Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Anton Albert Mwantona (13 total)

MHE. ANTON A. MWANTONA Aliuliza:-

Serikali ilifanya upembuzi yakinifu na kubaini kuwa jumla ya shilingi Bilioni 21 zinahitajika ili kukarabati miundombinu ya maji Mji wa Tukuyu:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha na kuanza ukarabati wa miundombinu hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Albert Anton Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Mji wa Tukuyu wanapata huduma ya maji safi na salama ya kutosha, Serikali imeendelea na mikakati ya muda mfupi na mrefu. Mkakati wa muda mfupi ulihusisha uboreshaji wa chanzo cha maji cha Masalala, ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 200,000 pamoja na ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa mita 750. Kazi hizo zimesaidia kuimarisha huduma ya maji kwa wakazi wa Mji wa Katumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mkakati wa muda mrefu wa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji safi katika Mji wa Tukuyu, Serikali kwa kutumia wataalam wa ndani wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira za Mbeya na Tukuyu inafanya mapitio ya usanifu wa mahitaji kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji katika Mji wa Tukuyu kwa kutumia chanzo cha Mto Mbaka. Kulingana na usanifu kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huu ni pamoja na ujenzi wa bomba kuu la kilometa 15.5, ujenzi wa bomba la usambazaji maji kilometa 20, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 2,000,000. Mradi huu utatengewa fedha katika mwaka wa fedha 2021/2022 na utekelezaji wake unatarajia kuanza mwezi Julai, 2021.
MHE. ANTON A. MWANTONA Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapima maeneo yote ya umma ikiwemo Shule, Vituo vya Afya na Zahanati kwa kutumia Sheria Na. 4 na Na. 5 ili kuondokana na matatizo ya migogoro ya mipaka kwa Wananchi, lakini pia kuondokana na hoja za ukaguzi ambazo zaidi ya asilimia 90 ya Halmashauri wanazipata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, ninaomba kujibu Swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa baadhi ya maeneo ya umma yaliyoainishwa na kutengwa kwa ajili ya utoaji wa huduma mbalimbali za umma zinazotolewa na Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa hayajapimwa na kuwekewa alama zinazoonekana kwa urahisi. Hali hii husababisha migogoro ya mara kwa mara ya ardhi na uvamizi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali imezielekeza halmashauri zote nchini kutenga fedha kila mwaka katika bajeti zao kwa ajili ya kupima maeneo yote ya taasisi za umma zilizo chini ya mamlaka hizo; ikiwa ni pamoja na kuweka alama zinazoonekana kwa urahisi ili kuepusha migogoro ya ardhi na kuzuia uvamizi unaofanywa na baadhi ya wananchi. Serikali ilishatoa maelekezo haya kwa Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; hivyo nitumie fursa hii kuzisisitiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinatenga fedha na kutekeleza maelekezo hayo. Ahsante sana.
MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza:-

Je, ni lini barabara ya Ibungu – Kafwafwa hadi Kyimo itafanyiwa upembuzi yakinifu na kuanza ujenzi kwa kuwa imetajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Ibungu –Kafwafwa – Kyimo ni barabara ya mkoa yenye urefu wa kilometa 68.2 ambapo kilometa 21.8 zipo Mkoa wa Mbeya na kilometa 46.4 zipo katika Mkoa wa Songwe. Barabara hii ni ya changarawe na udongo na inapita sehemu zenye miinuko mikali hivyo kupitika kwa shida wakati wa mvua kutokana na utelezi. Barabara hii ni muhimu kwa kuwa imekuwa ikitumika katika usafirishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara kwa kuwa imepita katika maeneo ya wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Ibara ya 55(c)(iv): Chama cha Mapinduzi kiliahidi kuielekeza Serikali kukamilisha/kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara mbalimbali hapa nchini zenye jumla ya urefu wa kilometa 7,542.75 ambapo miongoni mwa hizo ni hiyo Barabara ya Ibungu – Kafwafwa – Kyimo yenye urefu wa kilometa 68.2.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Ibungu – Kafwafwa – Kyimo ili hatimaye iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekuwa ikifanyia matengenezo mbalimbali ili kuhakikisha inapitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, nini mchango wa Serikali katika kuwawezesha vijana zaidi ya 100 waliomaliza Vyuo vikuu ambao wapo tayari kwa ajili ya kujiajiri katika kilimo Wilayani Rungwe kupitia Ofisi ya Mbunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBASS P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Rungwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa vijana katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya jamii nchini, imeendelea kuweka mazingira wezeshi ili vijana waweze kuanzisha na kuendesha shughuli zao za kujitegemea kwa kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali. Baadhi ya fursa hizo ni kama ifuatavyo: -

(i) Utengaji wa maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za vijana za kiuchumi zikiwemo shughuli za kilimo. Halmashauri zote nchini zimeagizwa kutenga maeneo hayo, ambapo Halmashauri ya Rungwe imetenga Ekari 88.9 kwa ajili ya shughuli za kilimo, viwanda na masoko.

(ii) Mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba kwa ajili ya mazao ya muda mfupi (mbogamboga). Mafunzo hayo yamenufaisha vijana 98 wa Halmashauri ya Rungwe kati yao 15 wamejifunza namna ya kujenga vitalu nyumba.

(iii) Mikopo isiyo na riba ya 4% iliyotengwa na Halmashauri hiyo ya Rungwe kwa mwaka wa fedha 2021/ 2022 imetenga zaidi ya shilingi milioni 133.7 kwa ajili ya vijana.

(iv) Mikopo yenye riba nafuu ikiwemo Mifuko na Program za uwezeshaji wananchi kiuchumi, ukiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo katika eneo hilo la Jimbo la Rungwe.

(v) Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeanzisha Mpango uitwao “Building a Better Tomorrow” unaowalenga Vijana wahitimu na wasio na kazi wajiingize katika kufanya shughuli katika sekta ya kilimo. Katika mpango huu, Ofisi ya Waziri Mkuu itakuwa na jukumu la kuwapatia mafunzo vijana. Vile vile Wizara ya Kilimo itakuwa na wajibu wa: kwanza, kutoa ardhi; pili, kuweka mitaji na kuwatafutia mitaji vijana hawa; na tatu, kuweka miundombinu katika mashamba ambayo yatakuwa yametengwa ya Agro Parks/Blocks pamoja na kuwaunganisha na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge kupitia ofisi yake awashauri na kuwahimiza vijana wa Rungwe waliohitimu Vyuo Vikuu kuzingatia fursa zinazotolewa na sisi tutaendelea kumpa ushirikiano popote atakapohitaji ili kuweza kuwaunganisha vijana na kuwaweka katika kazi. Ahsante.
MHE ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati majengo ya Zahanati ya Ukoma kuwa Kituo cha Afya cha Kata ya Kisondela Wilayani Rungwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Majengo ya Zahanati ya Makete, Ukoma yaliyokuwa yakitumika kwa wagonjwa wa ukoma ni chakavu. Aidha, kwa kuwa eneo la Kata hii halikidhi vigezo vya kuwa na Kituo cha Afya cha Kimkakati kwa kuzingatia idadi ya watu wasiofikia angalau 10,000, Serikali itaendelea kuitumia zahanati inayotumia moja ya majengo haya kutoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kata hiyo itakapokidhi vigezo vya kuwa na Kituo cha Afya cha kimkakati, Serikali itafanya maamuzi stahiki. Ahsante.
MHE.ANTON A. MWANTONA aliuliza:-

Je, ni lini mradi wa REA II utamalizika kwa Vijiji 25 vilivyobakia katika Jimbo la Rungwe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji 25 vilivyobaki katika Jimbo la Rungwe vitapatiwa umeme kupita Mradi wa REA III mzunguko wa pili ambapo kwa sasa Mkandarasi yupo eneo la mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mkataba, Mkandarasi wa kazi hiyo (ETDCO) atakamilisha kazi kwenye vijiji hivyo Mwezi Desemba, 2023. Ahsante sana.
MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, ni lini mradi wa maji wa Tukuyu utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imeendelea kutekeleza mradi wa maji wa Tukuyu Mjini ambapo kazi zilizopangwa ni pamoja na uhifadhi wa chanzo, ulazaji wa bomba kuu Kilometa 9.5, ulazaji wa mabomba ya usambazaji Kilometa 20 na ujenzi wa tenki la ukumbwa wa lita 1,500,000.

Mheshimiwa Spika, hadi sasa kazi zilizofanyika ni pamoja na uboreshaji wa chanzo cha maji na ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa Kilometa tatu.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huo ulianza mwezi Septemba, 2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi, 2023. Mradi huo utasaidia kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Tukuyu kutoka asilimia 67 na kufika asilimia 90.
MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa soko la Kimataifa la Ndizi katika Kata ya Kiwira utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na Soko la Kisasa la Ndizi, Kiwira, katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe. Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe imeanza maandalizi ya kutekeleza mradi huo kwa kufanya Upembuzi yakinifu, kuandaa michoro ya kihandisi, kupima udongo wa eneo la ujenzi na kuandaa andiko la kuomba fedha kwa ajili ya mradi huo.

Mheshimiwa Spika, andiko limewasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa uchambuzi na pindi litakapopitishwa, mradi utatengewa fedha za ujenzi kupitia utaratibu wa miradi ya kimkakati. Ahsante.
MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha Bajeti ya TARURA inazingatia mitandao ya Barabara katika Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la msingi la TARURA ni kuhakikisha kuwa bajeti inayotengwa inaendana na mtandao wa barabara zilizopo katika Halmashauri nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kendelea kutekeleza jukumu hili, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya barabara ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 962.48 kilitengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024. Kumekuwa na ongezeko la bajeti ambapo shilingi bilioni 2.31 zimetengwa kwa ajili ya kazi za barabara katika Wilaya ya Rungwe.
MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza:-

Je, lini Shule ya Sekondari Kayuki itafanyiwa ukarabati kama alivyoagiza Mheshimiwa Waziri Mkuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za kutekeleza agizo lililotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu la kukarabati Shule ya Sekondari Kayuki zinaendelea ambapo Halmashauri imekamilisha BOQ kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Sekondari Kayuki na imebainika kuwa shilingi milioni 776 zinahitajika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kupata fedha kwa ajili ya kukarabati shule hiyo unaendelea ambapo ukarabati mdogo kwenye hosteli na jengo la utawala umefanyika kwa shilingi milioni 17.4. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukarabati shule hii kama alivyoelekeza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Umeme wa REA katika vijiji na vitongoji ambavyo vimeshawekewa nguzo Jimbo la Rungwe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Rungwe, mkandarasi M/S State Grid Ltd. anakamilisha maandalizi ya vifaa vya ujenzi wa maeneo yaliyobaki na kazi zinatarajiwa kuanza tarehe 1 Julai, 2023 na kukamilika mwezi Oktoba, 2023. Pamoja na miradi mingine katika bajeti ya mwaka 2023/2024, kila Jimbo limetengewa bajeti ya kupelekewa umeme katika vitongoji 15 vya kuanzia wakati maandalizi ya mradi wa Hamlet Electrification Project (HEP) unaotarajiwa kuanza mwaka 2024/2025 yanakamilika, nakushukuru.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE K.n.y. MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, ni lini Mradi wa REA II wenye vijiji 25 na REA III wenye vijiji 33 utakamilika katika Jimbo la Rungwe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji takribani 25 vilivyokuwa vinatekelezwa chini ya Mradi wa REA II vimeshafanyiwa uhakiki ili kujua upungufu ambao haujafanyiwa kazi. Marekebisho ya upungufu uliobainika katika vijiji hivyo utarekebishwa ndani ya miezi mitatu kuanzia mwezi Julai, 2022. Kazi hizo zitatekelezwa na Mkandarasi M/S ETDCO.

Mheshimiwa Naibu S[pika, Mradi wa REA III Mzunguko wa II ambao unapeleka umeme katika vijiji 33 vya Wilaya ya Rungwe unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2022. Kwa sasa, Mkandarasi M/S Electrical Transmission and Distribution Construction and Maintenance Co. LTD anaendelea na kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo.
MHE. JOSEPH A. TADAYO K.n.y. MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza:-

Je, lini mradi wa maji wa Tukuyu utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na ukamilishaji wa Mradi wa Maji Tukuyu Mjini unaolenga kuhudumia wakazi wapatao 63,647 waishio kwenye Mitaa ya Mabonde, Kasyeto, Ndyonga, Batini, Bulyaga na Makandana. Utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 85 ambapo kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa banio katika chanzo cha Mto Mbaka, uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa bomba kuu kutoka kwenye chanzo kwenda kwenye tenki umbali wa Kilometa 9.5, uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa mabomba ya usambazaji, umbali wa kilometa 20 pamoja na ununuzi na ufungaji wa dira mpya za maji 125.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zilizosalia ni ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa lita 1,500,000 pamoja na ununuzi na ufungaji wa dira nyingine mpya 5,875 ambapo kazi zote hizi zinatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2024.