Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Francis Isack Mtinga (14 total)

MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza:-

Je ni lini Serikali itaweka vifaa vya maabara kwenye maabara zote za Shule za Sekondari katika Wilaya ya Mkalama zilizojengwa kwa nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ina jumla ya shule 20 za Sekondari ambapo 19 kati ya hizo ni shule za Serikali. Usambazaji wa vifaa vya maabara mashuleni huzingatia ukamilishaji wa vyumba vya maabara katika shule husika. Hadi Machi, 2021, Serikali imepeleka vifaa vya maabara kwenye shule 18 kati ya shule 19 za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, shule ya sekondari Kikhonda haijapelekewa vifaa kwa sababu haina vyumba vya maabara. Hata hivyo, Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi wa Kata ya Kikhonda wameanza taratibu za ujenzi wa maabara katika shule hiyo ili ujenzi utakapokamilika iweze kuingizwa kwenye mpango wa kupatiwa vifaa.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itaainisha mpaka kati ya Wilaya ya Mkalama na Hanang’ eneo la Singa na Limbadau ili kuondoa taaruki kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kuna mgogoro wa mipaka ya Vijiji kati ya Wilaya za Mkalama na Hanang ambao umekuwepo kwa muda mrefu licha ya jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ikwemo vikao vya ujirani mwema baina ya wahusika wa mgogoro, Serikali ilitekeleza uwekaji wa alama za mipaka iliyotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 266 la tarehe 14 Desemba 1973 lililotangaza Wilaya ya Mbulu na Hanang’. Chanzo kikubwa cha mgogoro huo ni baaadhi ya wananchi kutokukubaliana na alama za mipaka zilizopo kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 266 la uanzishwaji wa Wilaya ya Mbulu na Wilaya ya Hanang’.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri za Wilaya ya Hanang na Mkalama zimetenga jumla ya shilingi milioni 40 kwa ajili ya kupima Vijiji vya Singa na Limbadau ambavyo ndio vipo kwenye eneo la mgogoro. Serikali inatarajia mgogoro huo utamalizika, ahsante sana.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakarabati boma la kihistoria la Mjerumani lililopo Wilayani Mkalama ili liendelee kuweka historia na kumbukumbu kwa vizazi vijavyo na kuzalisha mapato kwa Serikali?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008, watu binafsi, Taasisi za Umma na Taasisi za Kidini, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinaruhusiwa kuhifadhi, kuendeleza na kunufaika na urithi wa malikale.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mambo ya Kale Sura 333 kifungu cha 16 kinazipa mamlaka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutunga sheria ndogo ndogo za kutunza na kuhifadhi maeneo ya malikale katika maeneo yao. Boma la kihistoria lililopo Wilaya ya Mkalama linasimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama. Hivyo, tunaishauri Halmashauri husika kulikarabati na kulihifadhi ili kiwe chanzo cha mapato na Halmashauri iweze kunufaika.

Mheshimiwa Spika, Wizara iko tayari kutoa ushirikiano na miongozo ya namna ya kulikarabati na kulihifadhi boma hilo la kihistoria lililopo Mkalama ili kulindwa kwa mujibu wa Sheria ya Mambo ya Kale. Ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasimamia ulipaji fidia kwa Wachimbaji Wadogo wa Kata ya Tumuli?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kukusu usimamizi wa Serikali juu ya fidia kwa wachimbaji wadogo wa Kata ya Tumuli, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, jitihada za pamoja baina ya Wizara na ufuatiliaji wa karibu sana wa Mheshimiwa Mbunge, mnamo tarehe 9 Agosti, 2021, malipo ya fidia ya shilingi 90,000,000.00 yalilipwa kwa wachimbaji wote 90 wa Kata ya Tumuli na malipo haya yalifanyika chini ya usimamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ili kupisha uwekezaji wa Kampuni ya PUBO Mining Limited. Ninakushukuru. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italirejesha Shamba la kupumzishia Mifugo la Kinyangiri kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa maeneo haya katika biashara ya mifugo na mazao yake, hususan kipindi hiki ambapo soko la nyama limezidi kuongezeka nje ya nchi, Serikali inakusudia kuendelea kuboresha maeneo yake yote ya mifugo ikiwa ni pamoja na eneo la Kinyangili ili kusudi biashara ya mifugo na biashara ya nyama nchini iweze kushamiri kwa kuzingatia viwango vyote vinavyotakiwa katika Soko la Kitaifa na Kimataifa. Ahsante. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya katika Halmashauri ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania inaendelea kutekeleza mpango wake wa kuhakikisha kuwa kila Wilaya inakuwa na jengo la Mahakama. Aidha kwa sasa miradi inayoendelea ni ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya 18. Ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mkalama umepangwa kufanyika katika mwaka huu wa fedha 2022/2023. Kwa sasa taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi zinaendelea. Ahsante. (Makofi)
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatambua mipaka ya Halmashauri ya Mkalama na Iramba ili kuondoa migogoro katika Kata za Tumuli, Kinyangiri na Gumanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mgogoro kati ya Kijiji cha Mgungia, Kata ya Maluga, Tarafa ya Kinampanda, Wilaya ya Iramba na Kijiji cha Milade, Kata ya Tumuli, Tarafa ya Kinyangiri Wilaya ya Mkalama ulikuwa ukisababishwa na shughuli za kilimo, ufugaji, pamoja na wananchi kutokuwa na ufahamu wa mipaka yao ya vijiji. Wananchi wa pande zote mbili zenye mgogoro walikubaliana na mipaka iliooneshwa na ndiyo iliyotumika katika zoezi la maandalizi ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi.

Mheshimiwa Spika, mgogoro kati ya Kijiji cha Maluga, Kata ya Maluga, Tarafa ya Kinampanda na Vijiji vya Tumuli na Kitumbili, Kata ya Tumuli, Tarafa ya Kinyangiri ulikuwa ukisababishwa na uwepo wa makosa katika ramani za upimaji wa vijiji ya mwaka 2010. Wataalam wamekutana uwandani na kufanikiwa kuonesha mpaka wa kila kijiji kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 446 la mwaka 2013 la uanzishwaji wa Wilaya.

Mheshimiwa Spika, mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Iramba, Kijiji cha Kisana, Kata ya Kisiriri na Wilaya ya Mkalama Vijiji vya Kinamkamba na Mghimba, Kata ya Gumanga unasababishwa na wananchi wa pande zote mbili kutotambua mipaka yao. Wataalamu wa ardhi na viongozi kutoka Wilaya zote mbili walifika uwandani mnamo tarehe 19 Januari, 2018 na kufanya zoezi la kuhakiki mpaka pamoja na kutoa eimu kwa wananchi juu ya haki ya umiliki wa ardhi na kutii sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepusha migogoro, ahsante sana.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, Serikali inatumia vigezo gani katika mgawanyo wa Watumishi wapya kwenye Halmashauri hususani walimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiajiri watumishi hususani Walimu kulingana na bajeti iliyotengwa kwa mwaka husika. Baada ya kuajiri walimu hugawanywa kila Halmashauri kwa kuzingatia idadi ya mikondo, kila shule kuwa na Walimu wasiopungua Nane na Uwiano wa Mwanafunzi kwa Mwalimu (Pupil Teacher Ratio) kwa shule za Msingi.

Mheshimiwa Spika, kwa shule za sekondari vigezo vinavyotumika kugawa Walimu ni kubainisha idadi ya wanafunzi wanaosoma somo kwa kila kidato, kukokotoa idadi ya mikondo ya madarasa ya wanafunzi kwa kila kidato (mkondo mmoja kuwa na wanafunzi 40 kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne na wanafunzi 35 kwa Kidato cha Tano na Sita. Kubainisha idadi ya vipindi vinavyotakiwa kufundishwa kwa kila somo kwa kuzingatia maelekezo ya mtaala na ukomo wa vipindi anavyofundisha Mwalimu kwa kila somo. Kadirio la juu mwalimu anatakiwa kufundisha vipindi vya dakika 40, thelathini na kadirio la chini visipungue ishirini na nne.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga majengo ya kisasa katika Vituo vya Afya vya Kinyangira na Mkalama katika Halmashauri ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kujenga na kukarabati vituo vya afya kwenye Kata za kimkakati ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa fedha shilingi bilioni 117 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 234 kwenye Tarafa na Kata za kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vituo vya Afya vya Kinyangiri na Mkalama ni miongoni mwa vituo vinavyoendelea kutoa huduma katika ngazi ya Kituo cha Afya pamoja na changamoto ya upungufu wa miundombinu hususan ya upasuaji wa dharura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya nchini kote vikiwemo vituo vya afya Kinyangiri na Mkalama. Ahsante.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu ya Umwagiliaji ikiwemo kuchimba visima virefu katika Bonde la Dominiki, Kata ya Mwangeza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Bonde la Dominiki lipo katika Kata ya Mwangeza Halmashauri ya Mkalama. Bonde hili ni kati ya maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji yaliyobainishwa na kutambuliwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ndani ya Halmashauri ya Mkalama. Bonde la Dominiki lina takribani hekta 800 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo kwa sasa wakulima wa bonde hili hutegemea kilimo cha mvua. Hii ni kutokana na kutokuwa na uwekezaji wa aina yoyote ya miundo mbinu ya umwagiliaji na chanzo cha kudumu cha maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mpango na bajeti ya mwaka 2023/2024 imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kupata gharama halisi za kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji katika Bonde hilo.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA K.n.y. MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza kulipa fidia kwa baadhi ya wananchi waliopisha uanzishaji wa Kambi ya Gereza la Kilimo Singa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi Singa ilianzishwa mwaka 1983 katika Kijiji cha Singa chini ya Magereza ya Mkoa wa Singida ikiwa na eneo la ekari 500 kama ilivyoombwa kutoka Serikali ya Kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ardhi (Land Ordinance 03, Cap 113) ya mwaka 1923 iliyokoma mwaka 2003 haikuruhusu ulipwaji wa fidia kwa maeneo yanayotwaliwa na Serikali ambayo hayajaendelezwa. Kwa kuzingatia sheria hiyo, wananchi walio na maeneo yaliyoendelezwa (kwa kupanda mazao ya kudumu) katika eneo lililogawiwa kwa gereza walilipwa fidia zao shilingi 300,000 kwa eneo lenye ukubwa wa ekari 10 na malipo ya mwisho yalifanyika mwaka 1997. Taratibu za umilikishaji rasmi wa eneo hilo kwa Jeshi la Magereza zinakamilishwa na Mamlaka husika, nashukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi Nduguti kwa kuwa ujenzi wake umesimama kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Wilaya ya Mkalama ambacho kinajengwa eneo la Nduguti ni kituo cha Daraja B na ujenzi wake ulisimama ukiwa umefikia hatua ya lenta. Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 ilitenga kiasi cha fedha shilingi 500,000,000 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kituo hicho. Mwezi Februari, 2023 Serikali ilitoa shilingi 300,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mkalama ambacho ni gofu la ghorofa kwa muda mrefu sasa ilhali Wilaya haina kituo chenye hadhi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi kinachojengwa katika Wilaya ya Mkalama ni Kituo cha Daraja A na ni cha ghorofa moja. Ujenzi wake umeanza Juni, 2015 na unatarajia kutumia jumla ya shilingi 792,450,000.00 hadi kumalizika kwake. Hadi sasa fedha zilizotumika ni shilingi 100,000,000.00 na kazi iliyobaki ni kumwaga silabu, kupaua na kazi za kumalizia. Katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 zimetengwa fedha kiasi cha shilingi 692,450,000 kwa ajili ya kumalizia kazi ya ujenzi wa kituo hicho. Nashukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaboresha Vituo vya Afya vya Kinyangiri na Mkalama katika Halmashauri ya Mkalama kwa kujenga majengo ya upasuaji na wodi ili kuwa na hadhi ya Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Kinyangiri na Mkalama vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ni miongoni mwa vituo vya Afya 199 chakavu ambavyo Ofisi ya Rais TAMISEMI imeviainisha kwa ajili ya kuvitafutia fedha na kuvifanyia ukarabati na upanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati na kuongeza majengo kwenye vituo vya afya chakavu kote nchini vikiwemo vituo vya afya vya Kinyangiri na Mkalama. Vituo hivi vitapewa kipaumbele kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya upasuaji na wodi mara fedha zitakapopatikana, ahsante.