Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Francis Isack Mtinga (21 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na nianze kwa kukusahihisha naitwa Mtinga, sio Mtenga. Mtenga ni Wachaga, Mtinga ni Wanyiramba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni mara ya kwanza naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai na leo hii nipo kwenye Bunge hili lakini pia niwashukuru wananchi wa Iramba Mashariki kwa kuniweka hapa na Chama changu kukubali wananchi wa Iramba Mashariki wanilete. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ni dakika tano naomba niuelekeze mchango wangu kwenye kilimo. Sote tumesema hapa kwamba kilimo ndiyo ajira kuu kwa Watanzania, lakini kuna mambo mengi sana kwenye kilimo ila jambo ambalo limeonekana ni ufumbuzi na halijafanyika vizuri mpaka sasa, ni suala nzima la kilimo cha umwagiliaji. Mabonde tunayo mengi na mengi yameshawekewa miundombinu, lakini hata hayo yaliyowekewa miundombinu bado yanafanya kilimo kidogo sana na sehemu kubwa inabaki haitumiki na hayo mengine ambayo yanafaa pia bado hajawekewa miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri katika kilimo; rafiki yangu Mheshimiwa Bashe nimemwona mara nyingi sana anaongelea global family na nimpongeze amepita maeneo mengi na kuona jinsi ambavyo Serikali imeweka fedha na wananchi bado hawatumii vizuri; nchi yetu tuna hazina kubwa ya watu waliosoma mambo ya kilimo, lakini pia tuna hazina kubwa ya watu waliofanya kilimo pamoja na kuwa hawajasoma. Sasa ningeshauri kwamba katika maeneo haya ya umwagiliaji, Serikali iwekeze kila kitu kwenye maeneo hayo, kuanzia miundombinu, lakini vile vile na kuweka na viwanda vidogo kwa maana ya kuya-add value yale mazao katika maeneo yale. Baada ya kukamilisha, wawakopeshe vijana kuanzia wale wasomi wa chuo kikuu mpaka vijana wa mtaani wa darasa la saba kwa kuwakabidhi maeneo yale na kuwasimamia, walime warejeshe ule mkopo na baada ya hapo maeneo hale yabaki kuwa ya kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna maeneo mengi na kama Serikali itasimamia kwa kuwekeza namna hii, nina hakika tutazalisha na wale vijana watakuwa wamepata ajira. Hii itatuletea kipato, itatuletea uhakika wa chakula, uhakika wa mazao ya biashara kwa ajili ya viwanda, lakini vile vile itatibu suala nzima la ajira. Kwa hiyo nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Bashe hiyo kazi aliyoianza aifanye vizuri zaidi aiendeleze na ahakikishe kwamba maeneo yale ambayo yamewekezwa yanafanya kazi iwezekanavyo na haya mapya fanyeni utaratibu wa kuwakopesha vijana wa nchi hii, wasomi wapo na wasiosoma wapo na wanahitaji wakabidhiwe vitu hivi kama mkopo, wakimaliza wanaendeleza na maeneo mengine yanaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka niende kwenye eneo lingine la ukuaji wa miji. Ni kweli Serikali yetu inawekeza kwenye miundombinu, leo hii ukipita Dar es Salaam unaona barabara za juu, unaona hizo interchange, lakini cha kusikitisha miji yetu haikui, miji mpaka sasa ina vibanda mjini, nyumba za ajabu ajabu, sasa mji haupendezi, mji una barabara za juu, lakini nyumba ni vimakuti vimejaa mjini na vibati vya ovyo ovyo, wakati huo huo watu wanaendelea kuwekeza nyumba za maana mbali na watu hawaendi kuishi huko. Kwa mfano, Kigamboni, nyumba za NSSF hazina watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri kwamba wizara inayohusika katika miji yetu iwatambue wale watu wenye maeneo yale ya zile nyumba ndogo ndogo na vibanda. Ikishawatambua ifanye utaratibu wa kubomoa na kujenga upya mji, maghorofa ya kutosha, baada ya hapo wale watu wapate unit title. Kwa hiyo tutakuwa tumejenga mji na wale ambao maeneo yao walivunja watapata unit title kwenye yale maghorofa na watu wengine sasa watapata miji na hapo Serikali kwanza itapata kodi lakini mji utapendeza na miji yetu itaendana na miundombinu inayojengwa kwa sasa. Tukiendelea kuacha vibanda mijini tunakwenda kujenga mbali, matokeo yake tuna barabara nzuri lakini mtu akiangalia anaona vibanda viko mjini na miji yetu haiendelei kupendeza na tunazidi kukosa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwenye miundombinu, nchi hii sasa inaunganishwa na tunawaza kuunganisha barabara za wilaya na wilaya. Hata hivyo, katika Mkoa wangu wa Singida na hasa katika jimbo langu barabara inayounganisha Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Singida ambao unapita kwenye Jimbo langu la Mkalama ni muhimu sana ikaangaliwa. Tumejenga daraja kubwa la Mto Sibiti zaidi bilioni 28, sasa tulitumie daraja lile kwa kuweka barabara ya lami ili kuunganisha mikoa hii. Pamba yote sasa inayotoka kule inasafirishwa kupitia njia hii ya vumbi, naamini barabara hii ikijengwa kwa haraka na ipo kwenye Ilani, itasaidia sana kukuza uchumi na kuunganisha mikoa yetu na kuendeleza Mkoa wangu wa Singida na hasa Jimbo langu la Mkalama ambapo barabara hii inapita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kengele imelia, dakika tano ni chache, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kupata nafasi hii muhimu sana ya kuchangia Wizara ambayo inabeba uchumi wa nchi hii. Kwa sababu miundombinu ndiyo inayobeba kila kitu; mazao, products za viwanda na kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwanza kwenye jimbo langu. Jimbo langu kwa barabara za TANROADS ina mtandao wa kilometa zipatazo 234.5, lakini katika mtandao huu neno lami kwetu sisi ni msamiati kwa sababu kuna kilometa 2.5 tu tena tumezibahatisha tu kwai le barabara inayokwenda Mwanza kwa kuibia kidogo pale Igugulu, kilometa mbili katika mtandao mzima wa barabara za TANROADS, kilometa 234. Sisi watu wa Mkalama lami kwetu ni msamiati.

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika barabara za TARURA, takribani kilometa 647 mtandao, hatuna hata robo kilometa ya lami. Sasa tunapofika kwenye suala hili la bajeti kama mwenzangu alivyotaka kuruka sarakasi hapa kwa kweli haka kamgawanyo ka bajeti katika nchi hii inabidi sasa kawe kanaangaliwa kwa vipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wakati wenzetu wanaomba bajeti za kuziba viraka vya lami ambazo wameshazitumia mpaka zimechakaa sasa wanataka wazibe, sisi hatuna hata kipande cha lami. Kwa hiyo, inapofika wakati huu kwa kweli sisi tunaporudi kwa wananchi wetu wanatuuliza hivi ninyi Bungeni kule mna nchi yenu tofauti, mbona wenzenu wana lami za kutosha, sisi tutatembea kwa vumbi mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unapofika wakati huu wa kugawa hizi bajeti lazima tuangalie vipaumbele. Hii habari ya kusema fedha zikipatikana zitajengwa, fedha zikipatikana, sisi mnatupa wakati mgumu, na sisi tuna wananchi ambao wanataka kula matunda ya nchi yao nzuri inayoongozwa na mama yetu Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ipo barabara ambayo ipo kwenye Ilani, inayoanzia pale Iguguno inapita kwenye Makao Makuu ya Wilaya Nduguti inakwenda mpaka Simiyu kupitia daraja la Sibiti ambalo limejengwa kwa fedha nyingi za nchi hii. Barabara hii ukiacha tu kwamba inaunganisha mikoa miwili; Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Singida na wote tunatambua kwamba Mkoa wa Singida ndiyo Mkoa ambao unalima Alizeti kwa wingi na ninyi mnafahamu tatizo kubwa la mafuta katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wote mnafahamu kwamba Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa mikubwa inayolima Pamba katika nchi hii. Kwa hiyo, tunapoongelea barabara hii ya Simiyu – Singida kuunganishwa kwa lami, tunaongelea uchumi wa nchi hii. Tunaongelea kuondoa changamoto za nchi hii. Kwa hiyo, naomba katika vipaumbele vya Wizara barabara hii ambayo ipo kwenye Ilani inayounganisha mikoa; hii sera ya kuunganisha mikoa ilianza tangu Awamu ya Nne, sisi bado hatujaunganishwa kati ya Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba barabara hii iwekwe kwenye umuhimu wa kipaumbele, hii habari ya kusubiri, najua Mheshimiwa Waziri anaweza akaja na majibu mepesi tu, kwamba fedha ikipatikana; naomba aje na majibu yanayoeleweka katika barabara hii ili nasi tuondoke kwenye unyonge wa kutokuwa na lami. Kwa kuanzia basi, angalau kwa kipaumbele, hata zile kilometa 42 tu za kutoka Iguguno mpaka Makao Makuu ya Wilaya zipate lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Singida Wilaya pekee ya Mkalama ndiyo inayounganishwa na vumbi na Makao Makuu ya Mkoa. Hata kwenye Kamati pale nimesikia wanasema vipaumbele, Makao Makuu ya Wilaya, kuunganishwa na Mkoa kwa lami. Kwa hiyo, angalau hizi 42 basi zije kwa bajeti ya dharura angalau tupate kilometa 42 za lami kutoka Makao Makuu ya Wilaya mpaka Makao Makuu ya Mkoa, kwa kuanzia katika barabara hii ambayo ipo kwenye Ilani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami sitaruka sarakasi, lakini kwenye kushika shilingi nikipata nafasi kama hamjaja na maneno mazuri kuhusu barabara hii kwa kweli tutaungana na Mheshimiwa Flatei, yeye akiruka sarakasi mimi nagaragara chini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena nirudi kwenye Jimbo langu. Lipo daraja linajengwa katika Mto Ndurumo, daraja la msingi; daraja lile linasuasua sana. Waziri sijui kama litaisha na ni muhimu sana, lakini kwa sababu daraja lile linaendelea, pale kuna daraja la dharura la jeshi ambalo linatumika. Namwomba Mheshimiwa Waziri na Walinzi wa Ulinzi pia, daraja lile la jeshi ambalo lipo pale, baada ya daraja kubwa kukamilika, daraja lile liendelee kuhifadhiwa kwa udharura wake ndani ya Mkalama, lisiondoke kwa sababu lipo bonde kubwa la mto ambalo linatenganisha vijiji karibu vitatu; vya Yulansoni, Lelembwe na Mulumba ambapo wanakuwa kisiwani wakati wa masika na watoto wanakufa wakati wa kwenda shuleni kule Katani ambapo Kata ipo Kinyangire na bonde lile linatenganisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba daraja lile la jeshi liendelee kuhifadhiwa kwa udharura wake, lakini ndani ya Mkalama lipelekwe katika bonde hili la Yulansoni. Wananchi wa eneo lile wana uchumi mkubwa lakini barabara imekuwa ni shida na hatuna kivuko. Kwa hiyo, daraja lile la jeshi litakapokamilika daraja hili kubwa, libaki pale Mkalama katika eneo la Yulansoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye eneo pia la TANROAD. Najiuliza sana, TANROAD kila mkoa wapo na wanapata bajeti, lakini pale kwangu Mheshimiwa Flatei alikuwa analalamika kwamba barabara zake ni za vumbi, lakini mimi ninapotoka Mkalama naenda kwa jirani yangu Manyara, kwa Mheshimiwa Flatei; ninapotembea na barabara za vumbi za Mkoa wa Singida, unapofika tu, “Sasa unaingia Manyara,” nakutana na utofauti kabisa wa barabara; za kwangu za TANROAD Singida zina mashimo, lakini ukiingia TANROAD Manyara unakuta nzuri. Kwa hiyo, nikaona hapa kuna uzembe katika suala la kusimamia Wakandarasi wanaokarabati hizi barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri mwangalie vizuri Meneja wa TANROAD Singida, ukarabati wa barabara za TANROAD mkoa wangu wa Singida zifanyike vizuri kwa fedha ndogo inayopatikana. Hata timing ya kutengeneza hizi barabara; unakuta barabara inatengenezwa wakati wa mvua. Bado hata Mkandarasi hajaondoka, ile iliyotengenezwa imeshabebwa na maji. Sasa sijui hizi program zao za utengenezaji zimekaaje! Naomba ziangaliwe vizuri; na kile kidogo cha ukarabati kinachofanyika kiweze kudumu na wananchi wafurahie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile imetengenezwa juzi tu pale, sasa hivi ni mashimo, lakini ukiingia Manyara unakuta barabara safi. Hii inaonyesha kabisa kuna uzembe katika suala la utendaji. Wengine wanafanya vizuri, fedha ni hiyo hiyo, usimamizi unakuwa mbovu. Naomba hili lifike na walisikie, najua watakuwa wameshalisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuongelea jimbo sasa niuongelee mkoa wangu. Singida tuna uwanja wa ndege na kwa bahati nzuri katika hotuba ya Rais iliyopita uliongelewa ni katika viwanja 11 vitakavyojengwa. Nataka niombe, katika vile viwanja 11, Uwanja wa Mkoa wa Singida unatakiwa upewe kipaumbele cha pekee, kwa sababu ni uwanja ulio jirani na Makao Makuu ya Nchi. Uchukuliwe kama uwanja wa dharura, pale inapotokea tatizo katika Uwanja wa Makao Makuu ya Nchi, uwanja wa dharura ulio karibu unapaswa kuwa uwanja wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ikitokea tatizo, ndege inabidi irudi Dar es Salaam kilometa zaidi ya 500, wakati hapa Singida ni kilometa 240. Kwa hiyo, naomba Wizara iangalie uwanja wa Mkoa wa Singida kama uwanja wa dharura. Hii ni Makao Makuu ya Nchi, wanatua Mabalozi hapa, wanatua Marais wa nchi mbalimbali hapa; litakapotokea tatizo lolote la kianga, uwanja pekee wa dharura ni uwanja wa Singida.

Kwa hiyo, naomba uwanja huu katika vile viwanja 11 wenyewe utazamwe kwa jicho la tofauti kama uwanja wa emergence pale linapotokea tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nisisitize hilo katika suala la Mkoa wangu wa Singida. Nawashukuru sana, najua ujumbe umefika. Kama ambavyo nimesema, Mheshimiwa Flatei akiruka, mimi nitagaragara, namwomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu ya kutosha katika maeneo haya ya Mkoa wangu wa Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii, ambayo ni nzuri na inatia moyo sana Watanzania. Nichukue nafasi hii kumupongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, kwa kuchukua mawazo ya Wabunge kwa kiasi kikubwa sana na kuyaweka kwenye bajeti hii. Hili linafanya hata sisi tunapochangia, tunakuwa na moyo kwa kuamini kwamba Serikali inatusikia. Kwa hiyo, nimshukuru sana kaka yangu Mwigulu na ukizingatia ni Jirani yangu pale Jimboni, basi najisikia furaha sana kwa jinsi kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa, tunarudia kukazia pale ambapo tunaona ni muhimu zaidi pia na kwa sababu jambo likisemwa na wengi linakuwa pia ni sauti ya Mungu, naomba tu nijikite kwenye suala la elimu haswa ya Sekondari. Nishukuru kwamba Serikali sasa inaenda kutujengea shule moja kwenye kila Kata, shule kamili hasa katika kata mpya na zile kata kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana kuikumbusha Serikali kuziimarisha shule zetu za Kata ambazo tumezijenga pamoja na wananchi nchi nzima. Shule hizi zilianza kwenye wakati mgumu, lakini zimeendelea kuimarika mpaka zimetoa wataalam wakubwa katika nchi hii. Hata hivyo, bado shule hizi zina changamoto kubwa. Kama tunavyofahamu kata zetu hazina tofauti na baadhi ya wilaya, kata zetu ni kubwa sana na shule hizi zimejengwa katika maeneo ambayo iweze kuhudumia angalau vijiji vya kwenye kata hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nchi yetu hii kijiji hadi kijiji kuanzia kilometa 10, 15 mpaka 20 ni jambo la kawaida kabisa. Kwa hivyo, watoto wetu wa kike na wa kiume wanatembea mwendo mrefu sana mpaka kufika shuleni. Huko wanakutana na majanga mbalimbali, watoto wa kike wanabakwa, watoto wa kiume wanajiingiza kwenye vitendo viovu mpaka kuvuta bangi. Hii inapelekea mpaka wazazi wanaamua sasa kuwapangishia vyumba watoto wao, karibu na maeneo ya shule katika mazingira magumu sana, vyumba vinaitwa mageto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Chemba, nimefika nakutana na watoto wanakaa geto. Sasa mtoto wa Form One, anaenda kusoma anakaa geto, ajitegemee, mazingira magumu, hakuna umeme, halafu tunategemea kwamba mtoto huyu apate elimu bora, ni jambo gumu sana. Hata Walimu wenyewe, inabidi wakatafute mahali pa kuishi mbali sana na shule. Wanatumia usafiri, wengine wanatembea kwa miguu, wengine wana pikipiki, anafika shuleni amechoka, atoe elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba nitoe ushauri kwamba, pamoja na hii nia nzuri ya kuanza kujenga shule mpya. Niombe Serikali iangalie jinsi ya kuimarisha hizi shule zetu, sasa tuzijengee mabweni ya wasichana na wavulana ili watoto wetu wakae shuleni. Kwa sababu, Serikali inalipa ada, mzazi tukimwambia alipie chakula kwenye hosteli atalipa. Atampa mtoto wake chakula kile ambacho angekula nyumbani, sasa atakipeleka hosteli ili mtoto akae shuleni aweze kula chakula kile kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali ijenge nyumba za Walimu ili Walimu wakae shuleni. Ni kweli tunalalamika kwamba, elimu yetu ina tatizo, watoto wetu wana akili sana, lakini mazingira tuliyowapa ni magumu. Shule hizi tulizianzisha, zimetusaidia, lakini tuendelee kuziimarisha. Naamini kabisa fedha ambayo inayotumika kujenga shule kila kata, ingetumika kuimarisha hizi shule kwa kujenga hosteli na mabweni, impact yake ingekuwa kubwa zaidi pengine kuliko hata hii shule moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikatai shule ni kitu kizuri, lakini kama ningeambiwa kipaumbele, ningeona ni bora tujenge hosteli kwanza kwenye hizi shule za wasichana na wavulana, ili shule hizi za kata zilizopo ziimarike. Kwa sababu, hata aliyepo mbali, hata aliyopo kwenye kata mpya kama shuleni kuna hosteli atakwenda kukaa kule na atapata elimu bora. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu hizi shule tusizisahau, tukaanza kujenga shule mpya kubwa kubwa, wakati kuna shule ambazo tukiziimarisha tutakuwa na impact kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihame niende kwenye suala la mikopo ya hawa vijana. Kwa kweli, Serikali yetu ina nia njema, imetenga fedha kwa ajili ya vijana, halmashauri hata kwenye Wizara, imetenga fedha kwa ajili ya akinamama, lakini, urejeshaji wa hii mikopo umekuwa mgumu sana. Vijana wamechukua fedha, miradi imekufa, halmashauri inashindwa kuwapeleka mahakamani na hata ukiwapeleka dhamana zenyewe hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ile fedha inapotea na vijana wengine ambao hawakupata mkopo wanakosa. Kwa hiyo, ningeshauri, tufike mahali tubadilishe mbinu ya jinsi ya kutoa hii mikopo. Serikali itengeneze mradi, mradi ukamilike. Kama ni mradi wa nyuki inunue mizinga, itundike, ikusanye vijana, iwape elimu jinsi ya kufuga nyuki, inawakabidhi, ni rahisi kuwa-monitor ili waweze kurudisha ile fedha. Kama ni ufugaji wa kuku inunue incubator, ijenge mabanda, itoe elimu kwa vijana, wanakabidhiwa pale, ni rahisi kuwa-monitor na kurudisha ile fedha na wengine wapate. Hii kuendelea kutoa cash tunapoteza fedha na hakuna impact tunayoiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba, tubadilishe huu mtindo, kuliko hii fedha ziendelee kupotea, tutengeneze miradi. Kwanza hii njia italeta ajira ya uhakika, kwa sababu ukitengeneza mradi unachukua vijana wote kuanzia wa darasa la saba mpaka wa chuo kikuu. Mle kutakuwa kuna watenda kazi, kuna mameneja, kuna kila kitu kwa sababu ule mchanganyiko unakuwa ni wa kutosha. Kwa hiyo niombe, Serikali ibadilishe mtindo, ili tupate impact ya hizi fedha za kukopesha vijana wetu. La sivyo, tutakuwa tunapoteza ajira bado hakuna na fedha zinaendelea kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia niende nikawasemee Madiwani. Kwanza niishukuru Serikali kwa kuwahamisha tu mahali pa kulipiwa fedha, kutoka kwenye halmashauri kwenda kwenye Mfuko Mkuu. Kilichopatikana hapo ni uhakika na kutokucheleweshwa na heshima, lakini kiukweli tatizo hasa kubwa bado, hawa Madiwani wanafanya kazi kubwa sana. Ule usumbufu wa matatizo ya wananchi tunaoupata sisi Wabunge kwenye Jimbo zima wao wanaupata pia, kwenye kata zao. Kwa hivyo, ni watu ambao wanahitaji wawe na angalau na peace of mind, hii posho ya Sh.300,000 ni ndogo mno. Ningeomba kwa sababu, Serikali Kuu imebeba mzigo wa hii shilingi 300,000, tuwaagize halmashauri, sasa Wakurugenzi wawaongeze hata shilingi 100,000 kama posho ya madaraka ili ukichanganya angalau ziwe shilingi 400,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walikuwa wanaweza kuwalipa shilingi 300,000, sasa kama Serikali kuu imechukua, tukisema wawaongezee hata shilingi 100,000 utakuwa ni mzigo mwepesi. Angalau bado hazitoshi, lakini angalau itapunguza hata kidogo. Kwa hiyo, tutakuwa tumewapa heshima ya kuwalipa kwenye Mfuko Mkuu lakini pia, tuwaongezee chochote, kiweze kupatikana. Hawa ni wenzetu na wana-deal na wananchi na wote tunaelewa, jinsi wananchi wanavyotegemea Wabunge, wanavyotegemea Madiwani na sisi ndio watu wa kutatua shida zao. Wenzetu hawa na wenyewe wakiwa katika hali nzuri na hata huko majimboni patatulia. Tukiwa huku na sisi tunapumua. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla naomba hili liangaliwe, ni jambo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwa Madiwani sasa hivi, hii posho ya vikao, vikao vyenyewe vya Baraza la Madiwani ni kama vinne tu kwa mwaka, lakini sasa kuna hii posho hii ya kikao inaitwa nyingine sijui ya kujikimu, Diwani inabidi akae kwenye kikao sijui mpaka kwenye saa 9.00 au saa 10.00 ndio alipwe ile fedha. La sivyo, siku nyingine anaambiwa wewe wa karibu, itabidi ulipwe nusu usipate night. Fedha yenyewe ndogo, bado ametoka huko Mheshimiwa Diwani amesafiri mwingine na pikipiki, anafika inabidi akae kwenye kikao walazimishe mpaka ifike saa 9.00 ndio ile fedha iingie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, hii shilingi 100,000 ukiachana na ile Sh.40,000/= ya sitting, hii shilingi 100,000 iitwe tu fedha ya kikao, ili hawa walipaji waweze kulipa hii fedha bila matatizo, lakini unapoita night sijui mpaka ifike saa 9.00, sijui mpaka saa ngapi kunakuwa kuna double standard, kuna vurugu kila wakati. Madiwani wangu wa Mkalama juzi wamekaa hapa wengine wamelipwa night, wengine hawajalipwa, mchanganyiko na naamini hii iko katika maeneo yote ya Wabunge wote. Hebu tuiite tu shilingi 100,000 ya kikao, shilingi 40,000 sitting, vikao vyenyewe mara nne kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na dada yetu Waziri wa TAMISEMI, wapeleke waraka. Waraka wamepeleka ule, wenzangu wa TAKUKURU kwa sababu, wenyewe wanafanya kazi yao, wakaingia nao pale kama hamjafika saa 9.00, fedha haitoki. Sasa inasababisha hata mambo mengine hayapiti, wanakwamisha tu Madiwani ili angalau ifike saa 9.00. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu niombe hii fedha ya shilingi 100,000 na shilingi 40,000 ya sitting utoke waraka, ni fedha ya kikao, ieleweke katika maeneo yote…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia itifaki hii ya huduma za kibiashara ya nchi za SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuwapongeza sana Wabunge wenzetu ambao wameendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais ya kuwapa kazi ya kumsaidia katika kuiongoza na kuiendesha nchi yake lakini pia niwape pongezi wale ambao wanaingia kwa mara ya kwanza na hususani Mwenyekiti wetu wa Kamati yetu Mheshimiwa Kihenzile Mwenyekiti wetu hodari sana kwakupata nafasi naamini yale ambayo alikuwa anayafanya mazuri sana kwenye Kamati yetu sasa anaenda kuyaonyesha kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kumpongeza sana Rais wangu kwa jinsi ambavyo anaendelea kuupiga mwingi na nchi yetu inaendelea kunufaika sana na mambo mengi ambayo Rais wetu anayafuatilia. Jimbo langu leo linaogelea mambo mengi sana ya kimaendeleo kwa sababu ya kazi nzuri anayoipiga Rais wetu. Naamini hata hao wachache ambao wamehamishwa hamishwa wataendelea kuyafanya hayo mambo ya kumsaidia Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono kwamba itifaki hii niombe Bunge liipitishe pamoja na kuchelewa kwa muda mrefu sana. Ni kweli miaka mingi imepita takribani kumi na moja tangu isainiwe mtu yeyote anaweza akawa na hofu kidogo kwanini imechelewa? lakini waswahili wanasema chelewa ufike. Tumechelewa lakini sasa tunafika ni jambo la msingi sana kulifanya kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niiombe Serikali sisi kama Bunge tunaridhia sasa lakini wao ndiyo watekelezaji wa hizi itifaki ambazo tunaridhia kwa maana ya kwamba wanakwenda sasa kufanya mikataba mbali mbali bilateral kati ya sekta zinazohusika katika utendendaji wa hizi itifakia ambazo tunazipitisha. Kwa hivyo ningewaomba sana Serikali washirikishe sana sekta binafsi kwa karibu sana katika utekelezaji wa hizi itifaki kwasababu wao ndiyo walaji wakubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tukichukulia tu suala la mabenki wafanyabiashara wetu wamekuwa na tabu sana wanapofanyabiashara katika nchi hizi na hasa ukizingia hata sasa kwa mfano tatizo la dola naamini kama nchi hizi zote za SADC mabenki yetu yatakua katika nchi hizo, ufanyaji wa biashara utakuwa mwepesi sana. Mtu anaweza akaenda hata nchi nyingine akatumia local currency yetu kwa kujua benki yetu iko kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Serikali iziwezeshe benki zetu lakini pia izishirikishe na kuzishauri na kua karibu nao katika kuwahamasisha kuanzisha mabenki katika nchi takribani zote tu za itifaki hii nchi za SADC ili hili suala la biashara liwe jepesi sana. Mfanyabiashara akienda nchi ya SADC yeyote akaikuta benki yake ya NMB au CRDB iko kule hata ile imani tu ya ufanyaji wa biashara anakuwanayo lakini pia usaidizi wa karibu wakupata hata anapopata tatizo lolote la kifedha au la kibiashara inakuwa rahisi sana. Kwasababu unahisi kama benki yako ndiyo kama uko kwenye nchi yako tu kwa sababu benki yako unayoijua na unayoiamini iko kule. Lakini vilevile benki yetu itaendelea kufanya biashara katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba sana Serikali iangalie kwa karibu sana jambo hili la kushirikisha mabenki kuhakikisha na kuyawezesha na kuyashauri kwa vyovyote inavyowezena ili kuweza kufungua katika hizi nchi za SADC na tuweze kulifaidi vizuri soko hili. Kwa sababu biashara ni fedha, usipokuwa na fedha hamna biashara ambayo utaweza kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuishauri Serikali katika suala la huduma ya afya niwaombe Serikali itimize ndoto ya Rais Jakaya Kikwete ya kuifanya Hospitali ya Benjamini Mkapa kuwa kituo cha kimataifa cha afya pamoja na utafiti. Nahakika kabisa kama tutafanya mambo ambayo yalikusudiwa pale huduma, vifaa na madaktari tunao wengi, madaktari wetu mabingwa wako katika nchi za watu wanatibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninahakika kama tukiwezesha hospitali hii kuwa kituo cha utafiti kikubwa na tiba basi Tanzania ndiyo itakuwa India ya hizi nchi zote za SADC na hivyo tutakuwa sasa tunatengeneza utalii, utalii wa kihuduma, utalii wa kimatibabu na hivyo kufanya nchi yetu kupata fedha nyingi za kigeni lakini vilevile kuwa tumeitendea haki itifaki hii katika sekta hii ya huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali hebu hili iliangalie kwa makini tayari kuna kitu kikubwa pale kimeanza ni kiasi cha kuongeza nguvu tu na tutasababisha nchi zote hizi zikaitegemea nchi yetu. Tiba ni vifaa na madaktari na naamini nchi yetu tuna uwezo mkubwa sana kama tumeweza kujenga mabwawa ya matrilioni, tumeweza kuweka hizi standard gauge za matrilioni hatuwezi kushindwa ku-invest kwenye afya hapa Benjamini Mkapa na hizi nchi zote zikatutegemea wakaachana na habari ya kwenda India, India yao ikawa hapa Dodoma hapa Tanzania na hivyo kuweza kufanya hii huduma tukatumia vizuri hili soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuangalia Serikali iwezeshe hizi biashara zetu ndogo ndogo kufanyika kwa urahisi Wafanyabiashara wetu wamekuwa wakiteseka sana. Unakuta mtu anaenda kwenye mpaka anabidhaa anaambiwa hii bidhaa hairuhusiwi kuingia huku, kwa mfano kuna nchi zinakataa nyama yetu wakati zipo nchi za jirani zinanua mifugo yetu, zinakwenda zinachinja huko zinapata nyama zinapeleka kwenye hizo nchi ambazo zinakataa, zinasingizia kwamba sisi hatuchanji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, unaona kuna vihujuma vidogo vidogo ambavyo vinafanyika. Sasa itifaki kama hizi ebu ziwe mwarubaini sasa wa kutibu hizi hujuma ndogo ndogo na Serikali iangalie kabisa kama tuna mahusiano ya kupeana huduma, huduma ziko za aina nyingi sasa huduma siyo tuhujumiane pia. Kwa hiyo, ningependa Serikali iwe makini sana kuhakikisha wafanyabiashara wetu hawateseki na wanafaidi hili soko kubwa kwa kuepukana na hizi hujuma ndogo ndogo ambazo zinafanyika katika biashara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuangalie sheria zetu, sheria zetu zingine zinatushika miguu sisi wenyewe, ningeomba Serikali ebu iangalie kwa makini sheria ambazo zimepitwa na wakati kuna mambo mengine tunajishika miguu wenyewe. Unakuta mtu anataka kupeleka nyama mahala anafika boarder au anafika bandarini anambiwa hebu lete cheti cha mionzi, wakati hata hiyo nchi inayopelekewa hizo nyama hata habari ya mionzi hawana, hawajui chochote kuhusu mionzi tunashikana miguu wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hebu tuangalie na vitu ambavyo sisi wenyewe vinafanya wafanyabiashara wetu wanashindwa kufanya biashara na hizi nchi na hivyo kufaidi hili soko kwa kuangalia zile sheria zilizopitwa na wakati turekebishe tufanye mambo ya biashara yawe rahisi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine amelisema mama wa afya ya akili hapa Mheshimiwa Jesca suala la watu kufahamu kupata elimu juu ya hizi itifaki. Niiombe Serikali ni kweli inapoleta suala la itifaki Bungeni ni suala la Kibunge lakini niiombe Serikali iwe na mtindo wa kuwaanda wananchi kwamba sasa tunapeleka itifaki fulani Bungeni, itafaki inayowahusu ninyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bungeni ndiyo mahali pekee ambako tunaweza kumuita mwananchi, tunaweza kumwita mdau tukaja tukamsikiliza anasema nini kuhusu itifaki tunayotaka kuipitisha. Kwa hiyo, niiombe Serikali ijenge tabia ya kuwahabarisha wananchi, kuwahabarisha wadau kwamba tunapeleka itifaki fulani Bunge inayohusu jambo fulani kule ndiyo mahala ambako mnaweza kwenda kusema. Kwa hiyo, jamii na wadau wanakuwa na habari kwamba kuna itifaki inakwenda bungeni inakwenda kujadiliwa inayotuhusu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Bunge tunapowaita sasa wadau njooni mseme kuhusu itifaki wanakuwa wanauelewa. Kwa hiyo, tunapata input za watumiaji wa hiyo itifaki kwa hiyo, linakuwa ni jambo letu wote tunapolipitisha sasa tunapokuwa hawana habari halafu tunapitisha jambo Bunge tukitangaza sisi Bunge tuna taratibu zetu za kutangaza watu waje. Kwamba njooni msikilize lakini jinsi watanzania wetu tulivyo watu wengine magazeti hawasomi, mitandao hawapitii. Sasa kama Serikali haijawahabarisha vizuri tunapotangaza wadau waje hawawezi kuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano sisi kwenye kamati yetu kuhusu jambo hili tumeaihirisha mara mbili tunataka wadau waje tuwasikilize kwa sababu tu watu wengine hawana information. Kwa hiyo, niiombe Serikali katika itifaki mbalimbali mnapotaka kuzileta Bungeni jengeni tabia ya kuwahabarisha wadau, habarisha wananchi kwamba tunapeleka itifaki Bungeni kule ndiyo mahala mnaweza kwenda kutoa input zetu ili tukipitisha linakuwa ni jambo letu na siyo la kutukana Bunge la kulaani Bunge kwa jambo ambalo sisi tumepitisha kwa nia njema, kwa nia ya kuwasaidia wao lakini kwa sababu hawakuwa na habari wanaona kama vile wamesalitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali ijenge hii tabia ili twende kwa pamoja na wadau wawe wanafaidi hizi itifaki kwa sababu wanakuwa wanazielewa zimepita kwa nini na kwa manufaa gani na hivyo kuzitumia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nihitimishe tu kwakusema niliombe Bunge lipitishe hii itifaki kwa sababu ina nia njema lakini twende kwa pamoja na sisi Wabunge katika maeneo yetu tuendelee kuwahabarisha wafanyabiashara na watu wengine wafaidi hizi itifaki ambazo tunazitumia. Kwa sababu nchi yetu ni nchi kubwa yenye kila namna yenye neema na tukiyatumia vizuri itifaki hizi tutaendeleza maisha ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja, ahsante sana.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi nami kuweza kuchangia Mpango huu wa Tatu. Kwa sababu nafasi yenyewe ni ya dakika tano, niende moja kwa moja kwenye mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu unajielekeza katika kutafuta fedha ambazo zitatusaidia kwenda kwenye TARURA ili Jimbo langu la Mkalama, Iramba Mashariki liweze kupata fedha za kutengeneza barabara. Yako mambo ambayo mara nyingi Serikali imekuwa ikiyatumia kupata fedha na mara nyingi sana wamekuwa wakienda kwenye vinywaji, lakini safari hii fedha ya uhakika ipo kwenye mafuta.

Mheshimiwa Spika, viko vifungu vingi sana ambavyo kwa ujumla wake vinatengeneza bei ya mafuta ya lita ambayo tunanunua kwa sasa. Katika vifungu hivyo, kimojawapo ni kifungu ambacho kinahusu marking, yaani kuweka alama ya mafuta ambayo yako on transit na yale ambayo yanatumika ndani ili kuepuka wanaokwepa kodi na kuepuka uchakachuaji.

Mheshimiwa Spika, kifungu hiki, kinafanywa na Kampuni ambayo imepata tender na gharama yake inayolipwa, ni shilingi 14 na senti 22 kwa lita moja. TBS pia wanapata pesa kutoka kwenye hivi vifungu vya mafuta, wenyewe wanapata kama shilingi moja na senti kadhaa hivi.

Mheshimiwa Spika, naona kazi hii ya kuweka marking, TBS wanaweza kuifanya kwa uhakika tu, kwa sababu ndiyo Shirika letu la Viwango. Kazi hii ikifanywa na TBS hata kama wataongezewa fedha kidogo kutoka kila shilingi moja tutaokoa fedha nyingi sana ambazo zinafanywa na kampuni; na kwa bahati nzuri kampuni hii muda wake umeisha lakini wamekuwa wakiongezewa ongezewa muda tu kwa miezi mitatu mitatu na EWURA sijui kwa utaratibu gani? Kama kazi hii itafanywa na TBS, hii shilingi 14 tukaamua kui-save, tutaipeleka TARURA.

Mheshimiwa Spika, naomba tu niseme jinsi fedha hii itakavyopatikana. Takribani kwa mwezi mmoja, mafuta yanayoingia nchini ni kati ya lita 390,000 mpaka 400,000 metric ton ambapo Metric ton moja ni sawa na lita 1,000. Kwa hiyo, ukibadili hizi metric ton 390,000 kuwa lita ni kama lita 390,000,000 kwa mwezi. Uki-compute hizi shilingi 14 kwa kila lita kwa mwezi mmoja, unapata takribani shilingi 5,545,800,000/=. Ukifanya mara 12 kwa mwaka unapata shilingi 66,549,000,000/=. Fedha hii ikienda TARURA, Majimbo yetu yatakuwa yamepoma na bado kazi ya marking inaweza ikafanywa na TBS.

Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri wa Fedha, hii ni shilingi bilioni tano kwa mwezi, ni hela ambayo anaweza kuipata mwezi ujao tu akiamua, kwa sababu hata hiyo Kampuni inayofanya kazi hiyo, muda wake umeisha. Kwa hiyo, ni kauli tu na maamuzi kwamba kazi hii sasa ifanywe na TBS na ile shilingi 14 kwa lita ambayo ilikuwa inachukuliwa na hii Kampuni ziende kwa ajili ya TARURA. Kila mwezi tuna uhakika wa kutengeneza shilingi bilioni tano ambapo wananchi wetu na barabara zetu zitapata fedha ya uhakika kiasi cha shilingi bilioni 66,549,000,000 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba hebu Waziri afanye maamuzi haya, kwa sababu ni maamuzi ambayo yana maslahi ya Watanzania hata Mungu ataona. Baada ya kutafuta pesa, naomba tu niseme, huu ni Mpango wa Tatu kuchangia, kuusikiliza tangu niingie Bunge hili kwa sisi ambao tunaitwa Form One. Mchango wa kwanza kwa Wabunge, ulikuwa unahusu Hotuba ya Rais; mchango wa pili, ulikuwa unahusu Rasimu ya Mpango huu; na sasa Mpango huu.

Mheshimiwa Spika, ambacho nakiona, Waheshimiwa Wabunge wanatoa michango mizuri sana yenye mashiko ya kuongoza nchi hii, lakini yanapokuja majibu ya Mawaziri, zile dakika tano tano, yanakuwa majibu mepesi ambayo hayaendani na uzito wa michango ambayo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiitoa.

Mheshimiwa Spika, nakuomba, ikikupendeza utengeneze Kamati Maalum ya Kudumu ambayo itakuwa inaangalia majibu, ili vitu ambavyo viko kwenye Hansard ambavyo Waheshimiwa Wabunge wameshauri Mawaziri, kila linapokuja Bunge linguine, wametekeleza kiasi gani? Ili tupate Hadidu za Rejea. Vinginevyo, tutakuwa tunasema vitu vizuri, watu wanavisikia, wanatupia simu wanatupongeza, lakini implementation yake haipo. Hata vikao vya kawaida huko nje, kuna yatokanayo na maazimio, lakini hapa tukisema, vinaenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ukitengeneza Kamati hii, Mawaziri watakuwa wanajua kabisa Bunge lijalo wataenda kuulizwa; hili lilichangiwa, hili lilichangiwa, limefanya kazi gani? Limefika wapi? Yako mambo mazito sana yamechangiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka nilisikia mchango mmoja wa Mheshimiwa Mbunge mmoja aliongelea suala la kiwanda kikubwa cha pamba kitakachomeza pamba yote ya nchi hii ambayo itatoa tija kwa wakulima, itatoa ajira kwa vijana, tutauza majora nje, lakini ilipofika kwenye majibu, sikusikia, imeishia vivyo hivyo hewani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisikia Mheshimiwa Mbunge alisema kuhusu mambo ya task force ambayo inasumbua wafanyabiashara, alisema Mheshimiwa Nape pale, lakini ilipokuja kwenye majibu, kimya. Mpaka niliposikia Mheshimiwa Rais wangu analiongelea juzi, wakati anasema watu wasisumbuliwe kuhusu kodi.

Mheshimiwa Spika, hebu tutengeneze Kamati ambayo itakuwa inafuatilia mambo haya kwa Mawaziri ili vitu vinavyosemwa humu, tuvione vinafanya kazi kwa sababu ni vitu vyenye mashiko, ni nondo zinashuka humu lakini zinaishia hewani hewani tu. Matokeo yake mpaka watu wengine huko nje wanaanza kusema viongozi sio asilimia 60, hatuna uwezo. Uwezo tunao. Kama watu hawawezi kutoa mrerejesho, wapishe wengine waweze kufanya hizi kazi.

Mheshimiwa Spika, fedha zinazopatikana TARURA, naamini kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu atalijibu hili, kwa sababu ni kauli yake tu inatupatia mabilioni ambayo yanakwenda kwenye mambo ya barabara.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kupata nafasi ya kufunga dimba kwa leo. Naomba nianze kwa kuwapa pole wananchi wote wa Mkoa wa Singida na hasa Waislam kwa kufiwa na Shehe wetu wa Mkoa na kesho tunakwenda kumzika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, japo imegusa mambo mengi ya msingi, lakini nataka niende kwenye kipengele cha afya hasa katika suala la maboma ya zahanati. Wananchi wetu walihamasishwa sana kipindi cha nyuma kwamba wajenge zahanati kwenye vijiji na vituo vya afya kwenye kata, wakifika hatua ya lenta Serikali itamalizia. Wananchi wangu wa Mkalama walifanya hivyo na tuna maboma zaidi ya 19.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara zinazohusika, wangetekeleza ahadi hii ambayo waliwaahidi wananchi wetu, kwa sababu wananchi wetu sasa wamevunjika moyo na tukiwaambia mambo mengine ya maendeleo wanakuwa wazito, kwa sababu wanasema mlituambia tujenge, tumejenga na sasa maboma yetu yana zaidi ya miaka saba, mengine miaka mitano, nguvu zao wanazitazama na Serikali imeshindwa kumalizia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi majengo mengine wizara inakuja na ramani mpya, wanasema ramani hii ni nyingine, sasa lile jengo lenu ramani imekuwa ya kizamani. Suala la chumba cha sindano kuchomwa au kupokea dawa wala sidhani kama lina uhusiano sana na ramani. Naomba sana Serikali imalizie majengo haya ili wananchi wetu waendelee na tabia yao nzuri ya kuchangia maendeleo ya Serikali pale wanapoambiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwa haraka suala la watumishi. Tunaweka hizi zahanati, tunaweka majengo mapya, hospitali na nini, lakini watumishi hatuajiri wakati nafasi zipo. Ningeiomba Wizara ya Utumishi zile nafasi ambazo ni replacement tunafahamu kwamba leo kuna watu wanastaafu, leo kuna watumishi wametangulia mbele ya haki, watumishi hao tayari wana bajeti tayari kwenye Wizara, wana mishahara ipo, kwa nini replacement haifanyiki mara moja mpaka kusubiri uje uombe wakati zile nafasi zipo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe wafanye recruitment kwa sababu watu ambao wana sifa tunao wengi, wako mtaani katika wizara mbalimbali, wawe wanasubiri tu ikitokea mtu amefariki, mtu amestaafu, anajazwa moja kwa moja ili inapokuja kuombwa ajira mpya, ziwe ajira mpya kweli siyo zile za replacement ambazo tayari zilikuwa kwenye bajeti. Kwa sababu inakuwa shida sana kuajiri watu kwa sababu ya bajeti, sasa zile nafasi ambazo watu wamefariki kwa nini watu wasiajiriwe moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta zahanati ina Nurse mmoja halafu wananchi wanalalamika zahanati inafungwa, Nurse huyo pia ana watoto, ana mume anatakiwa akamhudumie au mke, sasa akitaka kwenda nyumbani akifunga anaanza kulaumiwa, wakati pia yeye ni binadamu ana mambo ya kijamii. Kwa hiyo ningeomba hizi replacement zifanyike haraka, kwa wakati, wala siyo za kusubiri kibali, kwa sababu ni nafasi ambayo ipo na Wizara ya Utumishi ipo, watu wafanyiwe recruitment, wajazwe kwa wakati, inapofika kwa Rais tunaomba ajira ziwe mpya kwa maana ya mpya siyo zile za kujaza nafasi kama ambazo hizi zilizopo sasa hivi ni za kujaza nafasi. Kwa hiyo tuombe zingine mpya ili watu waajiriwe na kazi zipo kwa sababu tumejenga hospitali nyingi hazina watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa sababu naenda haraka sana, muda mwenyewe ndiyo wa mwisho, suala la hii miradi yetu ya kimkakati. Tumetengeneza miradi mingi lakini mradi mmojawapo ni wa mwendo kasi Dar es Salaam. Ni mradi mzuri wa kimkakati na hapa kwetu ni mradi ambao tulijua utatusaidia kuondoa suala la foleni Dar es Salaam, lakini leo hii ule mradi umekuwa ni kero, yaani kuingia kwenye mwendo kasi kama una ubavu huwezi, watu wanaanguka wanaibiwa wanafanya nini, niliingia mle juzi nikaogopa wasije wakajua mimi ni Mbunge, wakaanza kuniambia sisi tunateseka na ninyi mpo. Naomba kampuni mbili zifanye kazi kwenye mradi ule, kama haiwezekani basi daladala zile zirudishwe za Posta - Kimara kwa sababu watu wanapata shida sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ambayo inabeba asilimia 70 ya uajiri wa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Wilaya yangu ya Mkalama ina wakulima wa vitunguuu takribani 250, wanaolima karibia tani kuanzia 24,000 mpaka 94,000. Wakulima hawa wanalima kwa kilimo cha mvua na sio umwagiliaji, hivyo, inapofika wakati wa mavuno vitunguu vinajaa sokoni kwa wakati mmoja na hii inapelekea sasa wanunuzi kuamua wanunue kwa bei gani. Kwa hiyo, unakuta katika kipindi cha mwaka mmoja mkulima mwingine anauza gunia Sh.250,000/= mwingine anauza Sh.20,000/= kutokana na kwamba vitunguu vimejaa sokoni. Pia hali hii inasababisha wale wanunuzi kuamua kipimo cha kununua, mwingine anajaza gunia anaweka na kilemba juu kwa sababu vitunguu vimejaa sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara iwaangalie wakulima hawa wa vitunguu kwa kujenga maghala ya kutunzia vitunguu katika Kata yangu ya Mwangeza inayolima vitunguu. Hii itasaidia ili vitunguu vinapovunwa kwa wakati mmoja viwekwe kwenye maghala na viuzwe kwa utaratibu na siyo mtu auze vitunguu shilingi 20,000 kwa sababu vitunguu ni perishable, vinaoza haraka na mkulima anakuwa hana ujanja anapangiwa bei anayotaka mnunuzi.

Kwa hivyo, naomba Wizara ikajenge maghala na maghala ya vitunguu yanatakiwa yajengwe kitaalamu kwa sababu vitunguu ni perishable sio sawa na mahindi, ipeleke nguvu pale nguvu pale ijenge maghala ili kuwalinda wakulima hawa wa Mwangeza na Mkalama ambao wanalima kwa nguvu zao. Ndiyo maana tannage imeshuka kutoka 94,000 mpaka 24,000 kwa sababu hawana uhakika na soko limekuwa kama kamari, mnunuzi ndiye anaamua anunue kitunguu kwa bei gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara katika hotuba yao hawajaongelea kabisa kwa undani suala la kilimo cha mbogamboga na matunda. Katika kata yangu mojawapo ya Gumanga kuna kiwanda kimejengwa cha kusindika mazao ya mbogamboga kwa kutumia wananchi na shirika lisilo la Kiserikali la Helvetas, kiwanda hiki kimegharimu karibu milioni 106 hakifanyi kazi kwa sababu malighafi haipo.

Mheshimiwa Spika, niombe Wizara iwaangalie wakulima wa nyanya wa Gumanga kwa kuwawezesha kwa mbegu bora, visima vya umwagiliaji na utaalam ili kiwanda hiki kiweze kufanya kazi na kitasaidia hata mikoa ya jirani wanaolima mboga mboga na soko litapatikana hili ambalo tunahangaika kuimba sasa hivi kwa sababu kiwanda kimekaa tu hakina kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuombe rafiki yangu Bashe pamoja na Waziri, nenda pale Gumanga ukaangalie kiwanda hiki tuwawezeshe wakulima hawa waweze ku- supply material ya nyanya ya kutosha katika kiwanda ambacho wamekijenga wao kwa nguvu zao pamoja na shirika lisilo la Kiserikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile niende kwenye suala la alizeti. Wote tunafahamu shida ya mafuta tuliyonayo na zao la alizeti katika hotuba ya Rais iliyopita lilitajwa kama zao la mkakati. Lakini katika hotuba sijaona huo mkakati jinsi ambavyo umeongelewa vya kutosha. Leo hii wakulima wa Mkalama analima hekari moja anapata gunia tatu. Anaona haina tija kulima kwa sababu tatizo kubwa ni mbegu, mbegu ambayo inaonekana kidogo inafanya vizuri, mbegu ya hysan inatoka nje. Kilo mbili ni 70,000, mkulima hawezi kununua mbegu hii.

Mheshimiwa Spika, niiombe Wizara, wakati mnafanya utaratibu wa kutafuta mbegu na utafiti, basi angalau mbegu hii iangizwe kwa bulk na ikibidi iondolewe kodi ili wananchi waendelee kutumia mbegu hii hysun ili kuweza kupata kipato lakini vile vile kuondoa tatizo kubwa la mafuta katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana Mheshimiwa waziri na Naibu Waziri mliangalie sual ahili la hii mbegu ya Hysan. Hakika mkiitupia jicho itashuka bei na itatupunguzia suala zima la tatizo la mafuta. Wakati huo huo, mkifanya utaratibu wa kutosha wa kutafuta mbegu ya kisasa ya utafiti itakayofanyika katika nchi yetu ili zao hili la alizeti liendelee kuwa zao kongwe na zao ambalo litatuondolea shida ya mafuta katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Singida, alizetu watu wameshaanza kuacha kulima. Mtu angaalia anapata gunia tatu, bora alime karanga apate gunia 12 au bora alime mahindi apate angalau gunia 10 kuliko analima alizeti anapoteza muda anapata gunia tatu. Tatizo ni mbegu na mbolea na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri jambo hili la alizeti hamjaonesha mkakati mnaotaka kuufanya katika kulinyanyua. Hamjaliongelea vizuri katika hotuba yenu nimepitia vya kutosha, hebu mlitazame ili tuweze kuondoa tatizo la mafuta katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, kwa leo niliona niseme hayo. Nashukuru sana kwa nafasi hii. Naunga mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi kuchangia katika Wizara hii ambayo ni kichocheo kikubwa na muhimu sana cha maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza na wananchi wangu. Wilaya yangu ya Mkalama ina vijiji 70 na katika vijiji hivyo 20 bado havijapata umeme na katika vijiji hivi ambavyo havijapata umeme Mheshimiwa Waziri iko kata nzima ya Mwanga ambayo haijawahi kuona umeme kata hii. Mheshimiwa Waziri, tarehe 17 Aprili, 2020 ulikuja Mwanga na Serikali ikakosa pale kwamba kesho yake tu tarehe 18 nguzo za umeme zitamwagika kama maji pale, wananchi walishangilia sana. Lakini, mpaka leo Kata hii wananchi wa vijiji hivi vya Kata ya Mwanga ambavyo ni Msisai, Kidarafa, Mwanga, Kidigida, Msiu na Marera bado wanaota tu kwamba nguzo zitamwagika alisema Waziri. Nashukuru kwamba umeendelea kuwa Waziri katika Wizara hii na hivyo naamini sasa hutaiangusha kauli hii ya Serikali ambayo ilionesha kwamba nguzo zingemwagika kama mvua lakini mpaka leo kata hii haijapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Wziri nikuombe katika Awamu hii ya REA III kata hii iwe kata ya kwanza kupata umeme katika vijiji hivi 20 vilivyobaki. Mbaya zaidi Mheshimiwa Waziri, katika wakandarasi uliowaagiza kwenye Mkoa wa Singida ulimuagiza Ms Central Electrical International Limited kwenda kufunga umeme Singida. Lakini tulipomfuata akasema hana scope ya Mkalama. Scope yake ni Ikungi na Singida Rural. Kwa hiyo, mpaka hivi ninavyoongea REA Awamu ya III sisi hatuna mkandarasi, tuna kiini macho. Labda ningeomba katika majibu utakayokuja nayo utuambie mkandarasi wetu nani ili tumfuate tuweze kuona umeme unapatikana Mkalama.

Mheshimiwa Spika, nimuombe Waziri kweli bei tumeshusha shilingi 27,000 kuingiza umeme na ametangaza leo hakuna kuuziwa nguzo lakini umeme unapofika huko vijijini wananchi wanakuwa wengi sna wanasubiri kuwekewa umeme. Waliolipia 27,000 na ambao hawajalipia 27,000. Hawa wanaoweka umeme wanasema sababu za vifaa vingine ambavyo vinasababisha uweze kuwekewa umeme. Nguzo zenyewe za LV kwa mfano kwenye Jimbo langu nguzo zinatakiwa 1400, hakuna. Kuna waya za ABC milimeta 50, kilometa 74 zinatakiwa, hakuna! Hiyo ni reference najua na majimbo mengine itakuwa hakuna. Suspension clamp karibu 990 hamna! Tension clamp 60 hamna, staycompletewith 140 hamna.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuombe Mheshimiwa Waziri tunapopeleka tuwapelee na hivi vifaa ili ile foleni ya kuwekewa umeme sasa kwa 27,000 iweze kufanikiwa. Kwa sababu, tunasema 27,000 lakini wananchi wako wengi wameshafanya wiring wengine wanasubiri lakini ukiwagusa TANESCO hivi vifaa hawana na ukifuatilia kweli, hawana! Nakushukuru Mheshimiwa Waziri umekuwa mwepesi sana wa kuchukua hatua kw watendaji wazembe, hilo nikupongeze. Lakini nikuombe wapelekee na hivi vifaa ili unapowachukulia hatua wasiwe na sababu ya kulalamika hukuwapelekea vifaa halafu umewachukulia hatua kwamba ni wazembe ili hili zoezi la 27 na umeme kufika kule vijijini wananchi walipate kwa kuhakikisha basi vifaa hivi vinakwenda. (Makofi)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa kuna taarifa endelea.

T A A R I F A

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe Taarifa mzungumzaji anayezungumza sasa kwamba wako baadhi ya watu wenye uwezo wao ambao kutokana sasa na vifaa vile kutokuwepo wanakuwa tayari kwa hiari yao kulipa nguzo pamoja na zile gharama kwa hiari yao. Kwa hiyo, wale watu walioko kule nao wanashindwa kufanya hivyo hata kama wangeweza kufanya hivyo kutokana na kwamba bei imewekwa elekezi 27,000 wale wenye uwezo walio wachache.

SPIKA: Mheshimiwa Mtinga unapokea Taarifa hiyo?

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, naipokea lakini sifurahishwi sana na hii. Wenye uwezo wanaweza wakasababisha TANESCO wakalalia huko kwenye uwezo na wananchi wetu wenye vipato vidogo ikashindikana. Kwa hivyo, ningeomba tu vifaa viende halafu wananchi wote wapate umeme kwa hiyo 27,000 ambayo Serikali yetu imeiweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niusemee na Mkoa wangu, Mheshimiwa Waziri wakati unafungua matumizi ya gesi majumbani kule Lindi ulisema kwenye hotuba yako kwamba mikoa itakayofuata baada ya Dar es Salaam ni Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Singida uliitaja. Tulishangilia sana jambo hili kwamba sasa na sisi tutapata umeme wa gesi kupitia bomba ili kwenye nyumba zetu tuweze kusambaziwa gesi. Lakini katika hotuba yako nilikuwa nasikiliza kwa makini sana ili niweze kuona ule msukumo wa hotuba yako ukiendana na bajeti, sikulisikia hili.

Mheshimiwa Spika, nikuombe, jambo hili ni la muhimu sana, kupata gesi ya majumbani ambayo tumeweka bomba kwa gharama kubwa sana limefika Dar es Salaam na tunatumia kidogo mno kwa kiasi cha gesi inayofika pale.

Sasa huu mpango uliusema kwenye hotuba ambayo nilikuwa najua ni hotuba ya ukombozi hujalisema kwenye bajeti. Labda pengine utakapokuja kwenye kujumuisha useme huu mpango wa kutoa bomba lile la gesi kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro kuja Dodoma na hatimaye kufika Singida kwenye mkoa wangu kama upo au au haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niwaombe tu Serikali hivi vitu vingine kama bajeti inakuwa ngumu na miradi hii ni mikubwa, tusisahau private sector. Najua shirika la TPDC limepewa mamlaka ya kisheria kama hodhi kufanya hili jambo peke yake. Mzigo huu unakuwa mzito, private sector ipo na watu wana fedha. Mimi ningeshauri Wizara muwe mnaangalia na vitu vingine kama hivi vizuri mnaruhusu private sector isaidie basi huduma hizi zinaweza kufika haraka sana katika nyumba zetu.

Mheshimiwa Spika, hii gesi itasaidia sana kulinda mazingira, ni faida mtambuka, kwanza maisha ya wananchi yatashuka kwa maana gharama zitashuka kwa sababu wataacha kununua mkaa kwa bei kubwa lakini vile vile mazingira ya nchi katika mikoa yetu hii yataboreka kwa sababu watumiaji wakubwa sana wa mkaa wako mjini. Sasa kama mabomba ya gesi yakifika ina maana soko la mkaa litakufa na mazingira yetu yatapona na fedha nyingi zinazokwenda Wizara ya Mazingira kwa ajili ya kuokoa miti zitakuwa zimepona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, huu ni mradi ambao utakuwa ni wa kimkakati kabisa. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, jambo hili ulilisema wewe kama Serikali. Usiliweke kando. Ni jambo la muhimu sana, najua gesi ikifika Singida mwisho itakwenda mpaka Shinyanga na mwisho itamaliza nchi yetu yote. Mradi wa maji unatoka Ziwa Viktoria, upishane na gesi kwenda kule. Nchi yetu ni kubwa, ni soko tosha la miradi yetu ya kimkakati kwa hiyo tuitumie vizuri kwa kuhakikisha gesi hii inafika Singida kama ambavyo ulikuwa umesema kwenye hotuba yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sipendi sana kugongewa kelele. Naomba nishukuru na kuunga mkono hoja. Mheshimiwa Waziri uje na majibu kuhusu jambo hili la gesi. Ahsante sana na suala la umeme kule Mwanga na vijiji vilivyobaki. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa sababu ya muda shukrani zote zimeshakutosha. Nashukuru kupata nafasi hii ya kuchangia katika Kamati yangu ya LAAC.

Mheshimiwa Spika, uhai na uchumi wa nchi yetu umelalia kwenye halmashauri zetu na Ushahidi ni fedha zinazopelekwa huko ni mabilioni ya fedha za watanzania zinapelekwa kwenye halmashauri. Kwa sababu, fedha nyingi zinakwenda huko tunategemea kwamba, usimamizi mkubwa wa fedha na wa makini sana ufanyike huko na watu wanaohusika na usimamizi huu ni maafisa masuuli wakuu katika halmashauri zetu ambao ni wakurugenzi.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, tumehoji wakurugenzi wengi takribani 40 kwa mfano, lakini wakurugenzi hawa wanatofautiana kwa kiasi kikubwa sana katika uwezo wao pale wanapojibu maswali yetu na wanapowakilisha halmashauri zao. Sitaki kuwa na mashaka na uteuzi na mchakato wa jinsi wanavyopatikana, lakini ningependa kushauri kwa sababu, ya umuhimu sana wa watu hawa wanaoitwa wakurugenzi wa halmashauri, maafisa masuuli wa fedha nyingi za watanzania, ningeshauri kwamba, uteuzi wao uanzie kwenye usaili.

Mheshimiwa Spika, wako watanzania wengi sana wana uwezo mkubwa, wafanyiwe usaili wa kutosha, wafanyiwe vetting, baada ya hapo Mheshimiwa Rais sasa akabidhiwe kundi kubwa la watu kama 300 hivi afanye mamlaka yake ya uteuzi ndani ya watu ambao wamefanyiwa usaili, ili tupate watu watakaosimamia fedha hizi. Watu ambao ni makini kwa sababu uhai wa Watanzania uko kule kwenye halmashauri ambako kuna fedha nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upungufu wa watumishi kwenye halmashauri. Kama nilivyosema fedha nyingi ziko kule, lakini watumishi ni wachache sana, watu wanakaimu nafasi wanapewa fedha za acting allowance, kuna watumishi wanadai mpaka bilioni 80 tumewahoji kwa ajili tu ya ku-act, fedha hizi ni sawa na pension ya mtu mwingine. Kwa nini watu wasiajiriwe na watu wenye uwezo wapo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Serikali inadhani inaepuka mzigo wa ajira ikumbuke kwamba, inapoteza fedha nyingi zaidi kwa kutokuajiri watu ambao wana uwezo na kuweka watu wanao-act kwa kufanya maamuzi ya mabilioni ya watanzania ambayo yako kule. Kwa hiyo, niishauri Serikali, fedha nyingi inapeleka, isikwepe mzigo wa kuajiri watu wenye uwezo ili wasimamie fedha hizi tuweze kuona tija ambayo ya fedha hizi Mheshimiwa Rais anazipeleka kila siku kule katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la watumishi pia kukaa maeneo, sehemu moja. Unakuta mkuu wa idara ana miaka kumi katika eneo moja; ameshakuwa sawa na wakulima, ameshakuwa saw ana wafanyabiashara wa eneo husika, amejisahau kabisa kwamba, yeye ni mtumishi wa umma kwa sababu, ameshakaa muda mrefu. Matokeo yake anaingia kwenye migogoro ya ardhi, anaingia kwenye migogoro mingine, matokeo yake kunakuwa kuna matatizo mengi kwenye halmashauri ambayo yanakuja kama hoja kwa CAG. Kwa hiyo, ningeomba tatizo hili Serikali pia, iliangalie kwa macho mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hoja zangu hizi sasa nikupongeze kwa sababu, muda bado ninao, kwa kuchaguliwa. Na tunakushukuru ni Spika wa viwango, taratibu na kanuni zimejaa kwenye kichwa chako. Tuna hakika mambo yatakwenda vizuri katika Bunge letu. Ahsante sana, naunga mkono hoja hii, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Sita na Mkutano wa Saba wa Bunge pamoja na Uchambuzi wa Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa kwenye Mkutano wa Tatu na Mkutano wa Nne wa Bunge
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kidogo katika suala hili muhimu sana la sheria ndogo ambazo kiuhalisia ndiyo zinazowaongoza wananchi wetu katika kuishi katika maisha ya utawala bora na maendeleo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Mawaziri, lakini zaidi nimpongeze sana Rais wangu Mama Samia kwa jinsi ambavyo muda wote amekuwa akiwaza maendeleo ya Watanzania na maisha bora kwa Watanzania. Rais wetu amekuwa halali, hapumziki, kuhakikisha kwamba wananchi wetu tunazidi kupata maisha bora na kwa kweli tuendelee kumuombea Mungu ili atimize lengo lake la kufanya Watanzania tuwe tuna maisha bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ndogo zimetungwa au zipo kwa ajili ya kufanya sheria mama ambazo zinatungwa na Bunge pamoja na kanuni zinazotungwa na Mawaziri ziweze kufanya kazi kiuhalisia katika jamii. Kwa hivyo, sheria hizi zinapokuwa hazina uhalisia zinafanya maisha ya wananchi wetu kuwa magumu na pengine kuingia kwenye hatia bila kukusudia au kuingizwa kwenye hatia au kurudishwa nyuma kimaendeleo. Kwa hiyo, Kamati inaposema kwamba sheria hizi ndogo marekebisho yake yafanyiwe mapema tena kwa time line ni jambo la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano sheria kwenye TS No. 105 ya tarehe 25 Februari, 2022 sheria inayotoa mamlaka The Tax Administration Act Sura Na. 438 ambayo inaipa sheria ndogo The Tax Administration of Tax Ombudsman Service Regulation ya 2022 kanuni ya sita inakataza mtu aliyeajiriwa kuwa mchunguzi wa kikodi wa masuala yote ya matatizo ya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, unafahamu kwamba wafanyabiashara wamekuwa na matatizo mengi kuhusiana na kodi, sasa yuko mtu hapa anaitwa ombudsman ambaye kazi yake ni kuchukua yale matatizo yote ya wafanyabiashara halafu anapochukua haya matatizo anayakabidhi kwa Waziri, ili Waziri aweze kuchukuwa hatua katika sehemu zinazohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu huyu anaambiwa kwamba kwa kufanya kazi hii asifanye kazi nyingine yoyote inayompatia kipato cha mshahara anapofanya kazi hii. Kazi nyingine yoyote, lakini kanuni hii wala haijaeleza kwamba kazi zipi labda zinazoingiliana na kazi yake ile ya kupokea matatizo ya kikodi, imemzuia moja kwa moja. Kiuhalisia unaona kabisa kanuni hii haitekelezeki ina maana huyu mtu yaani anakuwa amekaa tu yani hata kuandika write up labda amuandikie mtu afanye biashara haruhusiwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kanuni hapa ailezi zile kazi hasa ambazo zina muingiliano na kazi yake ya kupokea matatizo ya kikodi imeacha tu wazi. Kwa hiyo tunaposema kanuni kama hii irekebishwe maana yake inampa mtu huyu utata, aidha, atakuwa lofa zaidi au kiuhalisia atafanya kazi kinyume kwa sababu kanuni haijamueleza kwamba kazi zipi hasa zinazoingiliana na kazi yake ya kupokea matatizo ya kikodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hapo hapo katika kifungu kinachohusu Administration Tax Ombudsman Service Complain Procedure Regulations of 2022 ambazo zimetungwa chini ya kifungu cha 28(g) kwamba huyu mtu akisha collect matatizo anamkabidhi Waziri, Waziri aweze kutoa maelekezo kwenye mamlaka kwa mfano TRA kuchukua hatua juu ya matatizo ya kikodi ambayo ameyapokea kutoka kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kanuni haijambana Waziri ndani ya muda gani aweze kutoa hayo maelekezo, kwa hiyo, Waziri anaweza akachukuwa akatia kwenye draw akaendelea na shughuli zake zingine, mwezi, miezi, mwaka wakati tatizo lile la kikodi kwa wale wafanyabiashara linawasumbua, pengine limefanya wengine wanafilisika kwa sababu tayari sheria zile zinaendelea kutumika wakati marekebisho, yanasubiliwa lakini sheria zinaendelea kutumika kwa sababu zimeshaanza kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kifungu hakijambana Waziri kwamba unapaswa sasa umeshapokea haya matatizo toa maelekezo ndani ya miezi mitatu, ndani ya mwaka. Kwa hiyo tunaposema kwamba marekebisho haya yafanyike haraka na ninashukuru kabisa kwamba Kamati imetoa mpaka muda maalum kwamba ndani ya muda fulani marekebisho yawe yamefanyika kwa sababu hivi vitu vinawaumiza watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mtu analalamika labda anatozwa kodi kubwa kutokana na biashara anayofanya Waziri ameshapelekewa, ametia kwenye draw, hakuna kifungu kinambana, mwaka unaisha, mwisho mtu anafilisika. Kwa hiyo, utaona kabisa kwamba ni kifungu kidogo sana, lakini kimesababisha maisha ya watu wengi kuharibika kama hakijafanyiwa marekebisho ndani ya wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wamesema wenzangu hapa zipo sheria kama hizi kwenye halmashauri, kwa mfano halmashauri inakuambia sasa utafuata kalenda kipindi cha kulima mahindi kimefika utalima mahindi, sasa mtu unakuta ana shamba la umwagiliaji, ana maji anataka kulima nyanya kalenda ya halmashauri inamwambia sasa unatakiwa ulime mahindi. Sasa huyu mtu unamtia umaskini, pengine ndio kipindi ambacho nyanya zinahitajika kwa wingi kalenda haisemi inakuambia tu ni kipindi cha kulima kitu fulani, kwa hiyo unakuta ni sheria ndogo imetungwa kwa lengo zuri, lakini kwa sababu haina uhalisia inasababisha maishi magumu kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaposema kwamba kanuni hizi zifanyiwe marekebisho haraka ni mambo ambayo yanawagusa wananchi, halmashauri inasema utafuga kwa idadi maalum, sasa unampangia mtu utajiri! Yaani mtu ana uwezo wa kufuga ng’ombe 1,000 wewe unataka unamwambie afuge ng’ombe wanne kwa hiyo sasa ina maana sheria sasa inaanza kubana watu wasitajirike wakati sisi tunataka watu watajirike, nchi ipate kodi na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo utaona hizi sheria ndogo zisipoangaliwa vizuri zinaweza zikasababisha umaskini ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, Maazio ya Kamati yanaposema sasa marekebisho yafanyike haraka na inaweka na muda tujue kabisa tunagusa mambo ya wananchi kuweze kuishi maisha bora waweze kupata utajiri na nchi iweze kupata maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nilitaka nisisitize hilo kwa kuunga mkono hoja kwamba hizi sheria ndogo ndio engine ya kufanya sheria mama zifanye kazi, ndio engine ya kufanya kanuni zile za Mawaziri zifanye kazi na niwaombe basi na hawa Mawaziri wanapotunga hizi kanuni wawe wanakumbuka kabisa wanaenda kugusa maisha ya watu na wasitoke nje ya sheria mama ambayo inakuwa imetungwa humu ndani ya Bunge na mara zote sheria zinazotungwa humu haziendi kuwakandamiza wananchi bali kuwaletea maendeleo katika nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba niunge mkono hoja ahsante. (Makofi)
Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jambo hili muhimu sana ambalo linajenga mustakabali wa kuijenga nchi yetu miaka inayokwenda mbele na miaka ya sasa. Naomba nianze kwa kuunga mkono kabisa hoja nzuri ambayo Mheshimiwa Ezra ameileta, hoja ya kukomboa kizazi chetu.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu sasa ni nchi ambayo inajiunga na forum mbalimbali ikiwepo East Africa na nchi zinazidi kuongezeka ndani ya East Africa na wenzetu wanasomesha watoto wao kwa nguvu kabisa. Katika nchi yetu mkombozi pekee aliyebaki katika suala la ajira ni kujiajiri. Sasa tunataka vijana wetu wajiajiri lakini tunataka kuepuka kuwasomesha, sasa sijui watajiari kwenye ajira gani? Nasema hivi kwa sababu wanashindana na wenzao katika East Africa ambao wamesoma sana na mipango ya kujiajiri lazima watu wawe wamesoma, kwa hiyo hiki ambacho kinatokea sasa tunakokwenda vijana watakuwa ni wafanyakazi sijui wafanya kazi za ndani sijui za mashambani? Maana yake tutakuwa hatuna wasomi ambao wamesoma ili waweze kujiajiri na kuajiri wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala hili, naomba kabisa Bunge lako tuje na solution ya haraka ili vijana wetu ambao wamefaulu vizuri waende wakasome. Huu utaratibu jinsi gani wanapata mikopo ya asilimia mbili, asilimia tatu pengine umefeli. Baada ya hao kuondoka, naomba Bodi ya Mikopo waje hapa watueleze formula hizi wanazitumia vipi, wanachagua vipi watu hawa. Tuwasaidie mawazo ikiwezekana, kwa sababu inaonekenana wamelemewa na huu mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema mwenzangu Mheshimiwa Kanyasu, huu ni mkopo wa aina gani? Mbona ni kama hisani. Wapo watoto wana division one mwaka jana hawakupata mikopo, wamekaa mwaka huu ndio wamebahatisha asilimia ndogo, wengine ndio wamefaulu na division one mwaka huu, hawajapata kabisa, afadhali hata yule aliyetolewa mfano ana viasilimia kidogo, wako wengi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe suala hili kwa kweli tutoke na muafaka hapa jinsi gani watoto wetu hawa ambao wamefaulu vizuri wanakwenda shule. Vinginevyo nchi yetu hii tuna idadi kubwa ya watu ndani ya East Africa, ukiacha Congo, lakini sasa sijui ndio tutaanza ku-provide wafanyakazi wa ndani kwa wenzetu. Kwa kweli inabidi sasa tuliangalie jambo hili kwa makini sana. Bajeti imeongezeka tulisikia hapa, bado marejesho yanafanyika, lakini sijui kitu gani kinatokea katika jambo hili. Jambo hili ni serious sana, hatuna urithi mwingine wa kuwarithisha vijana wetu na watoto wetu zaidi ya elimu, tukishampa elimu tunamwambia ardhi ile pale, mifugo hiyo hapo, nenda kajiajiri, lakini elimu wanayo, hivyo, atajua ata-convert vipi hiyo ardhi ili iweze kumpatia maslahi. Sasa hili atalifanya vipi kama hana elimu kichwani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningeomba niunge hoja suala hili na tulichukulie kwa makini, kwa u-serious mkubwa, hawa waende lakini Bodi ije hapa itueleweshe vizuri formula wanayotumia, tuwasaidie mawazo ili usawa upatikane. Watoto wengine wakishasoma private ndio kibali cha kunyimwa mkopo tayari. Pengine amesaidiwa huko wengine na compassion, wengine wamesaidiwa na Mbunge na wengine wamesaidiwa na mjomba. Mjomba ameshafariki, eti kwa sababu kasoma privatae tayari anaambiwa wewe huna sifa ya kuwa na mkopo. Kwa hiyo ningeomba hii formula iangaliwe upya kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache kwa uchungu sana naunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Rais wangu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza nchi kwa weledi mkubwa, na pia kuijaza jimbo langu fedha nyingi katika sekta zote. Leo hii tunajenga Vituo vya Afya, Gumanga pamoja na tunajenga Ilunda. vilevile leo hii tunajenga shule ya thamani ya milioni mia nne sabini katika Kata ya Ilunda, tumepata fedha za barabara na tunaunganisha kata zetu; yote haya yanatokana na Uongozi wake mzuri, nampongeza sana kwa hili.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, niiombe Serikali iunganishe haya mazuri kwa kutupatia kilomita arobaini na mbili za lami kutoka makao makuu ya wilaya kwenda makao makuu ya mkoa, ili wananchi wafaidi matunda hayo kwa kwenda vizuri katika mkoa wao na makao makuu ya wilaya yao.

Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye mchango wangu. Mimi ningependa kuongelea nia njema ya Serikali katika kulitizama upya suala la kilimo katika nchi hii. Nimeona nia njema ya Serikali sasa ya kupeleka fedha nyingi, na ushahidi tu ni juzi, Rais wetu amekabidhi takribani pikipiki 9,000 na vifaa vya kupima udongo kwa lengo la kuinua kilimo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo ninapata hofu kama nia hii njema itafanikiwa vizuri kutokana na kitendo cha kuzingunisha Idara zetu mbili katika Halmashauri, Idara ya Kilimo na Idara ya Mifugo kuwa Idara moja. Hizi Idara ni kubwa sana. Sote tunatambua umuhimu na ukubwa wa Idara ya Mifugo katika kuchangia pato la nchi hii na pia tunafahamu Idara ya Kilimo ilivyo muhimu. Kama ambavyo zipo Wizara mbili tofauti, Wizara ya Mifugo na Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, sijui ni busara gani imetumika katika kuunganisaha Idara hizi katika ngazi ya Halmashauri kuwa Idara moja. Tunafahamu Mkuu wa Idara atakuwa mmoja na kwa vyovyote lazima atabobea aidha, kwenye kilimo au kwenye mifugo; na kwa vyovyote utendaji wake utaendana zaidi na ubobezi wake. Sasa jambo hili la kuunganisha Idara hii kuwa moja wakati Mawaziri ni wawili na Idara zenyewe ni kubwa na zinapelekewa fedha sasa kwenda kuinua uchumi wa nchi, naona kama ni jambo ambalo tume-overlook kama Serikali.

Mheshimiwa Spika, mimi ningependa kuishauri Serikali, kwamba idara hizi zibaki kuwa idara mbili tofuati ili fedha nyingi hizi zinazopelekwa kwenye kilimo na kwenye mifugo ziweze kusimamiwa vizuri na wataalam katika kuleta tija katika nchi yetu. Kama kweli lengo ilikuwa ni kubana matumizi, sidhani, kwa sababu kwa kuunganisha idara hizi bado tumeongeza idara nyingine. Zilikuwa kama 19, sasa hivi ukiangalia idara na vitengo zinakaribia 23. Kwa hiyo mimi ningeomba niishauri Serikali yangu iliangalie upya suala hili la kufanya Idara hizi zisiwe moja ziwe Idara mbili tofauti kama ambavyo Wizara zipo tofauti, ili lengo jema hili hili la kuinua kilimo na mifugo iweze kufanikiwa vizuri katika Idara zetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, ningependa kuishauri Serikali yangu kuhusiana na suala la mipaka ya kiutawala katika nchi yetu. Mipaka ya mikoa, wilaya, kata, vijiji mpaka vitogoji ina migogoro mikubwa sana katika nchi yetu. Jambo hili linasababisha wananchi wetu wanagombana mpaka sehemu nyingine wanapoteza maisha; lakini vilevile maendeleo ya nchi yanarudi nyuma kwa sababu ya suala hili. Ipo mikoa imeanza hivi karibu kwa mfano, Mkoa wangu wa Singida ulikuwepo kabla ya Manyara. Manyara ilipoanzishwa, leo hii ukichukua GN ya Singida, ukichukua GN ya Manyara katika maeneo yanayopakana kila Mkoa unatambua eneo tofauti. Hivyo hivyo ukienda kwenye wilaya n ahata kwenye kata zetu.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi ningeshauri Serikali ifanye program maalum ya kuhuisha na kuangalia mipaka yote ya kiutawala katika nchi hii, ili kuleta utulivu wa nchi, kuleta maendeleo ya nchi na wananchi wetu wafanye kazi zao wakiwa katika hali yenye utulivu. Kwa hiyo ningependa kuishauri Serikali yangu…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mtinga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Festo Sanga.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, alolizungumza Mheshimiwa Mbunge ni sahihi kabisa. Hata kule Njombe na Mkoa wa Mbeya kuna changamoto kubwa ya mipaka ambayo imesababisha hata hili zoezi la uwekaji wa anuani za makazi kwenye nchi hii imekuwa changamoto sana maeneo ya mipakani. Kwa hiyo ni kweli anachokizungumza Mheshimiwa Mbunge, nilikuwa nataka kumpa taarifa kuhusu hilo.

SPIKA: Mheshimiwa Mtinga unaipokea taarifa hiyo.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hii kwa mikono miwili, na ninaamini hapa hata Wabunge wote wangepata nafasi wangekubaliana na jambo hili, ni tatizo kubwa, kwa hivyo niiombe Serikali ichukulie jambo hili kwa muhimu sana kwa sababu wananchi wetu wanapata tabu sana kwa kugombania mipaka. Tunashindwa kufanya nyingi kwa kusuluhisha migogoro hii. Kwa hivyo Serikali ilichukulie jambo hili ihuishe tu mipaka wananchi waelezwe, sisi Viongozi tuelezwe, mpaka unapita hapa, unapita pale ili kazi za nchi hii ziweze kuendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, mimi leo nilipenda nijikite katika maeneo hayo kwa sababu sipendi sana kupigiwa kengele. Lakini nikupongeze sana kwa jinsi ambavyo unaliongoza Bunge letu vizuri. Nilikuwa Mkoa wa Mbeya katika Halmashauri yako pale ya Manispaa hauna double road hata moja. Niombe Wizara ya Ujenzi pale panatia aibu, mji umebanana sana ule angalau iwepo double road pale katikati ili Mji wa Spika wetu ufanane na Jiji la Mbeya, ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangaia katika Mpango huu wa Serikali. Mchango wangu utajikita katika maeneo matatu kama muda utanitosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze na suala ambalo Serikali yetu hasa ilani ilitoa kwamba inataka kufikia ajira milioni nane kwa ilani hii tunayoendelea nayo. Hata hivyo jambo hili linakuwa gumu sana kutekelezeka kwa sababu vyuo vyetu vimejikita sana katika kuzalisha watu wa utawala, mambo ya kijamii lakini halijajikita katika kuzalisha watu wa production. Watu wa production ni watu ambao wamesoma mambo ya sayansi. Kwa sababu ukisema kilimo ni sayansi, kufuga ni sayansi, utawala tayari tuna watu wengi sana wa kutosha. Watu wa uhasibu, leo taasisi kubwa kama hii ya Bunge inahitaji Wahasibu labda wawili au watatu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli unapotaka kwenda kwenye production, kama unataka kufuga lazima uwe na watu wengi ambao wamesomea na wana uwezo. Ukitaka kulima ardhi hii ni kubwa na inahitaji watu wengi. Kwa hiyo, ningeshauri hivi vyuo vyetu vifike mahali viangalie production vinatoa watu wa aina gani katika vyuo vyao. Ukizingatia kwamba watu hawa wanakopeshwa mkopo na Serikali na inabidi walipe mkopo. Sasa kama ni watu ambao wanaweza kujiariri, ambao wanaweza kuzalisha ni rahisi kuwa-trace na kurudisha mikopo na watu wengine wakaendelea kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka huu mtindo wa ku- copy, sasa hivi ukiangalia UDSM na UDOM karibu course zote ni zile zile tu zinajirudia watu wa jamii, utawala na ndio nyingi. Kwa hiyo ningeomba mwelekeo wa vyuo vyetu uangalie kwamba unazalisha watu wa aina gani na hii itakuwa rahisi hata Serikali inapowakopesha fedha zile zirudi na uchumi wa nchi yetu kuweza kuchangamka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, lazima sasa niguse kwa mwajiri wangu ambaye ni wananchi wa Mkalama. Sasa hivi tunajenga barabara kutoka Manyara – Simiyu, barabara ya kimkakati kabisa. Barabara hii tunapojenga na tayari imetangazwa ni vizuri tukajenga katika mtazamo wa kibiashara pia ili Serikali iweze kukusanya mapato. Zipo baadhi ya barabara ndogo sana ambazo zikiwekwa pamoja na mradi huu ambao ni feeder roads zitasaidia sana kufanya barabara hii ichangamke kuleta mapato. Ikichukua barabara kutoka Iguguno inayopita Mkalama kwenda kuunganisha na barabara hii kule Sibiti na ukichukua barabara inayotoka Iyongero inakwenda kuunganisha na barabara hii kwenda kule Haidom, barabara hizi zinaunga barabara kubwa ya katikati ya nchi inayotoka Dar es Salaam mpaka Mwanza zinaunga na barabara hii ambayo itakuwa ni kubwa katika corridor upande wa kaskazini na huko ndiko kuna mbuga za wanyama na kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo utaona kabisa wananchi wanaotoka Nyanda za Juu Kusini watapita hapa katikati kwenye utalii wa ndani na kwenda kuchangamsha uchumi wetu kwenye mbuga za huku. Kwa hiyo utaona barabara hizi zitakuwa zimekaa kiuchumi zaidi na zitaleta faida kwa nchi yetu. Kwa hiyo ushauri wangu, kwa sababu sasa ujenzi wa barabara hii umeshatangazwa na unajengwa kwa EPC+F, basi na barabara hizi wataalam wetu waziunganishe katika barabara hii, hivi vipande viwili vidogo vya barabara nilivyovitaja, viwe kama feeder road ili barabara hii iwe na faida zaidi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nataka nisemee kwenye suala zima la mawasiliano. Mawasiliano ni muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu. Kitu kinachonishangaza sana, kaka yangu Mheshimiwa Nape juzi ameleta hapa Muswada wa kulinda habari binafsi, tukampitishia Muswada mzuri kabisa, lakini nataka alete tena Muswada mwingine wa kuhusu kulinda haki zetu. Mashirika haya yamekuwa yakituibia, hivi ni kwa nini bando zina-expire? Simu ni ya kwangu, nimenunua bando kwa fedha yangu, halafu unanilazimisha nitumie kwa muda unaotaka wewe, hii ni kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni sheria, basi iletwe hapa tuibadishe, kwa sababu tunawaibia wananchi. Anatafuta fedha kwa jasho, ananunua simu, anataka awasiliane ananunua bando limsaidie, anaambiwa ndani ya siku saba limeisha. Hivi hii sheria ni ya nchi gani? Kama ni sheria tunaomba ije hapa, kwa sababu tunaibia hawa wananchi na tunaibiwa huku tunaona, kwa nini unipangie kutumia bando langu? Mimi si ndiyo najua umuhimu wa mawasiliano ndiyo maana nikanunua lile bando la wiki moja! Kama nimeamua kulitumia taratibu, wiki moja imeisha nimeweka akiba kwa nini wewe ulikate? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningekuomba sana kwa hili uwe mkali, utuongoze hili jambo la kuibia wananchi wa Tanzania lifikie mwisho…

T A A R I F A

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa taarifa hiyo. Mimi bado naona kwamba kama utaratibu ni huo bado Bunge lako linahaja ya kutunga Sheria kuwalinda wananchi kuhusuiana na suala zima la matumizi ya bando, kwa sababu hata TANESCO tunanunua umeme kwa Tarif one na huo umeme ukifika unapata unit 75 unapofika mwisho wa Mwezi hujazimaliza zile unit zako zinabaki unaongeza zingine zinaendelea kukusaidia, hata ving’amuzi. Kwa hiyo, ninaomba bado kuna haja ya kuja hapa tutunge Sheria ya kuwalinda wananchi wetu na bando zao, akinunua bando atumie mpaka liishe kama sivyo hiyo huduma waitoe wasiiweke kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee na mchango wangu katika suala zima la kumuunga mkono Rais wetu. Mama yetu anao mpango mzuri wa kutaka wakina mama wapikie gesi safi, gesi asilia kwa sababu wanaumia sana na kupikia mkaa na kuni. Vilevile nchi inaisha kwa kukatwa miti kwa sababu ya mkaa. Nchi yetu tumebarikiwa tuna bomba la gesi linalotoka huko limefika Dar Es Salaam, lakini Bomba hili bado halijaenea katika nchi hii. Kwa hiyo, niombe katika mpango bomba hili litoke Dar es Salaam sasa lisambae katika nchi, lielekee Mwanza,Kigoma, Kaskazini, Arusha na kusini huku ili wananchi tuweze kutumia gesi asilia kwenye majumba yetu. Teknolojia ya magari sasa hivi inatumika, Dar Es Salaam sasa hivi magari karibu yote ya uber wanatumia gesi asilia

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilo moja ya gesi inakwenda mara mbili ya lita ya petroli na bei ya kilo moja ni karibu 1500 na huku petroli ni 3000 na kitu. Kwa hiyo katika mpango bomba la gesi liende likasambae hata kwa kipenyo kidogo sio sawa na kipenyo kikubwa sana kilichotoka kule kusini ili lisambae kwenye nchi ili tuweze kutumia gesi na tumuunge mkono Mama yetu kwa kuhakikisha kwamba tunatumia gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili litachangamsha uchumi kwa sababu miti itapona na tabianchi itabadilika kuwa positive, mvua itaongezeka mabwawa yetu yatajaa maji. Kwa hiyo hili jambo lina faida mtambuka lina faida kubwa sana kusambaza bomba ambalo tayari tunalo. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri katika mpango wako fikiria suala la Bomba kwenda Mikoani. Kama Mama anatoa Bilioni 100 kila Mwezi kwenye ruzuku ya mafuta anao uwezo pia wa kutoa fedha kwa aijili ya kujenga bomba ambalo litatuokoa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka tumuunge Mkono Mama yetu katika uchumi kwa kusambaza bomba wananchi wa Tanzania wafaidi bomba hili wakiwa bado hai na vizazi vijavyo pia waje wafaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niseme hayo kwa uchungu kabisa kwamba yakitekelezeka naamini Watanzania wengi watafurahi. Ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Kamati ya Maendeleo na Huduma za Jamii.

Mheshimiwa Spika, mimi nitaanza kwanza kwa kushukuru Kamati zote mbili kwa kutoa maazimio mazuri kabisa ambayo yakitekelezwa yatatusaidia sana, lakini naomba nijikite sana katika suala zima la malezi ya vijana wetu, watoto wa kiume na watoto wa kike.

Mheshimiwa Spika, niishukuru jamii na Serikali kwamba tumeweka mkazo sana kwa Watoto wakike kiasi kwamba matokeo yake tumeanza kuyaona, matokeo mazuri kabisa sekta muhimu katika nchi hii zimekamatwa na wanawake hata Bunge letu, hata nchi na zinaenda vizuri kabisa. Hili ni jambo jema ambalo tumelifanya kama jamii.

Mheshimiwa Spika, lakini mimi nataka tu nisikitike kidogo, tumesahau kabisa malezi ya watoto wa kiume. Watoto wa kiume wamekuwa kama kuku huria wale wa kienyeji ambao wanajichungia tu, hawana mtu wa kuangalia. Mambo mengi sasa hivi tunayoyafanya tunamwangalia mtoto wa kike tu, tumesahau kabisa kama mtoto wa kiume ni sehemu ya familia. Hata wazazi tumeishafikia hatua ukifika nyumbani unauliza Glory yuko wapi? Hawa yuko wapi? Ukiambiwa wako ndani wanajisomea inashia hapo, huulizi Shabani yuko wapi wala Omari yuko wapi, hata wakija nyumbani saa tano usiku. Jambo hili limefanya watoto wa kiume sasa wamekuwa siyo responsibility kabisa kwenye familia na huko tunakoenda sasa tunaandaa bomu ambalo tutakuja kushindwa kabisa jinsi ya kulidhibiti.

Mheshimiwa Spika, mimi ningeomba Wabunge, hasa wanawake wajiweke zaidi kwenye uzazi, wasiweke kwenye ule kutetea haki za wanawake, jiweke kama mzazi una watoto wa kike na wa kiume, halafu uangalie huyu mtoto wa kiume jinsi ambavyo sasa ameachwa na baadae tutakuwa na Taifa ambalo sijui litakuwa na muunganiko wa namna gani? Kwa sababu tu ukisema unajenga mabweni utasikia watoto wa kike, ukisema sijui unataka kufanya nini watoto wa kike. Sasa watoto wa kiume inatokea hata mchango wao sijui tunaandaa nini?

Mheshimiwa Spika, kwa mila na desturi za kwetu na kwa dini zetu zote haitaondoa hata siku moja kwamba mtoto wa kiume ni kichwa cha familia. Sasa sijui tunandaa hiki kichwa cha familia baadae kitakuwa kichwa cha namna gani? Kwa sababu tutafika mahala tutakuwa na watoto wa kiume ambao ni useless kwenye jamii. Angalia matokeo kama ya panya road sasa hivi, matokeo mengine yote yanaonesha kabisa watoto wa kiume, hakuna watu panya road watoto wa kike hawapo, ni watoto wa kiume kwa sababu wamesahaulika na jamii na mtazamo kiasi kwamba sasa tunatengeneza bomu kubwa sana.

Mheshimkiwa Spika, mimi nataka niitake Serikali ije sasa na mkakati maalum wa kumrudia mtoto wa kiume iliko muacha, kwa sababu tunakoenda tunakwenda mahali pa hatari sana, tumemuacha mtoto wa kiume na dunia hii haiwezi kukamilika bila wanaume, haiwezi hata siku moja, yaani itafika mahala tutaanza kuwatafuta wanaume mahala waliko, hawana uwezo wa kuzalisha kwa sababu wameishashughulikiwa vya kutosha, kwa sababu wameachwa na tutafika mahala tutakuwa sijui tuna Taifa la aina gani.

Mheshimiwa Spika, niitake Serikali sasa ikumbuke kwamba hili ni bomu tunalitengeneza na si la utani na matokeo yake tumeishaanza kuyaona, wala hayana muda mrefu yata-backfire kabisa. Kwa hiyo mimi nafikiri sasa tukae kama wazazi…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mtinga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mchangiaji kwamba inawezekana ana hoja anaijenga, lakini kiuhalisia mtoto wa kike alikuwa ameachwa mbali sana, alikuwa katika marginal group hata ukiangalia makazini ratio ya wanaume kwa wanawake bado ni ndogo sana. Hata ukiangalia composition ya Mawaziri huku ndani wanaume kwa wanawake, Mawazari wako wengi sana, popote pale utakapoenda.

Kwa hiyo, nilikuwa tu nataka nimpe taarifa kwamba bado watoto wakiume hawajafikia kiwango cha kuwa kama ni vulnerable kama unavyosema. Bado mtoto wa kike anatakiwa apewe kipaumbele ndiyo maana Serikali inawekeza hata kwenye mashule na kwingineko kuweza kumnyanyua huyu mtoto wa kike sasa ambaye pia ni victim katika mambo mengi mengi hata ukatili ambao tunazungumzia humu ndani. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Francis unaipokea taarifa hiyo? Mheshimiwa Francis Mtinga.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, huyu ni mate wangu tumesoma naye. Taarifa yake naipokea lakini mimi sijasema watoto wa kike hawana umuhimu; wana umuhimu mkubwa na ndiyo maana wanaongoza nchi leo na inaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachosema tumewasahau watoto wa kiume, tunatengeneza bomu la hatari, tutakapokuja kuwarudia hatutaweza, leo tumeweza kumchukua mtoto wa kike kwa sababu aliachwa, tumemfikisha hapa tulipofika, lakini jinsi tunavyomuacha mtoto wa kiume nyuma tutakapo mrudia hatutaweza ni bomu ambalo ni baya.

Mheshimiwa Spika, kwa mtoto wa kiume madhara ni makubwa, ameongelea ubakaji sasa watoto wa kiume wanalatiwa, sasa tunafika mahala…

SPIKA: Mheshimiwa Mtinga, hebu tuelewane kidogo hapo; ukiwa na watoto wawili mmoja wa kike, mmoja wa kiume kwa hali ilivyo sasa hivi utamlipia ada yupi kati ya hao wawili? (Makofi)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, mimi kama baba nitalipia watoto wangu wote ada.

SPIKA: Haya huyo ni wewe; mzazi wako wa kizazi chake ulipokuwepo wewe mtoto wa kiume na mtoto wakike alikuwa anamlipia ada yupi? (Makofi)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, historia inaonesha kwamba mtoto wa kike aliachwa nyuma, mimi sijakataa, na tumefanya juhudi kubwa kama Taifa kumkomboa mtoto wa kike na tumefanikiwa kiasi kikubwa. Nachofanya naikumbusha jamii...

SPIKA: Sawa sasa, ngoja tunaenda taratibu, ngoja kwanza.

Hoja yako ni nzuri na ni nzito, nataka ufike mahali unaposema kwa kumtazama mtoto wa kike mtoto, huyu mtoto wa kiume anaachwa nyuma wakati huyu wa kike mpaka sasa hivi kitakwimu yupo nyuma, anajaribu kusogezwa alipo huyu wa kiume na siyo kwamba wa kiume kaachwa, huyu msichana ameshampita huyo wa kiume halafu bado wa kiume kaachwa. Ni kwamba wa kike anasogezwa pale alipo wa kiume sasa, kama unazo takwimu tutaenda kwa takwimu, lakini aliyekupa taarifa hapa naye kaja na takwimu angalia hata humu ndani Wabunge wanawake wako wangapi humu ndani asilimia yao? (Makofi)

Wabunge wanaume humu ndani mko asilimia ngapi? Kwa hiyo, hoja yako ni nzito, lakini ujumbe unaoutuma ni kana kwamba mtoto wa kike ameshamkuta huyu mtoto wa kiume, ameshampita mtoto wa kiume, ameachwa wa kiume nyuma, hapana. Mtoto wa kiume bado yuko mbele anavutwa wakike amkute wakiume ili waende wote pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mtinga dakika moja malizia mchango wako. (Makofi)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, mimi nafurahi jinsi ulivyomalizia umenielewa kwamba mtoto wa kike tumemfikisha mahala pazuri na tutaendelea, lakini watoto wa kiume tusiwaache nyuma kwa sababu tunatengeneza bomu ambalo litakuja kutushinda. Kwa hiyo nakushukuru. (Makofi)

SPIKA: Sawa.

Mheshimiwa Mtinga nilikupa dakika moja na haya makofi lazima ujue yanaonesha wingi wa wanaume humu ndani, ndiyo yanaonesha wingi wa wanaume humu ndani kwa sababu hakuna namna wanawake watapiga makofi yafikie ya wanaume. (Makofi)

Haya sekunde thelathini malizia mchango wako (Makofi)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba nimalize hoja yangu kwa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote hasa wanawake, wabebe nafasi ya uzazi zaidi tusiwe feminist, tukumbuke katika uzazi tunawatoto wa kike na wa kiume wote wanahitaji huduma ya jamii na huduma ya familia, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara ambayo tumezoea kusema uti wa mgongo lakini leo Mwijage ameongeza ni Bajeti ya Taifa, kwa sababu tunagusa wananchi wa Tanzania kwa asilimia kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niwape pongezi Mawaziri, Waziri wa Wizara hii na Naibu Waziri wake, hawa vijana mimi nawafahamu akili ya Mheshimiwa Bashe naijua vizuri, mimi nilikuwa bosi wake nikiwa Katibu Mkuu wa Vijana, ana akili nyingi sana hapa ametumia robo tu. Kwa hiyo, nina hakika kama bajeti yake hii itatekelezwa yote tutafika mahali tutaongeza fedha nyingi zaidi kwa jinsi ambavyo wanaupiga mwingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mwanasheria Antony pia namfahamu, kwa kweli Mama amechagua vijana hawa ili baadaye tuwe na model, kwamba vijana wakipewa nchi au wakipewa kazi wanaweza kuifanya. Nami sina wasiwasi kabisa na ninyi vijana wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitagusa kwenye jambo ambalo linagusa sana Jimbo langu pia linagusa nchi kwa maana ya mbegu za mafuta ya kula na hususan alizeti. Tunalo tatizo kubwa la mafuta, tunalo ombwe kubwa la mafuta na tunaagiza nje ya nchi wakati sisi ni nchi ya wakulima. Katika kulima mbegu hizi Mkoa wa Singida na hususan Jimbo la Mkalama ndiyo uti wa mgongo haswa wa kulima zao la alizeti. Kwa hivyo, ninakuomba Waziri jambo ambalo ulilianza mwaka jana la kutoa mbegu kwa mkopo lilikuwa ni jambo zuri, katika bajeti yako umesema tena kwamba utatoa mbegu lakini ningeomba sasa niseme machache ambayo yalikuwa ni kasoro kidogo kwenye ugawaji wa mbegu zilizopita ili mbegu hizi utakazogawa sasa ifanyike kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni aina ya mbegu, wananchi walitegemea sana wapate Highsun, tunajua kwamba Highsun ni mbegu inayotoka nje ya nchi, umesema kwamba ASA watatutengenezea mbegu zetu wenyewe lakini ni process ambayo mbegu zitachukua muda kidogo, kama itakuwa bado katika msimu huu, ninaomba mbegu utakazoleta highsun iwepo kwa sababu wananchi wanahitaji highsun ili waweze kuzalisha mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbegu iliyokuja pia wameitoa kasoro kidogo, inatoa matawi mengi kwenye mti mmoja wa alizeti na vichwa vinakuwa vidogo, kwa hiyo, wananchi wangu hasa wa Mkalama ambao ni wakulima wakubwa wa alizeti wamelalamika na hii mbegu. Kwa hiyo, ninakuomba sana katika zoezi linalofuata hili tulirekebishe mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ugawaji wa hizi mbegu, ulitoa mbegu vizuri ukatupeleka Mkoani lakini hamkutoa waraka mzuri jinsi gani mbegu hii igawiwe. Sehemu nyingine Maafisa Ugani wakawa wanasema lazima ulipie kwanza, sehemu nyingine wanasema ukopeshwe, kwa hiyo kukawa na mchanganyiko hapa, hii imesababisha mbegu nyingi imebaki kwa sababu hakukuwa na waraka mzuri ulioeleza jinsi gani mbegu hii igawiwe au ikopeshwe. Kwa hiyo, nikuombe katika mbegu zinazofuata sasa jambo hili uliangalie kwa umakini sana ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni miundombinu. Umesema hapa kutakuwa na miundombinu ya kutosha, ruzuku na kila kitu, lakini ndugu zangu kutegemea mvua, mbegu hii ambayo imegawiwa pamoja na kasoro zake lakini nyingi imepelea mvua. Kwa hivyo, kilimo cha kutegemea mvua hakitufai kwa sasa katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ardhi ya kutosha, mabonde ya kutosha, mfano mimi katika Jimbo langu la Mkalama ukienda Kata ya Mwangeza - Dominic pale kuna eneo wanalima vitunguu, wakipata bwawa wakichimbiwa visima pale wanaweza kuzalisha muda wote wa mwaka. Pia kuna scheme ya umwagiliaji pale Mwangeza imekufa muda mrefu ikifufuliwa ila katika hizo scheme ambazo umesema utaziweka naomba kabisa Mwangeza katika ufufuaji wa scheme usije ukaicha katika Jimbo langu la Mkalama. Hii itatusaidia sana kuhakikisha tunapata mbegu za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri block farming ulikuwa muumini wa hili jambo, ulipokuwa backbencher ndugu yangu Bashe, nikiwa mtaani kila ukisimama nilikuwa najua aidha utaongelea block farming ama utamuandama Makamu wa Rais sasa kuhusu kwenye mambo ya fedha akiwa Waziri wa Fedha, hizo zilikuwa ajenda zako. Sasa Mungu ni fundi kweli kweli alivyojua unasema sana mambo block farming akakupa Unaibu, lakini ukawa unasingizia huingii Baraza la Mawaziri, Mungu alivyofundi akakuongezea Uwaziri. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa usipoe Mheshimiwa Bashe ndugu yangu, block farming ndiyo itakuwa ukombozi. Umesema tu pale kutakuwa na block farming lakini kwenye alizeti hujasema vizuri. Mimi nikushauri kwamba angalau kila Kata katika nchi hii hasa kwenye Jimbo langu la Mkalama, kule kuna block farm ambayo wale Maafisa Ugani uliowapa nyenzo, uliowashonea na jezi na kila kitu anakuwa ofisi yake ni block farm iliyopo kwenye Kata. Wanaomiliki ile block farm wanakuwa vijana wa kike na kiume ndani ya Kata. Kwa hiyo, uta-solve mambo matatu hapa, kwanza utatengeneza ajira kwa vijana, pili utazalisha mbegu za uhakika na tatu utawapima vizuri Maafisa Ugani wako kwa sababu watakuwa na ofisi ndani ya Kata ambalo ni shamba kubwa la block farm. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, ninakuomba katika hizi block farm peleka kwenye Kata hasa hizi za alizeti hapo utakuwa umetusaidia sana katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile viwanda vyetu vya mafuta, viwanda vikubwa kama Mount Meru na viwanda vingine, hawana mashamba makubwa ya kulima wanategemea wakulima wadogo wadogo. Naomba ufanye kama yalivyo mashamba ya miwa kwenye viwanda vya sukari. Kiwanda kinakuwa kina shamba outgrowers wanajazia tu. Kwa hiyo, viwanda vikubwa wapewe hekta za kutosha hata 10,000, wapewe na waambiwe walime, kwa hiyo anakuwa na mbegu za kiwanda lakini wananchi wanakuja kujazia kwa hiyo viwanda vyetu vitafanya kazi throughout the year na hii itatusababisha sisi tuweze kupata mafuta ya kutosha na tuokoe fedha zetu hizi ambazo tunazipoteza nyingi sana fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naomba niunge mkono hoja lakini nitakuona kuhusu suala la masoko Mheshimiwa Waziri ili tuliweke vizuri, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu inayogusa maisha ya Watanzania, Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye hoja kwa sababu muda wangu ni mfupi, na ninataka nijikite sana kwenye suala la ugawaji wa maeneo ya kiutawala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imesimamisha muda mrefu sana suala la ugawaji wa maeneo ya kiutawala. Zipo Kata zetu ni kubwa mno kiasi kwamba wananchi wanapata taabu sana kufuata huduma. Nikitoa mfano, Kata yangu ya Mwangeza, kutoka mwanzo wa Kata mpaka mwisho wa Kata ni takribani kilomita 70. Kata kama hii yenye wananchi takribani 30,000 ina vijiji sita tu. Kutoka Kijiji mpaka Kijiji hakuna barabara. Mtu akitaka kwenda Kijiji kingine aje Makao Makuu ya Wilaya ndiyo aende Kijiji kingine. Kwa hiyo, wananchi wanapata taabu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sensa za mfano, kwenye Kitongoji kimoja tu, kwa mfano cha Gajaroda katika Kata hii kulikuwa kuna kaya 280. Kitongoji kama cha Msanga kaya 265, na Kitongoji cha Midibwi kaya 315. Unaweza ukaona kwamba hivi ni Vitongoji, maeneo mengine kaya 300, unaongelea Kata. Sasa tunapokuwa hatugawanyi maeneo, tunawatesa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia maeneo ya utawala ndipo wananchi wanakopata huduma. Sasa wapo wananchi kuna maeneo yao ni madogo tu, wana vijiji vya kutosha, wana mitaa ya kutosha, wana-enjoy hii nchi nzuri inayoongozwa na Mama Samia anayemwaga mambo huku. Sasa inapokuja kwenye Kata hizi kubwa ambazo hazigawanywi, wananchi wanapata taabu, hawafurahii maisha mazuri ya Watanzania. Kwa sababu mtu anasafiri umbali mrefu kufuata shule, kufuata hospitali na Mahakama; na hivi vitu viko kwenye maeneo ya kiutawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Wizara sasa ifuatilie maombi ambayo tumeshayatuma mengi, ambayo tumeyaleta mara nyingi, yanawekwa kapuni. Mfano, tumesema kata kama hii, tunataka tupate Kata ya Dominiki, tupate kata ya Endasiku na tupate Kata yenyewe ya Mwangeza kutoka kwenye Kata moja. Kata kubwa kama ya Ibaga, tunataka tupate Kata ya Ibaga na Kata ya Mkalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya tunayoongea kama ni Matawi ya Chama, tunaongelea matawi mpaka 15, au 20, tunapata shida. Kwa hiyo, namwomba Waziri suala hili alichukulie umuhimu mkubwa. Nimeamua nibaki kwenye eneo hili kwa muda mrefu kwa sababu tumekuwa tunalisema tu na kulipapasa, hebu tugawe maeneo ili wananchi wapate huduma nzuri ambayo Rais wetu anaitoa, kwa sababu bila kugawa maeneo, huduma hizi haziwafikii, wananchi wengine anateseka maporini kwa sababu Serikali iko mbali na maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa nataka niseme kuhusu uhaba wa watumishi. Naomba wakati Waziri ana-wind up atueleze, hivi ni kwa nini tunashindwa kujaza ma-gap ya wafanyakazi ambao tayari walikuwa kwenye bajeti? Wafanyakazi waliostaafu na waliotangulia mbele ya haki. Kwa sababu mtu anapostaafu, anastaafu katikati ya mwaka; au mtu anapofariki, kifo ni ghafla, tunaweza tukapitisha bajeti leo, mtumishi akafariki kesho; tayari yuko ndani ya bajeti. Kwa nini, tusitumie kanzidata kujaza yale ma- gap kwa sababu tayari wako kwenye bajeti, ili Rais anapotangaza ajira mpya ziwe ajira mpya kweli? Kwa sababu hizi ajira mpya zinaishia kujaza ma-gap tu ya wastaafu na watu waliofariki, matokeo yake hatuoni ajira mpya zinafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waziri atueleze, tatizo ni nini? Kama tumeshapitisha bajeti ya watumishi kwa mfano 1,000, wakafariki 50, si wajazwe wale 50 kwa sababu wako kwenye bajeti? Hii ikiendelea tutapunguza hili gap la watumishi, kwa sababu wastaafu wanastaafu kila siku. Watu wanatangulia mbele ya haki kila wakati, lakini nafasi zao wako kwenye bajeti hazijazwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuelezwe tatizo liko wapi? Kama tumeshapitisha bajeti, tutumie kanzidata, mtu aandikiwe tu barua, nenda karipoti mahali fulani. Interview zinafanyika kila wakati, kwa hiyo, tunayo list ya watu wamesoma hawa, kuna walimu hawa, kuna manesi kuna madaktari, mtu anaandikiwa tu karipoti ujaze gap, ili hizi mpya zinapotoka ziwe mpya kweli. Hizi ajira tunasema mpya, siyo mpya hizi, kwa sababu ma-gap yamejaa kote huko. Kwa hiyo, hakuna cha ajira mpya, ndio maana tatizo hili halipungui kwa sababu hiyo. Kwa hiyo, naomba kabisa Waziri akija, aliambie Bunge hili, kwa nini hatujazi ma-gap wakati watumishi tunao na bajeti tunakuwa tumeipitisha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la watoto wetu kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu. Tatizo hili ni kubwa. Leo ukienda kwenye shule za msingi unaweza ukakuta zaidi ya watoto hata nusu, hata robo tatu au robo darasa, hawajui kusoma na kuandika. Hili tatizo halisababishwi na watoto. Watanzania hatuna watoto wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika. Haya yanasababishwa na matatizo mengine ambayo pengine sisi hatujayapa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo mojawapo kubwa kabisa ni la utoro; watoto kukosa chakula cha mchana shuleni. Watoto kama hivi hatugawanyi maeneo, wanakaa mbali. Mtoto anasafiri kilometa sita mpaka saba au 10, anaenda shuleni hajala; anafika anakaa shuleni muda wote hajala. Kwa hiyo, naomba hili tatizo la kutokuwapa watoto chakula kutoka shuleni, Wizara iliangalie upya.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mtoa taarifa, yuko wapi? Mheshimiwa Amar.

TAARIFA

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, KKK inasababishwa na upungufu wa waalimu na pia tatizo hilo la chakula. Nilikuwa nataka nimpe tu taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Isack unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine walishachangia, naomba unilinde muda wangu hata dakika moja nimalizie.

MWENYEKITI: Malizia dakika moja basi.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, tungeweza kupata chakula shuleni pia kupitia kuwafundisha watoto wetu somo la EK ambalo limefutwa. Shule zetu zina maeneo makubwa ya kulima, lakini watoto wetu tumeacha kuwafundisha EK, kwa hiyo, tukirudisha lile somo tukawafundisha watoto wetu jinsi ya kulima vizuri kisasa ili wakitoka wakasaidie jamii, watapata chakula na wazazi tukichangia kiasi kidogo kilichobaki watoto wetu wapate chakula shuleni, tuondoe hili suala la kutokujua kusoma, kuandika na kuhesabu. Linatutia aibu nchi yetu na Mama yetu anamwaga fedha huko kwa ili ya watoto wasome lakini watoto wetu wanakuwa hawajui kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu sana ambayo inashikilia maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kupongeza Wizara hii na hasa Waziri na Naibu kwa kutupatia mradi mkubwa sana wa skimu ya umwagiliaji ya Bwawa la Msingi takribani bilioni 34 kwenye Mto Ndurumo ambao umekuwa ukitusumbua sana. Bado tuna bonde lingine katika Kata ya Mtambala ambalo ni Mradi wa Tatazi, bonde kubwa kabisa katika mto huu pia utume wataalamu wako; na kule Ilamoto Kata ya Mwangeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo nataka nijikite kwenye zao la kimkakati, zao la mkonge. Tanzania imebarikiwa kuwa na zao la asili kabisa la mkonge, zao ambalo linastawi katika Mikoa ya Tanga, Morogoro na Kanda ya Ziwa. Sisi wa Kanda ya Kati tulikuwa tunatumia zao hili kuweka mipaka tu kwenye mashamba, lakini kupitia hiyohiyo mipaka tumevuna kiasi kwamba sasa wananchi wa Kata za Kokinda, iyunda wameanza kulima zao hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya 1964 zao hili lilikuwa linatoa karibuni tani 230,000 na lilikuwa linachangia asilimia 65 ya fedha za kigeni. Miaka ya 1997 lilishuka mpaka kufikia tani 19,000. Mwaka 2019 Serikali iliingilia kati na kulitangaza kuwa zao la kimkakati, na uhamasishaji ulifanyika wa kutosha na angalau 2022 uzalishaji ulifikia tani 48.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu za 2022 sekta ya mkonge imeajiri wafanyakazi takribani 475,302 kuanzia mashambani mpaka viwandani na hawa ni wafanyakazi rasmi wenye mikataba, achana na vibarua. Lakini pamoja na faida kubwa ya zao hili, kwa maana ya ajira katika nchi hii lakini vilevile fedha za kigeni zao hili ilakabwa koo na nyuzi za plastiki zinazoingizwa katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya 1970 mpaka 1990 zao hili liliuawa na nyuzi za plastiki. Serikali imeanza mkakati wa kupandisha lakini inaacha tena nuzi hizi za plastiki zinaingia nchini na sasa tunataka kwenda kulia tena zao ambalo wananchi wameshaanza kupata fedha na ajira inapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliahidi, takribani miezi nane iliyopita, kwamba itakuja na kanuni ya kuzuia matumizi ya nyuzi za plastiki kwenye vifungashio vya vyakula lakini mpaka sasa miezi nane imepita kanuni hakuna, wala katazo hakuna na nyuzi za plastiki zinaendelea kuingia katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano tu, Kiwanda cha 21 Century Holding Limited, kiwanda cha kamba kimefungwa ambacho kilikuwa na wafanyakazi 300, Kiwanda cha TPM 1998 Limited kiwanda kipo Morogoro, kimesimamisha line ya nyuzi za mkonge, kilikuwa kina wafanyakazi takribani 1,000, Highland Spinning Milling - Mdaula nacho kilifungwa, kilikuwa kina zaidi ya wafanyakazi 180, takribani wafanyakazi 1,480 wameachishwa kazi wakati tunatafuta ajira milioni nane, kwa sababu tu ya nyuzi za plastiki ambazo zinaingizwa nchini. Viwanda kama vitatu tu ndivyo vimebaki, na vinafanya kazi chini ya kiwango kwa sababu ya ukosefu wa soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, soko la ndani la kamba za mkonge ni la muhimu sana kwa sababu ambazo nimeshazitaja; kwanza ajira, lakini fedha za kigeni na hata utunzaji wa mazingira kwa kuondoa hizo nyuzi za plastiki, lakini bado halijaangaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Serikali ije sasa na hizo kanuni kwa haraka za kupiga marufuku matumizi ya nyuzi za plastiki kwenye vifungashio vya vyakula. Aidha, nimuombe Waziri, kwa sababu Serikali inaongea, wawasiliane na mwenzake wa mazingira, watekeleze haraka agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu alilolitoa Septemba 21 na kurudia tena agizo hilo hilo Novemba, 2021 alipotembelea Kiwanda cha Kamba cha Mkonge cha Sisilana la kumtaka Mheshimiwa Waziri Jafo akamilishe andiko lake la kikanuni la kuzuia Kamba za plastiki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninyi ni Serikali ongeeni ili agizo hili kubwa ambalo linaokoa maslahi ya nchi litekelezwe haraka kuokoa zao hili ambalo ni la ajira, zao la mkakati na zao muhimu sana kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kulinda maslahi ya mnyororo wa zao hili naiomba Serikali ichukulie umuhimu zao hili. Halmashauri zetu zinapata cess kubwa sana kupitia zao hili kwa maeneo ambayo wanalima mkonge, lakini sasa tunaacha wenyewe kitu ambacho kinatusaidia kwa ajira, kitu kinatusaidia kwa forex halafu tunamaliza kwa nyuzi za plastiki ambazo hazina faida yeyote; na si ajabu hata kodi sizani kama inalipa kuingiza nyuzi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyuzi hizi zinaingia kwa ajili ya nyavu, ziende huko kwenye nyavu. Kwa hiyo, ningeomba kabisa agizo liwe kali, kamba za mkonge zitengeneze vifungashio na soko la nje liwe ziada, soko la ndani pekee yake bado linaweza kulinda zao hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimebaki kwenye eneo hili kwa nguvu sana kwa sababu nataka kuokoa ajira za vijana wa Tanzania na tuendelee kuokoa tatizo la forex katika nchi hii. Zao hili ni la asili lilikufa, limeinuliwa na sasa tunataka kuliua tena. Serikali naomba waongee ili waweze kuhakikisha kwamba wanakuja na kanuni ya kuokoa zao hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize tena, kwa kumwomba Mheshimiwa Waziri…

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba control ya nyuzi za plastic sio tu kwa sababu ya kushindwa ku- control zinazoingia lakini hata wazalishaji wa ndani Serikali yenyewe bado haiwatambui. Mpaka tarehe 24 Aprili, ndio kwanza NEMC imetoa tangazo la kuwaambia wakajisajili.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtinga.

MHE. FRANCIS MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, napokea taarifa hiyo. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri ametupa bwawa kubwa la skimu ya umwagiliaji, lakini kuna Bonde kubwa la Dominiki linalima vitunguu. Hatuna sehemu ya kutega maji, lakini nina hakika katika mipango yake anaweza akachimba visima vikubwa na vitunguu vikalimwa katika bonde hili, nimwombe sana Waziri katika hili. Vilevile pale Mwangeza kuna skimu nyingine ambayo ilikuwa ya ASPD II zile zilizopita, ilikufa naomba tena Waziri apeleke wataalam wake waweze kufufua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mkalama inaweza kulisha Kanda ya Kati yote mpaka Magharibi katika zao la chakula, mahindi na mpunga na mabonde haya yapo. Namshukuru sana sasa ameamua kuwawezesha vijana wa Kitanzania kuwa matajiri hivyo na vijana wangu wa Mkalama wawe matajiri kwa kufufua mabonde haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ambayo ni uhai wa Watanzania, kwa sababu wote tunajua kwamba maji ni uhai. Naomba nianze kwa kumshukuru sana Waziri kwa jinsi ambavyo amekuwa akifanya kazi vizuri yeye na timu yake kazi ya kuwasikiliza Watanzania na kuwapelekea maji kama ambavyo Rais wetu amemuagiza.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia watendaji wake katika ngazi ya Mkoa. Namshukuru sana Meneja wa RUWASA wa Mkoa wa Singida ni mtu rahimu sana, anasikiliza watu na hivyo wananchi wa Mkoa wa Singida wanampenda sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha nimpe tena salamu Mheshimiwa Waziri kutoka Wananchi wa Mkalama uliwahamishia Meneja wao Engineer Mchunguzi. Wamenituma mimi ndiyo msemaji wao wanamuhitaji meneja wao arudi kwa sababu wana jambo lao. Kwa sababu anawasikiliza vizuri wangekuwa tayari sana kama angekuwa amepandishwa cheo wangemuacha aende lakini kwa sababu ameamishwa anaendelea kuwa Meneja kama alivyokuwa Mkalama na mimi kwa sababu ni msemaji Madiwani, Chama cha Mapinduzi na wananchi walimwambia mpaka Katibu Mkuu wa Chama kwamba wanamtaka Menejaager Mchunguzi arudi. Kwa hiyo, nimefikisha hili nijivue kwamba wanamuhitaji meneja wao Engineer Mchunguzi kwa sababu walimuelewa anafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi hatuna shaka hatujui aliyekuja lakini wenyewe wanamtaka wakwao waendelee nae. Kwa hiyo, nimeona hilo nikwambie ulijue na najua DG wa RUWASA yupo nilimpigia simu akanihaidi lakini mpaka sasa haijatekelezwa kwa hiyo nimeona niifikishe.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nikushukuru kwamba umeendelea kutupatia pesa, umetupatia milioni 165 kumalizia mradi wa maji pale Nkalakala tunakushukuru sana, umetupatia milioni 240 kumalizia mradi wa maji pale Maraja tunakushukuru sana. Vilevile nikushukuru nimekusumbua sana ukanipatia milioni 208 kuanza mradi pale Mbigigi wakati naingia Ubunge nilikuta umefanyika upembuzi wa kina na yalipoanza kujengwa maji kule kwenye kijiji nilikozaliwa wakadhani nimehamisha hela za Mbigigi. Kwa hiyo, nakushukuru sana umezileta milioni 208 na sasa mkandarasi anakwenda kukabidhiwa kazi kwa ajili ya mradi ule nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika bajeti hii umetupitishia shilingi milioni 208 bajeti hii itakapopita kwa ajili ya kwenda kupeleka maji katika kijiji cha Matongo na Isene watu hao wamepata shida sana ya maji kwa kutumia chanzo cha Isene sasa tutajenga mradi wa tank pale umetushia milioni 208 na itahudumia vijiji viwili nikushukuru sana kwa ajili ya hilo.

Mheshimiwa Spika vilevile umetupitishia milioni 300 kwenda kujenda miundombinu na umaliziaji katika jiji cha msingi kata ya Msingi nakushukuru sana wewe ni mtu rahimu sana. Vilevile umetupitishia milioni 378 kwa ajili ya kupanua mradi wa maji wa Tumuli ambao umeishajengwa sasa kwenda kuongeza vituo na ile kata nzima iweze kupata maji safi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haikutosha Mheshimiwa Waziri wewe ni mtu wa Mungu sana umetupitishia milioni 396 kwa ajili ya kwenda kuchimba visima kwenye vijiji vya Domoniki, Nkinto, Ilunda, Kitundili, Kisulwiga, Mwangeza, Kibii, Gumanga, Asanja na Lugongo yote hii umetupitishia katika bajeti hii na hakika bajeti hii itapita nikuombe Mheshimiwa Waziri mara tu baada ya kumaliza Bunge na tukapitisha finance bill hela hizi zianze kumwagika wananchi wa maeneo haya wameyasuburi maji haya kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri tu kidogo mradi ambao umeishafanyiwa upembuzi wa kina wa kutoa maji Ziwa Victoria na kuleta Dodoma. Mradi huu utapita kwenye Jimbo langu na ukishafika kijiji cha Kisana pale Mheshimiwa Dkt. Mwigulu mradi ule unakuja kwa gravity mpaka Dodoma kwa hiyo, ni economical sana. Kwa hiyo, nikuombe huu mradi msiuweke kapuni, mradi huu uendelee najua kwa sababu utapiata kwenye jimbo langu hakika sisi wa Mkalama tutaogelea maji cha ajili ya mradi huu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naupigia debe na kukumbusha kwa sababu upembuzi umeishafanyika na ni economical unatembea kwa gravity kuanzia Singida mpaka hapa hebu mradi hii uangalie ili tupate chanzo cha uhakika cha maji ambacho na hakika sasa wananchi wa Tanzania kama mama ambavyo anaendelea kututua ndoo tunakwenda kula matunda ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo alihaidi kumtua mama ndoo na anaendelea kumtua mimi nimuombee tu Rais wangu maisha marefu mpaka ifike hiyo 2030 na hakika nchi hii sasa itakuwa iko katika hali ambayo inategemewa kuwa kwa jinsi ambavyo tuna neema nzuri katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Singada na wananchi wa Tanzania tunacho muombea hicho kura zitamwagika, kwa sababu hatuna shaka ndiyo maana tunaongelea mpaka 2030 kwa sababu ndiyo mama yetu ambaye anatulea na Mungu ametubariki kupata viongozi wa namna hii ni bahati siyo wengi kama ambavyo wanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia muda nikushukuru sana siyo kwamba sio muhimu lakini umekuwa Spika wa viwango mpenda haki, Spika ambaye tukiwa humu ndani tunajisikia tuko sawa form one, form two, na hata waliyo form three wote tunajiona tuna haki. Kwa sababu ya uongozi wako na weledi wako mzuri Mungu akubariki akutie nguvu ili tuendelee ku–enjoy katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ahsante sana.

SPIKA: Ahsante sana.

MBUNGE FULANI: Unga mkono hoja.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ambayo inaunganisha nchi na inaunganisha uchumi. Naomba nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Rais wetu kwa jinsi ambayo amekuwa akiitendea haki Wizara hii ambayo ina miradi mikubwa yenye fedha nyingi na imeendelea bila kusimama na muda siyo mrefu nchi yetu itakuwa ipo katika hali ya juu sana katika miundombinu katika Afrika. Nimpongeze sana mtendaji wake mkubwa ambaye ni Waziri kwa jinsi ambavyo wanaitendea haki Wizara yao, wanafanya kazi vizuri na kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru pia Waziri, katika siku chache zilizopita amenikumbuka na mimi katika jimbo langu, amekubali tena kwa moyo mweupe katika bajeti hii kwamba atanipatia kilometa kumi za lami pamoja na taa katika Mji wangu wa Nduguti pale Wilaya mpya, katika barabara ambayo inatoka Iguguno kuelekea Bariadi mpaka Simiyu kupitia Sibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na kunipa hii, basi mipango yake ya kuhakikisha anaunganisha barabara hii kutoka Iguguno mpaka Simiyu asiiache mbali, kwa sababu ni barabara ya kiuchumi, kiasi kikubwa cha pamba kinachotoka Mkoa wa Mara, Mkoa wa Simiyu wanapita barabara hii na wanakuwa wameokoa kilomita nyingi sana badala ya kuzungukia Mwanza mpaka Shinyanga. Kwa hiyo, naomba ahakikishe barabara hii inaunganika ili wananchi wangu wa Mkalama na wa Mkoa wa Mara na Bariadi waweze kuunganishwa na nchi kirahisi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, reli yetu inayotoka Manyoni kwenda Singida, kipande hiki kimesahaulika. Sehemu kubwa ya reli ya zamani imekarabatiwa na inafanya kazi. Mpaka leo kwenda kaskazini kule, watu wanaenda kwa treni, lakini kipande hiki muhimu sana kilichojengwa tangu enzi ya mkoloni kimesahaulika. Hii reli ni muhimu sana inaweza kuwa feeder road ya kupeleka mizigo kwenye SGR pale Manyoni. Kwa hiyo, nakuomba sana katika bajeti za ukarabati wa reli, kipande cha reli cha kutoka Manyoni kwenda Singida…

MHE. ELIBARIKI I. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Taarifa.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji, kaka yangu Mheshimiwa Francis kwamba, siyo tu reli hii imesahaulika, bali Wana-Singida wanatamani kuona kipande cha SGR kinatoka Manyoni na kufika Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa mchangiaji taarifa kwamba vitunguu vyote wanavyokula mikoa karibu ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam, viazi vyote wanavyokula mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam, vinatoka Singida. Kwa hiyo, kwa kuikumbuka reli hii, itakuwa imeleta ukombozi mkubwa sana kwa mikoa hii mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa mchangiaji taarifa hii.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Francis, taarifa.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii kwa mikono miwili. Rafiki yangu Mheshimiwa Kingu amesahau, na kuku wote wa kienyeji katika nchi hii wanatoka njia hiyo. Kwa hiyo, kipande hiki ni cha muhimu. Hata ng’ombe, barabara zinaharibika kwa kupakia ng’ombe. Kwa hiyo, wakija na reli itakuwa ni vizuri. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, kipande hiki mkikumbuke, kinajenga uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tena nimwombe Mheshimiwa Waziri, katika reli yetu ya SGR, huduma karibu zitaanza. Nawaomba sana, wananchi wameisubiri reli hii kwa hamu kwamba huduma ya usafiri sasa itakuwa ni nyepesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata hofu kidogo, niliona uwezekano wa nauli zitakabvyokuwa, watu wa chini naona kama watakuwa wanapata shida. Naomba sana, ziwepo category zote za nauli. Starehe ya juu kabisa tunaotaka kulipa mamilioni sijui malaki, ziwepo; wale wa uwezo wa kati iwepo, vile vile ziwepo madaraja ya chini kabisa ambayo wananchi wanaweza wakapanda, wakatumia. Wote kwa pamoja kwa uwezo wetu tuweze kutumia reli hii ya SGR itakapoanza kufanya huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jamii huduma zote zipo. Leo hii wako akina dada wanaovaa wigi la bei ndogo, lakini wapo wanaovaa wigi la Shlingi laki tano. Leo hii wapo watu wanavaa suti za mtumba na wengine wanavaa suti ya mamilioni, ili mradi ipo, wewe utaenda kwa uwezo wako. Kwa hiyo, naomba katika SGR, yale mabehewa yatakapoanza kufanya kazi, ziwepo nauli za bei ya chini, wananchi wa kawaida wapande; ya kati na ya juu yenye starehe zote iwepo, ili mtu apande kutokana na uwezo wake. Isije wananchi wetu wa hali ya chini wakawa wanaangalia tu treni ya SGR inakwenda kwa kasi, wanaiona kwa macho, wao wanahangaika na usafiri wa kutumia saa nyingi kufika maeneo ambayo wanataka kwenda. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hili waliangalie sana huduma itakapoweza kuanza wakati huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo namwomba Mheshimiwa waziri, nashukuru kwamba barabara nyingi zinajengwa, lakini mpaka sasa nasikitika, bado kila barabara kubwa ukiiona, utaona wakandarasi ni Wachina, Wazungu ama vyovyote. Wakandarasi wetu wa ndani bado hawajapata kazi kubwa. Najua kitakachosemwa kikubwa ni mtaji. Hebu niombe kama Wizara, tuangalie namna ya kuwaunganisha Wakandarasi wetu wa ndani, ili waweze kuchukua kazi kubwa ili nasi fedha zetu za kigeni na uchumi wetu uweze kubaki ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba kwenye kilimo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Francis Mtinga.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nilikuwa naomba tu nimalizie kwamba nashukuru pale kwenye bwawa langu la msingi, mradi wa Shilingi bilioni 34 wamepewa Wakandarasi wazawa. Kwa hiyo, hata kwenye barabara kubwa kubwa wakipewa wazalendo tutaendelea kujenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ambayo ni mwanga wa nchi na uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu, maneno hayatoshi jinsi gani ya kumpongeza Rais kwa jinsi ambavyo ameamua kweli kututumikia Watanzania na kututoa hapa tulipo kutufikisha kwenye nchi ambayo ni ya asali na maziwa, kikubwa cha kumuombea ni uzima na afya njema ili malengo yake haya yatimie ya kuifanya nchi hii kuwa nchi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze Waziri na Naibu wake, vijana hawa wanamtendea Mama haki kwa sababu wanafanya kazi ile ambayo Mama anaitaka kwa weledi na kwa upendo na kwa uhakika mkubwa, ninawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, kichwa chako kimetulia mimi nakufahamu vizuri ni kichwa ambacho kinaweza kufanya mambo makubwa katika nchi hii. Nikutie moyo fanya kazi, sisi tuko nyuma yako tunakuamini na tutaendelea kukupa ushirikiano wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda leo mchango wangu ujikite sana TANESCO na TANESCO nataka niende kwenye suala la bei za umeme. TANESCO inafanya biashara ya umeme kwenye tariff lakini pia sehemu ndogo mimi ninaiita ndogo kwenye kuunganisha umeme. Kuunganisha umeme kwa shilingi 320,000 ni sehemu ambayo TANESCO inategemea iingize mapato, lakini watu wanaoweka umeme kwa shilingi 320,000 ambao ni watu wa mijini, rate yao ya kuweka umeme ni ndogo sana, kwa sababu ya gharama hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi ambacho ilitangazwa kwamba umeme uwekwe kwa shilingi 27,000 nchi nzima maombi ya kuweka umeme yalijaa TANESCO mpaka wakashindwa kufanya kazi lakini watu hawa ambao walipeleka maombi mengi ni watu wa mjini ambao wana matumizi makubwa ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona hii ni fursa ambayo tumeiacha, ni bora tungetumia gharama ya kuhakikisha tunaweka umeme kwa shilingi 27,000 lakini baada ya muda mfupi watu hawa wote wanatumia umeme na TANESCO wataingiza umeme kwa tariff kwa sababu watu wa mjini wana matumizi makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaweza kupeleka umeme zaidi ya kilometa 200 kutoka kijiji kimoja kwenda kijiji kingine na tunafika kwenye kijiji kile kaya zitakazoweka umeme ni kaya labda 10,15 mpaka 20, kama Serikali hii inakubali hiyo gharama ya kupeleka huduma hiyo kwa wananchi tunaachaje kumuwekea mwananchi wa mjini umeme kwa shilingi 27,000 ambaye nguzo moja, kuna maeneo ambayo nguzo moja ya umeme inaweza kubeba mpaka mita 10,15 nguzo moja. Sasa hiyo nguzo moja kwa shilingi 27,000 ikabeba nyumba 15 maana yake watu hao wa mjini ndiyo wenye friji, ndiyo wenye nini matumizi ni makubwa na TANESCO itaingiza fedha nyingi sana kupitia tariff za hawa watu kuliko kuwawekea shilingi 320,000 halafu hawavuti umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunakusanya property tax kubwa sana nchi hii kupitia mita za umeme. Leo hata mtu aliyeko kijijini mwenye nyumba ya tembe akivuta tu umeme atalipa shilingi 12,000 kwa mwaka ya property tax kwa sababu atalipa shilingi elfu moja moja kwenye mita kila mwezi. Kwa nini tusitumie hii fursa ya kukusanya property tax kubwa kwa kuhakikisha watu wengi wanavuta umeme na ili watu wengi wavute umeme maana yake tukifanya shilingi 27,000 watu wote watavuta umeme. TANESCO watafanya kazi masaa 24 ili kuweza kuweka haya maombi yaweze kutimia kwa sababu watu wote wa mijini wataweka umeme na matokeo yake ni kwamba property tax itakuwa kubwa kwa sababu watu wote hawa watakuwa wanatozwa shilingi 12,000 kwenye mita zao kwa mwaka kwa hiyo mapato ya Serikali yataongezeka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tena katika hili ina maana hata tunaweza tukaweka asilimia kidogo ya hii property tax ikaenda REA kwa sababu REA wanaongeza watu wa kutumia umeme matokeo yake wanaongeza property tax kuwa kubwa, maana yake kama tukichukua hata percent tatu tu kwenye ile property tax ikaenda REA maana yake tayari tutakuwa tumeipa REA uwezo mkubwa zaidi wa kuongeza watumiaji wa umeme kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano hii inayoenda kwenye vitongoji maana yake vitongoji vitakwenda vingi kwa wakati mmoja kama REA ina pesa na kadri wanavyoingia maana yake property tax inaongezeka, mapato ya Serikali yanaongezeka. Hii ni win win situation ambayo ningeomba hii property tax angalau ipelekwe asilimia chache ziende REA ili mita nyingi ziongezwe kwa shilingi 27,000. Nyumba ni nyingi mjini tuko wengi milioni 61 na nyumba ni nyingi hii ni fursa ya kukusanya mapato ambayo tunaiacha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri na TANESCO mkae muangalie hili suala la shilingi 27,000 liende nchi nzima ili watu waweke umeme wa kutosha tutapata mapato ya kutosha kwa TANESCO na tutapata mapato ya kutosha kwenye Serikali kupitia property tax. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye shilingi 27,000 kwa mfano mimi katika Jimbo langu, Iguguno ni kijiji, Nduguti ni kijiji, Makao Makuu ya Wilaya waliangalia geographical position hawajaangalia kwamba uchumi au wakaangalia kwamba sijui wana nyumba nyingi Hapana! Walichoangalia ni kwamba Nduguti ni katikati ya Wilaya ya Mkalama, hapa ndiyo patakuwa makao makuu lakini ni kijiji. Iguguno ni kijiji maisha ya wananchi ni ya kawaida ya kijijini. Sasa unapomwambia alipe shilingi 320,000 kuweka umeme ni kama ni kumnyima umeme tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri wakati unalifikiria hili la kuweka nchi nzima shilingi 27,000 basi haya kwenye maeneo yetu ya vijijini kama Iguguno na Nduguti ianze mara moja shilingi 27,000 kwa sababu ni wanakijiji kama walivyo wanakijiji wengine ili kuweza kuvuta umeme katika maeneo haya. Kwa kuwaambia watu wa Nduguti, watu wa Iguguno wavute umeme kwa shilingi 320,000 ni kuwaambia wasitumie umeme jambo ambalo kwa kweli sidhani kama ni jambo jema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine hapo hapo kwenye hizi mita, TRA wanatumia kukusanya property tax kwa mita lakini sasa uzembe wao pia wanataka kukuponza Mheshimiwa Waziri. Wamekadiria vibaya nyumba zao. Kuna nyumba zinatakiwa zilipe zaidi ya shilingi 12,000 kwa mwaka. Matokeo yake hawakuwaambia mwanzoni wakakata shilingi elfu moja moja yakajilimbikiza madeni, leo wanashtuka wanakwenda kujaza kwenye mita madeni ya mwaka mzima, lawama zinakuja kwako Waziri, lawama zinaenda TANESCO kwa uzembe wa TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kushtuka kwa nini wasingeingiza hata kidogo kidogo kwa sababu wao wenyewe walikadiria hawakuingiza kwenye mita madeni yanavyotakiwa. Leo hii kuna watu wanakuja kukosa kununua umeme kwa sababu amewekewa deni la mwaka mzima ambalo siyo makosa yake ni uzembe wa TRA kwenye kuingiza. Leo inaingizwa kwenye mita wewe Mheshimiwa Waziri unaonekana wewe kwenye mita zako ndiyo kuna tatizo. Kaa nao TRA uzembe wao wasikuponze wewe kijana tunakujua ni kijana mwema, mchapakazi, uzembe wa TRA usiingizwe kwako Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tena hapo hapo, TANESCO wamekuja sasa wanakusanya madeni yao ya nyuma mengine ya miaka 20 iliyopita. Waliokuwa wanadaiwa wameshakufa wengine, hawa-exist. Leo hii wameshtuka sijui wapi linakusanywa deni mtu unashangaa kwenye mita unaambiwa unadaiwa shilingi 2,000,000, 1,500,000 mwananchi wa kawaida deni hujui lilikotoka. Nyumba zingine mtu alishafariki nyumba wanaishi wapangaji wengine hata hawajui kilichotoka unaambiwa mnatakiwa mlipe deni. Naomba Mheshimiwa Waziri hili jambo TANESCO mkae chini muangalie upya namna ya kukusanya madeni, kuna madeni mengine yanatakiwa yafe tu. Mtu miaka 20 mlikuwa wapi siku zote?

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Isack.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba nimalizie kwa kusema kwamba TANESCO hili jambo waliangalie vinginevyo itabidi watu wengine wako tayari kushtaki, wanaenda EWURA kushtaki kwa jambo ambalo linaweza kukaa chini na kuzungumzika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia angalau kidogo kwenye Bajeti hii ya Serikali. Naomba nianze kwa kumpongeza sana Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ya kumwakilisha Mama yetu ambaye anaitumikia nchi hii kwa moyo wa upendo na moyo wa kutujali Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze tu moja kwa moja kumwomba Mheshimiwa Waziri kaka yangu, najua mengi yameshaongelewa lakini katika Jimbo langu la Mkalama na Jimbo lake la Iramba Magharibi na Iramba Mashariki TRA wanafanya kazi kwa kuijbanza kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pale Jimboni kwake, Jimboni kwangu wamepanga vyumba viwili, hatuna watumishi, hatuna Meneja, sasa hii inatupa shida sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, angalau atenge hata kidogo, japo milioni 150 kila wilaya ili angalau tupate Ofisi ili tuweze kulipa kodi vizuri na wananchi wetu wasipate shida wakati yeye ndiye Waziri wa Fedha, charity begins at home hiyo haikwepeki. Akija kuondoka hapo hajajenga Ofisi tutakuwa tunamnyooshea vidole, tunamwomba atenge fedha ajenge Ofisi pale Mkalama na pale Iramba Magharibi na Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimshauri Mheshimiwa Waziri, suala la kukwepa kodi kwa kutokuchukua risiti limezidi sana. Pia, hii inasababishwa na jinsi sheria yenyewe ilivyo. Kuna Mbunge mmoja hapa alitoa wazo kuhusu kutoa commission kwa watu watakaotudai risiti, hilo ni wazo zuri. Nami nataka niongeze jambo moja, Waziri amefanya vizuri sana kwa kuongeza kiwango kwamba mpaka milioni 200 ndipo mtu ataingia VAT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hiki kiwango cha kutoka milioni nne mpaka kufikia hiyo milioni 200 hakina madaraja, yaani ikishafika tu milioni nne Kwenda 11, Afisa wa kodi ndio anakaa anaangalia asilimia 3.5 ya mauzo. Ina maana mtu mwenye milioni 200 anapaswa kulipa milioni saba. Hiki kiwango ni kikubwa mno kinasababisha watu wakwepe kodi. Naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, hiki kiwango cha kutoka milioni nne mpaka milioni 200 kiwe na madaraja ambayo yatasababisha watu watumie EFD machine bila wasiwasi kwa sababu anajua daraja langu ikifika kiasi fulani nitalipa kiasi fulani. Pia, naomba nimshauri Waziri kuhusu madaraja ambayo mimi naona nafaa kupendekeza na wataalamu wako wataona, yako kama saba hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuanzia milioni nne mpaka milioni 11 wafanyabiashara wakilipa 150,000 itatosha. Kuanzia milioni 12 mpaka milioni 20 walipe 450,000. Kuanzia milioni 21 mpaka milioni 50 walipe 650,000. Kuanzia mauzo ya milioni 51 mpaka milioni 75 walipe 850,000. Kuanzia mauzo ya milioni 76 mpaka milioni 100 walipe milioni moja. Kuanzia milioni 101 mpaka milioni 150 walipie 1,500,000. Kuanzia mauzo ya milioni 150 mpaka hiyo milioni 200 waliyoweka walipe milioni mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mfanyabiashara wa daraja la chini, akienda kulipa kila baada ya miezi mitatu analipa 500,000, watu wengi watalipa kodi na hawatakwepa hiyo EFD. Atakuwa anatumia EFD, anatoa risiti hana wasiwasi, anajua nikifika milioni 200 nitalipa milioni mbili, nikifika 150 nitalipa milioni moja. Itakuwa hakuna suala la kukwepa na watu wengi sana watalipa kodi ambayo itakuwa haina maumivu wala nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la asilimia 3.5 ya mauzo kuanzia milioni 11, Afisa anakaa pale anakukadiria haiangalii ulipata hasara, haiangalii sijui mauzo na mtaji ule ni kiasi gani, mauzo yanaweza kuwa makubwa lakini faida ni kidogo, lakini unapigwa 3.5 na unatakiwa kutoa milioni saba, watu wataendelea kukwepa kulipa kodi kila siku. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri akae na wataalam wake, waweke haya madaraja, mimi nimetoa yangu, lakini mimi sio mtaalam wa kodi, lakini ninyi mnaweza mkayaboresha zaidi. Aidha, wakaongeza au wakapunguza. Haya madaraja yakiwepo watu watakuwa hawana hofu, anajua mimi daraja langu likifika nitalipa kiwango hiki, EFD itaonesha kwamba nimefikiwa hicho kiwango na watu watalipa kodi kabisa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, suala la kujenga Ofisi kwenye majimbo yetu mawili, langu na lake, sisi ni pacha asisahau. Ahsante sana. (Makofi)