishauri Wizara kuangalia explorer option ya kutokutunza dawa za wagonjwa wa nje au hospitalini tunasema outpatient, ili kuondoa mkanganyiko ambao unatokea kwamba Wizara inatoa taarifa kwamba kuna wizi wa dawa na upotevu wa vifaa tiba. Tukiimarisha bima yetu ya afya kwa wananchi wetu wote, bima ambayo ina tija ambapo mwananchi akienda private sector atapata huduma zote na akiingia hospitalini za Serikali atapata huduma zote. Kwa kufanya hivi inaweza ikatuondolea mkanganyiko huo wa kuona kwamba watoa huduma za afya pharmacist, doctors wanaiba dawa au vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuangalie sisi kama Wizara au Serikali kazi yetu ni kutoa huduma au tunahitaji tufanye business? Hii ni katika eneo hili la upotevu wa dawa na upungufu wa dawa na vifaa tiba. Naongea hivyo kwa maana tunaona kwamba private sector zinafanya vizuri ukilinganisha na vituo vya afya na zahanati za Serikali. Private sector anachojali ni kuangalia ana-provide service nzuri kwa mgonjwa au kwa mteja wake, hakuna suala la dokezo, hakuna kwamba dawa imeisha lazima niandike dokezo kwa Mganga Mkuu Mfawidhi au kikao cha management kiweze kupitia zile taratibu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaenda private sector kununua dawa hata kama hana, anakuambia subiri naenda store lakini kiuhalisia sio kwamba anaenda store anaenda kuangalia duka la jirani ili aweze kum-maintain huyu mgonjwa. Kwa hiyo, tuiangalie ni namna gani hii bima ya afya ikifanya kazi vizuri na tukajitahidi kuwa tuna-store dawa kwa ajili ya inpatient kwa maana ya wagonjwa ambao wamelazwa hospitali lakini wale wagonjwa ambao ni outpatient wapate bima yenye tija ili waweze kwenda nje kwenye private sector waweze kuhudumiwa, bima ambayo itakuwa na tija kwa maslahi ya mwananchi na sio kwa maslahi ya labda system, Serikali au Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta kama Serikali au Wizara tunakuwa na mzigo mkubwa ku-store dawa ambazo wakati mwingine ni brand. Unakuta kuna dawa ambazo ni brand ziko pale hospitali na tukiangalia kiuhalisia yale mafungu yetu matatu ambayo ni ya exemption kwa maana ya wazee, watoto na mama wajawazito zile brand ambazo tumezi-store pale hospitali kwa maana tumefungua duka la dawa la hospitali siyo yale makundi yanapata zile dawa na bado hatuweki kwa wingi unaotakiwa kumfanya yule mgonjwa akifika pale apate dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile clinicians anapata shida anapokuwa ana-prescribe medicine, labda anataka ampeleke mgonjwa kwenye third generation ya antibiotic, kwa sababu dawa zilizoko pharmacy ni first generation inabidi ampatie hiyo iliyopo. Tunajua kiuhalisia sisi Watanzania wote huku majumbani ni madaktari, before hujaenda hospitali umeshajitibu sana huku nyumbani. Kwa maana umeshaji-diagnosis wewe mwenyewe umeshakuwa mfamasia, ukisikia tumbo linauma unakunywa dawa metronidazole tunatengeneza resistance kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapokwenda kwa daktari tumeweka essential drugs ambazo ziko hospitali pale kwamba sisi kama hospitali au kama Wizara tumeweka item zetu ni 30 hizi hapa tukipungua chini ya hapo tutasema kwamba dawa hakuna lakini kama Wizara inapoenda kufanya supervision inakuta zile essential drugs ziko pale tunaambiwa kwamba dawa zinapatikana lakini kiuhalisia tungeweka bar yetu items za essential drugs zifike bar hata kwenye mia tukifika sabini ndio tuseme basi dawa zipo lakini sio tumeweka 30 and then tunasema kwamba dawa hapa zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo kwenye suala la bima ya afya na kuchanganya na hizi PPP, naomba niende kwenye suala la bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa. Hii CHF iliyoboreshwa bado haijawa na msaada kwa wananchi wetu, ina msaada wa kuonana na clinician’s au vipimo. Pia na yenyewe ina vipimo ambavyo haiwezi ku-clear na inampa shida mtoa huduma. Mfano kama kuna sehemu amekosea ku-request wanakatwa makato makubwa zaidi kiasi kwamba unakuta kituo kinarudi nyuma kwenye mapato. Mfano, ame-claim labda Sh.900,000/= lakini anakuja kupewa Sh.90,000/= jambo ambalo linamrudisha nyuma kuendesha shughuli za kituo. Wakati huo hapo kuna exemption za makundi matatu ambayo yanatakiwa yapate free medicine na kituo kinatakiwa kijiendeshe na pesa zote zimelala huku CHF. Nimuombe Waziri aangalie hii CHF basi hata iwe supported na NHIF ili hawa NHIF ambao wamesha-master vizuri kuangalia claim form zao zinakaaje na kama mtoa huduma amekosea wanajua namna gani ya kumwambia kwamba amekosea sehemu hii na hii tofauti na CHF.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala zima la bajeti. Suala siyo tatizo la bajeti, tatizo pesa hizi hazifiki kwenye vituo kama inavyotakiwa. Kwa hiyo, unakuta kama ni bajeti ya familia kwa mfano umepanga labda familia yangu inatakiwa kula kwa siku Sh.10,000/= baba ameacha shilingi 200 tunategemea nini? Kwa hiyo, haitaweza kufikia malengo, haya matatizo ya dawa na vifaa tiba kukosena yataendelea mara kwa mara. Tutajikuta hatutaweza kutatua tatizo kama kila siku tutakapokuwa tunakaa hapa kujadili bajeti mambo ni yale yale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee vituo vya afya ambavyo wananchi walijenga kwa nguvu zao wenyewe na Serikali kuna wakati imeweka mfuko ikakamilisha lakini majengo bado hayajakamilika. Kwa mfano, Kituo cha Igalula kimekamilika lakini hakina dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati. Nipende kumpongeza Waziri na Naibu wake Waziri kwa kazi nzuri. Nimpongeze Waziri kwa hotuba nzuri ambayo ameitoa, lakini vile vile nipongeze kwa kazi nzuri wanazozifanya hususan katika umeme wa REA vijijini. Pamoja na kazi nzuri wanazozifanya bado tuna changamoto nyingi hususan katika Mkoa wetu wa Tabora. Umeme umekuwa ni wa shida, umeme una katikatika katika wilaya zote zinazopatikana Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mradi mkubwa unaotarajiwa kutengeneza sub-station katika Wilaya ya Urambo pamoja na Sikonge. Urambo kwenda Kaliua mpaka Kigoma na Sikonge kwenda Katavi. Lakini umekuwa mradi ambao ulikuwa na malengo yake yalianza toka mwaka 2016 mpaka hivi sasa ni miaka mitano bado hatujaweza kufikia malengo. Na tatizo kubwa linalokuja hapa mkandarasi ameshapatikana lakini shida ni due diligence ambayo inayochelewesha sana kufikia ukamilishaji wa kupata transformer kuweza kupeleka kwenye huu mradi ulipangwa Urambo na Sikonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mradi huu toka umeanza kitu ambacho kimeweza kufanyika ni kujenga majengo ya kupokelea umeme na pamoja kuweza ku-identify njia za kupitishia umeme. Lakini changamoto za kupeleka transformer bado ni shida kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Waziri mwezi wa tatu alikuwa Wilaya ya Igunga pamoja na Uyui kuzindua umeme wa REA ambapo Wilaya ya Igunga waliweza kumueleza wanahitaji kutengenezewa vituo vya kupozea umeme pamoja na Uyui alizindua umeme katika Kijiji cha Ivumba na akaahidi utawaka kuanzia Aprili. Lakini mpaka leo wanakijiji wale wa Izumba wanasubiri sana umeme huo uweze kuwashwa lakini bado haujawashwa zaidi tu ya usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nilikuwa naiomba wizara iweze kuharakisha huu mpango na mchakato wa kuweza kuhakikisha transformer zinafika kwa wakati katika kujenga vituo vya kupozea umeme katika Wilaya ya Urambo. Tunachangamoto nyingi sana katika Mkoa wetu wa Tabora hususan ni hizi wilaya ambazo nimezitaja umeme unakatika, hatuwezi tukasema Tanzania ya viwanda kama bado hatujawa na umeme unaoweza kujitosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kusema watu wajiajiri kama bado tunawakwamisha katika kuhakikisha wanajitafutia kipato na kukuza uchumi wao. Inafikiwa wakati kuna kina mama ambao wengi wamejikiti kwenye kufanya biashara za saluni, vijana na wenyewe saluni za kiume lakini mtu ana mteja umeme unakatika; hakuna utaratibu kwamba leo tutakuwa tumewashiwa kwa siku tatu au nne lakini leo umekaa tu unamuweke mteja rollers umeme umekatika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa Mkoa wa Tabora wananchi wengi wamejikita katika uwekezaji wa mashine za kukoboa na kusaga. Mashine hizo zinatakiwa zitumie umeme, sasa kama umeme hauna nguvu ndio mtu ameweka tu mpunga kwenye mashine yake umeme katika haujulikani utawaka lini tunategemea huyu mtu mapato yake aweze kupata kwa wakati gani. Wakati huo huo TRA bado inamuhitaji kupeleka mapato ambayo yametokana na biashara anayofanya; biashara yenyewe inategemea umeme, umeme unakatika bila ya mpangilio tuweze kuangalia katika huu Mkoa wa Tabora ambao kidogo kila kitu naona kama kinakuwa kipo nyuma nyuma.

Mheshimiwa Spika, tunaomba wizara mturahisishie upatikanaji wa umeme wenye tija, wenye nguvu, ili wanawake hawa wa Mkoa wa Tabora wanaojikita katika shughuli zao za saluni wafanye kazi zao vizuri na shughuli zote zinazotumia umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)