Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Anton Albert Mwantona (1 total)

MHE. ANTON A. MWANTONA Aliuliza:-

Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais ya mwaka 2019 ya kufufua mradi wa uzalishaji wa makaa ya mawe Kiwira itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nami kwa vile nasimama kwa mara ya kwanza mbele ya Bunge lako Tukufu, nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia Mheshimiwa Rais kwa imani aliyonipatia kutumika katika utumishi huu mtukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Jimbo la Rungwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira ulikabidhiwa Serikalini kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mwaka 2013 kwa lengo la kuuendeleza. Katika jitihada za kuuendeleza mgodi huo ambao ni wa chini ya ardhi, STAMICO, kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaendelea na mpango wa pamoja wa muda mrefu wa kuzalisha umeme zaidi ya MW 200 kutoka katika mgodi huo. Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yako hatua za mwisho kukamilika kabla ya kuwasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mapitio.

Mheshimiwa Spika, tayari timu ya wataalamu wa STAMICO na TANESCO wametembelea eneo la mradi kwa lengo la kutambua mahitaji halisi ya uendelezaji wa mradi huo. Aidha, maandalizi ya kuhuisha taarifa ya upembuzi yakinifu ya mradi ya mwaka 2007 yanaendelea. Katika taarifa hiyo, tathmini ya awali inaonesha kwamba jumla ya mashapo yanayokadiriwa tani milioni 93 yapo katika eneo hilo na gharama zinakadiriwa ni jumla ya Dola za Kimarekani milioni 480 ambazo zitahusisha kuchimba makaa ya mawe, kujenga mtambo wa kuzalisha umeme na kujenga njia ya kusafirisha umeme kutoka eneo la mradi yenye urefu wa kilometa 100.

Mheshimiwa Spika, malengo ya muda mfupi ni kuendelea na uchimbaji wa makaa ya mawe kwa matumizi ya viwanda vya ndani na nje ya nchi. Kwa sasa uchimbaji huo unaofanywa na STAMICO unaendelea katika eneo la Kabulo ambapo tangu mwaka 2017 uchimbaji ulipoanza hadi kufikia Desemba, 2020 Shirika limezalisha tani 50,949 za makaa ya mawe na kuuza tani 29,686.56 zenye thamani ya shilingi 2,264,472,998.70. Baadhi ya makaa hayo yameuzwa kwenye viwanda vya simenti nchini vikiwemo viwanda vya Mbeya Cement, Lake Cement pamoja na kampuni ya Sanflag ya Jijini Arusha.

Mheshimiwa Spika, Shirika limefanya tathmini ya ukarabati wa miundombinu ya mgodi wa chini wa Kiwira kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe ili kuendelea kuvipatia viwanda malighafi hiyo, lakini pia ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uzalishaji mkubwa kwa ajili ya mitambo ya kuzalisha umeme pindi makabuliano na TANESCO yatakapokamilika. Aidha, shirika liko katika maandalizi ya mwisho ya kuanza ukarabati wa miundombinu hiyo. Ahsante.