Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mendard Lutengano Kigola (50 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Rais wetu.
Kwanza kabisa, naunga mkono hotuba hii ambayo ni hotuba nzuri kabisa ametoa kwa Watanzania wote na wamemuelewa vizuri sana.
Mheshimiwa Hotuba hii inatoa mvuto sana siyo kwa Watanzania tu ni watu wote ulimwenguni. Kuna Marais wengi sana wanatoa hotuba, lakini hotuba hii imekuwa ya mvuto kwa sababu amesema kile kitu ambacho wananchi wanakihitaji. Hotuba yake imetokana na jinsi alivyotembelea wakati wa kujinadi, amepita Wilaya zote za Tanzania na majimbo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kero za wananchi zinaeleweka na Rais ameweza kuelezea vizuri sana kwenye hotuba yake. Kwa mfano, ameelezea vizuri sana masuala ya maji, barabara, umeme na afya. Wabunge wote tunaungana na hotuba hii ambayo imekuwa kama mwongozo kwa shughuli zote ambazo Wabunge tunazifanya kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais ameongelea sana Tanzania iweje na ameliongelea kwa mapana yake. Kitu ambacho kimenifurahisha, ahadi zake ambazo alizitoa wakati wa kampeni, ndani ya miezi mitatu sasa hivi tukianzia mwezi Novemba, Disemba na sasa ni Januari tayari ameanza kutekeleza zile ahadi ambazo aliahidi. Ahadi ya kwanza ambayo sisi Watanzania tunahakikisha kwamba ameanza kuitekeleza, alisema kwamba elimu bure kwa watoto wetu na hili limeanza kutekelezwa. Hakuna mtu ambaye hasikii wala haoni, tumeshaona. Kufanya utekelezaji ndani ya miezi tatu duniani haijawahitokea kwa Rais yeyote, huyu ni namba moja. Kuna watu wengine wameanza kusema anatekeleza kidogo kidogo, wewe hata nyumbani kwako umetekeleza mangapi, hicho kidogo kidogo umeweza? Nataka niwaambie Rais tusimkatishe tamaa, Rais wetu ameshaanza kufanya kazi na inaonekana kwa Watanzania na lazima tumuunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili alisema atapunguza matumizi makubwa kwa Serikali, Rais ameanza kupunguza na vitu vinaonekana. Jambo la kwanza alisema atapunguza Baraza la Mawaziri na amepunguza kutoka Mawaziri 60 kuwa 34 ni hatua kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu alisema atapambana na mafisadi na tumeona TRA kilichotokea ndani ya mwezi mmoja ilikuwa ni balaa, ilikuwa ni mtafutano, hiyo yote ni ahadi alisema ataifanyia kazi. Pia alisema atapeleka watu mahakamani na tumeona ameanza kufanya kazi hiyo. Sasa nataka niseme, kwa mwenendo huu Tanzania ambayo tunaihitaji ndiyo inakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ameongelea sana masuala ya viwanda kwamba Tanzania itakuwa nchi ya viwanda. Uchumi wa nchi yoyote ukitaka upande lazima uhakikishe viwanda ndani ya nchi yako vinafanya kazi ya uzalishaji vizuri, mimi nakubaliana naye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kwamba Tanzania hatuna viwanda lakini havifanyi kazi kwa ile standard ya viwanda vilivyoko duniani. Kwa mfano, mimi natoka kwenye Jimbo la Mufindi Kusini, Wilaya ya Mufindi tuna viwanda vingi sana tukianza na Kiwanda cha Chai ambacho ni kikubwa katika Afrika; Kiwanda cha Karatasi pale MPL ni kikubwa sana katika East Africa na Kiwanda cha Pareto ni kikubwa katika dunia siyo Afrika. Tatizo kubwa ambalo tunalipata ili ku-improve uzalishaji ni miundombinu mibovu. Hivi sasa navyoongea kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini ambako kuna Kiwanda cha Chai na wakulima wa chai wako pale kuna magari mengi sana yanakwama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze Rais kipindi alipokuwa Waziri wa Ujenzi barabara ile alishaanza kuifanyia kazi. Nina maana kwamba upembuzi yakinifu alishamaliza tayari na kwenye ripoti ya RCC waliyotoa walisema kwamba upembuzi yakinifu uliisha Mei, 2015. Kwa hiyo, nataka nitoe taarifa kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi kwamba barabara ya kutoka Nyololo – Mtwango - Mgololo na kutoka Mafinga - Mgololo ambayo ina kilometa 84 na kutoka Nyololo - Mtwango ni kilometa 40 upembuzi yakinifu ulishaisha na Serikali iliahidi kwamba itaitengeneza kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, mategemeo yangu ni kwamba bajeti tunayokwenda kupitisha sasa hivi siyo ya upembuzi yakinifu tena ni ya kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha lami ile barabara ambayo aliahidi Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli na kwenye kampeni alisema ataijenga. Ninavyomfahamu tukimaliza bajeti hii ataanza kujenga kule kwa sababu amesema anataka kuimarisha viwanda na hizi barabara zote zimekuwa connected kwenye viwanda siyo kwamba zimejengwa tu, unapojenga barabara lazima uangalie inaenda wapi. Hizi barabara zimejengwa kwenye viwanda ambapo tumesema Tanzania inakuwa ya viwanda tu, viwanda hivyo vipo lakini miundombinu ni mibovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine la muhimu sana kwenye viwanda hivi ni lazima tuhakikishe tuna-improve masuala ya umeme. Bahati nzuri juhudi za Serikali ni nzuri maana tunazungumzia masuala ya gesi, kila mtu anasikia na juhudi tumeziona na tumeona REA wanavyofanya kazi, wanapeleka umeme kwa kila kijiji. Nashukuru sana Mungu Waziri wetu Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo amerudishwa tena kwenye Wizara hiyo kwa sababu alifanya kazi vizuri sana, vijiji vingi sana vilipata umeme. Kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna vijiji vingine hata ndoto tu kuota kwamba vitapewa umeme ilikuwa haipo sasa vilishapata umeme. Vijiji hivyo ni Kata ya Malangali, Ihoanza, Mbalamaziwa huo umeme unaelekea kwa jirani yangu wa Makambako. Ingawa juhudi ni nzuri lakini kuna vijijji kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini bado havijapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe ushauri kuhusiana na usambazaji huu wa umeme, tunataka umeme uende kwenye vitongoji kwa sababu utakuta umeme unafuata line kubwa tu. Sasa kuna kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata umeme kwenye vitongoji. Nadhani hili tutasaidiana kusimamia ili tuhakikishe vitongoji vyote vinapewa umeme. Kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna vitongoji vingi, nina vitongoji 365, vijiji 88, tutataka tuhakikishe vijiji vyote vinapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, huu umeme unaotoka Mbalamaziwa ambao unaelekea mpaka kule Kinegembasi, kuna vijiji vya Mtambule mpaka kule Kilolo, Hiyawaga, Kiyowela mpaka kule Itika na Iholo mpaka kule Idete havina umeme. Kwa mpango huu, naiomba Serikali, siwezi kutaja vijiji vyote lakini tuhakikishe kwamba kwa mwaka huu tunaosema kwamba tunataka nchi yetu iwe ya viwanda tushughulikie suala hili la umeme. Tunaposema viwanda kuna viwanda vikubwa, vya kati na viwanda vidogo vidogo. Hivi viwanda vidogo vidogo viko kwenye kata na ili wananchi wawe na viwanda hivyo lazima tuhakikishe miundombinu ya umeme imekaa vizuri.
Suala lingine ambalo ni la mwisho ni maji. Kila Mbunge akisimama hapa anauliza masuala ya maji. Bahati nzuri Serikali ilijitahidi sana kujenga matenki ya maji katika kila kijiji. Kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini, kuna matenki 11 hayafanyi kazi mpaka mimi Mbunge niliamua kuanza kuchimba visima tu lakini huwezi kuanza kuchimba visima kwenye maeneo ambayo mikondo ya maji ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji atambue kwamba hii siyo miradi mipya ni ukarabati wa miundombinu ya maji. Pale Igowole pameshakuwa mji kuna tenki la maji kubwa sana lakini halina maji, lina miaka zaidi ya 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda pale Nyololo kuna tenki la maji la muda mrefu, wananchi hawapati maji ya gravity system, mimi Mbunge nimechimba visima pale. Sasa namwomba Waziri haya matenki ambayo yapo ni miundombinu chakavu basi muweze kuitengeneza.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri kwenye swali la msingi lililokuwa limeulizwa hapa, anasema kwamba kuna shilingi trilioni moja imetengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji. Namuomba Waziri asisahau Jimbo la Mufindi Kusini. Nimeshaanza kutaja pale Igohole, Nyololo, Nyigo, Idunda, Itandula mpaka Iramba kuna matenki ya maji tayari, ni kutengeneza miundombinu na kuwawezesha wananchi maji yaingie kwenye tenki na ku-supply kwa wananchi basi. Hizo shilingi trilioni moja siwezi kuzimaliza, mimi hata ukinipa shilingi milioni 800 za kuanzia siyo mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri wa Maji kwenye mgao huu unaokuja asinisahau kwa sababu hayo matenki yapo tayari. Wakati tutakapokuwa tuna-discuss bajeti inayokuja mwezi Mei au Juni, nikiona bajeti ya vijiji vyangu haipo hiyo bajeti haitapita, nafuu nianze kusema mapema na nitakuwa namkumbusha kila wakati, haya ni masuala ya msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni masuala ya ardhi. Masuala ya ardhi imekuwa kero sana. Bahati nzuri Waziri ameanza mpango mzuri sana, ametugawia barua tuwasilishe matatizo. Kuna mgongano kati ya Maliasili na Ardhi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kigola muda wako umekwisha.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Waziri, Naibu Waziri wa Fedha pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kuandaa Mipango ya Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano, 2016/2017- 2020/2011. Naunga mkono hoja kwa sababu Mpango huu wanaonesha kusaidia kupunguza umaskini kwa wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa ushauri kwa Serikali kufanya utafiti kwa viwanda ambavyo havifanyi kazi ili kuangalia uwezekano wa kufufua, lakini kwa gharama ndogo, pia kuweka mfumo ambao utawezesha viwanda hivyo kuzalisha kwa faida. Viwanda vizalishe bidhaa ambayo inatakiwa kwa matumizi ya binadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ili kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa za viwanda unakamilika lazima viwanda vitumie gesi kwa bei nafuu ili kupunguza gharama za uzalishaji. Pia kusimamia bei ya mafuta; petroli, diseli na mafuta mengine ya kuendeshea mitambo katika viwanda. Bei ya mafuta ikiwa ndogo au ya chini itasaidia kuendesha viwanda kwa gharama ndogo na kupata faida kubwa ya uzalishaji wa bidhaa. Kuboresha huduma za jamii kama vile, kuboresha miundombinu ya barabara, umeme, maji na Vituo vya Afya itasaidia sana kukuza uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mufindi Kusini ni Jimbo pekee katika nchi yetu lenye viwanda vikubwa na vidogo. Tatizo kubwa tunaomba barabara ya Nyololo - Mtwango hadi Mgololo ambayo imepita katika Viwanda vya Chai, Mbao na Kiwanda cha Karatasi, Mgololo. Barabara hii ni muhimu sana kwa kukuza uchumi wa nchi, naomba ijengwe kwa kiwango cha lami. Serikali ilishafanya upembuzi yakinifu na Mheshimiwa Rais wa Tanzania aliahidi kujenga kiwango cha lami. Pia iko kwenye Ilani ya Chama cha mapinduzi kuwa barabara ya Nyololo – Mtwango kilomita 40, Madinga – Mgololo Kilomita 82 zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba ahadi zote za Mheshimiwa Rais ziingizwe kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/2017 - 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya makadirio ya mapato ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Pamoja na kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri, naomba Jimbo la Mufindi Kusini tuliahidiwa kujengewa barabara kwa kiwango cha lami, barabara ya Nyololo hadi Mtwango, Mafinga hadi Mgololo, barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Taifa, pia imepita kwenye maeneo ya Viwanda vya Chai, Karatasi, Mgololo na Mbao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme; naomba Serikali ipeleke umeme Kata ya Mtambula, Idunda, Itandula, Kiyowela, Idete, Makungu na katika maeneo ya vituo vya afya na maeneo ya shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji; naomba kutengenezewa miundombinu ya maji. Kuna matanki ya maji 12 hayafanyi kazi sababu miundombinu ya maji imeharibika, ilijengwa 1970, naomba Serikali iitengeneze miundombinu hii ili kuondoa adha kwa wananchi wa Kata ya Igowole, Nyololo, Idunda, Itanduka na Kibao ambao wanapata shida kubwa ya kukosa maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vituo vya Afya; naomba Serikali imalizie kujenga vituo vya afya katika Kata ya Mtwango, Mninga na Makungu. Wananchi wamejenga kuta bado kumalizia tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2016/2017
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufika siku ya leo. Kwa vile ni siku ya kwanza leo kuchangia humu Bungeni, nawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Mufindi Kusini kwa kunichagua na kunirudisha tena Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawashukuru Watanzania wote kwa ujumla wake kwa kumchagua Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Rais wa nchi hii. Tena narudia mara mbili, Watanzania walisema wenyewe tunataka Kiongozi anayefanya maamuzi ya haraka. Nadhani Watanzania hawajakosea, Rais wetu anajitahidi sana kufanya kazi pamoja na Waziri Mkuu na Viongozi wote waliochaguliwa wa ngazi za juu. Nawapongeza sana kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wameanza kulalamika masuala ya kutumbua majipu, kuna majipu ya aina tatu, kuna jipu ambalo linakuwa limeiva, sasa kazi ya Wabunge ni kutoa ushauri, ukiona jipu limeiva ni nafuu ujitumbue mwenyewe kwa sababu ukingoja kutumbuliwa inakuwa ni hatari. Serikali hii ya sasa hivi imejipanga vizuri kutekeleza mahitaji wa wananchi ambao wametuchagua. Wafanyakazi hewa ambao sasa hivi zoezi linaendelea, kama uliibia Serikali miaka ya nyuma jiandae hilo ni jipu tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite sana TAMISEMI, sasa hivi tumesema kwamba asilimia 40 ya fedha ya Bajeti ya Serikali inakwenda kwenye maendeleo. Bahati nzuri sana hata Rais wetu anasisitiza sana hilo, TAMISEMI imechukua asilimia kubwa sana ya maendeleo vijijini. Tatizo kubwa la Watanzania vijijini na Wabunge walio wengi wakija hapa wanalalamika sana masuala ya maji, maji ni tatizo sugu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kwa bajeti hii tujitahidi sana vijiji ambavyo havijapata maji viweze kupata maji. Haya maswali tunayouliza kila siku yanajirudia rudia, kwa mwaka huu tukifuata bajeti vizuri na kusiwe na ufisadi, wananchi watatatuliwa tatizo lao la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna matenki mengi sana ya maji yalijengwa mwaka 1970 mpaka leo hii, sasa hivi miundombinu imeharibika sana. Naiomba sana Serikali, ile miundombinu ambayo imeharibika sana, kwa bajeti hii TAMISEMI, Mawaziri wote waliochaguliwa TAMISEMI ni vijana halafu wapo makini sana na wanakwenda kwa speed.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tenki moja lipo pale Igowole, kuna tenki moja lipo pale Nyololo, tenki moja lipo Itandula, kuna tenki moja lipo Idunda na tenki moja liko Luhunga. Vile vijiji vyote ambavyo matenki ya maji yapo, miundombinu imechakaa, naomba Serikali ijitahidi kwa Bajeti hii waweze kutengeneza miundombinu ya maji ili watu waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la elimu. Kwanza namshukuru sana Rais kwa kuamua ile bilioni sita kupeleka kwenye madawati, ile amepiga bao tayari! Bahati nzuri sana amesema kila Mbunge atapewa madawati 500, lakini yale madawati yale nadhani mwezi wa Julai tunapoondoka madawati yangu nitayachukua mwenyewe. Kule kuna shule katika Jimbo langu la Mufindi Kusini hazina madawati, wananchi wameshasikia tayari na mimi yale madawati bahati nzuri mmesema tutapewa Wabunge nitasimamia vizuri, mtu akianza kuzungusha yale madawati sijui itabidi nitumbue jipu! Hili suala la kutumbua majipu tutatumbua mpaka kwenye vijiji kule. Sasa tatizo la madawati nadhani kwa nchi hii tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu, nataka nimshukuru Waziri wa Elimu kwa kuwa na vision nzuri sana. Wabunge ni washauri tunaishauri Serikali, naomba nimshauri Waziri, hii kubadilisha badilisha madaraja siyo tija sana, kwa ku-improve elimu. Tatizo kubwa ambalo lipo, hatuna Walimu wa sayansi katika sekondari zetu, ni tatizo kubwa sana Mheshimiwa Waziri. Unaweza ukaona mtoto anasoma, amechagua masomo ya sayansi kuanzia form three mpaka form four anaingia kwenye mtihani hana Mwalimu wa sayansi, tusitegemee kwamba atafaulu mtihani hata siku moja! Hilo ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Serikali imetoa msukumo mzuri sana wa kujenga maabara, Wakurugenzi pamoja na Wakuu wa Wilaya walijitahidi sana kusimamia maabara na tunaendelea kujenga maabara kule, shule nyingine vifaa vipo tayari, lakini hatuna Walimu wa sayansi, tusije tukategemea kwamba watapata division nzuri ,watafeli tu, kwa sababu hakuna Walimu na wao wanaingia kwenye mitihani hawajafundishwa masomo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matatizo makubwa ya Walimu wa sayansi pamoja na Walimu wa hesabu. Kama kweli tunalenga ku-improve elimu, tatizo siyo kubadilisha madaraja, sijui GPA haisadii! Tuhakikishe kwamba Serikali inasomesha Walimu wa sayansi, tena itoe motisha kwa mfano, Vyuo Vikuu wale wanao-opt masomo ya sayansi, basi walipiwe ada, wakilipiwa ada tutakuwa na Walimu wengi sana wa sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni katika Shule za Msingi. Shule za msingi bado kuna matatizo. Kwa mfano, wale tunaowaita Maafisa wa Tarafa Elimu, Afisa Tarafa Elimu anatembelea baiskeli, kwa mfano kwangu kule vijiji ni vikubwa, anatembea karibu kilometa 30 mpaka 40 kwa baiskeli, unategemea kweli ataweza kukagua shule zote za msingi? Ni ngumu sana, hebu mtafute hata pikipiki tu tumpe. Maafisa Elimu wa Kata tuwatafutie usafiri ili waweze kuzifikia zile shule, imekuwa ni tatizo kweli hata ofisi hawana wanashindwa kufanya kazi vizuri. Kwa sababu tunataka tu-improve elimu, naiomba Serikali ifanye mchakato kuhakikisha wanapata vyombo vya usafiri ili waweze kusimamia elimu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shule za msingi, kuna suala moja huwa linaleta matatizo sana, sijui sasa turudishe system ya zamani, hebu mliangalie na mlipime vizuri. Kuna Walimu wengine wanafanya biashara, badala ya kufundisha wanaanza kufanya biashara kwa sababu ya ugumu wa maisha. Serikali iangalie hilo tunafanyeje, sijui mrudishe teaching allowance, sasa ninyi mtaliangalia, zamani kulikuwa kuna teaching allowance, mtapima wenyewe lakini lazima muweke mazingira mazuri ya Walimu wa shule za msingi kwani wana mazingira magumu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni Wenyeviti wa Vijiji, TAMISEMI. Wenyeviti wa Vijiji kuanzia Mbunge kama anataka kufanya mkutano kwenye Kata yake, kwenye kijiji chake, ni lazima amwambie Mwenyekiti wa Kijiji. Mkuu wa Wilaya kama anafanya mkutano kwenye kijiji lazima amwambie Mwenyekiti wa Kijiji. Naiomba Serikali, Wenyeviti wa Vijiji angalau wapewe posho. Bahati nzuri sasa hivi tumesema kwamba kila mtu ni lazima afanye kazi, yule Mwenyekiti wa Kijiji anafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtendaji analipwa na Serikali lakini Mwenyekiti wa Kijiji halipwi mshahara, tutafute hata posho, tunapata shida kweli. Diwani kama anaitisha mkutano ni lazima amwambie Mwenyekiti wa Kijiji pale, Serikali lazima iangalie kwa makini suala hilo. Mwenyekiti wa Kijiji ana kazi kubwa kweli, kama Mtendaji analipwa hela, yeye halipwi na yeye ndiye mkuu, ndiye anayefungua hata vikao vya kijiji, ndiye anayeendesha maendeleo ya kijiji pale, halafu hapewi chochote, hii inaleta shida. Naiomba Serikali ifikirie vizuri juu ya hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Diwani anafanya kazi kama Mbunge, tukiwa hapa Bungeni sasa hivi Madiwani wako kule wanafanya kazi, wanasimamia miradi yote; miradi ya ujenzi wa Zahanati, miradi ya barabara, miradi ya maji anasimamia Diwani, tatizo kubwa la Madiwani wetu hawana vyombo vya usafiri. Kuna Kata kubwa sana anashindwa kuzifikia. Katika Kata moja unaweza kuona ina vijiji sita, karibu kilometa 12. Kwa mfano, kuna Kata moja kutoka Idepu…..
MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda, biashara na uwekezaji ni muhimu sana katika kuinua uchumi wa nchi yetu tunaomba Serikali kufufua viwanda vilivyokufa kwa kuzingatia gharama za kufufua viwanda hivyo. Kabla ya kuanza kazi ya kufufua viwanda hivyo, lazima kufanya cost analysis ili kujua gharama halisi ya viwanda hivyo, kama gharama ni kubwa ni heri kujenga viwanda vipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa viwanda vipya, kabla ya kujenga viwanda vipya, Serikali lazima kuangalia maeneo ya kujenga viwanda hivyo. Vitu vya kuangala ni miundombinu kwa mfano, barabara, umeme, gesi, umeme na ardhi, Serikali ihakikishe inaboresha miundombinu ili kuwezesha usafiri na uzalishaji wa bidhaa unakuwa imara na unaboreshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya viwanda. Serikali lazima kutumia technology katika kuimarisha viwanda vyetu, vijana wetu lazima wasomee elimu ya kuendesha viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu soko. Serikali lazima ihakikishe inatafuta soko la bidhaa ambazo zitakuwa zinazalishwa katika viwanda. Tunajua Serikali haifanyi biashara lakini inaweza kuwezesha wafanyabiashara kupata soko la bidhaa zinazozalishwa katika viwanda vyetu. Viwanda ambavyo Serikali inaweza kuviboresha ni viwanda vya chai, korosho, pamba, ngozi, sukari na viwanda vya mbao ambavyo vipo Wilaya ya Mufindi katika Mkoa wa Iringa. Ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa chombo cha habari ni muhimu sana katika kuhabarisha jamii masuala ya kiuchumi, kisiasa, kisayansi na kijamii naiomba Serikali kusimamia haki za wanahabari, hasa katika kuangaliwa upya maslahi ya wafanyakazi. Serikali iangalie kutoa msaada wa kuwasomesha waandishi wa habari ili kupata wanahabari ambao ni wataalamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa utamaduni ni sehemu ya maisha ya binadamu naiomba Serikali izidi kuboresha utamaduni wetu wa Afrika.
Tunakoelekea utamaduni wetu unaelekea kupotea kwa sababu tumeanza kuiga utamaduni wa Ulaya, kwa mfano mavazi, muziki na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sanaa. Tanzania ni nchi ambayo inatambulika dunia kwa sababu ya kudumisha sanaa katika nchi yetu. Ukienda Ulaya utakuta sanaa ambazo zimetoka Tanzania, kwa mfano vinyago, vikapu, mikeka, shanga zilizotengenezwa na kabila la Kimasai. Naiomba Serikali kuangalia jinsi ya kudumisha na kuboresha sanaa ya nchi yetu hasa kuwaongezea mitaji watu wanaoshughulika na masuala ya sanaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michezo ni sehemu ya kudumisha afya zetu, pia michezo inaongeza Pato la Taifa. Michezo inaleta ajira kwa vijana wetu. Naomba kujua Serikali ina mpango gani wa kudumisha michezo katika ngazi za Vijiji, Kata, Wilaya, Mikoa hadi Taifa, hasa mchezo wa mpira wa miguu na wa pete.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waimbaji wetu wanaibiwa sana nyimbo zao, je, sasa Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha kuwa hawa wasanii wetu hawaibiwi CD, DVD zao? Naunga mkono hoja
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi nichangie. Nami natoa pongezi sana kwa Waziri Muhongo kwa kazi nzuri aliyoifanya mwaka uliopita. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tena amerudi kwenye Wizara hii muhimu. Wabunge wengi sana wakisimama wanaomba umeme vijijini na tuna matumaini makubwa sana kwenye Awamu hii ya Tatu vijiji vile ambavyo vilikuwa vimebaki kwamba vitapewa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Serikali kwa kutoa ile service charge kwa sababu ilikuwa ina-discourage sana wananchi, lakini Serikali ilitangaza kwamba imetoa service charge kwa hiyo, wananchi saa hizi nadhani hata bei ya umeme imeshuka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nashukuru sana kwa kupunguza gharama za umeme hasa kwenye installation kwenye nyumba zetu. Hii italeta nafuu sana wananchi waweze kuingiza umeme kwa urahisi kwenye nyumba zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni masuala ya gesi. Naiomba Serikali, gesi isiwe mijini tu, hata watu wa vijijini wanahitaji kutumia gesi. Hata mwaka 2015 niliongea kwamba inabidi elimu itolewe kwa wananchi kuhusu matumizi ya gesi. Sasa na gharama kubwa sana; ukienda kununua au kubadilisha mtungi wa gesi unakuwa na gharama kubwa sana. Naomba Serikali ifikirie masuala ya gharama ya gesi. Tunasema kwamba wananchi wasitumie mkaa, mbadala wake watumie gesi, lakini gesi bado vijijini haijafika. Naiomba Serikali iweze kupeleka gesi vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna vijiji vingi havijapata umeme. Ni asilimia 37 tu ambavyo vimepata umeme. Naomba kwenye Kata ya Mtambula, Idunda, Kiyowela, Luhunga, Mninga, Kata zile zote pamoja na vijiji vyake; kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini nina vijiji 88. Kati ya vijiji hivyo kuna vijiji 50 havijapata umeme.
Sasa tunapopeleka umeme vijijini, naiomba Serikali kuwaambia wale Makandarasi, umeme unapelekwa kwenye kaya za watu, siyo kwenye barabara. Unaweza kuona umeme umepelekwa lakini bado haujaenda kwenye Vitongoji. Kwa mfano, mimi kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini, nina vitongoji 365. Kati ya vitongoji hivyo kuna vitongoji karibu 200 havijapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, umeme upelekwe kwenye vitongoji ili wananchi waweze kupata umeme. Kwa mfano, pale Malangali nashukuru kwanza REA wamepeleka umeme, lakini mpaka leo haujawaka na transformer wameshaweka tayari. Mheshimiwa Naibu Waziri nadhani nilikwambia, kwamba wananchi wa Malangali hata sasa hivi wameniandikia message; Kata ya Malangali, Mbalamaziwa na Kwatwanga kule Kata ya Ihohanza, umeme haujawaka lakini nyaya zipo pale. Kwa hiyo, watu wameangalia nyaya tu, umeme upo pale. Namwomba Naibu Waziri hili alichukulie kiundani zaidi, awashe umeme pale wananchi waanze kufaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine kuna vijiji vingine wanaangalia nguzo za umeme zilipitishwa miaka ya nyuma, kwa mfano Kijiji cha Lugolofu, nyaya zimepita tu juu pale, kwa hiyo, ina-discourage sana, wananchi wanalinda nguzo. Siku moja waliniambia tutashangaa wamekata nguzo zile zimedondoka chini, sasa itakuwa imeleta tatizo kubwa. Kwa hiyo, naiomba Serikali, vile vijiji ambavyo vinalinda nyaya, hebu muwapatie umeme basi na wenyewe wafaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika Jimbo langu la Mufindi Kusini, kuna Mto Nyalawa, tulifanya research, kuna maporomoko makubwa sana pale. Tungepata umeme kutoka katika Mto Nyalawa halafu tungeweza kupeleka kwenye vijiji vingi sana kwenye Jimbo langu la Mfindi Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, kwa sababu muda ni mdogo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mufindi Kusini tunaomba umeme katika Kata za Mtambula, Maduma, Idunda, Kiyowela, Magunguli, Itandula, Idete na Mninga. Pia, naomba umeme upelekwe kwenye Vituo vya Afya Kihanga, Mninga, Mtwango na Udumuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kwenye taasisi ni muhimu sana kupata umeme naomba sana shule za msingi, sekondari na taasisi za kidini kupelekewa umeme. Jimbo la Mufindi Kusini tuna tatizo kubwa la umeme, tunaomba Serikali ipeleke umeme katika Jimbo la Mufindi Kusini; vijiji vingine nyaya zimepita juu kwenye nyumba za watu, tunaomba Serikali kuangalia kwa huruma vijiji hivi, kwa mfano Kijiji cha Rugolofu, Kitasengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naipongeza Serikali kwa kufuta Service Charge na kupunguza gharama za uingizaji wa umeme katika nyumba.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mufindi Kusini tuna mgogoro wa ardhi kati ya Wizara ya Maliasili na wananchi wa kijiji cha Kitasengwa, Ihomasa, Udumuka na Kilolo, Iyegeya na Mninga. Kufuatana na ongezeko la watu, wananchi wamekosa maeneo ya kujenga nyumba na shughuli za kilimo. Mawaziri waliopita walifika katika vijiji hivi ni Mheshimiwa Maige na Mheshimiwa Ole-Medeye; walifika katika vijiji vya Ihomasa na Kutasengwa. Pia waliahidi kuwa maeneo ambayo yanatumika na wananchi wataachiwa maeneo hayo, lakini mpaka leo hii maeneo haya bado hayajaachiwa wananchi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini sasa Waziri wangu wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi atafika katika Jimbo la Mufindi Kusini na kuwaachia ardhi hiyo ili waweze kuendelea na shughuli za kilimo na kujenga nyumba zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia na mimi katika hoja hii muhimu sana. Mimi leo sehemu kubwa itakuwa ni ushauri kwa sababu Waziri anayeanza sasa hivi ni mara ya kwanza kushika nafasi hii ya Wizara ya Maliasili. Ila nataka niseme tu, Wizara ya Maliasili ni Wizara ngumu sana kwa sababu inagusa maeneo mengi sana ambayo yanahusu maslahi ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianza na masuala ya migogoro ya wananchi na Hifadhi. Kila kona Tanzania nzima kuna hifadhi ya misitu, na kule kwangu Mufindi kuna vijiji ambavyo viko ndani ya msitu lakini nataka niseme kwamba vile vijiji vilianza miaka mingi sana, miaka ya 1974, 1976, kwa hiyo misitu umekuta vijiji, kwa sababu ile misitu imepandwa mwaka wa 1977. Sasa namuomba Waziri, kuna vijiji vile ambavyo Mawaziri waliopita waliweza kutembelea vile vijiji na waliahidi kwamba wataachiwa na waliunda Tume, Tume ikafanya mchakato kule, na bahati nzuri sana wakasema kwa sababu siku hizi ni ushirikishwaji pamoja na wananchi, basi yale maeneo watawaachia wananchi waendelee kufuga na kulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuomba kuna kijiji cha Kitasengwa pale, Kitasengwa ni kijiji ambacho kinapakana na msitu pale na wananchi waliacha maeneo makubwa kuwaachia Wizara ya Misitu wakabakiwa na maeneo madogo na yale maeneo madogo Wizara ya Misitu inataka kuwanyang‟anya. Nakuomba Waziri yale maeneo madogo wawaachiwe wananchi wa Kitasengwa pale, na watu wa misitu wanaelewa na barua tulishaandika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuna kijiji cha Ihomasa, Mheshimiwa Waziri Ezekiel Maige alienda, hata kipindi cha Mheshimiwa Balozi Kagasheki alienda pale, na waliahidi kabisa kwamba yale maeneo wanayaachia wananchi. Lakini mpaka leo hawajayaachia wananchi wale, nakuomba Waziri, mimi Waziri Maghembe nakuamini sana. Kwa sababu na tume imeishaundwa noamba wananchi wa Ihomasa, wapewe lile eneo dogo waendelee kuishi; kwa sababu wanashindwa kulima na tunasababisha njaa. Kuna kijiji kingine kiko pale Kilolo ambacho kinaunganika na Udumuka, na wenyewe wana tatizo linalolingana na Kijiji cha Kitasengwa. Ni maneo ambayo wananchi wanapata chakula pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na wenyewe waweze kuachiwa maeneo hayo. Kuna hifadhi nyingine iko kwenye Kijiji cha Iyegeya, Iyegeya ni kijiji kiko Luhunga pale. Kile kijiji kuna hifadhi kubwa sana imebaki tu, hakuna wanyama wala nini, wanaita hifadhi, sasa mimi huwa nashindwa kuelewa hifadhi inahifadhi nini kwa sababu pale hakuna msitu. Ni eneo pori tu wanasema hifadhi, wananchi hawana sehemu ya kulima wala kufanya nini, naomba wawaachie wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mawaziri wote waliopita walishafika kule na wakaahidi kwamba wataachiwa, naomba na wewe basi umalizie ufanye mkutano na wale watu. Kwanza mikutano tulishafanya sana, ni kutoa amri tu, siku moja waendelee unakaa ofisini unaagiza Wizara yako, basi wananchi wanaweza kuachiwa maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo ningependa sana kuchangia ni kuhusu Jimbo la Mufindi Kusini ambapo wananchi walio wengi walihama kuachia maeneo Wizara ya Misitu. Na walifanya vizuri siwezi kusema walifananya vibaya, kwa sababu ule msitu sasa hivi ni Pato kubwa sana la Taifa. Na hatuwezi kusema Serikali inafanya biashara hapana, Serikali inatoa misaada, inatoa service kwa wananchi, na wananchi wale lazima wanufaike na misitu. Sasa cha ajabu inakuwa kinyume chake kwa nini? Tunashindwa kuelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano mdogo tu, kijiji cha Nyololo ni kijiji kikubwa sana, kijiji cha Igowole ni kijiji kikubwa sana, ukienda Igowole mpaka kule Sawala, mpaka kule Kibawa, mpaka Mninga vijjiji vyote hivi vilikuwa ndani msitu. Na waliachia Wizara kwamba wapande misitu, ili Taifa letu liweze kupata faida. Lakini cha ajabu sasa hivi vile vijiji vinavyozunguka ndani ya msitu havipati faida, kuna vitu vingine ni vidogo vidogo tu mimi nashangaa sana Wizara haifanyi kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunategemea kwa mfano Mji ule Nyololo pale ukiangalia ng‟ambo ya huku juu ni msitu mkubwa karibu kilometa 40, tumeachia Wizara, kijiji cha Nyololo hakina hata maji. Maji ambayo hata shilingi milioni 20 haiwezi ku-cost, kwa nini Wizara inashindwa kusaidia huduma za kijamii? Tunasema wawekezaji wasaidie huduma za kijamii kwenye vijiji vinavyohusika, lakini kijiji cha Nyololo hakina maji hakina barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata barabara tu Wizara ya Misitu mna magreda pale, magreda tukienda pale mpaka uandike barua uomboleze ufanye nini, na wale watu ndio wanaolinda msitu. Watu watapataje moyo wa kulinda msitu wakati hawana hata barabara, hata maji tu mnashindwa. Mimi Mheshimiwa Waziri Maghembe namuamini sana, naomba vijiji vinavyozunguka misitu lazima vipate huduma za kijamii. Na tunaposema huduma za kijamii ni zipi, nataka nikuambie Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifanya huduma ya maji, ukisaidia kujenga zahanati, ukasaidia kujenga kituo cha afya, wewe utakuwa umesaidia huduma za kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wizara utasikia tunatoa mafunzo jinsi ya utunzaji wa misitu na kulinda moto. Hivi wewe unalinda moto wakati una afya mbaya na kituo cha afya hakijajengwa na kiko ndani ya msitu? Mheshimiwa Waziri mimi nakuomba sana, kwa mfano ukienda pale Mninga tuna kituo cha afya pale, kituo kile kimejengwa miaka mitano, mpaka sasa hivi hakijaisha. Unaenda pale utasikia Wizara ya Misitu eti wametoa labda mbao 100, mbao 200, kwa nini usitoe msitu tu useme umemaliza kituo cha afya tumemaliza kila kitu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Mbunge nilienda pale nikatoa bati 200, mifuko ya simenti 100, Wizara inatoa mbao 20 au 10 hiyo haiwezi kukubalika kabisa hiyo. Mheshimiwa Waziri nataka nikuambie kitu kimoja, mwaka huu lazima tuone Wizara ya Misitu inatoa vitu vya kijamii vinaonekana. Kwa mfano, hapa nilikuwa nasoma hapa, mmesema mnategemea kukusanya shilingi bilioni sita, mwaka wa jana walikusanya shilingi bilioni nne, shilingi bilioni nne sisi wana Mufindi hatujafaidi. Sisi suala la madawati lilitakiwa liwe historia tu, hapa tunaanza kuongelea madawati sisi watu wa Mufindi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa juzi alisema anatuita Wabunge tuanze kuchangisha madawati, hatuchangii. Misitu ipo pale tuanze kuchangia kwa nini, lazima misitu ile ifanye kazi pale, hatuwezi kuwa tunasimamia kulinda misitu; halafu mnatubanabana sisi Wabunge na fedha ndogo ndogo hizi, wakati kuna shilingi bilioni sita iko hapa hiyo haiwezi kukubalika kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka madawati pale yakamilike. Mwaka jana mimi niliomba nikasema katika shilingi bilioni nne, mtupatie hata shilingi bilioni moja tu Wilaya ya Mufindi tutakuwa tumemaliza madawati, matokeo yake wanaenda kutoa madawati 100. Hatuwezi kudanganywa kama watoto wadogo, tutalindaje misitu? Haya umesema hapa kuna masuala ya mradi wa nyuki. Nilisikia siku moja kuna kikundi fulani kimechonga mizinga, badala ya kuwagawia wananchi wanaoishi kwenye misitu kule, wakaanza kufanya biashara wakasema kila mzinga shilingi 60,000 sasa tena ni biashara imetoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikajua mnawahamasisha ili wafuge nyuki, sasa utapeli tapeli huu unatoka wapi huu, hii inakuwa ni tatizo hatuwezi kuwa tuna matatizo tunayaona hivi na mwaka huu sisi tuko smart. Nadhani Wabunge wanaotoka Wilaya ya Mufindi watakuwa wakali sana kwa hili, hatuwezi tukawa tunahaibika na vitu vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya tunakuja kwenye ugawaji wa vibali. Ugawaji wa vibali unaenda kitapeli tapeli, mtu anafanya kama biashara ya kwake. Ile ni mali ya Serikali, ya wananchi wote, utakuta mtu mmoja anagawagawa vibali anagawa kwa wananchi anafanya biashara, kwa nini asishikwe apelekwe polisi ahukumiwe, mnamuangalia tu. Matokeo yake sisi Wabunge tunapata makashfa makubwa, sisi hatulali kule, mtu mwingine anakaa Dar es Salaam kule, amekusanya vibali analala usingizi, sisi kule tunalala tunalinda moto kule, mwenyewe anakuja kutapeli kule, hii haiwezi kukubalika hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri bajeti yake itapita, na kwa sababu ya mara ya kwanza tunamsamehe kwa leo, lakini ninayoyaongea haya, next time nikiona yametokea sitakubaliana kabisa. Watu wanaleta ujanja ujanja wa vibali, tumesema vibali mpeleke kwenye vijiji, vijiji vile ukisaidia Kijiji kimoja kibali kimoja tu wakajenga zahanati, kijiji kimoja utakuwa umesaidia watu zaidi ya 70, au zaidi hata 1000. Kijiji cha Mninga kiko ndani ya msitu hata zahanati miaka mitano hatujamaliza, kwa nini usiwape kibali pale?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jamani vitu vingine ni vitu rahisi rahisi tu, Serikali tutaanza kuilaumu kwa vitu vidogo sana. Hatuwezi kulaumu kwa vitu vidogo vya utekelezaji. Kwa kweli hii inaleta uchungu sana, kuna vitu vingine ni vitu vidogo vidogo lakini kwa ajili ya watu wachache wanatuletea gharama kubwa ya kuweza kuhutubia kila siku. Mwaka jana nakumbuka Waziri Mkuu alitutuma mimi na Waziri Nyalandu tukaenda Mufindi kule, Waziri Nyalandu alienda pale akafanya mkutano mzuri kwa wananchi, wananchi wakampigia makofi, kwenye utendaji ikawa zero kwa nini? Haiwezekani kabisa hii ndugu yangu, haiwezekani.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa muda na mimi nichangie. Kwanza na-declare interest mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti na nimefurahi sana kusoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, hotuba yake ni nzuri inajieleza vizuri sana kwa sababu imegusa maeneo muhimu yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala ambalo limenifurahisha sana ni kwamba, hotuba ya Waziri imegusa sana malengo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, mambo ambayo tuliahidi, Mheshimiwa Rais aliahidi na Wabunge huwa tunasema kwenye Majimbo yetu, yote yameandikwa humu. Tunakuombea sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha haya tuliyoandika Mungu atusaidie tuweze kukusanya vizuri kodi ili tuweze kutekeleza. Jambo lolote ili lifanyike vizuri lazima kuwe kuna fedha, bila fedha hatuwezi kufanya kitu chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimempenda sana Mheshimiwa Waziri ameweka mikakati jinsi ya kupata hizi trilioni 29. Kupata trilioni 29 ni nyingi sana ukilinganisha na mwaka 2015/2016 tulikuwa na bajeti ya trilioni 22 sasa hivi imeongezeka tuko trilioni 29, kukusanya mpaka tufike trilioni 29 ni muziki mkubwa. Ameeleza vizuri sana kwenye hotuba yake kwamba atapataje hizo trilioni 29, nampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, tumeeleza vizuri sana kwenye bajeti. Namwomba tu Waziri wakati anahitimisha hotuba yake hii aangalie na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti ni ya msingi na ukiyasoma vizuri pale utakuta kuna mambo mengine tunaenda sawa, kuna mambo mengine tumetoa ushauri. Jambo ambalo limenifurahisha, tumesema kwamba Tanzania itakuwa Tanzania ya viwanda na tumesema lengo kubwa kuwa Tanzania ya viwanda ni kugusa watu wa kima cha chini. Hiyo ni kweli kabisa nami hiyo nimeipenda sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya Viwanda ili ikamilike vizuri kuna mambo Mheshimiwa Waziri ameeleza, amesema kwamba, atahakikisha anajenga reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge. Tunajua ni mwaka huu wa fedha wa 2016/2017, lakini hatujui kwamba reli itakwisha kwa mwaka mmoja, tunaweza tukaanza mahali pazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri sana katika uchukuzi, ukiangalia bajeti ya Uchukuzi na ukachukua bajeti ya Ujenzi tuki-compare pamoja inatenga trilioni nne. Hizi trilioni nne zikisimamiwa vizuri, tukaanza kujenga vizuri hiyo reli ya kati, itatusaidia sana na hii concept ya viwanda itakwenda vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kitu kimoja, reli hizi tunazo nyingi sana. Tuna reli ya Kati, tuna TAZARA, tuna reli nyingine hii inatoka Tanga inakuja Moshi mpaka Arusha. Tunapozungumza viwanda maana yake malighafi zote tutatumia reli kwa kusafirisha mizigo yetu. Namwomba Waziri wa Fedha, tuna reli nyingine ile inayopita Makambako, kwenye Jimbo langu pale ya Mgololo, watuwekee station pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa na station ya reli ya TAZARA pale, tunajua wasafiri au wanaosafirisha mbao badala ya kutumia barabara ya lami ambayo tunajua barabara inaharibika kila siku, basi mbao zitasafirishwa kwa njia ya treni, hapo watakuwa wametusaidia sana. Kuna kituo kidogo sana, treni pale inasimama hata dakika tano haifiki, inakuwa ni shida sana pale, namwomba Waziri alifikirie suala hili pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine amegusia sana kwamba, ataimarisha bandari, ni kweli tukitumia bandari zetu za Tanzania tutakuwa tumefika mahali pazuri sana. Tunayo bandari ya Dar es Salaam, tuna bandari ya Tanga, tuna bandari ya Mtwara na sasa hivi kuna bandari moja tunajadili Bandari ya Bagamoyo, tuna Bandari ile ya kule Mbamba Bay. Bandari zote hizi zikiimarishwa vizuri uchumi wa Tanzania utakuwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri ameongelea vizuri sana kwenye elimu, nimempenda sana. Ametenga karibu trilioni 4.7. Tukiimarisha elimu, Watanzania tukipata elimu nzuri, watoto wetu wakisoma vizuri Vyuo Vikuu tutapata wataalam wazuri sana. Ukipata wasomi wazuri hata vitu vya kugombana gombana vidogo hivi wengine wanatoka toka, wanakimbia kimbia wakielimika itakuwa haipo. Hii elimu sasa hapa naona mwaka huu Waziri wetu wa Fedha ameamua, maana kutenga trilioni 4.7 haijawahi kutokea. Kwa hiyo, ameliangalia vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulisema hatuna wataalam wa gesi. Nashauri gesi itatutoa, gesi ni kitu kizuri sana katika uchumi wa nchi, tukipata wataalam wa gesi wakatengeneza vizuri, nchi yoyote duniani yenye gesi na mafuta uchumi unakua haraka sana tuki-contol vizuri, lakini tukishindwa ku-control gesi na mafuta, basi uchumi hauwezi kukua. Kama tunataka tufikie malengo lazima tuhakikishe gesi na mafuta tume-control vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji kwenye viwanda wengine wamesema sasa hivi wanashindwa kutumia gesi kwa sababu ni gharama kubwa. Nadhani Waziri wa Viwanda atatusaidia, kuna viwanda vingine havitumii gesi lakini ukitaka upate production kubwa, utumie cost ndogo lazima utumie gesi. Sasa wengine wanasema gesi ni gharama, wanakimbilia kutumia umeme, suala la gesi hii nataka nisisitize sana, Tanzania lazima tujikite vizuri kwenye gesi. Gesi na mafuta ndiyo neema pekee, ndiyo tutaondokana na umaskini. Ukisema unataka kuuvua umaskini, lazima tuhakikishe kwamba pato la Taifa limekua kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri ameeleza vizuri, amesema kwenye focus hapa kwamba mwaka 2016 pato la Taifa litafikia 7.2, hii kuipata siyo mchezo! Mwaka jana tulikuwa na point zero sasa hivi unasema point mbili, hii mbili kuipata siyo mchezo, lakini tuki-control vitu ambavyo ni vya uzalishaji tunaweza tukafikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukisema maisha ya kila mtu maana yake tunaangalia hata maisha ya vijijini. Maisha ya vijijini tunaangalia nini? Tunaangalia watu wana maji? miundombinu ya maji imejengwa? Vituo vya afya tumejenga? barabara zile ambazo hazipitiki zinapitika? Zahanati zimekwisha? Vituo vya Afya vinafanya kazi? Basi tukifanya vitu vya namna hii tutafikia mahali pazuri sana. Mpaka sasa hivi kwenye bajeti, wananchi sasa wana imani kubwa sana wanasema tutapata maisha bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri umesema utafufua viwanja vya ndege. Sasa kuna sehemu nyingine hata viwanja vya ndege watu wanasema sisi hatupandi ndege tunataka barabara. Nadhani barabara zile ziwekwe kwa kiwango cha lami ambacho Serikali iliahidi, itakuwa imefanya vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa sababu ni kitu kizuri sana. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Balozi zetu katika nchi mbalimbali hali siyo nzuri sana, Serikali iboreshe ukarabati wa majengo katika Balozi zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mabalozi waliostaafu bado wako nchi za nje, nashauri walipwe haki zao na kurudishwa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabalozi waitangaze nchi yetu kibiashara katika nchi mbalimbali kwa mfano watangaze Mlima Kilimanjaro kuwa upo Tanzania na siyo Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabalozi wawe na wataalam ambao wanaweza kufanya research katika nchi wanazowakilisha ili kupata mahusiano mazuri ya kibiashara na pia kupata ajira kwa vijana wetu katika nchi mbalimbali. Pia Serikali iwape fedha Mabalozi wetu kwa muda muafaka siyo kuchelewesha malipo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mpango wa Maendeleo ni wa muhimu katika maandalizi ya kutayarisha bajeti ya Taifa, nampongeza sana Waziri wa Fedha, Naibu Waziri pamoja na Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri ya kuandaa Mapendekezo ya Mpango wa Taifa kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ushauri; katika ukusanyaji wa Mapato Serikali iongeze juhudi ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili kuelewa kuwa kulipa kodi si adhabu ni wajibu wa kila mfanyabiashara. Ili kufikia lengo la kukusanya mapato ya Shilingi trilioni 32.946, Serikali inatakiwa kuhakikisha mikakati ya ukusanyaji kodi kutoka vyanzo mbalimbali kuwa wazi kwa kila mtu na kujua Serikali ina malengo makubwa ya kuboresha huduma za jamiii kama vile kuboresha miundombinu ya maji, barabara, afya, nishati na elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika matumizi ya bajeti kwa mwaka 2017/2018 lazima pawepo na uwazi wa matumizi ya bajeti kwa wananchi wetu ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, TRA watoe elimu kwa Watanzania juu ya utaratibu unaotumika katika ukusanyaji wa kodi, pia kujua aina ya kodi ambazo mfanyabiashara anatakiwa kulipa. Fedha ya maendeleo katika Halmashauri zetu zipelekwe kwa wakati bila kuchelewa ili kukamilisha miradi ambayo imepangwa. Pia Serikali iwe makini sana na miradi ambayo ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambazo ni ahadi za Mheshimiwa Rais wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea mwaka 2017/2018 Miradi ya maji, barabara, afya, itaendelea kutekelezwa kwa kufuata Bajeti ya Taifa na miradi ya kipaumbele ni ile ya ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia machache.
Kwanza kabisa nianze na pongezi, natoa pongezi kwa Waziri wa Nishati na Madini, pamoja na Naibu Waziri wamefanya kazi nzuri sana. Naibu Waziri alikuja mpaka kwenye jimbo langu akieleza mpango mzima wa Serikali wa umeme vijijjini. Ukweli katika ziara yake ilikuwa
nzuri sana na wanachi wanakupongeza sana walikuelewa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikinukuu speech za Naibu Waziri ambazo zilieleweka kwa kila mtu. Nilipenda sana usemi wake, alisema masuala ya umeme sio kwamba unapelekwa umeme halafu wananchi wanaanza kuangalia nguzo, kwa sababu tumeona kuna vijiji vingi sana
vinakuwa umeme umepita hasa huu umeme wa Gridi ya Taifa, vijiji vingi sana vinakuwa havijapewa umeme umepita tu pale. Lakini akasema kwamba Serikali itaangalia kwamba vijiji vinapewa umeme, umeme unaenda kwenye nyumba za watu, hiyo niliipemda sana na
akasema kwamba, vitongoji vyote vinapewa umeme, akasema kata zote zitapewa umeme, bahati nzuri sana alisema tarehe 15 Desemba, makandarasi wanaanza kusaini mikataba halafu wanaanza kazi ya Awamu ya III, umeme wa REA vijijini unaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi speech ni nzuri sana, naifurahia sana Serikali kwa mpango mzuri na bahati nzuri katika quotation yake ni kwamba zahanati zote zitapewa umeme, shule za msingi zote zitapewa umeme, vituo vya afya, pamoja na hospitali, hilo ni jambo zuri sana. Sasa niiombe tu Serikali kwa ushauri wangu kama tumepanga mpango umekamilika na tumeshawaambia wananchi, kwa mwaka huu wa fedha ambao tunaingia mwaka 2017/2018 basi tufanye utekelezaji ambao unaonekana kwa wananchi, isionekane tumepiga speech nzuri
halafu hazitekelezeki. Hii itatusaidia sana na wapiga kura wetu watatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kwenye jimbo langu nina kata 16, katika kata 16 ni kata sita tu zina umeme, ina maana kata 10 hazina umeme. Nina vijiji vingi sana, nikianza kuorodhesha hapa naweza nikachukua muda wote kwa kutaja vijiji tu. Sasa kwa sababu Naibu
Waziri alikuja kule aliahidi wananchi, naendelea kuiomba Serikali kwamba vile vijiji vyote vya Jimbo la Mufindi Kusini, ambavyo havijapatiwa umeme kwenye mwaka huu wa fedha angalau katika kata 10 tufikie hata nusu. Wakipata kama kata tano kwa mwaka 2017/2018 kwa kweli
nitaishukuru sana Serikali. Hiyo naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile leo tulikuwa tunajadili kwenye semina vifo vya mama na mtoto, na ni kweli sababu kubwa inaonekana kwenye zahanati na vituo vya afya hakuna umeme. Na unaweza ukaona mtoto amezaliwa labda hajafikia umri wake, mtoto anatakiwa
aongezewe labda oxygen kijijini hauweze kuongezewa oxygen kama hakuna umeme. Imekuwa ni tatizo kubwa sana. Kuna zahanati nyingine wanatumia kule zile taa tunaita koroboi, sasa hilo Serikali lazima iangalie vizuri sana ni tatizo kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili nakuja kwenye masuala ya miundombinu. Kwenye Jimbo la Mufindi Kusini kila siku huwa ninasema, sisi maeneo yetu ni maeneo ya mvua sana, bahati nzuri sana namuomba Waziri wa Ujenzi aangalie sana ahadi ambazo zilitolewa na Rais
na aangalie zile ahadi ambazo ziko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kuna barabara ambazo, upembuzi yakinifu ulishakamilika tayari. Hazihitaji kwamba tunaanza kuandaa upembuzi yakinifu, upembuzi yakinifu ulishakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa mfano kuna barabara hii ya Nyororo mpaka Mtwango pale kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini, kuna barabara kutoka Mafinga mpaka Mgololo, kuna barabara ya kutoka Kasanga mpaka Mtambula. Hizi barabara zimeandikwa mpaka
kwenya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba watatengeneza kwa kiwango cha lami, na kuna sababu sio suala la kutengeneza kiwango cha lami lazima kuwe na sababu kwa nini upeleke barabara kule? Kwenye Jimbo langu la Wilaya ya Mufindi kuna viwanda vingi sana, na
vile viwanda siku zote nasema, Pato la Taifa tunategemea katika viwanda vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Tanzania tumesema Tanzania ya viwanda, kuna viwanda vingine inabidi vifufuliwe au vijengwe vipya. Sisi kule hatufufui viwanda, viwanda viko tayari lakini tuna matatizo ya barabara. Na ninavyoongea saa hizi, mvua kule inanyesha sana, sisi hatuna uhaba wa mvua. Tumepewa neema na Mwenyezi Mungu, lakini zile barabara pamoja kwamba; tumeimarisha kwa kiwango cha kokoto inatakiwa tuweke kiwango cha lami. Bahati nzuri, kwenye Mpango wa Mwaka 2014/2015 upembuzi yakinifu mimi walishakamilisha
barabara ya Nyororo kilometa 40. Sasa naomba kwenye mwaka huu wa fedha ambao ni 2017 tunaounza kesho kutwa, kwenye bajeti ninaposoma nione kwamba tayari Wizara imejipanga kwa ajili ya kujenga ile barabara kiwango cha lami kama ilivyoahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nije kwenye masuala ya mawasiliano. Mawasiliano ndio yanayounganisha nchi, mawasiliano ndio inayounganisha vijiji, kata, na vitongoji. Nakumbuka mwaka 2013/2014 kipindi kile Waziri wa Mawasiliano alitoa taarifa alitupatia na barua kwamba minara ya simu itajengwa kwenye vijiji vile ambavyo hakuna minara ya simu, bahati nzuri na mimi nilipewa. Kuna kata moja ya Idete, ile kata kutoka Mafinga Mjini mpaka uikute hiyo kata ni kilometa 160. Kata ile ina vijiji vikubwa tatu, kuna Idete, Holo na Itika, ni vijiji vikubwa, yaani kijiji hadi kijiji sio chini ya kilometa 40 lakini hakuna mnara hata mmoja, hakuna mawasiliano.
Naomba vijiji vile vipewe mawasiliano kama waziri alivyoahidi wa nyuma; kwa sababu Waziri hata ukibadilishwa wizara, ofisi inakuwepo naomba vijiji vile vya Idete, Holo na Itika viweze kujengewa minara. Na kuna kata nyingine, hii kata ya Ihoanza ambayo hiyo kata tunapakana
na Mkoa wa Mbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kuna vijiji vingine kule kwa mfano kijiji cha Katangwa, Iyai hawana mawasiliano kabisa na makao makuu ya wilaya kwa sababu hakuna minara ya simu.
Naomba na ile sehemu yote ambayo Waziri niliwahi kumpa majina basi apelike huduma hii ya mawasiliano kama alivyoahidi. Hii itatusaidia sana kuhakikisha kwamba huduma kwa wananchi tunafikia kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wanaweza kuugua kijijini kule hakuna mawasiliano hata ya hospitali, wakinamama wengine, wanajifungulia porini au wanajifungulia nyumbani kwa sababu hakuna mawasiliano hata wakipiga simu tukajua kwamba kuna gari inabidi
ipelekwe kule ambulance kutoka Mjini Mafinga ni kilometa karibu 120 na kama hakuna mawasiliano basi tunampoteza mama huyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iwekee mkakati kuhakikisha kwamba sehemu zote nilizotaja zinaweza kujengewa minara ya simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono ila naomba Serikali ifanye utekelezaji, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana hotuba ya Waziri Mkuu kwa sababu imetaja maeneo ambayo Serikali inafanya kazi zake. Kwa kuwa maji ni muhimu kwa maisha ya binadamu Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba sana kuishauri Serikali kufanya ukarabati wa miundombinu ya maji ambayo imeharibika na wananchi wanashindwa kupata maji safi na salama. Jimbo la Mufindi Kusini tuna tatizo kubwa la maji Serikali iliweza kujenga matanki ya kutosha katika Jimbo la Mufindi Kusini lakini matanki hayo hayafanyi kazi sababu ya
miundombinu kuharibika katika Kata za Nyololo, Idunda, Itandula, Mtambula, Ihomasa, Igowole, Kibao na Sawala. Wananchi wanapata shida kubwa ya maji kutokana na kuwa na matanki ambayo hayawezi kuhifadhi maji kutokana na miundombinu mibovu. Nitashukuru sana kama Serikali itafanya ukarabati wa miundombinu hiyo ili wananchi wa Jimbo la Mufindi Kusini waondokane na tatizo hili la maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Umeme, naiomba sana Serikali kupeleka umeme katika Jimbo la Mufindi Kusini vijiji vingi bado havina umeme. Kata ya Idunda ina vijiji vitatu navyo havina umeme. Kata ya Itandula vijiji sita havina umeme, Kata ya kiyowela vijiji vinne havina umeme, Kata
ya Maduma vijiji vitatu havina umeme Kata ya Kasanga vijiji vitatu havina umeme, Kata ya Nyololo vijiji vinne havina umeme. Jumla ya vijiji 48 katika jimbo la Mufindi Kusini havina umeme. Naibu wa Nishati na madini alikuja na kuahidi kuwa Serikali itapeleka umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Afya, naomba sana Serikali kujenga kituo cha Afya katika Kata ya Makungu, Idete, Kiyowela, Luhanga, Mtambula, na Mtwango. Katika kata hizi wananchi wanapata shida kubwa ya kukosa vituo vya afya. Pia tuliomba gari la wagonjwa ambalo litahudumia kata tatu, Makungu, Kiyowela na Idete. Bado hilo gari hatujapata na Serikali iliahidi kutoa hilo gari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze na kuipongeza Serikali. Serikali ya Awamu ya Tano naamini kabisa iko makini sana; na tunaposema utawala bora maana yake ni kutimiza malengo ambayo uliwaahidi wananchi. Nakumbuka katika Mwaka wa Bajeti 2016/2017, naweza nikayakumbuka malengo ya Serikali 14 ambayo yamefanywa na Serikali na yametekelezeka tayari. Kwanza kabisa, lengo
la kwanza, katika ununuzi wa ndege, walisema watanunua ndege sita na sasa hivi kuna ndege mbili tayari ziko zinazunguka Tanzania nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika viwanja vya ndege ambavyo vimefanyiwa upanuzi na Serikali; na usafiri wa anga sasa hivi kila kona wenzetu Watanzania wameanza kusafiri na naomba kutoa ombi kwamba ndege inayotoka Dar es Salaam kuja Dodoma ipite Iringa iende Mbeya ili na
sisi watu wa Iringa tukitoka Dodoma tuweze kupata usafiri wa ndege mpaka Iringa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wengine wameanza kubeza hizi ndege; sisi wa Iringa tunahitaji ndege. Hata kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini tuna viwanja vidogo vitatu, wananchi wale wanataka ndege na wenyewe. Ukienda Ngwazi pale pana kiwanja cha ndege,
ukienda Luhunga pale kuna kiwanja kidogo cha ndege, ukienda Mgololo pale pana kiwanja kidogo cha ndege, tunahitaji ndege na sisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, katika utekelezaji wa Serikali kuhusu elimu bure. Serikali ilisema itatoa elimu bure kwa watoto wa Watanzania wote na imefanya hivyo, hiyo ni hatua kubwa sana. Kama jambo zuri limefanyika lazima tulisifu. Hata kwa Mungu kama unaanza kupiga maombi kwa Mungu wako wewe humsifii Mungu huwezi kupata Baraka hata siku moja, hilo niwaambie kabisa. Kitu kizuri kimefanyika tuseme hiki kizuri kimefanyika, elimu bure tayari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili suala la elimu bure watu wana-mislead, elimu bure sio kwamba ni na kujenga madarasa na mambo mengine, elimu bure maana yake ni ile ada. Watoto kuanzia shule ya awali, shule ya msingi na sekondari wanasoma bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, tatizo kubwa la madawati limepungua kwa asilimia kubwa sana, hata kwenye jimbo langu nilikuwa na tatizo kubwa sana lakini sasa hivi madawati tunaweza tukasema kuna sehemu nyingine wana ziada ya madawati. Watoto walikuwa wanakaa chini sasa hivi wanakaa kwenye madawati.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, tukitaka uchumi wa Tanzania ukue ni kutengeneza miundombinu ikae vizuri. Nimeifurahia sana mipango ya Serikali. Kwa mfano kuimarisha usafiri wa reli ni suala la msingi sana. Barabara zilikuwa zinaharibika kwa sababu zinabeba mizigo mizito. Kwa mfano watu wanasafirisha mbao kutoka Iringa mpaka Dar es Salaam,
kutoka Iringa mpaka hapa Dodoma kwenye barabara hizi za kawaida, za lami, barabara zinaharibika; lakini mpango wa Serikali wa kusema utaimarisha usafiri wa reli ni mpango mzuri mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pale Mgololo kuna barabara ya reli imepita, namwomba Waziri wa Uchukuzi, akiangalie kile kituo cha Mgololo; mbao zitoke pale Mafinga ziende moja kwa moja kwenye kituo cha reli ili waweze kusafirisha kwa njia ya treni ili tusiharibu hizi barabara za lami, ziweze kukaa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ni la msingi sana; tumesema Serikali iimarishe vituo vya afya. Bahati nzuri sisi Wabunge tulipewa semina moja ambayo mimi pia nilihudhuria, ilinisikitisha sana. Inasemekana kwa siku moja akinamama 30 wanakufa kwa ajili ya tatizo la uzazi. Sasa ukichukua 30 ukizidisha mara siku 30 maana yake akinamama 900 wanakufa kwa mwezi mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika takwimu pia walisema watoto 180 wanakufa kwa siku moja, ambayo ni hatari. Sasa nataka niiombe Wizara ya TAMISEMI, suala ya kuimarisha vituo vya afya ni suala la msingi sana. Tukitaka kuepukana na hili tatizo la uzazi kwa akinamama lazima
tuhakikishe vituo vya afya kule vijijini vimekaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri, naishukuru Serikali, nilisikia wanagawa ambulance, ambulance kama mia ngapi zilikuja lakini bahati mbaya sana kwenye jimbo langu sikupata. Kwenye kile Kituo cha Mgololo kuna takriban kata tano zinazotegemea kituo cha afya kimoja lakini hakuna ambulance. Kwenye bajeti yetu ya Halmashauri tulitenga 500,000,000 ili tuweze kununua ambulance tatu, matokeo yake mwaka wa fedha unakwisha lakini zile ambulance hatujanunua.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maswali yangu ya nyuma nilikuwa nauliza kuhusiana na ambulance ya Mgololo na Serikali ilikuwa inaniahidi kwamba watanunua ile ambulance, wataipeleka pale kituo cha Mgololo lakini mpaka leo hawajapeleka. Nitaiomba Serikali kwenye hilo, ili
kuepukana na hili tatizo watupelekee ambulance pale. Tukifikia kwenye Bajeti ya Wizara ya Afya lazima tuiangalie vizuri, tuiongeze ili ikae vizuri tuepukane na matatizo ya zahanati na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine linahusiana na umeme. Bahati nzuri sana Mheshimwia Waziri alitoa hotuba nzuri sana na wana mpango mzuri sana; lakini tumewaahidi wananchi kwamba kila Kijiji kitapewa umeme na wananchi kule wamekaa standby. Niiombe Serikali, kwenye suala la umeme tumesema kila kitongoji, kijiji na kila kaya watapewa umeme. Tunategemea kwenye vijiji, hasa kwenye Jimbo langu, nina vijiji na kata nyingi sana hazijapata umeme; kwamba tutakapomaliza Mwaka wa Fedha wa 2017/2018 vijiji vingi sana vitakuwa vimeshapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kutaja vijiji hapa ni vingi. Kuna kata karibu nane hazina umeme kabisa na ukizingatia Jimbo la Mufindi Kusini ndilo Jimbo linaloweza kuchangia kwenye pato la Taifa asilimia kubwa sana, lakini ukiangalia kwenye miundombinu ya umeme ni duni. Kwa
hiyo, naiomba Serikali kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kama Waziri alivyoahidi, kwamba mpango wa REA kwa mwaka huu wa fedha vijiji vyote vya Jimbo la Mufindi Kusini vitaweza kupewa umeme.
Mhesimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye upande wa barabara. Kuna barabara Serikali iliifanyia upembuzi yakinifu na ilishamaliza. Barabara kutoka Nyololo, Igowole mpaka. pale Mtwango. Upembuzi yakinifu ulishafanyika miaka miwili iyopita lakini sasa hivi hakuna kitu kinachoendelea na Serikali ilishaahidi kwamba itajenga barabara ya lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yale kijiografia mvua zinanyesha kila siku, kwa hiyo magari yanashindwa kusafirisha chai kule. Kuna viwanda ambavyo ni viwanda vikubwa katika East Africa. Ukisema Kiwanda cha Chai katika East Africa lazima uende pale Mufindi, lakini barabara ile ni tatizo na pato kubwa la Taifa linatoka katika kile kiwanda cha Chai Mufindi. Sasa naiomba Serikali, ile barabara ambayo
iliahidi kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, basi iweze kutekeleza ahadi yake hiyo. Bahati nzuri sana hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliwekwa nina imani kabisa watamaliza kujenga ile barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho; niseme kwamba naipongeza Serikali, nasema ikaze mwendo na sisi Waheshimiwa Wabunge tuko nyuma yako ili tuweze kutekeleza ahadi tulizoahidi kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MENDRARD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri kuhusu uharibifu wa mazingira. Binadamu wanaharibu sana mazingira kutokana na kilimo cha mabondeni. Nashauri, Serikali iendeleze kilimo cha umwagiliaji ili kuepusha kilimo cha mabondeni
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufugaji mbovu wa mifugo kwa mfano ng’ombe. Ushauri wangu ni kwamba, wafugaji
waelimishwe ili kufuga ng’ombe wachache kuepusha uharibifu wa mazingira na kusababisha mito kukauka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, carbon trade, naomba Serikali kuhamasisha wananchi kupanda miti kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kulinda mazingira pia ni biashara ya hewa ukaa ambayo itasaidia sana kuinua uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu, wananchi wapewe elimu ya kutosha kuhusiana na utunzaji wa mazingira, kwa mfano waepuke ukataji miti ovyo, kuchoma mkaa na ukataji wa kuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa mipango mizuri ya kuimarisha miundombinu ya barabara zinazounganisha mikoa na mikoa, wilaya na wilaya kwa kujenga kwa kiwango cha lami. Pia naipongeza Serikali kwa kujenga barabara ya kutoka Dodoma – Iringa na Iringa - Mafinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kumalizia kujenga barabara ya Mafinga hadi Chimara; Barabara ya Nyololo hadi Igowole - Kibao – Mtwango (kilomita 40); barabara ya Mafinga hadi Mgololo (kilomita 84) na barabara ya Igowole – Kasanga -Nyigo. Barabara hizi ni ahadi ya Rais pia mipango ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ukurasa wa 71 imeandikwa. Barabara ya Nyololo –Igowele - Mtwango (kilomita 40), upembuzi yakinifu ulishafanyika mwaka 2013/ 2014 na 2014/2015 Serikali iliahidi kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha Lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mufindi tunao mpango wa kujenga Hospitali ya Halmashauri ili kupunguza tatizo kubwa la huduma ya hospitali, naiomba Serikali kusaidia katika ujenzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kumalizia kujenga kituo cha afya cha kata ya Mtwango, kata ya Mninga, kata ya Makungu na kata ya Mtambula. Wananchi pamoja na Mbunge tumejitahidi kujenga majengo katika kituo cha afya cha kata ya Mninga na kata ya Mtwango bado kumalizia. Pamoja na vifaa kama vile vitanda, blanketi, shuka na vifaa vingine ambavyo vipo kwa vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kuleta watumishi katika zahanati za Jimbo la Mufindi Kusini hasa katika zahanati ya Mbalamaziwa, kata ya Itandula, zahanati ya Ihowanza zahanati ya Kibao na zahanati ya Makungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliahidi kuleta gari la wagonjwa katika kituo cha afya cha kata ya Makungu, gari hii litahudumia kata ya Idete, kata ya Kiyowela na kata ya Makungu. Wananchi wa kata hizi wanapata shida sana hasa akina mama wakati wa kujifungua, wanashindwa kufika katika kituo cha afya sababu ya umbali, zaidi ya kilometa 60 mpaka 80 hadi kituo cha afya cha kampuni ya MPM. Naomba sana Serikali kutuletea ambulance kwa ajili ya wanachi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Spika, pongezi kwa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuboresha mfumo wa habari Tanzania, pamoja na mambo mazuri yanayofanyika lakini nipende kutoa ushauri kwa yafuatayo:-

(1) Kuboresha zaidi televisheni ya TBC kwa mfano mitambo ya radio;

(2) TBC kusikika Tanzania nzima

(3) Maslahi ya wafanyakazi; na

(4) Mafunzo kwa wafanyakazi yawepo. Mheshimiwa Spika, kuhusu michezo nashauri:-
(1) Kuboresha viwanja vya michezo katika Wilaya na Mikoa;

(2) Kukuza michezo kwa vyuo, sekondari na shule za msingi;

(3) Vijijini kuna vijana wanaoweza kucheza mipira, riadha na michezo mbalimbali, lakini wanakosa msaada wa vifaa na viwanja vya michezo; na

(4) Viongozi ni tatizo kubwa wapo kwa ajili ya maslahi siyo kukuza vipaji vya michezo.

Mheshimiwa Spika, mwisho naomba mchezo wa ngumi na riadha itiliwe mkazo ili waliletee Taifa sifa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie kwenye Wizara hii muhimu ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Wizara ni ya muhimu sana kwa sababu inagusa uhai wa binadamu. Binadamu ili aweze kutembea, miili yetu lazima itumie maji. Kwa hiyo, tukitamka maji ni muhimu kwa kila mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu cha Mheshimiwa Waziri nimekisoma vizuri sana. Tunaposema maji, kuna wengine wanasema kwamba maji yanaenda kumkomboa mama. Maji tunaenda kukomboa binadamu wote pamoja na wanyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama wakiamka asubuhi saa 12.00 wanamwacha baba nyumbani na familia, wanatembea kilometa nne mpaka tano wanatafuta maji; na baba pale nyumbani anahangaika; kuna akinamama wengine wananyonyesha, anahangaika kuangalia watoto pale nyumbani. Ni shida kubwa! Kuna sehemu nyingine watu wanachota maji kilometa karibu nne kwa kufuata maji mbali na punda. Wakitoka saa 12.00 wanarudi saa 4.00 mpaka saa 5.00 asubuhi. Kwa hiyo, suala la maji ni suala la msingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kusoma kitabu hiki, mimi kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini, kwa kweli wakati nasoma kitabu hiki nimesikitika sana. Mwaka 2016/2017, kwenye bajeti Wilaya yetu ya Mufindi tulipangiwa shilingi bilioni
2.5 na bajeti ile ya mwaka 2016 imerudi kama ilivyo. Mwaka 2016 hatukupata hela yoyote. Kwa hiyo, imerudi ile ile shilingi bilioni 2.5. Kwa Wilaya nzima shilingi bilioni 2.5 tukagawanya Majimbo mawili, ni sawasawa na sifuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna miradi ambayo ina miaka mitano, mpaka leo tunavyoongea haijakwisha. Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri niliwaambia kwamba kwenye Jimbo langu tatizo kubwa, Serikali ilijitahidi sana kujenga matenki ya maji, miaka ya nyuma kama miaka kumi iliyopita. Yale matenki ya maji, yanahitaji ukarabati. Bahati Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Waziri waliniahidi, wakasema watatafuta fedha. Sasa leo nimesoma kwenye bajeti humu, bajeti hii hawajatenga kukarabati miundombinu ya maji katika Jimbo la Mufindi Kusini. Kwa kweli hii ni hatari sana. Kama tutakuwa tunakuja hapa tunatoa ahadi kwa wananchi kwamba miundombinu tutakarabati, lakini tusifanye hivyo, ni hatari.

Mheshimiwa Naibu spika, wanafunzi kwenye Shule za Sekondari na Msingi wanapata shida sana, hakuna maji. Watoto wanatoka na vidumu kutoka nyumbani wanapeleka maji shuleni. Badala ya kwenda kusoma, wanaanza kufuata masuala ya maji. Ukienda kwenye zahanati, kwenye hospitali hata Hospitali ya Mafinga pale mjini, maji ni shida kubwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri, matenki yale ambayo aliahidi kwamba atakarabati, wananchi waanze kupata maji, naomba hiyo kazi aifanye.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitaje matenki ambayo yalitengenezwa na Serikali na miundombinu yake imeharibika. Ukienda Nyororo kuna tenki moja, Igowole kuna tenki la pili, Ihomasa, Mkangwe, Ikangamwani, Kibao, Sawala, Kasanga, Ihawaga, Nanyigwe; sehemu hizi zote matenki yapo lakini maji hamna, miundombinu imeharibika. Kama kweli tuko serious na wananchi tumewaahidi, naomba matenki yale yaweze kutengenezwa wananchi waanze kutumia maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji vya Mufindi Kusini havina maji kabisa. Bahati nzuri mimi Mbunge nimechimba visima pale, lakini Serikali kwenye gravity system bado haijapeleka. Kwa mfano, ukienda Mninga pale hakuna maji, Mkalala, Ihawaga, Luhunga, Lugema, Kiyowela, Idete, Iholo, Itika, Kitasengwa, Itulituli, Kisasa, Ibatu, Mtambuka, hakuna maji vijiji hivi. Halafu napewa shilingi bilioni mbili ambayo ni ya mradi mmoja wa mwaka 2016 au mradi wa kijiji wa Kata ya Mtwanga. Mwaka huu sijapewa hela yoyote. Sasa mimi Mbunge ninayewakilisha wananchi nakuja hapa, naona sijapewa hela yoyote. Hii inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri nimeshamwambia, kwamba kwenye Jimbo langu hujapanga bajeti yoyote na ameniagiza, amesema nimwambie Mkurugenzi waandike proposal waweze kuleta. Ninavyoongea hivi, kama Mkurugenzi ananisikia, kesho aandike proposal hiyo, kesho kutwa nimpe afanye amendment. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sehemu nyingine ukiangalia kwenye kitabu hiki, unaweza ukaona kuna maeneo matano, Wilaya moja imepewa fedha shilingi bilioni 200; mimi napewa shilingi shilingi bilioni mbili. Kweli hiyo inakuja hiyo? Yaani Wilaya moja ukijumlisha hela za wafadhili, ukijumlisha hela za ndani, ukijumlisha na hela nyingine sijui miradi maalum wanapewa wilaya moja shilingi bilioni 200, sisi kule hatujapewa hela. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli tunakuja ndani ya Bunge, tunataka usawa tujadili vizuri, tunaomba miradi ya maji ifuate utaratibu. Hilo litakuwa ni suala la msingi sana, kila wilaya iweze kupewa fedha. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais; alisema kwamba ikifika mwaka 2020 masuala ya maji, asilimia kubwa atakuwa ametatua. Sasa atatatuaje kama wilaya moja ndiyo inapewa fedha nyingi, Wilaya nyingine hazipewi? Hii italeta tatizo kubwa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, katika kugawa fedha afanye analysis vizuri, agawe sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tulisema kila kijiji kitapewa shilingi milioni 50, kwa nini asiseme kila kijiji kitapewa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kutatua masuala ya maji ili tuwe sawa? Kuna watu wengine hapa wanashingilia wamepewa hela nyingi sana; anafika hapa anaanza kushangilia. Mimi nitashangiliaje kama Wilaya yangu hatujapewa fedha? Mimi nitakuwa Mbunge mwenye akili kweli! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja lakini lazima nitamletea Mheshimiwa Waziri proposal ili Jimbo langu la Mufindi Kusini liweze kupewa maji. Kama halitapewa maji, basi nitamwandikia Mheshimiwa Rais, nimwambie mimi hapa nitafanyeje? Sasa katika kuongoza, nitafanyeje mikutano pale kama hakuna maji? Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kusema kwamba Serikali yetu inafanya vibaya. Serikali ina malengo mazuri safi kabisa, lakini Watendaji wanatuangusha katika kugawa mahesabu. Kama wanashindwa, sisi Wabunge tugawe mahesabu kwa kila Wilaya. Haiwezekani wilaya moja ikapewa shilingi bilioni 600, shilingi bilioni 200, shilingi bilioni 100 na wengine wanapewa shilingi bilioni moja au shilingi milioni 500. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Mafinga nimesoma wamepewa shilingi milioni 500. Sasa mwingine anapewa shilingi bilioni 200, hii haiwezekani jamani! Hata kama kiasi ni kidogo, tunajua sawa ni ndogo, tugawane sawa basi! Tunajua kama fedha ni ndogo, hiyo ni collection ya revenue kwa mwaka, hatuwezi kupinga, lakini kile tunachokipata tugawanye sawa kila mmoja aridhike.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake kuwa sekta ya maliasili na utalii ni muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwamba nguzo za umeme ambazo zinazalishwa Sao Hill na mahali pengine ndani ya nchi yetu, zitumike ndani ya Tanzania na nchi nyingine, tuache kununua nguzo kutoka nje wakati tunazo nguzo zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vibali vya upasuaji mbao katika msitu wa Serikali uliopo Wilaya ya Mufindi Sao Hill kipaumbele ni vijiji vinavyozunguka misitu, vikundi vya vijana, wanawake wapewe vibali vya kupasua mbao; viwanda vidogo vidogo vipewe vibali na viwanda vikubwa vipewe vibali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa misitu inahifadhi udongo na vyanzo vya maji, nashauri Serikali kwenye vyanzo vya maji ipandwe miti ambayo inahifadhi maji kwa mfano, Miwengi ni miti ambayo inahifadhi maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo cha mabondeni, Serikali itoe mbadala kwa wananchi ili wananchi waweze kulima na kupata chakula; chakula ni muhimu kwa maisha ya binadamu. Kilimo cha mabondeni (vinyungu) hakuna madhara yoyote ya kukausha maji katika mabonde yetu. Kinachotakiwa ni kupanda miti ya kuhifadhi maji, kilimo cha mabondeni, viazi, miwa, nyanya, mpunga, mboga mboga na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wanapanda miti ili kusaidia kuinua uchumi wao. Mtu akiwa na tatizo anauza miti ili kutatua tatizo ambalo analo. Watu wengi wamejenga nyumba bora kutokana na biashara ya miti; wanasomesha watoto ndani ya nchi na nje ya nchi kutokana na biashara ya miti. Naiomba Serikali iache kuweka vikwazo kwa watu ambao wanapanda na kuvuna misitu yao. Mtu anatunza misitu kwa gharama kubwa ili kupata faida baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu katika haya maeneo mawili Hali ya Uchumi na Bajeti ya Serikali.

Kwanza kabisa nianze kumpongeza Waziri wa Fedha pamoja na Naibu Waziri na cabinet nzima ya Wizara ya Fedha kwa bajeti nzuri mliyoiandaa ambayo Watanzania tunaipokea kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze kwanza na masuala yanayohusiana na jimbo langu ambao kwenye jimbo langu tuna kazi kubwa ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ambayo mpaka sasa hivi Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi hatuna hospitali. Na bahati nzuri sana kwenye kamati zetu za madiwani vikao vya madiwani kwa pamoja tumesharidhia kwamba hospitali hiyo itajengwa katika Kata ya Igowole na bahati nzuri kata ile wameshatoa eneo kubwa sana. Na eneo lile tutajenga Makao Makuu ya Halmashauri pamoja na hospitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri katika fedha zake atusaidie katika ujenzi ule ambao kwenye plan tumeshauanza mwaka huu. Na kama halmashauri tumeshatenga shilingi milioni 100 ambayo inasaidia kuendeleza katika ujenzi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, naiomba Serikali watu wa Mgololo ambao walikuwa wanafanyakazi katika Kiwanda cha MPM watu wale walikuwa wanadai madai yao kati ya Serikali na Mwekezaji; bahati nzuri ile kesi ilienda mahakamani na imeisha na hukumu imetoka. Ninaomba kwa sababu wameshinda na wanatakiwa walipwe kama shilingi bilioni 18, naomba Serikali iwalipe wale wafanyakazi wamepata mateso ndani ya miaka karibu karibu kumi na moja, lakini hatima yake sasa hivi ilishafikia, sasa naiomba Serikali iweze kuwalipa ili wananchi wale watokane na matatizo ambayo wameyapata kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee masuala ya maji, tuna mradi mkubwa sana pale Sawala ambao ni mradi wa Serikali na ni muda mrefu sana, ni miaka sita sasa na mkandarasi tulikuwa tumempata. Yule mkandarasi alijenga matenki ya maji na system ya maji, lakini bado mradi ule haujaisha. Wananchi wa Kata ya Mtwango, Vijiji vya Sawala, Rufuna, Kibao wanapata shida sana ya maji. Na Serikali ilishaahidi kwamba mwaka huu inaweza kutimiza ahadi hiyona ikamaliza. Kwa sababu ujenzi ulianza, naiomba Serikali katika bajeti hii. Bahati nzuri nimeona kwenye bajeti mmetenga shilingi bilioni mbili basi itumike vizuri ili tuweze kumaliza mradi ule na wananchi wa Sawala waweze kupata maji vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pongezi kubwa sana kwa Serikali hii ya Mheshimiwa wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu amefanya vitu vingi sana ndani ya mwaka mmoja. Kila mtu anavijua na bahati nzuri Wabunge wenzangu wamesema mara mbili mara tatu wanarudia rudia na mimi napenda nirudie; kwa mikono miwili nampongeza sana Rais wetu John Pombe Magufuli kwa kazi yake anayoifanya nzuri na sisi Watanzania wote kwa pamoja lazima tumuunge mkono na tumuombe kwa Mwenyezi Mungu aweze kufanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana, kuna watu wengine wanatoa maeneno ya kupinga. Kwanza Rais wetu ni doctor. Wewe huwezi kuwa ukampinga doctor bila reason, lazima uwe na fact za kumpinga. Sasa huyu anaonesha kwa vitendo kwamba tukisema tuorodheshe vitu alivyofanya ndani ya mwaka mmoja kwa mtu mwenye akili timamu lazima atakubaliana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo tu kile cha kuanza kusema elimu bure amefanya na tumeona, kitendo cha kusema kununua ndege amenunua ndege tumeziona kwa macho siyo kwa kuambia tu tumeona kwa macho. Waheshimiwa Wabunge tulikuwa tuna tatizo kubwa sana ya madawati kwa kushauriana Wabunge pamoja na Rais wetu madawati amepeleka kwenye shule zetu na maswali tumepunguza. Mheshimiwa Rais alisema kwamba kujenga majengo pale Universty of Dar es Salaam wanafunzi walikuwa wanapata shida sana mabweni, amejenga. Sasa kuna watu hapa kama hatumpongezi hata Mungu atatushangaa. Lazima tumpe haki yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wakati anaingia madarakani alisema nchi hii ni tajiri, na sisi tunakubaliana alisema ina maziwa, ina mito, ina madini na akasema atadhibiti vizuri ile mianya ya ufisadi amefanya. Sasa mtu anaposisima anapinga maneno haya mazuri na anafanya kwa vitendo itakuwa ni wa ajabu. Juzi hapa tumeona katika ripoti sipendi sana nirudie Watanzania wengi sana tumeshangaa katika ripoti ile, na ripoti kweli imesikitisha kwamba fedha nyingi sana zilikuwa zinapotea lakini sasa hivi ameanza kudhibiti vizuri na bahati nzuri hata wale ambao alikuwa wanahusika na wafadhili wale wawekezaji wanakubaliana kwamba lazima wakae wazungumze lakini sisi lazima tukubaliane nalo. Sasa isionyeshe tena watu wengine wanapinga kitu ambacho kinaeleweka. Na zile hela tukipewa tunajua kabisa tukisema kwamba Tanzania itafikia uchumi wa kati, tukilipwa zile fedha lazima uchumi wa kati tutafikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema nchi hii ni ya viwanda, viwanda haviwezi kujengeka kama hatuna fedha. Lakini bahati nzuri sana ukikusanya mapato ya kutosha unaweza ukapanga mipango na ikapangika na kama huna fedha huwezi ukapanga mipango ikapangika. Lakini Rais wetu anatusaidia kutafuta fedha/vyanzo vya mapato. Hicho ni chanzo cha mapato tayari kwa sababu kudai madeni, kuziba mianya ni sehemu ya chanzo cha mapato cha kukusanya fedha ili tuweze kupata fedha nyingi tuweze kuendeleza miradi yetu ambayo inatukabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi, juzi hapa amesema ujenzi standard gauge, na tukijenga kweli standard gauge Tanzania hii lazima uchumi utakuwa wa kati. Kwa sababu mizigo yote ambayo inasafirishwa kwa njia ya barabara ambayo barabara zinaharibika kila siku, mizingo mizito ikasafirishwa kwenye reli halafu wasafirishaji wa abiria tukasafiri kwenye barabara za kawaida. Barabara zitaweza kudumu wa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nisizitize sana, Serikali imeahidi kupeleka umeme kila kijiji na kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini katika vijiji vyote 88 na bahati nzuri walisema watapeleka katika vitongoji vyote; wamesema watapeleka, naomba Serikali kwenye bajeti hii mwaka 2017/2018 ifanye kama ilivyokuwa imepangwa hili litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye masuala ya maji bahati nzuri Waziri wa Maji alisema tuandike proposal inahusiana na matenki yale nane ambayo yalikuwa bado hayajangwa ambapo lilikuwepo tanki la maji pale Igowole, Nyololo, Itandula, Idunda, Ihomasa na Sawala amesema atamalizia. Naomba afuate kama tulivyomwandikia proposal ile ambayo tumempelekea ili wananchi wa jimbo langu la Mufindi Kusini ili waweze kupata maji bila matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niwashukuru sana wafadhili wanaonisaidia ufadhili maji katika Jimbo langu Mufindi Kusini akiwepo Mr. Fill na Mama Jully mpaka sasa hivi tunavyoongea wako Mufindi, wale wanatusaidia sana kuchimba maji katika Jimbo langu la Mufindi Kusini na sasa hivi wameniahidi kwamba watasaidia kuchimba maji katika shule za msingi na Sekondari.

Kwa hiyo, wawekezaji hawa mimi nawapongeza sana na nawaomba Wizara ya Maji iwa-support hawa wafadhili. Pale wanapohitaji msaada basi watoe msaada ili waweze kupata moyo kuendelea kutoa msaada wa maji katika nchi yetu ya Tanznaia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naunga mkono bajeti ya Serikali kwa asilimia mia moja kwa sababu ni bajeti ambayo inaeleweka, kila mmoja anai-support na sisi tunawaombea kwa utekelezaji mwema, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu na mimi kupata nafasi, ili niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na kuipongeza Serikali, katika miaka miwili Serikali imefanya mambo makubwa sana na Wabunge kwa macho yetu kwa masikio yetu, tumesikia na tumeona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopanga mpango wa miaka ya mbele lazima uangalie miaka ya nyuma umefanya nini. Serikali miaka ya nyuma tukichukua reference kwa kweli, imefanya kazi nzito sana na mambo yanaonekena. Nikianza kutoa mifano, Serikali ilipanga kununua ndege na kweli ndege imenunua. Serikali ilipanga kutoa elimu bure na kweli kazi hiyo imeanza kutoa elimu bure kwa watoto wetu. Serikali ilipanga kupanua Bandari ya Dar es Salaam na kweli Serikali inapanua Bandari ya Dar es Salaam. Serikali ilipanga kujenga bomba la mafuta kutoka Tanga mpaka Uganda, Serikali inafanya na tunaona na tunasikia. Serikali ilipanga kununua meli kule Bukoba na Mheshimiwa Rais tumeona hata juzi akisema pale, tunaona Serikali inafanya. Serikali tunaona kila inachopanga na inasema, tulipanga hiki tumefanya moja, mbili, tatu, ndiyo utekelezaji tunaoutaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kweli, anasimamia vizuri. Ndiyo maana nataka tuende kwa data, ameahidi nini amefanya nini na anasema kila mmoja tunaona kitu kinachofanyika. Leo, sasa Serikali imeleta mapendekezo ya mpango, yaani Wabunge tutoe mapendekezo, sio tulaumu, tutoe mapendekezo tunataka nini. Sasa na mimi nataka nitoe mapendekezo yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nimesoma vizuri mwongozo, nimesoma vizuri mapendekezo ya Serikali ambayo imeleta kwa Wabunge tutoe mapendekezo. Kuna maeneo ambayo lazima tupendekeze ili Serikali ikae vizuri na Serikali ili ifanye kazi vizuri lazima iwe na fedha. Bahati nzuri Serikali imesema kuna mapungufu kidogo katika ukusanyaji wa kodi, hiyo na mimi nakubaliana kabisa, sasa tunafanyaje? Naomba niishauri Serikali, kwenye eneo hili lazima tuhakikishe kwanza tunatoa elimu ya kutosha kwa walipa kodi wetu ili mtu anapolipa kodi asione kama adhabu, aone kama ni hiyari yake kutoa kodi bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kinachotakiwa ni kutoa elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara, hilo la kwanza. Pili, vitendea kazi lazima viwepo. Kwa mfano, sasa hivi wafanyabiashara wengi zile mashine ambazo tunatumia kwa ajili ya kukata risiti mashine zile hazipo, bado ziko chache wengine hawana, nyingine wanasema mbovu. Kwa hiyo, hatuwezi kukusanya mapato kama vitendea kazi bado havieleweki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, sasa hivi ukusanyaji kodi sio lazima uende TRA, naomba Serikali itafute mfumo mzuri, wewe unaweza hata ukawa barabarani unatembea ukatumia hata M-Pesa ukalipa kodi. Kwa mfano, kama wewe ni mfanyabiashara au kama wewe mtu una magari yako kwa mfano hata insurance, kama mtu anataka kulipa insurance siyo lazima aende TRA au aende wapi, analipa kwa njia ya M-Pesa tu. Kwa hiyo, nataka niseme hivi tuhakikishe kwamba tunaweka vitendea kazi vimekaa vizuri kwa walipa kodi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la msingi sana, nimeona kwenye taarifa ni uvujaji wa mapato. Hii ni njia ambayo Serikali inaweza kuidhibiti na bahati nzuri mnajitahidi sana kudhibiti mianya, zile njia za panya, njia za nini sasa hivi hazipo zimepungua sana naipongeza. Na mimi naiomba Serikali iendelee kutafuta mbinu kuhakikisha kwamba, kile kiasi ambacho kinakusanywa kinatumika vizuri, hakivuji, hakuna mianya ile ya uvujaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naipongeza Serikali kwenye Wizara ya Afya. Wizara ya Afya hata Mheshimiwa Ummy leo amejibu swali hapa vizuri sana kwamba Wizara ya Afya zamani ilikuwa na uwezo wa kupewa shilingi bilioni 29, lakini sasa hivi tuna uwezo wa kuipatia Wizara ya Afya shilingi bilioni 296 kama sijakosea, ni kiwango kikubwa sana. Katika hiyo, tumekwenda vizuri, katika fedha hiyo bahati nzuri Serikali imeangalia kwamba umuhimu wa watu lazima tuwe na afya nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe msisitizo, Serikali ihakikishe kwamba vituo vya afya vijijini vinamaliziwa kujengwa, kuna maboma mengi sana, bado hatujamaliza vituo vya afya. Kuna zahanati, tuna maboma ya zahanati bado hayajaisha nchi nzima, lazima tujitahidi tuhakikishe kwamba kwenye sekta ya afya tunapeleka fedha za kutosha na bahati nzuri kwenye mpango umeongea, lakini bajeti inayokuja kwa sababu tunaongelea mpango halafu tunakuja kuupangia bajeti. Naomba kwenye sekta ya afya tuangalie tumeipatia fedha ya kutosha kwenye bajeti inayokuja na mpango ueleze vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya maji. Sekta ya maji vijijini naiomba Serikali, bado iongeze nguvu kubwa sana. Kwa sababu hata kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini wananchi wanapata taabu sana ya maji, lakini katika mpango, bahati nzuri Waziri wa Fedha ameeleza vizuri kwamba, ataiangalia sekta ya maji, naomba aiweke kipaumbele zaidi. Tuhakikishe kwamba miundombinu yote ya maji, kama kuna matenki, kama kuna visima, tuhakikishe kwamba wananchi wana uwezo wa kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya leo hii mwananchi hawezi kutembea kilometa 10, kilometa 20. Kuna sehemu nyingine nimeona watu wanachota na punda kilometa ngapi, hayo ni mambo ya zamani sana, naiomba Serikali ihakikishe kwamba sekta ya maji imekaa vizuri, wananchi wetu wapate maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye sekta ya umeme, bahati nzuri umeme vijijini Serikali imekaa vizuri na wameshafanya survey tayari kwenye vijiji vingi. Hata kwenye Jimbo langu la Mufindi Kusini wamekuja, tumeona wamefanya survey na Serikali imeahidi, imesema kila kitongoji kitapata umeme na kila kaya itapata umeme. Tumeona hatua zimeanza kufanyika, lakini nataka niiombe Serikali, tuhakikishe kila tulichopanga tunatengeneza time frame, tusije tukaahidi halafu tukachukua muda mrefu sana, kwa sababu sasa hivi tunaweka na muda, ukiahidi kitu lazima kuwe kuna progress ya kazi, lakini bahati nzuri kwenye vijiji vyetu mmenza tayari, survey imeshafanyika, sasa tunategemea Serikali ianze kupeleka nguzo katika vijiji vyetu na katika mitaa yote ambayo imeshapimwa tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee tena suala lingine ambalo ni la muhimu sana. Wenzangu wameshaongea, hasa Wabunge wanaotoka Rukwa ambalo ni suala la kilimo hasa kilimo cha mahindi inaonekana bado kuna tatizo na tatizo tunaongelea ni soko. Nafikiri kuna kilimo cha matumizi ya chakula, kuna kilimo cha biashara. Kwa mfano, nataka nikwambie Tanzania bahati nzuri kila mikoa imepata neema, ukienda Kaskazini wenzetu utakuta wanaongelea labda karafuu, ukienda Magharibi huku utakuta wanaongelea masuala ya pamba, ukienda Kusini wanaongelea masuala ya korosho, ukienda mikoa ya Rukwa Kusini tena wanaongelea masuala ya mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kwenye korosho Serikali inaweza ikatafutia soko korosho na ika-subsdise fedha. Kama kwenye pamba Serikali inaweza ikapeleka fedha kwenye pamba, basi ipeleke fedha hata kwenye kilimo cha mahindi ili watu wa mahindi waweze kuhakikisha kwamba kilimo kinaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuambie kitu kimoja, Tanzania ni nchi ambayo inategemea zaidi kilimo cha mahindi kuliko kilimo kingine. Nitoe ushauri kwamba kama Serikali itashindwa kununua mahindi ya wakulima, mahindi yakaozea kwenye maghala basi iruhusu ifanye open market, kama kuna uwezekano wa watu kuuza nje, wauze nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nataka nikumbuke Mheshimiwa Rais alisema vizuri sana, kwamba tusiwagandamize wakulima wa mahindi. Kama debe litauzwa hata shilingi 100,000 basi liuzwe laki moja ili mkulima apate. Wewe kama unaona unashindwa kununua basi lima. Na sasa hivi bahati nzuri mvua zinanyesha sehemu kubwa sana, lakini isionekane kwamba wakulima wa mahindi hatuwa-support, tuwape uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba inaweza ikatokea njaa, tuwafundishe jinsi ya kuhifadhi mahindi, lakini tusiwafundishe kuuza kwa bei ndogo ili wapate hasara, wakulima wanalalamika. Tuseme wahifadhi mahindi, lakini wawe wanaweza kulima zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimeliona, hili naipongeza Serikali kwa upande wa mbolea, Serikali imetoa bei elekezi kwa wafanyabiashara, imesimamia vizuri na imefanya vizuri sana. Sasa hivi wakulima wana uwezo wa kununua ile mbolea lakini ukienda kwenye Mjimbo yetu mbolea bado haijafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Jimbo la Mufindi Kusini hata Wilaya ya Mufindi sasa hivi ndio tunalima lakini mbolea ya kupandia haipo. Naomba Waziri wa Kilimo atusaidie kwenye hili, mbolea ya kupandia ifike miezi hii; miezi hii Mufindi kule ndio tunalima sasa hivi. Mbolea ya kupandia ukileta mwezi wa 12 hatuwezi kuoandia mahindi, tutakuwa tumeshachelewa, tunaenda na muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sanaSerikali kwa upande wa kilimo ihakikishe kwamba mbolea inafika kwa muda unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu gesi; hili suala la gesi kwanza ni neema. Tumepata neema kubwa sana kwamba uchumi wa nchi ili upande tumefanikiwa kupewa gesi na gesi inatoka Mtwara lakini ili gesi ipate soko ni lazima tupanue wigo. Kama kuna viwanda vinatakiwa kutumia gesi basi tuwaruhusu watumie gesi iliSerikali iweze kukusanya hela nyingi sana na fedha nyingi sana tunaweza tukapata kutoka kwenye masuala ya gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vingi kwa mfano mikoa ya Pwani hiyo nimeona wamejenga viwanda vingi sana. Sasa vile viwanda kama havitatumia gesi, tutazalisha gesi nyingi halafu tunasema soko tunashindwa kumbe viwanda vile havitumii gesi. Naiomba Serikali basi ihakikishe kwamba viwanda vyote vinatumia gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hata Mufindi tuna viwanda vingi sana, kama kweli mtatuletea gesi na viwanda vya Mufindi, kwa mfano tuna Kiwanda cha Chai kikubwa sana, katika Afrika nadhani ni kiwanda cha kwanza, tuna Kiwanda cha Karatasi, katika Afrika nadhani ni cha kwanza na tuna viwanda vya mbao. Vile viwanda vyote vikitumia gesi, nadhani gesi itapata soko kubwa sana na Serikali itakusanya mapato makubwa na bajeti tuliyopanga ya mwaka 2018/2019 tumesema Serikali itakusanya shilingi trilioni 32.47. Sasa hizi shilingi trilioni 32 kama hatutapata revenue kutoka kwenye gesi, tutapata wapi? Tukitaka kufanikiwa makusanyo makubwa lazima tuhakikishe tunafanya makusanyo makubwa kwenye gesi, tunaweza kufikisha hilo lengo la shilingi trilioni 32.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhakikishe tunakusanya mapato kutoka kwenye madini, tutapata hizo shilingi trilioni 32, tunapata mapato kutoka kwenye maliasili na utalii tunaweza kufanikiwa. Kama hatutakusanya kwenye vyanzo vikubwa tukategemea kwamba tutakusanya kutoka kwenye sigara, vinywaji maana kwenye vinywaji ndiyo tunapandisha hata bei, hii hatuwezi kufikia lengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuhakikishe kwamba kwenye vyanzo vikubwa kwanza vile tunakusanya mapato ya kukamilika halafu tunakuja kwenye vyanzo vidogo. Ukisema kwamba labda utategemea minada ya kuuza haya masoko ya pembeni ya wakulima wadogo wadogo hii haitasaidia. Tuhakikishe kwamba tunakusanya kutoka kwenye vyanzo vikubwa ili tufikie lengo tulilojiwekea la shilingi trilioni 32.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upande wa wafugaji na wenyewe lazima waheshimiwe sana. Kuna sehemu nyingine nataka nimshukuru Waziri wa Mambo ya Ndani, sasa hivi ule ugomvi wa wafugaji na wakulima umepungua sana, naipongeza sana Serikali, ni jambo zuri sana hilo, sasa hivi hatujasikia malalamiko makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali isimamie vizuri kuhakikisha kwamba wafugaji wanalindwa kwa sababu na wafugaji lazima tuwaheshimu, wanafuga ng’ombe na tunapata nyama, bila nyama hatuwezi kuishi. Ukiangalia katika Afrika nchi ya kwanza kwa ufugaji nadhani ni Ethiopia kama sikosei na ya pili ni Tanzania, kwa hiyo lazima tuwaenzi. Lazima kuwe kuna mpangilio mzuri ili isitokee kugombana kati ya wafugaji na wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali naona kwenye hilo imefanikiwa na sasa hivi inakwenda vizuri na huo mpango wa kudhibiti wafugaji na wakulima ili waende vizuri. Wafugaji wafuge mifugo hatuwakatalii, wakulima na wenyewe walime kama inavyowezekana, hii itakuwa ni vizuri sana na watu watakuwa na maisha mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapa, nakushukuru sana. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Wizara ya TAMISEMI na Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hizi ni nyeti sana kwa sababu ni Wizara ambazo zinaleta maendeleo ndani ya nchi yetu. Kwanza kabisa nitoe pongezi kubwa kwa Mheshimiwa Rais wetu John Pombe Magufuli kwa kazi yake nzuri anayoifanya. Pia nitoe pongezi kwa Mawaziri wote kwa ujumla wake, sana kwa Mawaziri hawa wa Wizara ambazo tunazijadili leo hii. Mheshimiwa Waziri Jafo kwa kweli kazi unafanya vizuri na Naibu Mawaziri wote wawili kazi wanafanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wakuu wa Mikoa nawapa pongezi sana kwa sababu nikitoa mfano, Mkuu wangu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina Masenza anafanya kazi nzuri sana nampa pongezi. Vilevile DC wetu pamoja na Mkurugenzi wetu, wote wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema utawala bora lazima tuwe makini sana. Kwanza wewe unayejadili utawala bora lazima ujipime. Kwa mfano, hawa watu niliowataja ukiangalia profile yao imesimama iko vizuri na wanafanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo, kwenye utawala bora binafsi naona wamekaa vizuri na nchi hii inapiga hatua na tukisema uchumi unakua ni kwa sababu ya utawala bora, kama utawala bora haupo uchumi hauwezi kukua, lakini sasa hivi Tanzania uchumi unakua na sasa tunakwenda 6.8, tuko mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya niliyochangia kwenye utawala bora, naishukuru Serikali kwa upande wa afya kwa kweli wameenda vizuri sana. Nikichukua kwa ujumla wake katika Wilaya yangu ya Mufindi tunaenda vizuri. Serikali imeangalia sana vituo vya afya na wameangalia Tanzania nzima, lakini wamekuja mpaka Wilaya ya Mufindi. Kwenye Jimbo langu la Mufindi wameleta milioni 400 na mpaka sasa hivi kituo cha afya cha Malangali kinatengenezwa vizuri sana na wananchi wanaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili tunajenga hospitali ya Wilaya ya Mufindi ambayo sasa hivi Serikali imeshatutengea 1.5 billion kwa ajili ya kujenga hospitali ya Wilaya. Tunawapa pongezi kubwa sana, naiomba Serikali tukimaliza ile hospitali ya Halmashauri, naomba ile hospitali ya Wilaya ambayo iko Mafinga basi tuifanye Hospitali ya Rufaa. Tukifanya hivi wananchi wanaweza wakatibiwa vizuri, tukiwa na hospitali ya rufaa tunajua huduma zitakuja zitakuwa nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye mpango, kwamba mna mpango wa kuboresha vituo vya afya vyote Tanzania nzima vikiwepo na vile vya Mafinga vya Wilaya Mfindi. Jana wakati nauliza swali la msingi niliuliza Vituo vya Afya vya Mninga na Mtwango pale. Bahati nzuri Serikali imejibu vizuri imesema tayari vifaa wameshaandaa na wamesema kufikia mwezi wa Tano watakuwa wameshamaliza, hiyo ni juhudi nzuri sana ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vizuri vinavyofanyika lazima tupongeze ukidharau na kile kizuri wewe tayari unafanya dhambi, binafsi naipongeza sana Serikali na Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Selemani Jafo, nakuomba sana hivi vituo vya afya ambavyo tayari na fedha unayo na mipango imekaa vizuri, basi umalizie kama ulivyosema mwezi wa Tano utakuwa umemaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee kidogo kwenye suala la viwanda, bahati nzuri Wilaya ya Mufindi tuna viwanda vingi sana, lakini tuna kero moja ya ukusanyaji wa kodi TRA pale. Mfanyabiashara anatakiwa alipe kodi lakini asidharaulike, hivyo, wakusanyaji wanaokusanya kodi wasiwadharau wafanyabiashara. Kuna kitu kinaitwa lugha ni kitu kidogo sana, ukienda kukusanya kodi ukisema kwamba asipolipa kodi labda utamfungia biashara yake tayari unamkatisha tamaa. Naiomba Serikali watu wanaotoa lugha mbaya kwa wafanyabiashara wasifanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine tunajua tuna viwanda vingi, bahati nzuri naipongeza Serikali na Mheshimiwa alikuwa anasema kule Mkuranga kuna viwanda karibu 80 na Mufindi tuna viwanda vingi tena ni viwanda vikubwa, tukitaja viwanda kuna viwanda vingine ni vikubwa. Kuna kiwanda kimoja mimi sijakipenda sana, kuna hiki kiwanda kinachochinja wanyama wanachinja sana punda, hiki kiwanda sijakipenda. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wanyama ambao wanatumika kwa binadamu kwa kazi za binadamu za kila siku, punda anatumika kubeba mizigo, punda anatumika katika kulima, lakini kwa nini tena punda uanze kumla? Hiyo sijaipenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka miaka ya nyuma Wahehe walikuwa wanachinja mbwa, lakini baada ya kugundua kwamba mbwa ni askari wa kulinda usiku wakaacha kumchinja. (Makofi/Kicheko).

Mheshimiwa Mwenyekiti, utamaduni wetu hatujazoea kuchinja punda, naomba punda wasichinjwe waachwe, kile kiwanda cha punda tusifuate Wachina, kama kwao wanachinja basi wawe ni Wachina, lakini kwetu huku tuna viwanda vingi ambavyo vinaweza vikatuingizia hela nyingi, tuachane na viwanda vya punda hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji, Waziri wa Maji nakupongeza sana alikuja kule Mufindi alifanya kazi moja nzuri sana. Ile kazi kwanza Wabunge na Madiwani alitupatia semina Waziri wa Maji ilikuwa nzuri sana. Bahati nzuri tukagawanya fedha tukasema kwamba ile Kata ya Nyororo sasa ipate maji ya gravity kwa sababu tulikuwa tunachimba tu visima na akasema tuachane na visima sasa maji ya bomba yatakuwepo, mlolongo ulikuwa mzuri sana pale Igowole tukafanya vilevile na mradi wa Sawala tukafanya vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Maji sasa kwa sababu fedha zipo, naomba usimamizi uende speed kwa vile tulisema kufikia mwezi wa Sita na Saba ile miradi itakuwa imekamilika. Sawala Mkandarasi yuko site, lakini bado speed ile ndogo sana, kwa sababu manunuzi tu yanachukua karibu miezi miwili. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa sababu system ya maji na vituo vya afya viko kwako tunaomba usimamizi wa maji ukae vizuri kama tulivyokuwa tumeahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya barabara hasa zile za vijijini. Barabara tumepeleka TARURA lakini usimamizi bado unalega sana kwa sababu zamani kwenye Halmashauri tulikuwa na mpango kila mwaka barabara zinatengenezwa, unaweza ukaona labda tumepanga barabara tano, kwa mfano pale Mafinga Wilaya ya Mufindi tuna Majimbo matatu kwa kila Jimbo kila mwaka kwa mfano kwa Mheshimiwa Mgimwa zilikuwa zinawezekana kutengenezwa hata barabara tano, kwenye Jimbo langu la Kusini zikatengenezwa barabara hata tano, lakini sasa hivi kwa mfano kwangu inatengenezwa barabara moja tu.

Naomba sasa kuna barabara ya Maguvani inakuja Mtambula mpaka Kilolo, imeharibika haipitiki kabisa na iko TARURA naomba ile barabara itengenezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna inatoka hapa Sawala inaenda Kata ya Luhunga mpaka kule Iyegelo, ni mbovu na maeneo yale kuna wakulima wa chai, wanashindwa kusafirisha chai, naomba ile barabara itengenezwe. Inaanzia Sawala inaenda kata ya Luhunga mpaka Iyegelo kuna wakulima wamekamilika, ni wafanyabiashara wazuri sana, sasa naomba TAMISEMI isimamie ile barabara iweze kutengenezwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine tuna ujenzi hospitali kubwa, bahati nzuri Serikali niipongeze mlishatutengea 1.5 bilioni, tunategemea mwaka huu tunaanza kujenga ile hospitali na niliomba ramani, mkitupatia mapema sana nategemea haiwezi kuchukua mwezi mzima kutafuta ramani tu, hiyo just a week labda wiki mbili, tatu ili tuanze ujenzi, wananchi kule wamelipokea vizuri sana, Wilaya ya Mufindi nzima wamewashangilia, wakati Waziri anajibu swali waliwashangilia sana wananchi kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameshaleta proposal tayari kwa Wabunge, wamesema ile hospitali ikijengwa basi hospitali ya Mafinga itakuwa Hospitali ya Rufaa na Mheshimiwa Mgimwa Mbunge wa Jimbo la Kaskazini tulikuwa tumekaa tumejadili kwamba ile hospitali tukikamilisha itasaidia Wilaya nzima na hospitali ya Mafinga tutawapunguzia idadi ya wagonjwa kutibiwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chumi kila siku analalamika hapa anasema ile hospitali inazidiwa, lakini kama hospitali ya Mafinga kwa mfano wagonjwa wale wakatibiwa kwenye hospitali hii ambayo tunajenga na hospitali ya Mafinga ikawa Hospitali ya Rufaa na ikaongezewa huduma tukapata Madaktari, basi Majimbo haya yatakuwa yamekaa vizuri na Wilaya nzima itakuwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali imepanga vizuri sana kwamba watatuletea fedha, lakini fedha zije haraka, bahati nzuri wananchi wa Wilaya yetu ni waaminifu sana walitoa eneo bure bila compensation, walitoa bure wakasema kwa sababu tunajenga hospitali, basi ngoja tutoe eneo, tumepewa tayari kubwa. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwenye hilo kwamba itasimamia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niongelee suala la umeme. Kwanza Serikali imefanya vizuri sana, watu wa REA wako speed na bahati nzuri wamezunguka katika Majimbo yote. Jimbo la Kaskazini wameenda kwa Mheshimiwa Mgimwa, kwangu Kusini kule wamekuja, katika vijiji vyote wanafanya vizuri, lakini kuna changamoto moja imejitokeza; wale wataalam wakifika pale kufanya survey walikuwa wanaishia sehemu; wanaonesha kwenye vitongoji vingine walikuwa hawendi, kwa hiyo kuna vitongoji bado havijafanyiwa survey. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wabunge tutaandika vitongoji vyote ambavyo hawajafanya survey ili tukuletee Waziri wa Nishati aingize kwenye ule mpango wa REA ili viweze kupewa, bahati nzuri Waziri wa Nishati yuko vizuri, hotuba zake huwa nazifuatilia vizuri sana na anafanya ziara kila Jimbo hata kwangu alishakuja pamoja na Naibu wake, wote wawili wako vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia speech zao ukizisikiliza ziko vizuri, walisema kwamba siyo issue ya kuweka nguzo watu tukaangalie nyaya walisema ni issue ya kupeleka kwenye kaya, tuone nyumba by nyumba zina umeme na wananchi nimeshawaambia nitapita kila nyumba nione kuna umeme unawaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja kwa mikono miwili. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na pongezi, Serikali inafanya vizuri sana. Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Mawaziri wanafanya kazi vizuri sana. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ushauri kidogo. Kila mwaka tunasoma hiki kitabu, bahati nzuri kitabu kinaandikwa vizuri sana, lakini kuna barabara ambazo zinafanyiwa upembuzi yakinifu kila mwaka na kuna barabara nyingine zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu, imeshapita hata miaka mitatu, minne lakini ujenzi bado haujaanza. Nataka niishauri Serikali, kwa barabara zile ambazo zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu, naomba zianze kujengwa sasa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, barabara ile ya Mafinga mpaka Mgololo, barabara ya Nyololo mpaka pale Mtwango, upembuzi yakinifu ulishafanyika toka mwaka 2013, ulishakamilika. Kwa hiyo, ujenzi bado. Mheshimiwa Waziri, naomba hiyo barabara kwa sababu Serikali iliahidi kwamba itajenga kiwango cha lami na ukizingatia kule kuna viwanda vingi sana, naomba ianzwe kujengwa kwa kiwango cha lami kama ilivyokuwa imeahidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara moja kubwa ambayo inatoka Mafinga kwenda Igawa, naishukuru sana Serikali imeanza kuitengeneza barabara hiyo vizuri sana.

Naiomba Serikali, ile barabara kuna sehemu naweza nikasema inapita kwenye vijiji vikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, pale Nyololo pana wafanyabiashara wengi sana, wanafanya biashara kuanzia asubuhi mpaka usiku. Sasa naomba wakitengeneza pale, ile barabara iwe pana halafu itengenezwe kama stendi, halafu ziwekwe na taa za barabarani kwa sababu pale pana wafanyabiashara wengi sana, itawasaidia sana wafanyabiashara wa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu naiomba tena Serikali kwa barabara hiyo hiyo, nadhani hata Mheshimiwa Rais atakuja kuifungua ile barabara. Pia pale Mbalamaziwa ni sawa na Nyololo, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri pale Mbalamaziwa basi patengenezwe stendi kubwa ambayo iko ndani ya barabara ili magari makubwa yanapopaki pale ajali zipungue, kwani kuna ajali huwa zinatokea mara nyingi sana. Kwa hiyo, naomba stendi ziimarishwe, zitengenezwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sehemu nyingine kuna vijiji vinaingia kwenye barabara, sasa kuna stendi ndogo; naomba na zile stendi ndogo basi zioneshwe vizuri ili tuhakikishe kwamba kwenye stendi ndogo ili kupunguza ajali, basi tupanue zile barabara ziwe pana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo la Mufindi Kusini kuna barabara ambazo ni za TANROADS. Zile barabara kwa kweli Serikali inatengeneza vizuri sana na ukizingatia kule Mufindi tuna mvua nyingi na tunaenda kwa kalenda; kuanzia mwezi wa Sita huu mpaka mwezi wa 12 barabara ndiyo zinatengenezwa. Sasa naomba ile bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 ambayo inaishia, naomba basi zile barabara za TANROADS zianze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, barabara ya kutoka Nyololo mpaka pale Mtwango ambayo Serikali iliahidi kwamba itajenga kwa kiwango cha lami, lakini itaendelea kuboresha kwa kujenga kiwango cha changarawe mpaka pesa itakapopatikana, basi mwaka huu mwezi wa Sita tuanze kuitengeneza ikae vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kutoka pale Mgololo inaenda mpaka Nyigo inapitia Nyihawaga na yenyewe ni barabara ya TANROADS, naomba basi Serikali na yenyewe ianze kuijenga. Kuna barabara ya kutoka Mbalamaziwa mpaka kule Kwatanga ni barabara ya TANROADS, naomba ianze kutengenezwa. Kuna barabara ambayo nairudia tena ya kutoka Mafinga hapa mpaka pale Sawala, imeharibika sana, naomba ianze kutengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utengenezaji wa barabara, naomba twende kiutaalam, ile mifereji (outlets) ya kutoa maji itengenezwe kiwango kizuri, kama kuna uwezekano tuweke hata kiwango cha kokoto ili maji yaweze kupita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na barabara zile za Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA). Kuna barabara kwa mfano kule Idete bado hazijatengenezwa kwa viwangovizuri. Kuna barabara ya kutoka Luhunga mpaka kule Iyegeya, haijatengenezwa vizuri. Kuna barabara ambayo inatoka Maguvani mpaka pale Mtambula mpaka Kasanga, wananchi wanalalamika sana ile barabara. Naomba sana waweze kuitengeneza ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni mawasiliano. Serikali iliahidi kwamba itajenga mnara katika Kata ya Idete, Kata ya Maduma, Kata ya Kasanga, pale Udumuka hakuna mawasiliano kabisa na pale Kiyowela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua mawasiliano ni ya muhimu sana. Sasa katika kata hizi nilizotaja, mawasiliano hakuna kabisa. Naomba Serikali kama ilivyokuwa inaahidi iweze kujenga minara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, naipongeza sana Serikali. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuongea machache.

Mheshimiwa mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuipongeza Serikali kwa mipango mizuri kabisa. Tunapojadili kuhusu maji tunajadili maisha ya watu na unapojadili maisha ya watu hakuna utani lazima tuwe serious, tufanye kazi na lazima tutekeleze kile ambacho tunakijadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Maji ni Wizara muhimu sana katika Wizara zote. Katika Wizara zote wananchi pamoja na Wabunge tunaweka macho kwenye Wizara ya Maji. Maji vijijini na mijini kama hakuna maji hakuna maisha. Tunasema maji ni uhai na tunapoesema maji ni uhai maana yake mwananchi lazima apate maji na tunaposema kumtua mama ndoo kichwani na iwe ni ukweli tunaitua hii ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, tukipanga bajeti ya maji na fedha lazima tuwape kama tulivyopanga. Ni vigumu sana Serikali ikiwa inapeleka kwenye Wizara hii fedha kidogo sana halafu miradi haiishi kwa muda unaotakiwa. Kuna wakandarasi wengi wako site mpaka sasa hivi hawajapata pesa, wanashindwa kutekeleza miradi ya maji kwa sababu fedha hawajapata, kwa hiyo, niiombe Serikali tuache mambo mengine yote, lakini tuhakikishe kwamba miradi ya maji inaisha kwa muda unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Mufindi Kusini kuna Mradi wa Maji Sawala unakwenda karibu mwaka wa 12, bahati nzuri sana leo Waziri nimeongea naye, Mawaziri wote wawili, Katibu Mkuu nimeongea nae pia, kwa kweli nilikuwa nimepanga tofauti lakini kufuatana na mazungumzo tuliyoongea naishukuru Serikali kwa mazungumzo tuliyofanya leo. Wamenihakikisha kuwa Mwezi Mei huu fedha zitapelekwa kule kwenye Kata ya Mtwango, kuhakikisha Mradi wa Sawala unatekelezwa kama ulivyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu kubwa mradi wa shilingi milioni 800 au mradi wa shilingi bilioni mbili unachukua miaka sita, saba ni aibu! Bahati nzuri sana Waziri tulienda siku ile kwenye Kata ya Mtwango tukasaini mkataba mbele ya wananchi. Wilaya imeleta maombi toka mwezi wa Machi mpaka leo hawajapata fedha na tuliwaahidi wananchi. Kwa vile Waziri leo umeniambia maneno mazuri ndiyo maana naipongeza Serikali kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine katika Jimbo la Mufindi Kusini kuna tatizo kubwa sana la maji, kuna matenki ya maji kule karibu Kata 11, matenki yapo Serikali ilijenga kwa ushirikiano na wananchi, miaka ya nyuma miaka ya 1980 ni ukarabati wa miundombinu. Mimi Mbunge nimeleta maombi mara nyingi kwamba kule siyo miradi mipya, ni miradi ambayo inatakiwa kufanyiwa ukarabati lakini hatufanyi hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali kwenye Kata ya Igowelo, wananchi wanapata taabu sana ya maji, matenki yapo na sources za maji zipo, ni ukarabati wa miundombinu, naomba sana Serikali Igowelo pale ipeleke maji. Ukienda pale Nyololo bahati nzuri Waziri unapita kila siku pale, siku nyingine nenda pale shuka omba maji kama watakupa maji pale, maji hayapo, tunatumia maji ya visima tu ndiyo vinatusaidia vingine visima vile vya kienyeji, wakati tuna mabwawa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Kata ya Nyololo ipewe maji, Itandula, Idunda, Mbalamaziwa, Nyololo, Luhunga hizi Kata zote maji hayapo ni habati nzuri sana nawashukuru sana wafadhili wamenisaidia sana wamenichimbia visima kule, sasa hivi tusingekuwa na visima vile ambavyo nilichimba mimi kwa kushirikiana na wafadhili wananchi wasingekuwa na maji mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali kwenye Jimbo la Mufindi Kusini naomba sana maji yapelekwe kwa muda kama tulivyopanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye bajeti kuna fedha imetengwa. Sasa hii fedha ambayo tumeipata hata ikiwa ni kidogo basi ikafanye kazi. Tukipanga shilingi bilioni mbili, basi ziende shilingi bilioni mbili siyo upange bajeti ya shilingi bilioni mbili wewe unapeleka shilingi bilioni moja inakuwa bado haisaidii. Wakandarasi wale wamekopa fedha kutoka benki na wanadaiwa na benki lakini Serikali bado haijawalipa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa sababu Mheshimiwa Waziri ameniahidi kwamba Mwezi Mei Mufindi hela zinakwenda. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye mapendekezo ya Serikali. Nianze na kuipongeza Serikali kwa kuleta mapendekezo ambayo yanalenga sisi Wabunge tutoe mapendekezo yetu ili bajeti itoke vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine Serikali imefanya vizuri sana, kwa mfano, ku-promote viwanda vya ndani na ili uweze ku-promote viwanda vya ndani lazima udhibiti bidhaa zinazotoka nje. Kwa hiyo, kupunguza kodi kwenye baadhi ya bidhaa ambazo tunaweza tukazalisha sisi wenyewe ni mpango mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona hata kwenye mafuta ambayo tunaweza tukazalisha, tunalima alizeti na tuna viwanda vya alizeti, ili ku-promote hivi viwanda vifanye kazi vizuri wamepandisha kodi kwenye mafuta yanayotoka nje, hiyo ni sawa, lakini lazima tuhakikishe tunapata soko la uhakika la ndani ili wazalishaji wafanye vizuri. Kwa hiyo, hilo na mimi nakubaliana nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu la pili ni bajeti. Bajeti ya mwaka huu 2018/2019 tumeenda na shilingi trilioni 32.5 mwaka jana tulikuwa na shilingi trilioni 31.6. Kuongezeka kwa bajeti ni kitu kizuri sana kwa sababu inalingana na mahitaji ambayo tunayo. Hatuwezi kusema mahitaji ya mwaka jana ni sawa na mahitaji ya mwaka huu. Kila mwaka mahitaji yanaongezeka na bajeti inaongezeka, huo ni mtizamo nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya Serikali kukusanya mapato siyo mibaya isipokuwa kwa sababu tumesema tunataka ku-promote vitu ambavyo tuna uwezo wa kufanya wenyewe ni jambo zuri sana. Kwenye ukusanyaji kwa mfano kuna Electronic Stamping Tax System, kama alivyoongea Mheshimiwa Zungu ni system nzuri sana kwa ajili ya kuongeza mapato ndani ya nchi yetu. Hapo naunga mkono kwa mtazamo wa kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi ni suala zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna issue ambayo Wabunge wengi tunajiuliza, hivi hatuna wataalam pale TRA, vijana wetu ambao wanasoma vyuo vikuu nje wakashindwa kusoma hii system, tukaidhibiti wenyewe, tukaanzisha ndani ya nchi na tukaitumia kukusanya, kwa hiyo, tumeshindwa kabisa? Kwa sababu unapofanya investment ukiona anaweza aka-recover within one year, atapata faida kubwa sana. Kwa mfano, yeye atawekeza kwa thamani ya shilingi bilioni 48 lakini katika hesabu za haraka haraka wamefanya analysis kwa mwaka mmoja anaweza akapata shilingi bilioni 66, tofauti yake ni shilingi bilioni 18 ambayo yote inaenda nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikawa ninajiuliza kama kuna zaidi ya shilingi bilioni 18 ndani ya mwaka mmoja, recoverage ya costs ikafanyika mwaka mmoja, kwa nini tusingesomesha vijana tukachukua hata shilingi bilioni 5 wakaenda kusoma nje wakarudi wakafanya kazi TRA wakakusanya kodi? Hili ni suala la kujiuliza sana. Hivi kuna umuhimu gani kuchukua makampuni ya nje waje wakusanye fedha yetu halafu wapeleke pale, sisi tukawa tumeshindwa. Mwaka wa pili kuna- possibility ya shilingi bilioni 66 zikaenda nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka siku moja tulifanya semina hapa, vijana wetu MaxMalipo vijana wetu wasomi wa hapa hapa Tanzania siku ile Wabunge tuliwapigia makofi sana pale ukumbuni wali-present issue za kukusanya kodi na wakasema kwamba wako worldwide sasa hivi. Hawa vijana wa MaxMalipo wameshindwa kufanya utafiti wa kukusanya kodi? Labda tuwaite, tuwaulize itakuwaje wameshindwa kufanya makusanyo ya humu ndani na wakienda kwenye nchi nyingine wanafanya vizuri na kusifiwa, lazima tuangalie sana. Halafu ule mkataba tumeweka mrefu sana ni mpaka miaka mitano. Tungeweka labda hata miaka mmoja au miwili ili tuangalie matazamio lakini miaka mitano, nadhani hii lazima iangaliwe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Bajeti tumependekeza vizuri sana, tumesema system siyo mbaya ni nzuri nia ni kudhibiti na tunataka tudhibiti hata uzalishaji wa maji. Tunajua maji ni muhimu, tulikuwa tunafikiria kufanya exemption kwenye product za maji ili watu waweze kupata maji, watumie maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naongea na Ndugu yangu hapa Mheshimiwa Charles Kitwanga, yeye alishafanya kazi Benki Kuu na utaalamu wa masuala ya electronics, nikamuuliza hivi wewe kama Mbunge mtaalam umeshindwaje ku-advise tuangalie hii system, kweli nimem- challenge hapa. Amefanya kazi BoT karibu miaka kumi na system ya tax collection anaijua. Ameshindwa kunijibu vizuri lakini naendelea kumuuliza lazima Wabunge wataalam watusaidie katika collection ya tax katika nchi hii na tunataka tax revenue iwe juu. Ndiyo maana kuna Wabunge wanachaguliwa wataalam. Kwa hiyo, nimeona hili suala ni la msingi sana nilielezee hapa ili siku nyingine tusianze kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nataka niipongeze Serikali kwenye mgao wa fedha hasa ile ya vijana na wanawake. Point ambayo nimeipenda pale, ile asilimia 5 kwa vijana na asilimia 5 kwa akina mama Serikali imesema hakuna interest, cha msingi ni usimamizi mzuri, hilo ni jambo zuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ni challenge hasa Wizara ya Fedha, ule Mfuko Mkuu fedha yote mtakusanya kutoka Halmashauri, kutoka Serikali za Mitaa, na sehemu zote mtakusanya pale, halafu Halmashauri ikitaka kutumia itaomba kufuatana na mahitaji. Challenge ambayo ipo pale urudishwaji wa fedha unachukua muda mrefu sana. Lazima tuwe makini, Wizara ya Fedha lazima iwe active
katika kurudisha fedha Halmashauri. Tunaweza tukawa tuna system nzuri ya kuweka kwenye akaunti moja lakini Halmashauri inaweza ikatuma maombi ya kupewa fedha ili watumie mkachelewesha. Hili lazima tutoe angalizo kwa Serikali, kwamba kama Halmashauri zimeeomba fedha on time basi wapewe fedha on time. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Mufindi kuna fedha ya maji na Waziri wa Maji aliahidi kwamba mwezi Mei angeweza kuipeleka ile fedha. Wameomba kuanzia Machi tunaenda Julai ile fedha hawajapewa mpaka leo. Ni mradi wa maji mmoja tu. Sasa najiuliza kama mradi mmoja Mkurugenzi wa Halmashauri akishirikiana na Engineer ameandika request, vigezo vyote viko pale, tena ni shilingi milioni 270 mpaka leo Juni mradi wa maji kule umesimama Kata ya Mtwango wananchi hawana maji. Kupeleka shilingi milioni 200 ni kazi ya siku moja tu, mimi nikikaa kwenye komputa just a minute nimeshapeleka transfer ya hela zile, lakini mpaka leo hazijapelekwa. Je, tukisema wapeleke shilingi trilioni kadhaa kwenye Halmashauri itachukua muda gani? Hii ni bajeti ya mwaka mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi Wizara ya Fedha ina shilingi trilioni 12 ambazo nyingi ni miradi zinapitia pale. Naomba Serikali, system ni nzuri ndiyo maana naiunga mkono, lakini utendaji kazi lazima tuongeze juhudi, lazima tuende na muda. Bahati mbaya sana sisi huwa hatujali muda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia Wizara hii muhimu sana. Kwanza kabisa nianze na pongezi kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, tumeona kazi nzuri, kila mtu anajua kazi inafanyika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mchango wangu una mambo machache tu. Jambo la kwanza, Mheshimiwa Waziri, tungeomba kujua vizuri masuala ya ardhi. Tukiangalia kuna Maliasili, kuna Wizara ya Ardhi, kuna sehemu fulani kama tunaingiliana. Kwa mfano sasa hivi ukiangalia kuna migogoro ya ardhi ambayo inajitokeza, watu wa Maliasili wanasema maeneo yale ni yao, tena ukienda Ardhi wanaweza wakasema yale maeneo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna mgongano kidogo pale. Ukiangalia watu wa Maliasili wenyewe wanaangalia vipimo vya miaka ya 1976. Ukiangalia population ya mwaka 1976 tulikuwa Watanzania wachache sana, tulikuwa kama milioni nane, sasa hivi Watanzania tuko milioni hamsini na nane na kila kijiji ukiangalia sehemu kubwa imechukuliwa na watu wa Maliasili. Wananchi sasa hivi hawana ardhi hata ya kufugia au kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi kwenye jimbo langu, Jimbo la Mufindi Kusini, watu wa Maliasili walichukua maeneo makubwa sana na sehemu nyingine zilichukuliwa na wawekezaji, kwa mfano wakulima wa chai walichukua maeneo makubwa sana. Mfano, ukienda pale Kijiji ha Mtwango wananchi wamekaa tu kwenye barabara ni sehemu ndogo sana, hata kufanya sehemu za kilimo hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ukienda Kijiji cha Sawala kile wananchi hata kwa kujenga makazi hakuna. Hata tukisema tukafanye upimaji wa ardhi kwa ajili ya wananchi tutashindwa. Sehemu kubwa imechukuliwa na watu wa maliasili. Naomba sasa unapotupa maelekezo masuala ya ardhi tupate ufafanuzi kwamba, Maliasili ana uwezo wa kujipimia ardhi au ardhi inapimwa na watu wa Ardhi? Hii itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nimesikia kuna upimaji kule wanafanya vizuri sana, Wilaya ya Kilombero, kuna program nzuri sana. Ile program nimeipenda na inaenda kwa bei nafuu sana, nadhani wanatumia simu tu kwa bei nafuu, kuna wafadhili nadhani, Waziri anaijua, ile program ingekuja Tanzania nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri kama anakuja wilaya nyingine namwomba kwenye Wilaya ya Mufindi basi aje apime. Kwa sababu sisi kule, kama nilivyoongea mara ya kwanza kwamba, wawekezaji wengi sana na sasa hivi tuna tatizo kubwa sana la ardhi. Kwa hiyo, tukija kupimiwa matumizi bora ya ardhi, halafu nasikia wanatoa hati bure, ile itatusaidia sana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri angalau atuangalie Wilaya ya Mufindi kwa ile program na sisi ije kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuna upanuzi wa ilikuwa vijiji, sasa hivi imekuwa miji tayari, tunaita miji midogo. Kwa mfano pale Igoole, Nyololo, Mninga na Kasanga, ile ni miji midogo, lakini kuna upimaji ulifanyika pale. Upimaji ule nadhani watu wa halmashauri walisema wapime, ni upimaji mzuri si mbaya, lakini ukipima makusanyo yote yanaenda kwa halmashauri, hiyo ni njia nzuri na ile fedha tunajua ni Basket Fund, halmashauri inagawanya katika wilaya nzima, lakini kijiji husika ambacho kimetoa ardhi hakipewi mgawo mkubwa, kinaweza kikapewa mgawo mdogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, kijiji husika basi kipewe percent kubwa, ili waweze kufanya maendeleo makubwa kwa sababu wale ndio waliotoa ardhi pale. Hii itakuwa imesaidia sana kuondoa migogoro ya ardhi ndani ya vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, tuna mgogoro pale kati ya mpaka wa Makambako na Mufindi. Kuna Kijiji kimoja pale Nyigo tunapakana na Makambako. Ukiangalia Serikali ilipatia Kijiji cha Nyigo, mipaka iko Kijiji cha Nyigo lakini wa Makambako na wenyewe wanasema ni sehemu yao, ule mgogoro ndio sasa unakuwa mkubwa. Naomba Wizara iingilie kati hilo suala la mgogoro wa ardhi ni mkubwa sana na unapanuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mwekezaji alitaka kuwekeza pale, lakini bado wananchi pale hawaelewi. Mheshimiwa Waziri nadhani ameiandika imekaa vizuri, lakini wananchi pale hawajui, kwa hiyo wangeenda pale wakawaelimisha wananchi itakuwa imetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine napongeza ugawaji wa viwanja, wamegawa viwanja vizuri, hata hapa Dodoma wametugawia viwanja vingi sana vya kununua. Hata hivyo mtu ukisema square metre moja Sh.6,000/= au Sh.12,000/=, bado hujawasaidia wananchi. Naishauri Serikali waweke bei nafuu, ila labda waweke masharti ya kujenga kwamba, wajenge nyumba ambayo ni reasonable, inaonekana ni nyumba, lakini viwanja wakiuza kwa bei kubwa, kwa mfano, sasa hivi watu wametoka Dar-es- Salaam, wametoka wapi, wamekuja wafanyakazi wamesema hapa ndio makao makuu wajenge nyumba, wanahangaika wanapanga huku na huku nyumba hazieleweki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusipunguze bei ya viwanja ili watu wajenge nyumba nzuri? Tukisema square metre moja Sh.12,000/= au Sh.6,000/=, mtu kusema anunue kiwanja sasa hivi milioni kumi, milioni ishirini, milioni thelathini, anunue kiwanja kwa hali ya sasa hivi nani atanunua? Itakuwa bado. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napendekeza. Kwa sababu, sisi ndio tunaishauri Serikali, vile viwanja kwa square metre moja hata ukifanya Sh.3,000/= kwa square metre moja, mtu akanunua kwa milioni mbili ama milioni tatu kwa kiwanja itakuwa ni reasonable; lakini ukisema milioni kumi na ngapi huko itakuwa ni ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hati miliki. Zile hati miliki ni nzuri sana; kwa mfano kwenye jimbo langu, walipima kwa ajili ya hati miliki, lakini bado wananchi ile hati miliki hawaelewi kama anaweza akakopea mkopo benki, bado haijakaa vizuri. Kama tumetoa hati miliki zile za kimila, mimi nazungumzia zile za kimila, naomba kama mtu ameshapewa basi itambulike benki. Akiweza kukopea maana mwananchi yule inamfaidisha ardhi yake, akafanya maendeleo makubwa, hii itakuwa imemsaidia sana mkulima na yule mwenye ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, migogoro ya ardhi kwa wakulima na wafugaji. Nadhani hili suala siku moja tuseme sasa mwisho hakuna migogoro tena na ili kulimaliza vizuri lazima elimu ipite vizuri. Mkulima akielimishwa na mfugaji akielimishwa watu hawatauana, lakini elimu bado. Kwa mfano, zamani unaweza ukaona mtu analima pia ni mfugaji lakini walikuwa hawagombani, lakini sasa hivi ardhi ya wakulima na wafugaji imekuwa ni mgogoro mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaiomba Serikali, nadhani Mheshimiwa Waziri wetu yuko vizuri, wakishauriana vizuri na labda na huyu Waziri wa Ulinzi na wengine wanaohusika katika Wizara nyingine tutakuwa tumefikia mahali pazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni huo.

Naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza nianze kutoa pongezi kwa Wizara ya Fedha. Wizara ya Fedha imeweza kufanya kazi kwa ufanisi mzuri sana. Bahati nzuri taarifa tuliyoisoma ipo wazi. Pale walipo-perform vizuri wanasema na pale wanapojua hawaja-perform wanasema. Huo ndiyo tunasema uwazi. Ndiyo maana kila mmoja anasema labda kwenye kilimo amepeleka asilimia kadhaa, ipo wazi; kuliko asingesema vitu ambavyo ame-perfom. Kwa hiyo, nimempongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa uwazi huo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Wizara ya Fedha ndiyo moyo wa Serikali, ndio moyo wa maendeleo ya nchi hii na ndiyo inayo-control mapato yote ya nchi hii. Ili Serikali i- perform vizuri, lazima Wizara ya Fedha ikae vizuri. Tunajua kwamba ili Serikali ifanye vizuri lazima makusanyo ya kodi yakae vizuri. Kuna Mbunge mmoja alisema kwamba Wizara hii inataja kodi tu, lazima itaje kodi tu kwa sababu isipotaja kodi haiwezi kupata fedha ya kuendesha shughuli za Kiserikali.

Kwa hiyo, nasema waendelee kutaja kodi tu ili na wananchi waelewe kwamba lazima wananchi walipe kodi ili Serikali ifanye vizuri kwenye miradi ambayo tunahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitaka kuangalia, wameeleza vizuri kwamba wanataka kupunguza umaskini. Nataka nijikite vizuri sana kwenye kupunguza umaskini. Wanataka wafanye ufuatiliaji kwenye vijiji ili waangalie umaskini umepungua percent ngapi? Tuna changamoto nyingi sana vijijini.

Mheshimiwa Spika, nataka niiombe Wizara ya Fedha, lazima isimamie vizuri kuhakikisha kwamba mahitaji ya wananchi kule vijijini kweli yanapungua. Nataka nitoe mfano mdogo tu, tukisema kupunguza umaskini kwa wananchi, lazima tuhakikishe miradi ile inayolenga wananchi inafanyika kiusanifu na kwa bei inayojulikana. Wengine wanasema, Serikali isifanye uhakiki, wanasema kila siku ni kuhakiki. Nasema kuhakiki kuongezeke kwa sasabu unaweza ukaona Serikali imelipa fedha nyingi sana lakini mradi wenyewe hauonekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani Serikali ikawa inatoa fedha nyingi, halafu mradi ule hauonekani. Kwa mfano, wanachimba kisima cha maji vijijini, wananchi hawajapata maji, lakini fedha zinaonekana zimetumika pale. Hii haitakubalika hata siku moja. Zamani miaka mitano iliyopita, unaweza ukaona wananchi wanahitaji maji pale kijijini, wanasema kwamba Mkandarasi ametumwa na Serikali, labda Wizara akachimbe kisima cha maji. Maji hajapata, unaenda kuangalia gharama kubwa pale zimetumika na wananchi hawajapata maji. Hii kweli itakubalika? Hii haiwezi kukubalika. Lazima tuone impact. Kama fedha zimetumika kwa ajili ya kuchimba kisima, basi wananchi wapate maji pale. Hilo lazima Serikali ihakikishe inafuatilia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna changamoto kubwa sana. Kwa mfano miradi ya maji. Naiomba Serikali, miradi ya maji mpaka sasa hivi kama tunapunguza umaskini, basi tupunguze kwenye mradi ya maji, tuhakikishe wananchi wetu wote wamepata maji. Kuna Wakandarasi wengine bado wanadai fedha hazijalipwa. Kwa mfano, hata kwenye Jimbo langu, kuna kata moja ya Sawala, Mkandarasi sasa hivi kuna miezi sita alishasaini mikataba lakini mpaka leo hajapata fedha na mradi ule umesimama na wananchi wanataka impact ya maji. Kama tunapunguza umaskini, basi tuwapelekee maji.

Mheshimiwa Spika, kuna sehemu nyingine wananchi wanatembea kwa mguu kilomita nne au kilomita tatu wanatafuta maji. Sasa tusipokijita vizuri, hata hii perception ya kusema tunapunguza umaskini, tutakuwa hatujapunguza umaskini. Wananchi wanataka wapate maji. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wananchi wanataka kupata maji. Miradi ile ya maji ambayo tumetenga kwenye bajeti, basi wapeleke tuhakikishe inafanyika kwa ufanisi kama ilivyopangwa ili wananchi waweze kupata maji.

Mheshimiwa Spika, suala lingine, kwenye makusanyo. Serikali ijitahidi kufanya makusanyo. Lazima kwanza itengeneze urafiki na wafanyabiashara, TRA watoe elimu ya kutosha ili kuhakikisha kwamba kila mtu anayelipa kodi asione kama adhabu, aone ni wajibu wake kulipa kodi. Ili ajue kwamba ni wajibu wake kulipa kodi, lazima utaratibu wa ulipaji kodi uwe mzuri. Kuna point moja nimeipenda sana kwamba Wizara ya Fedha kushirikiana na TRA wanataka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kila mtu anayelipa kodi asikwepe. Hiyo nimeipenda, huo ni mfumo mzuri wa kuhakikisha kwamba kila mtu analipa kodi, hiyo ni njia mojawapo. Hata hivyo, lazima tuhakikishe kwamba wale walipa kodi, tunajenga urafiki nao, tunawapa elimu, ili kila mmoja nayelipa kodi asione kama adhabu.

Mheshimiwa Spika, kuna masuala ya fedha zile zinazopelekwa kwenye Halmashauri za maendeleo. Naishauri Serikali kwa sababu wanapeleka quarterly, sijajua system ya kupeleka, lakini fedha ziende kwa muda unaotakiwa, on time. Unaweza ukaona Mkandarasi ameingia mkataba labda wa mwaka mmoja. Usipopeleka fedha on time kama mkataba unavyosema, matokeo yake ukichelewesha fedha, inatokea Mkandarasi baadaye anaanza kuidai Serikali, baadaye ule mradi bei inaongezeka, Serikali inaanza kulipa riba.

Mheshimiwa Spika, mradi wa shilingi bilioni moja baadaye inakuja kusomeka hata shilingi bilioni tano. Kwa hiyo, naiomba Serikali ipeleke fedha kwenye miradi mikubwa, kwenye Halmashauri kwa muda uliopangwa. Hii itasaidia sana kuhakikisha miradi ile inakwisha on time.

Mheshimiwa Spika, suala lingine nataka niipongeze Serikali kwenye point moja. Serikali kufikiri miradi mikubwa ya kimaendeleo ndani ya nchi yetu ndicho kinachotakiwa. Hatuwezi kuwa tunafikiri miradi midogo midogo tu halafu tunasema nchi itafikia uchumi wa kati, haiwezekani hata siku moja. Lazima ifikiri miradi mikubwa ambayo inajenga uchumi ndani ya nchi yetu. Kwa mfano, ule mradi wa umeme wa Rufiji ni mradi ambao utatutoa katika hali ya umaskini. Kwa sababu ule umeme tunaweza kuuza hata nje.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Malawi watanunua, Zambia watanunua na nchi nyingine za East Africa wanaweza wakanunua umeme kutoka pale. Ndiyo nchi yetu itapata fedha za kigeni, ndiyo tutafikia uchumi wa kati. Ukisema kwamba unataka kufikia uchumi wa kati, wewe una plan kulimalima mboga, bustani na kadhalika, uchumi wa kati utaufikia wapi? Lazima tuwe na miradi ya kimkakati ambayo inaleta uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, point nyingine ambayo nimeiona, Serikali kufikiria kujenga reli, hiyo ni point kubwa ana katika nchi zinazoendelea. Hata ukienda Ulaya utakuta kuna reli zimejengwa standard. Kwa mfano, sasa hivi kuna standard gauge, ni kitu cha msingi sana. Kwa hiyo, nataka niwaambie, kama tuna-plan uchumi, lazima tufikiri vitu vya kiuchumi ambavyo vinaleta hela kubwa ili uchumi wa kati ufikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna watu wengine wanakatisha tamaa, wanasema Serikali sijui haifanyi kazi. Sasa hivi tunaingia kwenye vitu vikubwa ambavyo ni pigo kubwa kwa uchumi ili kuinua uchumi wa nchi yetu. Tukitaka kupata fedha nyingi, lazima tufikiri vitu ambavyo vinaweza vikatuingizia. Hata wawekezaji wanapokuja, wanauliza vitu vya msingi. Kwa mfano, atauliza barabara, miundombinu ya umeme, maji, hospitali; wafanyakazi wakiugua wanatibiwa wapi? Hivyo ndivyo vitu wanavyouliza wawekezaji. Wewe huna barabara, umeme, maji wala hospitali halafu unasema unatafuta mwekezaji, utampata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali inapobuni vitu vya msingi lazima tui-support na sisi Waheshimiwa Wabunge. Bila kui-support Serikali kwa vitu vya msingi hatutaendelea hata siku moja. Kwa hiyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri wa Fedha, akaze buti, afikiri vitu vya msingi ili nchi yetu iweze kusonga mbele. Hatuwezi kuwa tunarudi nyuma kila siku, Waheshimiwa Wabunge tunauliza maswali madogo madogo ambayo Serikali inaweza kutatua kwa muda mfupi sana. Kwa hiyo, tunafuta maswali sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, hatupendi sisi Wabunge tukifika hapa tunauliza masuala ya maji, tunauliza kuhusu barabara ndogo ndogo, zahanati ndogo ndogo; Serikali inakuwa imeshatatua. Sasa ili kutatua lazima tujifunge mkanda. Bila kujifunga mkanda, kujibana vizuri hatuwezi kuendelea hata siku moja. Lazima Serikali ibane vizuri lakini ilete maendeleo, tuone impact. Siyo Serikali ibane halafu tuwe na njaa, hapana. Ubane vizuri, tunakula lakini tuhakikishe kila mmoja anafanya kazi kwa nafasi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine la utendaji kazi. Unaweza ukaona document moja inapelekwa kwenye ofisi, inazunguka miezi mitatu. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, document isizunguke. Mtu anatoka Halmashauri kule anafuatilia document hapa, inachukua siku mbili au tatu. Hii haiwezekani, unaweza ukaona gharama za ufuatiliaji wa document, inataka kukaribia mradi unaofuatiliwa. Hii inakuwa ni system mbaya sana. Kwa nini tusitafute system, mtu yuko Halmashauri kule, ana-lodge document yake mtaalam huko anasoma kwenye computer, analipa malipo, simple. Anaona hiki kipande nimeelezwa vizuri, ana
document.

Mheshimiwa Spika, mtu yuko Halmashauri kule ana- search tu document kwenye computer, mtaalam huku anasoma. Akishasoma ana-reply within the minute, yule kule atakuwa ameshaiona. Akishaiona, basi inajibiwa. Sasa mtu anaanza kufuatilia wiki moja, mbili, anafuatilia document. Hii inarudisha nyuma maendeleo. Kwa hiyo, nataka nihamasishe wafanyakazi, hasa wale wa Idara ya Fedha, kwenye hili wasimame vizuri, wasilimbikize kazi ambazo hazina msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni wastaafu. Kuna Mheshimiwa Mbunge aliuliza asubuhi kwamba wastaafu wao bado wanadai, wanalipwa kiasi kidogo sana. Wale wastaafu ni wa kuwaheshimu, wamefanya kazi nyingi sana mpaka sasa hivi nchi imefika hapa. Wewe mtu amestaafu, alifanya kazi nzuri, kwa nini usimlipe haki yake vizuri? Lazima tuhakikishe wale wazee ambao na wenyewe wanatuombea na sisi tufanye kazi vizuri, tuwalipe stahili zao kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani mstaafu unamlipa Sh.50,000/=. Kama sheria inasema alipwe Sh.100,000/=, mlipe Sh.100,000/= yake. Kama inasema Sh.200,000/= mlipe Sh.200,000/= yake, sasa mzee amestaafu anafuatilia mafao kuna watu wengine hawajapata mafao mpaka leo inachukua miezi mitatu na zaidi na mtu anastaafu yuko kwenye system. Kwa nini anastaafu leo, kesho humlipi hela yake? Mtu yuko kijijini, kwa mfano yuko Mufindi, afuatilie Dodoma au Dar es Salaam wakati system inasoma. Kwa nini asilipwe on time? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiunga mkono Serikali, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia mapendekezo ya mpango wa mwaka 2019/2020.

Kwanza na mimi nianze kwa kutoa pongezi kwa Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, hakuna mtu ambaye hakubaliani kwa utekelezaji wake, ndani ya miaka mitatu amefanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nichukue nafasi kupongeza Mheshimiwa Waziri wa Mipango pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri mliyoifanya bahati nzuri sana mimi niko kwenye Kamati ya Bajeti na ukisoma hivi vitabu ni vitabu ambavyo vinaeleweka vizuri kabisa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile hapa tunafanya ni mapendekezo ya mpango naona kuna watu wengi labda hapa hatujaelewa vizuri haya ni mapendekezo ya mpango ni mpango ambao tunaupendekeza sio mpango tunaoukosoa, sasa mimi naomba nipendekeza kwa sababu katika mpango inaonyesha kwamba malengo makubwa ni kupunguza umasikini na bahati nzuri sana ameonesha data kwamba kutoka 2012 mpaka 2020 kiwango cha umaskini kitapungua mpaka kitafika asilimia 16.7 hii nimeona ni nzuri sana. Sasa ili tufikie asilimia 16.7 ambayo tumepunguza kiwango cha umaskini nini kifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi sasa hivi walio wengi tunaomba sana tuimarishe sana na tuboreshe kwenye sekta ya maji. Sekta ya maji ni muhimu sana, bahati nzuri na kwenye mapendekezo umeeleza lakini nafuu niseme kwamba mpango unatuelekeza baadae tuweze kupangia bajeti sasa mimi napenda nipendekeze kwamba pamoja kwamba umeweka kwenye vipaumbele kuimarisha miundombinu ya maji kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata maji, kwenye eneo hili niombe Serikali tuwe makini sana lazima tuhakikishe kwamba tuliposema kwamba mwananchi kutafuta maji hatembei mita 400 ziwe mita 400 na kufikia mwaka 2019/2020 asilimia kubwa ya Watanzania wapate maji hilo litakuwa limetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti , jambo la pili ameonesha kwamba ataimarisha vituo vya afya, imeoneshwa hapa na mimi nakubaliana na wewe, lakini lazima tuweke mikakati, kuna vituo vya afya ambavyo havijaisha kwa hiyo tuhakikishe kwamba 2019/2020 vile vituo vya afya ambavyo hatujakamilisha vyote tuwe tumeshakamilisha, bahati nzuri sana Serikali imeanza kujenga hata maeneo kuna maeneo kuna Wilaya nyingine zinajengewa hospitali bahati nzuri hata Jimbo la Mufindi Kusini kule tunajenga hospitali/katika Wilaya Mufindi tunajenga hospitali na Serikali imeshatoa shilingi milioni 500 nimefurahi, lakini tuhakikishe kwamba tunaweka mikakati zile fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya kuboresha hospitali mpya zinasimamiwa vizuri, zinatumika vizuri kwa sababu ile ni kodi ya wananchi na kuhakikisha kwamba zile hospitali zinazojengwa zinakuwa nzuri na zinakuwa standard.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa sana la watumishi katika hospitali sasa hili lazima liende sambamba, tukimaliza hospitali basi na ajira mpya kwa watumishi hasa wa upande wa afya waweze kuajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo lingine la msingi sana kwa sababu tumesema tunapunguza umaskini sasa nataka niongeee kwenye upande wa REA. REA vijijini niombe Serikali tumeanza vizuri tumalize vizuri tunategemea kufikia mwaka 2020 vile vijiji vyote ambavyo havijapata umeme vimepata umeme vijiji vyote na bahati nzuri Waziri wa Nishati huwa anaongea vizuri sana kwamba kila kitongoji hiyo ni mikakati ya Serikali kwamba kila kijiji kila kitongoji na kila kaya ziweze kupata umeme hiyo ni mipango mizuri na tumeonautekelezaji unafanyika na makandarasi wako site hiyo naipongeza sana Serikali, ila mimi nisisitize tuzidi kuongeza juhudi saa hivi makandarasi hawaendi na speed ile ya mara ya kwanza, wakishaongeza juhudi ya makandarasi kufikia mwaka 2020 vitongoji vyote na vijiji vyote vikiwa vimepta umeme basi umasikini moja kwa moja automatically utakuwa umepungua.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo moja kwa moja ita-connect hata uboreshaji wa uzalishaji wa bidhaa katika viwanda vyetu. Tukitaka kuboresha viwanda lazima tuwe na umeme wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi sana kuona Serikali ina mpango mkubwa na ule umeme wa maji Rufiji wameonesha kwenye mipango tukiwa na umeme wa maji kutoka Rufiji nadhani tutakuwa tumetimiza lengo la kupeleka umeme vijijini kwa sababu tutakuwa tuna miundombinu mingi sana ambayo inaweza ku-connect kila kijiji na kila kitongoji kupewa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nilitaka niliongele kwenye elimu, elimu ameongea vizuri Waziri wa Mipango, ameeleza vizuri sana, lakini naomba tuongeze kipengele kingine Serikali iongeze juhudi kwa kujenga hosteli kila shule ya sekondari. Tuna tatizo kubwa ya hosteli kwenye mashule yetu watoto bado wanatembea kilometa mpaka 10 mtoto wa sekondari binti anatembea kilometa 10 na hii inasababishia wanafunzi wengi sana kupata mimba mashuleni. Sasa kwenye mipango yetu niombe Serikali tuhakikishe kila sekondari tunaweza kuijengea hosteli ili watoto wakae bweni, hili litasaidia sana kupunguza matatizo na kuongeza kiwango cha ufaulu kama watoto wetu watakuwa wanakaa hosteli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu tena bado kuna upungufu wa walimu wa sayansi, tuiwekee mikakati kabisa, niliwahi kuongea siku moja nilisema wanafunzi wanaosoma vyuo vikuu wanachukua elimu ya sayansi wapewe mkopo asilimia 100 na hii itasaidia ku-motivate wanafunzi wengi wajiunge na masomo ya sayansi ili tupate walimu wengi tutapata madaktari wengi na hiyo itasaidia na zile maabara ambazo tumejenga kwa sababu Serikali imehamasisha kuna maabara zimejengwa zimeshaisha lakini hakuna wanafunzi wanajitolea kusoma sekondari kwa sababu akienda Chuo Kikuu hapati mkopo asilimia 100. Sasa niombe Serikali kwenye hilo tuiliwekee kwenye mkakati kwenye mpango ionekane kwamba wale wanafunzi wanaojitolea kusoma sayansi wapewe asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine ambalo nimeliona kuwepo kuna upendeleo katika mikopo hasa watoto wa kike, watoto wa kike bado asilimia ile ya kupeleka hizi masomo ya juu bado kwa sababu mkopo hawapewi katika vyuo vikuu, sasa niishauri Serikali katika mipango utoaji wa mikopo mtoto wa kike apendelewe zaidi kuliko mtoto wa kiume kwa sababu mtoto wa kike kwa mfano hajapata mkopo anaanza kufuatilia bodi ya mikopo Dar es Salaama anakaa mwenzi mzima anafuatilia mkopo Dar es Salaama hii imeleta madhara makubwa sana kwa watoto wa kike matokeo yake wanaweza wakajiingiza kwenye mambo mengine ambayo hawakutegemea kwa sababu ya kufuatilia mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali ikitoa mikopo kwa watoto wa kike wote hii itakuwa inapunguza hata ile madhara ya kupata mimba mashuleni hii itakuwa imesaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono asilimia 100 mpango huu ambao ni mzuri ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia. Nianze na kuipongeza Serikali, tumeona mambo mengi kwenye elimu imefanya vizuri, Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake kazi inaonekana ni nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina machache tu ya kushauri; kwanza nipongeze kwa elimu bure, elimu bure ni kitu kizuri sana kwa Taifa letu na sasa hivi kuna ongezeko kubwa sana la watoto kuanza shule za awali, shule za msingi mpaka sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri sana na wazazi wamelielewa hilo na kufuatana na ongezeko la watoto, kuna shule nyingi sana sasa hivi zinajenga madarasa kwa ajili ya ongezeko la watoto, lakini na wazazi wako tayari kujenga madarasa kuhakikisha watoto wanasoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema elimu bure, wazazi walio wengi sasa hivi wameanza kupata uelewa, lakini zamani uelewa ulikuwa mdogo sana, walikuwa wanajua elimu bure ni kila kitu huruhusiwi kuchangia, lakini sasa hivi elimu waliyoitoa kwa wazazi nawashukuru sana wameanza kuelewa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watoto wanamaliza form four, bahati mbaya hawaendi high school wanaishia form four, sasa wale wanaoishia form four kwa kwenda sasa hivi hakuna na wale watoto kwa sababu bado hawajatimiza miaka 18 hawawezi kuajiriwa mahali popote, kwa hiyo basi Serikali ili kuwanusuru wale watoto ni kuhakikisha kwamba inajenga Vyuo vya VETA katika kila wilaya kama sera inavyosema. Kuna wilaya nyingine hazina VETA kabisa, kwa hiyo Serikali lazima ijikite kuhakikisha kwamba wale watoto wanaomaliza form four hawajachaguliwa kwenda high school waweze kwenda kwenye vyuo vya VETA, ili waweze kupata ujuzi na wakimaliza huko VETA waweze kujiajiri wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala la msingi sana, tulienda Arusha kwenye Kamati yetu ya Bajeti, tukatembelea viwanda pale, bahati nzuri tukakuta watoto waliomaliza VETA wamepata ajira pale, ni mafundi wazuri sana mpaka tukajifunza kwamba kumbe watoto wakipitia VETA wanaweza kupata ajira bila matatizo hata akiwa hajafika form four na anaweza akafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuboresha elimu, tukisema tunataka kuboresha elimu siyo kwamba kubadilisha mitaala kila wakati. Sasa hivi Open University – Chuo Kikuu Huria Walimu wengi sana wanapenda kujiendeleza kwa kusoma vyuo vikuu, lakini chuo kikuu rahisi kabisa ni Chuo Kikuu Huria ambao tunasema Open University. Sasa nataka niishauri Serikali ili kuongeza wingi wa Walimu wasomi na tumesema kwamba Walimu kuanzia Diploma, mpaka degree mpaka Masters, sasa hivi Walimu wenye degree wanafundisha shule ya msingi na hilo tumeliona na huko ndiyo kuboresha elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali tuseme elimu bure kwa Walimu, yaani Walimu wapewe elimu bure, Mwalimu anayejitolea kwenda chuo, anaenda kufanya degree kwenye Open University asome bure kwa sababu yeye akimaliza ni faida ya Taifa, anaenda kufundisha watoto katika shule zetu. Kuna Walimu wengine kufuatana na mshahara kuwa mdogo wanashindwa kujiendeleza kusoma degree, kwa sababu mshahara ni mdogo. Kwa hiyo, tukifanya hivyo, tutakuwa tumemsaidia sana Mwalimu kujiendeleza. Tunabadilisha mitaala kila wakati haitusaidii kama hatuboreshi elimu kwa Walimu wetu, hii itatusaidia sana. Kwa hiyo nasisitiza kwenye hilo na nawapongeza Walimu wale wanaopenda kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kuna jambo lingine ambalo siyo zuri sana, Mwalimu anamaliza Masters, anamaliza degree anarudi kufundisha shule, anakuja kupitwa mshahara na Mwalimu mwenye certificate, inamkatisha tamaa Mwalimu aliyesoma. Kwa hiyo ni lazima tuweke grading system ikae vizuri ili ku-motivate Walimu. Tumesema wafanye degree, wafanye diploma na ukiweka elimu bure na akimaliza shule aongezewe mshahara kufuatana na elimu yake, lakini anamaliza degree unampeleka shule ya msingi na mshahara ni mdogo, basi Mwalimu anakata tama, sasa hapo bado tutakuwa hatujaboresha. Nimeona hili niliongee kwa msisitizo sana kwa sababu kuna Walimu wengi sana wanapenda sana kusoma soma, nami nawapongeza ili kuhakikisha kwamba Walimu wanakuwa katika mazingira mazuri kwenye elimu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kuna hizi private school, Mheshimiwa Waziri siku moja alisema wataleta kiwango cha ada. Kuwa na private school ni jambo zuri sana na elimu bora kwenye private school ipo tunaiona, wanafundisha vizuri, lakini ada ni kubwa sana. Wewe unaweza ukaona ada ya private school mtoto analipa milioni kumi, milioni nane, jamani hicho ni Chuo Kikuu, ni shule ya sekondari, ni shule ya msingi. Wengine wanasema kama unaona mtoto wako huwezi kupeleka huko, peleka shule ya Serikali, ndiyo watu wanajitetea, lakini hiyo ni elimu na tunavyoongea hivi lazima tupime maana mtoto anataka apelekwe kuzuri na mzazi anataka ampeleke mtoto wake kuzuri ili apate elimu nzuri, lakini lazima kuwe na grading system ya ulipaji wa ada. Sasa kwa mfano, shule ya msingi mtu analipa milioni 12 unaweza kuona pale sawa ni lugha na elimu, sawa ni nzuri lakini lazima kuwe kuna fairness kwa watoto na kwa wazazi.

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Goodluck Mlinga, taarifa kwa ndugu yako.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimpe taarifa kaka yangu Mbunge anayezungumza kuwa hata kwenye mahoteli, kuna guest house Sh.15,000 mpaka Sh.2,000,000. Kwa hiyo, chaguo ni la kwake hawajatulazimisha, tupo nchi ya kidemokrasia hii. Kwa hiyo, kama mtoto wako unaona akasome St. Kayumba mpeleke zipo shule za private ada kuanzia Sh.300,000 mpaka hiyo Sh.10,000,000. Kwa hiyo, chagua ni lako. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Kigola unaonaje hapo, patamu eeh?

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku moja nilikuwa naongea nikasema hizi taarifa tunazozitoa tuwe makini maana unaweza ukatoa mfano ambao hauendani na elimu. Sasa wewe unatoa mfano wa gesti na elimu wapi na wapi, nashangaa, hizi taarifa tuwe makini sana. Academics na vitu vya biashara kama gesti haviingiliana hata siku moja. Hivyo Mheshimiwa hapo inabidi ujipime mwenyewe na taarifa yako. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uboreshaji wa mazingira ya walimu kufundishia. Walimu lazima waishi kwenye mazingira mazuri. Kwa mfano, kuna shule nyingine unaweza kuona mwalimu ana nyumba yake pale lakini nyumba haina jiko.

Mimi nimeona kwenye jimbo langu, siwezi kuongea kitu ambacho sijaona. Kwa hiyo, tunaposema tunajenga nyumba za walimu tuhakikishe nyumba ina jiko na choo safi. Miundombinu ya nyumba ikakaa vizuri basi mwalimu anayefundisha shule ile atajisikia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumesema nyumba zote za walimu ziwe na umeme, hilo ni jambo nzuri sana. Kama nyumba ina umeme ataandaa masomo jioni na atakaa vizuri lakini kama mazingira ni magumu unampa ugumu mwalimu kufanya maandalio. Kwa hiyo, hilo nalo ni suala la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la walimu wa sayansi, shule nyingi sana za sekondari walimu wa sayansi hakuna. Kuna siku moja tuliongea tukasema tutoe motisha kwa walimu wa sayansi, wale wanaosoma digrii ya sayansi wapewe mkopo asilimia 100, watu wengi watakimbia kuchukua masomo ya sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu pale Mgololo mwekezaji amejenga shule nzuri sana. Bahati nzuri sana namshukuru Makamu wa Rais alikuja pale na alikubali kwamba ile shule itakuwa ni high school iatakuwa ni sayansi tupu. Sasa ikiwa ni sayansi tupu, wale wanafunzi wanaomaliza, kwa mfano mtu amesoma PCB, PCM akimaliza anaenda kusoma engineering au digrii ya ualimu wapewe mkopo asilimia 100. Sasa utaona mwanafunzi amesoma masomo ya sayansi magumu anaenda chuo kikuu mkopo hapati basi wanafunzi wanakwepa yale masomo, wanasema si nafuu tusome masomo mepesi tuendee na maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni msisitizo ingawa lina connection na TAMISEMI ni upandaji madaraja walimu, walimu wanalalamika. Mwalimu alimaliza mwaka 2012 mpaka leo hajapanda daraja, kwenye jimbo langu wapo. Kuna mwalimu mwingine amemaliza mwaka 2014 hajapanda daraja mpaka leo. Kuna mwingine amemaliza 2014 amepanda daraja, wa mwaka 2012 hajapanda daraja. Sasa yule aliyeanza kuajiriwa hajapanda daraja aliyekuja kuajiriwa baadaye amepanda daraja, tayari yule ambaye hajapanda daraja inakuwa ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vibali vya kupandisha madaraja vitolewe. Ikitokea ongezeko la mshahara lazima yule aliyekuja kuajiriwa baadaye atapata mshahara mkubwa zaidi kwa sababu ndiye aliyeanza kupanda daraja yule aliyeajiriwa mwanzoni anakuwa na mshahara mdogo, kwa hiyo, inaleta shida kwa walimu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MENRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na nichangie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji ni suala la kipaumbele, bila maji hatuwezi kuifanya kitu chochote. Kwanza kabisa namshukuru sana Waziri pamoja na Naibu kwa kazi nzuri mnayoifanya. Na sisi Wabunge inabidi tukusaidie kwa kutoa ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inahitaji kupata fedha nyingi sana. Sisi Wabunge tuliangalia tozo ya mafuta ile shilingi 50 lakini tunaona kuna ugumu wake na ili Wizara ipate fedha nyingi, nilikuwa napendekeza kwa sababu kila Mbunge akisimama tunaomba maji, kuna vijiji, kata, kuna sehemu nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natoa mapendekezo kwamba mnaonaje kwenye Wizara hii vitu vyote vinavyohusiana na maji tufute kodi, tufute kodi vyote. Kwa mfano, vifaa vya maji tufute kodi, watu wanaochimba visima tufute kodi, miradi mikubwa ya maji, tufute kodi ili Wizara iweze kupata fedha za kutosha na watu wengi sana wanajitolea. Kuna mashirika mengi sana yanajitolea kuleta maji katika nchi yetu. Mtu yeyote anayeleta maji hafanyi biashara, hii ni huduma ya jamii. Sasa ili tuweke kipaumbele na wananchi wapate maji ya kutosha, basi vifaa vya maji inabidi viwe vya bei ya chini sana, hii itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya maji ambayo tumewapa wakandarasi wazawa, kuna uzembe mkubwa sana. Serikali inatoa fedha lakini miradi haiishi kwanini? Kuna miradi mingine imetengenezwa lakini haitoi maji. Ukienda kuangalia mabomba yanakaa siku mbili/tatu yameharibika. Hili ni tatizo kubwa sana. Unaweza ukaona fedha nyingi sana imekwenda lakini ukaenda kuangalia utekelezaji wake sio imara! Hilo ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwenye usimamizi wa miradi ya maji inabidi uongezeke mara tano, tusimamie vizuri sana kwenye miradi hii. Kwenye jimbo langu kuna miradi mikubwa ya maji Serikali ilitoa fedha, nataka nikuambie kuna mradi wa Mtwango ule, wa Sawala Mheshimiwa Waziri aliyepita alikuja na akasaini mkataba mbele ya wananchi. Naibu Waziri umekuja wewe ni shahidi, umeona pale mradi mpaka Serikali imeshatoa zaidi ya millioni 700. Mpaka leo tunavyoongea hivi, maji bado hayajatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mtiririko wa fedha, zinakwenda lakini mkandarasi hafanyi kazi na Serikali bado tunaangalia tu. Mkandarasi yule hafanyi kazi mpaka leo wananchi wa Kata ya Mtwango, vijiji karibu sita havina maji na Serikali imepeleka pesa. Zaidi ya miaka miwili, mradi unakwenda, mkandarasi yuko site. Ni tatizo! Tutafanyaje kulitoa hilo tatizo na tumesema wazawa, wakandarasi lazima wapewe kazi hii lakini hawafanyi kazi ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi mwingine kwenye Kata ya Itandula pale Kiliminzowo Serikali ilipeleka nilioni 800, milioni 800 zilikwenda pale, mradi ule mpaka leo unatoa maji ya kusua sua tu ya wasi wasi. Serikali imepeleka pesa, wakandarasi wako pale wananunua vifaa sijui vifaa gani vile, vinakaa siku mbili vimeharibika. Tunafanyaje hilo, ni tatizo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jimbo langu nina matenki karibu saba yalishachakaa, miundombinu imechakaa. Kwa mfano ukienda pale Nyololo, Waziri siku ile umekuja na uliniahidi kwamba watoe tenda pale mkandarasi aingie site. Nakupongeza sana Waziri, ulitoa bilioni 1.4 kwa Kata ya Nyololo lakini mpaka leo hii hawajatangaza tenda ile na wewe kibali ulishatoa. Wewe umetoa kibali tarehe 15 lakini tenda haijatangazwa mpaka leo na fedha zipo watu wanasuasua, tunafanyaje hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bilioni 1.4 iko Nyololo kwenye Jimbo langu, Waziri umetoa kibali, watu hawafanyi kazi wako ofisini. Hili ni tatizo kubwa sana hili. Kata ya Igowole ni kata kubwa sana, pale ni mjini, tenki la maji liko pale, lina miaka zaidi ya 10. Wananchi wanakunywa maji Mbunge nilichimba visima pale ambavyo mimi nilisaidia lakini na tenki la maji liko pale, kwenye bajeti tulitenga milioni 400, mpaka leo hakuna mradi pale, wananchi wanahangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na vyanzo vya maji Mufindi vimejaa, ni vingi! Sisi tuna vyanzo vya maji vingi sana, ile ya kuchimbachimba visima mimi Mbunge, nimechimba visima vingi pale kwenye jimbo langu lakini kuna vyanzo vingi vya maji ambavyo tunaweza tukatengeneza maji ya gravity system. Naiomba Serikali tusimamie vizuri sana kwenye miradi hii ya maji. Sasa hivi Serikali inafanya vizuri kwa kutoa fedha, naishukuru sana, Serikali ya Awamu ya Tano fedha inapeleka lakini usimamizi sio wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi hatuwezi kuilaumu Serikali jinsi ya kupeleka fedha kwenye majimbo, inapeleka! Lakini usimamizi mbovu sana na hii haitakubalika Serikali iwe inapeleka fedha halafu kuna watu wengine wanafanya mchezo hawafanyi kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ampongeza Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Yule huwa anawaweka ndani wazembe wa kazi, safi kabisa! Mkuu wa Mkoa wa Iringa, uendelee na mtindo huo. Weka wengi tu ili wajifunze kwa sababu sisi tunataka watu wafanye kazi inavyotakiwa na katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tunatekeleza vizuri na hakuna mtu anaweza akabishana na Ilani, imekaa vizuri lakini watendaji wanatudondosha hasa wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba kwenye Jimb o langu la Mufindi Kusini, Kata ya Mtambula, Itandula, Idunda, Mbalamaziwa, Malangali, Mtambula, Igowole, Mninga, Mtwango, Luhunga, sehemu zote zipewe maji. Bahati nzuri nawapongeza na wafadhili wangu RDO walipeleka mradi mkubwa sana Kata ya Luhunga, nawapongeza sana walifanya vizuri. Nawapongeza sana watu wa UNICEF wako vizuri, wametengeza mradi pale Ihowanza umekaa vizuri sana. Nalipongeza Shirika la Water for Africa ambalo tulianzisha pamoja na ninyi, wanafanya kazi nzuri sana nawaombe tuwapunguzie kodi ili wafanye kazi vizuri. Wafadhili wanaojitolea kwanini umtoze kodi na anatoa maji bure yeye hafanyi biashara. Kuna mashirika mengine ya dini yanatoa msaada wa maji, kwanini tuwatoze kodi? Wale hawafanyi biashara ni kwa wananchi. Hili lazima tuliangalie vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji tukiwekea unafuu wa vifaa itakuwa vizuri, wala hakuna inflation, wengine wanasema labda inflation itaharibu, hakuna hiyo! Na kipaumbele cha kwanza kwa wananchi ni maji. Maji ni uhai, hakuna kitu kingine. Hapa hata tukipiga kelele ni kipaumbele cha kwanza cha wananchi ni maji vijijini. Mijini sasa hivi Serikali imejitahidi sana hata hapa Dodoma naona watu tunapata maji. Lakini vijijini tatizo ni kubwa, kuna watu bado wanatembea kilometa nne kilometa tatu wanatafuta maji. Kuna watu wengine wanachota maji na punda. Ukipita hii njia ya Iringa, ukitoka hapa kwenda Iringa utakutana na punda humo njiani wanatafuta maji huko na huko. Hili tatizo lazima tulifute kabisa lisiwepo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu wa mapendekezo ya Mpango kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na jambo moja ambalo ni la msingi sana, kutoa pongezi kwa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa maelekezo kwa zile Halmashauri mpya kuhamia kwa wananchi ili kutoa huduma kwa wananchi kwa ujirani sana na hatua hizo zimeshaanza kutekelezwa. Nampngeza sana, nami Halmashauri yangu imeshahama tayari na wanafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nawapongeza wananchi wa Jimbo la Mufindi Kusini kwa kujiandikisha kupiga kura. Wananchi wamejiandikisha vizuri kabisa na uchaguzi ambao wenzangu wanaongelea wa kidemokrasia, nadhani kwenye Jimbo langu hakuna tatizo na tunakwenda vizuri kabisa. Nawapongeza sana wananchi wa Jimbo langu la Mufindi Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ni mapendekezo ya Mpango, nami napenda nitoe mapendekezo yangu. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri sana. Wameandaa Mpango sana. Nimesoma Mpango wiki nzima na bahati nzuri niko kwenye Kamati ya Bajeti, tulikuwa tunajadili pamoja, hakuna kitu walichoacha, kila kitu kimeandikwa vizuri na ukisoma vizuri, maana kuna utekelezaji wa miaka mitatu iliyopita na kuna mapendekezo ya Mpango kwa miaka inayokuja, wamefanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mapendekezo kwa TARURA. TARURA wanafanya kazi vizuri na ukiangalia tafsri ya TARURA ni Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini; na ukiangalia kazi zao wanavyofanya, kwa upande wa mijini na wenyewe wanajenga hata barabara za lami. Ukienda vijijini wanajenga barabara zile za kokoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia ile bajeti, tukisema tunawapa asilimia 30, fedha ile haitoshi. Sasa hivi nchi nzima barabara zinazoangaliwa ni zile ambazo ziko chini ya TARURA. Wenzetu wa TANROADS walifanya kazi vizuri, kutekeleza ile sera ya kuungalisha barabara za mikoa na mikoa na wilaya na wilaya. Walifanya kazi nzuri sana na barabara nyingi sana zimejengwa. Ukiangalia Tanzania nzima sasa hivi barabara za mikoa na wilaya zinapitika vizuri, lakini tuna tatizo kubwa kwa barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye Mpango huu mpya, naiomba Serikali ijielekeze sana kuiangalia TARURA kuweza kuiongezea uwezo ili wafanye kazi vizuri sana na tuhakikishe kwamba barabara za vijijini zile zinapitika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa hospitali katika wilaya 67. Ni jambo jema sana. Hizi hospitali zitasaidia sana wananchi na zimeenda kasi. Sasa zile hospitali ambazo Serikali ilitoa fedha, naweza nikasema kwamba wameshafikia asilimia kuanzia 80 mpaka 90 kwa kujenga, lakini wakimaliza tu kujenga, naiomba Serikali itazame, zile hospitali zianze kutumika mara moja haraka sana ili value for money ionekane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijenga hospitali zikakaa muda mrefu bila kutumika, itakuwa ni kazi bure. Kwa speed hiyo tuliyojenga, iende sambamba sasa na ununuzi wa vifaa vya hospitali, kuwaandaa watumishi ili waweze kufanya kazi katika hospitali zile. Kuna hospitali nyingi sana tuna tatizo la vifaa vya hospitali. Kwa mfano, hata pale Mjini Mafinga, tuna tatizo moja la X-Ray, hospitali haina X-Ray.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hospitali mpya hizi maandalizi ya vifaa yawepo ili kuhakikisha tunapomaliza majengo yote, watumishi na vifaa viwepo ili hospitali ianze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Serikali mwaka huu mmefanya vizuri sana. Kila ukimwuliza mwanafunzi anasema nimepata asilimia 100, asilimia 80, asilimia 90, Serikali imefanya vizuri, mikopo imeongezeka sana kwa wanafunzi. Nilikuwa nasoma hapa, hao wanafunzi wa mwaka wa kwanza karibu 41,000 wameshapata mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe pendekezo moja, kuna wanafunzi ambao wako mwaka wa pili na wa tatu, kuna wengi walikosa mikopa na mwaka huu hawajaomba; sasa wameona wenzao wamepata mikopo ambao wamekuja kwa mwaka huu na wale wa mwaka wa pili na wa tatu wana vigezo vya kupata mkopo; sasa kufuatana na bajeti ilikuwa kidogo, hawakupata mikopo. Naiomba Serikali, basi wale wa mwaka wa pili na wa tatu waruhusiwe sasa, wafungue dirisha ili waombe na wenyewe ili wale ambao walikopa waweze kukopeshwa tena. Kuna wanafunzi wanapata taabu sana wa mwaka wa pili na wa tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni changamoto hasa na tumejadili sana hata kwenye Kamati ni kumiliki akaunti za benki. Wananchi, hasa kwenye vikundi, imetuletea shida sana kwenye vikundi. Unaweza ukaona kikundi kina akaunti au kijiji kina akaunti, sasa kwa sababu wanaweka fedha kwa msimu, akiwa na fedha ndiyo anakwenda kuweka, kama hawana fedha wanaweza wakakaa hata miezi sita hawajaweka fedha. Kwa hiyo, akaunti yao inaonekana iko dormant. Sasa ikiwa dormant, wakipata fedha, wakitaka kwenda kuweka tena kwa mara ya pili (hata kwenye Vyama vya Ushirika hili tumeliona), wanasema akaunti yako imefungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni tatizo kubwa sana, naomba, Waziri wa Fedha, awaambie mabenki, mtu akiweka akaunti yake, kwa nini ifungwe? Kwa sababu akianza process upya, anasema nenda kachukue barua kwa Mwenyekiti, nenda sijui kwa Mtendaji, anaanza process upya. Hiyo inawakatika tamaa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi Wabunge kwa mfano hata kwenye Mfuko wetu wa Jimbo ukitaka kupeleka fedha kijijini kwa ajili ya maandalizi ya kununua vifaa kule kijijini, utasikia akaunti imefungwa. Kwa hiyo, unashindwa kupeleka fedha. Wananchi kule kuji-organize kuanza upya process inachukua muda mrefu na vijiji vyetu viko mbali sana na benki. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri atoe tamko kwamba benki vile kusema kwamba akaunti ziko dormant, hilo neno lisiwepo. Mtu ameonyesha ID number tu, akaunti inakuwa active; akiweka hata shilingi 10,000/= au shilingi 20,000/=, akaunti inakuwa active kwa sababu details zote zinakuwepo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine, Benki Kuu walifanya kitu kizuri sana katika kupunguza riba kwa mabenki. Ile ilikuwa kwamba, wanapunguza riba kwa mabenki ili mabenki yale yaweze kukopesha wananchi. Tunajua kule kwa wananchi kuna wafanyabiashara wadogo, wafanyabiashara wakubwa na wafanyabiashara mtu mmoja mmoja. Sasa impact kwa wananchi bado haijaonekana, yaani ile juhudi ya Serikali kuwaambia kwamba wapunguze riba kwa mabeki ili ilete impact kwa wananchi na wenyewe wale mabenki ya biashara yapunguze kwa wananchi, hayajafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi bado wanalalamika, riba ni kubwa sana, kubwa sana. Sasa na hilo naomba Serikali ifuatilie ili kuondoa malalamiko hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine, nimeona kwenye Mpango, umekaa vizuri kuhusu masuala ya umeme vijijini. Serikali imefanya kazi vizuri sana. Hata kwenye vijiji vyangu vyote, upimaji, survey imeshafanyika, ingawa kuna vijiji vingine bado kupeleka nguzo. Kuna sehemu nyingine nguzo zimelala tu chini, wananchi wanalalamika. Naomba twende speed. Tumesema mwaka 2021 vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme, vitongoji vyote vitakuwa vimepata umeme. Sasa ile kasi tuliyokuwa tumeanza nayo mwanzo iendelee, maana tunaona sasa Makandarasi kama wanafifia hivi, wananchi wanashindwa kuelewa vizuri. Tuwahamasishe wafanye kazi vizuri, kwa sababu Serikali ina lengo zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasema kwamba, kuna vijiji wanapita bila kupingwa kwenye uchaguzi. Kwa nini wasipite bila kupingwa kama wanaona umeme uko tayari pale? Wananchi wanachotaka ni huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaona mtandao wana maji, wako wako site. Ingawa kuna chagamoto ya maji, lakini watu wako site, sasa mtu atapinga nini? Wanaona majengo ya shule ambayo yalikuwa hayajaisha yanamalizika, wanaona Vituo vya Afya vinajengwa, Hospitali za Wilaya zipo; sasa mtu atalalamika nini? Barabara zinajengwa, sasa utalalamika kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, isipokuwa, tuishauri Serikali kuongeza speed ya kuhakikisha kwamba mazingira bora kwa wananchi yanakuwepo kujenga hospitali, kujenga Vitu vya Afya, kujenga Zahanati, barabara, umeme; tukiimarisha haya, ndiyo maisha bora kwa jamii tunayoyataka. Tukisema kupunguza umasikini, maana yake tunaangalia vitu kwa jamii vipo? Hospitali zipo? Madawa yapo? Hivi vitu vinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ni process, usije ukasema utafika siku moja, ukasema sasa tumetosheka kila kitu tunacho. Hata ukienda nchi za wenzetu zilizoendelea, barabara wanajenga mpaka leo. Hata ukienda pale Uingereza, London penyewe pale mjini, barabara mpaka leo hii wanajenga. Ukienda hata Marekani, barabara mpaka leo hii wanajenga. Kwa hiyo, hii ni process ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda wangu umeisha, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Serikali kwa kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari (‘O’ level).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu idadi kubwa ya kujiunga na shule za msingi; watoto wameongezeka kwa idadi kubwa sana. Hii imepelekea pia ongezeko la watoto wa sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Serikali na Waheshimiwa Wabunge kwa kununua madawati kwa shule za msingi. Sasa watoto wetu wanasoma vizuri wakiwa wanakaa kwenye madawati. Pongezi kwa kujenga maabara kwa shule za sekondari; pongezi kwa Serikali kwa kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri kwa Serikali:-

(a) Serikali iongeze kujenga hostel kwa ajili ya watoto wa shule za sekondari ili kupunguza umbali kwa watoto;

(b) Kuongeza idadi ya walimu hasa walimu wa masomo ya sayansi kwa shule za sekondari;

(c) Kuongeza nyumba za walimu;

(d) Kuongeza kujenga madarasa na ofisi kwa ajili ya walimu wetu;

(e) Posho iwepo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari;

(f) Kuongeza mishahara kwa walimu wote wa shule za msingi na sekondari; na

(g) Kuboresha mazingira ya walimu, kwa mfano, nyumba kuwekewa umeme, maji yawepo shuleni, vifaa vya kufundishia viwepo, usafiri wa shule uwepo kwa kila shule ya msingi na sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi sana kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa juhudi zake nzuri za kufufua na kujenga viwanda katika nchi yetu ya Tanzania. Tumeona jitihada kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano. Nakubaliana kabisa kuwa nchi ya Tanzania ni tajiri sana, ina kila kitu, lakini tatizo kubwa ilikuwa ni maamuzi magumu tu. Sasa tumepata Rais mwenye maamuzi magumu na sahihi. Serikali haijengi viwanda, lakini Serikali inasaidia katika kutoa miongozo ya kujenga viwanda na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mufindi Kusini tuna viwanda vingi sana kwa mfano, Kiwanda cha Chai (Uniliver Tea Company Limited), Mufindi Paper Mill Limited (MPM); Mufindi Tea Company Limited. (MTL), Kiwanda cha Pareto, Kiwanda cha Mbao (Sao Hill); pia kuna viwanda vidogo vidogo vingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri kwa Serikali, naomba Serikali ijenge miundombinu ya barabara, umeme na maji ili kuwezesha wawekezaji kufanikisha uzalishaji wa bidhaa bila matatizo. Viwanda vinashindwa kusafirisha bidhaa kwa sababu ya babaraba mbovu. Barabara hiyo ni Mafinga hadi Mgogolo, Nyololo hadi Mtwango. Kuna tatizo kubwa la stendi ya reli pale Mgololo ili bidhaa ziweze kusafirishwa kwa njia ya treni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni uti wa mgongo, pia Tanzania tunategemea sana kilimo katika maisha ya kila siku. Naomba Serikali iwezeshe tuwe na viwanda vya kusindika vyakula, viwanda vya nyama, viwanda vya samaki, matunda, juisi na viwanda vya maziwa ya ng’ombe. Tukiwa na viwanda, vijana wetu watapata ajira katika viwanda hivyo. Kwa hiyo, kuwa na viwanda vinavyotumia nafaka ya kilimo tunaweza kuendelea na kukuza uchumi kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba Serikali ipeleke mbolea kwa wakulima kwa muda unaotakiwa. Jimbo la Mufindi wakulima wanaanza kulima kuanzia mwezi wa Tisa hadi mwezi wa 11. Muda huo ndiyo mbolea inatakiwa kwa wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kupanga bei ya mbolea ambayo mkulima mdogo anaweza kumudu kununua kwa bei ya chini. Pia naomba Serikali ilipe madeni ya Wakala wa Mbolea. Wapo watu ambao wanaidai Serikali kwa sababu walikopa kwenye mabenki ili kuongeza mitaji yao, basi naomba Serikali iwalipe hao mawakala wa mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba Serikali ipeleke matrekta ili kulima kilimo cha kisasa. Matrekta yatasaidia sana kukuza kilimo katika nchi yetu. Pia iwepo mikopo ya pembejeo kwa wakulima wadogo wadogo. Kuwepo na vikundi vinavyojihusisha na kilimo, uvuvi na ufugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Wizara, kwa kazi nzuri mnayoifanya kutatua migogoro ya ardhi katika nchi yetu. Naiomba Serikali, kuendelea na juhudi ya kutatua migogoro ya ardhi katika Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji. Kuna migogoro ya kugombania mipaka kati ya wilaya na wilaya nyingine, mipaka ya kata na kata, kuna migogoro ya kijiji na kijiji. Ili kumaliza kabisa migogoro hii naishauri Serikali kupima ardhi yote ili kupata matumizi bora ya ardhi nchini. Kuna tatizo la ujenzi holela katika miji yetu naishauri Serikali, kusimamia upangaji wa miji yetu, kuwa na master plan ya miji na kuwaelimisha watu kufuata sheria ya mipango miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwapimie mashamba wakulima ili kila mkulima kuwa na shamba ambalo limepimwa na analipia. Katika upimaji naiomba Serikali iwapimie wananchi kwa bei nafuu ili hata watu wenye vipato vidogo, waweze kusajili mashamba yao na kupimiwa. Serikali ipunguze bei ya upimaji wa viwanja, wananchi wanashindwa kununua viwanja vya Serikali sababu bei ipo juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kutoa mchango kwenye Kamati hizi mbili; Kamati ya Miundombinu na Kamati ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kutoa pongezi nyingi sana kwa Serikali. Kuna watu wengine wamekuwa wanachangia; kwanza, nimesikitika sana kwa sababu kuna kitabu hapa ambacho ni taarifa ya Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda ukurasa wa 12 kuna kipengele kidogo, wameeleza vizuri Serikali imefanya nini? Imeeleza vizuri kabisa, kwamba katika miundombinu; ukichukua kipengele kimoja, sitaki nichukue vitu vingi, kwa mfano pale kwenye ujenzi wa reli na tulishaongea ili nchi iweze kusonga mbele, uchumi wa Taifa ukue ni lazima tuhakikishe kwamba tumeimarisha usafiri wa reli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nilikuwa nasoma kwamba Serikali katika mipango yake mizito kuna ujenzi wa reli wa Dar es Salaam – Morogoro kilometa 205; kuna ujenzi wa reli kutoka Morogoro – Makutupora kilometa 336; kuna ujenzi wa reli Makutupora – Tabora kilometa 295; kuna Tabora – Isaka, kilometa 133; kuna Isaka – Mwanza, kilometa 250; halafu mtu mwingine anasema haoni. Jamani, hayo ni maendeleo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, tukitaka uchumi wa nchi uendelee lazima Serikali ijikite kwenye miundombinu ya reli ili tuweze kusafirisha mizigo mizito kwenye reli zetu na barabara za lami tuweze kusafirisha mabasi yetu na magari madogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulishasema ndani ya Bunge hili, Serikali imefanya mambo mengi sana na tunayaona kwa macho. Nami kama Mbunge, naiunga mkono Serikali na iendelee na mikakati mizuri. Tunategemea kwamba tukifika mwaka 2020 nadhani maswali mengi sana yatakuwa yamejibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ujenzi wa barabara kuna barabara nyingine zina changamoto. Naishukuru sana Serikali kwamba kwenye mipango ile ya Serikali ilishawekwa tayari. Kuna barabara moja ambayo wanaisema kila siku na huko kuna viwanda vingi na tumesema nchi yetu ni ya viwanda; kuna barabara ile ya Mafinga – Mgololo kilometa 84. Naiomba Serikali kama ilivyokuwa imeahidi, basi utekelezaji wake ukianza kwenye bajeti inayokuja nitafurahi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, kuna barabara ile ya Nyororo mpaka pale Mtwani. Hiyo barabara ikiwekwa kiwango cha lami itatusaidia sana kwa sababu kule kuna viwanda vingi sana halafu maeneo yale mvua zinanyesha sana kiasi kwamba magari makubwa yanashindwa kupita na kusafirisha ile mizigo mizito. Kwa hiyo, naiomba Serikali, katika ukanda huu wa Kusini, ikitujengea zile barabara za lami, basi itakuwa imefanya vizuri ili wenye viwanda vikubwa waweze kusafirisha mizigo yao. Vile vile hii barabara tunajua kabisa tuna kiwanda kikubwa cha Mgololo ambacho kinatengeneza karatasi kule, kinashindwa kusafirisha mizigo mizito, kwa hiyo, itakuwa imetusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye nishati na madini kwa sababu muda ni mdogo; kwanza, nitoe pongezi kwa Serikali. Natoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini. Kwa kweli alifanya ziara kwenye Jimbo langu na aliongea na wananchi na kupongeza sana. Alichokiongea siku ile, utekelezaji wake umeanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo moja la Watanzania, unataka kitu kifanyike mara moja, siku moja; lazima kuwe kuna hatua. Mimi nampongeza Waziri, sasa hivi ninavyoongea mkandarasi yuko site, kama alivyoongea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, bahati nzuri ameandika kwenye ripoti yake; kuna maeneo yale ambayo yalirukwa. Katika survey kuna vitongoji vingine vimerukwa, naomba vile vitongoji ambavyo vimerukwa viweze kupewa survey tena ili viweze kupewa umeme kwa sababu wananchi wanalalamika, wanajua kama hawatapewa. Nakuomba kwenye majumuisho yako uwaambie wananchi kwamba yale maeneo yote ambayo yalikuwa yamerukwa, hayakufanyiwa survey kwamba mtafanya survey na watapewa umeme kama kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, zile gharama za uingizaji umeme, naomba kwenye majumuisho tuwaambie wananchi zijulikane vizuri. Kwa sababu kuna watu wengine wanasema ile ya 177,000 kuna wengine kuna ile 27,000, kwa hiyo, inaleta mchanganyo kidogo. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri anapotoa majumuisho, aliweke sawa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wengine wameanza kuchangia, wanasema wachangie fedha ya nguzo. Yaani mtu anataka aweke umeme pale, anaambiwa na TANESCO kwamba achangie fedha fulani. Mwananchi mmoja alisema anaambiwa achangie Sh.500,000 kwa ajili ya nguzo. Namwomba Mheshimiwa Waziri hili aliweke sawa, kwamba zile nguzo ni bure au kuna watu wengine wanatakiwa wachangie pale? Tunaona tunapata mchanganyiko sisi Wabunge tunaulizwa maswali ya namna hiyo. Kwa hiyo, leo tunategemea Mheshimiwa Waziri atupe majumuisho, masuala ya nguzo tuhakikishe kwamba kama ni bure ijulikane watu wanapelekewa bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu kuna shule nyingi tu zimerukwa. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri, zile Taasisi hasa shule, Zahanati na Vituo vya Afya, basi kama kuna exemption ya kuweka umeme kwenye hizi Taasisi, basi Mheshimiwa Waziri tunaomba majumuisho tuelezwe vizuri ili wananchi waelewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana juhudi za Serikali kwa kazi nzuri zinazofanyika kwa ajili ya manufaa ya wananchi. Naipongeza sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri hasa katika kuwezesha wananchi kuongeza kipato kwa kupitia mikopo kwa vijana na vikundi vya wanawake, SACCOS na VICOBA. Ushauri kwa Serikali, naomba Serikali kujenga Hostel kwa kila sekondari ili watoto wetu waweze kukaa shuleni na kuepukana na kupata mimba kwa watoto wa kike na kuongeza kiwango cha elimu kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, naishauri Serikali ipeleke umeme kila Shule ya Msingi na Sekondari, ijenge miundombinu ya shule kama vile ujenzi wa vyoo vya shule, nyumba za Walimu pamoja na kumalizia maboma ya madarasa ambayo wananchi wameshajenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kilimo, Serikali ipeleke mbolea na mbegu kwa wakati au kwa kufuata kalenda ya kilimo. Pia ilipe deni la Wakala ambao bado hajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali itatue tatizo la maji hasa vijijini na kuongeza Mfuko wa Maji ili bajeti ya Wizara ya Maji iwe inatosha. Pia kuanzisha Bodi ya Maji kila Wilaya; kuwe na chombo ambacho kitafuatilia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeshapeleka fedha nyingi na miradi hiyo haijakamilika. Serikali imalizie maboma ya Vituo vya Afya na Zahanati ambazo bado hazijakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, madini ni chanzo kizuri cha mapato kwa Taifa letu. Pongezi kwa Rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Mawaziri wote na Makatibu wote wa Wizara kwa kazi nzuri ya kusimamia Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali kama ifuatavyo:-

(i) Ifungue Ofisi za Utafiti kila Wilaya ili kufanya utafiti maeneo yote yenye viashiria vya madini.

(ii) Vibali vitolewe kwa watu wenye mitaji ya kutosha.

(iii) Usimamizi na ufuatiliaji wa walipa kodi katika sekta ya madini uboreshwa.
(iv) Elimu kwa wachimbaji wadogo wadogo itolewe na vifaa vya kuchimbia wachimbaji wadogo wapewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni baadhi ya ushauri wangu kwa Serikali ili madini yetu yawe na faida kwa Taifa letu. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kubwa kwa Serikali kwa juhudi kubwa inayofanya ya usimamizi wa mapato na matumizi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ubunifu wa kutoa vitambulisho vya wajasilimali wenye mitaji midogo. Hili litasaidia kuwatambua na kukuza mitaji yao. Hili ni jambo jema sana kwa Watanzania. Inakadiriwa vitambulisho 670,000 tayari vimetolewa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iongoze vizuri katika utoaji wa vitambulisho, sababu kuna wajanja wataanza kujifanya kuwa ni wajasilimali wadogo wadogo ili kukwepa kulipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya uchumi inaonekana ni nzuri, hii inatokana na Serikali kusimamia vizuri shughuli za kiuchumi. Kwa mfano, ongezeko la viwanda nchini, kuimarisha ujenzi wa barabara, umeme, maji, Vituo vya Afya na elimu bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iendelee kutoa elimu kwa Watanzania kuwa, uchumi wa nchi yetu unajengwa na Watanzania wenyewe. Kwa hiyo, kila mtu ana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii katika nafasi yake kama ni mkulima alime sana, kama ni mfanyabiashara afanye biashara sana, kama ni mfanyakazi wa kuajiriwa afanye kazi kwa bidii na uaminifu kwa maslahi ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Serikali kwa kusimamia vizuri suala la kupunguza mfumko wa bei kutoka 4.0 (2018) hadi 3.0 Januari, 2019. Hii ni hali nzuri kwa Watanzania. Serikali imesimamia vizuri hasa katika hali ya upatikanaji wa chakula ili kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata chakula cha kutosha na kupunguza njaa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanategema kilimo, naomba Serikali iimarishe viwanda vya pembejeo hasa viwanda vya mbolea ili wakulima wanunue kwa bei ndogo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na mazao ya biashara, kwa mfano, njegere, njugu, mbaazi, ufuta, maharage, alizeti na njugu. Haya ni mazao ambayo yanawasaidia sana wakulima wadogo wadogo kupata fedha kiurahisi na inasaidia sana kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani ni Wizara muhimu sana katika usalama wa raia na mali zao. Wizara hii inatakiwa Serikali kuwa na mikakati thabiti ya kutoa mafunzo kwa vijana wetu Askari ili kuwa imara kila wakati, kuboresha mazingira yao kwa kuwajengea nyumba, kupewa usafiri kama pikipiki, nyumba zao kuwekewa umeme, maji na kulipwa posho na kuongezewa mishahara yao. Pia kupandishwa vyeo kwa Askari hasa kitengo cha Polisi, Uhamiaji na Magereza, vyeo vyao vinachelewa sana, namaanisha kuwapandisha vyeo Askari wanaostahili kupandishwa. Naipongeza Serikali kwa kuwajengea nyumba Askari wa Uhamiaji wa hapa Dodoma. Hili ni jambo zuri sana kwa kuwajali Askari wetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi kwa Serikali kwa kutujengea Kituo cha Afya Malangali, Kata ya Malangali ambacho kitatoa huduma katika Kata tatu za Ihwanza, Idunda na Malangali yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi pia kwa kutujengea Hospitali ya Halmashauri ya Mufindi ambayo itahudumia kata 27 katika Wilaya ya Mufindi pia itatoa huduma kwa watu wote ndani na nje ya Watanzania sababu ni Halmashauri yenye wafanyakazi wengi sana na wawekezaji wengi wakubwa na wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kumalizia Kituo cha Afya cha Kata ya Mtwango na Kituo cha Afya cha Kata ya Mninga. Serikali imalizie ujenzi wa Zahanati katika Kijiji cha Nzivi, Kinegembasi, Iramba, Nyigo, Udumka na Ikaning’ombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali ituletee Watumishi katika vituo vyetu tuna tatizo kubwa la watumishi katika Jimbo la Mufindi Kusini. Nitashukuru sana kama Serikali itatekeleza kwa muda maombi hayo.

Ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Spika, barabara ya Mafinga – Mgololo, barabara ya Mgololo – Mtwango, barabara ya Kasanga – Mtambula – Nyigo ni za muhimu sana katika kuinua uchumi kwa wananchi wa Mufindi. Kuna viwanda vya Chai, Mbao na Karatasi (MPM). Naomba Serikali ianze kujenga kiwango cha lami ili ziweze kupitika kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali isimamie ujenzi wa barabara za vijijini ambazo zinatengenezwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA). Barabara ya Maguvani, Mtambale, Kilolo imeharibika sana wananchi wanashindwa kusafirisha mazao yao. Barabara ya Nyanyembe hadi Idunda, barabara ya Malangali hadi Idunda, barabara ya Sawala hadi Iyegeya, barabara ya Maduma hadi Makugali zipo chini ya TARURA, zimeharibika sana. Naomba Serikali itengeneze barabara hii ili wananchi waweze kusafirisha mizigo yao, pia kurahisisha shughuli zao za kila siku.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ijenge minara katika Kata ya Idete, Ihowanza, Idunda na Kiyowela. Maeneo haya hakuna mawasiliano kabisa, wananchi wanashindwa kupata mawasiliano kiurahisi.

Mhesimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, maliasili na utalii ni muhimu sana katika kukuza Pato la Taifa. Ili kukuza utalii Serikali inabidi kupunguza migogoro kati ya wananchi na Wizara. Kuna maeneo ya wananchi yamechukuliwa na Wizara, kwa mfano eneo la Iyegeya Kata ya Luhunga. Eneo hili limechukuliwa na hifadhi ilhali hakuna kitu chochote pale, wananchi hawana eneo la kulima na kufugia wanyama wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kuwarudishia wananchi maeneo ya Kitasengwa, Kata ya Mkangu, Ihomasa Kilolo, Kata ya Kasanga na Iyegeya Kata ya Luhunga. Maeneo hayo ni maeneo ambayo yapo ndani ya vijiji hivyo, wananchi wanakosa maeneo ya kulima ili kupata chakula na maeneo ya kufugia mifugo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mufindi tulikuwa na center ambayo ilikuwa kama chuo cha misitu ikiwa chini ya Wizara ya Misitu, sasa chuo hicho hakipo na mafunzo ambayo yalikuwa yakitolewa na Idara ya Misitu hayatolewi katika chuo hicho. Naomba Serikali kufufua Chuo cha Misitu Mufindi ambapo kuna shamba kubwa sana la misitu katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naiomba Serikali kuendeleza kutoa misaada kwa vijiji ambavyo vinazunguka Msitu wa Sao Hill. Vijiji hivyo ni; Kata za Nyololo, Igowole, Mninga, Mtwango, Mninga, Luhunga na Mkungu. Kata saba, vijiji 42 ambavyo vipo katika Wizara ya Maliasili na walitoa ardhi kwa Wizara hii ili kupata miti ya mbao, sasa wananchi wakosa misaada ya kijamii kama ukosefu wa maji, vituo vya afya kwa Kata ya Mninga na Kata ya Mtwango.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara kuendelea kusaidia shughuli za kijamii. Napendekeza kuwajengea majengo ya kituo cha afya au zahanati na si kutoa fedha. Pia, kuwakarabatia miundombinu ya maji pamoja na barabara ili wananchi waweze kukuza uchumi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Sheria hii ni muhimu sana hasa kwa matumizi ya binadamu, na imelenga maeneo nyeti kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kupitia taarifa hii, hasa napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, ameeleza vizuri sana kwenye ripoti yake ambayo na mimi nimekuwa very interested na hivi vitu kwa sababu vinatugusa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona dawa nyingi sana zikitumika lakini tusijue madhara yake na kama kutakuwa na kuna Mkemia Mkuu wa Serikali na sheria hii ikawa imekaa vizuri pale tukibaini kwamba dawa tunazotumia zina madhara makubwa kwa binadamu hii itatusaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano tumeona dawa nyingi sana zikichomwa moto, na hilo lilikuwa ni tatizo kubwa sana. Kuna dawa nyingine zinakuwa hazijagundulika lakini zinaweza zikatumika kwa binadamu na binadamu akapoteza maisha, sasa sheria imeweka wazi, na nashukuru sana kama hii tukiipitisha, nadhani itapita kwa sababu imekaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwamba kuna maduka mengie wanasema kwamba wanauza dawa ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu, na kuna sehemu nyingine hata vyakula vinauzwa lakini vinaoneka havifai kwa matumizi ya binadamu. Inaonekana kama uchunguzi ulikuwa bado haujafanyika vizuri, lakini tukiwa na maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ikiwa inapitisha maana wameandika majukumu hapa, wakiwa wanakagua kwa umakini tutaweza kunusu watu wetu na maisha ya watu yakakaa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwamba kuna dawa nyingine tukiwa tunatumia, unasikia dawa labda zimeingizwa lakini baada ya muda mfupi tu zime-expire. Kumbe inatakiwa mamlaka ifanye kazi ya kufuatilia hata kabla hazijaingizwa hizo dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo yameandikwa hapa hata kuna dawa nyingine zinatumika kukupima kwa matumizi ya maji na huko vijijini tunatumia sana maji bila kupima sasa kama Mkemia Mkuu wa maabara akiwa anasimamia vizuri binadamu tukiwa tuna uhakika kwamba yale maji tunayotumia yanapimwa hatuwezi kupata magonjwa mbalimbali ambayo binadamu tunayapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niongelee sana masuala ya bodi, kama ilivyopendekeza mimi naunga mkono kabisa bodi imekaa vizuri, members wakiwa tisa, bodi ikiwa kubwa sana itashindwa kufanya kazi yakevizuri lakini tukiwa na watu wachache wanaweza wakafanya kazi vizuri kwa ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi hapa naungana na Waziri kwamba hapa mapendekezo haya yamekaa vizuri, tusiweke bodi kubwa sana ambayo baadaye ianweza ikaleta usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ambayo yameguswa hasa kwenye vinasaba, nadhani bahati nzuri Dkt. Kigwangalla yupo pale ametuelekeza vizuri sana, na hapa nimeona vinasaba vinasumbua sana. Kuna watu wengi sana hasa; samahani sana Waheshimiwa mtanisamehe kidogo; Watanzania wengi sana wanaweza wakabambikizwa hata watoto kwa sababu hawajui vitu kama hivyo. Sasa hapa sheria ikikaa vizuri kwenye vinasaba hapa nimesoma vizuri ikikaa vizuri nadhani hata uchunguzi wa watoto wetu utakuwa unasaidia kila mtu ajue familia yale vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nimeona kwamba kuna sehemu nyingine inatokea anaenda mtu utasikia amezika mtu ambaye sio wa kwake ameshindwa kutambua, sasa hii sheria itasaidia hata ufanisi wa kazi watu wanajua mtu kama amekufa amewekwa pale mortuary kwenye watu wengi waliokufa utambuzi ndio utakaomsaidia yule ndugu kutambua kama ni ndugu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona watu wengi sana wanazika mtu mapaka mtu anazikwa kabisa halafu baadaye wanasema kwamba tunaenda kufukua ilikosewa baada ya siku kadhaa, kwa hiyo, nadhani usumbufu huu iitakuwa imesaidia sana.
Vilevile tumeona hata katika historia ya utawala wa huko nyuma kwenye vinasaba imeelekeza vizuri sana. Wengi tulikuwa hatujui lakini sasa hii sheria ikikaa vizuri nadhani tutakuwa tunajua hata historia ya huko nyuma ilikuwaje.
Mheshimiwa Naibu Spika ukiangalia kwenye Sheria ya Vinasaba Sura ya 73, Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwanda, nataka niseme kwamba viwandani kule; namshukuru sana Naibu Waziri wa Afya umefanya kazi nzuri sana, tumeona kwamba mkitembelea kule viwandani. Kuna dawa zinatumika katika production kwenye viwanda na zile dawa zinazotumika kwenye production hatujajua kwamba zina madhara gani kwa binadamu. Kwa sababu tumeona kwa mfano ukipita nje ya kiwanda na kiwanda kimejengwa vizuri lakini ukipita maeneo yale kuna harufu kali kutokana na zile dawa. Sasa hatujui kama zile dawa zina madhara makubwa kwa binadamu, na kuna wafanyakazi wanafanya na wenyewe hawajui kama kuna harufu tu ile ya production nzima, dawa zinapotumika pale zina effect zipi kwa binadamu kwa hiyo hii sheria itatusaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, na tumeona, nataka nitoe mfano kule kwangu tuna kiwanda kimoja cha karatasi pale, ukipita maeneo yale kuna harufu kubwa sana. Sasa wataalamu wanasema hiyo ishapimwa haina effect, sasa ile harufu bado tunaona kwa sababu ni chemical, inaweza ikawa na madhara makubwa. Nadhani masuala kama haya tutakuwa tunaiuliza Serikali kwa sababu tutakuwa tuna Mkemia Mkuu wa Serikali, atupe majibu sahihi ya matumizi ya hizi dawa katika production kwenye viwanda vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, nakumbuka tulipata shida sana mwaka 2012/2013; hata kile kikombe cha babu pale, nayo ile ni dawa ambayo inatumika. Lakini pamoja na kwamba ilikuwa inatumika inawezekana ilikuwa nzuri kwa binadamu au sio nzuri. Tulipata shida sana katika upimaji wa hiyo dawa. Mpaka sasa hivi majibu ndiyo yaliyotoka; lakini bado inawezekana ile dawa tumeacha kutumia kumbe ni nzuri au ni mbaya kwa matumizi ya binadamu kwa sababu hatuna majibu sahihi, lakini tungekuwa na majibu sahihi kama sasa kungekuwepo na sheria. Sasa tunashindwa tumuulize nani. Sasa zile dawa ambazo zinatumika kwa matumzi ya binadamu hii sheria itatusaidia. Na tumeona kuna dawa za aina mbili; kwa mfano kuna dawa hizi za asili na zenyewe nadhani kwa Mkemia Mkuu zitapita kwa sababu tukishaweka utaratibu tutasema hata hizi dawa za asili ziwe zinapimwa, hatuwezi kusema hazifai wakati hazijapimwa. Kwa hiyo, wakipima tutakuwa tunajua kama zinafaa au hazifai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna dawa nyingi sana zinatumika hasa kwa matumizi ya binadamu. Tuchukulie wanasema kuna dawa inaongeza maumbile ya mwili; sasa hatujui hizi dawa zinaongeza maumbile kwa kiasi gani na effect yake ni ipi na daktari leo utatusaidia. Kwa mfano mtu anapaka sehemu ya makalio halafu yanakuwa makubwa, ni sehemu hiyo tu, lakini bado hatujagundua effect yake kubwa kwa matumizi haya. Nadhani hii itatusaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tumeona, kwa mfano kuna vidonge vingine mtu akimeza anabadilika anakuwa mzungu siku baada ya siku, lakini bado na yenyewe hatujagundua effect yake kubwa. Sasa hii itatusaidia sana, yaani mtu ni mweusi halafu anabadilika ghafla anakuwa mweupe, anakuwa mzungu, hivyo ni lazima ufanyike utaalamu wa kimaabara tuone.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna magonjwa mengi tutasikia kansa inatokea sijui inawezekana hizi dawa zinatusababishia na hii tukigundua kwamba ni matatizo kwa matumizi ya binadamu tunakuwa na uwezo wa kuyazuia kuingia kwenye nchi yetu, lakini lazima tufanye study ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano huwa najiuliza mara nyingi sana hii dawa ina uwezo wa kubadilisha mtu awe kama mzungu lakini haina uwezo wa kubadlisha mzungu kuwa mweusi. Kwa hiyo, lazima utafanyika utafiti ambao unatosha kwenye maabara kama hizi. Lazima tuwe makini sana na hivi vitu tusije tukawa tunabadilisha tu hatujui umakini wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, hii nadhani ni point ya mwisho, nataka tujikite vizuri sana na wataalamu watatusaidia, juu masuala ya vyakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna vyakula vingi sana vinatoka nje, na bahati nzuri sasa hivi tunasema hapa ni viwanda tu. Hivi viwanda lazima tujikite hasa chakula kwenye chakula, viwanda vizalishe chakula cha kwetu hapa hapa, tu-process sisi wenyewe. Kuna vyakula ambavyo vinaagizwa nje mimi bado nina wasiwasi, tuna vyakula vingi sana vinatoka nje lakini havijapita kwenye maabara tukaona umakini wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kama kuna dawa nyingine; tunasikia huko wanachoma dawa hazifai sijui kuna duka fulani, lakini kwenye vyakula hatujaona vyakula vikichomwa moto. Lakini tukiwa na sheria na Mkemia Mkuu wa Serikali akisimamia pamoja na Bodi yake; na bahati nzuri nimesoma anasema wanataka wa-propose hata kila kanda kuwe kuna centers zake hii itakuwa imetusaidia kwa sababu Tanzania hii ni pana. Kwa mfano tukiwa na Kanda ya Mbeya, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Mashariki ya Pwani; hii itatusaida sana kuhakikisha kwamba ufanisi wa kazi unakuwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii ya msingi sana kwa maisha ya binadamu, naungana na taarifa ya Mheshimiwa Waziri. Ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa huduma za habari ni muhimu sana katika kuhabarisha jamii katika masuala mbalimbali yanayohusu maisha ya watu katika shughuli zao za kila siku. Kwa hiyo, katika kuhabarisha jamii lazima ziwepo sheria ambazo zitalinda haki ya mwananchi. Hii itasaidia kutooneana katika utoaji wa habari. Ipo tabia ya kuchafua watu bila kufuata sheria.
Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali na Wizara ya Habari kwa kuleta Muswada huu ili kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya sheria ambavyo haviendani na mazingira ya siku hizi. Mwandishi wa Habari lazima awe na taaluma ya habari ili aweze kutoa habari ambayo ina quality ya habari. Kwa mfano, unatoa habari inayohusu masuala ya uchumi wa nchi, lazima uwe na uelewa au elimu ya uchumi ili usiweze kupotosha habari inayohusiana na suala hilo la uchumi wa nchi ambayo unaitolea habari.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mwandishi wa Habari lazima awe amesoma masuala ya Uandishi wa Habari, pia kujua kanuni na Sheria ya Habari. Habari lazima izingatie haki za binadamu ili kuhakikisha utu wa binadamu unalindwa. Ili wananchi kupata habari sahihi inayohusiana na taarifa ya jamii katika maeneo ya kisiasa, elimu, kiafya, kiuchumi na kijamii lazima taarifa au habari iwe na usahihi ili kuepuka upotoshaji ambao unaweza kuhatarisha usalama wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana kabisa kuwa vyombo vya habari ni vya muhimu sana katika kuhabarisha jamii katika masuala mbalimbali, lakini kwa kufuata Sheria ya Habari ambayo imetungwa na Bunge kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia machache. Kwanza kabisa, nianze kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya kuleta Muswada huu wa PPP ambao ni wa muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, PPP itasaidia sana katika kuinua maeneo kama manne. Eneo la kwanza ni kiuchumi, kwa sababu uchumi ukitaka kukua lazima nchi ishirikiane na private sector. Kwa sasa hivi naona Mheshimiwa Waziri ameamua jambo la msingi sana, nami sitaki nijikite sana kwenye sheria kwa sababu tulijadili vizuri sana kwenye Kamati, nami naunga mkono asilimia mia moja kwa yale majadiliano ambayo tulikuwa tumefanya kwenye Kamati. Ripoti ya Kamati imeeleza vizuri na hotuba ya Mheshimiwa Waziri imekaa vizuri na sasa hivi tuna matumaini makubwa sana kwamba PPP itasaidia sana kuinua uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba lazima sasa Serikali ijipange vizuri kuchagua ile miradi ambayo nchi inaweza ikaingia na private sector ambayo italeta manufaa.kuna miradi mikubwa sana na tunalenga kwamba PPP siyo kwamba itafanya kila mradi, lazima kuwe kuna miradi ile ambayo ni kipaumbele cha Taifa. Tuna miradi mingi sana, lakini lazima tuangalie ile miradi ambayo inaleta faida. Kwa mfano, tunaweza tukawa tuna wawekezaji wakajikita kwenye kilimo. Taifa zima hili linaweza likawa na wakulima kumi tu, wakaingia katika PPP na hao waka-supply chakula cha kutosha na Serikali ikatoa support, hii itatuletea manufaa sana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ku-supply umeme kwenye vijiji vyetu; Serikali inafanya vizuri sana lakini ni mzigo mkubwa sana. Tukiingia na private sector waka-supply umeme kwenye nchi hii gharama za uzalishaji wa umeme badala ya Serikali kuingia sasa tutakuwa tumepunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kupunguza madeni makubwa ya kitaifa. PPP itapunguza deni badala ya kwenda kukopa na tunasema deni la Taifa linakua kila siku, sasa deni lile litapungua. Badala ya kukopa tujenge miundombinu ya umeme, kuna watu watajitokeza watafanya biashara. Kwa sababu PPP ni biashara, mtu atakuja hapa ili apate profit ila hawezi kupata faida bila kufanya miradi ambayo inaleta faida kwake. Siyo kwamba yule private company apate faida, cha kwanza tunaangalia Taifa letu linanufaika na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho nimekifurahia sana ni kwamba itaandaliwa mikataba na wataalam. Hapo ndiyo mahali pa kuzingatia sana. Kwenye mikataba hapa huwa panakuwa na matatizo makubwa sana. Hii PPP inaweza ikatuletea faida kubwa au ikatuletea hasara kubwa, itategemea na mikataba itakavyokuwa imeandaliwa. Kwa mfano, sasa hivi nimeona kwenye mpango kwamba tutakuwa PPP center ambayo itakuwa inashughulikia sasa kufanya analysis ya mikataba yote na kwenye PPP center pale wataajiriwa wataalamu. Nimefurahi sana kwenye hotuba ya Waziri amesema kwamba wataandaa wataalamu halafu wataenda kusoma. Kwa hiyo Serikali itasomesha watu. Kweli pale wanatakiwa wataalam ambao wamebobea kwenye sheria na miradi mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni muhimu sana na itasaidia kwa sababu tunaweza tukaingia kwenye PPP, kama hakuna wataalam wazuri tukaingia kwenye hasara kubwa sana kitu ambacho kitu hatukutegemea. Tukiwa na wataalam ambao wanafanya analysis ya project zote kubwa tutapata faida kubwa sana. Advantage moja ambayo ni kubwa ni kupunguza deni kubwa la Taifa. Kwa sababu ile miradi yote itajengwa na private sector ikishirikiana na Serikali. Hili litakuwa jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, hata kijamii, kwa sababu watu wengi sana watapata ajira. Haya makampuni makubwa yatakayokuja kufanya kazi hapa yatatoa ajira na watakaofanya kazi ni Watanzania. Kwa hiyo, itatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu vilevile kwa mfano, miradi ya barabara, hizi flyovers na hapa Dodoma nadhani Serikali ina mpango wa kujenga flyovers. Ni jambo zuri sana, miji yote inayokua barabara za flyovers ni za muhimu sana, tukiingia kwenye Public Private Partnership itasaidia sana. Badala ya Serikali kupeleka hela nyingi basi zile hela inazi- diverge inapeleka kwenye mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengine wanafikiri PPP itajihusisha hata kwenye miradi ile midogo midogo ambayo Serikali ingeweza kufanya kwa kushirikiana na wananchi wa kwa kawaida. Kuna mtu mmoja akawa ananiambia kwamba labda vyoo vya shule vimebomoka PPP itafanya siyo hivyo, watu wanatafsiri tofauti. Ni lazima iwe ni ile miradi mikubwa yenye kipaumbele cha Serikali ambayo italeta mafanikio makubwa kwa Taifa, hii itakuwa imesaidia sana. Tukisema PPP itasaidia hata ile miradi midogo midogo, sisi tukabweteka, tukasema kuna PPP tusifanye, itakuwa siyo sahihi. Lazima tuwe tuna selective ya miradi ambayo itatujengea sifa na Serikali itaondoa gharama za kuingiza fedha nyingi sana kwenye hiyo miradi mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutapata faida nyingi sana, hata ukienda kwenye utaalam, teknolojia sasa hivi inakua. Kwenye utaalam, wageni watakuja, wataleta ma-expert, kwa hiyo, unaweza ukaona wameleta hata mashine nyingine katika production ambazo sisi hatuzijui, vijana wetu watajifunza vitu vingi sana. Bahati nzuri hata kwenye viwanda, kuna mashine sasa hivi zinakuja mpya. Sasa ile itasaidia hata kutoa elimu kwa vijana wetu kwa practical ili waweze kumudu zile mashine ambazo zimetoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ushirikiano tu wa Kimataifa, nchi kama imeingia mikataba na nchi nyingine, kunakuwa na mahusiano, yale mahusiano yanajenga udugu.

Sasa hivi dunia imekuwa kama kijiji kimoja kwa sababu ya mawasiliano, watu wanatembeleana, wanafanya miradi pamoja, hii inasaidia sana. Tukijifungia hivi, tunasema wale wataalam wa nje wasije hapa tutafanya sisi wenyewe, kiteknolojia itakuwa bado hatujakua. Sasa hivi tutapanuka, kwa mfano, China wakileta miradi mikubwa hapa wakaajiri vijana wetu, watajifunza na tunakuwa na mahusiano mazuri ambayo yanajenga udugu katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, labda nisisitize tu kwamba lazima mikataba iangaliwe kwa makini sana. Ile PPP center ambayo itaundwa na Serikali lazima iangalie wataalam ambao watatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema kwamba tutakuwa na Steering Committee ambayo itapitia ule mchakato uliofanywa na PPP Center ili kumpelekea Mheshimiwa Waziri wafanya maamuzi na ile lazima iwe ya wataalam. Hata kama itakuwa ya viongozi wakubwa wamewekwa lazima wawe mtaalam wa kuangalia kwa sababu ile mchanganuo wa miradi ni wa kiufundi sana. Kwa hiyo, ni lazima wawepo wataalam ambao wanaweza wakaangalia vizuri kwamba miradi hii inaweza ikaleta manufaa kwa Taifa letu.

Mheshiimiwa Mwenyekiti, yangu ni hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Taaluma ya Walimu Tanzania ni jambo zuri kama itafanya kazi kwa kuwasaidia walimu wa Tanzania, walimu wana mahitaji mengi sana ambayo wanahitaji kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Walimu iangalie isije ikaanza kufanya kazi za Chama cha Ualimu Tanzania (CWT). Majukumu ya Bodi na CWT yawekwe bayana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wana michango mingi sana kwa mfano kuchangia CWT; Bima ya Afya; PAYE; LAPF/PPF na sasa Bodi ya Walimu. Makato haya yanaweza sababisha mwalimu kupata mshahara mdogo sana na kufanya maisha ya mwalimu kuwa magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupima kiwango cha elimu ya mwalimu siyo kazi ya Bodi, mwalimu anapimwa na chuo alichosoma ndiyo maana wanafanya mitihani. Labda Bodi isaidie katika kuangalia haki na maslahi ya mwalimu pamoja na mazingira ya kazi ya mwalimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kuangalia tabia ya mwalimu hii inaweza saidia kama Bodi itakuwa inaratibu semina na mafunzo mbalimbali kwa walimu ili wasijisahau katika kazi zao. Ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.