Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hamad Hassan Chande (1 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. HAMAD HASSAN CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mtu wa awali katika wachangiaji kwa jioni hii ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah-wataala ambaye ametuwezesha sisi kufika katika jengo hili na ametujalia kuwa na rasilimali ya uhai ambayo ndiyo inatoa thamani ya ubinadamu. Maana yake bila rasilimali ya uhai, basi binadamu anakosa thamani ya ubinadamu. Ushahidi wa hilo, moja kati ya sisi akipoteza uhai tu, basi wapenzi wake wa karibu ikiwemo familia yake, wanakaa kwa pamoja vikao tofauti kujadili wapi wanaenda kumweka na kumtoa kwenye nyumba hata kama ni nzuri aliyoijenga kwa gharama kubwa. Kwa hiyo, tumshukuru Mungu kutujalia rasilimali hii ya uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, nakishukuru sana Chama changu Cha Mapinduzi kwa kunipa nafasi hii, kuniteua tangu awali mpaka kufika hapa leo, kwa sababu ni chama makini chenye viongozi imara sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukurani hizo, naomba kwa ruhusa yako nianze na neno la Mungu kutoka katika Kitabu cha Qurani aya ya nane, Sura ya 102 inayosema:

Kisha kwa hakika mtaulizwa siku hiyo juu ya neema mlizopewa, mmezitumiaje? Kwa hakika tumepewa neema nyingi sana. Mungu ametujalia neema nyingi sana katika nchi yetu ya Tanzania pande zote, sisi ni wa kujivunia kwa neema hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mimi ni Mbunge kutoka Jimbo la Kojani na Wakojani tunajulikana sana kwa shughuli za uvuvi, naomba tu nijielekeze huko kwenye masuala ya uvuvi. Neema hizi ambazo ametupa Mungu hasa katika suala la uvuvi baharini na hata kwenye maziwa, zipo kanuni ambazo zimewekwa na baadhi ya watendaji wetu wa Wizara ama Idara ambazo zimekuwa vikwazo vya kutumia vizuri neema hizo.

Kwa mfano, Kanuni ya 58A(1) na (2) inayomtaka mvuvi lazima atumie mtego wenye urefu wa mita 144. Hiki ni kikwazo kikubwa sana kwa wavuvi wetu, inayotaka uvue samaki wa sentimeta 26. Kwa kweli baadhi ya samaki ambao wala hatuharibu mazingira, tunawahitaji kuwapata, lakini inakuwa ni ngumu sana kwa wavuvi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni ya pili ambayo ni kikwazo kidogo ni 58A ya uvuvi wa dagaa. Inataka dagaa wanaovuliwa wawe ni wa sentimeta tano. Kwa kweli dagaa wa sentimeta tano hadi saba, unaweza ukamwita sio dagaa tena huyo, anaweza kuwa ni samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kanuni ya 66(1)(hh), taa za utumiaji katika uvuvi wakati wa usiku. Kanuni inataka taa ziwe ni za watts 50. Ni mwanga mdogo sana unaopatikana hasa kwa jiografia kwa baadhi ya maziwa kama vile Tanganyika au Bahari Kuu. Kuvua kwa watts 50 ni ndogo sana, samaki au dagaa hawezi kushawishika kuja katika mwanga na kuweza kumvua kwa urahisi. Kwa hiyo, ni vyema angalau iwe inafikia watts 200 au 300 kama kawaida ambavyo tunavua sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni nyingine ambayo ni kikwazo ni ile inayomtaka mvuvi asivue wakati wa mbalamwezi, lazima avue mwezi unapokuwa giza. Sasa hizi sisi wavuvi kwa mfano wa ring net ambao tunavua usiku wote ikiwa ni wa mbalamwezi au wa giza, ukisema tuvue msimu huo, ukifika wakati wa mbalamwezi tukale wapi jamani? Au tusubiri mpaka uingie usiku mwingine wa giza, siku 15 zile, au siku 10; nadhani hiki ni kikwazo kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubaya wa kanuni hizi, zinawafanya wavuvi wetu kutoroka katika nchi yetu na kwenda nchi za jirani. Baya zaidi, sisi tunafuga samaki, tunawalea, wanakua, wenzetu wa jirani ndio wanavua na kutumia samaki hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa hili ni kwamba, hizi kanuni zitakapowekwa au zitakapotungwa ni vyema kuwashirikisha na wavuvi, sio wataalam wa uvuvi peke yao ambao wanajisomea tu kwenye meza na viti. Walengwe kabisa wavuvi wenyewe kusudi washiriki kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nashauri kwa kuwa ni wa mwanzo nilinde kidogo; kanuni hizi zisiwe uzi wa buibui. Nadhani unaujua; spider yule. Kanuni hizi zilikuwa zinamnasa yule mdogo tu, kama vile uzi wa buibui, akipita kurumbiza, inzi, kipepeo, wanakamatwa na ule uzi; lakini akipita njiwa tu, anaondoka nao uzi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakusudia kusema kwamba kanuni hizi zinapowekwa na idara zetu ni vyema ziwe zinakamata wale wakubwa na wadogo. Siyo wadogo tu ambao wanakamatwa hatimaye nyavu zao kuchomwa moto, tukasababisha watu kukataliwa majumbani kwao, tukaongeza idadi ya wajane na vijana wanaotelekezwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Hamad.

MHE. HAMAD HASSAN CHANDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)