Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Edwin Enosy Swalle (18 total)

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa barabara hii imekuwa ikipata ahadi nyingi sana za Serikali hasa kila wakati wa Uchaguzi mwaka 2015 imeahidiwa haikujengwa na leo inaahidiwa tena ndani ya Bunge lako Tukufu, wananchi wa Lupembe wanapenda kujua kuna utofauti gani wa ahadi za nyuma ambazo hazikutekelezwa na ahadi hii ya leo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia wananchi ambao wataathirika na barabara hii hasa katika maeneo ya Nyombo, Kidegembye, Matembwe, Lupembe Barazani, Igombola, Mfiriga mpaka Madeke? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi za Serikali si za kubahatisha na namuomba nimuhakikishie kwamba ahadi ninayomwambia leo ni ahadi ya ukweli, awasiliane na uongozi wa TANROADS watamweleza wako kwenye taratibu za mwisho kabisa kutangaza hii barabara hizi kilomita 50 ili zianze kujengwa kwa kiwango cha lami na hasa tukitambua ni barabara ambayo inaunganisha mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro kupitia Mlimba Ifakara hadi Mikumi. Kwahiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge.

Swali lake la pili ni kuhusu fidia ni kweli tathmini ilishafanyika watu walishatambuliwa na gharama za ulipaji wa fidia ulishahakikiwa nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wote wa vijiji na kata alizozitaja watalipwa fidia yao kabla ya ujenzi kuanza. Hili litakwenda sambamba wakati ujenzi utakapokuwa unaanza wanafanya mobilization Serikali itakuwa inaendelea na kuwalipa ama kuwalipa fidia wananchi ambao watakuwa wameathirika na mradi huu ahsante.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru pia kwa majibu mazuri ya Serikali kuhusu swali hili. Ninalo swali moja tu la nyongeza.

Kwa kuwa zao hili la parachichi limeanza kupata msukumo mkubwa na wananchi wengi wanaendelea kulima zao hili katika mikoa mbalimbali hapa nchini ikiwemo mikoa ya nyanda za juu kusini hasa katika Mikoa ya Mbeya, Njombe, Songwe na Rukwa ; na wananchi wengi wanalima zao hili kwa njia za asili bila kufuata taratibu za kilimo bora: Je, Serikali haioni haja sasa kulisimamia zao hili kwa ukaribu ili wakulima walime kwa tija kwa kuzingatia kilimo bora cha parachichi. (Makofi).
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyosema kwamba zao hili la parachichi ni kati ya mazao ambayo kwa sasa kwa kweli yameleta matumaini makubwa kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wetu. Ndiyo maana kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Serikali imeanza kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaweza wakazalisha zao hili kwa wingi zaidi na katika mazingira bora zaidi ili kuweza kukidhi ushindani uliopo Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba sehemu ya mkakati huo ni pamoja na Wizara ya Kilimo kuanza kujikita kutayarisha mkakati wa kulima mazao ya mboga mboga. Mkakati unaoanzia mwaka 2021 mpaka mwaka 2030 ambao pamoja na mambo mengine utahakikisha kwamba kunakuwa na mbegu bora, kunakuwa na kilimo ambacho kina tija; pia Serikali imeanza kuangalia zaidi katika masoko hayo ya Kimataifa ambayo tumesema kwa kweli ni mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kuangalia uzalishaji wetu bado ni tani 4,000 wakati dunia nzima zinahitajika zaidi ya tani 2,000,000. Kwa hiyo, fursa bado zipo na ndiyo maana tumeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanaweza wakazalisha kwa ubora zaidi.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali juu ya mpango wa zao hili la chai. Ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa tatizo kubwa la wakulima wa chai sasa hivi nchini ni kutokulipwa kwa wakati na wawekezaji; na viongozi wetu wa Serikali wamekuja Mkoa wa Njombe akiwemo Waziri wetu Mkuu na alitoa maelekezo wakulima walipwe kwa wakati lakini mpaka sasa wakulima hawajalipwa hela yao ya chai. Je, ni kauli ipi ya matumaini ya Serikali juu ya wananchi kulipwa fedha zao za chai? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa wawekezaji wengi waliopo sasa hasa Mkoa wa Njombe wanaonekana kutokuwa na uwezo na wakulima wamehamasika kufufua mashamba yao mengi ya chai hivi sasa.

Je, Serikali haioni haja sasa ya kutafuta wawekezaji wengine kwa ajili ya zao la chai Mkoani Njombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Swalle kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwa niaba ya Serikali kwamba Wabunge wa maeneo ya Mufindi, Lupembe na Mkoa wa Njombe kwa ujumla wamekuwa wakifanya jitihada kubwa sana kufanya follow-up kuonesha stability ya zao la chai. Na nipitie Bunge lako hili na kuwahakikishia Wabunge kwamba kampuni zinazosuasua ni kampuni mbili; Uniliver nalipa vizuri na hana matatizo na wakulima wote wanaomhudumia. Tumebaki na changamoto na Kampuni ya DL na mwekezaji wa Lupembe Tea Company Ltd.

Kwa hiyo, kupitia Bunge lako nataka tu niwahakikishie Wabunge kwamba tumewa-summon hawa wawekezaji wawili na tutakutana nao katika Ofisi ya Wizara ya Kilimo, Mwenyezi Mungu akitujaalia kabla ya tarehe 30. Na kwa kuwa Wabunge mtakuwepo, tutawahusisha katika kikao hicho ili tuweze kufikia solution. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu mwekezaji wa Kampuni ya Lupembe, hana option either ku-implement tulichokubaliana ama apishe menejimenti kwa sababu Chama cha Ushirika ni sehemu ya shareholders wa ile kampuni; kaongoza kwa muda mrefu hatujaona performance, tutaweka menejimenti ya muda ambayo itahusisha watu watakaotoka ndani ya Serikali na ushirika na yeye ili waweze kuendesha kile kiwanda kwa sababu kwa muda mrefu tumempa nafasi na ameshindwa kutimiza wajibu wake.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza niishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri ambayo inafanywa kwenye sekta hii muhimu sana ya zao la chai nchini. Nasi wananchi wa Jimbo la Lupembe kwa taarifa tu ni kwamba wananchi sasa wameanza kulipwa mazao yale vizuri, Serikali pia imetupatia fedha kwa ajili ya barabara za kwenye mashamba ya chai, naipongeza sana Serikali na kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara hii ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa, Mpango wa Serikali sasa ni kwenda mbele kuboresha hili zao la chai, Lupembe tulikuwa na mgogoro wa Kiwanda kwa muda mrefu kwa miaka 17 ambao sasa umefikia mwisho. Tumekubaliana kiwanda kirudishwe kwa wabia, kwa maana ya wakulima pamoja na Serikali. Lakini mpaka sasa mchakato wa ukaguzi wa kile kiwanda ili kiweze kukabidhiwa kwa wananchi haujafika mwisho.

Je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba ukaguzi huu unafanyika haraka na kiwanda kile kiweze kwenda kwa wananchi ambao ni wakulima wa chai? (Makofi)

Jambo la pili; ndani ya Bunge lako Tukufu pamekuwa na ahadi ya muda mrefu ya Serikali, ya kuanzisha mnada wa zao la chai Dar es Salaam ambapo kwa muda mrefu chai yetu nchini inauzwa Mombasa.

Je, ni lini mnada huu wa chai utaanzishwa nchini Tanzania ili kukuza bei ya chai ya wananchi wa Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Enosy, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana na sisi kama Wizara ya Kilimo tunamshukuru kwa dhati kabisa kama Mbunge wa eneo la Lupembe, namna alivyoshiriki katika kuhakikisha kwamba mgogoro uliodumu miaka 17 unafika hatma tunakushukuru sana kwa support uliyoitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali baada ya huu mgoogro kuwa muda mrefu na mgogoro huu tumeanza kuhangaika nao kwa zaidi ya miaka 17. Hivi sasa tumefikia tamati na tumesaini makubaliano kupitia Solicitor General kati ya pande ambazo zilikuwa zinavutana na hivi sasa ninavyoongea, Kamati kutoka Ofisi ya TR inafanya tathmini ya kuangalia baadhi ya misitu iliyokuwa sehemu ya mgogoro huo na sasa hivi ninavyoongea wako Lupembe wakifanya kazi hiyo na wameripoti siku ya jana katika Mkoa wa Njombe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ni kufanya tathmini ya investment iliyowekwa na mwekezaji ili tuone kwamba, hatutaki siku ya mwisho kudhulumu haki ya mtu. Tunataka hii situation iondoke na tuweze kufanya tathmini kwa hiyo, tunamuomba Mheshimiwa Mbunge atupe muda. Sisi kama Wizara tumeshawasiliana na Wizara ya Fedha na Ofisi ya TR, kuhakikisha kwamba mgogoro huu tunaumaliza mapema. Ili mwakani kiwanda kile kianze kazi chini ya management mpya na yule Mwekezaji tuwe tumemalizana naye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mnada nataka tu nimwambie kwamba dhamira na maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kwamba, mnada huu unatakiwa uanze mwaka huu Disemba.

Mheshimiwa Mwenuekiti, nataka nitoe tu taarifa katika Bunge lako Tukufu leo hii hii tumemaliza kikao cha wadau, kwa sababu wazalishaji wa chai walikuwa wanahofu namna ambavyo tunauweka huu mnada na ile rule book ambayo tunaipitisha. Tumejadiliana na kuweza kukubaliana juu ya mambo yote ambayo walikuwa na hofu nayo. Sasa tunaenda hatua ya pili mnada wa chai unahitaji kuwepo kwa kusajiliwa kwa brokers ambao watafanya hiyo kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na gharama tumekubaliana tutawasajili ma-broker kutoka nchi ya Kenya na kutoka nchi ya Sri Lanka ili mnada wetu uweze kuwa na International Picture na mwisho tutawasajili bure. Leo ndiyo tumekubaliana hivi vitu, nataka nimuombe Mheshimiwa Mbunge na wadau wa chai watupe muda tutahakikisha mnada unatokea, kuna changamoto chai yetu volume ni ndogo, tunaongea na wenzetu wa Burundi ili chai yao nayo ipite katika soko la Dar es Salaam tuko katika hatua nzuri. Tunasaini MOU na Serikali ya Rwanda kati ya Wizara ya Kilimo ya Tanzania na Wizara ya Kilimo ya Rwanda Juu ya namna ambavyo nao chai yao iweze kupita katika mnada wetu. Kwa hiyo, tuko katika hatua nzuri tumeshakuwa na rule book, tumeshamaliza structure zote tumeshaweka platform na sasa tunaanza kusajili madalali watakaoshiriki katika mnada huu na mnada huu utatokea. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi, lakini pia niipongeze sana Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongeza fedha nyingi sana kwa wasomi wa elimu ya juu. Kwa taarifa tu ni kwamba kati ya uamuzi mkubwa na wa kihistoria uliofanywa mwaka jana na Serikali, ilikuwa ni kusitisha tozo ya asilimia sita na riba ya asilimia 10 kwenye mikopo ya elimu ya juu jambo hili lilikuwa ni ni jambo la kheri sana.

Mheshimiwa Spika, ninayo maswali mawili ya nyongeza swali la kwanza; kwa kuwa Serikali ilisitisha fine ya asilimia sita na riba ya asilimia 10, lakini imesitisha kwa kutoa tamko ndani ya Bunge lako na sheria haijafutwa. (Makofi)

Je, Serikali haioni haja sasa ya kuleta hii sheria Bungeni, ili iweze kufutwa kabisa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili; kwa kuwa baada ya tamko hili la Serikali la kusitisha fine na riba ya asilimia sita na asilimia 10, watu wengi wamejitokeza kwenda kulipa fedha kwenye Bodi ya Mikopo. Lakini wamekuwa wakisumbuliwa kwamba walipe na madeni ya nyuma kabla ya tamko hilo la Serikali.

Ninaomba kauli ya Serikali kusitishwa kwa ulipaji wa riba ya asilimia sita na fine ya asilimia 10, inahusu madeni ya kuanzia lini kwa wananchi wa Tanzania? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Swalle, Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mbunge kwa kuwapigania Watanzania wote, lakini vilevile tupokee shukurani zake kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuona changamoto ya tozo hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la kwanza la sheria nimtoe hofu Mbunge na Bunge lako Tukufu pamoja na kwamba Sheria ile bado haijaletwa hapa Bungeni, lakini bado utendaji wake haulazimishi uwepo wa tozo zile. Kwa hiyo, hata kama haitakuja bado katika utendaji wetu kwa sababu kanuni ndio ambayo inampelekea Mheshimiwa Waziri aweze kuweka kiwango gani cha tozo hizo za kulipwa. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi tunakwenda kufanya tathmini ya kina kwenye eneo hilo la sheria, kama tukiona kuna haja ya kuzileta hapa Bungeni tutaweza kuzileta kwa ajili ya marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili ni eneo la madeni; ninaomba nimhakikishie Mbunge baada ya kauli ile ya kuondoa tozo zile pale pale makato yale yote kwa yule ambaye atakayekuwa hajalipa, hakupaswa kulipa tena na wale ambao wanaokuja baadae nao vilevile hawakupaswa kulipa. Kwa hiyo, kwa namna yoyote ile kama kuna mtu anaona kwamba anadaiwa hayo madeni ya nyuma basi tupate taarifa zake ili tuweze kuzifanyia kazi, lakini kwa mujibu wa sheria pamoja na tamko lile siku ile ile tulipozungumza hapa Bungeni makato yale na madeni yale yali-seize automatically. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza; swali la kwanza kwa kuwa watuhumiwa wengi wanakaa muda mrefu mahabusu na kesi zao zinachelewa kwa sababu ya upelelezi. Ni lini Serikali italeta sheria Bungeni kuweka ukomo wa makosa ya jinai?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa makosa mengi ambayo watu wanakaa muda mrefu kwenye mahabusu hayana dhamana; ni lini Serikali italeta Bungeni sheria ili kuruhusu makosa yote kuwa na dhamana?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Bunge lako limekuwa linafanya marekebisho ya mara kwa mara ya sheria zetu hasa zile zinazohusu Penal Laws na Criminal Procedure Act ambayo kwa kumbukumbu nzuri Mheshimiwa Mbunge katika Bunge la mwezi Februari moja ya sheria inayohusu upelelezi ililetwa hapa katika mabadiliko madogo ya sheria na yako mabadiliko tuliyoyafanya ikiwemo kuruhusu sasa upeleleze ukamilike kwanza kabla kesi hazijapelekwa mahakamani.

Mheshimiwa Spika, lakini hata hivyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 13 katika issue za presumption of innocence nayo pia imesisitiza juu ya kuwepo kwa haki jinai ambazo zinataka mtu asiukumiwe kwanza isipokuwa kila mtu mbele ya sheria aonekane si mkosefu mpaka pale mahakama itakapodhibitisha jambo hilo.

Kwa hiyo, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na kuhakikishia Bunge lako lote kwamba Serikali chini ya uongozi wa Rais wetu mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya mabadiliko ya sheria ili kukidhi haki ya jinai kama ambavyo umetaka ifanyiwe marekebisho.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru sana Waziri wa Katiba na Sheria na Naibu Waziri, lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kupanua wigo wa haki za binadamu nchini Tanzania, nina swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa mwongozo huu ni mwarobaini mzuri wa kusimamia haki za raia wetu nchini. Ni kwa nini mwongozo huu sasa usiingie kama sheria rasmi za nchi yetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kimsingi wazo lake tunalichukua na tutakwenda kulifanyia kazi kuona tuilete kama sheria au iendelee kusimamia kwenye kanuni hizi. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi. Maeneo mengi nchini wananchi wamehamasika kuomba umeme kwenye vitongoji vyao na vijiji. Katika Jimbo la Lupembe wananchi wangu wa Upami, Iyembela na maeneo mengine wamejaza fomu za kulipia umeme lakini kwa muda mrefu hawapewi.

Je, ni nini maelekezo ya Serikali inapotokea wananchi wamelipia umeme lakini hawaingiziwi kwenye maeneo yao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Swalle wa Jimbo la Lupembe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna kipindi ambapo mahitaji ya umeme yalikuwa makubwa sana kwa sababu ya mazingira tuliyokuwa nayo kuliko uwezo wa TANESCO wa kuunganisha kwa wakati. Tunaendelea kujipanga na Serikali imeelekeza inapoanza Julai hatutarajii na hatutakiwi kuwa na kiporo cha zaidi ya mwezi mmoja nyuma, ndiyo mpango wa Serikali na imeongeza bajeti katika maeneo ya uunganishaji ili kuhakikisha kwamba basi mtu anapoomba umeme angalau ndani ya mwezi mmoja awe ameupata kuhakikisha kwamba anaweza kuutumia kwa wakati kwa mahitaji yake. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, asante sana Halmashauri ya Njombe DC ambayo ni Jimbo la Lupembe lina kata 12; na kata 4 kati ya hizo kata ya Ninga, Ikuna, Kichiwa,

Mtwango na Igongolo ziko halmashauri ya Makambako na Jimbo la Makambako na hii inaleta ugumu sana kwenye utawala wa shughuli za maendeleo.

Je, ni lini Serikali itarudisha kata hizi kwenye Halmashauri ya Njombe DC kwa ajili ya kiutawala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa suala hili pia linahusu wenzetu wa upande Ofisi ya Rais-TAMISEMI, na kwa kuwa suala la halmashauri linasimamiwa chini ya Sheria za Serikali ya Mtaa Sura ya 287 na 288 pamoja na mwongozo wa uanzishwaji wa maeneo ya utawala wa mwaka 2014. Ninaomba nimshauri Mheshimiwa Mbunge muendelee kufuata utaratibu wa vigezo na masharti ili kusudi kuweza kukamilisha jambo hilo; kwa kuanzia katika Serikali za vijiji kwenda kwenye DCC kwenda kwenye RCC halafu mkoa mama utatuletea sisi mapendekezo. Ahsante. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza niipongeze sana Wizara ya Katiba na Sheria kwa hatua mbalimbali ambazo wanachukua za kuboresha mfumo wa katiba na sheria nchini.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa watuhumiwa wengi wa makosa ya mauaji wanakaa rumande kwa muda mrefu sana wakisubiri mashauri yao kusikilizwa na watuhumiwa wengi wengine wanafia rumande wakisubiri kesi zao. Naomba kujua ni kwa nini Serikali isiteue Majaji wa muda mfupi ad hoc judges au acting judges wakasikilize mashauri haya kwa haraka?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa kesi nyingi za mauaji zinacheleweshwa kwa sababu ya Idara ya Upelelezi kuchelewa kufanya wajibu wake, aidha kwa makusudi au kwa bahati mbaya. Je, ni lini Serikali italeta Bungeni sheria ya kuweka ukomo wa makosa ya mauaji ambayo upelelezi haukamiliki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nipende kumjibu Mheshimiwa Mbunge maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza pamoja na uhaba wa Majaji tulionao, bado sisi kama Serikali Waziri wakishauriana na Mheshimiwa Jaji Mkuu, wamefanya zoezi la kuwaongezea mamlaka wale Mahakimu ambao ni wa mahakama hizi za ngazi mbalimbali ambazo zinaendesha kesi ambazo hazina mamlaka wao kusikiliza kesi za mauaji. Kwa hiyo, tunao Mahakimu nje ya Majaji 153 ambao wameongezewa mamlaka za kusikiliza kesi za mauaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukiliangalia suala la kesi hizi upande wa mahakama haina kuchelewesha kesi, isipokuwa kwenye eneo hili la upelelezi ambalo kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, tumeamua kuunda timu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ambapo tumemshirikisha Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, pamoja na Ofisi ya DPP, kuharakisha upelelezi wa hizi kesi ili kuhakikisha kwamba zinaisha kwa wakati. Mpaka sasa tayari timu iko mikoani na inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mpaka kufikia mwishoni mwa Mei, hili suala la mrundikano wa kesi utakuwa umekwisha.

Mheshimiwa Spika, hili suala la kuja na sheria, bado tuna taratibu na kanuni na sheria vilevile zinazoonyesha kipindi cha upelelezi cha kesi, lakini matukio ni mengi sana kwa sasa hivi, kwa hiyo, kila siku kesi za mauaji nyie wenyewe mtakuwa mashahidi zinazaliwa kila siku. Kwa hiyo, ndiyo maana tumekuja na huu mkakati ambao tutakuwa tunatumia hawa Mahakimu ambao hawapo katika vigezo vya kusikiliza kesi za mauaji kuwaongezea nguvu. Vile vile tutahakikisha kwamba tunakimbiza hizi kesi na zinakwenda kumalizika kwa wakati, bila kuchelewesha aina yoyote kesi za mauaji.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa barabara hii ina ahadi ya muda mrefu; Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kwenda Jimboni Lupembe kuwaambia wananchi juu ya ahadi hii nzuri ya Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, wananchi wa Nyombo, Kidegembye, Matembwe, Barazani, Madeke na Mfiriga nyumba zao zimewekwa X tangu mwaka 2014. Ni upi mpango wa Serikali sasa kuwalipa fidia wananchi hawa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo nimeshaitembelea. Na kwa kuwa tunaenda kuanza niko tayari baada ya kikao hiki cha Bunge kwenda jimboni kwa Mheshimiwa Mbunge na kuweza kuongea na wananchi, kuwaeleza nini tutakachokifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tulikuwa tumefanya tathmini muda na tayari tumeshamu-engage consultant kwa ajili ya kuhuisha ule uhakiki uliofanyika, ili sasa tuweze kupata taarifa za sasa kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi hawa ambao wote waliwekewa alama za “X” ili tuanze ujenzi.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Hii barabara ya Kibena – Lupembe – Madeke mpaka Morogoro ni barabara ya Kimkoa na ni kero ya muda mrefu ya wananchi wangu. Tarehe 19 Bungeni hapa Serikali iliahidi kuanza ujenzi wa kilometa 25 na sasa tuko kwenye bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Naomba kauli ya Serikali barabara hii inaanza ujenzi lini? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge ni kweli ni barabara inayounganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro, pia yalitolewa maelekezo maalum na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwamba barabara hiyo ni lazima ianze kujengwa. Nami nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Lupembe kwamba katika bajeti hii tayari tumeshaanza taratibu za kuanza kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami, na tutaanza na kilometa 25 kwa kuanzia upande wa Mkoa wa Njombe, upande wa Morogoro tayari tuna kilometa 100 ambazo zinaendelea kujengwa na ziko kwenye taratibu za manunuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande kilichobaki African Development Bank watakifanyia usanifu ili barabara yote iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi. Mji wa Mtwango, Jimbo la Lupembe ni eneo ambalo linakua kwa kasi sana. Serikali ina mpango gani wa kujenga lami katika eneo la Mtwango na barabara ya kwenda Ikuna? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika naomba kujibu swali la uhitaji wa barabara ya lami katika Mji wa Mtwango ambao unaunganisha Ikuna na Mtwango.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mji wa Mtwango unakua kwa haraka sana lakini tulishaelekeza Meneja wa TARURA kuweka vipaumbele vya ujenzi wa barabara za lami, katika Halmashauri zetu zote katika zile fedha za Bajeti za TARURA tulielekeza kwamba angalau kuwe na kipaumbele cha kuanza ujenzi wa barabara za lami.

Mheshimiwa Spika, naomba nisisitize kwamba Meneja wa TARURA Wilaya ya Njombe asimamie maelekezo hayo, lakini kama fedha ile ya bajeti haitoshelezi afanye tathmini na kuleta Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuweze kuona uwezekano wa kupata fedha zingine kwa ajili ya kuongeza nguvu ya utekelezaji wa mradi huo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kata ya Kichiwa hasa vijiji vya Kichiwa, Tagamenda, Upami na maeneo mengine kuna ahadi ya muda mrefu ya kupelekea maji kwa wananchi. Je, ni lini ahadi hii ya Serikali itakwenda kutekelezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo haya aliyoyataja yapo katika mipango ya Wizara katika kuhakikisha maji yanawafikia wananchi. Kata hizi tutakwenda kuzitekeleza kadri ya jiografia yake, endapo bomba kuu itachukua muda mrefu kuwafikia basi visima virefu vitahusika lengo ni kuhakikisha maji yanapatikana bombani. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi. Jimbo la Lupembe katika Vijiji vya Lyalalo, Mfiriga, Itambo, Madeke na Kanikelele wamepata umeme wa REA, lakini tangu mwaka 2021 zimewekwa nguzo na hakuna ambacho kinaendelea. Wananchi hawa wangependa kujua nini mpango wa Serikali kufunga umeme hayo maeneo ambayo wananchi wangu wana nguzo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Swalle, Mbunge wa Lupembe kama ufuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema hapo awali, kulitokea mabadiliko makubwa sana ya vifaa vya dukani hasa vinavyotengenezwa kwa kutumia chuma, alminium na Copper. Tumemaliza mazungumzo sasa ya kuona gharama ambazo zimeongezeka na Serikali inayo fedha ya kuongeza katika utekelezaji wa mradi huu, kutoka ile Shilingi trilioni 1,250.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika muda mfupi ujao wakandarasi watarudi site wakiwa sasa wamepata fedha ya nyongeza ya kununua vile vifaa ambavyo gharama zake zilikuwa zimepanda na mradi utaendelea kama uvyoanza na plan ilivyo.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Jimbo la Lupembe, wananchi wamejenga zahanati nyingi sana. Tunazo zahanati mpya za Welela, Havanga, Lima, Tagamenda, Ikondo na kila mahali. Pia kuna vituo vya afya kama Ikondo, Mtwango, ni vipya kabisa: Ni nini mpango wa Serikali kupeleka watumishi wa afya kwenye vituo hivi ili vianze kufanya kazi mapema? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa afya ni pamoja na kuwa na magari ya wagonjwa, Serikali ina mpango gani wa kupeleka gari la wagonjwa kwa maana ya ambulance katika Jimbo la Lupembe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nawapongeza wananchi wa Jimbo la Lupembe kwa kujitolea nguvu zao na kujenga zahanati na kuanza ujenzi wa vituo vya afya. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri. Kwa hakika Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuleta fedha katika Wilaya ya Njombe na katika Jimbo la Lupembe.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa tunaongelea Kituo cha Afya cha Ikuna kinaendelea kujengwa, lakini pia zahanati zimepata fedha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji. Vile vile watumishi wataendelea kuletwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa maana ya watumishi wa kada za afya kama ambavyo zilishapelekwa 72, lakini ajira nyingine zinazofuata watatoa kipaumbele katika Halmashauri hii.

Mheshimiwa Spika, siku tatu zilizopita Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amegawa magari ya wagonjwa 199 katika halmashauri zetu zote na magari ya usimamizi wa huduma za afya na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Jimbo la Lupembe limepata gari hilo. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba gari lipo njiani linafika wakati wowote kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nitumie nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kutukumbuka watu wa Lupembe kupata barabara ya Agri-Connect. Sasa, hii Barabara ya Lupembe – Kanikelele – Ukalawa ambayo ni Kilometa 18.5 inaishia nyuma kidogo ya Makao Makuu ya Kata ya Ukalawa, umbali kama wa Kilometa moja tu kwenye Makao Makuu ya Kata ya Ukalawa yenyewe.

Je, Serikali haioni haja ya kuongeza hii Kilometa moja ili wafikishe pale Makao Makuu ya Kata ya Ukalawa yenyewe? (Makofi)

Swali langu la pili, ziko barabara kwa mfano ya pale Lupembe Jimboni, kupita kwa Mzee Msambwa kwenda Idamba, kwenda mpaka Mfiriga. Ni lini barabara hii na yenyewe itafanyiwa usanifu na kuanza ujenzi wa lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Swalle, swali lake la kwanza hili la kilometa moja hii ya nyongeza katika zile kilometa 18.5 ili kuweza kufika katika Makao Makuu ya Kata ya Ukalawa, nimtoe mashaka Mheshimiwa Swalle kwamba, mradi huu wa Agri-Connect upo katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya pamoja na Songwe. Hivyo basi, katika usanifu wa awamu inayofuata nitahakikisha kwamba na hicho kipande pia kinaweza kumalizika kuweza kufika katika Makao Makuu ya Kata ya Ukalawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la usanifu kwa barabara nyingine ambazo amezitaja. Kama ambavyo nimemjibu swali lake la nyongeza la kwanza, katika hatua inayofuata Serikali itaangalia kwa sababu mradi huu bado upo, ni kweli wanazalisha sana chai katika Jimbo lake kule la Lupembe, Serikali itaangalia pia barabara hizi ambazo zimesalia ili ziweze kuweka katika mipango inayofuata. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kata ya Mtwango tumejenga kituo cha afya kwa mapato ya ndani, pia tumejenga jengo kwa ajili ya mortuary, lakini hatuna jokofu. Kwa kuwa nimemsikia Mheshimiwa Waziri kwamba Kibaha Vijijini kuna jokofu na hawana jengo la mortuary; je, Serikali iko tayari kuchukua hili jokofu kwenda pale Mtwango? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Jimbo la Lupembe na Mheshimiwa Mbunge kwa kujenga Kituo cha Afya cha Mtwango kwa mapato ya ndani. Pia nimhakikishie tu kwamba tunafahamu kwamba kuna jengo la kuhifadhia maiti halina mashine kwa maana ya jokofu la mortuary na tayari Serikali hii imeshapeleka fedha zaidi bilioni 150 kwenye halmashauri zote kote nchini ndani ya miezi mitatu, minne iliyopita kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kipaumbele yakiwemo majokofu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatoa kipaumbele kupata jokofu katika Kituo cha Afya cha Mtwango, ahsante. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, swali lilikuwa, kuna jokofu mahali halina chumba, kwa hiyo, limehifadhiwa, halafu kuna mahali kuna chumba ambapo hakuna jokofu. Haliwezi kutolewa hili jokofu ambalo kwa sasa limehifadhiwa halihifadhi maiti likapelekwa kwenye chumba ambacho kipo tayari? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru; jokofu hili lilipelekwa na Bohari ya Dawa kwa maana ya MSD na tulishapata taarifa na tayari taratibu za kulihamisha kupeleka sehemu ambayo tayari jengo limekamilika zinaendelea. Baada ya Kibaha kukamilisha jengo watapelekewa tena jokofu lao. Kwa hiyo, naomba nisilete commitment kwamba tunapeleka Lupembe, lakini tunapeleka sehemu ambayo tayari MSD wameshafanya tathmini na wameona uhitaji kwa sasa ili lisikae bila kufanya kazi, ahsante.